Kuokoa Uhai kwa Damu—Jinsi Gani?
“Chagua uzima . . . [kwa] kuitii sauti yake [Mungu] . . . , kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako.”—KUMBUKUMBU 30:19, 20.
1. Ni jinsi gani Wakristo wa kweli walivyo wa pekee katika heshima yao kwa uhai?
WATU wengi husema kwamba wao huheshimu uhai, wakitoa uthibitisho wa maoni waliyo nayo juu ya adhabu ya kifo, utoaji mimba, au uwindaji. Hata hivyo, kuna njia fulani ya pekee ambayo katika hiyo Wakristo wa kweli huonyesha staha kwa uhai. Zaburi 36:9 husema hivi: “Kwako Wewe [Mungu] iko chemchemi ya uzima.” Uhai ukiwa ni zawadi kutoka kwa Mungu, Wakristo huchagua kufuata maoni yake juu ya damu ya uhai.
2, 3. Kwa nini tumfikirie Mungu kwa habari ya damu? (Matendo 17:25, 28)
2 Uhai wetu hutegemea damu, ambayo hupeleka oksijeni sehemu zote za mwili wetu, huondoa kaboni dayoksaidi, hutuacha tujirekebishe kulingana na mabadiliko katika halijoto, na hutusaidia kupigana na maradhi. Yule aliyeandaa uhai wetu alibuni pia na kuandaa ile tishu ya umajimaji mzuri ajabu wenye kuendeleza uhai uitwao damu. Hiyo huonyesha upendezi wake wenye uendelevu katika kuhifadhi uhai wa kibinadamu.—Mwanzo 45:5; Kumbukumbu 28:66; 30:15, 16.
3 Wakristo na hata watu kwa ujumla wapaswa kujiuliza hivi: ‘Je! damu yaweza kuokoa uhai wangu kwa kazi zayo za kiasili tu, au damu ingeweza kuokoa uhai kwa njia ya kina kirefu hata zaidi?’ Ingawa watu walio wengi hutambua ufungamano uliopo kati ya uhai na zile kazi za kawaida za damu, kwa kweli kuna mengi zaidi yenye kuhusika. Maadili ya Wakristo, Waislamu, na Wayahudi yote hukaza fikira juu ya Mpaji-Uhai aliyeeleza maoni yake mwenyewe juu ya uhai na juu ya damu. Ndiyo, Muumba wetu ana mengi ya kusema juu ya damu.
Msimamo Imara wa Mungu Juu ya Damu
4. Mapema katika historia ya kibinadamu, Mungu alisema nini juu ya damu?
4 Damu imetajwa mara zaidi ya 400 katika Neno la Mungu, Biblia. Kati ya mara zilizo za mapema zaidi ni amri hii ya Yehova: “Kila kiendacho kilicho hai kitakuwa chakula chenu . . . Bali nyama pamoja na uhai, yaani, damu yake, msile.” Aliongezea hivi: “Hakika damu yenu ya uhai wenu nitaitaka.” (Mwanzo 9:3-5) Yehova alisema hivyo kwa Noa, babu wa kale wa familia ya kibinadamu. Hivyo, jamii yote ya kibinadamu ilipashwa habari kwamba Muumba huiona damu kuwa inasimamia uhai. Kila mmoja ambaye hudai kumtambua Mungu kuwa Mpaji-Uhai apaswa basi atambue kwamba Yeye huchukua msimamo imara juu ya kutumia damu ya uhai.
5. Ni nini iliyokuwa sababu kubwa zaidi ya Waisraeli kukataa kula damu?
5 Mungu alitaja tena damu alipokuwa akiipa Israeli fungu layo la Sheria. Walawi 17:10, 11, kulingana na fasiri ya Tanakh ya Kiyahudi, yasomeka hivi: “Mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni waketio kati yao, atakayekula damu, ya aina yo yote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake. Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu.” Sheria hiyo ingeweza kuwa na manufaa za afya, lakini mengi zaidi yalihusika. Kwa kuchukua damu kuwa ya pekee, Waisraeli walipaswa kuonyesha tegemeo lao juu ya Mungu kwa uhai. (Kumbukumbu 30:19, 20) Ndiyo, sababu kuu kwa nini walipaswa kuepuka kutwaa damu ndani yao haikuwa kwamba ingeweza kukosesha afya, bali kwamba damu ilikuwa na maana ya pekee kwa Mungu.
6. Kwa nini twaweza kuwa na uhakika kwamba Yesu aliunga mkono msimamo wa Mungu juu ya damu?
6 Ukristo wasimama wapi kuhusu kuokoa uhai wa kibinadamu kwa damu? Yesu alijua aliyoyasema Baba yake juu ya kutumia damu. Yesu “hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake.” Hiyo yamaanisha aliishika Sheria kikamilifu, kutia na ile sheria juu ya damu. (1 Petro 2:22) Hivyo aliweka kigezo kwa wafuasi wake, kutia na kigezo cha kuheshimu uhai na damu.
7, 8. Ilipataje kuwa wazi kwamba sheria ya Mungu juu ya damu hutumika kwa Wakristo?
7 Historia yatuonyesha lililotukia baadaye wakati kikoa cha baraza lenye kuongoza la Kikristo kilipoamua juu ya kama ilikuwa lazima Wakristo washike sheria zote za Israeli. Chini ya mwongozo wa kimungu, walisema kwamba Wakristo hawana wajibu wa kushika lile fungu la sheria za Kimusa bali kwamba ni ‘lazima kuendelea kushika mwiko wa vitu vinavyotolewa dhabihu kwa sanamu na wa damu na wa vitu vinavyonyongwa [nyama isiyoondolewa damu] na wa uasherati.’ (Matendo 15:22-29, NW) Hivyo wao walielewesha wazi kwamba kuepuka damu ni jambo la maana kiadili kama kuepuka ibada ya sanamu na ukosefu mbaya sana wa adili.a
8 Wakristo wa mapema waliunga mkono katazo hilo la kimungu. Akieleza juu ya hilo, mwanachuo Mwingereza Joseph Benson alisema: “Katazo hili la kutokula damu, alilopewa Noa na vizazi vyake vyote, na likarudiwa kwa Waisraeli . . . halijafutwa kamwe, bali, kinyume cha hivyo, limefanywa imara chini ya Agano Jipya, Matendo 15; na hivyo likafanywa kuwa la wajibu wa daima.” Hata hivyo, je! yale ambayo Biblia husema juu ya damu yangekataza kabisa matumizi ya tiba ya ki-siku-hizi, kama vile kutia damu mishipani, ambayo kwa wazi hayakutumiwa katika siku ya Noa wala katika wakati wa mitume?
Damu Katika Tiba au Ikiwa Tiba
9. Damu ilitumiwaje kitiba nyakati za kale, tofauti na msimamo gani wa Kikristo?
9 Utumizi wa damu kitiba si wa ki-siku-hizi hata kidogo. Kitabu Flesh and Blood (Mnofu na Damu), kilichotungwa na Reay Tannahill, chaonyesha wazi kwamba kwa karibu miaka 2,000, katika Misri na kwingineko, “damu ilionwa kuwa ndiyo dawa kubwa kupita zote kwa ajili ya ukoma.” Waroma waliamini kwamba kifafa kingeweza kuponywa kwa kula damu ya kibinadamu. Tertuliano aliandika hivi juu ya utumizi huo wa “kitiba” wa damu: “Fikiria wale ambao kwa kiu yenye pupa, kwenye wonyesho katika uwanja, hutwaa damu iliyotoka sasa hivi ya wahalifu waovu . . . na kuichukua wakaponye kifafa chao.” Hilo lilitofautiana kabisa na lile ambalo Wakristo walifanya: “Sisi hatuna hata damu ya wanyama kwenye milo yetu . . . Kwenye majaribio ya Wakristo nyinyi huwatolea soseji zilizojazwa damu. Bila shaka, nyinyi mwasadiki kwamba [hiyo] si halali kwao.” Fikiria limaanishwalo: Badala ya kula damu, ambayo iliwakilisha uhai, Wakristo wa mapema walikuwa na nia ya kuchagua kufa.—Linganisha 2 Samweli 23:15-27.
10, 11. Kwa nini yaweza kushikiliwa kwamba kiwango cha Mungu juu ya damu chakataza kukubali kutiwa damu mishipani?
10 Bila shaka, huko nyuma damu haikuwa ikitiwa mishipani, kwa maana majaribio ya kutia damu mishipani yalianza karibu tu na karne ya 16. Hata hivyo, katika karne ya 17, profesa mmoja wa umbo la mwili kwenye Chuo Kikuu cha Copenhagen alikataa hivi: ‘Wale ambao huendelea kutumia damu ya kibinadamu kwa maponyo ya kindani ya maradhi yaonekana huitumia vibaya na kutenda dhambi kwa uzito. Wala-watu hulaaniwa. Mbona sisi hatuchukizwi kabisa na wale watiao uchafu katika koo yao kwa damu ya kibinadamu? Ndivyo ilivyo na kupokea damu ya kigeni kutoka mshipa uliokatwa, ama kupitia kinywani ama kwa vyombo vya kutia mishipani. Wenye kuanzisha upasuaji huo ni chukizo sana kwa sheria ya kimungu.’
11 Ndiyo, hata katika karne zilizopita, watu waliona kwamba sheria ya Mungu ilikataza kutia damu ndani ya mishipa na pia kuila kupitia kinywani. Kufahamu jambo hilo kwaweza kusaidia watu leo waelewe msimamo ambao Mashahidi wa Yehova huchukua, mmoja ambao hupatana na msimamo wa Mungu. Ingawa Wakristo wa kweli wanathamini uhai na kushukuru kwa matibabu, wao huheshimu uhai kuwa zawadi kutoka kwa Muumba, na hivyo basi hawajaribu kuendeleza uhai kwa kutiwa damu.—1 Samweli 25:29.
Je! Inaokoa Uhai Kitiba?
12. Watu wanaofikiri waweza kufikiria jambo gani juu ya kutiwa damu mishipani wakiwa na sababu nzuri?
12 Kwa miaka wastadi wamedai kwamba damu huokoa uhai. Huenda madaktari wakasimulia kwamba mtu fulani aliyepoteza damu nyingi alitiwa damu mishipani akapata nafuu. Hivyo basi watu hujiuliza hivi, ‘Ni kwa kadiri gani msimamo wa Kikristo ulivyo au usivyo wa hekima kitiba?’ Kabla ya kufikiria utaratibu wowote wa kitiba ulio mzito, mtu mwenye kufikiri ataamua manufaa ziwezekanazo, na hatari ziwezazo kutokea pia. Namna gani juu ya kutiwa damu mishipani? Ukweli ni kwamba kutiwa damu mishipani huambatana na hatari nyingi. Zaweza hata kuua.
13, 14. (a) Ni nini nyingine za njia ambazo kutiwa damu mishipani kumethibitika kuwa hatari? (b) Yaliyompata papa yalitoaje kielezi cha hatari za damu kwa afya?
13 Hivi majuzi, Mdkt. L. T. Goodnough na J. M. Shuck waliona hivi: “Jumuiya ya kitiba imekuwa na habari kwa muda mrefu kwamba ingawa akiba ya damu ni salama kwa kadiri ambavyo sisi twajua kuifanya, sikuzote kutia damu mishipani kumekuwa na hatari. Tatizo la mara nyingi zaidi la kutia damu mishipani laendelea kuwa hepataitisi isiyo ya A na isiyo ya B (NANBH); matatanishi mengine yawezayo kuwapo ni kutia na hepataitisi B, kusitawisha mwilini antibodi za kupigana na damu ngeni iliyotiwa mwilini, utendeano mbaya wa damu baada ya kutiwa mishipani, kinga iliyokandamizwa, na kujazana mno kwa chuma.” Ikikadiria ‘kwa kadirio la kiasi’ juu ya moja tu ya hatari kubwa hizo, ripoti hiyo iliongezea hivi: “Yatazamiwa kwamba karibu watu 40,000 [katika United States tu] watapata NANBH kila mwaka na kwamba kufikia asilimia 10 ya hao watapata ugonjwa wa kunyauka ini na/au hepatoma [kansa ya ini].”—The American Journal of Surgery, Juni 1990.
14 Kwa kadiri ambavyo hatari ya kuambukizwa maradhi kutokana na damu iliyotiwa mishipani imepata kujulikana kwa mapana zaidi, ndivyo watu wanavyofikiria upya maoni yao juu ya kutiwa damu mishipani. Kwa kielelezo, baada ya yule papa kupigwa risasi katika 1981, alitibiwa kwenye hospitali moja na kuachwa atoke. Baadaye alilazimika kurudi huko kwa miezi miwili, na hali yake ilikuwa mbaya sana hata ikaonekana ni kama angelazimika kuacha kazi akiwa asiyejiweza. Kwa nini? Alipata ambukizo la saitomegalovairasi kutokana na damu aliyopewa. Huenda watu fulani wakajiuliza, ‘Ikiwa hata damu yenye kupewa papa si salama, namna gani kutiwa damu katika mishipa yetu sisi watu wa kawaida?’
15, 16. Kwa nini kutiwa damu mishipani si salama hata ikiwa damu hiyo imepimwa ionwe kama ina maradhi?
15 ‘Lakini je! kwani wao hawawezi kupima damu kuona kama ina maradhi?’ huenda mtu fulani akauliza. Basi, kama kielelezo fikiria kupima damu kuona kama ina hepataitisi B. Jarida Patient Care (Februari 28, 1990) lilionyesha wazi hivi: “Kutokea kwa hepataitisi iliyofuata kutiwa damu mishipani kulipungua baada ya damu iwayo yote kuwa ikipimwa ili kuona kama ina [ugonjwa huo], lakini asilimia 5-10 ya visa vya hepataitisi ifuatayo kutiwa damu mishipani vingali vyasababishwa na hepataitisi B.”
16 Kasoro ya upimaji huo yaonekana pia kuhusiana na hatari nyingine ambayo huwa katika damu—UKIMWI. Mweneo mkubwa wa UKIMWI umeamsha watu kwa mfoko wa kushtusha, wakaiona hatari ya damu yenye kuambukizwa. Ni wazi kwamba sasa kuna majaribio ya kupima damu kuona kama ina dalili za kiini hicho. Hata hivyo, damu haipimwi katika mahali pote, na yaonekana kwamba huenda watu wakabeba kiini cha UKIMWI katika damu yao kwa miaka mingi bila kiini hicho kugundulika kwa majaribio ya upimaji wa wakati huu. Hivyo basi wagonjwa waweza kupata UKIMWI—tena wamepata UKIMWI—kutokana na damu iliyopimwa na kupitishwa!
17. Ni jinsi gani huenda kutiwa damu mishipani kukafanya madhara ambayo huenda yasionekane wazi mara hiyo?
17 Mdkt. Goodnough na Shuck walitaja pia “ukandamizi wa kinga za mwili.” Ndiyo, ithibati yazidi kuongezeka kwamba hata damu iliyolinganishwa ili kupatanishwa na nyingine yaweza kuharibu mfumo wa kinga ya mgonjwa, ikifungua mlango wa kupata kansa na kifo. Hivyo, uchunguzi mmoja wa Kikanada juu ya “wagonjwa wenye kansa ya kichwa na shingo ulionyesha kwamba wale waliotiwa damu mishipani wakati wa kuondolewa kivimbe walipata baadaye upungufu mkubwa sana wa hali ya kinga.” (The Medical Post, Julai 10, 1990) Madaktari kwenye Chuo Kikuu cha Kalifornia Kusini walikuwa wameripoti hivi: “Kadiri ya kurudi kwa kansa zote za kikoromeo ilikuwa asilimia 14 kwa wale wasiopokea damu na asilimia 65 kwa wale waliopokea. Kwa kansa ya umio wa mdomo, na pua au pango la pua, kadiri ya kurudi ilikuwa asilimia 31 bila kutiwa damu mishipani na asilimia 71 kwa kutiwa damu mishipani.” (Annals of Otology, Rhinology & Laryngology, Machi 1989) Kinga yenye kukandamizwa yaonekana pia kuhusika na uhakika wa kwamba wale wenye kupewa damu wakati wa upasuaji huelekea zaidi kupata maambukizo.—Ona sanduku, ukurasa wa 10.
Je! Kuna Njia Zilizo Badala ya Damu?
18. (a) Hatari zenye kuhusika katika kutiwa damu mishipani zinageuza matabibu kwenye nini? (b) Ni habari gani juu ya njia zilizo badala ambayo wewe ungeweza kuishiriki pamoja na tabibu wako?
18 Huenda watu fulani wakahisi, ‘Kutiwa damu mishipani ni hatari, lakini je, kuna njia zozote zilizo badala?’ Kwa uhakika sisi twataka matibabu ya hali ya juu yaliyo na matokeo mazuri, kwa hiyo je, kuna njia zozote halali zenye matokeo mazuri za kutatua matatizo mazito ya kitiba bila kutumia damu? Kwa kufurahisha, ndiyo. Jarida The New England Journal of Medicine (Juni 7, 1990) liliripoti hivi: “Matabibu, kwa kuzidi kuwa na habari juu ya hatari za [UKIMWI] na maambukizo mengine yapitishwayo kwa kutiwa damu mishipani, wanafikiria upya hatari na manufaa za kutiwa damu mishipani na wanageukia njia zilizo badala, kutia na ile ya kuepuka kabisa kutia damu mishipani.”b
19. Kwa nini wewe waweza kuwa na uhakika kwamba waweza kukataa damu na bado utibiwe kitiba kwa mafanikio?
19 Mashahidi wa Yehova wamekataa kwa muda mrefu kutiwa damu mishipani, si kwa sababu hasa ya hatari za afya, bali kwa sababu ya utii kwa sheria ya Mungu juu ya damu. (Matendo 15:28, 29) Hata hivyo, madaktari wenye ujuzi wamefanikiwa kutunza wagonjwa Mashahidi bila kutumia damu, ikiwa na hatari zenye kuambatana nayo. Ni kama vile tu kielelezo kimoja kati ya vingi vilivyoripotiwa katika fasihi ya kitiba, Archives of Surgery (Novemba 1990) kilivyozungumza juu ya kupandikiza moyo juu ya wagonjwa Mashahidi ambao dhamiri zao ziliruhusu utaratibu huo bila kutia damu. Ripoti hiyo ilisema hivi: “Miaka zaidi ya 25 ya kufanya upasuaji wa moyo juu ya Mashahidi wa Yehova imefikia upeo katika kupandikiza moyo kwa mafanikio bila kutumia vitu vyenye damu . . . Hakuna vifo vyovyote vya wakati wa upasuaji vimetukia, na machunguzo ya mapema yaliyofanywa ili kufuatilia yameonyesha kwamba miili ya wagonjwa hao haikuelekea kuwa na kadiri kubwa zaidi za kukikataa kiungo kile kilichopandikizwa.”
Damu Yenye Kuthaminika Zaidi
20, 21. Kwa nini Wakristo wapaswa kujihadhari wasije wakakuza ule mtazamo wa kwamba “Damu ni dawa mbaya”?
20 Hata hivyo, kuna swali la kuchunguza nafsi ambalo kila mmoja wetu ahitaji kujiuliza. ‘Ikiwa mimi nimeamua kutokubali kutiwa damu mishipani, kwa nini nimefanya hivyo? Kwa uhaki, ni nini sababu yangu hasa, iliyo ya msingi?’
21 Tumetaja kwamba kuna njia zenye matokeo mazuri zilizo badala ya damu ambazo haziingizi mtu katika nyingi za hatari zifungamanazo na kutiwa damu mishipani. Hatari kama vile hepataitisi au UKIMWI hata zimeongoza wengi kukataa damu kwa sababu zisizo za kidini. Watu fulani wana sauti kubwa sana juu ya jambo hilo, kukaribia kuwa ni kama wanapiga miguu wakiwa chini ya beramu inayosema, “Damu Ni Dawa Mbaya.” Yawezekana kwamba Mkristo angeweza kuvutwa aingie katika mpigo huo wa miguu. Lakini huo ni mpigo wa miguu katika barabara yenye kikomo. Jinsi gani hivyo?
22. Ni maoni gani ya uhalisi juu ya uhai na kifo ambayo ni lazima tuwe nayo? (Mhubiri 7:2)
22 Wakristo wa kweli wang’amua kwamba hata kukiwa na matibabu yaliyo bora kabisa katika hospitali zilizo bora kabisa, wakati fulani watu hufa. Kwa kutiwa au kwa kutotiwa damu mishipani, watu hufa. Kusema hivyo si kuonyesha kwamba kuna ajali ambayo huwa imetangulia kupangwa iwafikie watu. Ni kuwa na maoni ya uhalisi. Kifo ni uhakika wa maisha leo. Watu wapuuzao sheria ya Mungu juu ya damu mara nyingi hupata kutokana na damu madhara ya mara hiyo hiyo au yenye kukawia. Wengine wao hata hufa kutokana na damu iliyotiwa mishipani. Na bado, kama vile ni lazima sisi sote tufahamu, wale waendeleao kuwa hai baada ya kutiwa damu mishipani hawajapata uhai wa milele, hivyo basi damu haithibitiki kuokoa uhai wao daima. Kwa upande mwingine, walio wengi wakataao damu, kwa sababu za kidini na/au za kitiba, na hata hivyo ambao hukubali matibabu ya badala huendelea vema sana kitiba. Hivyo huenda wakarefusha maisha yao kwa miaka mingi—lakini si bila kikomo.
23. Sheria za Mungu juu ya damu zahusianaje na kuwa kwetu wenye dhambi na katika uhitaji wa ukombozi?
23 Jambo la kwamba wanadamu wote walio hai leo ni wasiokamilika nao wanakufa pole kwa pole hutuongoza kwenye wazo kuu la yale ambayo Biblia husema juu ya damu. Mungu aliambia ainabinadamu yote wasile damu. Kwa nini? Kwa sababu yawakilisha uhai. (Mwanzo 9:3-6) Katika lile fungu la Sheria, yeye aliweka wazi sheria zenye kutaja uhakika wa kwamba wanadamu wote ni wenye dhambi. Mungu aliwaambia Waisraeli kwamba kwa kutoa dhabihu za wanyama, wangeweza kuonyesha kwamba dhambi zao zilihitaji kufunikwa. (Walawi 4:4-7, 13-18, 22-30) Ingawa hilo silo atakalo kwetu leo, lina umaana sasa. Mungu alikusudia kuandaa dhabihu ambayo ingeweza kulipia kikamili dhambi za waamini wote—ule ukombozi. (Mathayo 20:28) Hiyo ndiyo sababu sisi twahitaji kuwa na maoni ya Mungu juu ya damu.
24. (a) Kwa nini lingekuwa kosa kuchukua hatari za afya kuwa ndilo wazo kuu kuhusu damu? (b) Kwa kweli ni nini wapasa kuwa msingi hasa wa maoni yetu juu ya kutumia damu?
24 Lingekuwa kosa kukaza fikira zote hasa juu ya hatari za damu kwa afya, kwa sababu hilo silo jambo lililokaziwa fikira na Mungu. Huenda ikawa Waisraeli walipata manufaa fulani za afya kwa kutokula damu, kama vile huenda wakawa walinufaika kwa kutokula mnofu wa nguruwe au wa wanyama walao mizoga. (Kumbukumbu 12:15, 16; 14:7, 8, 11, 12) Ingawa hivyo, kumbuka kwamba Mungu alipompa Noa haki ya kula nyama, hakukataza kula mnofu wa wanyama hao. Lakini alitangaza kwamba ni lazima wanadamu wasile damu. Mungu hakuwa akikaza fikira sana-sana juu ya hatari za afya ambazo zingewezekana kuwapo. Hilo silo lililokuwa jambo muhimu kwa amri yake juu ya damu. Waabudu wake walipaswa kukataa kuendeleza uhai wao kwa damu, si kwa sababu hasa kufanya hivyo hakukuwa jambo la afya, bali kwa sababu hakukuwa jambo takatifu. Walikataa damu, si kwa sababu ilikuwa chafu, bali kwa sababu ilikuwa ya thamani kubwa. Ni kwa damu ya dhabihu tu kwamba wangeweza kupata msamaha.
25. Damu yaweza kuokoaje uhai daima?
25 Jambo hilo ni kweli kwa habari yetu. Kwenye Waefeso 1:7, mtume Paulo alieleza hivi: “Katika yeye huyo [Kristo], kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.” Ikiwa Mungu husamehe dhambi za mtu na kumwona huyo kuwa mwadilifu, mtu huyo ana tazamio la uhai usiokoma. Hivyo basi damu ya ukombozi ya Yesu yaweza kuokoa uhai—daima dawamu, naam, milele.
[Maelezo ya Chini]
a Amri hiyo ilimalizia hivi: “Ikiwa kwa uangalifu nyinyi mnajiepusha wenyewe na vitu hivyo, nyinyi mtafanikiwa. Afya njema kwenu nyinyi!” (Matendo 15:29, NW) Elezo “Afya njema kwenu nyinyi” halikuwa ahadi ya kwamba, ‘Mkishika mwiko wa damu au wa uasherati, nyinyi mtakuwa na afya nzuri zaidi.’ Ulikuwa ni umalizio tu kwa barua hiyo, kama vile, ‘Bakini salama salimini.’
b Njia nyingi zilizo badala ya kutia damu mishipani zimezungumzwa katika ile broshua How Can Blood Save Your Life?, iliyochapishwa katika 1990 na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
Wewe Waweza Kueleza?
◻ Ni nini hasa sababu ya Mashahidi wa Yehova kukataa kutiwa damu mishipani?
◻ Ni ithibati gani huhakikisha kwamba msimamo wa Kibiblia juu ya damu si usio na sababu nzuri kitiba?
◻ Ukombozi wahusianaje na sheria ya Biblia juu ya damu?
◻ Ni nini njia pekee ambayo katika hiyo damu yaweza kuokoa uhai daima?
[Sanduku katika ukurasa wa 10]
KUTIA DAMU MISHIPANI NA AMBUKIZO
Baada ya mazungumzo mengi sana ya kuona kama kutiwa damu kwaweza kufanya mgonjwa aelekee zaidi kupata ambukizo, Dkt. Neil Blumberg alikata shauri hivi: “Kati ya machunguzo 12 ya kikliniki [juu ya jambo hilo], 10 yalipata kwamba kutia damu mishipani kulishirikishwa kwa njia yenye kutokeza na ya peke yake kuwa huongezea hatari ya ambukizo la viini vibaya . . . Tena, kutia damu mishipani wakati fulani wa mapema kabla ya upasuaji huenda kukaathiri nguvu za mgonjwa za kukinza ambukizo ikiwa matokeo ya kudhuru kinga ya mwili kwa kutiwa damu mishipani ni ya muda mrefu kama vile machunguzo fulani hudokeza . . . Ikiwa habari hizo zaweza kurefushwa na kuthibitishwa, yaonekana kwamba maambukizo ya baada ya upasuaji yangeweza kuwa ndilo tatizo moja tu lililo la kawaida sana lenye kushirikishwa na kutia mishipani damu ya namna moja.”—Transfusion Medicine Reviews, Oktoba 1990.
[Picha katika ukurasa wa 8]
Chembe nyekundu za damu zilizonenepeshwa. “Kila maikrolita ya damu ina chembe nyekundu za damu kuanzia milioni 4 hadi milioni 6.”—“The World Book Encyclopedia”
[Hisani]
Kunkel-CNRI/PHOTOTAKE NYC