Tamasha Kutoka Bara Lililoahidiwa
Yerusalemu—Kitovu cha Matukio ya Kibiblia
Ingawa mataifa yaliyo mengi yana jiji kuu lililo makao makuu ya serikali, wanafunzi wa Biblia wangeweza kufikiria Yerusalemu kuwa jiji kuu kwa ajili ya wanadamu. Ndivyo ilivyo kwa sababu mambo makubwa yaliyotukia huko ni ya maana kwetu sote.
Hapa juu, unaweza kuona mandhari ambayo ungeona ukisimama mahali palipoinuka kusini mwa Yerusalemu.a Mabonde mawili yalikutana mahali pale palipo na kisehemu cha miti ya rangi kijani-cheusi. Bonde la Kidroni hushuka chini kutoka upande wa kulia; upande wa magharibi, au kushoto, ndiko liliko Bonde la Hinomu lililotokeza jina la Kibiblia Gehena. (Mathayo 10:28; 23:33) Humo katikati (mahali panapoonekana katika kisehemu kilichoangaziwa na jua mbele ya kuta zilizopo) ndimo lilimojengwa Jiji la Daudi la kale. Ndani ya kuta hizo yamo majengo mawili mashuhuri ya kiislamu katika mahali pa kihistoria. Karibu zaidi na ukuta lipo lile kuba la musikiti lililo na rangi ya fedha-samawati, na nyuma yalo lipo lile zege kubwa zaidi la dhahabu la Kuba la Mwamba.
Lakini kwa nini Yerusalemu, na hasa eneo lililotandazwa yalipo sasa hayo majengo mawili yenye kuba, liwe la maana kwako? Basi, picha ya kondoo mume aliyefunganika kwa kukwama katika mti inaleta usimulizi gani wa Kibiblia katika akili yako? Labda ule wa Abrahamu. Ndiyo, yeye ndiye alisafiri pamoja na Isaka mwana wake kwenda Mlima Moria, ambao ithibati inaonyesha ulikuwa kwenye au karibu na mwinuko wa miamba-miamba mahali ambapo unaona zile kuba mbili. Kwa imani, Abrahamu alikuwa na nia ya kudhabihu mwana wake mpendwa, lakini malaika akazuia mkono wake. Ndipo Abrahamu alipopata ‘kondoo mume amenaswa pembe zake katika kichaka’ na kumdhabihu “badala ya mwanawe.” Kwa hiyo kutazama mandhari ya Yerusalemu huenda kukaleta akilini tukio hilo la kutazamisha.—Mwanzo 22:1-13.
Dhabihu nyingine zilitokeza wazi baadaye wakati Sulemani alipomjengea Yehova hekalu lenye fahari kubwa katika uwanja uliotandazwa mahali fulani karibu na pale yalipo sasa yale majengo yenye kuba. (2 Nyakati 3:1) Jaribu kuwazia Waisraeli wakija hapa kutoka sehemu zote za bara wakiwa na dhabihu za wanyama wao kwa ajili ya sikukuu za kila mwaka. Iliyo na umakini mzito zaidi ya zote ilikuwa Siku ya Upatanisho. Siku hiyo, mbuzi mmoja alichaguliwa na ‘kupelekwa jangwani kwa ajili ya Azazeli,’ yawezekana akiteremka chini kuingia Bonde la Kidroni halafu kusini-mashariki kuingia jangwa la Yudea. Mbuzi mwingine na ng’ombe mume walichinjwa na damu yao ikatumiwa kufanya upatanisho kwa ajili ya makuhani na watu. Damu ya kiasi fulani hata ilipelekwa upande wa pili wa pazia kuingizwa katika Patakatifu Zaidi pa hekalu. Kwa hiyo unaweza kuitazama picha ya jiji ukiwa na fikira hiyo akilini.—Walawi 16:1-34.
Dhabihu zote hizo katika Yerusalemu zilielekeza mbele kwenye dhabihu kamilifu ya Yesu Kristo. Katika usiku wake wa mwisho duniani, uliokuwa karibu na wakati wa mwezi mpevu, Yesu aliwakusanya pamoja mitume wake kuadhimisha sikukuu ya mwisho ya Kupitwa iliyo halali. Hiyo ilikuwa katika chumba cha juu kinachofikiriwa kwamba kilikuwa katika sehemu iliyoinuka zaidi ya jiji upande wa kushoto (magharibi) wa eneo la hekalu. Baada ya Yesu kuanzisha Mlo wa Jioni wa Bwana, alipeleka mitume kwenye Mlima wa Mizeituni, ulio ng’ambo ya Bonde la Kidroni, upande wa mashariki (kulia) wa hekalu.—Luka 22:14-39.
Kusaidia kuona jambo hilo akilini, tazama picha iliyoko chini, iliyopigwa kwa kutazama upande wa mashariki kutoka ndani ya Yerusalemu, yawezekana kutoka kwenye eneo ambapo Yesu alifanyia Mlo wa Jioni wa Bwana. Kutokea upande huo, kutoka upande wa chini zaidi kushoto unaona lile kuba (linaloonekana la samawati hivi katika nuru ya mwezi) la musikiti ulio katika eneo la hekalu na mlima. Mbali kidogo upande wa mashariki ndiko liliko Bonde la Kidroni (chini ya mstari wa upeo wa macho) halafu miti ya Bustani ya Gethsemane. Juu kidogo upande wa kulia ndiko uliko Mlima wa Mizeituni.
Mwezi utakuwa unakaribia kupevuka siku ya Machi 22, 1989 pia, wakati ambapo makundi ya Mashahidi wa Yehova duniani pote yatakapokutana (baada ya jua kushuka) kwa ajili ya Mlo wa Jioni wa Bwana, wakifanya ukumbusho wa kifo cha kidhabihu cha Yesu.b Tafadhali upange kuwapo. Siku hiyo, huenda wewe ukataka kutafakari pia juu ya baadhi ya matukio ya wakati uliopita ambayo kitovu cha kutendeka kwayo kilikuwa katika Yerusalemu na kandokando yayo kwa kuhusiana na kumimina kwa Yesu nafsi yake katika kifo. Hivyo Yesu aliondoa malawama juu ya uadilifu wa Yehova na akaikomboa katika dhambi na kifo aina ya binadamu yenye kuitikadi.—1 Wakorintho 11:23-26; Waebrania 9:11-28.
[Maelezo ya Chini]
a Picha hii imo kwa kadiri kubwa zaidi katika 1989 Calendar of Jehovah’s Witnesses
b Ona Mnara wa Mlinzi, Februari 15, 1978, ukurasa 23, kwa maelezo zaidi kuhusu njia ya kuhesabu wakati wa kuadhimisha Mlo wa Jioni wa Bwana.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est