KUHANI MKUU
Mkuu ambaye aliwawakilisha watu mbele za Mungu. Vilevile alikuwa na jukumu la kuwasimamia makuhani wengine wote.
Biblia inatumia maneno tofauti-tofauti kumzungumzia kuhani mkuu, kwa mfano, “kuhani mkuu” (Hes 35:25, 28; Yos 20:6), “kuhani aliyetiwa mafuta” (Law 4:3), “mkuu wa makuhani” (2Nya 26:20; 2Fal 25:18), “mkuu” (2Nya 24:6), au, “kuhani” (2Nya 26:17). Katika mfano huo wa mwisho, muktadha unaonyesha kwamba kuhani mkuu ndiye anayezungumziwa. Katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, inaonekana kwamba maneno “mkuu wa makuhani” yalimaanisha wanaume wenye mamlaka kati ya makuhani, waliotia ndani makuhani wakuu wa zamani waliokuwa wameondolewa na labda, kwa kuongezea, viongozi wa vikundi 24 vya makuhani.—Mt 2:4; Mr 8:31.
Haruni, kuhani mkuu wa kwanza katika Israeli, aliwekwa rasmi na Mungu. (Ebr 5:4) Cheo cha kuhani mkuu katika Israeli kilianza na Haruni na kilipitishwa kwa baba kwenda kwa mwana mzaliwa wa kwanza, isipokuwa iwe kwamba mwana huyo alikufa au hakustahili, kama ilivyokuwa katika kisa cha wana wawili wa kwanza wa Haruni waliomtendea Yehova dhambi na kufa. (Law 10:1, 2) Mfalme Sulemani alimwondoa kuhani mkuu ili kutimiza unabii kutoka kwa Mungu na badala yake akamweka mtu mwingine aliyestahili kutoka katika ukoo wa Haruni. (1Fal 2:26, 27, 35) Baadaye, taifa hilo lilipokuwa likitawaliwa na Watu wa Mataifa, watawala hao wa Mataifa waliwaondoa na kuwaweka wakuu wa makuhani kama walivyotaka. Hata hivyo, inaonekana ukoo wa Haruni ulifuatwa kwa makini katika historia yote ya taifa hilo hadi Yerusalemu lilipoharibiwa mwaka wa 70 W.K., lakini huenda kulikuwa na mabadiliko, kwa mfano, Menelao aliyeitwa pia Onia (Jewish Antiquities, XII, 238, 239 [buku la 1]), ambaye kitabu cha 2 Wamakabayo 3:4, 5 na 4:23 kinaonyesha kwamba alikuwa Mbenyamini.
Matakwa na Sifa za Kustahili Kuwa Kuhani Mkuu. Kupatana na heshima ya cheo hicho, ukaribu wa kuhani mkuu pamoja na Yehova alipoliwakilisha taifa mbele zake, na vilevile umuhimu wa cheo hicho, matakwa ya kustahili yalikuwa ya kiwango cha juu.
Andiko la Mambo ya Walawi 21:16-23 lina orodha ya kasoro za mwili ambazo zingemfanya mtu asistahili kuwa kuhani. Kulikuwa na masharti ya ziada kwa ajili ya kuhani mkuu: Alipaswa tu kuoa bikira Mwisraeli; hakupaswa kuoa mjane. (Law 21:13-15) Isitoshe, hakupaswa kujichafua kwa kugusa maiti, yaani, hakupaswa kugusa maiti ya binadamu, hata iwe maiti ya baba au mama yake, kwa sababu hilo lingefanya asiwe safi. Alipaswa kutunza nywele zake na hakupaswa kurarua mavazi yake kwa ajili ya mtu yeyote aliyekufa.—Law 21:10-12.
Biblia haitaji kihususa umri ambao mtu alipaswa kuwa nao ili astahili kuwa kuhani mkuu. Ingawa inataja kwamba Walawi walistaafu wakiwa na umri wa miaka 50, haitaji kwamba makuhani walistaafu, na inaonyesha kwamba kuhani mkuu aliendelea kuwa na cheo hicho hadi alipokufa. (Hes 8:24, 25) Haruni alikuwa na miaka 83 alipoenda na Musa mbele ya Farao. Inaonekana aliwekwa rasmi kuwa kuhani mkuu mwaka uliofuata. (Kut 7:7) Alikuwa na umri wa miaka 123 alipokufa. Alitumikia kipindi hicho chote bila kustaafu. (Hes 20:28; 33:39) Mpango wa majiji ya makimbilio unaonyesha muda ambao kuhani mkuu alitumikia, kwa kutaja kwamba muuaji asiyekusudia alipaswa kukaa katika jiji la makimbilio hadi kuhani mkuu alipokufa.—Hes 35:25.
Kuwekwa Rasmi. Maoni ya Yehova kuhusu cheo cha Haruni yanaonekana kupitia mapendeleo ambayo alimpa muda mfupi baada ya Waisraeli kutoka Misri. Walipokuwa nyikani wakielekea Sinai, Haruni ndiye aliyeagizwa achukue mtungi wa mana na kuuweka mbele za sanduku la Ushahidi kama kitu kilichopaswa kuhifadhiwa. Hilo lilifanywa kabla ya mpango wa hema la ibada au sanduku la agano kuanzishwa. (Kut 16:33, 34) Baadaye, Haruni ndiye aliyesimamia hema la ibada na Sanduku la Agano. Haruni na wanawe wawili, pamoja na wanaume wazee 70 wa Israeli, walitajwa kihususa kwamba wangepata pendeleo la kupanda Mlima Horebu, ambapo waliona maono ya Mungu.—Kut 24:1-11.
Lakini Yehova alitaja kihususa kwa mara ya kwanza kwamba alikusudia kumtenga Haruni na wanawe kwa ajili ya ukuhani alipompa Musa maagizo kuhusu kutengeneza mavazi ya makuhani. (Kut 28) Baada ya kutoa maagizo hayo, Mungu alimfafanulia Musa utaratibu wa kuwaweka rasmi makuhani na kutaja kihususa kwamba: “Ukuhani utakuwa wao, nayo itakuwa sheria ya kudumu.”—Kut 29:9.
Ili kudumisha utukufu na usafi wa Yehova, Haruni na wanawe walipaswa kwanza kutakaswa na kuwekwa rasmi kupitia utaratibu hususa ili watimize majukumu ya ukuhani. (Kut 29) Musa, ambaye alikuwa mpatanishi wa agano la Sheria, alisimamia utaratibu huo wa kuwaweka rasmi. Sherehe ya kuwaweka rasmi iliyofanywa kwa siku saba kuanzia Nisani 1 hadi 7, 1512 K.W.K., ilianzisha rasmi mpango wa ukuhani, nao wakapewa mamlaka kamili ya kuwa makuhani. (Law 8) Siku iliyofuata, Nisani 8, sherehe ya kwanza ya kufunika dhambi ilifanywa kwa ajili ya taifa (utaratibu ulifanana na sikukuu ya Siku ya Kufunika Dhambi ambayo kulingana na sheria ilisherehekewa Tishri 10; kitabu cha Mambo ya Walawi sura ya 9 kinafafanua mgao wao wa kwanza wakiwa makuhani). Hilo lilikuwa jambo muhimu sana kwa sababu Waisraeli walihitaji kutakaswa kutokana na dhambi zao, kutia ndani dhambi iliyohusiana na yule ndama wa dhahabu.—Kut 32.
Katika kumweka rasmi kuhani mkuu, jambo moja la pekee ambalo Musa alifanya ni kumtia Haruni mafuta matakatifu kichwani yaliyotengenezwa kwa njia ya pekee kulingana na mwongozo wa Mungu. (Law 8:1, 2, 12; Kut 30:22-25, 30-33; Zb 133:2) Makuhani wakuu waliotumikia baada ya Haruni wanaitwa “watiwa mafuta.” Ingawa Biblia haitaji pindi ambazo walitiwa mafuta kihalisi, inataja sheria hii: “Mavazi matakatifu ya Haruni yatatumiwa na wanawe baada yake watakapotiwa mafuta na kuwekwa rasmi kuwa makuhani. Mwana wa Haruni atakayewekwa kuwa kuhani baada yake na ambaye ataingia katika hema la mkutano ili kuhudumu mahali patakatifu atayavaa mavazi hayo kwa siku saba.”—Kut 29:29, 30.
Mavazi Rasmi. Ingawa kuhani mkuu alivaa mavazi ya kitani yaliyofanana na ya makuhani wa cheo cha chini katika shughuli zake za kawaida, katika pindi fulani alivaa mavazi ya pekee yaliyokuwa maridadi na yenye utukufu. Kitabu cha Kutoka sura ya 28 na39 kinafafanua muundo wa mavazi hayo na jinsi yalivyotengenezwa chini ya mwongozo wa Musa kama alivyoagizwa na Mungu. Vazi la ndani kabisa, (isipokuwa suruali fupi iliyofunika “kuanzia kiunoni mpaka mapajani” ambayo ilivaliwa na makuhani wote “ili kufunika uchi wao”; Kut 28:42) lilikuwa kanzu (Kiebr., kut·toʹneth) iliyotengenezwa kwa kitani bora (huenda cheupe) chenye mirabamiraba. Inaonekana kanzu hiyo ilikuwa na mikono mirefu na ilikuwa ndefu kufikia kwenye vifundo vya miguu. Inawezekana kwamba ilifumwa kwa kitambaa kimoja. Ukumbuu uliofumwa kwa kitani bora kilichosokotwa kwa uzi wa bluu, zambarau, na rangi nyekundu ulifunika mwili wa kuhani, inawezekana kuanzia kiuno kwenda juu.—Kut 28:39; 39:29.
Kilemba cha kuhani mkuu kilitengenezwa pia kwa kitani bora, na inaonekana kilikuwa tofauti na cha makuhani wa cheo cha chini. (Kut 28:39) Upande wa mbele wa kilemba ulikuwa na bamba linalong’aa la dhahabu safi lenye maneno haya yaliyochongwa “Utakatifu ni wa Yehova.” (Kut 28:36) Bamba hilo liliitwa “ishara takatifu ya wakfu.”—Kut 29:6; 39:30.
Juu ya kanzu ya kitani walivalia joho la bluu lisilo na mikono (Kiebr., meʽilʹ). Inawezekana kwamba lilifumwa kwa kitambaa kimoja, na sehemu ya juu ilikuwa na upindo thabiti uliofumwa ili joho hilo lisiraruke. Mtu alivaa joho hilo kuanzia juu kupitia kichwani. Joho hilo lilikuwa fupi kuliko ile kanzu ya kitani, na sehemu ya chini lilikuwa na mapambo ya kengele za dhahabu na makomamanga yaliyotengenezwa kwa nyuzi za bluu, sufu ya zambarau, na kitambaa chekundu. Kengele hizo zilisikika kuhani mkuu alipokuwa akihudumu ndani ya patakatifu.—Kut 28:31-35.
Efodi, vazi lililokuwa kama aproni yenye sehemu ya mbele na nyuma, lilifika chini ya kiuno na lilivaliwa na makuhani wote na wakati mwingine na watu wasio makuhani. (1Sa 2:18; 2Sa 6:14) Lakini efodi ya kuhani mkuu ilikuwa maridadi na ilifumwa kwa njia ya pekee. Ilitengenezwa kwa kitani kilichosokotwa kwa nyuzi za sufu ya bluu, kitambaa cha rangi nyekundu, na mabamba membamba ya dhahabu yaliyokatwa na kuwa nyuzi. (Kut 39:2, 3) Inawezekana kwamba upande wa nyuma wa efodi ulikuwa na vipande vya mabegani kila upande kuanzia mabegani hadi kwenye mshipi. Juu ya vipande vya mabegani kulikuwa na vifuko vya dhahabu, kila kimoja kikiwa na jiwe la shohamu, na kila jiwe lilikuwa limechongwa majina sita ya wana wa Israeli (Yakobo) kulingana na walivyozaliwa. Mkanda uliotengenezwa na kitambaa kilekile cha efodi ulifungwa kiunoni juu ya efodi na ulivaliwa kama sehemu ya efodi.—Kut 28:6-14.
Bila shaka, bamba la kifuani la hukumu lilikuwa sehemu ya bei ghali zaidi na yenye utukufu zaidi kati ya mavazi ya kuhani mkuu. Lilitengenezwa kwa kitambaa kama cha efodi, lilikuwa na umbo la mstatili na urefu wake ulikuwa mara mbili ya upana wake, lakini urefu huo ulikunjwa na kutokeza mraba wenye sentimita 22 (inchi 9) kila upande. Urefu ulipokunjwa ulitokeza mfuko au pochi. (Tazama KIFUKO CHA KIFUANI.) Kifuko cha kifuani kilipambwa kwa mawe 12 ya thamani yaliyowekwa kwenye vifuko vya dhahabu, kila jiwe likiwa limechongwa jina la mwana wa Israeli. Mawe hayo ya zabarijadi, topazi, zumaridi, na mawe mengine ya thamani, yalipangwa katika safu nne. Minyororo miwili iliyosokotwa ya dhahabu ilitengenezwa kwenye kifuko cha kifuani, na pete za dhahabu ziliwekwa kwenye pembe za kifuko hicho; pete mbili za juu ziliunganishwa na vipande vya mabegani vya efodi kwa kutumia mnyororo wa dhahabu. Pete mbili za chini ziliunganishwa na vipande vya mabegani kwa nyuzi za bluu, juu ya mshipi.—Kut 28:15-28.
Musa aliweka Urimu na Thumimu kwenye “kifuko cha kifuani.” (Law 8:8) Haijulikana kihususa Urimu na Thumimu zilikuwa nini. Baadhi ya wasomi wanaamini kwamba vilikuwa vitu vilivyotumiwa kupiga kura vilivyowekwa kwenye kifuko cha kifuani, navyo vilitumiwa kwa mwongozo wa Yehova kutoa jibu la “ndiyo” au “hapana.” Ikiwa ndivyo, huenda viliwekwa kwenye “pochi” ya kifuko cha kifuani. (Kut 28:30, AT; Mo) Hilo linadokezwa kwenye andiko la 1 Samweli 14:41, 42. Hata hivyo, wengine wanaamini kwamba kwa njia fulani Urimu na Thumimu zilihusiana na mawe yaliyokuwa kwenye kifuko cha kifuani, lakini inaelekea kwamba maoni hayo si sahihi. Marejezo mengine ya Urimu na Thumimu yanapatikana kwenye Hesabu 27:21; Kumbukumbu la Torati 33:8; 1 Samweli 28:6; Ezra 2:63; na Nehemia 7:65.—Ona URIMU NA THUMIMU.
Kuhani mkuu alivaa mavazi hayo maridadi alipoenda mbele za Yehova ili kuuliza swali kuhusu jambo muhimu. (Hes 27:21; Amu 1:1; 20:18, 27, 28) Vilevile, katika Siku ya Kufunika Dhambi, baada ya dhabihu za dhambi kutolewa, kuhani mkuu alivua mavazi yake meupe ya kitani na kuvaa mavazi maridadi yenye utukufu. (Law 16:23, 24) Inaonekana hata katika pindi nyingine alivaa mavazi hayo maridadi yenye utukufu.
Maagizo kuhusu Siku ya Kufunika Dhambi, kwenye Mambo ya Walawi sura ya 16, hayaonyeshi kihususa kwamba baada ya kuhani mkuu kuvaa mavazi yenye utukufu alipaswa kuinua mikono yake na kuwabariki watu. Hata hivyo, katika simulizi kuhusu sherehe ya kufunika dhambi iliyofanywa siku moja baada ya ukuhani kuanzishwa rasmi, shughuli ambayo ililingana sana na utaratibu wa Siku ya Kufunika Dhambi, tunasoma hivi: “Kisha Haruni akainua mikono yake kuelekea watu, akawabariki.” (Law 9:22) Yehova alikuwa ametoa maagizo kuhusu jinsi ambavyo kuhani angebariki watu alipomwagiza hivi Musa: “Mwambie hivi Haruni na wanawe: ‘Hivi ndivyo mtakavyowabariki Waisraeli. Waambieni: “Yehova na awabariki na kuwalinda. Yehova na awaangazie nuru ya uso wake, na kuwapa kibali chake. Yehova na ainue uso wake kuwaelekea na kuwapa amani.”’”—Hes 6:23-27.
Wajibu na Majukumu. Heshima, majukumu, na uzito wa cheo cha kuhani mkuu unakaziwa na ukweli huu kwamba ikiwa angetenda dhambi angewaletea watu hatia. (Law 4:3) Kuhani mkuu peke yake ndiye aliyeruhusiwa kuingia Patakatifu Zaidi katika hema la ibada, siku moja tu kwa mwaka, yaani, Siku ya Kufunika Dhambi. (Law 16:2) Alipoingia katika hema la mkutano siku hiyo, hakuna kuhani mwingine aliyeruhusiwa kuingia ndani ya hema hilo. (Law 16:17) Alisimamia shughuli zote za Siku ya Kufunika Dhambi. Alitoa dhabihu za kufunika dhambi kwa ajili ya nyumba yake na kwa ajili ya watu kwenye pindi za pekee (Law 9:7) na alienda mbele za Yehova kwa niaba ya watu hasira ya Yehova ilipowaka dhidi yao. (Hes 15:25, 26; 16:43-50) Masuala yanayohusu taifa zima yalipoibuka, yeye ndiye aliyeenda mbele za Yehova akiwa na Urimu na Thumimu. (Hes 27:21) Alisimamia kuchinjwa na kuchomwa kwa ng’ombe mwekundu, ambaye majivu yake yalitiwa katika maji kwa ajili ya kutakasa.—Hes 19:1-5, 9.
Kuhani mkuu angeweza kutimiza jukumu lolote la ukuhani au kushiriki katika sherehe yoyote, ikiwa angependa. Kufikia kipindi cha Mfalme Daudi, idadi ya makuhani ilikuwa imeongezeka. Ili wote wapate nafasi ya kuhudumu, Daudi aliwapanga makuhani katika vikundi 24. (1Nya 24:1-18) Mfumo huo uliendelea kipindi chote kulipokuwa na mpango wa ukuhani. Hata hivyo, kuhani mkuu hakupangiwa wakati fulani hususa wa kutimiza huduma katika hema la ibada, kama ilivyokuwa kwa makuhani wa cheo cha chini, kuhani mkuu angeweza kushiriki wakati wowote. (Makuhani wa cheo cha chini wangeweza kusaidia wakati wowote, lakini majukumu fulani yalitengwa kwa ajili ya makuhani wa vikundi fulani hususa.) Kama ilivyokuwa kwa makuhani wa cheo cha chini, vipindi vya sherehe ndivyo vilivyokuwa vipindi vyenye shughuli nyingi zaidi kwa kuhani mkuu.
Kuhani mkuu ndiye aliyesimamia hema la ibada, utumishi uliofanywa humo, na hazina. (2Nya 12:7-16; 22:4) Inaonekana kwamba cheo hiki kilikuwa pia na kuhani wa pili ambaye alimsaidia kuhani mkuu. (2Fal 25:18) Katika nyakati za baadaye, msaidizi huyo, aliyeitwa Sagani, angesimamia mambo kwa niaba ya kuhani mkuu ikiwa kuhani mkuu angeshindwa kuwepo. (The Temple, cha A. Edersheim, 1874, uku. 75) Eleazari, mwana wa Haruni, alipewa jukumu la pekee la kusimamia.—Hes 4:16.
Kuhani mkuu aliongoza pia katika kulifundisha taifa sheria za Mungu.—Law 10:8-11; Kum 17:9-11.
Kuhani mkuu na viongozi wengine (Yoshua, Waamuzi, na wakati wa wafalme, mfalme) ndio waliokuwa mahakama kuu ya taifa. (Kum 17:9, 12; 2Nya 19:10, 11) Baada ya Sanhedrini kuanzishwa (nyakati za baadaye), kuhani mkuu ndiye aliyesimamia baraza hilo. (Kulingana na mapokeo fulani, hakusimamia kila kesi—alisimamia ikiwa angependa.) (Mt 26:57; Mdo 5:21) Kuhani Mkuu Eleazari alishirikiana na Yoshua kuigawanya nchi kati ya yale makabila 12.—Yos 14:1; 21:1-3.
Kifo cha kuhani mkuu kilitangazwa katika majiji yote ya makimbilio nchini; kilimaanisha kwamba watu walioishi katika majiji hayo wangewekwa huru kutokana na hatia ya kuua bila kukusudia.—Hes 35:25-29.
Ukoo wa Kuhani Mkuu. Ili upate ukoo wa kuhani mkuu na majina ya wale waliokuwa na cheo hicho, tafadhali tazama chati iliyoambatanishwa. Biblia inataja kihususa majina ya watu wachache waliokuwa na cheo hicho, lakini ina orodha ya ukoo wa Haruni. Bila shaka, wengi kati ya wale walioorodheshwa kwenye ukoo wa kuhani mkuu walitumikia wakiwa makuhani wakuu, hata ingawa Biblia haitaji pindi ambazo walitumikia wala kutaja kihususa kwamba walikuwa makuhani wakuu. Haiwezekani kwamba wachache hao wanaotajwa ndio tu waliotumikia katika kipindi chote, hasa tangu mwaka wa 1512 K.W.K. ukuhani ulipoanzishwa hadi mwaka wa 607 K.W.K., Yerusalemu lilipoharibiwa. Vilevile, kuna majina yanayokosekana kwenye ukoo wa kuhani mkuu, kwa hiyo, inawezekana kwamba kuna baadhi ambao hawajatajwa waliokuwa na cheo hicho. Kwa hiyo, chati hiyo haikusudiwi kumpa msomaji orodha kamili na iliyo sahihi ya ukoo wa kuhani mkuu bali inaweza kumsaidia kuelewa vizuri ukoo huo.
Ukuhani wa Melkizedeki. Kuhani wa kwanza anayetajwa katika Biblia ni Melkizedeki, aliyekuwa “kuhani wa Mungu Aliye Juu Zaidi” na pia mfalme wa Salemu (Yerusalemu). Abrahamu alikutana na kuhani huyo aliyekuwa mfalme alipokuwa akirudi baada ya kuwashinda wafalme watatu waliokuwa wameungana na Mfalme Kedorlaoma wa Elamu. Abrahamu alionyesha kwamba alitambua Melkizedeki alipewa mamlaka na Mungu kwa kumpa sehemu ya kumi kati ya matunda ya ushindi wake na kwa kukubali baraka kutoka kwa Melkizedeki. Biblia haitaji ukoo wa Melkizedeki, kuzaliwa kwake, wala kifo chake. Hakuna mtu mwingine aliyetumikia katika mgao huo kabla au baada yake.—Mwa 14:17-24; ona MELKIZEDEKI.
Ukuhani Mkuu wa Yesu Kristo. Kitabu cha Waebrania kinataja kwamba tangu Yesu Kristo alipofufuliwa na kurudi mbinguni, aliwekwa kuwa “kuhani mkuu milele kama Melkizedeki.” (Ebr 6:20; 7:17, 21) Mwandikaji wa kitabu hicho anafafanua jinsi ukuhani wa Kristo ulivyo mkuu na bora kuliko ukuhani wa Haruni kwa kutaja kwamba Melkizedeki alikuwa mfalme na kuhani aliyechaguliwa na Mungu Aliye Juu Zaidi, bali si kupitia urithi. Kristo Yesu, hakutokana na kabila la Lawi, bali la Yuda katika ukoo wa Daudi, hivyo, hakurithi cheo hicho kutoka kwa Haruni, bali alikipata kwa kuteuliwa moja kwa moja na Mungu, kama Melkizedeki. (Ebr 5:10) Mbali na ahadi iliyo kwenye Zaburi 110:4: “Yehova ameapa naye hatabadili nia yake: ‘Wewe ni kuhani milele kwa mfano wa Melkizedeki!’” jambo linalomfanya kuwa Mfalme na Kuhani mbinguni, Kristo pia ana mamlaka ya Ufalme kwa sababu ni uzao wa Daudi. Na kwa sababu hiyo, anakuwa mrithi wa ufalme kupatana na ahadi ya agano la Daudi. (2Sa 7:11-16) Kwa hiyo, ana vyeo viwili, mfalme na kuhani, kama Melkizedeki.
Ubora wa ukuhani wa Kristo unaonekana kupitia wazo la kwamba Lawi, ambaye alitokeza ukoo wa makuhani Wayahudi, alimpa Melkizedeki sehemu ya kumi, kwa maana bado Lawi alikuwa katika viuno vya Abrahamu alipompa sehemu ya kumi mfalme wa Salemu aliyekuwa pia kuhani. Isitoshe, hilo linamaanisha kwamba Lawi alibarikiwa pia na Melkizedeki, na ukweli ni kwamba mdogo hubarikiwa na mkubwa. (Ebr 7:4-10) Vilevile, mtume Paulo anataja kwamba Melkizedeki “hana baba wala mama, hana ukoo, na hana mwanzo wa siku wala mwisho wa uzima” akiwakilisha ukuhani wa milele wa Yesu Kristo, ambaye amefufuliwa na kupewa “uzima usioweza kuharibika.”—Ebr 7:3, 15-17.
Hata hivyo, ingawa Kristo harithi ukuhani kutoka kwa Haruni, wala hana kuhani anayemtangulia wala atakayerithi cheo chake, anatimiza mambo yaliyowakilishwa na kuhani mkuu Haruni. Mtume Paulo anaweka hilo kuwa wazi kabisa anapoonyesha kwamba hema la ibada lililotengenezwa nyikani lilikuwa mfano wa “hema la kweli, ambalo limesimamishwa na Yehova, na si mwanadamu” na kwamba makuhani Walawi walitoa “utumishi mtakatifu kwa mfano wa uhalisi na kivuli cha vitu vya mbinguni.” (Ebr 8:1-6; 9:11) Anaendelea kusema kwamba Yesu Kristo hakuwa na dhabihu ya wanyama bali alitoa mwili wake mkamilifu, na hivyo kuondoa uhalali wa dhabihu za wanyama; kisha Yesu aliingia “katika mbingu,” “si kwa damu ya mbuzi na ya ng’ombe dume wachanga, bali kwa damu yake mwenyewe, mara moja kwa wakati wote, na kupata ukombozi wa milele kwa ajili yetu.” (Ebr 4:14; 9:12; 10:5, 6, 9) Aliingia katika mahali patakatifu palipofananishwa na Patakatifu Zaidi ambapo Haruni aliingia, yaani, “mbinguni kwenyewe, hivi kwamba sasa anaonekana mbele za Mungu kwa ajili yetu.”—Ebr 9:24.
Dhabihu ya Yesu akiwa Kuhani Mkuu haikuhitaji kutolewa tena na tena kama walivyofanya makuhani wa ukoo wa Haruni, kwa sababu dhabihu yake iliondoa dhambi. (Ebr 9:13, 14, 25, 26) Isitoshe hakuna kuhani wa ukoo wa Haruni ambaye angeishi kwa muda mrefu na hivyo kuokoa kikamili au kuleta ukamilifu kwa wale aliowahudumia, lakini Kristo “anaweza pia kuwaokoa kikamili wale wanaomkaribia Mungu kupitia yeye, kwa sababu sikuzote yuko hai ili kuwaombea.”—Ebr 7:23-25.
Mbali na kutoa dhabihu, kuhani mkuu katika Israeli aliwabariki watu na alikuwa mfundishaji mkuu wa sheria za Mungu za uadilifu. Ndivyo ilivyo pia na Yesu Kristo. Alipoenda mbele za Baba yake mbinguni, “alitoa dhabihu moja kwa ajili ya dhambi daima na kuketi kwenye mkono wa kuume wa Mungu, tangu wakati huo akisubiri mpaka adui zake wawekwe kuwa kiti cha miguu yake.” (Ebr 10:12, 13; 8:1) Kwa hiyo, “mara ya pili atakapotokea itakuwa bila dhambi, naye ataonwa na wale wanaomtazamia kwa bidii kwa ajili ya wokovu wao.”—Ebr 9:28.
Ukuu wa cheo cha Yesu akiwa Kuhani Mkuu unaonekana kwa njia nyingine pia. Kwa sababu alikuwa mwanadamu mwenye damu na mwili kama “ndugu” zake (Ebr 2:14-17), alijaribiwa kikamili; alipatwa na upinzani na mateso ya kila aina, na mwishowe akafa kifo cha kuaibisha. Biblia inasema: “Ingawa alikuwa mwana, alijifunza kutii kutokana na mateso yaliyompata. Na baada ya kufanywa kuwa mkamilifu, akawa na daraka la wokovu wa milele kwa ajili ya wote wanaomtii.” (Ebr 5:8, 9) Paulo anataja faida tunazapota kutokana na mateso ya Yesu: “Kwa kuwa yeye mwenyewe aliteseka alipokuwa akijaribiwa, anaweza kuwasaidia wale wanaojaribiwa.” (Ebr 2:18) Wale wanaohitaji msaada wake wanahakikishiwa kwamba yeye ni mwenye huruma na atawasikitikia. Paulo anasema: “Kwa maana hatuna kuhani mkuu ambaye hawezi kuusikitikia udhaifu wetu, bali tuna yule ambaye amejaribiwa katika mambo yote kama tulivyojaribiwa, lakini hakutenda dhambi.”—Ebr 4:15, 16.
Makuhani Wakristo wa Cheo cha Chini. Yesu Kristo ndiye kuhani pekee aliye “mfano wa Melkizedeki” (Ebr 7:17), lakini kama ilivyokuwa kwa Haruni kuhani mkuu wa Israeli, Yesu Kristo ana kikundi cha makuhani wa cheo cha chini aliopewa na Yehova, Baba yake. Makuhani hao wameahidiwa kuwa warithi pamoja naye mbinguni, ambako watashiriki pia kuwa wafalme katika Ufalme wake. (Ro 8:17) Wanajulikana kuwa “ukuhani wa kifalme.” (1Pe 2:9) Katika maono ya kitabu cha Ufunuo wanaimba wimbo mpya na kusema kwamba Kristo aliwanunua kwa damu yake na “[ku]wafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu, [na kwamba] watatawala wakiwa wafalme juu ya dunia.” (Ufu 5:9, 10) Baadaye, maono hayo yanaonyesha kwamba idadi yao ni 144,000. Vilevile wanafafanuliwa kuwa “wamenunuliwa kutoka duniani,” wakiwa wafuasi wa Mwanakondoo, ambao “walinunuliwa kutoka kati ya wanadamu wakiwa matunda ya kwanza kwa Mungu na kwa Mwanakondoo.” (Ufu 14:1-4; linganisha Yak 1:18.) Katika sura hiyo ya kitabu cha Ufunuo (14), onyo linatolewa kuhusu alama ya mnyama wa mwituni, na hivyo kuonyesha kwamba “watakatifu [watahitaji] uvumilivu” ili kukataa alama hiyo. (Ufu 14:9-12) Wale 144,000 ambao wamenunuliwa ndio wanaovumilia kwa uaminifu, kisha wanakuwa hai na kutawala wakiwa wafalme pamoja na Kristo, nao “watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala wakiwa wafalme pamoja naye ile miaka 1,000.” (Ufu 20:4, 6) Utumishi wa Yesu akiwa kuhani mkuu unawasaidia kufikia cheo hicho chenye utukufu.
Wale Wanaonufaika na Ukuhani wa Mbinguni. Maono ya Yerusalemu Jipya yanaonyesha wale watakaonufaika na huduma za Kuhani Mkuu na makuhani wa cheo cha chini watakaotawala pamoja naye mbinguni. Haruni na familia yake, pamoja na makuhani wa kabila la Lawi, waliwahudumia watu wa makablia 12 katika nchi ya Palestina. Kuhusu Yerusalemu Jipya, “mataifa yatatembea kwa nuru yake.”—Ufu 21:2, 22-24.
Ona pia KUHANI.
[Chati kwenye ukurasa wa 1114-1116]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
UKOO WA KUHANI MKUU KATIKA ISRAELI
Ukoo wa makuhani wakuu unapatikana kwenye 1 Mambo ya Nyakati 6:1-15, 50-53 na Ezra 7:1-5. Maandiko hayo hayataji majina yote; baadhi ya watu hawajatajwa, kama ilivyo kawaida kwenye orodha nyingi za ukoo waWaebrania. Josephus na marabi Wayahudi waliongeza baadhi ya majina, lakini usahihi wake unatiliwa shaka. Alama ya kuuliza baada ya majina yaliyoandikwa kwa herufi nzito inaonyesha wale ambao huenda walitumikia wakiwa makuhani wakuu (na kuna uwezekano mkubwa kwamba baadhi yao walitumikia) lakini ambao wanaorodheshwa tu katika ukoo wa kuhani mkuu katika Biblia ingawa haitajwi kihususa kwamba walitumikia wakiwa makuhani wakuu.
Lawi (Mwana wa Yakobo.—Mwa 29:34)
Kohathi (Mwa 46:11; Kut 6:16; 1Nya 6:1)
Ishari
Hebroni
Uzieli
Gershoni
Merari
1512 K.W.K.—MWANZO WA UKUHANI KATIKA ISRAELI
Musa
HARUNI (Kut 6:20; 1Nya 23:13)
ELEAZARI (Kut 6:23; Law 10:1-7; Hes 20:25-28; 1Nya 6:3)
Nadabu (alikufa) (Kut 6:23; 1Nya 24:1, 2)
Abihu (alikufa)
Ithamari
(Sanduku la agano lilipokuwa Shilo tangu Waisraeli walipoingia katika nchi ya ahadi [karibu na 1467 K.W.K.] hadi kipindi cha Eli, na wakati lilipokuwa Betheli kwa muda mfupi.—Yos 18:1; Amu 20:18, 26-28)
FINEHASI (Yehova afanya agano la ukuhani kwa ajili ya ukoo wake.—Kut 6:25; Hes 25:10-13; Yos 22:13; Amu 20:27, 28)
ABISHUA? (1Nya 6:4, 5; Ezr 7:5)
UZI? (1Nya 6:5, 6; Ezr 7:4)
Merayothi (1Nya 6:6, 7; Ezr 7:3, 4)
Amaria (1Nya 6:7)
Ahitubu (2Sa 8:17; 1Nya 6:7, 8; 18:16)
(Inaonekana kwamba ukoo wa Ithamari ndio uliotumikia katika kipindi hiki)
ELI (Kuhani mkuu katika ukoo wa Ithamari; aliyerithi cheo chake kutoka kwa Abishua au Uzi, kulingana na Josephus, Jewish Antiquities, V, 361, 362 [xi, 5]; VIII, 12 [i, 3]; linganisha 1Nya 24:3)
Hofni
Finehasi
(Sanduku la Agano latekwa na Wafilisti. Eli na wanawe wakafa. Sanduku la Agano lilikaa katika eneo la Wafilisti kwa miezi 7. [1Sa 4:17, 18; 6:1] Sanduku la Agano larudishwa, kwa muda mfupi huko Beth-shemeshi, kisha likapelekwa huko Kiriath-yearimu [Baale-yuda] katika nyumba ya Abinadabu kwa miaka mingi, hadi muda mfupi baada ya Daudi kuteka Sayuni.—1Sa 6:14, 15; 7:2; 2Sa 6:2, 3)
Ikabodi (1Sa 4:19-22)
AHIYA (Huenda ni ndugu ya Ahimeleki. Aliyetumikia kwenye hema la ibada huko Shilo.—1Sa 14:3)
(Daudi ajaribu kuleta Sanduku la Agano Yerusalemu; Uza auawa. Daudi apeleka Sanduku la Agano kwenye nyumba ya Obed-edomu Mgathi; Sanduku la Agano lakaa huko kwa miezi mitatu; kisha Daudi alihamishia Yerusalemu.—2Sa 6:1-11)
AHIMELEKI (Alimsaidia Daudi; aliuawa makuhani 85 wa Nobu walipouawa na Sauli.—1Sa 21:1-6; 22:9-18)
ABIATHARI (Alikimbia na kujiunga na Daudi. [1Sa 22:20-23; 23:6, 9; 30:7] Lakini baadaye alimuunga mkono Adoniya kisha Sulemani akamwondoa kwenye cheo hicho. Nyumba ya Eli yaondolewa kwenye ukuhani, na hivyo kutimiza maneno ya Yehova kwenye 1 Samweli 2:30-36.—1Fal 2:27, 35)
Cheo hicho charudi kwenye ukoo wa Eleazari
SADOKI (Huenda alikuwa kuhani wa “pili” wakati wa utawala wa Daudi. [Ona 2Fal 25:18; Yer 52:24.] Alibaki mshikamanifu kwa Daudi Adoniya alipojaribu kuchukua utawala. Sulemani alimweka kuwa kuhani mkuu baada ya kumwondoa Abiathari.—2Sa 8:17; 15:24-29; 19:11; 1Fal 1:7, 8, 32-45; 2:27, 35; 1Nya 24:3)
(Sanduku la Agano lawekwa katika hekalu jipya lililojengwa na Sulemani.—1Fal 8:1-6)
AHIMAAZI? (2Sa 15:27, 36; 17:20; 1Nya 6:8)
AZARIA (I)? (1Fal 4:2; 1Nya 6:9)
(Inaonekana majina matatu, Amaria, Yehoyada, na Zekaria, hayakuorodheshwa kwenye 1Nya 6:1-15)
AMARIA (Katika nyakati za Mfalme Yehoshafati.—2Nya 19:11)
YEHOYADA (Katika nyakati za Ahazia, Athalia, na Yehoashi.—2Fal 11:4–12:9; 2Nya 22:10–24:15)
ZEKARIA? (Alipigwa mawe na kufa kwa agizo la Mfalme Yehoashi.—2Nya 24:20-22)
YOHANANI? (1Nya 6:10)
AZARIA (II) (Huenda ndiye kuhani aliyempinga Mfalme Uzia alipotenda kwa kimbelembele.—1Nya 6:10; 2Nya 26:17-20)
(Huenda majina mawili yanayofuata, Uriya na Azaria, hayakuorodheshwa kwenye 1Nya 6:1-15)
URIYA? (Kuhani aliyejenga madhabahu kama ya wapagani huko Damasko, kwa agizo la Mfalme Ahazi.—2Fal 16:10-16)
AZARIA (II au III) (Wa ukoo wa Sadoki; alitumikia katika kipindi cha Mfalme Hezekia. Huenda ndiye Azaria II, aliyetajwa awali au mwingine aliyekuwa na jina hilo.—2Nya 31:10-13)
AMARIA? (1Nya 6:11; Ezr 7:3)
AHITUBU (Ne 11:11; 1Nya 6:11, 12; 9:11; Ezr 7:2)
MERAYOTHI? (Alikuwa kuhani, mzao wa Ahitubu, lakini huenda hakutumikia kama kuhani mkuu.—1Nya 9:11; Ne 11:11)
SADOKI? (1Nya 6:12; 9:11; Ezr 7:2; Ne 11:11)
SHALUMU? (Meshulamu) (1Nya 6:12, 13; 9:11; Ezr 7:2; Ne 11:11)
HILKIA (Katika nyakati za Mfalme Yosia.—2Fal 22:4-14; 23:4; 1Nya 6:13; 2Nya 34:9-22)
AZARIA (III au IV)? (1Nya 6:13, 14)
SERAYA (Aliuawa na Nebukadneza huko Ribla baada ya Yerusalemu kuharibiwa mwaka wa 607 K.W.K.—2Fal 25:18-21; 1Nya 6:14; Ezr 7:1; Yer 52:24-27)
YEHOSADAKI? (Nebukadneza alimpeleka uhamishoni huko Babiloni mwaka wa 607 K.W.K. Mwana wake Yeshua [Yoshua] na huenda wana wengine walizaliwa walipokuwa uhamishoni. Bila shaka, hangeweza kutimiza majukumu hekaluni.—1Nya 6:14, 15; Ezr 3:2)
(Sanduku la Agano latoweka; halikuwa katika mahekalu yaliyojengwa baadaye huko Yerusalemu)
BAADA YA KURUDI KUTOKA UHAMISHONI
YOSHUA (Yeshua) (Alirudi mwaka wa 537 K.W.K. pamoja na Zerubabeli.—Ezr 2:2; 3:2; Ne 12:10; Hag 1:1; Zek 3:1; 6:11)
YOYAKIMU? (Ne 12:10, 12; alikuwa kuhani wakati Ezra aliporudi Yerusalemu, kulingana na Josephus, Jewish Antiquities, XI, 121 [v, 1])
ELIASHIBU (Siku za Nehemia.—Ne 3:20; 12:10, 22; 13:4, 6, 7)
YOYADA? (Ne 12:10, 11, 22; 13:28)
YOHANANI (Yonathani?) (Ne 12:11, 22, 23)
YADUA? (Huenda ni wakati au “mpaka” siku za Dario Mwajemi.—Ne 12:11, 22)
KUANZIA KIPINDI CHA DARIO (II) MWAJEMI
(Kuanzia kipindi hiki vitabu vya Kiapokrifa, yaani, kitabu cha Kwanza na cha Pili cha Wamakabayo na maandishi ya Josephus, Jewish Antiquities [XI-XX], ndiyo vyanzo vya orodha ya makuhani wakuu hadi kufikia kipindi cha Wamakabayo. Josephus anaorodhesha makuhani wengi wakuu kuliko kitabu cha Kwanza cha Wamakabayo. Kuanzia wakati wa Wamakabayo mpaka Yerusalemu lilipoharibiwa mwaka wa 70 W.K., chanzo kikuu ni Josephus. Biblia inataja majina matatu peke yake [Anasi, Yosefu Kayafa, na Anania]. Inaonekana kwamba katika visa vingi ukoo wa kuhani mkuu ulifuatwa, ingawa watawala wapagani waliwaondoa na kuwaweka makuhani wakuu kama walivyopenda.)
ONIA I
SIMONI I
ELEAZARI
MANASE
ONIA II (Imeendelezwa kwenye safu ya kulia)
SIMONI II
ONIA III
YOSHUA (Kigr., Yesu); pia Yasoni
ONIA (Pia anaitwa Menelao)
YAKIM (Katika Kigiriki, Alkimu); pia Yakimu
WAFALME NA MAKUHANI WAKUU WAMAKABAYO
YONATHANI
SIMONI (Ndugu ya Yonathani)
YOHANA HIRAKANO
ARISTOBULO I
ALEKSANDA YANAO
HARIKANO II (Aristobulo II alinyakua utawala kwa muda mfupi)
ANTIGONA
BAADA YA HERODE MKUU KUWA MFALME (Mt 2:1)
(Waliochaguliwa na Herode)
HANANELI (Kilatini cha Kigr., Ananelo)
ARISTOBULO III
HANANELI (mara ya pili)
YESU (mwana wa Fabeti)
SIMONI (mwana wa Boetho)
MATIA (Matathia) (mkwe wa Boetho)
YOAZARI (mwana wa Boetho)
(Waliochaguliwa na Arkelao, Mfalme wa Yudea—Mt 2:22)
ELEAZARI (mwana wa Boetho)
YESU (mwana wa Sie) (umati wamrudisha Yoazari)
(Waliochaguliwa na Kirenio, Gavana wa Siria—Lu 2:2)
ANASI (Ananu) (mwana wa Sethi) (Alichaguliwa na Kirenio; aliondolewa na Valerio Grato, gavana wa Yudea, karibu mwaka wa 15 W.K. Alikuwa baba mkwe wa Kayafa. Baada ya kuondolewa, aliendelea kuwa na ushawishi mkubwa.—Lu 3:2; Yoh 18:13, 24; Mdo 4:6)
(Waliochaguliwa na Valerio Grato, Gavana wa Yudea)
ISMAELI (mwana wa Fabi)
ELEAZARI (mwana wa Anasi)
SIMONI (mwana wa Kamithu)
YOSEFU KAYAFA (Alikuwa kuhani mkuu wakati wa huduma ya Yesu duniani na mwanzoni mwa huduma ya mitume. Akiwa kuhani mkuu mbele ya Sanhedrini pamoja na Anasi, baba mkwe wake, alisimamia kesi ya Yesu. [Mt 26:3, 57; Lu 3:2; Yoh 11:49, 51; 18:13, 14, 24, 28] Yeye na Anasi waliwaita Petro na Yohana mbele zao na kuwaamuru waache kuhubiri. [Mdo 4:6, 18] Kayafa ndiye kuhani mkuu aliyeidhinisha Sauli apewe barua kwa ajili ya sinagogi huko Damasko zenye maagizo ya kuwakamata Wakristo.—Mdo 9:1, 2, 14)
(Waliochaguliwa na Vitelio, Gavana wa Siria)
YONATHANI (Mwana wa Anasi)
THEOFILO (Mwana wa Anasi)
(Waliochaguliwa na Herode Agripa I)
SIMONI (Kanthera) (mwana wa Boetho)
MATIA (Matathia) (mwana wa Anasi)
ELIONAI (mwana wa Kanthera)
(Waliochaguliwa na Herode, Mfalme wa Kalsi)
YOSEFU (mwana wa Kamidi)
ANANIA (mwana wa Nedebayo) (Alisimamia Sanhedrini wakati wa kesi ya Paulo.—Mdo 23:2; 24:1)
(Waliochaguliwa na Herode Agripa II)
ISMAELI (mwana wa Fabi)
YOSEFU (Kabi) (mwana wa Simoni, kuhani mkuu wa zamani)
ANASI (Ananu) (mwana wa Anasi)
YESU (mwana wa Damenayo)
YESU (mwana wa Gamalieli)
MATIA (Matathia) (mwana wa Theofilo)
FANASI (Faniasi au Finehasi; mwana wa Samweli) (Hakuchaguliwa kuwa kuhani mkuu na Herode Agripa bali watu ndio waliomchagua wakati wa vita dhidi ya Roma)
[Picha kwenye ukurasa wa 1111]
Mavazi ya kuhani mkuu wa Israeli