Onyesha Kwamba Unajali
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Kanada
Maumivu makali yaliyojificha miongoni mwa raia wenye umri mkubwa katika nchi ya Kanada yanawafanya wajiue kwa kiwango cha kutisha. Ripoti moja katika gazeti la habari la Vancouver Sun yaonyesha kwamba huku kisa 1 kati ya 200 vya majaribio ya kujiua ya vijana kikisababisha kifo, kiwango hicho ni 1 kati ya 4 kwa wale walio na umri unaozidi miaka 65. Na hata yaaminiwa kwamba ni “idadi ndogo tu ya visa vya kujiua miongoni mwa watu wazee-wazee inayoripotiwa, kwa sababu huenda iwe vigumu kutofautisha baina ya kujiua na vifo vinavyosababishwa na matatizo ya kiasili ya raia wenye umri mkubwa walio na matatizo mabaya ya kiafya.”
Ni kwa nini watu wengi wazee-wazee hawapendi kuishi? Daktari wa magonjwa ya akili katika Chuo Kikuu cha British Columbia Oluwafemi Agbayewa, na ambaye ni mtaalamu wa suala la kujiua miongoni mwa raia wenye umri mkubwa, anataja sababu zinazochangia kujiua kuwa mshuko wa moyo, kujitenga na jamii, na upweke. Gerry Harrington, mkurugenzi wa kituo cha Suicide Information and Education katika Calgary, Alberta, asema kwamba watu wazeekapo, “wanapoteza staha yao, uvutano wao juu ya wengine, uwezo wao wa kuongoza mambo. . . . Na kwa ghafula, hakuna mtu yeyote anayewauliza maoni yao tena kamwe. Raia wengi wenye umri mkubwa huishia katika hospitali za kibinafsi wakiwa hawana kitu cha kufanya ila kuketi tu, kucheza karata na kutazama televisheni.” Jambo linalozidisha hisia hiyo ni uhakika wa kwamba jamii huthamini sana ujana, na vilevile kujitegemea, uzalishaji, na wepesi —sifa ambazo hupunguka mtu azeekapo.
Hata hivyo, watu wazee-wazee wanathaminiwa sana na Yehova Mungu. Uthibitisho wa kwamba yeye anaelewa sana mahitaji yao ya kihisia-moyo waweza kuonwa katika sheria aliyowapa watu wa Israeli ya kale: “Mwondokeeni mtu mwenye mvi; heshimuni uso wa mtu mzee; nawe mche Mungu wako.” —Mambo ya Walawi 19:32.
Ni jinsi gani basi, tuwezavyo “kuwaonyesha ufikirio” watu wazee-wazee? Tunapaswa kuwaonyesha staha hata ingawa huenda mara nyingine wasiseme maneno ya hekima na huenda hata kutokamilika kwao kukazidishwa na uzee.Onyesha kwamba unajali. Waonyeshe heshima na kuwafahamu kwa kujifunza kutokana na ufahamu wenye kina na hekima yao, na hasa wanapokuwa wameishi maisha yao kwa kuongozwa na roho ya Mungu na uelewevu sahihi wa Neno lake.
Neno la Mungu hufunza mengi zaidi kuhusu habari hii ya kuwatunza na kuwaheshimu wazee-wazee. Kwa habari zaidi, tafadhali andikia wachapishaji wa jarida hili na uombe kitabu Siri ya Kupata Furaha ya Familia.