Majiji ya Makimbilio—Uandalizi Wenye Rehema wa Mungu
“Majiji haya sita yatatumikia kuwa makimbilio, kwa yeyote apigaye nafsi hadi kufa bila kukusudia, kutorokea.”—HESABU 35:15, NW.
1. Mungu ana maoni gani kuhusu uhai na hatia ya damu?
YEHOVA MUNGU huona uhai wa binadamu kuwa mtakatifu. Na uhai umo katika damu. (Mambo ya Walawi 17:11, 14) Kwa hiyo, Kaini, binadamu wa kwanza kuzaliwa duniani, alipata hatia ya damu alipomuua kimakusudi ndugu yake Abeli. Kwa sababu hiyo, Mungu alimwambia Kaini: “Damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi.” Damu iliyochafua ardhi mahali pa mauaji ilitoa ushuhuda ulio kimya lakini wa wazi juu ya uhai uliokuwa umekatizwa kikatili. Damu ya Abeli ilimlilia Mungu alipize kisasi.—Mwanzo 4:4-11.
2. Staha ya Yehova kwa uhai ilisisitizwaje baada ya Furiko?
2 Staha ya Mungu kwa uhai wa binadamu ilisisitizwa baada ya Noa mwadilifu na familia yake kutoka katika safina wakiwa waokokaji wa Furiko la duniani pote. Wakati huo Yehova alipanua lishe ya wanadamu itie ndani nyama ya wanyama lakini si damu. Pia aliamuru hivi: “Damu yenu ya uhai wenu nitaitaka; na kwa mkono wa kila mnyama nitaitaka; na kwa mkono wa mwanadamu, kwa mkono wa ndugu ya mtu nitataka uhai wa mwanadamu. Atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu; maana kwa mfano wake Mungu alimfanya mwanadamu.” (Mwanzo 9:5, 6) Yehova alitambua haki ya mtu wa ukoo wa karibu zaidi wa mtu aliyeuawa kumuua muuaji ampatapo.—Hesabu 35:19.
3. Sheria ya Kimusa iliweka mkazo gani juu ya utakatifu wa uhai?
3 Katika Sheria iliyotolewa kwa Israeli kupitia nabii Musa, utakatifu wa uhai ulisisitizwa mara nyingi. Kwa kielelezo, Mungu aliamuru hivi: “Hupaswi kuua kimakusudi.” (Kutoka 20:13, NW) Staha kwa uhai pia ilionekana wazi katika maneno ya Sheria ya Kimusa juu ya kifo kinachohusu mwanamke mwenye mimba. Sheria ilisema kihususa kwamba mwanamke huyo au mtoto wake aliye tumboni akifa kiaksidenti kwa sababu ya mng’ang’ano baina ya wanaume wawili, waamuzi walipaswa kupima hali na kadiri ambayo mambo yalifanywa kimakusudi, lakini adhabu ingekuwa “uhai kwa uhai.” (Kutoka 21:22-25) Lakini, je, muuaji kimakusudi Mwisraeli kwa njia fulani angeponyoka matokeo ya tendo lake la jeuri?
Himaya kwa Wauaji Kimakusudi?
4. Nje ya Israeli, ni mahali gani pa himaya pamekuwapo nyakati zilizopita?
4 Katika mataifa yasiyo Israeli, wauaji kimakusudi na wahalifu wengine walipewa ulinzi au himaya. Ndivyo ilivyokuwa katika mahali kama hekalu la mungu wa kike Artemi katika Efeso la kale. Kuhusu mahali pengi panapofanana na hapo, yaripotiwa hivi: “Sehemu nyingine za ibada zilikuwa mahali pa kukuza wahalifu; na mara nyingi ikawa lazima kupunguza hesabu za sehemu za kutoa himaya. Katika Athene ni sehemu fulani tu za himaya zilizotambuliwa na sheria kuwa makimbilio (kwa kielelezo, hekalu la Thesio kwa watumwa); katika wakati wa Tiberio makundi ya wahalifu katika sehemu za ibada yalikuwa hatari hivi kwamba ni majiji machache tu yaliyopewa haki ya kutoa Himaya (katika mwaka wa 22).” (The Jewish Encyclopedia, 1909, Buku la 2, ukurasa 256) Baadaye, makanisa ya Jumuiya ya Wakristo yakawa mahali pa kutoa himaya, lakini hilo lilielekea kutoa uwezo kutoka kwa mamlaka za kiraia hadi kwa makasisi na hilo lilikinza utekelezaji wa haki kwa njia ifaayo. Kutumiwa vibaya kwa himaya za kanisa hatimaye kukafanya mpango huo ufutiliwe mbali.
5. Kuna ushuhuda gani kwamba Sheria haikuruhusu ulegevu kuwa dai la kuomba rehema mtu alipouawa?
5 Miongoni mwa Waisraeli, wauaji kimakusudi hawakupewa ulinzi au himaya. Hata kuhani Mlawi anayetumikia kwenye madhabahu ya Mungu alipaswa kuondolewa akauawe kwa ajili ya uuaji kimakusudi aliopanga kwa hila. (Kutoka 21:12-14) Isitoshe, Sheria haikuruhusu ulegevu uwe dai la kuomba rehema mtu alipouawa. Kwa kielelezo, mtu alipaswa kuweka ukuta kandokando ya dari la nyumba yake mpya. La sivyo, nyumba hiyo ingekuwa na hatia ya damu ikiwa mtu angeanguka kutoka kwenye dari na kufa. (Kumbukumbu la Torati 22:8) Na zaidi, ikiwa mwenye fahali aliye na zoea la kupiga watu kwa pembe alionywa lakini hakumchunga mnyama huyo naye akaua mtu, huyo mwenye fahali alikuwa na hatia ya damu naye angeweza kuuawa. (Kutoka 21:28-32) Uthibitisho zaidi wa staha nyingi ya Mungu kwa uhai unaonekana wazi kwa jambo la kwamba mtu yeyote apigaye mwizi hata akamuua alikuwa na hatia ya damu ikiwa kisa hicho kilitokea mchana ambapo mwizi huyo angeweza kuonwa na kutambulishwa. (Kutoka 22:2, 3) Basi, kwa wazi sheria za Mungu zilizosawazika kikamilifu hazikuruhusu wauaji kimakusudi kuponyoka adhabu ya kifo.
6. Sheria ya “uhai kwa uhai” ilitimizwaje katika Israeli la kale?
6 Ikiwa mtu fulani aliuawa kimakusudi katika Israeli la kale, damu ya mtu huyo ilikuwa ilipiziwe kisasi. Sheria ya “uhai kwa uhai” ilitimizwa muuaji kimakusudi alipouawa na “mlipiza kisasi cha damu.” (Hesabu 35:19, NW) Mlipiza kisasi alikuwa mtu wa ukoo wa kiume wa karibu zaidi. Lakini namna gani juu ya wauaji wasiokusudia?
Uandalizi Wenye Rehema wa Yehova
7. Mungu alifanya uandalizi gani kwa wale walioua mtu bila kukusudia?
7 Kwa wale walioua mtu kiaksidenti au bila kukusudia, kwa upendo Mungu aliwaandalia majiji ya makimbilio. Kuwahusu, Musa aliambiwa: “Sema na wana wa Israeli, na ni lazima uwaambie, ‘Mnavuka Yordani hadi bara la Kanaani. Na ni lazima mchague majiji yawafaayo nyinyi. Yatawatumikia yakiwa majiji ya makimbilio, na ni lazima muuaji atorokee huko anayepiga nafsi bila kukusudia hata ikafa. Na hayo majiji lazima yatumikie kwenu yakiwa makimbilio kutoka kwa mlipiza kisasi cha damu, ili muuaji asije akafa mpaka asimame mbele ya kusanyiko kwa ajili ya hukumu. Na majiji mtakayotoa, majiji sita ya makimbilio, yatawatumikia. Majiji matatu mtayatoa upande huu wa Yordani, na majiji matatu mtayatoa katika bara la Kanaani. Hayo yatatumikia kuwa majiji ya makimbilio . . . kwa yeyote apigaye nafsi hadi kufa bila kukusudia, kutorokea.’”—Hesabu 35:9-15, NW.
8. Majiji ya makimbilio yalikuwa wapi, na wauaji wasiokusudia walisaidiwaje kuyafikia?
8 Waisraeli walipoingia Bara Lililoahidiwa, kwa utii walianzisha majiji sita ya makimbilio. Matatu kati ya majiji hayo—Kedeshi, Shekemu, na Hebroni—yalikuwa magharibi mwa Mto Yordani. Upande wa mashariki mwa Yordani mlikuwa na majiji ya makimbilio ya Golani, Ramothi, na Bezeri. Majiji sita ya makimbilio yalikuwa sehemu zilizofaa kwenye barabara zilizotunzwa vizuri. Katika mahali pafaapo kandokando ya barabara hizo, palikuwa ishara zenye neno “makimbilio.” Ishara hizo zilielekezea jiji la makimbilio, naye muuaji asiyekusudia alikimbilia uhai wake kwa jiji lililokuwa karibu zaidi. Hapo angepata ulinzi kutokana na mlipiza kisasi cha damu.—Yoshua 20:2-9.
9. Kwa nini Yehova aliandaa majiji ya makimbilio, nayo yaliandaliwa kwa faida ya nani?
9 Kwa nini Mungu aliandaa majiji ya makimbilio? Yaliandaliwa ili bara lisichafuliwe kwa damu isiyo na hatia na watu wasipate kuwa na hatia ya damu. (Kumbukumbu la Torati 19:10) Majiji ya makimbilio yaliandaliwa kwa faida ya nani? Sheria ilisema: “Kwa ajili ya wana wa Israeli, na kwa ajili ya mkazi-mgeni na kwa ajili ya setla aliye kati yao majiji haya sita yatatumikia yakiwa makimbilio, kwa yeyote apigaye nafsi hadi kufa bila kukusudia, kutorokea.” (Hesabu 35:15, NW) Hivyo, ili kufuatia haki na kuitekeleza huku akitumia rehema, Yehova aliwaambia Waisraeli watenge majiji ya makimbilio kwa wauaji wasiokusudia waliokuwa (1) Waisraeli wa asili, (2) wakazi-wageni katika Israeli, au (3) masetla kutoka nchi nyinginezo waliokuwa wakiishi katika bara hilo.
10. Kwa nini yaweza kusemwa kwamba majiji ya makimbilio yalikuwa uandalizi wenye rehema uliofanywa na Mungu?
10 Lafaa kuonwa kwamba hata ikiwa mtu alikuwa muuaji asiyekusudia, alipaswa kuuawa chini ya sheria ya Mungu: “Atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu.” Kwa hiyo, ilikuwa tu ni uandalizi wenye rehema wa Yehova Mungu kwamba muuaji asiyekusudia aweze kutorokea mojapo majiji ya makimbilio. Yaonekana kwamba kwa ujumla watu walimhurumia mtu yeyote aliyekuwa akimtoroka mlipiza kisasi cha damu, kwa kuwa wote walijua kwamba wanaweza bila kukusudia kufanya kosa ilo hilo na kutafuta makimbilio na rehema.
Mbio ya Kupata Makimbilio
11. Katika Israeli la kale, mtu angefanya nini ikiwa alimuua kimakusudi mfanyakazi mwenzake?
11 Kielezi hiki chaweza kuzidisha uthamini wako wa mpango wa rehema wa Mungu wa kuandaa makimbilio. Ebu wazia kwamba ulikuwa mtu akataye kuni katika Israeli la kale. Tuseme kichwa cha shoka kilitoka ghafula kwa mpini wacho na kumpiga mfanyakazi mwenzako hata akafa. Ungefanya nini? Naam, Sheria ilifanya uandalizi wa hali iyo hiyo. Bila shaka, ungetumia uandalizi huo kutoka kwa Mungu: ‘Na hii ndiyo hukumu ya mwenye kuua mtu, atakayekimbilia jiji la makimbilio awe hai; atakayemwua mwenziwe pasipo kukusudia, wala hakumchukia tangu hapo; kama aingiapo mtu na mwenziwe mwituni kwenda kukata kuni, akapeleka mkono wake na shoka ili kukata mti, likatoka shoka katika mpini, likampiga yule mwenziwe hata akafa; basi na akimbilie katika majiji haya mojapo awe hai.’ (Kumbukumbu la Torati 19:4, 5) Hata kama ulienda katika jiji la makimbilio, huwezi kukosa kuwa na madaraka yote juu ya kile kilichotendeka.
12. Ni utaratibu gani ambao ungefuatwa baada ya muuaji asiyekusudia kufika jiji la makimbilio?
12 Ingawa ulikaribishwa vizuri, ilikuwa lazima ueleze wazee hali yako katika lango la jiji la makimbilio. Baada ya kuingia katika jiji, ungerudishwa kwa kesi mbele ya wazee wanaowakilisha kutaniko la Israeli kwenye malango ya jiji linalosimamia mahali pa mauaji. Huko ungepata fursa ya kuthibitisha kwamba huna hatia.
Wauaji Walipokuwa Kesini
13, 14. Ni yapi baadhi ya mambo ambayo wazee wangetaka kuhakikisha katika kesi ya muuaji?
13 Wakati wa kesi mbele ya wazee kwenye lango la jiji linalosimamia eneo hilo, bila shaka ungeona kwa shukrani kwamba mwenendo wako wa zamani ulitiliwa mkazo mwingi. Wazee wangepima kwa uzito uhusiano wako na yule aliyeuawa. Je, ulimchukia huyo mtu, ukamwotea, na kumpiga kimakusudi hadi akafa? Ikiwa ndivyo, wazee watalazimika kukutoa kwa mlipiza kisasi cha damu, nawe ungekufa. Wanaume hawa wenye madaraka wangejua takwa la Sheria kwamba ‘hatia ya damu isiyo na makosa iondolewe katika Israeli.’ (Kumbukumbu la Torati 19:11-13, NW) Kwa kulinganisha, katika tendo la kihukumu leo, wazee Wakristo wahitaji kujua Maandiko vema, wakitenda kwa kupatana nayo huku wakifikiria mtazamo na mwenendo wa awali wa mtenda-makosa.
14 Wakiuliza maswali kwa upole, wazee wa jiji wangetaka kujua ikiwa ulimnyemelea yule aliyeuawa. (Kutoka 21:12, 13) Je, ulimshambulia kutoka mahali pa kujificha? (Kumbukumbu la Torati 27:24) Je, uliwaka hasira dhidi yake hivi kwamba ukafanya mbinu fulani ya hila ya kumuua? Ikiwa ndivyo, ungestahili kifo. (Kutoka 21:14) Hasa wazee wangehitaji kujua kama kumekuwa na uadui, au chuki, kati yako na yule mtu aliyeuawa. (Kumbukumbu la Torati 19:4, 6, 7; Yoshua 20:5) Tuseme wazee walipata kwamba huna hatia na kukurudisha jiji la makimbilio. Ungekuwa mwenye shukrani kama nini kwa sababu ya rehema uliyoonyeshwa!
Maisha Katika Jiji la Makimbilio
15. Muuaji asiyekusudia aliwekewa matakwa gani?
15 Muuaji asiyekusudia alilazimika kubaki ndani ya jiji la makimbilio au kutoenda umbali wa dhiraa 1,000 (karibu futi 1,450) nje ya kuta zalo. (Hesabu 35:2-4) Angevuka mpaka huo, angeweza kukutana na mlipiza kisasi cha damu. Katika hali hizo, mlipiza kisasi angemuua yule muuaji bila kuwa na hatia. Lakini yule muuaji hakufungwa minyororo au kufungwa gerezani. Akiwa mkazi wa jiji la makimbilio, ilikuwa lazima ajifunze biashara fulani, awe mfanyakazi, na kutumikia akiwa mshiriki afaaye wa jamii.
16. (a) Muuaji asiyekusudia alilazimika kubaki katika jiji la makimbilio kwa muda gani? (b) Kwa nini kifo cha kuhani mkuu kilifanya iwezekane kwa muuaji kuondoka jiji la makimbilio?
16 Muuaji asiyekusudia alipaswa kubaki katika jiji la makimbilio kwa muda gani? Labda kwa maisha yake yote. Kwani, Sheria ilisema: ‘Ilimpasa kukaa ndani ya jiji lake la makimbilio hata kifo chake kuhani mkuu; lakini kuhani mkuu atakapokwisha kufa huyo mwuaji atarudi aende nchi ya urithi wake.’ (Hesabu 35:26-28) Kwa nini kifo cha kuhani mkuu kingemruhusu muuaji asiyekusudia kuondoka jiji la makimbilio? Kuhani mkuu alikuwa mmojawapo watu mashuhuri zaidi katika taifa. Hivyo, kifo chake kingekuwa tukio kubwa sana hivi kwamba kingejulikana kotekote katika makabila yote ya Israeli. Hivyo wakimbizi wote katika majiji ya makimbilio wangerudi nyumbani mwao bila hatari ya walipiza kisasi wa damu. Kwa nini? Kwa sababu Sheria ya Mungu ilikuwa imeamuru kwamba fursa ya mlipiza kisasi cha damu ya kuua muuaji ilikwisha kwa kifo cha kuhani mkuu, na kila mtu alijua jambo hili. Ikiwa mtu wa ukoo angelipiza kisasi cha kifo baada ya tukio hilo, yeye angekuwa muuaji kimakusudi naye hatimaye angepata adhabu ya kuua kimakusudi.
Matokeo ya Kudumu
17. Ni matokeo gani ambayo yangeweza kutokea kwa sababu ya vikwazo vilivyowekewa muuaji asiyekusudia?
17 Ni matokeo gani ambayo yangeweza kutokea kwa sababu ya vikwazo vilivyowekewa muuaji asiyekusudia? Vilikuwa vikumbusha kwamba alikuwa amesababisha kifo cha mtu. Yaelekea kwamba sikuzote baada ya hapo angeona uhai wa binadamu kuwa mtakatifu. Isitoshe, hangeweza kusahau kwamba alikuwa ametendewa kwa rehema. Kwa kuwa alikuwa ameonyeshwa rehema, hakika angetaka kuwa mwenye rehema kwa wengine. Mpango wa majiji ya makimbilio pamoja na vikwazo vyao pia ulinufaisha watu kwa ujumla. Kwa njia gani? Ni lazima uliwakazia kwamba hawapaswi kuchukua ovyo-ovyo au kutojali uhai wa binadamu. Basi Wakristo wapaswa kukumbushwa juu ya uhitaji wa kuepuka hali za ovyo-ovyo ambazo huenda zikasababisha kifo cha kiaksidenti. Kisha pia, mpango wenye rehema wa Mungu wa majiji ya makimbilio wapaswa kutusukuma kuonyesha rehema ifaapo.—Yakobo 2:13.
18. Ni kwa njia zipi mpango wa Mungu wa majiji ya makimbilio ulikuwa na mafaa?
18 Uandalizi wa Yehova Mungu wa majiji ya makimbilio pia ulikuwa na mafaa katika njia nyinginezo. Watu hawakufanyiza vikundi vya kutoa adhabu vya kufuata muuaji wakidhani kwamba ana hatia kabla ya kufanyiwa kesi. Badala ya kufanya hivyo, wao walimwona kuwa hana hatia ya kuua kimakusudi, hata wakimsaidia apate usalama. Isitoshe, uandalizi wa majiji ya makimbilio ulikuwa tofauti kabisa na mipango ya sasa ya kufunga gerezani wauaji kimakusudi, ambamo wanategemezwa kifedha na umma na mara nyingi hugeuka kuwa wahalifu wabaya zaidi kwa sababu ya kushirikiana kwao na wakosaji wengine. Katika mpango wa jiji la makimbilio, haikuwa lazima kujenga, kudumisha, na kulinda magereza yenye thamani kubwa yaliyozingirwa kuta na kuwekewa vikingo vya chuma ambayo mara nyingi wafungwa hujaribu kutoroka. Ni kama muuaji alienda kutafuta “gereza” na kuishi humo kipindi cha muda uliowekwa. Alipaswa pia kufanya kazi, hivyo akifanya kitu chenye kufaidi wanadamu wenzake.
19. Ni maswali gani yanayozushwa kuhusu majiji ya makimbilio?
19 Kwa kweli, mpango wa Yehova wa majiji ya makimbilio ya Israeli ili kulinda wauaji wasiokusudia ulikuwa wa rehema. Uandalizi huo hakika uliendeleza staha kwa uhai. Hata hivyo, je, majiji ya kale ya makimbilio yalikuwa na maana yoyote kwa watu waishio katika karne ya 20? Je, tungekuwa wenye hatia ya damu mbele ya Yehova Mungu bila kutambua kwamba twahitaji rehema yake? Je, majiji ya makimbilio ya Israeli yana umaana wowote wa kisasa kwetu?
Ungejibuje?
◻ Yehova huonaje uhai wa binadamu?
◻ Mungu alifanya uandalizi gani wenye rehema kwa wauaji wasiokusudia?
◻ Muuaji alifikiaje jiji la makimbilio, naye alipaswa kubaki huko kwa muda gani?
◻ Ni matokeo gani ambayo yangeweza kutokea kwa sababu ya vikwazo vilivyowekewa muuaji asiyekusudia?
[Ramani katika ukurasa wa 12]
Majiji ya makimbilio ya Israeli yalikuwa katika sehemu zilizofaa
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
KEDESHI Mto Yordani GOLANI
SHEKEMU RAMOTHI
HEBRONI BEZERI