Shekemu—Lile Jiji Katika Bonde
KATIKATI kabisa ya nchi ambayo Mungu aliwachagulia watu wake, kati ya Mlima Ebali na Mlima Gerizimu, mlikuwa na jiji la Shekemu. Humo ndimo—karibu miaka elfu nne iliyopita—Yehova alimwahidi Abrahamu hivi: “Uzao wako nitawapa nchi hii.”—Mwanzo 12:6, 7.
Kwa kupatana na ahadi hiyo, Yakobo mjukuu wa Abrahamu alipiga kambi Shekemu, akajenga madhabahu aliyoita “Mungu, Mungu wa Israeli.” Labda Yakobo alichimba kisima katika eneo hili ili kuandalia familia yake na vikundi vyake maji, kisima ambacho karne nyingi baadaye kingejulikana kuwa “bubujiko la Yakobo.”—Mwanzo 33:18-20, NW kielezi-chini; Yohana 4:5, 6, 12.
Hata hivyo, si washiriki wote wa familia ya Yakobo walioonyesha bidii kwa ajili ya ibada ya kweli. Dina, bintiye, alitafuta waandamani miongoni mwa wasichana Wakanaani wa Shekemu. Dina, aliyekuwa angali kijana wakati huo, aliacha usalama wa mahema ya familia yake, akaanza kuzuru hilo jiji la karibu, na kufanya marafiki huko.
Wanaume vijana wa hilo jiji wangemwonaje bikira huyu kijana aliyezuru jiji lao kwa ukawaida—yaonekana akiwa bila mwandamani? Mwana wa mkuu “akamwona akamtwaa, akalala naye, akambikiri.” Kwa nini Dina alitafuta hatari kwa kushirikiana na Wakanaani wasio wenye adili? Je, ni kwa sababu alikuwa akihisi kwamba alihitaji ushirika wa wasichana wa umri wake mwenyewe? Je, alikuwa mwenye kichwa kigumu na mwenye kujitegemea sawa na baadhi ya ndugu zake? Soma simulizi la Mwanzo, na ujaribu kufahamu ule msononeko na aibu ambayo lazima Yakobo na Lea walihisi kwa sababu ya matokeo yenye kuhuzunisha ya ziara za binti yao huko Shekemu.—Mwanzo 34:1-31; 49:5-7; ona pia Mnara wa Mlinzi, Juni 15, 1985, ukurasa 31 (la Kiingereza).
Karibu miaka 300 baadaye, matokeo ya kupuuza miongozo ya kitheokrasi yalizuka mara nyingine tena. Katika Shekemu, Yoshua alipanga mojawapo ya makusanyiko ya kustahili kukumbukwa zaidi katika historia ya Israeli. Ebu iwazie mandhari katika hilo bonde. Watu zaidi ya milioni moja—wanaume, wanawake, na watoto—wa makabila sita ya Israeli wasimama mbele ya Mlima Gerizimu. Ng’ambo ya bonde karibu idadi iyo hiyo ya watu kutoka yale makabila mengine sita yasimama mbele ya Mlima Ebali.a Na huko chini, kando ya sanduku la agano na kati ya hayo matungamano mawili ya Waisraeli, wasimama makuhani na Yoshua. Ni mandhari iliyoje!—Yoshua 8:30-33.
Kwa umati huo mkubwa, hiyo milima miwili inatokeza hali tofauti sana ya uzuri na ukame. Miteremko ya juu ya Gerizimu yaonekana yenye mimea ya kijani kibichi na yenye rutuba, hali ile ya Ebali yaonekana hasa kuwa bila mimea na kame. Je, waweza kuhisi ule msisimuko huku Waisraeli wangojapo wakati Yoshua atakaposema? Kila mvumo watoa mwangwi mahali hapa palipo kama mahali pa michezo.
Katika ule muda wa saa nne hadi sita ambao Yoshua achukua ili kusoma ‘kitabu cha sheria ya Musa,’ watu pia wanashiriki. (Yoshua 8:34, 35) Yaonekana kwamba, wale Waisraeli mbele ya Gerizimu wasema Ameni! baada ya kila moja ya zile baraka, hali Ameni! ya wale walio mbele ya Ebali yakazia kila laana. Labda hali ya ukame ya Mlima Ebali yawakumbusha hao watu juu ya matokeo mabaya ya kutotii.
“Na alaaniwe amdharauye baba yake au mama yake,” aonya Yoshua. Kwa umoja, sauti zaidi ya milioni moja zaitikia: “Amina!” [“Ameni!” NW] Yoshua angojea itikio hilo lenye kunguruma lififie kabla ya kuendelea: “Na alaaniwe aondoaye mpaka wa jirani yake.” Mara nyingine tena yale makabila sita, yaliyoandamanwa na wakazi wengi watokao nchi nyingine, yapaaza sauti: “Amina!” (Kumbukumbu la Torati 27:16, 17) Ikiwa ungalikuwa huko, je, ungalipata wakati wowote kusahau mkutano huo uliofanywa kati ya hiyo milima? Je, uhitaji wa utii usingalikuwa umetiwa chapa isiyofutika akilini mwako?
Muda mfupi kabla ya kufa, miaka ipatayo 20 baadaye, Yoshua alilikusanya taifa mara nyingine tena huko Shekemu ili lipate kuimarisha azimio lalo. Aliweka mbele yalo chaguo ambalo ni lazima kila mtu afanye. “Chagueni hivi leo mtakayemtumikia,” akasema. “Lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA.” (Yoshua 24:1, 15) Kwa wazi, mikusanyiko hiyo yenye kuchochea imani katika Shekemu ilipenya moyoni. Kwa miaka mingi baada ya kifo cha Yoshua, Waisraeli waliiga kielelezo chake chenye uaminifu.—Yoshua 24:31.
Karne zipatazo 15 baadaye Yesu alipokuwa akipumzika chini ya kivuli cha Mlima Gerizimu, kulikuwa na mazungumzo ya kuchangamsha moyo. Akiwa amechoka kwa sababu ya safari ndefu, Yesu alikuwa ameketi kando ya bubujiko la Yakobo wakati mwanamke Msamaria alipokuja akiwa na mtungi wa maji. Huyo mwanamke alishangaa sana Yesu alipomwomba kinywaji, kwa kuwa licha ya kuongea na Wasamaria, Wayahudi hata hawakunywa kutoka vyombo vyao. (Yohana 4:5-9) Maneno ya Yesu yaliyofuata yalimshangaza hata zaidi.
“Kila mtu anayekunywa kutokana na maji haya atapatwa na kiu tena. Yeyote yule anywaye kutokana na maji ambayo hakika mimi nitampa hatapatwa na kiu hata kidogo, lakini maji ambayo hakika mimi nitampa yatakuwa katika yeye bubujiko la maji linalobubujika ili kutoa uhai udumuo milele.” (Yohana 4:13, 14) Ebu uwazie upendezi wa huyo mwanamke katika ahadi hiyo, kwa maana kuchota maji katika kisima hiki chenye kina kulikuwa kazi ya juhudi. Yesu akaendelea kueleza kwamba ujapokuwa umaana wapo wa kihistoria, wala Yerusalemu wala Mlima Gerizimu hapakuwa mahali muhimu pa kidini ili kumfikia Mungu. Mtazamo wa moyo na mwenendo, wala si mahali, ndio uliokuwa wa maana. ‘Waabudu wa kweli watamwabudu Baba kwa roho na kweli,’ akasema. “Kwa maana, kwa kweli, Baba anawatafuta wa namna hiyo wamwabudu yeye.” (Yohana 4:23) Lazima maneno hayo yalikuwa yenye kufariji kama nini! Mara nyingine tena bonde hilo likawa mahali ambapo watu walisihiwa sana kumtumikia Yehova.
Leo jiji la Nablus liko kando ya magofu ya Shekemu la kale. Mlima Gerizimu na Mlima Ebali ingali mikubwa katika bonde hilo, ikiwa imesimama kama mashahidi kimya wa mambo ya wakati uliopita. Kisima cha Yakobo, kilicho chini ya milima hiyo, chaweza kuzuriwa bado. Tutafakaripo mambo yaliyotukia huko, tunakumbushwa umaana wa kutegemeza ibada ya kweli, sawa na vile Yoshua na Yesu walivyotufundisha tufanye.—Linganisha Isaya 2:2, 3.
[Maelezo ya Chini]
a Yale makabila sita mbele ya Mlima Gerizimu yalikuwa Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari, Yusufu, na Benyamini. Yale makabila sita mbele ya Mlima Ebali yalikuwa Reubeni, Gadi, Asheri, Zebuloni, Dani, na Naftali.—Kumbukumbu la Torati 27:12, 13.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.