Yemeni-Nchi Inayoshangaza Sana
ILE Peninsula ya Uarabuni! Watu wafikiripo juu ya sehemu hii ya kipekee ya ulimwengu, mara nyingi wao huona vilima vya mchanga, ngamia, na misafara. Lakini ingawa sehemu kubwa ya eneo hili ina vilima vya mchanga vya jangwa na joto jingi zaidi, pia ina mambo mengine ambayo yaweza kukushangaza sana.
Kwa kielelezo, fikiria nchi ya Yemeni, ambayo ni bara lenye umbo la kiko cha mkono linalokabili Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden. Mbali na kuwa eneo kubwa la mchanga, Yemeni ni nchi ya milima na mabonde; nchi ya mizabibu, maembe-asali, na matunda mengineyo matamu; nchi ya usanii wa kustaajabisha. Ingawa joto kali la jangwa huchoma ukanda wa pwani wa Yemeni, huenda ukashangaa kujua kwamba kuna hali nzuri sana ya hewa katika milima yayo. Hata hivyo, jambo lenye kuwapendeza sana Wakristo ni historia yayo yenye mambo mengi—historia inayoanzia nyakati za Biblia.
Njia ya Ubani
Katika nyakati za kale sehemu hii ya Ulimwengu ilipata utajiri mwingi kupitia tu mambo ya asili—zile pepo za daima za Bahari ya Hindi zilizopeleka unyevu katika ukanda wa pwani wa kusini mwa Arabia. Pepo hizo zenye kujaa unyevu zilisaidia kuweka hali nzuri ya kukuza aina ya mti msandarusi wenye gome lenye kutokeza utomvu wa sandarusi uitwao ubani.a Ukifukizwa, ubani hutoa manukato, jambo linalofanya upendwe zaidi katika sherehe za kidini. Ile nchi inayoitwa Yemeni wakati huu ilikuja kuwa maarufu katika biashara ya ubani.
Huenda ikawa Yemeni ilikuwa pia mahali pa Ofiri ya kale—ambayo wakati mmoja ulikuwa chanzo cha dhahabu bora zaidi. (Ayubu 22:24; 28:15, 16; Zaburi 45:9) Iwe Ofiri ilikuwa huko ama la, Yemeni ilikuwa katikati ya njia za misafara ya kale ya ngamia yenye kubeba dhahabu, ubani, na vikolezo kutoka sehemu za mbali, kama vile Palestina na Tiro za kale. (Ezekieli 27:2, 22-25) Hilo lilileta utajiri mwingi kwa wafanya biashara wenyewe na vilevile kwa falme kadhaa zilizokuwa kandokando za njia na ambazo zilitoza kodi misafara iliyokuwa ikipita.
Ule ufalme wa Sheba, ambao uliaminiwa kuwa ulikuwa katika ile sehemu ambayo sasa ni mashariki mwa Yemeni, ulikuja kudhibiti njia hiyo ya msafara. Ufalme huo wa Sheba ulikuja kuwa maarufu katika biashara ya ubani, manemane, dhahabu, vito, na pembe za ndovu. (Isaya 60:6) Katika siku za Sulemani, malkia wa Sheba alisafiri kutoka “pande za mwisho za dunia” ili asikie mwenyewe hekima ya mfalme. (Mathayo 12:42) Kulingana na masimulizi ya Biblia, alienda Yerusalemu akiwa na “wafuasi wengi sana, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani.” (1 Wafalme 10:1, 2) Wayemeni wengi leo bado hukumbuka malkia huyo wa kale. Ingawa hatajwi katika Koran, mapokeo ya Kiislamu yamwita Bilqīs—jina linaloonekana kwenye bidhaa nyingi zinazotengenezwa nchini Yemeni.
Karne Nyingi za Kupoteza Umaarufu
Kwa karne nyingi Yemeni ilifurahia utajiri mwingi, kiasi cha kwamba Warumi waliipa jina la Kilatini Arabia felix, au “Arabia Yenye Furaha.” Lakini Warumi walipofanya Ukristo wa uasi-imani kuwa dini ya Taifa, haja ya ubani ilikwisha. Jambo lililofanya Yemeni ianguke zaidi lilikuwa ni kubomoka kwa bwawa kubwa sana katika Marib kulikoleta msiba mkubwa—kitovu cha mfumo mkubwa mno wa unyweshaji mashamba kilichokuwa kimenywesha sehemu hiyo tangu karne ya nane K.W.K.
Yemeni ilikuja kupata umaarufu wa muda kwa sababu ya kupendwa kwa bidhaa nyingine tena—kahawa. Karibu 1610 Wazungu waligundua yale manukato na ladha nzuri ya mbegu hizo za kipekee kutoka milima ya Yemeni. Lile jiji la Mocha lililoko sehemu ya mwisho ya kusini mwa Bahari Nyekundu lilikuja kuwa bandari kuu ya kusafirishia kahawa. Jina “Mocha” likaja kuhusiana sana na kahawa ya Arabia na likaja kujulikana sana katika Kizio cha Kaskazini.
Lakini haikuchukua muda mrefu kabla ya mibuni (miti ya kahawa) kusafirishwa nchi nyinginezo na kukuzwa huko kwa mafanikio. Matokeo yakawa kwamba jiji la Mocha likaanza kupoteza umaarufu. Ingawa kahawa ingali bidhaa kuu ya Yemeni ya kusafirishwa nje, leo jiji la Mocha ni bandari tu ya uvuvi.
Kutazama Jiji Kuu la Yemeni
Ingawa utukufu walo wa zamani umepotea polepole, Yemeni ingali ina mambo ya kusisimua na yenye kushangaza sana. Jiji kuu, San‘a, liko kwenye uwanda wa juu sana wa kimo zaidi ya meta 2,000, likifurahia halijoto ya wastani yenye kupendeza. Wengi wa wakazi milioni 12 wa Yemeni—ambao ni theluthi moja ya idadi yote ya Arabia—huishi katika uwanda huo wa juu na kwenye milima mingi iliyoko kotekote nchi hiyo bali si katika jangwa lenye joto jingi sana.
San‘a limekuwapo kwa miaka elfu moja, mambo yalo ya kale yakionekana wazi katika miundo ya majengo yalo. Majengo ya mawe yana mapambo ya mistari-mistari ya chokaa kandokando ya madirisha, matao yenye viunzi, na vioo vyenye rangi nyingi zilizochorwa kama vigae. Katika sehemu fulani za mji, majengo ya kale na mapya yamejengwa upande kwa upande, yakiwa magumu zaidi kutofautishwa. Lakini katika vichochoro vya mji wa kale wa San‘a, majengo—mengine yakiwa na orofa nane au zaidi—ambayo yamekuwapo kwa karne kadhaa yaweza kuonwa.
Ukitoka mji wa kale wa San‘a, utapitia lile lango kubwa la kale la jiji na kuzungukazunguka katika sehemu za mashambani zenye milima-milima. Vikiwa na minara-mviringo yenye vina vya orofa nne au zaidi na kuwa na kuta za ulinzi ambazo zilijengwa bila simiti wala chokaa, kila kijiji huonekana kama ngome kubwa iliyojengwa kando ya mlima. Kwa kweli, baadhi ya vijiji hivyo hufanana sana na mazingira yavyo hivi kwamba vyaweza kuonwa tu kwa ukaribu sana.
Mtu anaweza kushangaa kwamba watu waweza kuishi katika miinuko ya juu kadiri hiyo. Lakini atazamapo juu zaidi, aona vijiji vingine vingi vikiwa katika miinuko ya juu zaidi. Mitelemko yenye ukuta katika sehemu zilizoinuka sana huzunguka vijiji hivi vya milimani.
Wayemeni
Wageni wanaotoka nchi za Magharibi hutarajia kupata Wayemeni kuwa watu wa ajabu. Lakini kwa kweli wao ni watu wa ajabu hata zaidi ya mataraja hayo. Watu wa makabila ya milimani huenda wakaonekana kuwa wakali sana kwa mara ya kwanza. Wao huvaa fuuta, ambayo ni kikoi, na mshipi mpana ambao hubeba jambia inayoonekana waziwazi. Katika vijiji watu wengi hata hubeba bunduki kubwa za kumimina-risasi mabegani mwao.
Naam, wanaume wa Yemeni huzionea fahari sana silaha zao. Sehemu kubwa-kubwa za sokoni hutengwa kwa uuzaji wa jambiyya, au jambia. Kwa kawaida jambia hubebwa na wavulana wa miaka 14 na zaidi ikiwa wonyesho wa kwamba wamekuwa wanaume. Hata hivyo, hata wavulana wadogo waweza kuonwa wakiwa nazo. Vishikio vya jambia vyaweza kutengenezwa kwa plastiki, mbao, au pembe ya kifaru yenye bei ghali sana, na mara nyingi ala ya jambia hupambwa kimaridadi kwa madini ya fedha. Jambia yenyewe huwa kali sana. Kwa uzuri, majisu hayo hutumika mara nyingi yakiwa maridadi tu. Kwa hakika wanaume wa Yemeni ni wakaribishaji sana na wao huthamini jaribio lolote la mgeni kuzungumza nao.
Kwa maoni ya mtu kutoka nchi za Magharibi, wanawake wa Yemeni ni wa ajabu vilevile. Wao huvaa mavazi meusi nao hufunikwa kabisa, hata na macho yao. Hawana maisha rahisi. Katika vijiji vya milimani, wanawake hufanya kazi ngumu kwa muda mrefu wakibeba maji, chakula cha mifugo, na kuni. Familia kubwa-kubwa hufuata desturi.
Ukizuru masoko utaona jinsi watu hao wa kustaajabisha waishivyo. Maduka ya vikolezo yana manukato sana. Mate humdondoka mtu anapoona makomamanga, maembe-ulaya, maembe-asali, zabibu, na lozi. Mafundi wanakuwa na shughuli nyingi wakifanya kazi za ngozi, dhahabu, madini ya fedha, na vyuma vingine.
Waweza pia kupata suq, au masoko kadhaa katika soko kubwa, yanayouza miraa. Inapotafunwa au kufyonzwa, miraa huchochea mwili kidogo; watu wengine husema kwamba hiyo huleta uzoelevu. Hali iwe nini, kutafuna miraa ni sehemu kubwa ya maisha ya Wayemeni. Sehemu kubwa za kandokando za milima zinatumiwa kukuza miraa. Vikundi vya wanaume vitatafuna miraa kwa muda mrefu huku wakifurahia mazungumzo. Watu wengine pia hutafuna miraa wanapofanya kazi—hata wanapoendesha gari.
Hata hivyo, kutafuna miraa kunagharimu sana, ikigharimu kufikia theluthi moja ya mapato ya familia ya Wayemeni. Na baadhi ya watu wanataja hatari za kiafya, kutia ndani kuharibika kwa umbo la shavu, kupata matatizo ya usingizi na kukosa hamu ya chakula, na magonjwa ya tumbo. Kwa hiyo maofisa fulani wa serikali wameshutumu dawa hiyo ya kulevya. Lakini kufikia sasa, hakuna ishara kubwa kwamba Wayemeni wanaacha kutumia miraa.
Lakini, kuna uthibitisho kwamba maisha ya kidesturi yanaanza kupotezwa na umamboleo wa Magharibi. Wanaume wengi wameenda nchi za nje kufanya kazi. Familia nyinginezo zimehamia majijini, jambo linalohatarisha vijana kwa uvutano wa muziki ulioingizwa nchini na vidio za kigeni. Inaeleweka kwamba si wote wanaopenda kuona nchi yao ikigeuka kuwa ya ulimwengu wa kisasa.
Kwa hiyo itakuwa jambo la kupendeza kuona wakati ujao wa nchi hii utakavyokuwa. Ni uchimbuzi mdogo tu ambao umefanywa katika kuvumbua magofu ya kale ya nchi hii, na labda uchimbuzi wa wakati ujao utagundua siri nyinginezo zenye kustaajabisha za wakati uliopita wa Yemeni uliokuwa maarufu sana. Kwa wakati huu, kuna sababu nyingi za kufanya msafiri mwenye kujasiri azuru nchi hii ya Yemeni inayoshangaza sana.—Imechangwa.
[Maelezo ya Chini]
a Hii ni aina ya miti ya Boswellia, ambayo ni jamii ya miti inayohusiana na miti ya tapentini, au terebinthi.
[Picha katika ukurasa wa 24, 25]
Bab-el-Yemeni, lango la San‘a kwenye mji wa kale
[Picha katika ukurasa wa 26]
Kulia: Soko la jambia katika San‘a
[Picha katika ukurasa wa 26]
Chini: Miji midogo hufanana sana na mazingira yayo