Mandhari Kutoka Bara Lililoahidiwa
Kwenda Shilo Watoto Wema na Wabaya
UNAPOFIKIRI juu ya majiji, miji, au maeneo ya Bara Lililoahidiwa, je, wanaume na wanawake fulani mashuhuri huja akilini mwako? Labda ndivyo, kwani masimulizi mengi ya Kibiblia huhusisha watu wazima. Lakini namna gani watoto wa wakati huo? Je! wewe huwawazia katika mandhari hizo?
Mandhari iliyo juu yaweza kutusaidia kukazie fikira masimulizi yanayohusisha vijana, baadhi yao ambao walikuwa vielelezo vizuri kwa Wakristo na baadhi yao ambao walikuwa vielelezo vya kuonya. Kile kilima cha mviringo katikati yaelekea ndipo lilipokuwa Shilo.a
Yaelekea unakumbuka kwamba Israeli walipoingia Bara Lililoahidiwa, waliweka tabenakulo ya Mungu kwanza katika Gilgali karibu na Yeriko. (Yoshua 4:19) Lakini bara hilo lilipokuwa likigawanywa, hema hilo takatifu—mahali pakuu pa ibada ya Israeli—lilihamishwa huku Shilo. (Yoshua 18:1) Mahali hapo palikuwa karibu kilometa 30 kaskazini mwa Yerusalemu katika jimbo lenye milima la Efraimu. Wanaume na wanawake kutoka kotekote Israeli walisafiri hadi Shilo; vikundi vya watu viliweza kukusanyika katika bonde lililokuwa kusini mwa mahali ambapo yaelekea hiyo tabanekulo ilikuwa. (Yoshua 22:12) Je! wewe waweza kuwazia watoto wakija huku?
Wengine walikuja. Kielelezo mashuhuri zaidi tunachopaswa kujua juu yacho ni kile cha Samweli mchanga. Wazazi wake, Elkana na Hana, waliishi katika mji uliokuwa ng’ambo ya vilima vilivyo upande wa magharibi. Kila mwaka walisafiri huku, labda wakiwaleta baadhi ya watoto wa mke yule mwingine wa Elkana. Mwishowe Yehova alimbariki Hana kwa kumpa mwana, aliyeitwa Samweli. Baadaye wazazi wake walimleta aishi Shilo ili aweze kutumika kwenye tabenakulo pamoja na kuhani mkuu Eli.—1 Samweli 1:1–2:2:11.
Mvulana huyo alikuwa na kazi za kikawaida za kufanya kwenye nyumba ya Mungu, na ni lazima iwe alikuwa na nafasi nyingi za kutembea-tembea katika vilima vya karibu. (1 Samweli 3:1, 15) Baadhi yavyo vilikuwa na matuta na kujaa mizeituni, kama ionekanavyo katika picha kwenye kurasa 9. Angalia ule mnara mdogo wa mawe. Wakulima au wachungaji walio peke yao wangeweza kuchunga kutoka kwa mnara wa jinsi hiyo, lakini waweza kuwazia Samweli mchanga akipanda ili aweze kutazama pia. (Linganisha 2 Mambo ya Nyakati 20:24.) Hapo pangekuwa mahali pazuri pa kulinda kwa ajili ya wanyama wa pori.
Wakati huo, kulikuwako miti mingi kuliko sasa, hata misitu ambamo wanyama wa pori walizunguka-zunguka. (Yoshua 17:15, 18) Twajua hilo kutokana na kisa kilichotukia wakati Elisha alipokuwa amekwisha kuwa nabii mkuu wa Mungu. Elisha alikuwa akisafiri akipanda kutoka Yeriko kuelekea Betheli, kwa hiyo alikuwa katika eneo hili, karibu kilometa 16 kusini mwa Shilo. Yeye angalipokewaje na watu wa Betheli, iliyokuwa imekuwa kitovu cha ibada ya ndama wa dhahabu? (1 Wafalme 12:27-33; 2 Wafalme 10:29) Yaonekana kwamba watu wazima walimpinga nabii wa Yehova, na mtazamo wao yaonekana uliwaathiri wazao wao pia
Wafalme wa Pili 2:23, 24 hutuambia kwamba kikundi cha vijana walimfanyia mzaha nabii wa Mungu hivi: “Paa wewe mwenye upaa! Paa wewe mwenye upaa!” Kwa kuitikia, Elisha “akawalaani kwa jina la BWANA [Yehova, NW]. Wakatoka dubu wawili wa kike mwituni, wakawararua vijana arobaini na wawili miongoni mwao.” Dubu hao wa Siria wa rangi kahawia wangeweza kuwa wakali sana waliposhtushwa au wakati ilipoonekana vitoto vyao vilitishwa. (2 Samweli 17:8; Mithali 17:12; 28:15) Mungu aliwatumia watekeleze hukumu ya kimungu dhidi ya wale waliodharau sana mwakilishi wake na hivyo kumdharau Yehova mwenyewe.
Jambo la kwamba mtoto angeweza kukutana na wanyama wa porini katika vilima vilivyozunguka Shilo lapaswa kutusaidia tuthamini zaidi imani ambayo wazazi wa Samweli walionyesha katika kumleta akatumike kwenye tabenakulo.
Mwabudu mwingine wa kweli alikuwa ameonyesha mapema zaidi imani na ujitoaji huohuo—Mwamuzi Yeftha. Aliishi katika eneo la Gileadi lenye vilima upande wa mashariki wa Yordani. Akiwa na bidii kwa ajili ya Yehova dhidi ya Waamoni waliokuwa maadui, Yeftha alitoa nadhiri kwamba wa kwanza wa nyumba yake aliyetoka kumpokea angetolewa dhabihu kwa Yehova. Binti yake bikira alithibitika kuwa mtu huyo. Kwa hiyo alimleta mtoto wake wa pekee kwenye patakatifu pa Mungu katika Shilo, alikoishi mtoto huyo na kutumika kwa uaminifu kwa miaka mingi.—Waamuzi 11:30-40.
Ujitoaji mwaminifu ambao Samweli na binti ya Yeftha walionyesha katika eneo la Shilo kwa hakika ni tofauti nzuri kwa kulinganishwa na kile kielelezo kisichofaa cha wale watoto watundu 42 waliomfanyia mzaha nabii wa Yehova katika eneo lilo hilo.—Linganisha 1 Wakorintho 10:6, 11.
[Picha katika ukurasa wa 7]
a Kwa picha kubwa zaidi, ona 1992 Calender of Jehovah’s Witnesses.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 8]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 9]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 9]
Safari Zoo, Ramat-Gan, Tel Aviv