Yerusalemu Katika Nyakati za Biblia—Akiolojia Yafunua Nini?
UTENDAJI mbalimbali wenye kupendeza wa kiakiolojia umetukia katika Yerusalemu, hasa tangu mwaka wa 1967. Mahali pengi palipochimbuliwa sasa paonekana wazi na watu wote, kwa hiyo acheni tutembelee baadhi yapo tuone jinsi ambavyo akiolojia hufaana na historia ya Biblia.
Yerusalemu la Mfalme Daudi
Sehemu ambayo Biblia hurejezea kuwa Mlima Zayoni, ambapo Jiji la Daudi la kale lilijengwa, huonekana kuwa isiyo na maana ikilinganishwa na makao makuu ya Yerusalemu la kisasa. Uchimbuaji wa Jiji la Daudi, ulioongozwa na hayati profesa Yigal Shiloh kati ya mwaka wa 1978-1985, ulifunua muundo wa jiwe, au ukuta wenye kutegemeza, upande wa mashariki wa kilima.
Profesa Shiloh alidai kwamba lazima uwe mabaki ya ngazi kubwa sana za mawe zilizoegemea ardhi iliyoinama, hivyo kufanyiza msingi ambao juu yao Wayebusi (wakazi kabla ya ushindaji wa Daudi) walijenga husuni. Alieleza kwamba huo muundo wa jiwe alioupata juu ya ngazi hizo za mawe ulikuwa wa ngome mpya iliyojengwa na Daudi mahali pa husuni ya Wayebusi. Kwenye 2 Samweli 5:9, twasoma: “Daudi akakaa ndani ya ngome hiyo, akaiita mji wa Daudi. Kisha Daudi akajenga toka Milo na pande za ndani.”
Karibu na muundo huo kuna miingilio ya mifumo ya kale ya maji ya jiji, ambayo sehemu zayo zaonekana kuwa ni za toka wakati wa Daudi. Baadhi ya taarifa zilizo katika Biblia juu ya mfumo wa mfereji wa maji wa Yerusalemu zimezusha maswali. Mathalani, Daudi aliwaambia wanaume wake kwamba “yeye atakayewapiga Wayebusi, na apande kwenye mfereji wa maji, [na akutane]” na adui. (2 Samweli 5:8) Yoabu kamanda wa Daudi alifanya hivyo. Msemo “mfereji wa maji” wamaanisha nini hasa?
Maswali mengine yamezushwa juu ya Mtaro wa Siloami unaojulikana sana, yamkini ulichimbwa na mafundi wa mitambo wa Mfalme Hezekia katika karne ya nane K.W.K. na warejezewa kwenye 2 Wafalme 20:20 na 2 Mambo ya Nyakati 32:30. Je, vikundi hivyo viwili vya wachimba-mitaro, kutoka pande mbalimbali kabisa, vingewezaje kukutana? Kwa nini walichagua kijia chenye kupindika-pindika, kikifanya mtaro uwe mrefu sana kuliko kuwa ulionyooka? Walipataje hewa ya kutosha ya kupumua, hasa kwa kuwa yamkini wangetumia taa za mafuta?
Gazeti Biblical Archaeology Review limetoa majibu yawezayo kukubalika kwa maswali hayo. Dan Gill, mwanajiolojia-mwelekezi wa uchimbuaji huu, anukuliwa akisema: “Sehemu ya chini ya Jiji la Daudi kuna mfumo uliositawi vizuri wa karst ya asili. Neno karst ni la kijiolojia linalofafanua eneo lisilo la kawaida la mashimo, mapango na mifereji inayosababishwa na maji ya chini ya ardhi yanapopenya na kutiririka kupitia miundo ya miamba ya chini ya ardhi. . . . Uchunguzi wetu wa kiakiolojia wa mifumo ya maji ya chini ya ardhi iliyo chini ya Jiji la Daudi waonyesha kwamba ilifanyizwa kimsingi na binadamu kwa kutanua kwa ustadi mifereji (karstic) ya asili iliyosababishwa na mmomonyoko na mashimo ambayo yaliunganishwa kuwa mifumo ya ugawaji-maji yenye kufaa kazi.”
Huenda hilo likasaidia kueleza jinsi Mtaro wa Siloami ulivyochimbwa. Ungaliweza kufuatia mwendo uliopindika-pindika wa mfereji wa asili chini ya kilima. Vikundi vilivyokuwa vikifanya kazi kutoka kila upande vingalichimba mtaro wa muda tu kwa kubadili mapango ya ardhini yaliyokuwapo. Kisha mfereji wenye kuteremka ulichimbwa ili maji yatiririke kutoka chemchemi ya Gihoni hadi Kidimbwi cha Siloami, ambacho labda kilikuwa ndani ya kuta za jiji. Huo ulikuwa ufundi wa mitambo wenye uhodari kwelikweli kwa kuwa tofauti ya kimo kati ya pande hizo mbili ni sentimeta 32 tu licha ya urefu wake wa meta 533.
Kwa muda mrefu wasomi wametambua kwamba chanzo kikuu cha maji ya jiji la kale kilikuwa chemchemi ya Gihoni. Kilikuwa nje ya kuta za jiji lakini karibu vya kutosha kuruhusu mtaro na shimo lenye urefu wa meta 11 kuchimbuliwa, ambao ungewezesha wakazi wachote maji bila kwenda nje ya kuta zenye kinga. Hilo lilijulikana kuwa Warren’s Shaft, likiitwa kwa jina la Charles Warren ambaye alivumbua mfumo huo katika mwaka wa 1867. Lakini mtaro na shimo vilifanyizwa lini? Je, vilikuwako wakati wa Daudi? Je, mtaro huu wa maji ulitumiwa na Yoabu? Dan Gill hujibu: “Ili kujaribu kama Warren’s Shaft lilikuwa kwa hakika shimo la asili, tulichunguza ganda la kipande cha chokaa kutoka kuta zalo zisizo laini ili kupata carbon-14. Halikuwa na kitu, hilo likionyesha kwamba ganda hilo lina miaka zaidi ya 40,000: Hilo latoa uthibitisho ulio wazi kwamba hilo shimo halingaliweza kuwa lilichimbwa na mwanadamu.”
Mabaki Kutoka Wakati wa Hezekia
Mfalme Hezekia aliishi wakati taifa la Ashuru lilipokuwa likishinda kila kitu njiani mwalo. Katika mwaka wa sita wa utawala wake, Waashuri walishinda Samaria, jiji kuu la ufalme wenye makabila kumi. Miaka minane baadaye (732 K.W.K.) Waashuri walirudi tena, wakitisha Yuda na Yerusalemu. Kitabu cha Mambo ya Nyakati cha Pili 32:1-8 hufafanua mkakati wa kujihami wa Hezekia. Je, kuna vithibitisho vyovyote vyenye kuonekana kutoka kipindi hiki?
Ndiyo, katika mwaka wa 1969 Profesa Nahman Avigad alivumbua mabaki kutoka kipindi hiki. Uchimbuaji ulionyesha sehemu ya ukuta mkubwa sana, sehemu ya kwanza ikiwa na urefu wa meta 40, upana wa meta 7, na, kulingana na makadirio kimo cha meta 8 juu. Ukuta ulisimama kwa sehemu juu ya msingi wa mwamba na kwa sehemu juu ya nyumba mpya zilizobomolewa. Ni nani aliyejenga ukuta huo na lini? “Mafungu mawili katika Biblia yalisaidia Avigad kuonyesha tarehe na kusudi la huo ukuta,” gazeti la kiakiolojia laripoti. Mafungu hayo yasomeka hivi: “Akapiga moyo konde, akaujenga ukuta wote uliobomoka, akauinua sawa na minara, na ukuta wa pili nje.” (2 Mambo ya Nyakati 32:5) “Mkazibomoa nyumba ili kuutia nguvu ukuta.” (Isaya 22:10) Leo wageni wanaweza kuona sehemu ya huu yenye kuitwa kwa kawaida Ukuta Mpana katika Jewish Quarter ya Old City.
Uchimbuaji mbalimbali pia waonyesha kwamba Yerusalemu wakati huo lilikuwa jiji kubwa zaidi kuliko lilivyokuwa limefikiriwa hapo awali, labda kwa sababu ya kumiminika kwa wakimbizi kutoka ufalme wa kaskazini baada ya kushindwa na Waashuri. Profesa Shiloh alikadiria kwamba jiji la Yebusi lilikuwa na eneo lipatalo hekta sita hivi. Wakati wa Solomoni lilikuwa na mweneo wa karibu hekta 16. Kufikia wakati wa Mfalme Hezekia, miaka 300 baadaye, sehemu iliyoimarishwa ya jiji hilo iliongezeka hadi hekta zipatazo 60 hivi.
Makaburi ya Kipindi cha Hekalu la Kwanza
Makaburi ya kipindi cha Hekalu la Kwanza, yaani, kabla ya Wababiloni kuharibu Yerusalemu katika 607 K.W.K., yamekuwa chanzo kingine cha habari. Mavumbuzi yenye kustaajabisha yalifanywa wakati kikundi cha mapango ya kuzikia kwenye miteremko ya Bonde la Hinnomu yalipochimbuliwa katika mwaka wa 1979 na wa 1980. “Katika historia yote ya akiolojia ya utafiti katika Yerusalemu, hayo ni mojawapo ya makumbusho machache sana ya Hekalu la Kwanza kupatikana na vitu vyayo vyote vikiwamo. Yalikuwa na vitu zaidi ya elfu moja,” asema mwakiolojia Gabriel Barkay. Yeye aendelea hivi: “Tumaini kubwa la kila mwakiolojia anayefanya kazi Israeli, na hasa Yerusalemu, ni kuvumbua habari iliyoandikwa.” Hatikunjo mbili za fedha zilipatikana, zikiwa na nini?
Barkay aeleza: “Nilipoona kipande cha fedha kisichokunjwa na kukiweka chini ya kiookuzi, ningeweza kuona kwamba uso wacho ulifunikwa na herufi zilizofanywa kwa uangalifu sana, ambazo ziliandikwa kwa kifaa kikali juu ya shiti ya fedha iliyo rahisi kuharibika. . . . Jina la Mungu ambalo huonekana wazi katika huo mwandiko lina herufi nne za Kiebrania zilizoandikwa katika maandishi ya Kiebrania cha kale, yod-he-waw-he.” Katika kichapo cha baadaye, Barkay aongeza hivi: “Kwa mshangao wetu mabamba yote mawili ya fedha yaliandikwa yakiwa na virai vya dua ambavyo karibu vyafanana na zile Baraka za Kikuhani za kibiblia.” (Hesabu 6:24-26) Hiyo ilikuwa ndiyo mara ya kwanza ambayo jina la Yehova lilipatikana katika mwandiko uliovumbuliwa katika Yerusalemu.
Wasomi waliamuaje tarehe ya hatikunjo hizo za fedha? Hasa kwa muktadha wa kiakiolojia ambamo zilivumbuliwa. Zaidi ya vipande 300 vya udongo wa mfinyanzi viwezavyo kupewa tarehe vilipatikana katika hayo makumbusho, vikielekeza hadi karne ya saba na ya sita K.W.K. Hayo maandishi, yanapolinganishwa na miandiko mbalimbali iliyo na tarehe, huonyesha kwamba ni ya tangu kipindi hichohicho. Hatikunjo hizo zimeonyeshwa katika Israel Museum katika Yerusalemu.
Uharibifu wa Yerusalemu Katika 607 K.W.K.
Biblia husema kuhusu uharibifu wa Yerusalemu katika mwaka wa 607 K.W.K. katika 2 Wafalme sura ya 25, 2 Mambo ya Nyakati sura ya 36, na Yeremia sura ya 39, ikiripoti kwamba jeshi la Nebukadreza lilichoma moto jiji hilo. Je, uchimbuaji wa juzijuzi umethibitisha simulizi hilo la kihistoria? Kulingana na Profesa Yigal Shiloh, “uthibitisho wa [uharibifu wa Babiloni katika Biblia . . . umekamilishwa na uthibitisho dhahiri kabisa wa kiakiolojia; uharibifu kamili wa majengo mbalimbali, na pambano ambalo liliharibu sehemu mbalimbali za mbao za nyumba hizo.” Yeye alieleza zaidi hivi: “Dalili za uharibifu huo zimepatikana katika kila ya uchimbuaji uliofanywa Yerusalemu.”
Wageni wenye kuzuru wanaweza kuona mabaki kutokana na uharibifu huo uliotukia zaidi ya miaka 2,500 iliyopita. Majina Israelite Tower, Burnt Room, na Bullae House ni ya mahali mbalimbali pa kiakiolojia penye kujulikana sana palipohifadhiwa na kuwekwa wazi kwa ajili ya watu wote. Mwakiolojia Jane M. Cahill na David Tarler walifanya muhtasari katika kitabu Ancient Jerusalem Revealed: “Uharibifu mkubwa zaidi wa Yerusalemu uliofanywa na Wababiloni uko wazi si katika safu kubwa za mabaki yaliyochomeka ambayo hayajafukuliwa katika majengo kama vile Burnt Room na Bullae House tu, bali pia katika kifusi cha jiwe kutoka majengo yaliyoporomoka kilichopatikana kimefunika mteremko wa mashariki. Ufafanuzi wa kibiblia wa uharibifu wa jiji hilo . . . unakamilisha uthibitisho wa kiakiolojia.”
Hivyo, picha ya Biblia ya Yerusalemu kutoka wakati wa Daudi hadi uharibifu katika mwaka wa 607 K.W.K. katika njia nyingi umethibitishwa na uchimbuaji wa kiakiolojia uliofanywa wakati wa miaka 25 iliyopita. Lakini vipi Yerusalemu la karne ya kwanza W.K.?
Yerusalemu Katika Siku ya Yesu
Uchimbuaji, Biblia, mwanahistoria Myahudi wa karne ya kwanza Josephus, na vyanzo vingine husaidia wasomi waone Yerusalemu la siku ya Yesu, kabla ya Waroma kuliharibu katika mwaka wa 70 W.K. Kigezo kimoja, kinachoonyeshwa nyuma ya hoteli moja kubwa katika Yerusalemu, hufanywa upya kwa ukawaida kulingana na yale ambayo uchimbuaji mpya hufunua. Sehemu kuu ya jiji hilo ilikuwa jengo la Temple Mount, ambalo Herode alilifanya liwe maradufu likilinganishwa na lile la wakati wa Solomoni. Lilikuwa ndilo jukwaa kubwa zaidi lililotengenezwa na watu katika ulimwengu wa kale, karibu meta 480 hivi kwa meta 280. Baadhi ya mawe ya kujengea yalikuwa na uzito wa tani 50, moja hata likiwa na tani karibu 400 na “lisilolinganika katika ukubwa kokote katika ulimwengu wa kale,” kulingana na msomi mmoja.
Si ajabu kwamba watu fulani walishtuka walipomsikia Yesu akisema: “Vunjeni hekalu hili, na hakika katika siku tatu nitaliinua.” Walifikiri kwamba alimaanisha lile jengo kubwa sana la hekalu, ijapokuwa alimaanisha “hekalu la mwili wake.” Kwa hiyo, wakasema: “Hekalu hili lilijengwa kwa miaka arobaini na sita, nawe je, utaliinua katika siku tatu?” (Yohana 2:19-21) Kutokana na uchimbuaji wa mazingira ya Temple Mount, wageni wenye kuzuru sasa wanaweza kuona sehemu za kuta na sehemu nyingine za usanifu-majengo kuanzia wakati wa Yesu na hata wanaweza kutembelea hatua ambazo yamkini alitembea mpaka kwenye malango ya kusini mwa hekalu.
Karibu na ukuta wa magharibi wa Temple Mount, katika Jewish Quarter ya Old City, pana mahali pawili pa uchimbuaji palipotengenezwa vizuri kutoka karne ya kwanza W.K., pajulikanapo kuwa Burnt House na Herodian Quarter. Baada ya uvumbuzi wa Burnt House, mwakiolojia Nahman Avigad aliandika hivi: “Sasa ilikuwa wazi kwamba jengo hili lilichomwa na Waroma katika mwaka wa 70 A.D., wakati wa uharibifu wa Yerusalemu. Kwa mara ya kwanza katika historia ya uchimbuaji katika hili jiji, uthibitisho dhahiri na ulio wazi wa kiakiolojia wa kuchomwa kwa hili jiji ulikuwa umefunuliwa.”—Ona picha katika ukurasa wa 12.
Baadhi ya mavumbuzi hayo hufumbua baadhi ya matukio katika maisha ya Yesu. Majengo yalikuwa katika Jiji la Juu, ambapo watu wenye mali wa Yerusalemu waliishi, kutia ndani makuhani wa cheo cha juu. Idadi kubwa ya bafu za kidesturi zilipatikana katika hizo nyumba. Msomi mmoja atoa wazo hili: “Idadi kubwa ya bafu yathibitisha ufuataji kamili wa sheria za utakato wa kidesturi uliozoewa na wakazi wa Jiji la Juu wakati wa kipindi cha Hekalu la Pili. (Sheria hizi zimerekodiwa katika Mishnah, ambayo hutenga sura kumi zinazoeleza habari yote ya mikveh.)” Habari hiyo hutusaidia kung’amua maelezo ya Yesu kwa Mafarisayo na waandishi kuhusu desturi hizi.—Mathayo 15:1-20; Marko 7:1-15.
Kwa kushangaza idadi kubwa ya vyombo vya mawe pia imepatikana katika Yerusalemu. Nahman Avigad aandika hivi: “Basi, kwa nini, yalitokea ghafula hivyo na kwa idadi kubwa hivyo katika nyumba ya Yerusalemu? Jibu lapatikana katika milki ya halakhah, sheria za Kiyahudi za utakato wa kidesturi. Hiyo Mishnah hutuambia kwamba vyombo vya mawe ni miongoni mwa vitu vile ambavyo si vyepesi kupatwa na ukosefu wa usafi . . . Jiwe halikuwa jepesi kupatwa na uchafu wa kidesturi.” Yadokezwa kwamba hii hueleza sababu kwa nini yale maji ambayo Yesu aligeuza yawe divai yalihifadhiwa katika vyombo vya mawe badala ya vyombo vya udongo wa mfinyanzi.—Mambo ya Walawi 11:33; Yohana 2:6.
Ziara katika Israel Museum itatuonyesha hifadhi mbili za mifupa zisizo za kawaida. Gazeti Biblical Archaeology Review laeleza hivi: “Hifadhi za mifupa zilitumiwa hasa katika miaka ikadiriwayo kuwa mia moja iliyotangulia uharibifu wa Yerusalemu uliofanywa na Waroma katika mwaka wa 70 W.K. . . . Mfu aliwekwa katika ufa uliochongwa kwenye ukuta wa pango la kuzikia; baada ya mwili kuoza, mifupa ilikusanywa na kuwekwa katika hifadhi ya mifupa—chombo ambacho kwa kawaida kilikuwa cha jiwe la chokaa lililopambwa.” Hizo mbili zinazoonyeshwa zilipatikana Novemba 1990 katika pango la kuzikia. Mwakiolojia Zvi Greenhut aripoti hivi: “Neno . . . ‘Caiapha’ juu ya hizo hifadhi mbili za mifupa katika kaburi zaonekana hapa kwa mara ya kwanza katika muktadha wa kiakiolojia. Labda ni jina la familia la Kuhani wa Cheo cha Juu Kayafa, anayetajwa . . . katika Agano Jipya . . . Ilikuwa kutoka nyumba yake katika Yerusalemu ambapo Yesu alipelekwa mbele ya wakili Mroma Pontio Pilato.” Hifadhi moja ya mifupa ilikuwa na mifupa ya mwanamume aliyekuwa na umri upatao miaka 60 hivi. Wasomi wanadhani kwamba hiyo kwa kweli ni mifupa ya Kayafa. Msomi mmoja huyarejesha hayo mavumbuzi kwenye wakati wa Yesu: “Sarafu iliyopatikana katika mojawapo ya hifadhi nyingine ya mifupa ilipigwa chapa na Herode Agripa (37-44 W.K.). Huenda ikawa hizo hifadhi mbili za Kayafa za mifupa ni za tangu mwanzo wa karne.”
William G. Dever, profesa wa akiolojia wa Near Eastern kwenye Chuo Kikuu cha Arizona, alieleza hivi kuhusu Yerusalemu: “Si kutia chumvi kusema kwamba tumejifunza mengi zaidi juu ya historia ya sehemu hii kuu katika miaka 15 iliyopita kuliko katika jumla ya miaka 150 iliyotangulia.” Mwingi wa utendaji wa kiakiolojia katika Yerusalemu wakati wa miongo ya majuzi bila shaka umetoa mavumbuzi yanayofafanua historia ya Biblia.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 9]
Utokezaji upya wa Jiji la Yerusalemu wakati wa Hekalu la Pili - wapatikana katika uwanja wa Hoteli ya Holyland Yerusalemu
[Picha katika ukurasa wa 10]
Juu: Pembe ya kusini-magharibi ya jengo la Temple Mount la Yerusalemu
Kulia: Kushuka kuingia Warren’s Shaft