Umedi-Uajemi—Ile Serikali Kubwa ya Nne ya Ulimwengu Katika Historia ya Biblia
Wamedi na Waajemi walihusika katika matukio mengi ambayo yanasimuliwa katika Biblia. Wao wanatajwa pia katika maunabii kadhaa ya Biblia. Je! wewe ungependa kujua mengi zaidi juu ya hizi jamii za watu wa kale wenye kupendeza?
WAMEDI na Waajemi wa kale walikuwa wakipiga miguu kusonga mbele! Mwenye kuwaongoza alikuwa Sairasi Mkuu, ambaye tayari alidhibiti milki. Sasa yeye alikaza fikira zake juu ya Babuloni wenye uweza, ile serikali kubwa ya ulimwengu katika siku hiyo.
Ndani ya mji mkuu wa Babuloni, Mfalme Belshaza, ambaye Biblia inasema alikuwa “chini ya mavutano ya divai,” alikuwa akiandaa karamu kwa ajili ya wageni mashuhuri elfu moja. Wakiwa katika karamu ya ulevi yenye makelele, wao walisifu miungu yao ya sanamu, huku wakinywa kutokana na vyombo vitakatifu vilivyokuwa vimetolewa Yerusalemu katika hekalu la Yehova. (Danieli 5:1-4) Wao walihisi wakiwa salama salimini ndani ya kuta imara za Babuloni.
Hata hivyo, kule nje jeshi la Sairasi lilikuwa limekengeusha maji ya Mto Eufrate ambayo yalipita katika Babuloni. Kizuizi hicho cha kiasili kilipoondolewa, askari zake walitembea chubwi-chubwi katika sakafu ya mto—wakazipita moja kwa moja zile kuta za Babuloni na kuingia ndani ya mji ule kupitia malango wazi yaliyoelekeana na mto huo. Kabla ya jua kuchomoza, Belshaza alikuwa mfu, Babuloni ulikuwa umeanguka, na Umedi-Uajemi ukawa ndio serikali kubwa ya nne ya ulimwengu katika historia ya Biblia! Lakini Wamedi na Waajemi hawa walikuwa akina nani?
Wamedi walikuja kutoka jimbo la nyanda za juu zenye milima-milima, kuelekea mashariki mwa Ashuru. Michoro fulani ya kuchongelewa, ambayo imepatikana katika Ashuru, inawaonyesha wakiwa wamevaa zile zinazoonekana kuwa koti za ngozi za kondoo juu ya majoho mepesi, na wakiwa wamevaa viatu vya buti vyenye kufungwa kwa kamba. Mavazi hayo yalifaa kwa kazi yao ya uchungaji katika hizo nyanda za juu. Ni kadiri ndogo mno ya kumbukumbu zilizoandikwa ambayo Wamedi waliacha. Nyingi za habari ambazo sisi tunajua juu yao ni zile tunazojifunza kutokana na Biblia, kutokana na maandishi-awali ya Kiashuri, na kutokana na wanahistoria Wagiriki. Hapo awali Waajemi waliendesha maisha ambayo mara nyingi yalikuwa ya kuhama-hama katika lile jimbo lililo kaskazini mwa Hori ya Uajemi. Milki yao ilipozidi kukua, wao walisitawisha upendezo mwingi ajabu wa kupenda raha.
Hapo kwanza, Wamedi walikuwa ndio wenye nguvu zaidi za utawala, lakini katika 550 K.W.K. Sairasi Mkuu, wa Uajemi, alipata ushindi wa haraka sana juu ya mfalme Astyages Mwamedi. Sairasi aliunganisha desturi na sheria za hizo jamii mbili za watu, akaunganisha kwa umoja falme zao, na kupanua ushindi wao mwingi. Ingawa Wamedi walikuwa wenye kujinyenyekeza sana kwa Waajemi, ni wazi kabisa kwamba milki hiyo ilikuwa ya muungano wa makundi mawili. Wamedi walishikilia cheo kikubwa na ndio walioongoza majeshi ya Kiajemi. Watu wa nchi za kigeni walinena juu ya Wamedi na Waajemi, au walipotumia mtajo mmoja tu, huo ulikuwa “Mmedi.”
Kabla ya Wamedi na Waajemi kushambulia Babuloni, nabii Danieli alikuwa amepewa njozi ya kondoo dume mwenye pembe mbili ambaye aliwakilisha taifa hili lenye sehemu mbili. Danieli aliandika hivi: “Na zile pembe mbili zilikuwa ndefu, lakini ile moja ilikuwa ndefu kuliko ile nyingine, na ile ndefu zaidi ndiyo iliyokuja juu baadaye.” Hakukuwa na swali juu ya utambulishi wa kondoo dume huyo, kwa maana malaika aliambia Danieli hivi: “Yule kondoo dume ambaye wewe uliona akiwa na zile pembe mbili anasimamia wafalme wa Umedi na Uajemi.”—Danieli 8:3, 20, NW.
Danieli alikuwa ndani ya Babuloni wakati ulipoanguka na alishuhudia kufika kwa Wamedi na Waajemi. Dario Mmedi, yule mtawala wa kwanza wa jiji lililokuwa limeshindwa karibuni, aliweka rasmi watu 120 ‘watoa himaya kwa ile milki’ na akaweka maafisa watatu juu yao. Danieli alikuwa mmoja wa hao watatu. (Danieli 5:30–6:3) Kwa sababu ya Danieli kuwa na cheo kikubwa cha usimamizi kabla na baada ya Babuloni kuanguka, ingekuwa vigumu kuwazia kwamba Sairasi hakujulishwa kwamba—karne mbili mapema—unabii wa Kiebrania ulikuwa umesema Babuloni ungeshindwa na mwanamume mwenye jina Sairasi.—Isaya 45:1-3, NW.
Yerusalemu Warudishwa
Anguko la Babuloni liliandaa jukwaa kwa mwinuko wa mji mwingine—Yerusalemu. Huo ulikuwa umelala ukiwa magofu kwa karibu miaka 70 tangu ulipoharibiwa na Wababuloni katika 607 K.W.K. Maunabii ya Biblia yalikuwa yamesema kwamba kupitia Sairasi Yerusalemu ungejengwa upya na msingi wa hekalu lao uwekwe.—Isaya 44:28.
Je! jambo hilo lilitukia? Ndiyo. Ezra kuhani, mwanachuo na mwandishi, huripoti kwamba Sairasi alitoa uamuzi kwamba waabudu wa Yehova wangeweza “kupanda waende Yerusalemu, ambao umo katika Yuda, na kujenga upya ile nyumba ya Yehova Mungu wa Israeli—yeye ndiye Mungu wa kweli—ambayo ilikuwa katika Yerusalemu.” (Ezra 1:3, NW ) Watu wapatao 50,000 walifunga ile safari ya miezi minne kurudi Yerusalemu, wakiwa na zile hazina za hekalu. Katika 537 K.W.K. nchi ilianza tena kukaliwa—miaka 70 barabara baada ya Yerusalemu kuwa umeanguka.—Yeremia 25:11, 12; 29:10.
Uchimbuzi wa vitu vya kale umehakikisha kwamba uamuzi huo ulipatana na mwongozo wa Sairasi. Juu ya silinda iliyopatikana katika magofu ya Babuloni, Sairasi anasema: “Mimi niliyarudishia majiji (haya) matakatifu . . . sehemu zayo zilizo takatifu ambazo zimekuwa magofu kwa muda mrefu, mifano ambayo (ilipata) kuishi humo na nikaisimamishia imara sehemu takatifu za kudumu. Mimi nilikusanya (pia) wote (waliokuwa) wakaaji wayo na kurudisha (kwa hao) makazi yao.”
Baadaye maadui wa Kisamaria wa Wayahudi walisababisha kujengwa upya kwa hekalu kukomeshwe na marufuku ya mfalme mwenye koloni hilo. Hagai na Zekaria manabii wa Yehova waliwachochea watu, na ile kazi ya kujenga ikaaanzwa tena. “Dario mfalme” aliagiza kuwe na utafutaji wa uamuzi wa awali wa Sairasi uliotoa mamlaka ya kurudishwa kwa hekalu. Biblia inasema kwamba hati-kunjo ilipatikana Ekbatana, kao la Sairasi wakati wa kiangazi, ikiwa na maandishi ya kumbukumbu kuthibitisha uhalali wa ile kazi ya hekalu. Kazi hiyo ilimalizwa katika mwaka wa sita wa mfalme Mwajemi Dario 1.—Ezra 4:4-7, 21; 6:1-15, NW.
Ithibati Kuhusu Fahari
Katika njozi iliyotajwa mapema zaidi, Danieli alikuwa ametangulia kuona yule “kondoo dume [wa Umedi-Uajemi mwenye pembe mbili] akijirusha-rusha kuelekea magharibi na kuelekea kaskazini na kuelekea kusini, na hakuna wanyama-mwitu [mataifa mengine] walioendelea kusimama mbele yake, na mara nyingi hakukuwa na mtu mwenye kufanya ukombozi wo wote kutoka mkononi mwa huyo. Naye alitenda kulingana na mapenzi yake, naye alijishaua sana.” (Danieli 8:4, NW ) Angalau kufikia wakati wa Dario, njozi hiyo ilikuwa imetimizwa. Katika kushuhudiza matendo yake hodari, Dario Mkuu aliagiza kwamba yeye mwenyewe awakilishwe juu ya mchoro mkubwa sana wa kuchongelewa, ambao unaweza bado kuonwa ukiwa umeinuka juu ya uso wa genge la mawe kule Bisitun, katika ile barabara ya zamani kati ya Babuloni na Ekbatana. Zaidi ya kushinda Babuloni, yule “kondoo dume” aliye Umedi-Uajemi alikuwa amebamba eneo katika pande tatu kubwa-kubwa: kaskazini kuingia Ashuru, magharibi kupitia Esia Ndogo, na kusini kuingia Misri.
Kilometa zipatazo 640 kuelekea kusini-mashariki mwa kao lao la wakati wa kiangazi huko Ekbatana, wamaliki Waajemi walijenga jumba kubwa mno la kifalme kule Persepolisi. Mchoro wa kuchongelewa ulio huko unaonyesha Dario akiwa juu ya kiti chake cha ufalme, na juu ya maandishi yaliyochongelewa anajisifu hivi: “Mimi ni Dario, mfalme mkuu, mfalme wa wafalme, mfalme wa mabara . . . ambaye alijenga hili jumba la kifalme.” Nguzo kadhaa zilizoinuka juu kama minara za huu mji mkuu wenye fahari zingali zipo leo. Mji mkuu mwingine ulikuwa huko Susa (Shushani), ambao ulikuwa katikati ya Babuloni, Ekbatana, na Persepolisi. Huko Dario Mkuu alijenga jumba la kifalme jingine la kuvutia sana.
Dario alifuatwa katika cheo na Zaksizi mwana wake, ambaye inaonekana alikuwa ndiye “Ahasuero” wa kitabu cha Biblia cha Esta. Kitabu hicho kinasema kwamba Ahasuero “alikuwa akitawala akiwa mfalme kutoka India mpaka Ethiopia, juu ya wilaya za kiutawala zaidi ya mia moja na ishirini na saba,” huku akiketi juu ya “kiti cha kifalme chake, ambacho kilikuwa katika Shushani ile ngome ya kifalme.” Hapo ndipo Ahasuero alifanya Esta kijana mrembo awe malkia wake. (Esta 1:1, 2; 2:17, NW ) Katika jumba la makumbusho lililoko Louvre katika Paris, wewe unaweza kuona ng’ombe dume aliyepambwa sana katika sehemu ya juu kabisa ya nguzo iliyoinuka sana katika hilo jumba la kifalme, na pia mapambo ya ukutani yanayowakilisha watupa-mishale Waajemi wenye kiburi, na wanyama wenye fahari. Magudulia ya alabasta (marimari), vitu vya majohari, na bidhaa nyingine ambazo zilipatikana humo zinafaana vizuri na taarifa za Biblia juu ya madoido mengi ambayo Esta alifanyiwa, na pia ile anasa iliyokuwa katika Shushani.—Esta 1:7; 2:9, 12, 13.
Hadithi zilizosimuliwa na maadui Wagiriki wa Zaksizi zilitia ndani habari ya kwamba mfalme wa Uajemi alikuwa na magumu ya ndoa na zikatia ndani ule msemekano wa kwamba maafisa wa barazani mwake walitawala maoni yake. Ingawa huenda mambo ya uhakika yakawa yamevurugwa na kupotoshwa, hadithi hizo zinaonekana ni kama zinaonyesha mambo fulani makuu juu ya kitabu cha Esta, ambacho kinasema mfalme alimwondolea cheo Malkia Vashti mwenye kichwa kigumu na kuweka Esta mahali pake, na kwamba Mordekai binamu ya Esta alipata cheo cha mamlaka kubwa katika milki hiyo.—Esta 1:12, 19; 2:17; 10:3.
Hisani Yaonyeshwa Kuelekea Waabudu wa Yehova
Katika mwaka 468 K.W.K., Artazaksizi (Longimano) mfuata Zaksizi katika cheo alimpa mamlaka kuhani Ezra, ambaye aliishi katika Babuloni baada ya Sairasi kufungua Wayahudi hapo awali, ili warudi Yerusalemu na kuendeleza ibada safi ya Yehova huko. Wanaume wapatao 1,500 na jamaa zao—labda watu 6,000 kwa ujumla—waliandamana na Ezra, wakileta pamoja nao mchango mkubwa kwa ajili ya hekalu la Yehova.—Ezra 7:1, 6, 11-26.
Pia ilikuwa ni katika jumba la kifalme kule Shushani kwamba Artazaksizi huyu huyu, akiwa katika mwaka wake wa 20 (455 K.W.K.), alikubalia ombi la Nehemia la kutaka kurudishwa akajenge upya Yerusalemu na kuta zao. Amri hiyo ya kufanya hivyo ilitia alama mwanzo wa yale “majuma sabini” ya miaka ya unabii wa Danieli, ambao ulielekeza mbele kwenye mtokeo wa Yesu akiwa “Mesiya Kiongozi” katika wakati barabara mwakani 29 W.K. a—Danieli 9:24, 25; Nehemia 1:1; 2:1-9, NW.
Hati fulani zilizoandikwa juu ya mafunjo katika lugha ya Kiaramu zilipatikana Elephantine, kisiwa kilicho katika Mto Naili wa Misri. Hati hizo zinaonyesha usahihi uliotumiwa na Ezra na Nehemia waandikaji wa Biblia kueleza hali zilizokuwako wakati wa utawala wa Kiajemi na pia mawasiliano yaliyotumiwa kati ya maafisa. Katika Biblical Archaeology, Profesa G. Ernest Wright anataarifu hivi: “Sasa . . . sisi tunaweza kuona kwamba Kiaramu cha Ezra kinalingana barabara na kile cha muda huo, na zile hati za serikali ni za namna ile ya ujumla ambayo sisi tumezoea kuishirikisha na utawala wa Kiajemi.” Moja ya hati hizo ilikuwa na agizo la mfalme wa Uajemi kuhusu kuadhimishwa kwa sikukuu ya Kupitwa na lile koloni la Kiyahudi katika Misri.
Umedi-Uajemi Wajiacha Ushindwe na Ugiriki
Katika njozi, Danieli alikuwa ameona Umedi-Uajemi ukiwakilishwa kama kondoo dume mwenye pembe mbili. Halafu, karne mbili kabla ya jambo hilo kutukia, yeye aliona “dume la akina mbuzi likija kutoka machweo ya jua [magharibi]” na likienda kasi sana hivi kwamba “halikuwa likiigusa dunia.” Yule mbuzi dume mwenye kwenda kasi akaanza “kupiga hata chini yule kondoo dume na kuvunja pembe mbili zake, na hakukuthibitika kuwa na nguvu zo zote katika yule kondoo dume ili asimame mbele yake.” (Danieli 8:5-7, NW ) Je! historia inaonyesha kwamba jambo hilo lilitukia kweli kweli kwa Umedi-Uajemi?
Ndiyo, katika mwaka 334 K.W.K. Aleksanda Mkuu alitoka Ugiriki akaja magharibi. Akiwa na mwendo-umeme kama ule wa mbuzi dume, yeye alipita akikumba Esia yote, akipata ushindi baada ya ushindi juu ya Waajemi. Hatimaye, katika 331 K.W.K., huko Gaugamela, yeye alitawanya jeshi moja la Kiajemi lenye wanaume milioni moja. Kiongozi walo Dario wa 3 alikimbia, na baadaye akauawa na wale ambao wakati mmoja walikuwa rafiki zake. Ile serikali kubwa ya nne ya ulimwengu ikawa imepigwa hata chini, pembe zayo zikavunjwa, na milki ya Aleksanda ikawa ya tano ya zile serikali kubwa za ulimwengu katika historia ya Biblia. Hiyo itazungumziwa katika toleo letu la Aprili 15, 1988.
Serikali Kubwa ya Ulimwengu ya Umedi-Uajemi ilikuwa imekuwako kwa muda unaozidi kidogo tu karne mbili—kutoka ule usiku ambao ilipindua Babuloni katika 539 K.W.K. mpaka ilipoanguka kwa Aleksanda. Huo ni wakati unaokaribia kulingana urefu na wakati ambao umepita tangu yale Mapinduzi Makubwa ya Kifaransa au tangu United States ya Amerika ilipoanzishwa. Katika kipindi hicho ambacho kwa kadiri fulani ni kifupi, bila kukusudia Wamedi na Waajemi walihusika sana katika hatua-hatua za utimizo wa makusudi ya Yehova Mungu na utimizo wa maunabii yake yasiyoshindwa kutimia.
[Footnotes]
a Ili upate zungumzo la urefu juu ya unabii huu na utimizo wao, ona kitabu “Ufalme Wako Uje,” kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, inc., kurasa 56-66.
[Map/Picture on page 26]
(For fully formatted text, see publication)
Milki ya Umedi-Uajemi
INDIA
Ecbatana
Susa (Shushani)
Persepolisi
Babuloni
YerusalemU
MISRI
[Picture]
Magofu ya Persepolisi, mji mkuu wa kisherehe wa Uajemi
[Credit Line]
Manley Studios
[Picture on page 29]
Kaburi la Sairasi katika Iran