Kitabu Cha Biblia Namba 15—Ezra
Mwandikaji: Ezra
Mahali Kilipoandikiwa: Yerusalemu
Uandikaji Ulikamilishwa: c. (karibu) 460 K.W.K.
Wakati Uliohusishwa: 537–c. (karibu) 467 K.W.K.
1. Ni unabii gani mbalimbali uliotoa uhakikisho wa kurejeshwa kwa Yerusalemu?
MWISHO wa miaka 70 iliyotabiriwa ya ukiwa wa Yerusalemu chini ya Babuloni ulikuwa wakaribia. Kweli, ilikuwa sifa ya Babuloni kwamba haikuwa ikiachilia kamwe watumwa wayo, lakini neno la Yehova lingethibitika kuwa lenye nguvu zaidi ya uwezo wa Kibabuloni. Kuachiliwa kwa watu wa Yehova kulikuwa kwakaribia. Hekalu la Yehova lililokuwa limebomolewa lingejengwa upya, na madhabahu ya Yehova ingepokea dhabihu za upatanisho kwa mara nyingine. Kwa mara nyingine Yerusalemu lingejua kelele na sifa ya mwabudu wa kweli wa Yehova. Yeremia alikuwa ametabiri urefu wa ukiwa huo, na Isaya alikuwa ametabiri jinsi watumwa wangefunguliwa. Isaya alikuwa hata ametaja Koreshi wa Uajemi kuwa ‘mchungaji wa Yehova,’ ambaye angeporomosha Babuloni yenye kiburi kutoka cheo chayo ikiwa mamlaka ya tatu ya ulimwengu ya historia ya Biblia.—Isa. 44:28; 45:1, 2; Yer. 25:12.
2. Babuloni ilianguka lini na chini ya hali gani?
2 Maafa yalipata Babuloni usiku ule wa Oktoba 5, 539 K.W.K. (kalenda ya Gregory), Belshaza mfalme wa Babuloni na waheshimiwa wake walipokuwa wakinywa kwa kuheshimu miungu yao ya roho waovu. Kuongezea ufisadi wao wa kipagani, walikuwa wakitumia vyombo vitakatifu kutoka hekalu la Yehova kuwa vikombe vyao vya ulevi! Jinsi ilivyofaa kwamba Koreshi alikuwa nje ya kuta za Babuloni usiku huo ili atimize unabii!
3. Ni tangazo gani lililotolewa na Koreshi ambalo liliwezesha kurejeshwa kwa ibada ya Yehova miaka 70 kamili baada ya ukiwa wa Yerusalemu kuanza?
3 Tarehe hii 539 K.W.K. ni tarehe ya msingi, yaani, tarehe ambayo yaweza kupatanishwa na historia ya kilimwengu na ya Kibiblia. Wakati wa mwaka wake wa kwanza akiwa mtawala wa Babuloni, Koreshi ‘alipiga mbiu katika ufalme wake wote,’ akiwapa ruhusa Wayahudi wakwee kwenda Yerusalemu kujenga upya nyumba ya Yehova. Amri hiyo kwa wazi ilitolewa mwishoni-mwishoni katika 538 K.W.K. au mapema katika 537 K.W.K.a Baki jaminifu lilisafiri kurejea Yerusalemu kwa wakati unaofaa ili kusimamisha madhabahu na kutoa dhabihu za kwanza katika “mwezi wa saba” (Tishri, unaolingana na Septemba-Oktoba) wa mwaka 537 K.W.K.—miaka 70 kufikia mwezi uliofuatia ukiwa wa Yuda na Yerusalemu ulioletwa na Nebukadreza.—Ezra 1:1-3; 3:1-6.
4. (a) Ni nini hali inayozunguka kitabu cha Ezra, na ni nani aliyekiandika? (b) Ezra kiliandikwa lini, nacho chahusu kipindi gani?
4 Kurejeshwa! Hiyo ndiyo hali inayozunguka kitabu cha Ezra. Matumizi ya usemi wa kutaja mtu binafsi katika usimulizi tangu sura ya 7 mstari 27 hadi sura ya 9 kwa wazi yaonyesha kwamba mwandikaji alikuwa ni Ezra. Akiwa “mwandishi mwepesi [stadi, NW] katika sheria ya Musa” na mwanamume wa imani yenye kutumika ‘aliyeelekeza moyo wake kuitafuta sheria ya Yehova, na kuitenda na kuifundisha,’ Ezra alistahili sana kuandika historia hiyo, kama vile alivyoandika Mambo ya Nyakati. (Ezra 7:6, 10) Kwa kuwa kitabu cha Ezra ni mwendelezo wa Mambo ya Nyakati, kwa ujumla huaminiwa kwamba kiliandikwa wakati ule ule, yapata 460 K.W.K. Kinahusisha miaka 70, tangu wakati ambao Wayahudi walikuwa taifa lililovunjwa-vunjwa na lililotawanywa na kutiwa alama kuwa ‘wana wa mauti’ hadi kukamilishwa kwa hekalu la pili na kutakaswa kwa ukuhani baada ya Ezra kurejea Yerusalemu.—Ezra 1:1; 7:7; 10:17; Zab. 102:20, NW, kielezi-chini.
5. Kitabu cha Ezra kina uhusiano gani na kitabu cha Nehemia, nacho kiliandikwa katika lugha zipi?
5 Jina la Kiebrania Ezra lamaanisha “Msaada.” Vitabu vya Ezra na Nehemia hapo awali vilikuwa hati-kunjo moja. (Neh. 3:32, NW, kielezi-chini) Baadaye Wayahudi waligawanya hati-kunjo hiyo na kuiita Ezra wa Kwanza na wa Pili. Biblia za kisasa za Kiebrania huita vitabu hivyo viwili Ezra na Nehemia, sawa na Biblia nyingine za kisasa. Sehemu ya kitabu cha Ezra (4:8 hadi 6:18 na 7:12-26) iliandikwa katika Kiaramu na iliyosalia katika Kiebrania, Ezra akiwa stadi katika lugha zote mbili.
6. Ni nini kinachothibitisha usahihi wa kitabu cha Ezra?
6 Leo sehemu kubwa ya wasomi hukubali usahihi wa kitabu hicho cha Ezra. Kuhusu kukubaliwa kwa Ezra, W. F. Albright aandika hivi katika makala yake The Bible After Twenty Years of Archaeology: “Hivyo data za akiolojia zimeonyesha uawali wa kadiri kubwa wa Vitabu vya Yeremia na Ezekieli, vya Ezra na Nehemia kukawa hakuna shaka lolote; zimethibitisha wazo la tangu zamani la matukio, na pia utaratibu wayo.”
7. Kitabu cha Ezra chaonyeshwaje kweli kweli kuwa sehemu ya maandishi ya kimungu?
7 Ingawa huenda kitabu cha Ezra kisinukuliwe (kisitajwe) wala kurejezewa moja kwa moja na waandikaji wa Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, hakuna shaka juu ya mahali pacho katika vitabu vyenye kukubaliwa vya Biblia. Kina maandishi ya shughuli za Yehova pamoja na Wayahudi hadi kufikia wakati wa kukusanywa kwa orodha ya vitabu vya Kiebrania, kazi ambayo kulingana na mapokeo ya Kiyahudi ilitimizwa kwa sehemu kubwa na Ezra. Zaidi ya hayo, kitabu cha Ezra chatetea unabii wote unaohusu kurejeshwa kule na kwa hiyo chathibitisha kwamba kwa hakika hicho ni sehemu halisi ya maandishi ya kimungu, ambayo chapatana nayo kabisa. Kuongezea hayo, kinaheshimu ibada yenye kutakata na hutukuza jina kuu la Yehova Mungu.
YALIYOMO KATIKA EZRA
8. Eleza mfululizo wa matukio yaliyoongoza kwenye mwisho wa miaka 70 ya ukiwa.
8 Baki larejea (1:1–3:6). Roho yake ikiwa imeamshwa na Yehova, Koreshi mfalme wa Uajemi atoa amri kwa Wayahudi warejee na kujenga nyumba ya Yehova katika Yerusalemu. Awasihi Wayahudi wale ambao huenda wakabaki Babuloni wachange kwa ukarimu kuelekea kazi hiyo na apanga kwa Wayahudi wanaorejea wachukue vyombo vya lile hekalu la awali. Mmoja ambaye ni kiongozi kutoka kabila la kifalme la Yuda na mzao wa Mfalme Daudi, Zerubabeli (Sheshbaza), apewa mgawo wa kuwa liwali ili kuongoza waliofunguliwa, na Yeshua (Yoshua) ndiye kuhani mkuu. (Ezra 1:8; 5:2; Zek. 3:1) Baki ambalo huenda hesabu yalo ilikuwa 42,360 la watumishi wa Yehova waaminifu, kutia wanaume, wanawake, na watoto, lafunga safari hiyo ndefu. Kufikia mwezi wa saba, kulingana na kalenda ya Kiyahudi, wamekalia miji yao, na kisha wakusanyika kule Yerusalemu ili kutoa dhabihu kwenye kituo cha madhabahu ya hekalu na kuadhimisha Sikukuu ya Vibanda katika vuli ya 537 K.W.K. Hivyo miaka 70 ya ukiwa yamalizika kwa wakati barabara!b
9. Kazi ya hekalu yaanzaje, lakini ni nini kinachotukia katika miaka inayofuata?
9 Kujenga upya hekalu (3:7–6:22). Vifaa vyakusanywa, na katika mwaka wa pili wa kurejea kwao, msingi wa hekalu la Yehova wawekwa kukiwako kelele za shangwe na kukiwako kulia kwa wanaume wazee waliokuwa wameona nyumba ya awali. Majirani, wapinzani, wajitolea kusaidia na ujenzi, wakisema wanatafuta Mungu uyo huyo, lakini baki la Kiyahudi lakataa katakata kufanya mapatano yoyote nao. Wapinzani waendelea kujaribu kudhoofisha na kuvunja moyo Wayahudi na kuvuruga kazi yao, tangu utawala wa Koreshi hadi ule wa Dario. Hatimaye, katika siku za “Artashasta” (Bardiya au yawezekana Mmagi anayejulikana kuwa Gaumata, 522 K.W.K.), wakomesha kazi hiyo kwa nguvu kwa kufuata amri ya kifalme. Marufuku hiyo yaendelea “hata mwaka wa pili wa kutawala kwake Dario, mfalme wa Uajemi” (520 K.W.K.), ambao ni miaka 15 baada ya kuwekwa kwa msingi.—4:4-7, 24.
10. (a) Kitia-moyo kutoka kwa manabii wa Mungu chaunganaje na agizo la mfalme katika kukamilisha kazi? (b) Ni shangwe gani inayotia alama kuwekwa wakfu kwa hekalu hili la pili?
10 Sasa Yehova apeleka manabii wake Hagai na Zekaria wakachochee Zerubabeli na Yeshua, na kazi ya ujenzi yaendelezwa kwa bidii mpya. Kwa mara nyingine wapinzani walalamikia mfalme, lakini kazi yaendelea kwa nguvu zisizopungua. Dario 1 (Haistaspo), akiisha kurejezea amri ya awali ya Koreshi, aagiza kazi iendelee bila kizuizi na hata aamuru wapinzani watoe vifaa vya kuwezesha ujenzi. Kwa kitia-moyo chenye kuendelea kutoka kwa manabii wa Yehova, wajenzi wakamilisha hekalu kwa muda unaopungua miaka mitano. Hii ni katika mwezi wa Adari wa mwaka wa sita wa Dario, au karibu na vuli ya 515 K.W.K., na ujenzi wote umechukua miaka kama 20 tu. (6:14, 15) Nyumba ya Mungu sasa yazinduliwa kwa shangwe kubwa na kwa dhabihu zinazofaa. Kisha watu washerehekea Kupitwa na wachukua hatua ya kuadhimisha “sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu kwa furaha, kwa muda wa siku saba.” (6:22) Ndiyo, shangwe na kushangilia vyatia alama kuwekwa wakfu kwa hekalu hili la pili kwa sifa ya Yehova.
11. Mfalme amkubaliaje Ezra “matakwa yake yote,” na itikio la Ezra ni nini?
11 Ezra arejea Yerusalemu (7:1–8:36). Karibu miaka 50 yapita, hiyo ikituleta kwenye 468 K.W.K., mwaka wa saba wa Artashasta mfalme Mwajemi (aliyejulikana kuwa Longimano kwa sababu ya mkono wake wa kulia ulio mrefu zaidi ya ule wa kushoto). Mfalme huyo amkubalia Ezra mnakiliji stadi “matakwa yake yote” kuhusiana na safari ya kwenda Yerusalemu ili kutoa msaada unaohitajiwa sana huko. (7:6) Katika kumpa ruhusa, mfalme atia moyo Wayahudi waandamane naye na ampa Ezra vyombo vya fedha na dhahabu kwa ajili ya matumizi ya hekaluni, na pia ampa ngano, divai, mafuta, na chumvi. Aondolea makuhani na wafanya kazi wa hekalu takwa la kulipa ushuru. Mfalme huyo ampa Ezra daraka la kufundisha watu na ajulisha rasmi kuwa ni kosa linalostahili kifo kwa yeyote kutokuwa mtendaji wa sheria ya Yehova na sheria ya mfalme. Katika kushukuru Yehova kwa ajili ya wonyesho huo wa fadhili zake za upendo kupitia mfalme, Ezra achukua hatua bila kukawia kuhusu utume huo.
12. Yehova athibitishaje kuwa na kikundi cha Ezra wakati wa safari hiyo?
12 Kufikia hapa Ezra aanza simulizi lake la mambo aliyojionea mwenyewe, akiandika kwa kujielekezea. Akusanya Wayahudi wenye kurejea kwenye mto Ahava kwa ajili ya maagizo ya mwisho, na aongezea Walawi kwenye kikundi hicho cha watu wazima wa kiume karibu 1,500 ambao tayari wamejikusanya. Ezra atambua hatari za njia itakayopitiwa lakini haombi mfalme walinzi, isije ikaonwa kuwa ni ukosefu wa imani katika Yehova. Badala yake, atangaza juu ya kufunga kula na kuongoza kambi hiyo katika kusihi Mungu. Sala hiyo yajibiwa, na mkono wa Yehova wathibitika kuwa juu yao katika safari yao yote iliyo ndefu. Hivyo, wakaweza kuleta hazina zao (za thamani inayozidi dola 43,000,000 kwa thamani ya kisasa) salama kwenye nyumba ya Yehova katika Yerusalemu.—8:26, 27, NW, na vielezi-chini.
13. Ezra atendaje katika kuondoa uchafu miongoni mwa Wayahudi?
13 Kutakasa ukuhani (9:1–10:44). Lakini mambo yote hayakuendelea vizuri wakati wa miaka 69 ya kukalia bara lililorejeshwa. Ezra apata habari juu ya hali zenye kuhangaisha, kwa kuwa watu, makuhani, na Walawi wameoana na Wakanaani wapagani. Ezra mwaminifu aduwaa. Aweka jambo hilo mbele za Yehova katika sala. Watu waungama makosa yao na kumwuliza Ezra ‘awe na moyo mkuu akatende.’ (10:4) Aamuru Wayahudi waondoshe wake zao wa kigeni ambao wamewachukua kwa kutotii sheria ya Yehova, na uchafu waondolewa katika muda wa miezi mitatu hivi.—10:10-12, 16, 17.
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
14. Kitabu cha Ezra chaonyesha nini kuhusu unabii mbalimbali wa Yehova?
14 Kitabu cha Ezra ni chenye mafaa, kwanza, katika kuonyesha usahihi usio na kosa ambao katika huo unabii mbalimbali wa Yehova hutimizwa. Yeremia, ambaye alikuwa ametabiri kwa usahihi sana ukiwa wa Yerusalemu, pia alitabiri kurejeshwa baada ya miaka 70. (Yer. 29:10) Kwa wakati barabara, Yehova alionyesha fadhili zake za upendo katika kuleta watu wake, baki jaminifu, kurejea tena katika Bara la Ahadi ili kuendeleza ibada ya kweli.
15. (a) Hekalu lililorejeshwa lilitimizaje kusudi la Yehova? (b) Ni katika habari gani lilikosa utukufu wa hekalu la kwanza?
15 Hekalu lililojengwa upya lilitukuza ibada ya Yehova miongoni mwa watu wake, na lilisimama kuwa ushuhuda wa kwamba yeye hubariki kwa ajabu sana na kwa rehema wale wanaomgeukia wakiwa na tamanio kwa ajili ya ibada ya kweli. Ingawa halikuwa na utukufu wa hekalu la Sulemani, lilitumikia kusudi lalo kwa kupatana na mapenzi ya kimungu. Fahari ya kihalisi haikuwapo tena. Pia lilikuwa duni katika hazina za kiroho, kati ya vitu vingine, likiwa halina sanduku la agano.c Wala kuzinduliwa kwa hekalu la Zerubabeli hakukulingana na kuzinduliwa kwa hekalu katika siku ya Sulemani. Dhabihu za ng’ombe na kondoo hazikufikia hata asilimia moja ya dhabihu kwenye hekalu la Sulemani. Hakuna utukufu wowote wa namna ya wingu uliojaza nyumba hiyo ya baadaye, kama vile katika ile ya awali, wala moto haukushuka kutoka kwa Yehova ili kuteketeza sadaka za kuteketezwa. Hata hivyo, mahekalu yote mawili yalitumikia kusudi la maana la kutukuza ibada ya Yehova, Mungu wa kweli.
16. Lakini ni hekalu gani jingine linalozidi utukufu wa mahekalu ya kidunia?
16 Hekalu lililojengwa na Zerubabeli, tabenakulo iliyojengwa na Musa, na mahekalu yaliyojengwa na Sulemani na Herode, pamoja na sehemu mbalimbali zayo, yalikuwa kifananishi, picha ya kimbele. Hayo yaliwakilisha “ile hema ya kweli, ambayo Bwana [Yehova, NW] aliiweka wala si mwanadamu.” (Ebr. 8:2) Hekalu hilo la kiroho ni ule mpango wa kufikia Yehova katika ibada kwa msingi wa dhabihu ya upatanisho ya Kristo. (Ebr. 9:2-10, 23) Hekalu kuu la kiroho la Yehova ni bora mno katika utukufu na halilinganiki katika uzuri na utamaniko; fahari yalo haichakai na yapita ile ya jengo lolote halisi.
17. Ni masomo gani yenye thamani yanayopatikana katika kitabu cha Ezra?
17 Kitabu cha Ezra kina masomo yenye thamani ya juu zaidi kwa Wakristo leo. Humo twasoma juu ya watu wa Yehova wakitoa matoleo ya hiari kwa ajili ya kazi yake. (Ezra 2:68; 2 Kor. 9:7) Twatiwa moyo kwa kujifunza juu ya mpango wa Yehova usioshindwa na baraka yake kwa mikusanyiko kwa ajili ya sifa yake. (Ezra 6:16, 22) Twaona kielelezo chema katika Wanethimu na wageni wengine walioamini wakati wakweapo pamoja na baki ili kutegemeza kwa moyo wote ibada ya Yehova. (2:43, 55) Fikiria, pia, toba ya unyenyekevu ya watu waliposhauriwa juu ya mwendo wao wenye kosa katika kuoana na majirani wapagani. (10:2-4) Mashirika mabaya yaliongoza kwenye kupoteza kibali cha kimungu. (9:14, 15) Bidii ya shangwe kwa ajili ya kazi yake ilileta kibali na baraka zake.—6:14, 21, 22.
18. Ni kwa nini kurejeshwa kwa watu wa Yehova ni hatua ya maana yenye kuongoza kwenye kutokea kwa Mesiya, Mfalme?
18 Ingawa mfalme hakuketi kamwe kwenye kiti cha enzi cha Yehova kule Yerusalemu, kurejeshwa kuliamsha tazamio kwamba Yehova kwa wakati wake angetokeza Mfalme wake aliyeahidiwa katika ukoo wa Daudi. Taifa hilo lililorejeshwa sasa lilikuwa katika hali ya kulinda matamko rasmi matakatifu na ibada ya Mungu hadi wakati wa kutokea kwa Mesiya. Kama baki hilo halingeitikia kwa imani kwa kurejea katika bara lao, Mesiya angekuja kwa nani? Kweli kweli, matukio ya kitabu cha Ezra ni sehemu ya maana ya historia inayoongoza kwenye kutokea kwa Mesiya na Mfalme! Ni chenye mafaa kabisa kwa ajili ya utafiti wetu leo.
[Maelezo ya Chini]
a Insight on the Scriptures, Vol.1, pages 452-4, 458.
b Insight on the Scriptures, Vol.2, page 332.
c Insight on the Scriptures, Vol.2, page 1079