Mambo Makuu ya Biblia Esta 1:1–10:3
Taifa Laokolewa na Mungu Lisiangamizwe
Mauaji ya kushtua yatafanyika bila tatizo: vijana kwa wazee, watoto kwa wanawake, waangamizwe bila kuachilia ye yote. Hakuna mtu atakayethubutu kupinga hila hiyo, kwa maana agizo la kuua lina muhuri ya mfalme. Ndiyo, Wayahudi watakufa kama mifugo walio hoi!
Angalau hayo ndiyo maoni ya Hamani, waziri mkuu wa Uajemi ya kale. Yeye ametunga mpango huo wa kuua halaiki ya watu kwa sababu ya kumchukia Mordekai Myahudi bila akili. Lakini wakati Hamani anapongojea ushindi kwa kinaya, taifa la Kiyahudi linasali kuomba likombolewe. Matokeo yanakuwa nini? Yanafunuliwa katika kitabu cha Biblia cha Esta chenye mambo ya kutazamisha. Kitabu hicho kiliandikwa na Mordekai mwenyewe, nacho ni masimulizi yenye kutia imani nguvu juu ya jinsi usaidizi wa kimungu—na imani ya mwanamke kijana—ulivyookoa taifa.
Esta Anakuwa Malkia
Tafadhali soma Esta 1:1–2:23. Karibu na mwaka 484 K.W.K., mfalme Mwajemi Ahasuero (Sakse wa Kwanza) anaandaa karamu kubwa. Lakini Malkia Vashti anakataa kutii miito yake ya kuja karamuni. Mfalme huyo mwenye hasira nyingi anamnyang’anya cheo chake na kuanza kutafuta malkia mwingine. Baada ya kukagua wanawake walio warembo zaidi katika milki hiyo, anachagua mwanamke ambaye jina lake ni Hadasa, naye ametayarishwa na Mordekai binamu yake kwa ajili ya daraka hilo. Mwanamke huyo kijana anaficha jambo la kwamba yeye ni Myahudi, huku akitumia jina lake la Kiajemi, Esta.
♦ 1:3-5—Kwa sababu gani sherehe hizo zilifanywa?
Kulingana na mwanahistoria Herodoto, wakati mmoja Sakse aliita kusanyiko lipange shughuli ya kijeshi dhidi ya Ugiriki. Labda kusanyiko hili linalofanyika sasa ndilo lililotajwa na mwanahistoria huyo. Inaelekea kuwa Sakse alijionyesha kwa kuwafanya waone utukufu na utajiri mwingi wa ufalme wake ili kusadikisha wakubwa hao kwamba alikuwa na uwezo wa kuitekeleza shughuli hiyo dhidi ya Wagiriki.
◆ 1:8—Sheria ilisema nini juu ya kunywa?
Inaelekea kuwa kwamba Waajemi walikuwa na desturi ya kuhimizana wanywe kiasi fulani kilichotajwa wazi kwenye makusanyiko ya namna hiyo. Lakini, katika pindi hii mfalme hakutaka iwe hivyo. Kama hatua hiyo ilifanya watu wanywe kwa kiasi au kwa njia isiyo ya kujizuia, Biblia haisemi.
◆ 2:19, 20—Kwa sababu gani Mordekai ‘aliketi katika lango la mfalme’?
Inaonekana Mordekai alikuwa mmoja wa maafisa wa Mfalme Ahasuero. Kwa ujumla wanaume wenye mamlaka namna hiyo waliketi langoni, wakingoja hapo ili waweze kuitikia wakiombwa na mfalme wafanye jambo fulani. Bila shaka cheo cha Mordekai kilikuwa chenye daraka kubwa. Au sivyo, Hamani angaliweza kuwa amemfukuza bila kukawia. Hivyo Mordekai alikuwa katika cheo cha kuweza kupata habari za hila yenye kutungwa kuua mfalme kisha aitangue.
Somo Kwetu Sisi: Esta alionyesha ubora wa kuwa na kiasi kwa kutokuomba vito vya thamani au mavazi mazuri kabla ya kuingia mbele ya mfalme. Yeye aliuacha utu wa siri wa moyo wake, pamoja na “roho ya upole na utulivu” ya utu huo, impatie upendeleo wa mfalme. (1 Petro 3:1-5) Kwa njia inayofanana na hiyo, wale wa mabaki wapakwa mafuta waliokusanywa tangu mwaka 1919 wamejipatia upendeleo wa Mfalme Yesu Kristo.
Hila Aliyoitunga Hamani
Soma 3:1–5:14. Ahasuero anamfanya awe waziri mkuu Mwamaleki anayeitwa Hamani. Lakini Mordekai, kwa kukumbuka kwamba Yehova alikuwa ameamua kabisa ‘kuwa na vita na Amaleki kizazi baada ya kizazi,’ anakataa kumsujudia Hamani. (Kutoka 17:8-16) Kwa kulipa kisasi, Hamani mwenye kiburi anamsihi mfalme awaangamize Wayahudi!
Mordekai anamwomba Esta akatize jambo hilo, akimkumbusha kwamba, akinyamaza, “ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine.” Kwa kuwa hali ya wakati ujao ya watu wa Yehova na hukumu yake dhidi ya Waamaleki inahusika, Mordekai ana uhakika kwamba Mungu atatoa njia ya kuokokea. (1 Samweli 12:22) Esta anamfikia mfalme bila kuombwa afanye hivyo—jambo linaloweza kufanya mtu apewe adhabu ya kifo! Ingawa hivyo, Ahasuero anampa haki ya kubaki hai naye anahudhuria karamu inayoandaliwa na Esta. Hamani anaporudi nyumbani anapanga kumuua Mordekai akiwa amekasirika tena kwa sababu Mordekai amekataa kumsujudia.
◆ 3:7—Ni nini kilichohusika katika kutupa kura ya Puri?
Inaonekana kwamba “Puri” ni neno la Kiajemi linalomaanisha “kura ya kutupwa.” Mara nyingi kura zilikuwa zikitupwa na wanajimu kama namna fulani ya uaguzi. Inaelekea kwamba jambo hilo lilifanywa ili kuamua wakati uliomfaa kabisa Naamani atekeleze mpango wake wa kuliangamiza taifa.
◆ 4:3—Kwa sababu gani Mordekai na Wayahudi walifunga?
Kwa sababu mabaya ya kitaifa yalikuwa yakikaribia sana, huo ulikuwa wakati wa mawazo mazito, yenye huzuni. (Mhubiri 3:4) Walihitaji sana uongozi wa kimungu. Hivyo kufunga kulimaanisha kumgeukia Yehova ili wapewe nguvu na hekima iliyohitajiwa. Unapokabiliwa na majaribu, je! wewe pia unamgeukia Mungu katika sala?—Waebrania 5:7.
◆ 5:6-8—Kwa sababu gani Esta alikawia kumpasha mfalme habari?
Hakika ushujaa wa Esta haukumkatisha tamaa, kwa kuwa alikuwa amekwisha kujijasirisha kuelekeana na kifo. Lakini, labda kwanza alitaka kujipatia nia njema ya mfalme. Kwa hiyo, Esta alimkaribisha mfalme kwenye karamu ya pili. Mwelekezo wa kimungu ulihusika pia, kwa kuwa kipindi kilichokuwa kati ya karamu ya kwanza na ya pili kiliruhusu matukio fulani yatendeke.
Somo Kwetu Sisi: Esta alionyesha imani, ushujaa, na nia ya kufuata shauri la Mordekai. Wale ambao wamekuwa sehemu ya mabaki wapakwa mafuta tangu mwaka 1919 wameonyesha imani, ushujaa, na nia inayolinganika na hiyo ili wafanye kazi pamoja na washiriki wenye umri mkubwa zaidi wa bibi-arusi wa Kristo. Ni mifano myema kweli kweli!
Hila Iliyotungwa Yatanguliwa
Soma 6:1–7:10. Ahasuero anapatwa na hali ya kukosa usingizi, bila shaka ikiwa imetokezwa na Mungu. Akihisi kuna uwezekano wa kwamba ameshindwa kufanya jambo fulani vizuri, anaagiza kwamba asomewe kitabu cha kumbukumbu, labda jarida la kifalme la maandishi ya kila siku. Anapogundua kwamba Mordekai hakupewa thawabu alipofunua hila ya kumuua mfalme, mfalme anamwomba Hamani apendekeze thawabu inayofaa. Hamani anajiwazia kuwa ndiye amehesabiwa heshima ya kupewa thawabu hiyo, naye anapendekeza kuwe na sherehe yenye mambo mengi. Lakini anagutuka ajabu anapoamriwa ampe Mordekai heshima hizo! Washauri wa Hamani wanaiona hiyo kuwa dalili mbaya ya kwamba atapatwa na anguko.
Mara tu tukio hilo lenye kushusha heshima yake linapomalizika, Hamani anasindikizwa kwenye karamu ya pili ya Esta. Kule mfalme anamkaribisha Esta aombe anachotaka. “Nipewe maisha yangu kuwa dua yangu, na watu wangu kuwa haja yangu,” anaomba malkia huyo shujaa. Akifunua kwamba yeye ni mwanamke Myahudi, anaisema wazi hila iliyotungwa na Hamani. Hamani mwenye hofu nyingi anaomba sana uhai wake uachiliwe lakini anauawa—juu ya mti ule ule uliokusudiwa Mordekai!’
◆ 7:4—Kwa sababu gani kuharibiwa kwa Wayahudi kungeletea mfalme hasara?
Kama Hamani angalitunga mpango wa kuwauza Wayahudi utumwani, inaelekea kwamba jambo hilo lingalimletea Ahasuero faida kubwa. Lakini uharibifu wa taifa zima ungeleta hasara ya kifedha iliyo kubwa kuliko zile talanta 10,000 ambazo Hamani alikuwa ameahidi kulipa. Kama hila iliyotungwa kuangamiza taifa zima ingalifanikiwa, mfalme angalimpoteza malkia wake pia—hasara ya kibinafsi kweli kweli!
◆ 7:8—Kwa sababu gani uso wa Hamani ulifunikwa?
Si Hamani aliyejifunika mwenyewe uso kwa sababu ya aibu au majonzi. Kwa wazi maafisa wa nyumba ndio waliomfunika uso, labda hiyo ikiwa ni njia ya kufananisha hali ya kuaibisha au msiba wa kuangamizwa. Inaelekea kwamba hiyo ndiyo hatua ya kwanza iliyochukuliwa katika kutekeleza hukumu ya kifo.
Somo Kwetu Sisi: Ajapohatarisha uhai wake, Esta alitumia alifunua kwa ushujaa kwamba ni Myahudi. Tangu mwaka 1931, watu wa Mungu pia wamejijasirisha kupatwa na mateso kwa kujitangaza kuwa Mashahidi wa Yehova! (Isaya 43:10-12) Je, wewe ni shujaa kadiri hiyo?
Watu wa Mungu Waokolewa!
Soma 8:1–10:3. Mordekai anakuwa waziri mkuu badala ya Hamani. Akijasirisha uhai wake tena, Esta anamfikia mfalme bila kukaribishwa na kuomba kwamba hatua zichukuliwe ili kuuharibisha mpango uliokusudiwa na Hamani. Mfalme anakubali na kumruhusu Mordekai aagize kwamba amri ya kupinga hiyo iandikwe kwa jina la Ahasuero. Ingawa kulingana na desturi ya Kiajemi agizo lile la kwanza la kuangamiza Wayahudi haliwezi kufutwa, sheria mpya hii inawaruhusu Wayahudi wajitetee.
Sauti za shangwe zinatokea kati ya Wayahudi! Kwa kuwa wao si mawindo hoi tena, sasa wana miezi kadha ya kutengeneza utetezi wao. Mwishowe, tarehe ya 13 ya mwezi Adari (Februari-Machi) inafika. Watu kama 75,000 ‘waliowachukia’ wanauawa na Wayahudi. Ili wasije wakasahau kwamba ushindi huo uliletwa na Yehova, Mordekai anatoa amri kwamba Sikukuu ya Purimu ya kila mwaka ifanywe tarehe 14 na 15 za mwezi Adari.
◆ 8:5—Esta alionyeshaje utambuzi?
Esta alipima maneno yake kwa uangalifu, akamsihi mfalme aharibishe hati za Hamani mpanga ubaya, ‘alizoziandika yeye’ (NW) Esta alitumia busara kwa kuepuka kutaja kwa njia yo yote kwamba mfalme alihusika katika kuandikishwa kwa jambo hilo. Vivyo hivyo Wakristo wanatumia busara wanapotoa ushahidi mbele ya maafisa wa serikali.
◆ 8:17 (NW)—Watu ‘walijitangazaje kuwa Wayahudi’?
Biblia ya Septuagint inasema kwamba Waajemi hao “walikuwa wakitahiriwa na kugeuka wafuate Uyahudi.” Kwa wazi Waajemi wengi waliliona tendo la kuandikwa kwa amri ya kupinga ile ya kwanza kuwa ishara ya kwamba Mungu alikuwa akiwaunga mkono Wayahudi, na hivyo wao wakawa waongofu wa Kiyahudi. Vivyo hivyo leo, “mkutano mkubwa” wa “kondoo wengine” wamechukua msimamo wao kando ya mabaki wapakwa mafuta.—Ufunuo 7:9; Yohana 10:16; Zekaria 8:23.
◆ 9:10, 15, 16—Kwa sababu gani Wayahudi hawakuteka nyara?
Amri ya mfalme iliwapa mamlaka ya kuteka nyara. Lakini, kukataa kwao kufanya hivyo kulionyesha wazi kwamba kusudi lao lilikuwa kujihifadhi wenyewe, wala si kujitajirisha.
Somo Kwetu Sisi: Kama Wayahudi wa siku za Esta, Kwa kufaa Mashahidi wa Yehova wanasihi serikali na mahakama ziwalinde na adui. Hasa wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili kulikuwa na uhitaji mkubwa wa kufanya hivyo kwa sababu ya mashambulio yaliyochochewa na viongozi wa kidini dhidi ya watu wa Mungu. Kwa baraka ya Yehova, wamejipatia ushindi katika mimenyano mingi mikubwa ya mahakamani.
Kitabu cha Esta kinatumika kuwa chanzo cha tumaini na kitiamoyo kwa Mashahidi wa Yehova leo. Wao wanajua kwamba chuki nyingi sana anayowaonea Shetani itafikia upeo karibuni kwa kuwafanyia jaribio la kufa au kupona akitaka kuwaangamiza. Bado inangonjwa ionwe ni njia gani hasa atakayoitumia Yehova kulinda watu wake. (Ezekieli 38:16-23) Lakini tumaini lao hakika ni kwamba, kama ilivyokuwa katika siku za Esta, Yehova hatawaacha watu wake. Katika wakati unaofaa, yeye atawaandalia “msaada na wokovu.”