Wala Theluji Wala Mvua Wala Wingi Havizuii Upelekaji Barua
“Maadamu kuna wapelekaji barua, maisha yatasisimua.” —William James, mwanafalsafa wa U.S. (1842-1910)
KARIBU kila mtu ana hadithi ya kuudhi ya kusema kuhusu huduma ya upelekaji barua. Barua aliyopeleka iliwasili ikiwa imechelewa majuma au hata miezi kuliko vile ilivyotazamiwa, gharama za posta zinapanda upesi sana, au kungoja kwenye foleni katika posta huchosha. Kule nyuma katika Oktoba 1966, msiba ulitisha mfumo wa posta. Msemaji wa Huduma ya Posta wa U.S. aliliambia Amkeni! kwamba “lile lililokuwa wakati huo jengo kuu zaidi la posta la U.S., lililo kwenye njia panda jijini Chicago, lilikuwa karibu lifungwe liliposongamana kwa barua na likashindwa kuzishughulikia.”
Ni nini kimefanywa ili kuhakikisha kwamba upelekaji barua haukomi na kwamba barua yako itafika? Je! kuna jambo lolote unaloweza kufanya ili kufanyia maendeleo utumishi unaopokea? Je! njia za kupeleka barua na kutegemeka kwazo zimebadilika sana kwa muda wa karne?
Huduma ya Posta ya Kale
Huduma ya posta iliyopangwa ya mapema zaidi ilikuwa kwa ajili ya utumizi wa serikali pekee. Mifumo hiyo ilikuwako Uchina, Misri, Ashuru, Umedi, na Ugiriki ya kale. Mfumo wa posta wa Kirumi uliitwa cursus publicus, kihalisi “njia ya umma”; hata hivyo, hiyo kwa msingi ilikuwa kwa ajili ya huduma ya serikali pekee. Kwa kupendeza, barua za mwandikaji wa Biblia Paulo kwa makundi katika Efeso na Kolosai, na kwa Filemoni zilipelekwa kwa mipango ya binafsi na si kwa huduma ya posta ya serikali ya Rumi.—Waefeso 6:21, 22; Wakolosai 4:7-9; Filemoni 21, 22.
Ingawa usafirishaji na upelekaji wa barua haukubadilika sana hadi karne ya 19, maoni kuhusu kudhibiti au kuondoa huduma ya kibinafsi ya kupeleka barua yalianza kutokea mapema. Kwa nini? Kwa sababu wenye mamlaka waliona uhitaji wa usimamizi wa uwasiliano wa faragha. Katika kitabu chake The Universal Postal Union, George A. Codding, Jr., atoa sababu mbili kuu za kufanyizwa kwa usimamizi wa pekee wa serikali juu ya huduma za posta. Kwanza, mapato yalikuwa “njia bora ya kuimarisha huduma rasmi.” Pili, ulinzi uliotolewa ulisaidia katika kudhibiti mawasiliano ya maadui wa Taifa.
Hivyo, Posta ya Kifalme ya Ufaransa ilianza kushughulikia barua za umma mwaka 1464. Katika 1635, Charles 1 wa Uingereza alianzisha huduma ya Kifalme ya Upelekaji Barua kwa umma. Serikali nyinginezo zilifanya vivyo hivyo na hivyo huduma ya posta ikashughulikiwa nazo pekee, zikidhibiti mbadilishano huo kati ya watu.
Uingereza ilisimamia mfumo wa mapema wa Amerika, kama vile ambavyo Milki ya Rumi ilivyokuwa imeeneza kazi yayo ya posta hadi Uingereza. Mfumo wa Rumi ulifanana sana na ule wa Umedi, ambao ulikuwa mfumo wa posta wa wapelekaji barua kwa farasi wakifanya kazi kwa kupokezana ulioanzishwa katika karne ya sita K.W.K. Hivyo, mambo mengi ya mifumo mingi ya posta yalianzia Umedi.
Mfumo wa posta wa Amerika wa kikoloni ulianza rasmi kushu-ghulikia barua za ng’ambo katika 1639, na barua za nchini, kati ya Boston na Jiji la New York, katika 1673. Njia hiyo ya barua ambayo haikudumu sana ilikuja kuitwa Barabara ya Posta ya Boston, sasa sehemu ya Barabara Kuu 1 ya U.S. Kufikia katikati ya karne ya 19, barua zilikuwa zikisafirishwa kwa gari la kukokotwa kwa farasi, mashua, na garimoshi. Kupelekwa kwa barua hadi San Francisco, California, kutoka Jiji la New York kulichukua karibu mwezi mmoja au zaidi kwa meli na muda mrefu zaidi kwa gari la kukokotwa kwa farasi.
Upelekaji Barua Upesi kwa Farasi
Ili kuharakisha upelekaji barua barani katika United States, jambo jingine badala ya gari la kukokotwa kwa farasi na meli lilihitajiwa. Utatuzi ungekuwa nini? Njia iliyotumiwa kwa karne nyingi ya mpelekaji barua na farasi ilitumiwa. History of the U.S. Postal Service 1775-1984 chanukuu matangazo ya gazeti kutoka Machi 1860:
“Watakikana: Vijana wembamba, wenye nguvu wasiozidi miaka 18. Lazima wawe waendeshaji farasi stadi walio tayari kujihatirisha kufa kila siku. Mayatima wapendekezwa.”
Wale walioajiriwa “waliwajibika kuapa kwa Biblia wasilaani, wasipige, au kutenda vibaya wanyama wao na kujiendesha kwa unyoofu.” Huo ndio uliokuwa upelekaji barua upesi kwa farasi wenye umashuhuri, ambao ulipunguza wakati wa upelekaji kufikia siku kumi kwenye njia ya kilomita 3,200 kati ya St. Joseph, Missouri, na pwani ya magharibi mwa United States. Kupanda farasi kwa kasi kabisa kwa kilomita 15 hadi 25, kisha kubadilisha farasi bila kuchelewa, wapandaji hao wachanga walienda kasi juu ya milima, nyanda, na mito katika kila aina ya hali ya anga. Katika muda wote wa kuwapo kwa upelekaji barua upesi kwa farasi, kwa sababu ya kuwa na farasi wenye kwenda kasi sana, wapelekaji barua wenye kujasiria waliwaacha mbali Wahindi na majangili; hata hivyo, mpandaji farasi mmoja aliuawa.
Hekaya imeongeza sifa kwa huduma hiyo ya posta yenye ujasiri, iliyoendelea kuanzia Aprili 3, 1860, hadi Oktoba 26, 1861. Iliacha kufanya kazi huduma ya simu ya barani ilipoanza, hivyo ikikomesha mojawapo sehemu zenye kuvutia zaidi za historia ya upelekaji barua ya Amerika.
Njia za Kisasa
Acheni tupeleke barua leo na tuone jinsi inavyoshughulikiwa. Wakati wa kuipeleka waweza kutofautiana ikitegemea jinsi unavyotumia huduma hiyo.
Unapomaliza kazi yako ya siku, barua zilizorundamana hupelekwa. Kwa kuwa hiyo ndiyo kawaida yetu, barua nyingi huingia mkondo wa posta katika sehemu ya mwisho wa siku. Hivyo, kupeleka barua mapema katika siku kunakunufaisha kwa saa chache na kunaweka barua zako mstari wa mbele wa barua nyingi. Katika 1991, kiasi cha wastani cha kila siku cha barua hizo katika United States kilikuwa barua milioni 454, barua milioni 13.3 zikienda Jiji la New York; Ufaransa, barua milioni 71, milioni 5.5 zikienda Paris; Japan, milioni 62.5, milioni 17 zikienda Tokyo; na Uingereza, milioni 60.
Barua zinazotiwa katika sanduku barabarani au katika posta ndogo hupelekwa kwenye posta kubwa zaidi. Kutia barua yako kabla tu ya wakati wa kukusanywa na, ikiwezekana, karibu na posta kubwa zaidi, huharakisha kupelekwa kwayo.
Kwenye posta ya kwenu, barua yako huwekwa kwenye mfuko, kisha inapelekwa hadi kwenye kituo cha posta kiitwacho kituo cha eneo ambapo vifaa vya otomatiki vya kupambanua barua hutumiwa. Hapa, kwa msaada wa mashine zilizofanyizwa kwa ustadi, barua huchanwa na kugeuzwa kiotomatiki zinapoenda juu ya mishipi ya kuchukulia vitu na kuchaguliwa, kupangwa, kupigwa muhuri, kuchanganuliwa, na kuomekwa. Kifaa kimoja kama hicho, kiitwacho mashine ya kupiga muhuri, hushughulikia kwa kasi barua 27,000 kwa saa kikitia muhuri na kutia alama ya posta.
Wakati wa alasiri na kuendelea hadi usiku, barua zinazopelekwa huchanganuliwa. Barua zenye anwani zinazosomeka kwa urahisi—ambazo zimepigwa kwa taipureta, zimechapwa, au zimeandikwa kwa mkono—zaweza kuchanganuliwa kwa mashine. Mashine mpya zaidi huweza kusoma mistari miwili yenye nambari ya eneo au ya posta; jiji, jimbo, au wilaya; na anwani ya barabara.
Mashine hizo na vifaa vinginevyo vyaweza “kusoma” kiotomatiki anwani na kuchapa nambari za pekee za barua kwenye maelfu ya barua kwa saa. Barua za haraka ambazo haziwezi kushughulikiwa na mashine lazima zichanganuliwe kwa mkono, kwa wastani wa barua 800 kwa saa. Anwani inayosomeka kwa urahisi, yenye nambari ya eneo katika United States (nambari ya posta katika nchi nyinginezo nyingi) huruhusu barua yako ishughulikiwe kwa njia za haraka, zenye matokeo zaidi.
Barua zinazoenda hupelekwa kwa ndege au gari. Barua za haraka kwa kawaida hupelekwa usiku-kucha kwenye majiji na vituo vya eneo hususa, katika muda wa siku mbili kwenye majimbo ya karibu yaliyoonyeshwa, na katika siku tatu mahali pengine popote katika United States. Katika Uingereza, asilimia 90 ya barua za haraka zapaswa kuwa zimepelekwa siku ya kazi inayofuata na asilimia 97.4 ya barua zisizo za haraka kufikia siku ya tatu. Uchunguzi wa posta wa Ufaransa uliochapishwa katika Mei 1992 ulionyesha kwamba asilimia 81 ya barua za humohumo nchini zilipelekwa usiku-kucha na kwamba asilimia 96.3 ya vifaa vya posta vilipelekwa katika muda wa siku mbili, bila kutia Jumapili na sikukuu. Hivyo, usiku sana barua hizo zinazopelekwa huwa zinaingia kwenye vituo vinavyoshughulikia barua za eneo na kisha kwenye posta zinakoenda. Usiku wote hadi mapema asubuhi, barua zinazoingia huchanganuliwa ili zipelekwe.
Wateja wakubwa wa posta, kama vile Watchtower Society, hutayarisha barua zao ili posta izikubali zikipelekwa kwa trela kutoka kwenye makao ya mpelekaji. Barua hizo husafirishwa na posta moja kwa moja nchini kote hadi kwenye wafanyakazi wa posta wenye kuzipeleka. Huduma za posta zinazidi kutumia njia za mawasiliano ya haraka zaidi, kama vile barua za umeme (barua za umeme; habari inayopelekwa kwa kompyuta kwa njia ya simu). Mfumo wa Ufaransa ulipeleka barua za umeme milioni kumi mwaka jana.
Ingawa taratibu za posta huenda zikatofautiana nchi kwa nchi, barua nyingi za ulimwengu hushughulikiwa kwa njia inayofanana na ile ambayo tumeeleza ya Huduma za Posta za U.S., ambazo hushughulikia asilimia 40 ya barua zote za ulimwengu.
Huduma Nyinginezo za Posta
Mifumo ya posta huandaa huduma zaidi ya kupeleka barua. Posta ya U.S. itakusaidia kupata pasipoti. Unaweza kuweka akiba katika posta ya Japan au Girobank ya Uingereza (iliyokuwa ikimilikiwa na huduma za posta za Uingereza). Pia, mali inayopelekwa yaweza kufanyiwa bima au kusajiliwa ili gharama ilipwe iwapo inapotea au kuharibiwa. Ikiwa kitu kinachopelekwa chahitaji ithibati tu ya kukipeleka, hakigharimu sana ikiwa kinapelekwa kikiwa kimeidhinishwa kuliko ikiwa kinasajiliwa. Watu wanaweza kupata bima ya maisha kutoka kwa huduma ya posta ya Japan.
Zinapoombwa, posta fulani, kama zile za United States, zitakuandalia habari za kusahihisha anwani. Andika “Maombi ya Kusahihisha Anwani” au “Usipeleke” kwenye upande wa mbele wa bahasha chini tu ya anwani yako. Bila gharama ya ziada, barua za haraka zitarudishwa kwako zikiwa na anwani mpya (ikiwa haizidi muda wa mwaka mmoja) au na sababu nyingine kwa kutoipeleka.
Kwa ajili ya huduma hiyo na nyinginezo, ulimwengu unategemea sana mfumo wa posta. Ripoti ya Evaluation of the United States Postal Service husema: “Huduma ya posta inafanya kazi nzuri kwa kushughulikia kiasi kikubwa cha barua, lakini makosa ambayo hayawezi kuondolewa yapaswa kuendelea kuonyeshwa ili umma ujue mambo halisi ya kutazamia kutoka kwa posta.” Katika United States, ikiwa asilimia 5 tu ya barua za haraka karibu 250,000,000 za kiasi cha kila siku zinacheleweshwa, hiyo hujumlika kuwa barua zaidi ya 12,000,000 kwa siku. Hiyo hutokeza malalamiko mengi ya kuchelewa kupelekwa.
Hali za kiuchumi zisizofaa zimeathiri mifumo ya posta. Gharama zinazopanda, vifaa vinavyoharibika, barua zilizocheleweshwa, na tekinolojia ya kisasa zilichochea kushindana na huduma zilizodhibitiwa na serikali. Ingawa njia za kisasa zimefanyia maendeleo ushughulikiaji barua, mkazo ulio juu ya mashirika yote hufanya mifumo ya posta ifanye kazi chini ya mkazo. Huduma ya Posta ya U.S. ilikuwa na kasoro ya dola za huko 1,500,000,000 katika 1991. Hatua kubwa, kama vile kuongeza gharama za kupeleka barua na kupunguza wafanyakazi, huenda zikahitajiwa ili kuendelea kutoa huduma za sasa.
Kuanzia na mtiririko mdogo katika nyakati za kale hadi kijito kinachofurika leo, barua zinazidi kuongezeka kujapokuwa matatizo, hivyo zikitosheleza uhitaji uliorithiwa wa kuwasiliana.—Imechangwa na mfanyakazi wa posta.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]
Kupeleka Barua Mtindo wa Kiajemi
Mahali penyewe ni milki ya Uajemi ya kale. Hati zilizoandikwa zilitayarishwa kwa uangalifu, zikatiwa muhuri rasmi, na kupelekwa kwa huduma za posta za serikali. Watu wengi wangekufa ikiwa amri hazingepelekwa mara hiyo na kufuatwa bila kukawia. Lakini barua hizo zingepelekwaje? “Barua hizo zilipelekwa na matarishi walioendesha farasi zilizotoka kwa mazizi ya mfalme. . . . Kwa hiyo matarishi hao wakiwa juu ya farasi za kifalme, walitumwa kwa kasi sana wakiwa na amri ya mfalme ya haraka,” yasema The New English Bible, kwenye Esta 8:10, 14.
Wapandaji hao wenye kupokezana waliotegemeka, wakiwa na farasi waliowekwa tayari kwa umbali wa karibu kilomita 23, walikuwa njia iliyopendelewa ya kupeleka amri ya kupinga ya Mfalme Ahasuero ambayo ingeokoa Wayahudi wasiuawe wakati wa karne ya tano K.W.K. Mwanahistoria Herodotas alisema kwamba wapelekaji barua hao “hawakuzuiwa kumaliza mwendo walioenda kwa kasi sana, wala kwa theluji, wala mvua, wala joto, wala giza la usiku.” Huo ulikuwa mfumo wa mawasiliano wa serikali wa kila siku ulioendeshwa kotekote katika Milki ya Uajemi.
[Picha katika ukurasa wa 17]
Mashine husoma herufi na kuchanganua kiotomatiki maelfu ya barua kwa saa
[Hisani]
Picha ya USPS