“Ni Nani Aliyetia Hekima Katika Safu za Mawingu”?
“MWONAPO wingu likizuka katika sehemu za magharibi, mara moja nyinyi husema, ‘Dhoruba inakuja,’ na huwa hivyo. Nanyi mwonapo kwamba upepo wa kusini unavuma, nyinyi husema, ‘Kutakuwa na wimbi la joto,’ nalo hutukia.” Maneno haya ya Yesu yaliyoandikwa na mwandikaji wa Gospeli Luka, ni vielelezo vya utabiri mbalimbali wa hali ya hewa kama ulivyofanywa huko Palestina ya kale. (Luka 12:54, 55) Katika hali fulani, watu wa kale wangeweza kusoma ishara na kutoa utabiri sahihi wa muda mfupi.
Leo, wanaoshughulika na hali ya hewa hutumia vifaa vya hali ya juu kama vile setilaiti zinazozunguka dunia, rada ya Doppler, na kompyuta zenye uwezo mwingi, ili kupima mielekeo ya hali ya hewa kwa vipindi virefu. Lakini mara nyingi utabiri wao huwa na makosa. Kwa nini?
Mambo mengi hufanya isiwe rahisi kutabiri hali ya hewa kwa usahihi. Kwa kielelezo, mabadiliko yasiyotazamiwa ya joto, unyevuanga, kanieneo ya hewa, na mwendo wa upepo na upande uendako, hivi vyote vyaweza kufanya mambo yawe magumu. Kwa kuongezea hayo, kuna maingiliano ya jua, mawingu, na bahari, ambayo wanasayansi hawajaelewa kikamili. Kwa sababu hiyo, utabiri wa hali ya hewa bado ni sayansi isiyo sahihi.
Ujuzi mdogo wa mwanadamu kuhusu hali ya hewa watukumbusha maswali aliyoulizwa Ayubu: “Ni nani aliyeyazaa matone ya umande? Kwa kweli barafu yatoka katika tumbo la nani? . . . Waweza kupaaza sauti yako hata kwenye wingu, ili wingi wa maji yavurumikayo ukufunike? . . . Ni nani aliyetia hekima katika safu za mawingu, au ni nani aliyeelewesha ajabu za anga? Ni nani awezaye kuyahesabu mawingu hasa kwa hekima au ni nani awezaye kuzimimina chupa za maji za mbinguni?”—Ayubu 38:28-37, NW.
Jibu la maswali haya yote ni, Si mwanadamu bali ni Yehova Mungu. Naam, hata wanadamu wawe wanaonekana kuwa na hekima jinsi gani, hekima ya Muumba wetu ni kuu sana. Kwa kweli ni jambo lenye upendo kwake kutujulisha hekima yake katika Biblia, ili tuweze kufanikisha njia yetu.—Mithali 5:1, 2.