Mti Ambao Huimba
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KENYA
KATIKA mbuga pana za Afrika mna mti ambao huimba. Mti huo ni jamii ya mkakaya nao huitwa whistling thorn, au mti ambao huimba. Kwa nini? Kwa sababu upepo uvumapo, matawi yake mepesi huonekana kana kwamba yanatoa sauti inayofanana na mbinja.
Sauti tamu ya kujirudia-rudia hutokezwa wakati miiba yake mirefu sana na iliyo myembamba inapotikisika kwenye upepo. Kwa kuongezea wimbo huo wa miiba, vinundu vyenye mashimo vya mti huo hutokeza sauti inayofanana sana na sauti itolewayo wakati chupa iliyo tupu inapopuliziwa hewa mdomoni. “Ala” hizo hutengenezwa na chungu, ambao inasemekana hujenga vinundu hivyo, ambavyo ni makao ya chungu yenye umbo la tufe, na kutoboa milango midogo-midogo. Kwa sababu vinundu hivyo na milango hiyo hutofautiana kwa ukubwa, vinatoa sauti zenye mkazo tofauti-tofauti. Sauti hizo huongezea upekee na umaridadi wa mkakaya ambao huimba.
Mti huu hutukumbusha maneno ya mtunga-zaburi ambaye alitangaza hivi kitamathali: “Miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha mbele za BWANA.” (Zaburi 96:12, 13) Kwa kweli, upepo uvumapo kupitia miiba na vinundu vilivyo kama filimbi, huo hutokeza wimbo mtamu wa Afrika wenye kuamsha hisia.