Blanketi la Kipupwe
JE, UMEPATA kukazia macho, kuduwazwa na theluji inayoanguka? Ikiwa ndivyo, bila shaka utakubali kwamba haya ni mojawapo maono yenye kupendeza zaidi na yenye utulivu zaidi—hasa ukiwa salama na mwenye ujoto nyumbani na huna uhitaji wa haraka wa kusafiri. Kadiri blanketi jeupe liongezekapo, huonekana kusambaza amani na kimya chenye kina zaidi kila mahali. Hata makelele ya jiji huzimwa kadiri mamilioni ya magamba mepesi yaangukavyo.
Lakini, je, haishangazi sana jinsi kitu chenye uanana kama vile theluji yenye kuanguka iwezavyo kuangamiza? Majiji yenye shughuli nyingi kama vile New York—ambalo mara nyingi limefafanuliwa kuwa “jiji lisilolala kamwe”—yaweza kufanywa kuwa kimya theluji ikirundamana hadi juu kabisa.
Basi, haishangazi kwamba Mungu alimwuliza yule mtu mwaminifu Ayubu: “Je! umeziingia ghala za theluji, au umeziona ghala za mvua ya mawe, nilizoziweka akiba kwa wakati wa misiba, kwa siku ya mapigano na vita?” (Ayubu 38:22, 23) Kwenye udhibiti wa Muumba wayo, Yehova Mungu, theluji yaweza kuwa silaha yenye kutisha sana.
Hata hivyo, theluji mara nyingi huhifadhi uhai badala ya kuleta maangamizi. Kwa kielelezo, Biblia husema kwamba Mungu “ndiye atoaye theluji kama sufu.” (Zaburi 147:16) Theluji ikoje kama sufu? Biblia hutumia theluji na sufu kuwakilisha weupe na utakato. (Isaya 1:18) Lakini kuna ufanani mwingine wa maana. Theluji na sufu ni vihifadhi joto. The World Book Encyclopedia husema hivi: “Sufu . . . huhifadhi baridi na joto.” Na kwa habari ya theluji, World Book chaandika kwamba hiyo pia “hutumika kama kihifadhi joto kizuri. Theluji husaidia kulinda mimea na wanyama walio katika usingizi mzito kutokana na hewa yenye baridi ya kipupwe.”
Kwa hiyo, wakati ujao ukitazama theluji ikianguka kutoka angani, huenda ukataka kufikiria nguvu za Mungu zenye kutisha. Au huenda ukafikiria ulinzi mwanana aandaao anaposambaza blanketi jeupe juu ya uumbaji wake, kama vile tu mzazi mwenye upendo awezavyo kufunika mtoto wake kwa usalama kitandani.