Rehema ya Yehova Hutuokoa Kutoka Katika Hali ya Kukata Tamaa
“Ee Mungu, unirehemu, sawasawa na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, uyafute makosa yangu.”—ZABURI 51:1.
1, 2. Mmoja wa watumishi wa Yehova anaweza kuathiriwaje na dhambi nzito?
SHERIA ya Yehova haiwezi kuvunjwa bila hofu ya kupata adhabu. Hilo laonekana wazi kama nini tukitenda dhambi nzito dhidi ya Mungu! Ingawa huenda ikawa tumemtumikia Yehova kwa uaminifu kwa miaka mingi, kuvunja sheria yake kwaweza kusababisha hangaiko kubwa au mshuko wa moyo wenye kina. Huenda tukahisi kwamba Yehova ametuacha na kwamba hatustahili kumtumikia tena. Dhambi yetu huenda ikaonekana kama wingu kubwa mno linalozuia nuru ya upendeleo wa Mungu.
2 Wakati mmoja Mfalme Daudi wa Israeli wa kale alijipata mwenyewe katika hali hiyo. Hali hiyo ilikuaje?
Hatua Zisizofaa Zaweza Kuongoza Kwenye Dhambi Mbaya Sana
3, 4. Ni nini kilichompata Mfalme Daudi wakati wa pindi ya ufanisi?
3 Daudi alimpenda Mungu lakini alichukua hatua zenye kosa zilizoongoza kwenye dhambi nzito. (Linganisha Wagalatia 6:1.) Hilo laweza kutukia kwa binadamu yeyote asiyekamilika, hasa ikiwa ana mamlaka juu ya wengine. Akiwa mfalme mwenye ufanisi, Daudi alifurahia umaarufu na uwezo. Ni nani aliyethubutu kupinga neno lake? Watu wenye uwezo walikuwa tayari kumtumikia, na watu walikuwa na hamu ya kufanya alichoomba. Hata hivyo, Daudi alikosea kwa kujiongezea wake na kuwahesabu watu.—Kumbukumbu la Torati 17:14-20; 1 Mambo ya Nyakati 21:1.
4 Katika pindi hiyo ya ufanisi wa vitu vya kimwili, Daudi alitenda dhambi nzito dhidi ya Mungu na mwanadamu. Kwani, dhambi moja iliongoza kwenye nyingine kama nyuzi zenye kufumwa pamoja za nguo iliyobuniwa na Shetani! Huku Waisraeli wenzake walipokuwa wakipigana na Waamoni, kutoka juu ya dari yake Daudi alimtazama Bath-sheba, mke mrembo wa Uria, akioga. Uria akiwa vitani, Daudi aliamuru mwanamke huyo aletwe kwenye jumba lake la kifalme akafanya uzinzi naye. Ebu wazia mshtuko wake alipopata kujua kwamba mwanamke huyo alikuwa mja-mzito! Daudi alituma Uria aitwe, akitumaini kwamba Uria angetumia usiku huo pamoja na Bath-sheba na kumwona mtoto huyo kuwa wake mwenyewe. Ingawa Daudi alimfanya Uria alewe, Uria alikataa kulala na Bath-sheba. Akiwa amekata tamaa, Daudi alimpelekea kamanda Yoabu amri za siri za kumweka Uria kwenye mstari wa mbele vitani ambako kwa hakika angekufa. Uria aliuawa katika pigano, mjane wake akashika kipindi cha kawaida cha kuomboleza, na Daudi akamwoa kabla ya watu kupata kujua juu ya mimba yake.—2 Samweli 11:1-27.
5. Ni nini kilichotukia baada ya Daudi kutenda dhambi pamoja na Bath-sheba, na dhambi zake zilimwathirije?
5 Kupitia nabii Nathani, Mungu alifunua dhambi za Daudi akasema hivi: “Nitakuondokeshea uovu katika nyumba yako.” Basi, mtoto aliyezaliwa na Bath-sheba akafa. (2 Samweli 12:1-23) Mwana mzaliwa wa kwanza wa Daudi, Amnoni, alimnajisi dada nusu yake mwenyewe Tamari naye akauawa na ndugu ya Tamari. (2 Samweli 13:1-33) Absalomu, mwana wa mfalme, alijaribu kujitwalia kiti cha utawala akamfedhehesha baba yake kwa kufanya ngono na masuria wa Daudi. (2 Samweli 15:1–16:22) Vita ya wenyewe kwa wenyewe iliisha kwa kifo cha Absalomu na kwa huzuni nyingine zaidi kwa Daudi. (2 Samweli 18:1-33) Hata hivyo, dhambi za Daudi zilimnyenyekeza na kumfanya atambue uhitaji wa kukaa karibu na Mungu wake mwenye huruma. Tukikosea, acheni tutubu kwa unyenyekevu na kumkaribia Yehova.—Linganisha Yakobo 4:8.
6. Kwa nini Mfalme Daudi alikuwa na hatia hasa?
6 Daudi alikuwa na hatia hasa kwa sababu alikuwa mtawala Mwisraeli aliyeifahamu Sheria ya Yehova kikamili. (Kumbukumbu la Torati 17:18-20) Hakuwa farao wa Misri au mfalme wa Babuloni waliokosa ujuzi huo na ambao huenda ikawa walifanya kwa kawaida mambo yasiyokubaliwa na Mungu. (Linganisha Waefeso 2:12; 4:18.) Akiwa mshiriki wa taifa lililowekwa wakfu kwa Yehova, Daudi alijua kwamba uzinzi na uuaji wa kimakusudi zilikuwa dhambi mbaya sana. (Kutoka 20:13, 14) Wakristo pia wanajua sheria ya Mungu. Hata hivyo, kama vile Daudi, wengine wao huivunja kwa sababu ya hali yenye dhambi ya asili, udhaifu wa kibinadamu, na kishawishi kisichokingwa. Hilo likitokea kwa yeyote kati yetu, hatuhitaji kubaki katika hali ya giza inayofanya kuona kwetu kiroho kusiwe dhahiri na inayofanya tufunikwe na hali ya kukata tamaa sana.
Kuungama Huleta Kitulizo
7, 8. (a) Ni nini kilichompata Daudi alipojaribu kuficha dhambi zake? (b) Kwa nini mtu aungame na kuacha dhambi yake?
7 Ikiwa tuna hatia ya makosa mazito dhidi ya sheria ya Mungu, huenda tukaliona kuwa jambo gumu kuungama dhambi zetu, hata kwa Yehova. Ni nini laweza kutukia chini ya hali hizo? Katika Zaburi 32, Daudi alikiri hivi: “Niliponyamaza [badala ya kuungama] mifupa yangu ilichakaa kwa kuugua kwangu mchana kutwa. Kwa maana mchana na usiku mkono wako [wa Yehova] ulinilemea. Jasho langu likakauka hata nikawa kama nchi kavu wakati wa kaskazi.” (Mistari 3, 4) Kujaribu kuficha dhambi yake na kutuliza dhamiri yenye hatia kulimchosha Daudi aliyetenda kinyume cha sheria. Maumivu makali yalipunguza nguvu zake sana hivi kwamba alikuwa kama mti uliokumbwa na ukame bila unyevu wenye kutoa uhai. Kwa kweli, huenda sana ikawa alipatwa na matokeo mabaya kiakili na kimwili. Kwa vyovyote vile, alipoteza shangwe yake. Ikiwa yeyote kati yetu tunajipata katika hali kama hiyo, twapaswa kufanya nini?
8 Ungamo kwa Mungu laweza kuleta msamaha na kitulizo. “Nalikujulisha dhambi yangu, wala sikuuficha upotovu wangu,” akaimba Daudi. “Nalisema, Nitayakiri maasi yangu kwa BWANA [Yehova, NW], nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu.” (Zaburi 32:5) Je! unasononeka juu ya dhambi fulani iliyofichwa? Je! lisingekuwa jambo bora zaidi kuiungama na kuiacha ili kupokea rehema ya Mungu? Kwa nini usiwaite wazee wa kundi na kujaribu kupata uponyaji wa kiroho? (Mithali 28:13; Yakobo 5:13-20) Roho yako ya toba itakubaliwa, na hatimaye shangwe yako ya Kikristo yaweza kurudishwa. “Heri [mwenye furaha ni, NW] aliyesamehewa dhambi na kusitiriwa makosa yake,” akasema Daudi. “Heri [mwenye furaha ni yule, NW] BWANA [Yehova, NW] asiyemhesabia upotovu, ambaye rohoni mwake hamna hila.”—Zaburi 32:1, 2.
9. Zaburi 51 ilitungwa wakati gani, na kwa nini?
9 Daudi na Bath-sheba walipaswa kumtolea Yehova Mungu hesabu kwa ajili ya kosa lao. Ingawa wangaliweza kuuawa kwa ajili ya dhambi zao, Mungu aliwarehemu. Alikuwa mwenye rehema hasa kwa Daudi kwa sababu ya agano la Ufalme. (2 Samweli 7:11-16) Mtazamo wa kutubu wa Daudi kuelekea dhambi zake zilizohusu Bath-sheba waonwa katika Zaburi 51. Zaburi hiyo yenye kugusa moyo ilibuniwa na mfalme huyo mwenye kutubu baada ya nabii Nathani kuifahamisha dhamiri yake juu ya ukubwa wa kosa lake dhidi ya sheria ya kimungu. Moyo mkuu ulihitajiwa ili Nathani aweze kuelekeza fikira za Daudi kwenye dhambi zake, sawa na vile ni lazima wazee wa Kikristo waliowekwa rasmi wawe na moyo mkuu ili kufanya mambo hayo leo. Badala ya kukanusha shtaka hilo na kuamuru Nathani auawe, Mfalme aliungama kwa unyenyekevu. (2 Samweli 12:1-14) Zaburi 51 yaonyesha yale aliyomwambia Mungu katika sala kuhusu matendo yake mabaya na inafaa sana kutafakari kwa sala, hasa ikiwa tumekosea na twatamani rehema ya Yehova.
Twapaswa Kumtolea Mungu Hesabu
10. Daudi angeweza kupataje uponyaji wa kiroho?
10 Daudi hakujaribu kutolea udhuru dhambi yake lakini aliomba hivi: “Ee Mungu, unirehemu, sawasawa na fadhili [kulingana na fadhili-upendo, NW] zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, uyafute makosa yangu.” (Zaburi 51:1) Kwa kukosea, Daudi alikuwa amekiuka mipaka ya Sheria ya Mungu. Hata hivyo, kulikuwako tumaini la kupona kwake kiroho, ikiwa Mungu angemwonyesha upendeleo kulingana na fadhili-upendo yake, au upendo mwaminifu-mshikamanifu. Wingi wa rehema za Mungu za wakati uliopita ulimpa mfalme huyo mwenye kutubu msingi wa imani kwamba Mfanyi wake angefutilia mbali makosa yake.
11. Dhabihu za Siku ya Upatanisho zilidokeza nini, na ni nini kinachohitajiwa ili kuwe na wokovu leo?
11 Kupitia ufananisho mbalimbali wa kiunabii wa dhabihu za Siku ya Upatanisho, Yehova alionyesha kwamba alikuwa na njia ya kuwasafisha wenye kutubu dhambi yao. Twajua sasa kwamba rehema na msamaha wake unanyooshwa kwetu kwa msingi wa imani yetu katika dhabihu ya fidia ya Yesu Kristo. Ikiwa Daudi, akiwa tu na mifano na ufananisho mbalimbali ya dhabihu hiyo akilini, angeweza kutumaini katika fadhili-upendo na rehema za Yehova, watumishi wa Mungu wa siku hizi wanapaswa kwa kadiri kubwa zaidi kama nini kuzoea imani katika fidia iliyoandaliwa kwa ajili ya wokovu wao!—Warumi 5:8; Waebrania 10:1.
12. Kutenda dhambi kunamaanisha nini, na Daudi alihisije juu ya kosa lake?
12 Katika kumsihi Mungu, Daudi aliongeza hivi: “Unioshe kabisa na uovu wangu, unitakase dhambi zangu. Maana nimejua mimi makosa yangu, na dhambi yangu i mbele yangu daima.” (Zaburi 51:2, 3) Kutenda dhambi ni kukosa shabaha kwa habari ya viwango vya Yehova. Kwa hakika Daudi alikuwa amefanya hivyo. Hata hivyo, yeye hakuwa kama mwuaji wa kimakusudi au mzinzi asiyehangaikia kosa lake, akisononeka tu juu ya adhabu yake au juu ya uwezekano wa kupata ugonjwa. Akiwa mmoja ampendaye Yehova, Daudi alichukia mabaya. (Zaburi 97:10) Alichukizwa na dhambi yake yenyewe na alitaka Mungu amsafishe na dhambi hiyo kabisa. Daudi alitambua kikamili makosa yake na alisikitika sana kwamba alikuwa ameacha tamaa yake yenye dhambi imshinde. Dhambi yake ilikuwa mbele yake daima, kwani dhamiri yenye hatia ya mtu mwenye kumhofu Mungu haitulizwi kamwe mpaka kuna toba, ungamo, na msamaha wa Yehova.
13. Kwa nini Daudi angeweza kusema kwamba alikuwa ametenda dhambi dhidi ya Mungu peke yake?
13 Akikiri kupaswa kwake kumtolea Yehova hesabu, Daudi alisema hivi: “Nimekutenda dhambi Wewe peke yako, na kufanya maovu mbele za macho yako. Wewe ujulikane kuwa una haki unenapo, na kuwa safi utoapo hukumu.” (Zaburi 51:4) Daudi alikuwa amevunja sheria za Mungu, alikuwa ameshusha heshima ya cheo cha kifalme, na ‘bila shaka kumtenda Yehova bila staha,’ akimweka Yeye wazi kwenye shutumu. (2 Samweli 12:14, NW; Kutoka 20:13, 14, 17) Matendo ya Daudi yenye dhambi yalikuwa pia makosa dhidi ya jamii ya Israeli na washiriki wa familia yake, kama vile mkosaji aliyebatizwa leo anavyosababisha huzuni au msononeko katika kundi la Kikristo na miongoni mwa wapendwa. Ingawa mfalme huyo mwenye kutubu alijua kwamba alikuwa ametenda dhambi dhidi ya wanadamu wenzake kama vile Uria, alitambua daraka kubwa zaidi kwa Yehova. (Linganisha Mwanzo 39:7-9.) Daudi alikiri kwamba hukumu ya Yehova ingekuwa yenye uadilifu. (Warumi 3:4) Wakristo ambao wametenda dhambi wanahitaji kuwa na maoni ayo hayo.
Hali Zenye Kusababisha Dhambi
14. Ni hali zipi zenye kusababisha dhambi zilizotajwa na Daudi?
14 Ingawa Daudi hakujaribu kujitetea mwenyewe, alisema hivi: “Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; mama yangu alinichukua mimba hatiani.” (Zaburi 51:5) Daudi alizaliwa akiwa mwenye kosa, na mama yake alipatwa na maumivu ya kuzaa kwa sababu ya hali yenye dhambi iliyorithiwa. (Mwanzo 3:16; Warumi 5:12) Maneno yake hayamaanishi kwamba ngono za ndoa zifaazo, kuchukua mimba, na kuzaa ni dhambi, kwa kuwa Mungu aliandaa ndoa na uzazi; wala Daudi hakuwa akirejezea dhambi yoyote mahususi ya mama yake. Alichukuliwa mimba katika dhambi kwa sababu wazazi wake walikuwa wenye dhambi kama vile wanadamu wote wasio wakamilifu.—Ayubu 14:4.
15. Ingawa huenda Mungu akafikiria hali zenye kusababisha dhambi, hatupaswi kufanya nini?
15 Ikiwa tumetenda dhambi, twaweza kutaja katika sala kwa Mungu hali zozote ambazo huenda ikawa zilisababisha kosa letu. Lakini acheni tusigeuze fadhili-upendo ya Mungu kuwa udhuru wa mwenendo mlegevu au kutumia hali yenye dhambi iliyorithiwa kuwa kisetiri cha kujificha ili tusichukue daraka kwa ajili ya dhambi yetu. (Yuda 3, 4) Daudi alikubali daraka kwa ajili ya kuwa na mawazo machafu na kushindwa na kishawishi. Acheni tusali kwamba tusishindwe na kishawishi na kisha tuchukue hatua kupatana na sala hiyo.—Mathayo 6:13.
Sihi ya Kusafishwa
16. Mungu hufurahia sifa gani, na hilo lapasa kuathirije mwenendo wetu?
16 Watu huenda wakaonekana kuwa watu wema wenye kujitoa kwa Mungu, lakini yeye hutazama chini ya sura za juu-juu na huona tulivyo ndani. Daudi alisema hivi: “Tazama, wapendezwa [Yehova] na kweli iliyo moyoni; nawe utanijulisha hekima kwa siri.” (Zaburi 51:6) Daudi alikuwa na hatia ya kutenda kwa uwongo na udanganyifu kwa kuelekeza kifo cha Uria kwa mbinu za werevu na kujaribu kuficha mambo ya hakika juu ya mimba ya Bath-sheba. Hata hivyo, alijua kwamba Mungu hupendezwa na ukweli na utakatifu. Hilo lapasa liathiri mwenendo wetu katika njia nzuri, kwani Yehova angetuhukumu ikiwa tungekuwa wadanganyifu. (Mithali 3:32) Daudi alitambua pia kwamba ikiwa Mungu ‘angemjulisha hekima kwa siri,’ akiwa mfalme mwenye kutubu, angeweza kufuata viwango vya kimungu katika maisha yake yaliyosalia.
17. Umaana wa kusali kutakaswa kwa hisopo ulikuwa nini?
17 Kwa sababu mtunga zaburi aliona uhitaji wake wa kupata msaada wa Mungu katika kushinda mielekeo ya dhambi, aliendelea kusihi hivi: “Unisafishe kwa hisopo nami nitakuwa safi, unioshe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji.” (Zaburi 51:7) Miongoni mwa mambo mengine, mmea wa hisopo (labda marjoramu, au Origanum maru) ulitumiwa katika usafishaji wa kisherehe wa watu waliokuwa wameambukizwa na ukoma. (Mambo ya Walawi 14:2-7) Kwa hiyo ilifaa kwamba Daudi asali kusafishwa dhambi kwa hisopo. Wazo la utakaso linahusiana pia na sihi yake kwamba Yehova amwoshe ili aweze kuwa safi kabisa, mweupe hata kuliko theluji ambayo haijapata moshi mweusi au takataka nyingine. (Isaya 1:18) Ikiwa yeyote kati yetu tunapatwa sasa na maumivu makali ya dhamiri juu ya kosa fulani, acheni tuwe na imani kwamba tukijaribu kupata msamaha wa Mungu kwa kutubu, yeye aweza kututakasa na kutusafisha kwa msingi wa dhabihu ya fidia ya Yesu.
Sihi ya Kurudishwa
18. Hali ya Daudi ilikuwa nini kabla ya yeye kutubu na kuungama, na kujua hilo kwaweza kusaidiaje leo?
18 Mkristo yeyote ambaye amepata kuwa na dhamiri yenye hatia wakati wowote aweza kuyaelewa maneno haya ya Daudi: “[Yehova] unifanye kusikia furaha na shangwe, mifupa uliyoiponda ifurahi.” (Zaburi 51:8) Kabla ya Daudi kutubu na kuungama dhambi zake, dhamiri yake iliyotaabika ilimfanya ahuzunike. Hata hakupata furaha katika nyimbo za furaha na za kushangilia zilizoimbwa na waimbaji wazuri na wanamuziki stadi. Maumivu ya Daudi mwenye dhambi juu ya kukosa kibali cha Mungu yalikuwa makali sana hivi kwamba alikuwa kama mtu ambaye mifupa yake yalikuwa yamepondwa kwa uchungu. Alitamani msamaha, kupona kiroho, na kurudishwa kwa ile shangwe aliyoona kabla ya hapo. Mkosaji mwenye kutubu leo anahitaji pia msamaha wa Yehova ili kupata tena ile shangwe aliyokuwa nayo kabla ya yeye kufanya jambo fulani lililohatarisha uhusiano wake pamoja na Mungu. Kurudishwa kwa “shangwe ya roho takatifu” kwa mtu mwenye kutubu kunaonyesha kwamba Yehova amemsamehe na ampenda. (1 Wathesalonike 1:6, NW) Hilo laleta shangwe lililoje!
19. Daudi angehisije ikiwa Mungu angeyafuta makosa yake yote?
19 Daudi aliendelea kusali hivi: “Usitiri uso wako usitazame dhambi zangu; uzifute hatia zangu zote.” (Zaburi 51:9) Yehova asingeweza kutazamiwa atazame dhambi kwa kibali. Kwa hiyo, aliombwa asitiri uso wake asitazame dhambi za Daudi. Mfalme huyo alisihi pia kwamba Mungu ayafute makosa yake yote, afutie mbali ukosefu wa uadilifu wake wote. Ikiwa tu Yehova angefanya hivyo! Hilo lingemchangamsha Daudi, lingeondoa mzigo wa dhamiri iliyotaabika, na kumwacha mfalme huyo aliyetubu sasa ajue kwamba alikuwa amesamehewa na Mungu wake mwenye upendo.
Namna Gani Ikiwa Umetenda Dhambi?
20. Ni nini linalopendekezwa kwa Mkristo yeyote ambaye ametenda dhambi nzito?
20 Zaburi 51 huonyesha kwamba watumishi wowote wa Yehova waliojiweka wakfu ambao wametenda dhambi nzito lakini ambao ni wenye kutubu wanaweza kumwomba kwa uhakika awaonyeshe upendeleo na kuwasafisha dhambi yao. Ikiwa wewe ni Mkristo ambaye amekosea katika njia hiyo, kwa nini usijaribu kupata msamaha wa Baba yetu wa kimbingu kwa sala ya unyenyekevu? Kiri uhitaji wako wa kupata msaada wa Mungu ili kusimama ukiwa na kibali mbele zake, na umwombe akurudishie shangwe uliyokuwa nayo. Wakristo wenye kutubu wanaweza kwa uhakika kumwendea Yehova katika sala wakiwa na maombi ya jinsi hiyo, kwani ‘atawasamehe kabisa.’ (Isaya 55:7; Zaburi 103:10-14) Bila shaka, wazee wa kundi wanapaswa waitwe ili waweze kutoa msaada wa kiroho unaohitajiwa.—Yakobo 5:13-15.
21. Tutachunguza nini baadaye?
21 Rehema ya Yehova huokoa watu wake kutoka katika hali ya kukata tamaa. Lakini acheni tuchunguze sihi nyingine zenye kuhisiwa moyoni za Daudi mwenye kutubu katika Zaburi 51. Funzo letu litaonyesha kwamba Yehova hadharau moyo uliovunjika.
Ungejibuje?
◻ Dhambi nzito yaweza kuathirije mmoja wa watumishi wa Yehova?
◻ Daudi aliathiriwaje alipojaribu kuficha dhambi yake?
◻ Kwa nini Daudi alisema kwamba alikuwa ametenda dhambi dhidi ya Mungu peke yake?
◻ Ingawa huenda Mungu akafikiria hali zenye kusababisha dhambi, hatupaswi kufanya nini?
◻ Mkristo apaswa kufanya nini ikiwa ametenda dhambi nzito?