Mafunzo Juu ya Maandiko Yenye Pumzi ya Mungu na Habari ya Msingi Yayo
Funzo Namba 2—Wakati na Maandiko Matakatifu
Laeleza migawanyo ya wakati itumiwayo katika Biblia, kalenda zinazotumiwa kwa ukawaida, tarehe za msingi za Biblia, na mambo ya kupendeza kwa habari ya “mkondo wa wakati.”
1, 2. Sulemani aliandika nini kuhusu wakati, na kwa sababu ya asili ya wakati ya kupita mbiombio, twapaswa kufanya nini nao?
BINADAMU hufahamu sana upitaji wa wakati. Kwa kila mdundo wa saa, yeye husonga hatua nyingine zaidi katika kijia cha wakati. Kweli kweli, yeye ni mwenye hekima, endapo anatumia vizuri wakati wake. Ni kama Mfalme Sulemani alivyoandika: “Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; wakati wa kupanda, na wakati wa kung’oa yaliyopandwa; wakati wa kuua, na wakati wa kupoza; wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga; wakati wa kulia, na wakati wa kucheka.” (Mhu. 3:1-4) Jinsi wakati unavyopita mbiombio! Ile miaka 70 ya urefu wa maisha ya kawaida ni wakati mfupi mno kwa mtu kutwaa wingi wa maarifa na kuonea shangwe vitu vinginevyo vyote vizuri ambavyo Yehova ametayarishia binadamu kwenye dunia hii. “Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho.”—Mhu. 3:11; Zab. 90:10.
2 Yehova mwenyewe huishi katika umilele wa wakati. Kwa habari ya viumbe vyake, imempendeza kuviweka katika mkondo wa wakati. Malaika wa mbinguni, kutia ndani Shetani mwasi, wajua vizuri sana juu ya mpito wa wakati. (Dan. 10:13; Ufu. 12:12) Kuhusu ainabinadamu imeandikwa hivi, “wakati na tukio lisilotazamiwa huwapata wote.” (Mhu. 9:11, NW) Mwenye furaha ni mtu ambaye nyakati zote hutia Mungu ndani ya mawazo yake na ambaye hukaribisha mpango wa Mungu wa “chakula kwa wakati wake”!—Mt. 24:45.
3. Wakati na anga vina nini kinachofanana?
3 Wakati Huelekea Upande Mmoja. Ingawa wakati ni wa ulimwengu mzima wote, hakuna binadamu aliye hai anayeweza kusema huo ni nini. Ni usio na mwisho kama vile anga. Hakuna anayeweza kueleza ni wapi mkondo wa wakati ulianza au unaelekea wapi. Mambo hayo ni mali ya maarifa yasiyo na mpaka ya Yehova, ambaye huelezwa kuwa Mungu “tangu milele hata milele.”—Zab. 90:2.
4. Yaweza kusemwa nini kuhusu upitaji wa wakati?
4 Kwa upande mwingine, wakati una vitambulisho fulani vinavyoweza kueleweka. Kiwango chao cha upitaji kilicho wazi chaweza kupimwa. Kuongezea hilo, huo husonga kuelekea upande mmoja tu. Kama vile motokaa katika barabara ya kupitiwa na magari ya kuelekea upande mmoja, wakati husonga daima kuelekea upande huo mmoja—kwenda mbele, daima mbele. Hata kasi yao ya kusonga mbele iwe nini, wakati hauwezi kamwe kurudishwa nyuma. Sisi twaishi katika sasa iliyo punde. Hata hivyo, sasa hii inasonga, daima ikitokomea nyuma. Hakuna cha kuisimamisha.
5. Kwa nini yaweza kusemwa kwamba wakati uliopita ama umetumiwa vizuri au ukapotezwa?
5 Wakati Uliopita. Wakati uliopita umetokomea, ni historia, na hauwezi kurudiwa kamwe. Jaribio lolote la kurudisha wakati uliopita ni jambo lisilowezekana kama vile kujaribu kufanya poromoko la maji likwee kilima au mshale upae kurudi kwenye upinde ulioufyatusha. Makosa yetu yameacha alama yayo katika mkondo wa wakati, alama ambayo Yehova pekee ndiye aweza kuifuta. (Isa. 43:25) Vivyo hivyo, vitendo vyema vya binadamu katika wakati uliopita vimefanyiza kumbukumbu ambayo “atarudishiwa” ikiambatana na baraka kutoka kwa Yehova. (Mit. 12:14; 13:22) Wakati uliopita umeshindwa au kupotezwa. Hauwezi kuongozeka tena. Juu ya waovu imeandikwa hivi: “Maana kama majani watakatika mara, kama miche mibichi watanyauka.”—Zab. 37:2.
6. Wakati ujao ni tofauti jinsi gani na wakati uliopita, na kwa nini twapaswa hasa kupendezwa nao?
6 Wakati Ujao. Wakati ujao ni tofauti. Sikuzote hutuelekea. Kwa msaada wa Neno la Mungu, twaweza kutambua vizuizi vinavyoinuka mbele yetu na kujitayarisha kukutana navyo. Twaweza kujiwekea akiba “hazina mbinguni.” (Mt. 6:20) Hazina hizi hazitafagiliwa mbali na mpito wa wakati. Zitakaa pamoja nasi na zitavumilia kuingia wakati ujao wa milele wenye baraka. Sisi twapendezwa na utumizi wenye hekima wa wakati, kwa kuwa hilo lahusu wakati wetu ujao.—Efe. 5:15, 16.
7. Yehova amewapa binadamu viishara gani vya wakati?
7 Viishara vya Wakati. Saa zetu za kisasa ni viishara vya wakati. Hutumika kama rula za kupimia wakati. Vivyo hivyo Yehova, aliye Muumba, ametia mwendoni viishara vikubwa vya wakati—dunia yenye kuzunguka juu ya mhimili wayo, mwezi unaozunguka dunia, na jua—hivi kwamba kwa msimamo wake duniani, binadamu aweza kujua wakati kwa usahihi. “Na Mungu akaendelea kunena: ‘Acha vimulikaji vije kuwapo katika upana wa mbingu vifanye mgawanyo kati ya mchana na usiku; navyo lazima vitumike kuwa ishara na kwa ajili ya majira na kwa ajili ya siku na miaka.’” (Mwa. 1:14, NW) Kwa hiyo, yakiwa umati wa vitu vyenye makusudi yanayokamatana, madude hayo ya kimbingu husonga katika duru zayo kamilifu, bila kukoma na bila kukosa yakipima mwendo wa kuelekea upande mmoja wa wakati.
8. Neno “siku” hutumiwa katika Biblia likiwa na maana zipi tofauti-tofauti?
8 Siku. Neno “siku” katika Biblia hutumiwa likiwa na maana kadhaa tofauti-tofauti, sawa na ambavyo hutumiwa kwa njia mbalimbali katika nyakati za kisasa. Dunia ifanyapo duru moja kamili juu ya mhimili wayo, hiyo hupima siku moja ya saa 24. Katika maana hii, siku moja hufanyizwa na mchana na usiku, jumla ya saa 24. (Yn. 20:19) Hata hivyo, kipindi cha mchana chenyewe, ambacho kwa kawaida kina wastani wa saa 12, huitwa pia siku. “Mungu akaiita nuru Mchana, na giza akaliita Usiku.” (Mwa. 1:5) Hilo hutokeza mtajo wa wakati “usiku,” kipindi ambacho kwa kawaida kina wastani wa saa 12 za giza. (Kut. 10:13) Maana nyingine ni ambapo neno “siku” hurejezea kipindi cha wakati kilicho ule ule mmoja na mtu fulani mwenye kutokeza. Kwa kielelezo, Isaya aliona njozi yake “siku za Uzia na Yothamu na Ahazi na Hezekia” (Isa. 1:1), na siku za Nuhu na za Lutu hutajwa kuwa za kiunabii. (Luka 17:26-30) Kielelezo kingine cha utumizi mnyumbufu au wa kitamathali wa neno “siku” ni usemi wa Petro wa kwamba “kwa Bwana [Yehova, NW] siku moja ni kama miaka elfu.” (2 Pet. 3:8) Katika simulizi la Mwanzo, siku ya uumbaji ni kipindi kirefu hata zaidi cha wakati—mamileani. (Mwa. 2:2, 3; Kut. 20:11) Muktadha wa Biblia huonyesha maana ambayo neno “siku” hutumika.
9. (a) Ugawanyaji wa siku kuwa saa 24 za dakika 60 kila moja ulianzaje? (b) Ni viishara vipi vya wakati vinavyotajwa katika Maandiko ya Kiebrania?
9 Saa. Mgawanyo wa siku kuwa saa 24 ulianzia Misri. Mgawanyo wetu wa ki-siku-hizi wa saa kuwa dakika 60 asili yao ni hesabu ya Kibabuloni, ambayo ilikuwa mfumo wa kutegemea namba 60. Hakuna mtajo wowote wa mgawanyo katika saa katika Maandiko ya Kiebrania.a Badala ya kugawanya siku kuwa saa fulani hasa, Maandiko ya Kiebrania hutumia semi kama vile “asubuhi,” “adhuhuri,” “mchana-kati,” na “wakati wa jioni” kuwa viishara vya wakati. (Mwa. 24:11; 43:16; Kum. 28:29, NW; 1 Fal. 18:26, NW) Usiku uligawanywa kuwa vipindi vitatu vilivyoitwa ‘makesha ya usiku’ (Zab. 63:6), viwili vyavyo hutajwa waziwazi katika Biblia: “zamu ya kati” (Amu. 7:19) na “zamu ya alfajiri.”—Kut. 14:24; 1 Sam. 11:11.
10. Wayahudi walihesabuje saa katika wakati wa Yesu, na kujua hilo hutusaidiaje kujua wakati wa kifo cha Yesu?
10 Hata hivyo, kuna mtajo wa mara nyingi wa “saa” katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo. (Yn. 12:23; Mt. 20:2-6) Saa zilihesabiwa tangu mapambazuko, au karibu saa 12 asubuhi. Biblia hutaja “saa ya tatu,” ambayo ingekuwa karibu saa 3 asubuhi. “Saa ya sita” hutajwa kuwa wakati ambapo giza lilifunika Yerusalemu wakati wa kutundikwa kwa Yesu. Hiyo ingelingana na saa 6 adhuhuri. Kukata roho kwa Yesu katika kifo penye mti wa mateso huelezwa kuwa kulitukia “karibu saa ya tisa,” au karibu saa 9 alasiri.—Mk. 15:25, NW; Luka 23:44, NW; Mt. 27:45, 46, NW.b
11. Utumizi wa “juma” kuwa kipimio cha wakati ni wenye umri gani?
11 Juma. Ilikuwa mapema katika historia yake kwamba binadamu akaanza kuhesabu siku zake katika duru saba-saba. Katika kufanya hivyo, alifuata kielelezo cha Muumba wake, ambaye alichukua hatua ya kufikisha kwenye upeo siku zake sita za uumbaji kwa kipindi cha saba ambacho pia kiliitwa siku. Nuhu alihesabu siku katika duru saba-saba. Katika Kiebrania, “juma” kwa halisi hurejezea kizio au kipindi cha mara saba.—Mwa. 2:2, 3; 8:10, 12; 29:27.
12. Mwezi wa ki-anga ni nini, nao hutofautianaje na miezi yetu ya ki-siku-hizi?
12 Miezi ya Ki-anga. Biblia husema juu ya “miezi ya ki-anga.” (Kut. 2:2; Kum. 21:13; 33:14; Ezra 6:15, NW) Miezi yetu ya kisasa si miezi ya ki-anga, kwa maana haiamuliwi na mwezi wa angani. Kuna migawanyo 12 pekee ya mwaka wa jua iliyobuniwa. Mwezi wa ki-anga ni mwezi unaoamuliwa na mwezi mwandamo. Kuna awamu nne za mwezi, ambazo hufanyiza mwezi mmoja kamili wenye wastani wa siku 29, saa 12, na dakika 44. Analotakwa mtu kufanya tu ni kutazama muundo wa mwezi akadirie mwezi wa ki-anga una umri wa siku ngapi.
13. Furiko liliandikwaje kwa usahihi kwa habari ya wakati?
13 Badala ya kutumia kabisa miezi halisi, yaonekana Nuhu alitunza maandishi ya matukio kwa miezi ya siku 30 kila mmoja. Kwa kuangalia maandishi ya matukio ya kila siku aliyotunza Nuhu katika safina, twaelewa kwamba maji ya Furiko yalifuliza kufunika dunia kwa kipindi cha miezi mitano, au “siku mia na hamsini.” Ilikuwa baada ya miezi 12 na siku 10 kwamba dunia ilikauka kuwezesha abiria wa safina watoke nje. Kwa hiyo, matukio hayo yenye kufanyiza muhula yaliandikwa kwa usahihi kwa habari ya wakati.—Mwa. 7:11, 24; 8:3, 4, 14-19.
14. (a) Yehova alifanyaje mpango kwa ajili ya majira? (b) Mpango wa majira utaendelea kwa muda gani?
14 Majira. Katika kutayarisha dunia ikaliwe, Yehova alifanya mipango yenye hekima na yenye upendo ya majira. (Mwa. 1:14) Yapo kwa sababu ya dunia kuwa imeegama, au kulala kidogo, kwa mlalo wa digrii 23.5 kwenye mhimili wayo wa kusafiri kulizunguka jua. Matokeo ya hilo kwanza ni kuegemezwa kwa Kizio cha Kusini cha dunia kuelekea jua na kisha, miezi sita baadaye, Kizio cha Kaskazini cha dunia, hivi kwamba majira hutukia kwa utaratibu. Badiliko hili la majira hufanyiza hali tofauti na vipeo na huongoza nyakati za kupanda na kuvuna. Neno la Mungu hutuhakikishia kwamba mpango huu wa badiliko na vipeo vya majira katika mwaka ni wa kuendelea milele. “Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma.”—Mwa. 8:22.
15, 16. (a) Majira yenye mvua katika Bara Lililoahidiwa yaweza kugawanyaje? (b) Eleza juu ya majira ya mvua na uhusiano wa majira hayo na utendaji wa kilimo.
15 Mwaka katika Bara Lililoahidiwa kwa ujumla waweza kuganywa kuwa majira ya mvua na majira ya ukame. Tangu karibu na katikati ya Aprili mpaka katikati ya Oktoba, mvua kidogo sana hunya. Majira ya mvua yaweza kugawanywa kuwa mvua ya mapema, au “vuli,” (Oktoba-Novemba); mvua kubwa ya kipupwe na halihewa baridi zaidi (Desemba-Februari); na mvua ya mwisho, au “masika,” (Machi-Aprili). (Kum. 11:14; Yoe. 2:23) Migawanyo hiyo ni ya kukadiria, majira hayo huingiliana kwa sababu ya tofauti za hali ya anga katika sehemu mbalimbali za bara hilo. Mvua ya mapema hufanya ardhi kavu kuwa tope, hivi kwamba Oktoba-Novemba huwa wakati wa “kulima” na wa “kupanda mbegu.” (Kut. 34:21; Law. 26:5) Wakati wa mvua kubwa ya kipupwe kuanzia Desemba mpaka Februari, uangukaji wa theluji si jambo lisilo la kawaida, na katika Januari na Februari, halijoto huenda ikashuka chini ya kiwango cha kuganda kwenye miinuko iliyo juu zaidi. Biblia hunena juu ya Benaya, mmoja wa mashujaa wa Daudi, akiua simba “wakati wa theluji.”—2 Sam. 23:20.
16 Miezi ya Machi na Aprili (yakaribia kuwa miezi ya Kiebrania ya Nisani na Iyyari) ndiyo miezi ya “mvua wakati wa masika.” (Zek. 10:1) Hii ni mvua ya mwisho, inayohitajiwa ili kufanya nafaka iliyopandwa katika vuli iumuke, kusudi mavuno mazuri yatokee. (Hos. 6:3; Yak. 5:7) Pia haya ndiyo majira ya mavuno ya mapema, na Mungu aliamuru Israeli watoe malimbuko ya mavuno mnamo Nisani 16. (Law. 23:10; Rut. 1:22) Huo ni wakati wa uzuri na furaha yenye upendezi. “Maua yatokea katika nchi, wakati wa kupelea umefika, na sauti ya mwigo husikiwa kwetu. Mtini wapevusha tini zake, na mizabibu inachanua, inatoa harufu yake nzuri.”—Wim. 2:12, 13.
17. (a) Mazao hunyweshwaje wakati wa majira ya ukame? (b) Fikiria chati “Mwaka wa Waisraeli” na ugawanye mwaka kwa kulingana na majira kama inavyozungumzwa katika mafungu 15-17. (c) Ni wakati gani uliokuwa wa mavuno ya mapema, mavuno ya nafaka, na wakati ambapo matunda yote yalikusanywa, na ni sikukuu zipi zilizofanyika wakati mmoja na matukio hayo?
17 Karibu na katikati ya Aprili majira ya ukame huanza, lakini karibu katika kipindi chote hiki, na hasa kwenye nyanda za pwani na mitelemko ya magharibi ya milima, wingi wa umande hunywesha mazao ya kiangazi. (Kum. 33:28) Wakati wa Mei, nafaka huvunwa, na ilikuwa mwishoni mwa mwezi kwamba Sikukuu ya Majuma (Pentekoste) ilisherehekewa. (Law. 23:15-21) Ndipo, halihewa inapokuwa yenye ujoto zaidi na ardhi kukauka zaidi, zabibu katika mizabibu huiva na kuvunwa, zikifuatwa na matunda yale mengine ya kiangazi, kama vile zeituni, tende, na tini. (2 Sam. 16:1) Majira ya ukame yamalizikapo na mvua ya mapema kuanza, mazao yote ya bara huwa yamekwisha vunwa, na ndipo (karibu na mwanzo wa Oktoba) Sikukuu ya Vibanda, au Tabenakulo, iliadhimishwa.—Kut. 23:16; Law. 23:39-43.
18. (a) Ni kwa nini maana ya neno la Kiebrania “mwaka” lafaa? (b) Kwa habari ya dunia ni nini mwaka halisi wa jua?
18 Mwaka. Uchunguzi wetu wa wakati katika Biblia sasa watuleta kwenye usemi “mwaka.” Tangu mwanzo wa historia ya binadamu, unatajwa. (Mwa. 1:14) Neno la Kiebrania kwa “mwaka,” sha·nahʹ, hutokana na shina linalomaanisha “rudia; fanya tena” na hutoa wazo la duru ya wakati. Hilo lilifaa, kwa kuwa kila mwaka wa duru ya majira ulirudiwa. Mwaka wa kidunia ni wakati uchukuao dunia kukamilisha duru, au safari moja, kuzunguka jua. Wakati kamili unaotuchukua sisi hapa duniani kukamilisha safari hiyo ni siku 365 saa 5 dakika 48 sekunde 46, au karibu siku 365 1/4. Huo huitwa mwaka halisi wa jua.
19. (a) Miaka ya kale ya Biblia ilichukuliwaje? (b) Baadaye Yehova alitoa amri ya “mwaka mtakatifu” upi?
19 Miaka ya Biblia. Kulingana na maoni ya Kibiblia, mwaka ulianzia vuli mpaka vuli. Hilo lilifaa hasa maisha ya kilimo, mwaka ukianzia na ulimaji na kupanda mbegu, kuelekea sehemu ya kwanza ya mwezi wetu wa Oktoba, na kumalizikia na ukusanyaji katika mavuno. Nuhu alihesabu mwaka kuanzia na vuli. Yeye aliandika Gharika kuwa ikianza “katika mwezi wa pili,” ambao ungelingana na sehemu ya pili ya Oktoba na sehemu ya kwanza ya Novemba. (Mwa. 7:11, NW, kielezi-chini) Hadi leo hii, vikundi vingi vya watu wa dunia wangali wanaanza mwaka mpya wao katika vuli. Wakati wa Kutoka Misri, katika 1513 K.W.K., Yehova aliagiza kwamba Abibu (Nisani) wapasa kuwa “mwanzo wa miezi” kwa ajili ya Wayahudi, hivi kwamba sasa wakawa na mwaka mtakatifu, ukianzia masika mpaka masika. (Kut. 12:2) Hata hivyo, Wayahudi katika siku yetu huadhimisha mwaka wa kilimwengu, au kibinadamu, kuanzia vuli, Tishri ukiwa ndio mwezi wa kwanza.
20. Mwaka wa mwezi wa ki-anga ulirekebishwaje upatane na mwaka wa jua, na miaka ya mwezi wa ki-anga na jua ni nini?
20 Mwaka wa Mwezi wa Ki-anga na Jua. Hadi wakati wa Kristo, mataifa yaliyo mengi yalitumia miaka ya mwezi wa ki-anga kuhesabia wakati, yakitumia njia mbalimbali za kurekebisha mwaka ukaribie kupatana na mwaka wa jua. Mwaka wa mwezi wa ki-anga wa kawaida wa miezi 12 una siku 354, miezi hiyo ikiwa ya siku 29 au 30, pia ikitegemea kutokea kwa kila mwezi mwandamo. Kwa hiyo mwaka wa mwezi wa ki-anga unapungua kwa karibu siku 11 1/4 mwaka halisi wa jua wa siku 365 1/4. Waebrania walifuata mwaka wa mwezi wa ki-anga. Jinsi ambavyo walirekebisha mwaka huu upatane na mwaka wa jua na majira mbalimbali haielezwi katika Biblia, lakini lazima wawe waliongeza miezi ya ziada, au ya mpenyezeo-kalenda, ilipohitajiwa. Mpango huo wa miezi ya mpenyezeo-kalenda uliratibiwa baadaye katika karne ya tano K.W.K. kuwa ile iitwao leo duru ya Meto. Hiyo iliruhusu mwezi wa mpenyezeo-kalenda uongezwe mara saba kila miaka 19, na katika kalenda ya Kiyahudi, iliongezwa baada ya mwezi wa 12, Adari, na uliitwa Veadari, au “Adari ya pili.” Kwa kuwa ndivyo kalenda ya mwezi wa ki-anga inavyorekebishwa kupatana na jua, miaka yenyewe, ambayo ni ya miezi 12 au 13, hujulikana kuwa miaka ya mwezi wa ki-anga na jua.
21. (a) Kalenda ya Julius ni ipi? (b) Ni kwa nini kalenda ya Gregory ni sahihi zaidi?
21 Kalenda ya Julius na Gregory. Kalenda ni mfumo wa kuweka mwanzo, urefu, na migawanyo ya mwaka na kuipanga migawanyo hiyo kwa utaratibu. Kalenda ya Julius ilianzishwa na Kaisari Julius katika 46 K.W.K., ili kuwapa Warumi mpango wa wakati wa mwaka wa jua badala ya mwaka wa mwezi wa ki-anga. Kalenda ya Julius ina siku 365 katika mwaka, isipokuwa kwamba kila mwaka wa nne (mwaka-mruko), siku moja huongezwa, ili kuufanya siku 366. Hata hivyo, baada ya muda, ilipatikana kwamba kalenda ya Julius kwa kweli ina urefu wa dakika 11 zaidi ya mwaka halisi wa jua. Kufikia karne ya 16 W.K., kasoro ya siku kumi kamili ilikuwa imerundana. Kwa hiyo, katika 1582, Papa Gregory wa 13 alianzisha rekebisho dogo, akaanzisha ile inayoitwa sasa kalenda ya Gregory. Kwa barua yenye muhuri wa papa siku kumi ziliondolewa kutoka mwaka 1582, hivi kwamba siku ya kufuatia Oktoba 4 ikawa Oktoba 15. Kalenda ya Gregory hutaka kwamba karne zisizogawanyika kwa 400 zisionwe kuwa miaka-mruko. Kwa kielelezo, tofauti na mwaka 2000, mwaka 1900 haukufanywa mwaka-mruko kwa sababu namba 1,900 haigawanyiki kwa 400. Kalenda ya Gregory ndiyo ambayo sasa hutumika kwa ujumla katika sehemu nyingi za ulimwengu.
22, 23. Mwaka wa kiunabii ni wenye urefu gani?
22 “Mwaka” wa Kiunabii. Katika unabii wa Biblia neno “mwaka” hutumiwa mara nyingi kwa maana ya pekee kuwa ulinganifu wa miezi 12, kila mwezi ukiwa na siku 30, kuwa na jumla ya siku 360. Angalia anachosema mjuzi mmoja katika kutoa maelezo juu ya Ezekieli 4:5, 6: “Lazima tudhani kwamba Ezekieli alijua mwaka wa siku 360. Huu si mwaka halisi wa jua wala si mwaka wa mwezi wa ki-anga. Ni mwaka wa ‘wastani’ ambao katika huo kila mwezi una siku 30.”c
23 Mwaka wa kiunabii huitwa pia “wakati,” na uchunguzi mmoja wa Ufunuo 11:2, 3 na 12:6, 14 hufunua jinsi “wakati” mmoja unavyoonwa kuwa siku 360. Pia katika unabii, pindi kwa pindi mwaka huwakilishwa kimfano na “siku” moja.—Eze. 4:5, 6.
24. Vikundi-vikundi vya watu wa kale vilianzaje hesabu yavyo?
24 Hakuna Mwaka Sifuri. Vikundi-vikundi vya watu wa kale, kutia ndani Wagiriki walioelimika, Warumi, na Wayahudi, hawakuwa na wazo la sifuri. Kwao, kila kitu kilianzia na moja. Ulipojifunza nambari za Kirumi shuleni (I, II, III, IV, V, X, n.k.), je! ulijifunza tarakimu ya sifuri? La, kwa sababu Warumi hawakuwa na yoyote. Kwa kuwa Warumi hawakutumia namba sifuri, Wakati wa Kawaida ulianza, si na mwaka sifuri, bali na 1 W.K. Hilo pia lilitokeza mpangilio wa namba ordinal, kama vile kwanza, pili, ya (wa) tatu, ya (wa) kumi, na ya (wa) mia. Katika hesabu ya ki-siku-hizi, binadamu huwazia kila kitu kikianzia na sifuri, au ziro. Yawezekana sifuri ilibuniwa na Wahindu.
25. Namba ordinal hutofautianaje na namba cardinal?
25 Kwa hiyo huwa kwamba wakati wowote namba ordinal zinapotumiwa, ni lazima tuondoe moja ili tupate namba kamili. Kwa kielelezo, tunaponena juu ya tarehe fulani katika karne ya 20 W.K., je! humaanisha kwamba kumekuwako karne 20 kamili? La, humaanisha karne 19 kamili kuongezea miaka kadhaa. Ili kuonyesha namba kamili, Biblia, na pia hesabu ya ki-siku-hizi, hutumia namba cardinal, kama vile moja, mbili, tatu, kumi, na mia moja. Hizo pia huitwa “namba kamili.”
26. Ungejuaje ni mingapi (a) miaka tangu Oktoba 1, 607 K.W.K., mpaka Oktoba 1, 1914 W.K.? (b) miaka 2,520 tangu Oktoba 1, 607 K.W.K.?
26 Sasa, kwa kuwa Wakati wa Kawaida haukuanzia na mwaka sifuri bali ulianzia na 1 W.K., na kalenda ya miaka ya kabla ya Wakati wa Kawaida haikuhesabu kuanzia mwaka sifuri bali ilianza na 1 K.W.K., tarakimu inayotumiwa kwa ajili ya mwaka katika tarehe yoyote kwa uhalisi ni namba ordinal. Yaani, 1990 W.K. kwa uhalisi huwakilisha miaka kamili 1989 tangu mwanzo wa Wakati wa Kawaida, na tarehe Julai 1, 1990, huwakilisha miaka 1,989 kuongezea nusu mwaka tangu mwanzo wa Wakati wa Kawaida. Kanuni iyo hiyo hutumika kwa tarehe za K.W.K. Kwa hiyo ili kujua ni miaka mingapi ilipita baina ya Oktoba 1, 607 K.W.K., na Oktoba 1, 1914 W.K., ongeza miaka 606 (kuongezea miezi mitatu ya mwisho ya mwaka uliotangulia) kwenye 1,913 (kuongezea miezi tisa ya kwanza ya mwaka unaofuata), na tokeo ni 2,519 (kuongezea miezi 12), au miaka 2,520. Au endapo wataka kujua ni tarehe gani ingekuwa miaka 2,520 baada ya Oktoba 1, 607 K.W.K., kumbuka kwamba 607 ni namba ordinal—huwakilisha miaka kamili 606—na kwa kuwa twahesabu, si kutoka Desemba 31, 607 K.W.K., bali kutoka Oktoba 1, 607 K.W.K., ni lazima tuongeze kwa 606 miezi mitatu ya mwishoni mwa 607 K.W.K. Sasa toa 606 1/4 kutoka miaka 2,520. Baki ni 1,913 3/4. Hiyo yamaanisha kwamba miaka 2,520 kutoka Oktoba 1, 607 K.W.K., hutupeleka miaka 1,913 3/4 ndani ya Wakati wa Kawaida—miaka kamili 1,913 hutuleta kwenye mwanzo wa 1914 W.K., na kwa kuongezea robo tatu za mwaka hutuleta kwenye Oktoba 1, 1914 W.K.d
27. Tarehe za msingi ni nini, na kwa nini ni zenye thamani kubwa?
27 Tarehe za Msingi. Kronolojia (matukio na tarehe yayo) yenye kutegemeka ya Biblia msingi wayo ni tarehe fulani za msingi. Tarehe ya msingi ni tarehe ya kalenda katika historia ambayo inakubaliwa kwa msingi thabiti na inayolingana na tukio fulani kamili lililoandikwa katika Biblia. Kisha yaweza kutumiwa kuwa mahali pa kuanzia ambapo kutoka hapo mfululizo wa matukio ya Biblia waweza kujulikana kwenye kalenda kwa uhakika. Mahali hapo pa msingi pakiisha wekwa, hesabu ya mbele au nyuma kuanzia tarehe hii hufanywa kutokana na maandishi sahihi katika Biblia yenyewe, kama vile urefu wa maisha ya watu ulioelezwa au muda wa tawala za wafalme. Kwa hiyo, kwa kuanzia mahali fulani palipoimarishwa, twaweza kutumia kronolojia ya kindani yenye kutegemeka ya Biblia yenyewe kuyapa tarehe matukio mengi ya Biblia.
28. Ni tarehe gani ya msingi inayotolewa kwa Maandiko ya Kiebrania?
28 Tarehe ya Msingi kwa Maandiko ya Kiebrania. Tukio moja maarufu lililoandikwa katika Biblia na katika historia ya kilimwengu ni kupinduliwa kwa mji wa Babuloni na Wamedi na Waajemi chini ya Koreshi. Biblia imeandika tukio hilo kwenye Danieli 5:30. Vyanzo mbalimbali ya kihistoria (kutia ndani Diodoro, Afrikano, Eusebio, Ptolemy, na mabamba yenye miandiko ya Kibabuloni) huunga mkono 539 K.W.K. kuwa mwaka wa Babuloni kupinduliwa na Koreshi. Simulizi la tarehe za matukio ya Nabondio huonyesha mwezi na siku ya kuanguka kwa jiji hilo (mwaka haupo). Kwa hiyo wataalamu wa kronolojia wa kilimwengu wameweka tarehe ya kuanguka kwa Babuloni kuwa Oktoba 11, 539 K.W.K., kulingana na kalenda ya Julius, au Oktoba 5 kulingana na kalenda ya Gregory.e
29. Amri ya Koreshi ilitolewa wakati gani, hilo likiruhusu nafasi ya nini?
29 Kufuatia kupinduliwa kwa Babuloni, na wakati wa mwaka wake wa kwanza akiwa mtawala wa Babuloni iliyoshindwa, Koreshi alitoa amri yake ijulikanayo sana ya kuruhusu Wayahudi warejee Yerusalemu. Kufuatia maandishi ya Biblia, amri hiyo yaelekea ilitolewa mwishoni-mwishoni katika 538 K.W.K. au kuelekea masika ya 537 K.W.K. Hilo lingetoa nafasi ya kutosha kwa Wayahudi wakalie tena bara la nyumbani kwao na kukwea Yerusalemu wakarejeshe ibada ya Yehova katika “mwezi wa saba,” Tishri, au kama Oktoba 1, 537 K.W.K.—Ezra 1:1-4; 3:1-6.f
30. Tarehe ya msingi pamoja na unabii uliotimizwa vyauweka wakati wa ubatizo wa Yesu, na wa kuzaliwa kwake kuwa upi?
30 Tarehe ya Msingi kwa Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo. Tarehe ya msingi kwa Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo huamuliwa na tarehe ambayo Kaisari Tiberia alimrithi Maliki Augusto. Augusto alikufa mnamo Agosti 17, 14 W.K. (kalenda ya Gregory); Tiberia alitangazwa maliki na Bunge la Rumi mnamo Septemba 15, 14 W.K. Huelezwa kwenye Luka 3:1, 3 kwamba Yohana Mbatizaji alianza huduma yake katika mwaka wa 15 wa utawala wa Tiberia. Endapo miaka ilihesabiwa tangu kifo cha Augusto, mwaka wa 15 ulianzia Agosti wa 28 W.K. mpaka Agosti wa 29 W.K. Ukihesabiwa tangu wakati Tiberia alipotangazwa kuwa maliki na Bunge, mwaka huo ulianzia Septemba wa 28 W.K. mpaka Septemba wa 29 W.K. Muda mfupi baadaye, Yesu, aliyekuwa mdogo wa kama miezi sita kuliko Yohana Mbatizaji, alikuja kubatizwa, alipokuwa “kama miaka thelathini.” (Luka 3:2, 21-23; 1:34-38) Hilo lakubaliana na unabii kwenye Danieli 9:25 kwamba “majuma” 69 (majuma ya kiunabii ya miaka 7 kila moja, hivyo kujumlika kuwa miaka 483) yangekwisha tangu “kuwekwa amri ya kutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu” na ukuta walo mpaka kutokea kwa Mesiya. (Dan. 9:24, NW, kielezi-chini) “Amri” hiyo ilitolewa na Artashasta (Longimano) katika 455 K.W.K. na kutekelezwa na Nehemia katika Yerusalemu katika sehemu ya mwisho ya mwaka huo. Na miaka 483 baadaye, katika sehemu ya mwisho-mwisho wa 29 W.K., alipobatizwa na Yohana, Yesu alipakwa mafuta pia kwa roho takatifu ya Mungu, hivyo akawa Mesiya, au Mpakwa Mafuta. Ya kwamba Yesu alibatizwa na kuanza huduma yake katika sehemu ya mwisho-mwisho ya mwaka huo hukubaliana pia na unabii wa kwamba angekatiliwa mbali “kwa nusu ya juma” la miaka (au baada ya miaka mitatu na nusu). (Dan. 9:27) Kwa kuwa alikufa katika masika, huduma yake ya miaka mitatu na nusu lazima iwe ilianzia kuelekea vuli ya 29 W.K.g Vilevile, njia hizo mbili za uthibitisho zaonyesha pia kwamba Yesu alizaliwa katika vuli ya 2 K.W.K., kwa kuwa Luka 3:23 huonyesha kwamba Yesu alikuwa karibu miaka 30 alipoanza kazi yake.h
31. (a) Kwa nini mwendo wa upitaji wa wakati huonekana ukitofautiana? (b) Kwa hiyo vijana wana faida gani?
31 Jinsi Wakati Unavyosonga Kasi Zaidi. Kuna usemi wa kale kwamba “nyungu inayotazamwa-tazamwa huwa haichemki kamwe.” Ni kweli kwamba tunapotazama-tazama wakati, tunapouhisi-hisi, tunapongojea jambo fulani litokee, ndipo unapoonekana ukipita polepole kama nini. Hata hivyo, endapo tuna shughuli, endapo tunapendezwa na kushughulishwa mno na tunalofanya, ndipo kikweli inapoonekana kwamba “wakati wakimbia sana.” Zaidi ya hilo, kwa watu wenye umri mkubwa zaidi wakati huonekana kuwa wapita haraka zaidi kuliko kwa watoto wachanga. Ni kwa nini iko hivyo? Mwaka mmoja ulioongezwa kwenye maisha ya mtoto wa mwaka mmoja humaanisha ongezeko la asilimia 100 katika maono ya maishani. Mwaka mmoja uliongezwa kwa mtu wa miaka 50 humaanisha asilimia 2 zaidi tu. Kwa mtoto, mwaka mmoja huonekana kuwa wakati mrefu mno. Mtu mwenye umri mkubwa zaidi, endapo ana shughuli na afya nzuri, huona kwamba miaka yaonekana ikipita mbio zaidi na zaidi. Yeye huja kuelewa kwa kina kirefu zaidi maneno ya Sulemani: “Jambo jipya hakuna chini ya jua.” Kwa upande mwingine, watu wachanga wangali wana miaka ya kufanyizwa utu ambayo huonekana ni ya polepole. Badala ya “kujilisha upepo” kwa ulimwengu wa ufuatiaji mali, wanaweza kutumia miaka hiyo kwa faida kwa kulimbika utajiri wa maarifa ya kimungu. Maneno ya Sulemani yafuatayo baadaye yanafaa: “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, kabla hazijaja siku zilizo mbaya, wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.”—Mhu. 1:9, 14; 12:1.
32. Wanadamu wanawezaje kufikia kuthamini kwa ukamili zaidi maoni ya Yehova juu ya wakati?
32 Wakati—Watu Waishipo Milele. Hata hivyo, kuna siku zenye shangwe mbele ambazo hazitakaribiwa na ubaya. Wapenda uadilifu, ambao ‘nyakati zao zimo mkononi mwa Yehova,’ waweza kutazamia uhai wa milele katika makao ya Ufalme wa Mungu. (Zab. 31:14-16; Mt. 25:34, 46) Chini ya Ufalme, kifo hakitakuwapo tena. (Ufu. 21:4) Uzembe, maradhi, ukimwa, na ubatili vitakuwa vimetokomea. Kutakuwako kazi ya kufanya, yenye kushughulisha mno na yenye kutaka utaalamu, ikitaka utumizi wa uwezo mbalimbali mkamilifu wa binadamu na kuleta uradhi tele wa utimizo. Miaka hiyo itaonekana ikipita kasi zaidi na zaidi, na akili zenye uthamini na kushika zitaendelea kutajirishwa kwa kumbukumbu za matukio yenye furaha. Kwa kadiri mileani zitakavyopita, bila shaka wanadamu katika dunia hii watakuja kuthamini kwa ukamili zaidi maoni ya Yehova juu ya wakati: ‘Maana miaka elfu machoni pa Yehova ni kama siku ya jana.’—Zab. 90:4.
33. Kwa habari ya wakati, ni baraka gani ambayo Yehova ameamuru?
33 Kwa kuutazama mkondo wa wakati kwa maoni ya kibinadamu ya sasa na kufikiria ahadi ya Mungu ya ulimwengu mpya wenye uadilifu, jinsi mibaraka inayotazamiwa ya siku hiyo ilivyo yenye kuleta shangwe: “Maana ndiko BWANA [Yehova, NW] alikoamuru baraka, naam, uzima hata milele”!—Zab. 133:3.
[Maelezo ya Chini]
a Neno “saa” huonekana katika King James Version kwenye Danieli 3:6, 15; 4:19, 33; 5:5, kutokana na Kiaramu; hata hivyo, Concordance ya Strong, Hebrew and Chaldee Dictionary, hutoa maana ya neno hilo kuwa “tazamo, yaani, punde ya wakati.” Hutafsiriwa kuwa “punde ya wakati” katika New World Translation of the Holy Scriptures.
b Ona vielezi-chini vya maandiko hayo, NW.
c Biblical Calendars, 1961, cha J. Van Goudoever, ukurasa 75.
d Insight on the Scriptures, Buku 1, ukurasa 458.
e Insight on the Scriptures, Buku 1, kurasa 453-4, 458; Buku 2, ukurasa 459.
f Insight on the Scriptures, Buku 1, ukurasa 568.
g Insight on the Scriptures, Buku 2, kurasa 899-902.
h Insight on the Scriptures, Buku 2, kurasa 56-8.
[Chati katika ukurasa wa 281]
MWAKA WA WAISRAELI
Jina la Mwezi Nisani (Abibu)
Walingana na Machi - Aprili
Mwaka Mtakatifu mwezi wa 1
Mwaka wa Kilimwengu mwezi wa 7
Mitajo Kut. 13:4; Neh. 2:1
Sikukuu Nisani 14 Kupitwa
Nisani 15-21 Sikukuu ya Keki Zisizochachwa
Nisani 16 Toleo la malimbuko
Jina la Mwezi Iyyari (Zivu)
Walingana na Aprili - Mei
Mwaka Mtakatifu mwezi wa 2
Mwaka wa Kilimwengu mwezi wa 8
Mtajo 1 Fal. 6:1
Jina la Mwezi Sivani
Walingana na Mei - Juni
Mwaka Mtakatifu mwezi wa 3
Mwaka wa Kilimwengu mwezi wa 9
Mtajo Esta 8:9
Sikukuu Sivani 6 Sikukuu ya Majuma
(Pentekoste)
Jina la Mwezi Tamuzi
Walingana na Juni - Julai
Mwaka Mtakatifu mwezi wa 4
Mwaka wa Kilimwengu mwezi wa 10
Mtajo Yer. 52:6
Jina la Mwezi Abi
Walingana na Julai - Agosti
Mwaka Mtakatifu mwezi wa 5
Mwaka wa Kilimwengu mwezi wa 11
Mtajo Ezra 7:8
Jina la Mwezi Eluli
Walingana na Agosti - Septemba
Mwaka Mtakatifu mwezi wa 6
Mwaka wa Kilimwengu mwezi wa 12
Mtajo Neh. 6:15
Jina la Mwezi Tishri (Ethanimu)
Walingana na Septemba - Oktoba
Mwaka Mtakatifu mwezi wa 7
Mwaka wa Kilimwengu mwezi wa 1
Mtajo 1 Fal. 8:2
Sukukuu Tishri 1 Siku ya mlipuo wa tarumbeta
Tishri 10 Siku ya Uachilio
Tishri 15-21 Sikukuu ya Vibanda
Tishri 22 Kusanyiko la umuhimu
Jina la Mwezi Heshvani (Buli)
Walingana na Oktoba - Novemba
Mwaka Mtakatifu mwezi wa 8
Mwaka wa Kilimwengu mwezi wa 2
Mtajo 1 Fal. 6:38
Jina la Mwezi Kislevi
Walingana na Novemba - Desemba
Mwaka Mtakatifu mwezi wa 9
Mwaka wa Kilimwengu mwezi wa 3
Mtajo Neh. 1:1
Jina la Mwezi Tebethi
Walingana na Desemba - Januari
Mwaka Mtakatifu mwezi wa 10
Mwaka wa Kilimwengu mwezi wa 4
Mtajo Esta 2:16
Jina la Mwezi Shebati
Walingana na Januari - Februari
Mwaka Mtakatifu mwezi wa 11
Mwaka wa Kilimwengu mwezi wa 5
Mtajo Zek. 1:7
Jina la Mwezi Adari
Walingana na Februari - Machi
Mwaka Mtakatifu mwezi wa 12
Mwaka wa Kilimwengu mwezi wa 6
Mtajo Esta 3:7
Jina la Mwezi Veadari
Walingana na (Mwezi-Mpenyezo)
Mwaka Mtakatifu mwezi wa 13