Sura ya 26
“Hakuna Mkaaji Atakayesema, Mimi Mgonjwa”
1. Kwa nini maneno ya Isaya 33:24 yanafariji?
“VIUMBE vyote vinafuliza kupiga kite pamoja na kuwa katika maumivu pamoja hadi sasa.” Ndivyo alivyosema mtume Paulo. (Waroma 8:22) Licha ya maendeleo katika sayansi ya tiba, ugonjwa na kifo zaendelea kuwataabisha wanadamu. Basi, ahadi inayofikisha sehemu hii ya unabii wa Isaya kwenye upeo ni bora kama nini! Hebu wazia wakati ambapo “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.” (Isaya 33:24) Ahadi hiyo itatimizwa lini na jinsi gani?
2, 3. (a) Taifa la Israeli lina ugonjwa kwa njia gani? (b) Ashuru inatumikaje kama “fimbo” ya Mungu ya kutia nidhamu?
2 Isaya anaandika ahadi hiyo wakati ambapo watu wa agano wa Mungu ni wagonjwa kiroho. (Isaya 1:5, 6) Wameasi na kukosa adili sana hivi kwamba wahitaji nidhamu kali kutoka kwa Yehova Mungu. Ashuru yatumiwa kama “fimbo” ya Yehova ya kutoa nidhamu hiyo. (Isaya 7:17; 10:5, 15) Kwanza, ufalme wa Israeli wa makabila kumi washindwa na Waashuri mwaka wa 740 K.W.K. (2 Wafalme 17:1-18; 18:9-11) Miaka michache baadaye, Mfalme Senakeribu wa Ashuru aanzisha mashambulio ya kufa na kupona dhidi ya ufalme wa kusini wa Yuda. (2 Wafalme 18:13; Isaya 36:1) Jeshi kubwa la Ashuru lifagiapo nchi yote, yaonekana kwamba uharibifu kamili wa Yuda lazima ufike.
3 Lakini Ashuru, ambayo inapita mamlaka yake ya kuwatia nidhamu watu wa Mungu, sasa inafuatia tamaa yake yenye pupa ya kuushinda ulimwengu. (Isaya 10:7-11) Je, Yehova atakosa kuiadhibu Ashuru kwa sababu ya kuwatenda kinyama watu Wake? Je, ugonjwa wa kiroho wa taifa hilo utapata kuponywa? Twasoma majibu ya Yehova kwa maswali hayo katika Isaya sura ya 33.
Kumharibu Aharibuye
4, 5. (a) Ashuru itapata badiliko gani? (b) Isaya atoa sala gani kwa niaba ya watu wa Yehova?
4 Unabii huo waanza: “Ole wako uharibuye ila hukuharibiwa, utendaye hila wala hukutendwa hila! Utakapokwisha kuharibu, utaharibiwa wewe; na utakapokwisha kutenda kwa hila, wao watakutenda hila wewe.” (Isaya 33:1) Isaya azungumza moja kwa moja na aharibuye, yaani, Ashuru. Taifa hilo chokozi linapofikia upeo wa nguvu zake, yaonekana kuwa haliwezi kushindwa. ‘Limeharibu ila halikuharibiwa,’ limeharibu kabisa miji ya Yuda, na hata limenyakua mali kutoka kwa nyumba ya Yehova—na yaonekana limefanya hivyo bila kuadhibiwa! (2 Wafalme 18:14-16; 2 Mambo ya Nyakati 28:21) Hata hivyo, mambo yatabadilika sasa. “Utaharibiwa wewe,” Isaya atangaza kwa ujasiri. Unabii huo unawafariji kama nini watu waaminifu!
5 Katika kipindi hicho chenye kutia hofu, waabudu waaminifu-washikamanifu wa Yehova watahitaji kumtegemea ili awasaidie. Basi Isaya asali: “Ee BWANA, uturehemu; tumekungoja wewe; uwe wewe mkono wetu [wa nguvu na tegemeo] kila asubuhi, na wokovu wetu pia wakati wa taabu. Kabila za watu wamekimbia wakisikia kelele za fujo; mataifa wametawanyika ulipojiinua nafsi yako.” (Isaya 33:2, 3, Chapa ya 1989) Kwa kufaa, Isaya amwomba Yehova awakomboe watu Wake kama vile ambavyo Amefanya mara nyingi nyakati zilizopita. (Zaburi 44:3; 68:1) Na mara baada ya Isaya kutoa sala hiyo, yeye atabiri jibu la Yehova kuihusu!
6. Ni nini litakaloipata Ashuru, na kwa nini hilo lafaa?
6 “Na mateka yako [Waashuri] yatakumbwa kama wadudu wakumbavyo, wataruka juu yake kama arukavyo nzige.” (Isaya 33:4) Yuda inafahamiana na uvamizi wa nzige wenye kuangamiza. Hata hivyo, wakati huu adui za Yuda ndio watakaoangamizwa. Ashuru itashindwa kwa aibu, na wanajeshi wake watalazimika kukimbia, wakiacha nyuma mateka mengi yatakayokusanywa na wakazi wa Yuda! Yafaa kwamba Ashuru, inayojulikana kwa sababu ya ukatili wake, ipate uharibifu.—Isaya 37:36.
Ashuru wa Leo
7. (a) Ni nani leo wawezao kufananishwa na taifa la Israeli lenye ugonjwa wa kiroho? (b) Ni nani atakayetumika kama “fimbo” ya Yehova ya kuharibu Jumuiya ya Wakristo?
7 Unabii wa Isaya unatimiaje leo? Taifa la Israeli lenye ugonjwa wa kiroho laweza kufananishwa na Jumuiya ya Wakristo. Kama vile Yehova alivyotumia Ashuru kama “fimbo” ya kuadhibu Israeli, ndivyo atakavyotumia “fimbo” fulani kuiadhibu Jumuiya ya Wakristo—na vilevile sehemu zilizobaki za milki ya ulimwengu ya dini isiyo ya kweli, “Babiloni Mkubwa.” (Isaya 10:5; Ufunuo 18:2-8) “Fimbo” hiyo itakuwa mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa—shirika ambalo katika Ufunuo lafananishwa na hayawani-mwitu mwenye rangi-nyekundu-nyangavu aliye na vichwa saba na pembe kumi.—Ufunuo 17:3, 15-17.
8. (a) Ni nani awezaye kufananishwa na Senakeribu leo? (b) Senakeribu wa leo atapata ujasiri wa kumshambulia nani, na matokeo yatakuwaje?
8 Ashuru wa leo ashambuliapo eneo lote la dini isiyo ya kweli, itaonekana kwamba shambulizi hilo halizuiliki. Akiwa na mtazamo kama ule wa Senakeribu, Shetani Ibilisi atapata ujasiri wa kushambulia—hatashambulia tu mashirika yenye kuasi yanayostahili adhabu, bali atashambulia Wakristo wa kweli pia. Kwa kushirikiana na mabaki ya wana wa kiroho watiwa-mafuta wa Yehova, mamilioni ya watu ambao wametoka katika ulimwengu wa Shetani, unaotia ndani Babiloni Mkubwa, wanajipanga upande wa Ufalme wa Yehova. Shetani, aliye “mungu wa huu mfumo wa mambo,” huku akiwa amekasirishwa na msimamo wa Wakristo wa kweli wa kukataa kumpa heshima, ataanzisha mashambulio ya kufa na kupona dhidi yao. (2 Wakorintho 4:4; Ezekieli 38:10-16) Mashambulio hayo yajapokuwa yenye kutisha jinsi gani, watu wa Yehova hawatahitaji kutetemeka kwa hofu. (Isaya 10:24, 25) Mungu amewahakikishia kwamba atakuwa ‘wokovu wao wakati wa taabu.’ Yeye ataingilia kati na kumharibu Shetani na umati wake. (Ezekieli 38:18-23) Kama vile ilivyokuwa nyakati za kale, ndivyo wale wanaojaribu kuwaharibu watu wa Mungu watakavyoharibiwa wenyewe! (Linganisha Mithali 13:22b.) Jina la Yehova litatakaswa, na wenye kuokoka watathawabishwa kwa kuwa wametafuta “hekima na maarifa [na] kumcha BWANA.”—Soma Isaya 33:5, 6.
Onyo kwa Wasio na Imani
9. (a) “Mashujaa” na “wajumbe wa amani” wa Yuda watafanya nini? (b) Ashuru itaitikiaje hatua za Yuda za kutafuta amani?
9 Hata hivyo, wasio na imani nchini Yuda watapatwa na nini? Isaya afafanua kwa njia yenye kutia hofu jinsi Ashuru atakavyowaangamiza. (Soma Isaya 33:7.) “Mashujaa” wa kijeshi wa Yuda watalia kwa hofu shambulizi la Ashuru likaribiapo. “Wajumbe wa amani,” yaani, mabalozi waliotumwa kufanya mapatano ya amani na Waashuri wenye kupenda vita, watadhihakiwa na kutwezwa. Watalia kwa uchungu kwa sababu ya kushindwa kwao. (Linganisha Yeremia 8:15.) Ashuru mkatili hatawahurumia. (Soma Isaya 33:8, 9.) Atapuuza kwa ukatili maagano ambayo amefanya na wakazi wa Yuda. (2 Wafalme 18:14-16) Ashuru ‘ataidharau miji’ ya Yuda, akiidharau na kuidhihaki, pasipo kujali uhai wa kibinadamu. Hali itakuwa mbaya sana hivi kwamba itakuwa kana kwamba nchi yenyewe inaomboleza. Lebanoni, Sharoni, Bashani, na Karmeli vivyo hivyo zitauombolezea uharibifu huo.
10. (a) “Mashujaa” wa Jumuiya ya Wakristo watathibitikaje kuwa wasiofaa chochote? (b) Ni nani atakayewalinda Wakristo wa kweli wakati wa siku ya taabu juu ya Jumuiya ya Wakristo?
10 Hapana shaka hali kama hizo zitatokea karibuni, mataifa yaanzapo kushambulia dini. Kama ilivyokuwa katika siku ya Hezekia, kupambana kihalisi na majeshi hayo hakutafaa kitu. “Mashujaa” wa Jumuiya ya Wakristo—wanasiasa wake, watu wanaoipa fedha, na watu wengine wanaoichochea—hawataweza kuisaidia. “Maagano” ya kisiasa na ya kifedha, yanayokusudiwa kuyalinda masilahi ya Jumuiya ya Wakristo, yatavunjwa. (Isaya 28:15-18) Jitihada za majonzi za kuzuia uharibifu kupitia mapatano ya amani zitashindwa. Shughuli za kibiashara zitakoma, huku mali na vitega-uchumi vya Jumuiya ya Wakristo vikitwaliwa au kuharibiwa. Yeyote aliye na maoni ya kirafiki kuelekea Jumuiya ya Wakristo hatafanya lolote ila kusimama mbali na kuombolezea uharibifu wake. (Ufunuo 18:9-19) Je, Ukristo wa kweli utafagiliwa mbali pamoja na ule usio wa kweli? La, kwa sababu Yehova mwenyewe ahakikisha hivi: “Basi, sasa nitasimama; asema BWANA; sasa nitajiinua, sasa nitajitukuza.” (Isaya 33:10) Hatimaye, Yehova ataingilia kati kwa niaba ya watu waaminifu, kama Hezekia, na kuyakomesha mashambulizi ya Ashuru.—Zaburi 12:5.
11, 12. (a) Maneno ya Isaya 33:11-14 yatimizwa lini na jinsi gani? (b) Maneno ya Yehova yana onyo gani leo?
11 Watu wasio waaminifu hawawezi kuutegemea ulinzi huo. Yehova asema: “Ninyi mtachukua mimba ya makapi, mtazaa majani makavu; pumzi yenu ni moto utakaowateketeza wenyewe. Nao mataifa watakuwa kama kuchoma chokaa, kama miiba iliyokatika, iteketezwayo motoni. Sikieni, ninyi mlio mbali, niliyoyatenda; na ninyi mlio karibu, kirini uweza wangu. Wenye dhambi walio katika Sayuni wanaogopa; tetemeko limewashika wasiomcha Mungu; Ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto ulao; ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto uteketezao milele?” (Isaya 33:11-14) Yaonekana maneno hayo yahusu wakati ambapo Yuda yakabili adui mpya, yaani, Babiloni. Baada ya kifo cha Hezekia, Yuda yarudia maovu yake. Kwa makumi kadhaa ya miaka inayofuata, hali nchini Yuda zawa mbaya kufikia hatua ya taifa lote kuchomwa kwa moto wa hasira ya Mungu.—Kumbukumbu la Torati 32:22.
12 Mipango na mbinu mbovu ambazo watu waovu wamepanga ili kuepuka hukumu ya Mungu zaambulia patupu kama vile majani makavu. Kwa hakika, roho yenye kiburi na uasi ya taifa hilo ndiyo itakayochochea matukio yatakayosababisha kuharibiwa kwake. (Yeremia 52:3-11) Waovu “watakuwa kama kuchoma chokaa”—wataharibiwa kabisa! Wakazi wa Yuda wenye kuasi washikwa na hofu yenye kutisha watafakaripo uharibifu huo unaokuja. Maneno ya Yehova kwa Yuda isiyo na uaminifu yaeleza hali ya washiriki wa Jumuiya ya Wakristo leo. Wasipotii onyo la Mungu, wakati ujao wenye huzuni wawangojea.
“Aendaye kwa Haki”
13. Ni ahadi gani anayopewa yeye “aendaye kwa haki,” na ahadi hiyo ilitimizwaje kuhusiana na Yeremia?
13 Kinyume cha mambo hayo, ndipo Yehova asema: “Ni yeye aendaye kwa haki, anenaye maneno ya adili; ni yeye anayedharau faida ipatikanayo kwa dhuluma; akung’utaye mikono yake asipokee rushwa; azibaye masikio yake asisikie habari za damu; afumbaye macho yake asitazame uovu. Huyu ndiye atakayekaa juu; majabali ni ngome yake; atapewa chakula chake; maji yake hayatakoma.” (Isaya 33:15, 16) Kama mtume Petro alivyosema baadaye, “Yehova ajua jinsi ya kukomboa watu wenye ujitoaji-kimungu kutoka katika jaribu, bali kuweka akiba watu wasio waadilifu kwa ajili ya siku ya hukumu ili kukatiliwa mbali.” (2 Petro 2:9) Yeremia alikombolewa hivyo. Wakati wa mazingiwa ya Babiloni, watu walilazimika ‘kula mkate kwa kuupima, na kwa kuutunza sana.’ (Ezekieli 4:16) Hata wanawake fulani walikula nyama ya watoto wao wenyewe. (Maombolezo 2:20) Ingawa hivyo, Yehova alihakikisha kuwa Yeremia ametunzwa.
14. Wakristo leo waweza ‘kuendaje kwa haki’?
14 Vivyo hivyo Wakristo leo wapaswa ‘kwenda kwa haki,’ wakifuata viwango vya Yehova kila siku. (Zaburi 15:1-5) Ni lazima ‘wanene maneno ya adili’ na wakatae kusema uwongo. (Mithali 3:32) Labda upunjaji na rushwa ni mambo ya kawaida katika nchi nyingi, lakini hayo ni chukizo kwa yeye “aendaye kwa haki.” Lazima pia Wakristo wawe na “dhamiri yenye kufuata haki” katika shughuli za kibiashara, wakijitahidi kuepuka shughuli za udanganyifu au za upunjaji. (Waebrania 13:18; 1 Timotheo 6:9, 10) Na mtu “azibaye masikio yake asisikie habari za damu; afumbaye macho yake asitazame uovu” atateua muziki na vitumbuizo. (Zaburi 119:37) Wakati wa siku yake ya hukumu, Yehova atawalinda na kuwategemeza waabudu wake, wanaoishi kupatana na viwango hivyo.—Sefania 2:3.
Kumwona Mfalme Wao
15. Ni ahadi gani itakayowategemeza wahamishwa Wayahudi waaminifu?
15 Kisha Isaya ataja kidogo mambo yenye kusisimua kuhusu wakati ujao: “Macho yako yatamwona mfalme katika uzuri wake, yataona nchi iliyoenea sana. Moyo wako utatafakari hofu ile; Yuko wapi yeye aliyehesabu? yuko wapi yeye aliyeupima ushuru? yuko wapi yeye aliyeihesabu minara? Hutawaona watu wale wakali; watu wa maneno magumu usiyoweza kuyafahamu; wenye lugha ya kigeni usiyoweza kuelewa nayo.” (Isaya 33:17-19) Ahadi ya Mfalme wa Kimesiya wa wakati ujao na Ufalme wake itawategemeza Wayahudi waaminifu wakati wa miongo mingi ya miaka wakiwa uhamishoni huko Babiloni, hata ingawa waweza tu kuuona Ufalme huo kwa mbali. (Waebrania 11:13) Utawala wa Mesiya upatapo kuwa uhalisi hatimaye, utawala wa mabavu wa Babiloni utakuwa umekwisha toweka. Wenye kuokoka shambulizi la Ashuru watauliza hivi kwa furaha: “Wako wapi maofisa wa mtawala wa mabavu, waliotutoza kodi, kutushtaki, kuchukua ushuru wetu?”—Isaya 33:18, Moffatt.
16. Watu wa Mungu ‘wamemwona’ Mfalme wa Kimesiya tangu lini, na tokeo limekuwa nini?
16 Ijapokuwa maneno ya Isaya yatoa uhakikishio wa kurudishwa kutoka utekwani Babiloni, itabidi Wayahudi mmoja-mmoja wangojee ufufuo ili wapate utimizo kamili wa sehemu hii ya unabii huo. Namna gani watumishi wa Mungu leo? Tangu mwaka wa 1914, watu wa Yehova ‘wamemwona,’ au kumtambua, Mfalme wa Kimesiya, Yesu Kristo, katika uzuri wake wote wa kiroho. (Zaburi 45:2; 118:22-26) Tokeo ni kwamba wamekombolewa kutokana na uonevu na udhibiti wa mfumo mwovu wa Shetani. Wakiwa chini ya Sayuni, makao makuu ya Ufalme wa Mungu, wanafurahia usalama wa kweli wa kiroho.
17. (a) Ni ahadi gani zinazotolewa kuhusu Sayuni? (b) Ahadi za Yehova kuhusu Sayuni zatimizwaje kwa Ufalme wa Kimesiya na kwa wale wanaouunga mkono duniani?
17 Isaya aendelea: “Angalia Sayuni, mji wa sikukuu zetu; macho yako yatauona Yerusalemu umekuwa kao la raha; hema isiyotanga-tanga; vigingi vyake havitang’olewa, wala kamba zake hazitakatika. Bali huko BWANA atakuwa pamoja nasi, mwenye adhama; mahali penye mito mipana na vijito, pasipopita mashua na makasia yake; wala hapana merikebu ya vita itakayopita hapo.” (Isaya 33:20, 21) Isaya atuhakikishia kuwa Ufalme wa Kimesiya wa Mungu hauwezi kung’olewa wala kuharibiwa. Isitoshe, kwa wazi ulinzi huo unawafikia watu waaminifu duniani leo wanaounga mkono Ufalme. Hata ikiwa watu wengi mmoja-mmoja wajaribiwa vikali, raia za Ufalme wa Mungu wamehakikishiwa kwamba juhudi zozote za kutaka kuwaangamiza wakiwa kutaniko hazitafaulu kwa vyovyote. (Isaya 54:17) Yehova atawalinda watu wake kama vile handaki au mto zilindavyo mji. Adui yeyote yule atakayeinuka dhidi yao—hata awe mwenye nguvu kama “mashua na makasia yake” au “merikebu ya vita”—ataangamizwa!
18. Yehova hukubali wajibu gani?
18 Hata hivyo, kwa nini wapendao Ufalme wa Mungu wanaweza kuutumainia sana ulinzi huo? Isaya aeleza: “Kwa maana BWANA [“Yehova,” “NW”] ndiye mwamuzi wetu; BWANA ndiye mfanya sheria wetu; BWANA ndiye mfalme wetu; ndiye atakayetuokoa.” (Isaya 33:22) Yehova hukubali wajibu wa kuwalinda na kuwaelekeza watu wake, wanaotambua cheo chake akiwa Mwenye Enzi Mkuu. Watu hao hujitiisha kwa hiari chini ya utawala wake kupitia Mfalme wake wa Kimesiya, wakitambua kuwa Yehova ana mamlaka ya kutunga sheria na vilevile kuzitekeleza. Ingawa hivyo, kwa kuwa Yehova hupenda uadilifu na haki, utawala wake kupitia Mwana wake si mzigo kwa waabudu wake. Badala yake, wao ‘hupata faida’ kwa kujitiisha kwa mamlaka yake. (Isaya 48:17) Yeye hatawaacha kamwe waaminifu-washikamanifu wake.—Zaburi 37:28.
19. Isaya aelezaje hali ya kutoweza chochote ya adui za watu waaminifu wa Yehova?
19 Isaya awaambia adui za watu waaminifu wa Yehova: “Kamba zako zimelegea; hawakuweza kukaza sana shina la mlingoti wao; hawakuweza kulikunjua tanga; ndipo mapato ya mateka yaligawanywa, hata wachechemeao walipata mateka.” (Isaya 33:23) Adui yeyote anayekaribia hataweza lolote dhidi ya Yehova kama vile merikebu ya vita yenye mlingoti unaolegea na isiyo na matanga. Kuharibiwa kwa adui za Mungu kutatokeza mateka mengi hivi kwamba hata wasiojiweza watashiriki kuyatwaa. Basi twaweza kuwa na uhakika kwamba kupitia Mfalme Yesu Kristo, Yehova atapata ushindi dhidi ya adui zake katika “dhiki kubwa” inayokuja.—Ufunuo 7:14.
Uponyaji
20. Watu wa Mungu watapata uponyaji gani, nao wataupata lini?
20 Sehemu hii ya unabii wa Isaya yamalizia kwa ahadi yenye kusisimua: “Hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa; watu wakaao humo watasamehewa uovu wao.” (Isaya 33:24) Ugonjwa anaoutaja Isaya ni wa kiroho hasa, kwa maana wahusianishwa na dhambi, au “uovu.” Katika utimizo wa kwanza wa maneno hayo, Yehova aahidi kwamba baada ya kuachiliwa kwao kutoka utekwani Babiloni, taifa hilo litaponywa kiroho. (Isaya 35:5, 6; Yeremia 33:6; linganisha Zaburi 103:1-5.) Baada ya kusamehewa dhambi zao za awali, Wayahudi wanaorudi wataanzisha tena ibada safi huko Yerusalemu.
21. Waabudu wa Yehova leo hupata uponyaji wa kiroho kwa njia zipi?
21 Hata hivyo, unabii wa Isaya unatimizwa leo pia. Watu wa Yehova leo pia wameponywa kiroho. Wamekombolewa kutoka katika mafundisho yasiyo ya kweli kama vile kutokufa kwa nafsi, Utatu, na moto wa mateso. Wao hupata mwelekezo wa kiadili, unaowaweka huru kutoka kwa mazoea ya ukosefu wa adili na kuwasaidia kufanya maamuzi yanayofaa. Na kwa sababu ya dhabihu ya fidia ya Yesu Kristo, wao wana msimamo safi mbele za Mungu na wana dhamiri safi. (Wakolosai 1:13, 14; 1 Petro 2:24; 1 Yohana 4:10) Uponyaji huo wa kiroho una faida za kimwili. Kwa kielelezo, kuepuka ngono ya ukosefu wa adili na utumizi wa bidhaa za tumbaku huwalinda Wakristo dhidi ya maradhi ya kuambukizwa kingono na aina fulani za kansa.—1 Wakorintho 6:18; 2 Wakorintho 7:1.
22, 23. (a) Andiko la Isaya 33:24 litapata utimizo gani mkubwa wakati ujao? (b) Waabudu wa kweli leo wameazimia kufanya nini?
22 Zaidi ya hayo, maneno ya Isaya 33:24 yatatimizwa kwa njia kubwa zaidi baada ya Har–Magedoni, katika ulimwengu mpya wa Mungu. Chini ya utawala wa Ufalme wa Kimesiya, wanadamu wataponywa kimwili na kiroho. (Ufunuo 21:3, 4) Muda mfupi baada kuharibiwa kwa mfumo wa mambo wa Shetani, hapana shaka miujiza kama ile ambayo Yesu alifanya akiwa duniani itafanyika duniani kote. Vipofu wataona, viziwi watasikia, vilema watatembea! (Isaya 35:5, 6) Hiyo itawawezesha watakaookoka wa dhiki kubwa washiriki katika kazi tukufu ya kuigeuza dunia kuwa katika hali ya kiparadiso.
23 Baadaye, ufufuo utakapoanza, yaonekana wale wanaorudi kwenye uhai watainuliwa wakiwa na afya njema. Lakini dhabihu ya fidia itakapoendelea kutumiwa zaidi, faida nyingi zaidi za kimwili zitatokea, hadi wanadamu watakapofikia ukamilifu. Ndipo waadilifu ‘watakapokuja kwenye uhai’ kwa ukamili. (Ufunuo 20:5, 6) Wakati huo, kwa njia ya kiroho na pia ya kimwili, “Hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.” Hiyo ni ahadi nzuri kama nini! Waabudu wote wa kweli leo na waazimie kuwa miongoni mwa wale watakaopata utimizo wake!
[Picha katika ukurasa wa 344]
Isaya asali kwa Yehova akiwa na uhakika
[Picha katika ukurasa wa 353]
Kwa sababu ya dhabihu ya fidia, watu wa Yehova wana msimamo safi mbele zake
[Picha katika ukurasa wa 354]
Katika ulimwengu mpya, kutakuwapo uponyaji mkubwa wa kimwili