Kunguru—Ni Nini Kinachomfanya Awe Tofauti?
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KANADA
NI NANI awezaye kufikiri kwamba ndege huyu mwenye rangi nyeusi na mlio wa kuomboleza ni wa kipekee? Kwani, kwa mtu asiyefahamu ndege, kwa mara ya kwanza aweza kuonekana kama aina ya kunguru-mdogo ambaye amekua kupita kiasi. Yeye havutii uangalifu haraka kama kungurumrembo, ambaye ni binamu yake maridadi mwenye manyoya ya rangi buluu nyangavu. Ni watu wachache wanaoweza kuchukulia sauti ya kunguru iliyo kama ya chura kuwa wimbo, ingawa ameainishwa miongoni mwa ndege waimbaji. Hata hivyo, usimchukulie ndege huyo vivi-hivi. Kile anachokosa ili awe na wimbo mtamu na umaridadi analipia zaidi kwa njia nyinginezo. Kunguru ana urembo wake na tabia zake za kipekee. Hakika, wastadi wengi wa ndege huainisha kunguru katika tabaka yake peke yake.
Mambo Yanayomtofautisha
Kunguru wa kawaida (Corvus corax) ndiye mkubwa zaidi na mwenye adhama zaidi katika familia nzima ya kunguru (Corvidae). Anaweza kuwa mzito mara mbili kuliko kunguru-mdogo na kuwa na urefu wa sentimeta 60, mabawa yake yakipanuka kwa karibu meta 1. Yeye ni tofauti na kunguru-mdogo kwa sababu ana mdomo mzito zaidi na mkia mrefu wenye umbo la kabari. Ukimchunguza kwa karibu zaidi utaona pia manyoya yake ya koo ambayo hayajalainika ambayo humtambulisha. Hewani, yeye ni maarufu kwa kupaa juu sana, huku kunguru wengine wakipendelea kupiga mabawa na kunyiririka.
Kunguru huonwa kuwa ndege mkubwa zaidi kati ya ndege wote ambao huchuchumaa wapumzikapo. Kumwona ndege huyu mkubwa akiwa amechuchumaa kwenye tawi akipumzika kwafanya ujiulize ni kwa nini hawezi kuanguka. Yeye ana ukucha wenye nguvu sana nyuma ya kila mguu wa kushika nao tawi; hata hivyo, siri ya kuchuchumaa kwake imo katika chombo chake cha ndani cha kujifunga. Misuli na mishipa huvuta vidole vijikunje kwa namna ya kushika kitu mara achuchumaapo. Miguu yenye nguvu ya kunguru ambayo hufanya kazi mbalimbali pia hufaa kwa kutembea na kuchakura, hivyo ikimwezesha kupata chakula katika malisho ya aina mbalimbali.
Mweneo na Kuruka kwa Huyu “Radi Nyeusi”
Ni ndege wachache ambao wameenea sana kama kunguru. Kwa kweli yeye ni mzururaji. Aweza kupatikana katika sehemu nyingi za Kizio cha Kaskazini. Yeye huishi katika maeneo yanayotofautiana kama vile jangwani; katika misitu ya misunobari ya Kanada na Siberia, ambako yeye hutengeneza kiota tata kwa vijiti na vitu vinginevyo vinavyopatikana katika miti mirefu; katika majabali ya bahari katika Amerika Kaskazini na nchi za Skandinavia; na katika nyanda za Aktiki na visiwa vya Bahari-Kuu ya Aktiki. Pori yaonekana kuwa mahali ambapo yeye hupatikana sana, kwa kuwa mara nyingi kunguru ni ndege wa pori.
Mifano ya makao yake yenye kutofautiana yaweza kupatikana katika bara la Biblia, ambako aina mbili za kunguru-mkubwa mweusi huishi. Aina moja huishi katika tambarare kubwa za jangwa katika kusini, na aina nyingine huishi katika eneo la kaskazini. Kunguru weusi hufanyiza viota sehemu zilizositiriwa katika miamba kandokando ya mabonde. Kunguru walitumiwa na Yehova kumlisha Eliya alipokuwa amejificha katika bonde la mvo la Kerithi. (1 Wafalme 17:3-6) Simulizi la Isaya la kunguru wanaoishi katika “ukiwa na timazi ya utupu” ya Edomu pia hufafanua makao yao.—Isaya 34:11.
Kunguru ni warukaji wa ajabu. Wao huvutia sana wanapopaa bila jitihada yoyote wakizunguka-zunguka kwa mapana, wakichunguza chini kwa ajili ya chakula. Wao hufanya tamasha za hewani kwa ustadi—wakipinduka-pinduka hata wakiruka kwa muda mfupi wakiwa chali—hasa wakati wa kujamiiana na, inaonekana, nyakati nyingine kwa kujifurahisha tu. Mruko wa kunguru wafafanuliwa vizuri na Bernd Heinrich katika Ravens in Winter: “Yeye hupiga mbizi na kupinduka-pinduka kama radi nyeusi angani au huenda kwa kasi na kwa uanana.” Yeye aongezea kwamba kunguru ni “mrukaji hodari sana, na ana uwezo mwingine zaidi.” Nguvu ya kunguru ya kuruka imesemwa kuwa ndiyo sababu iliyofanya Noa amchague kuwa kiumbe cha kwanza kutumwa nje ya safina wakati wa Gharika.—Mwanzo 8:6, 7.
Wezi Stadi Wenye Kubadilikana na Hali
Wataalamu wa mambo ya asili humwona kunguru kuwa mojawapo ya ndege walio stadi sana na wenye kubadilikana na hali. Kama chanzo kimoja cha habari kinavyosema, “ujanja wake ni mashuhuri.” Kunguru akabilipo hali yoyote ile, yeye hufaulu kubadilikana na hali hizo, hasa kwa habari ya chakula. Bila shaka, kutokuwa mteuzi wa chakula humsaidia! Kunguru hula karibu kila kitu apatacho—matunda, mbegu, kokwa, samaki, mizoga, wanyama wadogo, takataka. Na yeye hajali anapata wapi chakula, hata akifikia hatua ya kuchimba theluji ili kupata mifuko yenye vyakula vilivyotupwa katika halihewa yenye baridi sana katika sehemu za kaskazini za eneo lake. Pia kunguru hufuata wawindaji na wavuvi kwa siku nyingi, kwa njia fulani wakihisi kwamba watapata chakula kwa wakati ufaao.
Washiriki wa familia ya kunguru-mdogo ni wezi sugu na kunguru hawakosi tabia hiyo. Wao hawaogopi kuibia ndege au wanyama wengine chakula nao wameonekana wakihadaa mbwa. Kunguru wawili huchukua zamu—mmoja akimkengeusha mbwa huku mwingine akinyakua chakula. Mchoro wa Wainuit huonyesha kunguru mjanja akiiba samaki kutoka kwa mvuvi mmoja wa barafuni.
Kunguru hupenda sana mbwa-mwitu, kwa kawaida wakifuata makundi ya mbwa-mwitu. Wao hula wanyama waliouawa na mbwa-mwitu, na hapa tena wao huonekana kufurahia sana visanga wanapofanya hivyo. Mwanabiolojia wa mbwa-mwitu L. David Mech arekodi kuona kunguru wakiwachezea shere mbwa-mwitu. Yeye asimulia juu ya kunguru mmoja aliyemwendea mbwa-mwitu aliyekuwa akipumzika, akaudonoa mkia wake na kuruka kando mbwa-mwitu alipotaka kumwuma. Mbwa-mwitu alipomnyemelea huyo kunguru, ndege huyo alimwacha afike futi moja kutoka kwake kabla ya kuruka. Kisha alitua futi chache tu mbele ya mbwa-mwitu na kurudia mchezo huo. Simulizi jingine lasimulia kunguru akicheza mchezo wa kugusana na watoto wa mbwa-mwitu. Watoto hao walipochoka na mchezo huo, huyo kunguru akaanza kulia mpaka watoto hao wakaanza kucheza tena.
Gazeti Canadian Geographic larejezea tangazo la redio kutoka Yellowknife, Mkoa wa Kaskazini-Magharibi, lililosimulia juu ya kunguru wakiwa kwenye paa za mabati zilizoinama za majengo ya kibiashara, inaonekana wakingoja watu wanaopita chini wasio na habari ili waweze kuwamwagia theluji iliyorundamana juu. Si ajabu kwamba Wahaida wa pwani ya magharibi ya Kanada huita kunguru mjanja!
Sauti na Uwezo wa Kujifunza
“Misamiati” ya kunguru ni mingi na yenye kutofautiana. Kwa kuongezea ile sauti ya ndani kama ya chura inayotambulika kwa urahisi—ambayo huonwa kuwa ishara ya kusumbuliwa—inasemekana sauti yake huonyesha wororo, furaha, mshangao, msisimko, na hasira. Pia kunguru aweza kuiga milio ya ndege wengine ambao wanaweza kuiga, hasa wakiiga kabisa sauti ya kunguru-mdogo.
Imebishaniwa kadiri ambavyo kunguru aweza kufundishwa kusema. Hata hivyo, Candace Savage, katika kitabu chake Bird Brains, asema juu ya masimulizi ya kunguru waliofugwa waliofundishwa kuiga usemi wa wanadamu. Hekaya zasema kwamba mwanashairi Edgar Allan Poe alipata kunguru na kumfundisha kwa bidii kusema katika sauti yake kama ya chura neno “nevermore,” jambo lililochochea shairi lake mashuhuri The Raven, ambalo linasimulia “kijana akiomboleza kifo cha mpendwa wake.”
Hakuna ubishi juu ya uwezo wa kunguru wa kujifunza. Ikiwa ndege waweza kuainishwa kulingana na akili zao, inaonekana kunguru anaweza kuwa wa kwanza. Mwanabiolojia wa viumbe Bernd Heinrich asema kwamba kunguru “huonwa kuwa mwerevu zaidi miongoni mwa ndege.” Yeye asema kwamba “wanapotahiniwa, kunguru huonyesha ufahamu wenye kina.” Katika jaribio moja, baada ya muda wa saa sita, kunguru mmoja aligundua njia ya kupata nyama iliyokuwa imening’inizwa kwa kamba, na kunguru-wadogo bado walikuwa wakijaribu kutatua jambo hilo siku 30 baadaye. Kunguru hata wamepata kufundishwa kuhesabu. Huenda ujuzi wao huchangia urefu wa maisha yao, kwani kunguru huishi kwa zaidi ya miaka 40 porini na kufikia miaka 70 utekwani. Bila shaka, uwezo wowote wa kunguru ni lazima umetokana na hekima ya Muumba wake.
Ndege huyu ni mashuhuri sana, na anastahiwa na wale wanaofahamu sifa zake za kipekee. Anaweza kupatikana katika hekaya za watu kotekote ulimwenguni. Sifa zake zimeenezwa na waandikaji wa wakati uliopita na wa sasa. (Ona sanduku, ukurasa 24.) Ndiyo, kunguru ni ndege mwenye kupendeza sana. Lakini ni nini kiwezacho kusemwa juu ya urembo wake?
Urembo Wake wa Kipekee
Je, hujapata kusikia juu ya ‘nywele nyeusi kama kunguru’? (Wimbo Ulio Bora 5:11) Manyoya yake meusi ti na buluu ya kijivu yanayometameta pamoja na mmeremeto wa kizambarau—sehemu za tumbo wakati mwingine zikiwa na rangi hafifu ya kijani—hufafanua kikamili neno “kunguru.” Ebu wazia kunguru akipaa na huo ukubwa wake wenye kuvutia na manyoya meusi yenye kumetameta, akiwa tofauti kabisa na utupu wa makao yake ya jangwa. Au wazia tofauti iliyoko kati ya ndege huyo mweusi ti na theluji safi na nyeupe iliyotoka tu kunyesha. Wasanii wamenasa urembo wa kunguru. Mchoraji Robert Bateman akumbuka: “Nilivutiwa na miinuko mizuri ajabu yenye theluji ya Hifadhi ya Yellowstone, mandhari nyangavu kabisa ambayo ilipatana kabisa na mwili wenye nguvu wa kunguru.”
Hakika, yaweza kusemwa kwamba kwa habari ya urembo, historia, mweneo, urukaji, ujanja, na uvumilivu, kunguru ni ndege wa kipekee.
Kunguru kwenye kurasa 23-25: © 1996 Justin Moore
[Sanduku katika ukurasa wa 24]
Kunguru Katika Hekaya na Fasihi
HEKAYA:
Hekaya za Kichina, Kimisri, Kigiriki, Kiyahudi, na za Siberia huonyesha kunguru kuwa mtabiri wa dhoruba au wa hali mbaya ya hewa. Labda hekaya hizo zilitokana na Noa na Furiko.
Kunguru hufananisha uhai na uumbaji katika hekaya za Siberia na yeye ni mungu-muumba wa Wenyeji wa Amerika Kaskazini.
Katika hekaya za Kiafrika, za Asia, na za Ulaya, kunguru ni ishara ya kifo.
FASIHI:
Katika Biblia kunguru ana sifa ya kuwa ndege wa kwanza kutajwa humo.—Mwanzo 8:7.
Kunguru katika vitabu vya Shakespeare huonyeshwa hasa wakiwa waovu (Julius Caesar, Macbeth, Othello) na pia wanaonyeshwa kuwa wafadhili wanaolisha watoto waliotupwa.—Titus Andronicus, The Winter’s Tale.
Charles Dickens alionyesha kunguru kuwa kitu cha vichekesho katika Barnaby Rudge.
Katika shairi lake The Raven, Edgar Allan Poe alishirikisha kunguru na mapenzi yaliyopotea na mtamauko.
[Sanduku katika ukurasa wa 25]
Mambo ya Kujifunza
Kuna mambo ya kujifunza kutokana na kunguru. Ni Mwana wa Mungu mwenyewe aliyesema: “Angalieni vema kwamba kunguru hawapandi mbegu wala hawavuni, nao hawana bohari wala ghala, na bado Mungu huwalisha.” (Luka 12:24) Kwa kuwa mara nyingi yeye huishi katika sehemu tupu, ni lazima watafute chakula mbali. Kunguru huchagua mwenzi mmoja tu kwa maisha nao ni wazazi wenye kujitoa. Wanapolea makinda, wao huhitaji kuleta chakula daima ili kunyamazisha vilio vikubwa vya makinda wenye njaa. Alipokuwa akifundisha Ayubu somo kuhusu hekima inayoonyeshwa na uumbaji, Yehova alitia ndani mfano wa kunguru. (Ayubu 38:41) Kwa kuwa Mungu humwandalia kunguru, ambaye alitangazwa kuwa si safi kulingana na Sheria ya Kimusa, twaweza kuwa na hakika kwamba yeye hataacha watu wanaomtumaini.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]
Kunguru katika ukurasa wa 23-5: © 1996 Justin Moore