Sura ya 29
Mfalme Apata Thawabu kwa Sababu ya Imani Yake
1, 2. Hezekia alithibitikaje kuwa mfalme bora kuliko Ahazi?
HEZEKIA alikuwa na umri wa miaka 25 alipokuwa mfalme wa Yuda. Je, angekuwa mtawala wa aina gani? Je, angemwiga baba yake, Mfalme Ahazi, na kuwachochea raia zake waabudu miungu isiyo ya kweli? Au angewaongoza watu wamwabudu Yehova, kama alivyofanya baba yake wa zamani, Mfalme Daudi?—2 Wafalme 16:2.
2 Muda mfupi baada ya Hezekia kuanza kutawala, ikawa wazi kwamba alikusudia ‘kufanya yaliyo mema machoni pa BWANA.’ (2 Wafalme 18:2, 3) Katika mwaka wake wa kwanza, aliagiza hekalu la Yehova lirekebishwe na utumishi wa hekalu urejeshwe. (2 Mambo ya Nyakati 29:3, 7, 11) Kisha akapanga sherehe kubwa ya Sikukuu ya Kupitwa ambapo taifa zima lilialikwa—pamoja na makabila kumi ya Israeli kaskazini. Karamu hiyo ilikumbukwa kama nini! Hapakuwa karamu kama hiyo tangu siku za Mfalme Solomoni.—2 Mambo ya Nyakati 30:1, 25, 26.
3. (a) Wakazi wa Israeli na Yuda waliohudhuria Sikukuu ya Kupitwa ambayo Hezekia alipanga walichukua hatua gani? (b) Wakristo leo wanajifunza nini kutokana na hatua ya dhati iliyochukuliwa na watu waliohudhuria Sikukuu ya Kupitwa?
3 Mwishoni mwa sherehe ya Sikukuu ya Kupitwa, waliohudhuria walichochewa kuzivunja-vunja nguzo takatifu, kuyakata-kata maashera, kubomoa mahali pa juu na madhabahu ya miungu yao isiyo ya kweli, kisha wakarudi katika miji yao, huku wakiwa wameazimia kumtumikia Mungu wa kweli. (2 Mambo ya Nyakati 31:1) Mtazamo huo wa kidini ulikuwa kinyume kama nini cha ule wa awali! Wakristo wa kweli leo waweza kujifunza kutokana na mambo hayo umuhimu wa ‘kutoachilia mbali kukusanyika pamoja wao wenyewe.’ Makusanyiko hayo, yawe katika makutaniko ya kwao au katika makusanyiko na mikusanyiko mikubwa zaidi, hutimiza fungu muhimu katika kuwapa kitia-moyo na kuhamasishwa na udugu na vilevile na roho ya Mungu ili “kuchocheana kwenye upendo na kazi zilizo bora.”—Waebrania 10:23-25.
Imani Yajaribiwa
4, 5. (a) Hezekia ameonyeshaje uhuru wake kutoka kwa Ashuru? (b) Senakeribu amechukua hatua gani ya kijeshi dhidi ya Yuda, na Hezekia achukua hatua gani ili kuepuka shambulio la upesi dhidi ya Yerusalemu? (c) Hezekia afanya matayarisho gani ya kulinda Yerusalemu dhidi ya Waashuri?
4 Majaribu mazito yalikuwa mbele ya Yerusalemu. Hezekia amevunja mwungano ambao Ahazi, baba yake asiye na imani, alifanya pamoja na Waashuri. Hata amewatiisha Wafilisti, ambao ni washirika wa Ashuru. (2 Wafalme 18:7, 8) Hayo yamemkasirisha mfalme wa Ashuru. Basi twasoma: “Ikawa, katika mwaka wa kumi na nne wa kumiliki kwake mfalme Hezekia, Senakeribu, mfalme wa Ashuru, akapanda ili kupigana na miji yote ya Yuda yenye boma, akaitwaa.” (Isaya 36:1) Hezekia, labda akitumaini kulinda jiji la Yerusalemu lisishambuliwe upesi na jeshi lenye ukatili la Ashuru, akubali kumpa Senakeribu ushuru mkubwa wa talanta 300 za fedha na 30 za dhahabu.a—2 Wafalme 18:14.
5 Kwa kuwa hazina ya mfalme haina dhahabu na fedha ya kutosha kulipa ushuru huo, Hezekia atwaa vito vyovyote awezavyo kupata hekaluni. Yeye pia aing’oa milango ya hekalu, ambayo imetandwa kwa dhahabu, na kuipeleka kwa Senakeribu. Hilo lamridhisha Mwashuri, lakini kwa muda mfupi tu. (2 Wafalme 18:15, 16) Labda Hezekia atambua kuwa Waashuri hawataachana na Yerusalemu kwa muda mrefu. Kwa hiyo, sharti matayarisho yafanywe. Watu waziba chemchemi za maji ambapo Waashuri wanaovamia waweza kupata maji. Hezekia pia aimarisha ngome za Yerusalemu na kukusanya zana za vita, zikiwemo “silaha na ngao tele.”—2 Mambo ya Nyakati 32:4, 5.
6. Hezekia amtumaini nani?
6 Hata hivyo, Hezekia hatumaini mbinu za vita zenye ujanja wala katika ngome, bali amtumaini Yehova wa majeshi. Awahimiza wakuu wake wa kijeshi: “Iweni hodari, na wa moyo mkuu, msiogope, wala msifadhaike kwa sababu ya mfalme wa Ashuru, wala kwa majeshi yote walio pamoja naye; kwa maana yupo mkuu pamoja nasi kuliko aliye pamoja naye; kwake upo mkono wa mwili; ila kwetu yupo BWANA [“Yehova,” NW], Mungu wetu, kutusaidia, na kutupigania mapigano yetu.” Kwa kuitikia, watu waanza ‘kuyategemea maneno ya Hezekia, mfalme wa Yuda.’ (2 Mambo ya Nyakati 32:7, 8) Hebu piga picha ya matukio yenye kusisimua yanayofuata tuchunguzapo sura ya 36 hadi 39 ya unabii wa Isaya.
Rabshake Atoa Hoja Yake
7. Rabshake ni nani, na kwa nini atumwa Yerusalemu?
7 Senakeribu amtuma Rabshake (ni jina la cheo cha kijeshi, wala si jina la mtu binafsi) pamoja na wakuu wengine wawili kwenda Yerusalemu ili kulilazimisha jiji kusalimu amri. (2 Wafalme 18:17) Eliakimu msimamizi wa nyumba ya Hezekia, Shebna mwandishi, na Yoa mwana wa Asafu mwenye kuandika tarehe, ambao ni wawakilishi watatu wa Hezekia wawalaki watu hao nje ya ukuta wa jiji.—Isaya 36:2, 3, kielezi-chini.
8. Rabshake ajaribu kuuvunjaje upinzani wa Yerusalemu?
8 Lengo la Rabshake ni moja tu, yaani, kushawishi Yerusalemu kusalimu amri pasipo pigano. Huku akiongea katika Kiebrania, kwanza apaaza sauti: “Ni tumaini gani hili unalolitumainia? . . . Unamtumaini nani hata ukaniasi mimi?” (Isaya 36:4, 5) Kisha Rabshake awadhihaki Wayahudi waliojaa woga, akiwakumbusha kuwa wameachwa peke yao kabisa. Waweza kumwendea nani awasaidie? Je, wauendee ‘mwanzi uliopondeka,’ yaani, Misri? (Isaya 36:6) Wakati huu, Misri yafanana na mwanzi uliopondeka; kwa kweli, Ethiopia imeishinda kwa muda serikali hiyo ya ulimwengu ya awali, na Farao wa sasa wa Misri, Mfalme Tirhaka, si Mmisri bali ni Mwethiopia. Na Ashuru yakaribia kumshinda. (2 Wafalme 19:8, 9) Kwa kuwa Misri haiwezi kujiokoa, haitafaa kitu kwa Yuda.
9. Yaelekea ni nini kinachomfanya Rabshake aamue kwamba Yehova atawaacha watu Wake, lakini ukweli wa mambo ni nini?
9 Rabshake sasa abisha kwamba Yehova hatawapigania watu Wake kwa sababu wamemchukiza Yeye. Rabshake asema: “Lakini ukiniambia, Tunamtumaini BWANA [“Yehova,” “NW”], Mungu wetu, je! si yeye ambaye Hezekia ameondoa mahali pake mlimoinuka, na madhabahu zake?” (Isaya 36:7) Ni wazi kwamba Wayahudi wamemrudia, wala siyo kumkataa, Yehova hasa kwa kuondoa mahali pa juu na madhabahu nchini.
10. Kwa nini si kitu iwapo walinzi wa Yuda ni wengi au ni wachache?
10 Kisha Rabshake awakumbusha Wayahudi kwamba wao ni hoi kabisa kijeshi. Atoa mwito huu wenye dhihaka: “Nitakupa farasi elfu mbili, ikiwa wewe kwa upande wako waweza kupandisha watu juu yao.” (Isaya 36:8) Hata hivyo je, kweli ni kitu iwapo askari wapanda-farasi waliozoezwa wa Yuda ni wengi au ni wachache? La, kwa sababu wokovu wa Yuda hautegemei nguvu kubwa za kijeshi. Andiko la Mithali 21:31 laeleza mambo hivi: “Farasi huwekwa tayari kwa siku ya vita; lakini BWANA [“Yehova,” NW] ndiye aletaye wokovu.” Kisha Rabshake asema Yehova awabariki Waashuri, wala si Wayahudi. Kama sivyo, yeye adai, Waashuri wasingaliweza kamwe kupenya kadiri hiyo katika eneo la Yuda.—Isaya 36:9, 10.
11, 12. (a) Kwa nini Rabshake asisitiza kusema katika “lugha ya Kiyahudi,” naye ajaribuje kuwashawishi Wayahudi wanaosikiliza? (b) Huenda maneno ya Rabshake yakawaathirije Wayahudi?
11 Wawakilishi wa Hezekia wahangaikia athari za hoja za Rabshake juu ya watu wanaomsikia wakiwa juu ya ukuta wa jiji. Maofisa hao Wayahudi waomba hivi: “Tafadhali, sema na watumishi wako kwa lugha ya Kiashuri; maana tunaifahamu; wala usiseme nasi kwa lugha ya Kiyahudi, masikioni mwa watu wote walio ukutani.” (Isaya 36:11) Lakini Rabshake hanuii kusema katika lugha ya Kiashuri. Ataka kutia shaka na hofu katika Wayahudi ili wasalimu amri na jiji la Yerusalemu lishindwe pasipo pigano! (Isaya 36:12) Kwa hiyo, Mwashuri asema tena katika “lugha ya Kiyahudi.” Awaonya wakazi wa Yerusalemu: “Hezekia asiwadanganye, kwa maana hataweza kuwaokoa.” Baada ya kusema hayo, ajaribu kuwashawishi wale wanaomsikiliza kwa kufafanua jinsi ambavyo maisha yangekuwa kwa Wayahudi chini ya utawala wa Ashuru: “Fanyeni suluhu na mimi, mkatoke mnijie, mkale kila mtu matunda ya mzabibu wake na matunda ya mtini wake, mkanywe kila mmoja maji ya birika yake mwenyewe; hata nije nikawachukue mpaka nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai, nchi ya mkate na mashamba ya mizabibu.”—Isaya 36:13-17.
12 Wayahudi hawatavuna mwaka huu—uvamizi wa Ashuru umewazuia wasipande mimea. Hapana budi kwamba tazamio la kula zabibu tamu na kunywa maji safi lawavutia sana watu wanaosikiliza ukutani. Lakini Rabshake bado aendelea kujaribu kuwadhoofisha Wayahudi.
13, 14. Licha ya hoja za Rabshake, kwa nini mambo yaliyolikumba Samaria hayafai kwa hali ya Yuda?
13 Rabshake atoa silaha nyingine ya maneno kutoka katika ghala ya hoja zake. Awaonya Wayahudi wasimwamini Hezekia iwapo asema: “BWANA [“Yehova mwenyewe,” “NW”] atatuokoa.” Rabshake awakumbusha Wayahudi kuwa miungu ya Samaria haikuweza kuwazuia Waashuri wasiyashinde yale makabila kumi. Na je, vipi kuhusu miungu ya mataifa mengine ambayo Ashuru imeshinda? “Wako wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi?” yeye adai. “Wako wapi miungu ya Sefarvaimu? Je! wameiokoa Samaria na mkono wangu?”—Isaya 36:18-20.
14 Ni wazi kwamba Rabshake, mwabudu wa miungu isiyo ya kweli haelewi kwamba kuna tofauti kubwa kati ya Samaria lenye kuasi na Yerusalemu linalotawaliwa na Hezekia. Miungu isiyo ya kweli ya Samaria haikuwa na nguvu zozote za kuuokoa ufalme huo wa makabila kumi. (2 Wafalme 17:7, 17, 18) Kwa upande mwingine, Yerusalemu linalotawaliwa na Hezekia limeikataa miungu isiyo ya kweli nalo limerudia kumtumikia Yehova. Hata hivyo, wale wawakilishi watatu Wayudea hawajaribu kumweleza Rabshake jambo hilo. “Wakanyamaza kimya; wala hawakumjibu hata neno moja; maana ilikuwa amri ya mfalme, kwamba, Msimjibu neno.” (Isaya 36:21) Eliakimu, Shebna, na Yoa wamrudia Hezekia na kutoa ripoti rasmi ya maneno ya Rabshake.—Isaya 36:22.
Hezekia Afanya Uamuzi
15. (a) Hezekia akabili uamuzi gani sasa? (b) Yehova awapaje watu wake uhakikishio?
15 Mfalme Hezekia apaswa kufanya uamuzi sasa. Je, Yerusalemu litajisalimisha kwa Waashuri? litaungana na Misri? au litakazana na kupigana? Hezekia amebanwa sana. Aenda kwa hekalu la Yehova huku akiwatuma Eliakimu na Shebna, pamoja na wazee wa makuhani, kupata habari kwa Yehova kupitia nabii Isaya. (Isaya 37:1, 2) Huku wakiwa wamevaa nguo za magunia, wajumbe wa mfalme wamwendea Isaya, wakisema: “Siku hii ni siku ya dhiki, na aibu, na matukano . . . Yamkini BWANA, Mungu wako, atayasikia maneno ya huyo amiri ambaye mfalme wa Ashuru, bwana wake, amemtuma ili amtukane Mungu aliye hai; na BWANA, Mungu wako atayakemea maneno aliyoyasikia.” (Isaya 37:3-5) Naam, Waashuri wanashindana na Mungu aliye hai! Je, Yehova atazingatia dhihaka zao? Yehova awahakikishia Wayahudi hivi kupitia Isaya: “Usiyaogope maneno uliyoyasikia, ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenitukana. Tazama, nitatia roho ndani yake, naye atasikia kivumi, na kurudi hata nchi yake mwenyewe, nami nitamwangusha kwa upanga katika nchi yake mwenyewe.”—Isaya 37:6, 7.
16. Senakeribu atuma barua za aina gani?
16 Wakati huohuo, Rabshake aitwa kwenda kumsaidia Senakeribu mfalme wakati huyo anapopigana vitani huko Libna. Senakeribu atalishughulikia Yerusalemu baadaye. (Isaya 37:8) Ingawa hivyo, kuondoka kwa Rabshake hakuondoi mkazo juu ya Hezekia. Senakeribu atuma barua zenye vitisho zinazoeleza mambo ambayo wakazi wa Yerusalemu waweza kutarajia iwapo wakataa kusalimu amri: “Umesikia habari ya mambo yote, ambayo wafalme wa Ashuru wamezitenda nchi zote, kwa kuziangamiza kabisa je! utaokoka wewe? Je! miungu ya mataifa, ambao baba zangu waliwaangamiza kabisa, wamewaokoa? . . . Yuko wapi mfalme wa Hamathi, na mfalme wa Arpadi na mfalme wa mji wa Sefarvaimu, wa Hena, na wa Iva?” (Isaya 37:9-13) Kwa jumla, Mwashuri amaanisha kwamba ni upumbavu kupinga—upinzani utaleta matata zaidi tu!
17, 18. (a) Hezekia ana nia gani amwombapo Yehova ulinzi? (b) Yehova amjibuje Mwashuri kupitia Isaya?
17 Akiwa anahangaikia sana matokeo ya uamuzi ambao lazima afanye, Hezekia azitandaza barua za Senakeribu mbele za Yehova hekaluni. (Isaya 37:14) Yeye amwomba Yehova kwa dhati ili asikie vitisho vya Mwashuri, akimaliza sala yake kwa maneno: “Basi sasa, BWANA, Mungu wetu, utuokoe na mkono wake, falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe BWANA [“Mungu,” “NW”], wewe peke yako.” (Isaya 37:15-20) Ni wazi kutokana na hayo kwamba Hezekia hahangaikii hasa ukombozi wake mwenyewe, bali aibu itakayolipata jina la Yehova iwapo Ashuru itashinda Yerusalemu.
18 Yehova ajibu sala ya Hezekia kupitia Isaya. Yerusalemu halipasi kujisalimisha kwa Ashuru; lazima lisimame imara. Akizungumza kana kwamba anasema na Senakeribu, Isaya ataarifu kwa ujasiri ujumbe wa Yehova kwa Mwashuri: “Bikira, binti Sayuni, anakudharau, anakudhihaki sana; binti Yerusalemu anatikisa kichwa chake [kwa dhihaka] juu yako.” (Isaya 37:21, 22) Ni kana kwamba Yehova aongeza kusema: ‘Wewe ni nani hata umdhihaki Mtakatifu wa Israeli? Nayajua matendo yako. Una tamaa kubwa za makuu; unajisifu sana. Umezitumaini nguvu zako za kijeshi nawe umeshinda nchi nyingi. Lakini wewe waweza kushindwa. Nitabatilisha mipango yako. Nitakushinda. Ndipo nitakapokutenda wewe kama ulivyowatenda wengine. Nitatia kulabu katika pua yako na kukurudisha hadi Ashuru!’—Isaya 37:23-29.
“Kwako Wewe Dalili Ndiyo Hii”
19. Yehova ampa Hezekia dalili gani, nayo yamaanisha nini?
19 Hezekia ana uhakika gani wa kwamba unabii wa Isaya utatimia? Yehova ajibu: “Kwako wewe dalili ndiyo hii; mwaka huu mtakula vitu vimeavyo vyenyewe; na mwaka wa pili mtakula mazao ya mbegu za vitu hivyo; na mwaka wa tatu pandeni mbegu, kavuneni; mkapande mizabibu katika mashamba, mkale matunda yake.” (Isaya 37:30) Yehova atawapa chakula Wayahudi waliozuiliwa. Ijapokuwa hawawezi kupanda mbegu kwa sababu ya uvamizi wa Waashuri, watakula masazo ya mavuno ya mwaka uliotangulia. Mwaka unaofuata, ambao ni mwaka wa sabato, lazima wayaache mashamba yao yapumzike, licha ya hali yao ngumu. (Kutoka 23:11) Yehova aahidi kuwa watu wakiitii sauti yake, nafaka ya kutosha kuwalisha itamea mashambani. Kisha, mwaka unaofuata, watu watapanda mbegu kama kawaida na kupata matunda ya kazi yao.
20. Wale wanaookoka shambulizi la Ashuru ‘watatiaje mizizi chini na kuzaa matunda juu’?
20 Sasa Yehova awalinganisha watu wake na mmea usioweza kung’olewa rahisi: “Mabaki yaliyookoka . . . ya nyumba ya Yuda, yatatia mizizi chini, na kuzaa matunda juu.” (Isaya 37:31, 32) Naam, wanaomtumaini Yehova hawana cha kuhofu. Wao pamoja na wazao wao watadumu imara nchini.
21, 22. (a) Ni unabii gani unaotolewa kumhusu Senakeribu? (b) Maneno ya Yehova kuhusu Senakeribu yatimizwa lini na jinsi gani?
21 Namna gani vitisho vya Waashuri dhidi ya Yerusalemu? Yehova ajibu: “Yeye hataingia ndani ya mji huu, wala hatapiga mshale hapa, wala hatakuja mbele yake kwa ngao, wala hatajenga boma juu yake. Njia ile ile aliyoijia, kwa njia hiyo atarudi zake, wala hataingia ndani ya mji huu.” (Isaya 37:33, 34) Kwani, hapana pigano litakalotokea kati ya Ashuru na Yerusalemu. Kwa kushangaza, Waashuri, wala si Wayahudi, ndio wanaoshindwa pasipo pigano.
22 Kupatana na neno lake, Yehova atuma malaika anayewaua watu hodari katika jeshi la Senakeribu—watu 185,000. Yaonekana hayo yafanyika huko Libna, na Senakeribu mwenyewe aamka na kukuta viongozi, wakuu, na watu hodari wa jeshi lake wamekufa. Yeye arudi Ninawi akiwa na aibu, lakini licha ya kushindwa kabisa, aendelea kwa ushupavu kumwabudu Nisroki, mungu wake asiye wa kweli. Miaka kadhaa baadaye, wana wawili wa Senakeribu wamwua akiabudu katika hekalu la Nisroki. Mara nyingine tena, Nisroki asiye na uhai athibitika kuwa hana nguvu za kuokoa.—Isaya 37:35-38.
Imani ya Hezekia Yazidi Kuimarishwa
23. Hezekia ashikwa na wasiwasi gani Senakeribu ajapo kwanza dhidi ya Yuda, na ni mambo gani yanayohusika katika wasiwasi huo?
23 Karibu wakati Senakeribu ajapo kwanza dhidi ya Yuda, Hezekia awa mgonjwa mahututi. Isaya amwambia kwamba atakufa. (Isaya 38:1) Mfalme huyo mwenye umri wa miaka 39 avunjika moyo kabisa. Yeye ahangaikia, si hali njema yake pekee, bali pia ya wakati ujao wa watu. Yerusalemu na Yuda zimo katika hatari ya kuvamiwa na Waashuri. Hezekia akifa, ni nani atakayeongoza pigano? Wakati huo, Hezekia hana mwana wa kuchukua utawala. Kupitia sala yenye bidii, Hezekia amwomba Yehova amrehemu.—Isaya 38:2, 3.
24, 25. (a) Yehova ajibuje sala ya Hezekia kwa rehema? (b) Yehova afanya mwujiza gani, kama inavyoelezwa kwenye Isaya 38:7, 8?
24 Kabla Isaya hajaondoka katika nyua za jumba la mfalme, Yehova amtuma tena kwa mfalme anayeugua akiwa na ujumbe mwingine: “Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano. Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu.” (Isaya 38:4-6; 2 Wafalme 20:4, 5) Yehova ataithibitisha ahadi yake kwa ishara ya ajabu: “Tazama, nitakirudisha nyuma kivuli madaraja kumi, ambayo kilishuka juu ya duara ya Ahazi kwa sababu ya jua.”—Isaya 38:7, 8a.
25 Kwa mujibu wa mwanahistoria Myahudi Josephus, kulikuwepo ngazi ndani ya jumba la mfalme, labda kukiwa na nguzo karibu nayo. Miale ya jua ilipoimulika nguzo hiyo, ilitia kivuli juu ya ngazi. Ingewezekana kupima saa kwa kutazama urefu wa kivuli hicho kwenye ngazi. Sasa Yehova atafanya mwujiza. Baada ya kivuli kushuka chini ya ngazi kama kawaida, kitarudi nyuma madaraja kumi. Ni nani amewahi kuyasikia hayo? Biblia yataarifu: “Basi jua likarudi madaraja kumi katika hiyo duara, ambayo limekwisha kushuka.” (Isaya 38:8b) Muda mfupi baadaye, Hezekia apona ugonjwa wake. Habari za mambo hayo zasambaa mbali hadi Babiloni. Mfalme wa Babiloni anapopata habari, atuma wajumbe Yerusalemu ili wapate ukweli wa mambo.
26. Ni jambo gani moja linalotokana na kurefushwa kwa maisha ya Hezekia?
26 Karibu miaka mitatu baada ya Hezekia kupona kwa mwujiza, mwanawe wa kwanza aitwaye Manase azaliwa. Anapokua, Manase akosa kuthamini huruma ya Mungu, ambayo iwapo isingalionyeshwa hangalizaliwa! Badala yake, Manase afanya kwa kiwango kikubwa yaliyo mabaya machoni pa Yehova kwa muda mwingi wa maisha yake.—2 Mambo ya Nyakati 32:24; 33:1-6.
Uamuzi Wenye Kosa
27. Hezekia aonyeshaje shukrani kwa Yehova?
27 Hezekia ni mtu mwenye imani kama vile Daudi baba yake wa zamani. Analithamini sana Neno la Mungu. Kulingana na Mithali 25:1, alifanya mpango wa kukusanywa kwa maandishi ambayo sasa yapatikana katika Mithali sura ya 25 hadi 29. Watu fulani huamini kwamba yeye alitunga pia Zaburi ya 119. Wimbo wa shukrani wenye kusisimua anaotunga Hezekia baada ya kupona ugonjwa wake waonyesha kuwa yeye ni mtu mwenye shukrani sana. Akata kauli kwamba jambo muhimu zaidi maishani ni kumsifu Yehova hekaluni Mwake “siku zote za maisha yetu.” (Isaya 38:9-20) Sote na tuwe na maoni kama hayo juu ya ibada safi!
28. Hezekia afanya kosa gani katika uamuzi wakati fulani baada ya kuponywa kwa njia ya mwujiza?
28 Ingawa Hezekia ni mwaminifu, yeye si mkamilifu. Afanya uamuzi wenye kosa zito muda fulani baada ya Yehova kumponya. Isaya aeleza: “Wakati huo Merodaki-baladani, mwana wa Baladani, mfalme wa Babeli, alipeleka barua na zawadi kwa Hezekia; kwa maana amepata habari kwamba amekuwa hawezi, na kwamba amepona. Hezekia akawafurahia, akawaonyesha nyumba yake yenye vitu vyake vya thamani, fedha na dhahabu, na manukato, na marhamu ya thamani, na nyumba yote yenye silaha zake za vita, na vitu vyote vilivyoonekana katika hazina zake; hapakuwa na kitu nyumbani mwake wala katika ufalme wake asichowaonyesha.”—Isaya 39:1, 2.b
29. (a) Huenda Hezekia ana nia gani awaonyeshapo wajumbe wa Wababiloni mali zake? (b) Matokeo ya uamuzi wenye kosa wa Hezekia yatakuwa nini?
29 Hata baada ya kushindwa kabisa na malaika wa Yehova, Ashuru yaendelea kuwa tisho kwa mataifa mengi, kutia ndani Babiloni. Labda Hezekia alitaka kumfurahisha mfalme wa Babiloni ili awe mshirika wake wakati ujao. Hata hivyo, Yehova hataki wakazi wa Yuda washirikiane na adui zao; anataka wamtumaini yeye! Kupitia nabii Isaya, Yehova amfunulia Hezekia mambo ya wakati ujao: “Siku zinakuja, ambazo vitu vyote vilivyomo nyumbani mwako, na hivyo vilivyowekwa akiba na baba zako hata leo, vitachukuliwa mpaka Babeli; hapana kitu cho chote kitakachosalia . . . Na baadhi ya wana wako utakaowazaa, watakaotoka kwako, watawachukulia mbali; nao watakuwa matowashi katika jumba la mfalme wa Babeli.” (Isaya 39:3-7) Naam, taifa lilelile ambalo Hezekia alijaribu kulifurahisha hatimaye litapora hazina za Yerusalemu na kuwatumikisha raia zake. Hatua ya Hezekia ya kuwaonyesha Wababiloni hazina zake yachochea tu tamaa yao yenye pupa.
30. Hezekia alionyeshaje mtazamo mzuri?
30 Labda likirejezea tukio ambalo Hezekia aliwaonyesha Wababiloni hazina zake, andiko la 2 Mambo ya Nyakati 32:26 lataarifu hivi: “Hezekia akajinyenyekeza kwa ajili ya huku kutukuka kwa moyo wake, yeye na wenyeji wa Yerusalemu, hata haikuwajia hasira ya BWANA siku za Hezekia.”
31. Hatimaye mambo yalimwendeaje Hezekia, na hilo latufundisha nini?
31 Licha ya kutokamilika kwake, Hezekia alikuwa mtu mwenye imani. Alijua kwamba Mungu wake, Yehova, ni mtu halisi aliye na hisia. Akiwa chini ya mkazo, Hezekia alisali kwa Yehova kwa bidii, na Yehova akamjibu. Yehova Mungu alimpa amani kwa siku zilizobaki za maisha yake, na Hezekia akawa mwenye shukrani kwa hayo. (Isaya 39:8) Yehova apasa kuwa halisi jinsi hiyo kwetu leo. Matatizo yanapozuka, sisi, kama Hezekia, na tumtegemee Yehova atupe hekima na njia ya kutokea, “kwa maana yeye huwapa wote kwa ukarimu na bila kushutumu.” (Yakobo 1:5) Tukiendelea kuvumilia na kudhihirisha imani katika Yehova, twaweza kuwa na uhakika kwamba atakuwa “mthawabishaji wa wale wanaomtafuta kwa bidii,” sasa na wakati ujao.—Waebrania 11:6.
[Maelezo ya Chini]
a Thamani ya dola (za Marekani) zaidi ya milioni 9.5 kwa viwango vya kisasa.
b Baada ya kushindwa kwa Senakeribu, mataifa jirani yalimletea Hezekia zawadi za dhahabu, fedha, na vitu vingine vyenye thamani. Twasoma kwenye 2 Mambo ya Nyakati 32:22, 23, 27 kwamba “Hezekia akawa na mali nyingi mno na heshima” na kwamba “hata yeye akatukuka tangu wakati ule machoni pa mataifa yote.” Huenda zawadi hizo zilimwezesha kujaza tena nyumba yake ya hazina, ambayo alikuwa ameiacha tupu alipowalipa Waashuri ushuru.
[Picha katika ukurasa wa 383]
Mfalme Hezekia amtumaini Yehova akabilipo jeshi la Ashuru
[Picha ya ukurasa mzima katika ukurasa wa 384]
[Picha katika ukurasa wa 389]
Mfalme atuma wajumbe kwa Isaya ili kusikia shauri la Yehova
[Picha katika ukurasa wa 390]
Hezekia asali kwamba jina la Yehova litukuzwe kupitia kushindwa kwa Ashuru
[Picha katika ukurasa wa 393]
Malaika wa Yehova aua Waashuri 185,000