-
Kumtambua Mjumbe wa Aina InayofaaMnara wa Mlinzi—1997 | Mei 1
-
-
7, 8. Isaya alikuwa na ujumbe gani wenye kupuliziwa kwa ajili ya Babiloni, na maneno yake yalimaanisha nini?
7 Yuda na Yerusalemu zilikuwa ziwe ukiwa kabisa, bila mkazi wa kibinadamu, kwa miaka 70. Hata hivyo, Yehova alijulisha kupitia Isaya na Ezekieli kwamba hilo jiji lingejengwa upya na bara hilo kukaliwa kwa wakati barabara aliokuwa ametabiri Yehova! Huo ulikuwa utabiri wenye kushangaza. Kwa nini? Kwa sababu Babiloni lilikuwa na sifa ya kutoachilia kamwe wafungwa walo. (Isaya 14:4, 15-17) Kwa hiyo ni nani ambaye angeweza kwa kweli kuwaweka huru mateka hawa? Ni nani ambaye angeweza kushinda Babiloni lenye uweza, likiwa na kuta zalo kubwa mno na mto ukiwa mfumo wa ulinzi? Yehova Mweza Yote angeweza! Naye aliyesema angefanya hivyo: “Nami [ndiye] . . . niviambiaye vilindi [yaani, maji ya mto yaliyolinda hilo jiji], Kauka, nami nitaikausha mito yako; nimwambiaye Koreshi [“Sairasi,” NW], Mchungaji wangu, naye atayatenda mapenzi yangu; hata ataunena Yerusalemu, Utajengwa; na hilo hekalu, Msingi wako utawekwa.”—Isaya 44:25, 27, 28, linganisha NW.
8 Wazia hilo! Mto Frati, uliokuwa kizuizi kikubwa mno kwa wanadamu, kwa Yehova ulikuwa kama tone la maji juu ya uso wenye moto mwingi sana! Mara moja ungekauka! Babiloni lingeanguka. Ingawa ilikuwa miaka 150 hivi kabla ya kuzaliwa kwa Sairasi Mwajemi, Yehova alimfanya Isaya atabiri kunasa kwa mfalme huyo Babiloni na kuachwa huru kwa Wayahudi walio mateka kwa kutoa kwake amri ya kurudi kwao ili kujenga upya Yerusalemu na hekalu lalo.
-
-
Kumtambua Mjumbe wa Aina InayofaaMnara wa Mlinzi—1997 | Mei 1
-
-
11. Kwa nini wakazi wa Babiloni walihisi usalama?
11 Kufikia wakati ambapo Sairasi alipiga hatua dhidi ya Babiloni, wakazi walo walihisi kwamba walikuwa salama salimini. Jiji lao lilizingirwa na handaki la maji lenye kina kirefu na lililo pana, ambalo lilifanyizwa na Mto Frati. Mahali ambapo mto ulipita jijini, kulikuwa na gati lenye kuendelea kandokando ya ukingo wa mashariki wa huo mto. Ili kulitenganisha na jiji, Nebukadreza alijenga kile alichokiita “ukuta mkubwa, ambao kama mlima, hauwezi kusogezwa . . . Kilele chao [alikiinua] juu kama mlima.”a Ukuta huu ulikuwa na malango yenye milango mikubwa mno ya shaba. Ili mtu aingie, ilimbidi akwee mteremko huo kutoka ukingo wa mto. Si ajabu wafungwa wa Babiloni walikata tamaa ya kupata kuwekwa huru!
12, 13. Maneno ya Yehova kupitia mjumbe wake Isaya yalitimiaje wakati Babiloni lilipoanguka mikononi mwa Sairasi?
12 Walakini Wayahudi walio mateka waliokuwa na imani katika Yehova hawakukata tamaa! Walikuwa na tumaini jangavu. Kupitia manabii wake, Mungu alikuwa ameahidi kuwaweka huru. Mungu alitimizaje ahadi yake? Sairasi aliamuru majeshi yake yageuzie mbali mkondo wa Mto Frati mahali fulani, kilometa nyingi kaskazini ya Babiloni. Hivyo, ulinzi mkuu wa hilo jiji ukawa sakafu ya mto iliyokauka kwa kadiri fulani. Usiku huo wa maana, walevi waliokuwa wakinywa humo Babiloni waliacha bila kujali ile milango yenye sehemu mbili kandokando ya sehemu ya jiji iliyokuwa ikikabili Frati. Yehova hakuivunja ile milango ya shaba vipande vipande kihalisi; wala hakuyakata-kata mapingo ya chuma yenye kuifunga, lakini mbinu yake ya kuiacha ikiwa wazi bila kuzuiwa ilikuwa na matokeo hayohayo. Kuta za Babiloni zilikuwa bure. Vikosi vya Sairasi havikuhitaji kuzipanda kuta hizo ili kuingia ndani. Yehova alikwenda mbele ya Sairasi, akipasawazisha “mahali palipoparuza,” ndiyo, vizuizi vyote. Isaya alithibitishwa kuwa mjumbe wa kweli wa Mungu.
-