Sura 4
Jitihada ya Kutafuta Kisichojulikana Kupitia Mizungu na Uwasiliani-Roho
1. Paulo aliwaambia nini Waathene juu ya Areopago? Kwa nini?
“ENYI watu wa Athene, katika mambo yote naona ya kuwa ninyi ni watu wa kutafakari sana mambo ya dini [“hofu ya viabudiwa,” NW].” (Matendo 17:22) Hayo ndiyo mtume Mkristo Paulo aliambia umati uliokusanyika kwenye Areopago, au Kilima Mihiri, katika jiji la kale la Athene, Ugiriki. Paulo alisema hayo kwa sababu hapo mapema alikuwa ameona “jinsi jiji hilo lilivyojaa sanamu.” (Matendo 17:16) Yeye alikuwa ameona nini?
2. Ni nini kilichoonyesha hofu ya Waathene kwa viabudiwa?
2 Bila shaka, Paulo alikuwa ameona vijimungu mbalimbali vya Kigiriki na Kiroma katika jiji hilo la kimataifa, na ilikuwa wazi kwamba maisha ya watu hao yalikuwa yametiwa sana katika ibada yao ya viabudiwa. Wakihofu kwamba huenda ikatokea wasahau kuheshimu kiabudiwa fulani cha maana au chenye nguvu na hivyo kiweze kukasirika, Waathene hata waliingiza katika ibada yao “Mungu Asiyejulikana.” (matendo 17:23) hilo kwa wazi lilionyesha hofu yao ya viabudiwa.
3. Je! ni Waathene peke yao wenye hofu ya viabudiwa?
3 Bila shaka, hofu ya viabudiwa, hasa visivyojulikana, haikuwa ya Waathene wa karne ya kwanza peke yao. Kwa maelfu ya miaka, imeongoza karibu ainabinadamu wote. Katika sehemu nyingi za ulimwengu, karibu kila sehemu ya maisha ya watu inahusiana kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja na kiabudiwa fulani au na roho za namna fulani. Kama tulivyokwisha kuona katika sura iliyotangulia, ngano za Wamisri, Wagiriki, Wachina, na watu wengine wa kale zilitegemea sana mawazo juu ya vijimungu na roho, vilivyoongoza sana mambo ya kibinafsi na ya kitaifa. Wakati wa Enzi za Katikati, hadithi juu ya waalkemia, walozi, na wachawi zilikuwa tele katika milki yote ya Jumuiya ya Wakristo. Na hali leo inafanana na hiyo.
Desturi na Ushirikina Leo
4. Ni nini baadhi ya desturi zinazopendwa na wengi ambazo kwa wazi zakamatana na viabudiwa au roho?
4 Iwe watu wanajua hilo au la, mambo mengi wanayofanya yanakamatana na mazoea na imani za kishirikina, mengine yakiwa yanahusiana na viabudiwa au roho. Kwa kielelezo, je! ulijua kwamba kuadhimisha siku ya kuzaliwa chanzo chayo ni unajimu, ambao hufungamanisha umaana mkubwa kwenye tarehe kamili aliyozaliwa mtu? Vipi keki ya siku ya kuzaliwa? Yaelekea yahusiana na kijimungu-kike cha Ugiriki Artemi, ambacho siku yacho ya kuzaliwa ilisherehekewa kwa keki za asali zenye umbo la mwezi na juu yake zikiwa na mishumaa. Au je! ulijua kwamba kuvaa nguo nyeusi kwenye maziko hapo awali ilikuwa ni njia ya kuepuka uangalifu wa roho zenye uovu zilizosemekana zaotea-otea katika pindi hizo? Baadhi ya Waafrika weusi hujipaka rangi nyeupe, na waombolezaji katika mabara mengine huvaa rangi zisizo za kawaida ili roho zisiwatambue.
5. Ni baadhi ya ushirikina gani unaopendwa na wengi unaojua?
5 Kando ya desturi hizo zinazopendwa na wengi, watu kila mahali wana ushirikina na hofu zao. Katika nchi za Magharibi, kuvunja kioo, kuona paka mweusi, kutembea chini ya ngazi, na, ikitegemea ulipo, Jumanne au Ijumaa ya tarehe 13 vyote huonwa kuwa ni mkosi unaotangulia kitu kiovu. Katika nchi za Mashariki, Wajapan huvaa kimono yao upande wa kushoto ikiwa imekunjwa juu ya ule upande wa kulia, kwa maana upande ule mwingine ni akiba ya maiti. nyumba zao hujengwa bila dirisha wala milango kuelekea kusini-mashariki ili roho waovu, wanaosemwa kuwa huja kutoka upande huo, wasione mahali pa kuingilia. Katika Ufilipino, watu huvua viatu vya wafu na kuviweka kando ya miguu kabla ya kuzikwa ili “Mtakatifu” Petro awakaribishe. Wazee huwaambia vijana wawe wenye adabu wakiwatajia kwamba lile umbo kwenye mwezi ni “Mtakatifu” Mikaeli, anayetazama na kuandika vitendo vyao.
6. Watu wanajihusisha na uwasiliani-roho kwa kadiri gani leo?
6 Hata hivyo, imani katika roho na viabudiwa haihusu tu desturi na ushirikina usio na madhara. Katika jumuiya za kikale na za kisasa, watu wametumia njia mbalimbali kusudi wazuie au kutambikia roho zenye kuhofisha na ili wapate upendeleo wa zile zenye kufadhili. Kiasili, huenda kwanza tukafikiria watu katika mapori na milima ya mbali wanaokwenda kwa wawasiliani-roho, walozi, na washamani (makahini wa mizungu) wanapokuwa wagonjwa au wanapokuwa taabani. Lakini watu katika miji mikubwa na midogo pia huwaendea wanajimu, wasoma akili, wapiga-ramli, na wapiga bao ili waulizie juu ya wakati ujao au wapate msaada katika kufanya maamuzi ya maana. Watu fulani, hata ingawa kwa jina ni wa dini hii au ile, hufuatia mazoea hayo kwa idili. Wengine wengi wamefanya kuwasiliana na roho, uchawi, na mafumbo kuwa dini yao.
7. Twahitaji kufikiria maswali gani?
7 Ni nini chanzo au asili ya mazoea na ushirikina huo? Je! hayo ni njia tofauti-tofauti tu za kumfikia Mungu? Na la maana zaidi, yanawafanyia nini wale wanaoyafuata? Ili kupata majibu ya maswali hayo, ni lazima tuangalie nyuma katika historia ya binadamu na kutupia macho njia zake za mapema za kuabudu.
Jitihada ya Kufikia Kisichojulikana
8. Ni sifa gani maalumu inayotenganisha wanadamu na viumbe vya chini zaidi?
8 Kinyume cha ambavyo wana-mageuzi huenda wakadai, binadamu ana hali ya kiroho inayomfanya kuwa tofauti na bora zaidi ya viumbe vya chini zaidi. Yeye huzaliwa akiwa na tamaa ya kufanya jitihada ya kutafuta kisichojulikana. Daima hung’ang’ana na maswali kama vile: Maana ya uhai ni nini? Huwaje baada ya mtu kufa? Ni uhusiano gani wa mwanadamu na ulimwengu uonekanao, kwa kweli, ulimwengu wote mzima? Pia yeye huongozwa na tamaa ya kujitahidi kufikia kitu kilicho juu zaidi au chenye nguvu zaidi yake ili kusudi atawale kwa kadiri fulani mazingira yake na maisha yake.—Zaburi 8:3, 4; Mhubiri 3:11; Matendo 17:26-28.
9. Msomi mmoja husimuliaje ‘ukiroho’?
9 Ivar Lissner katika kitabu chake Man, God and Magic alieleza hilo hivi: “Jitihada yenye ustahimilivu ambayo binadamu, katika historia yake yote, ametia ili afikie yaliyo nje yake inastaajabisha. Nishati zake hazikuelekezwa kwenye utafutaji wa riziki ya maisha peke yake. Daima yeye alikuwa akitafuta, akipapasa-pasa njia yake mbele zaidi, akijitahidi kupata kisichofikilika. Tamaa hii ya ajabu na ya urithi ndani ya binadamu ni ukiroho wake.”
10. Ni nini kinachoonyesha kwamba binadamu ana tamaa ya kiasili ya kujitahidi kumfikia Mungu?
10 Bila shaka, wale wasioamini Mungu hawayaoni mambo kwa njia hiyo kabisa. Kwa ujumla wao wanasema mwelekeo huo wa kibinadamu ni kwa sababu ya mahitaji ya mtu, ya kisaikolojia au mengineyo, kama tulivyoona katika Sura 2. Hata hivyo, je! sivyo ilivyo kwa ujumla kwamba wanapokabiliwa na hatari au hali yenye mashaka, itikio la watu wengi ni kumlilia Mungu au nguvu fulani kubwa kwa ajili ya msaada? Ndivyo ilivyo leo sawa na ilivyokuwa wakati uliopita. Kwa hiyo, Lissner aliendelea kusema hivi: “Hakuna yeyote ambaye amefanya utafiti kati ya vikundi vya watu wa zamani zaidi, wa kikale aweza kushindwa kuelewa kwamba wote wanawaza juu ya Mungu, kwamba wanatambua kwa vitendo kuwapo kwa mtu aliye mkuu zaidi.”
11. Ni matokeo gani ya jitihada ya binadamu ya kufikia kisichojulikana? (Linganisha Warumi 1:19-23.)
11 Jinsi walivyojitahidi kutosheleza tamaa hiyo ya kuzaliwa nayo kwa kutafuta kisichojulikana lilikuwa jambo tofauti. Wawindaji-wahamaji na wachunga-mifugo walitetemekea nguvu za wanyama-mwitu. Wakulima walijipatanisha hasa na mabadiliko katika hali ya hewa na majira. Wenye kukaa maporini waliitikia tofauti na watu walioishi katika majangwa au milimani. Kwa sababu ya hofu na mahitaji hayo mbalimbali, watu walisitawisha mazoea ya kidini mbalimbali yenye kuduwaza ambayo kupitia kwayo walitumaini kulilia vijimungu vyenye kufadhili na kutambikia vile vyenye kuhofisha.
12. Ni mambo gani yenye kufanana yanayoonekana katika mazoea ya kidini ya watu kila mahali?
12 Hata hivyo, ujapokuwa utofautiano huo mkubwa kuna mambo fulani yenye kufanana yanayoonekana katika mazoea hayo ya kidini. Kati ya hayo ni staha nyingi na hofu ya roho zilizotakata na nguvu zinazozidi zile za kibinadamu, matumizi ya mizungu, kufanya uaguzi wa wakati ujao kwa kutumia ishara na mikosi, unajimu, na mbinu nyingi mbalimbali za kutabiri matukio mema au mabaya. Tuchunguzapo sehemu hizo, tutaona kwamba zimetimiza fungu kubwa katika kuathiri kuwaza kwa watu katika ulimwengu wote na katika enzi zote, hata kutia na watu wa leo.
Roho Zilizotakata na Nguvu Zinazozidi Zile za Kibinadamu
13. Ni mambo gani huenda yakawa yalikuwa ya kutatanisha watu katika nyakati zilizopita?
13 Maisha ya watu katika nyakati za mapema-mapema yaelekea kuwa yalijawa na fumbo. Walizungukwa na matukio yasiyoelezeka na yenye kutatanisha. Kwa kielelezo, hawakuweza kuelewa ni kwa nini mtu mwenye afya kamili ashikwe na ugonjwa ghafula, au ni kwa nini anga ikose kutoa mvua kwenye majira ya kawaida, au kwa nini mti usio na uhai, wenye kuonekana hauna uhai, ugeuke kuwa wa kijani-kibichi na kuchanua wakati fulani wa mwaka. Hata kivuli cha mtu mwenyewe, mdundo wa moyo, na pumzi vilikuwa ni mafumbo.
14, 15. Kwa sababu ya kukosa kuelewa na mwongozo, binadamu alisema sababu ya kisichofafanulika ni nini? (Linganisha 1 Samweli 28:3-7.)
14 Binadamu akiwa na mwelekeo aliozaliwa nao wa kiroho, lilikuwa ni jambo la asili tu ahesabie mambo na matukio hayo ya kifumbo nguvu fulani inayozidi ile ya kibinadamu. Hata hivyo, kwa kukosa mwongozo na uelewevu unaofaa, upesi ulimwengu wake ukajawa na nafsi, roho, mazimwi, na mashetani. Kwa kielelezo, Wahindi Walgonqui wa Amerika ya Kaskazini huita nafsi ya mtu otahchuk, ikimaanisha “kivuli chake,” na Wamaleya wa Asia ya Kusini-mashariki huamini kwamba binadamu afapo, nafsi yake huponyoka kupitia mianzi ya pua yake. Leo, imani katika roho na mizimu—na majaribio ya kuwasiliana nazo kwa mtindo fulani—karibu ni ya ulimwenguni pote.
15 Kwa jinsi iyo hiyo, vitu vingine katika mazingira ya asili—jua, mwezi, nyota, bahari, mito, milima—vilielekea kuwa hai na vyenye uvutano wa moja kwa moja juu ya utendaji wa kibinadamu. Kwa kuwa vitu hivyo vilionekana vikiwa na ulimwengu wavyo vyenyewe, vilionwa kuwa roho na viabudiwa, baadhi yavyo vikiwa vyenye kufadhili na kusaidia, vingine vikiwa vyenye uovu na vyenye kudhuru. Ibada ya vitu vilivyoumbwa ikaja kuchukua mahali mashuhuri karibu katika dini zote.
16. Ibada ya roho, viabudiwa, na vitu vitakatifu ilidhihirikaje?
16 Twaweza kupata imani za aina hiyo katika dini za karibu kila ustaarabu wa kale. Wababuloni na Wamisri waliabudu vijimungu vyao vya jua, mwezi, na vikundi vya nyota. Wanyama na hayawani-mwitu pia walikuwa kati ya vitu walivyoheshimu sana. Wahindu wanajulikana kwa ajili ya vikundi vya vijimungu vyao, vinavyofikia hesabu ya mamilioni. Wachina sikuzote wamekuwa na milima mitakatifu yao na vijimungu-mito vyao, nao huonyesha uchaji wao wakiwa watoto katika ibada ya wazazi wa kale waliokufa. Wadruidi wa kale wa Visiwa vya Uingereza walichukua miti oku kuwa mitakatifu, na walitoa heshima kubwa maalumu kwa vimelea vilivyokua juu ya mti oku. Baadaye, Wagiriki na Waroma walichangia sehemu yao; na imani katika roho, viabudiwa, nafsi, mashetani, na vitu vitakatifu vya kila namna ikatia mizizi imara.
17. Ibada ya vitu vilivyoumbwa ingali yaonekanaje leo?
17 Ingawa baadhi ya watu leo huenda wakaona imani hizo zote kuwa ushirikina, mawazo hayo yangali yapatikana katika mazoea ya kidini ya watu wengi kuuzunguka ulimwengu. Wengine wangali wanaamini kwamba milima fulani, mito, miamba yenye umbo la ajabu-ajabu, miti ya kale, na vitu vingine vingi ni vitakatifu, na wanaviabudu kuwa vitu vya kujitoa kwavyo. Hujenga madhabahu, vihekalu, na mahekalu kwenye sehemu hizo. Kwa kielelezo, Mto Ganges ni mtakatifu kwa Wahindu ambao kutaka kwao kwenye tamaa kubwa kabisa ni kuoga humo wakiwa wangali hai na majivu yao yatapanywe juu ya mto huo baada ya kufa. Wafuasi wa Dini ya Buddha huliona kuwa tukio lisilo la kawaida kuabudu kwenye kihekalu katika Buddh Gaya, India, ambako yasemekana Buddha alipata mnurisho chini ya mti bodhi. Wakatoliki hutambaa kwa magoti yao kwenye Basilika ya Mama Yetu wa Guadalupe katika Meksiko au kuoga katika maji “matakatifu” kwenye kikanisa kule Lourdes, Ufaransa, wakijitahidi kutafuta maponyo ya kimwujiza. Kuheshimu mno vitu vilivyoumbwa badala ya Muumba kungali kwaonekana sana leo.—Warumi 1:25.
Kutokea kwa Mizungu
18. Imani katika roho na viabudiwa iliongoza kwenye nini?
18 Imani ya kwamba ulimwengu usio na uhai ulijaa roho wema na wabaya ilipokwisha kuimarishwa, jambo hilo liliongoza kwa urahisi kwenye hatua iliyofuata—majaribio ya kupashana habari na roho wale wema kwa ajili ya mwongozo na baraka na kutambikia wale wabaya. Matokeo yakawa ni zoea la mizungu, ambalo limesitawi karibu katika kila taifa la wakati uliopita na wakati huu.—Mwanzo 41:8; Kutoka 7:11, 12; Kumbukumbu la Torati 18:9-11, 14; Isaya 47:12-15; Matendo 8:5, 9-13; 13:6-11; 19:18, 19.
19. (a) Mizungu ni nini? (b) Kwa nini mizungu yaonekana ni yenye kuaminika kwa watu wengi?
19 Katika maana yao ya msingi, mizungu ni jitihada ya kuongoza au kulazimisha kani za asili na zile zenye nguvu zinazozidi za kibinadamu zifanye atakavyo binadamu. Wakiwa hawajui kisababishi halisi cha matukio mengi ya kila siku, watu katika jumuiya za mapema zaidi waliamini kwamba kurudia maneno fulani ya kimizungu au kutabana, au kufanya sherehe fulani za ibada, kungeweza kutokeza matokeo fulani yanayotakwa. Kilichosaidia aina hii ya mizungu ipate kutegemeka ni kwa vile sherehe fulani za ibada zilifanikiwa kikweli. Kwa kielelezo, waganga—sana sana wafanya mizungu au walozi—wa Visiwa vya Mentawai magharibi ya Sumatra waliripotiwa kuwa wenye matokeo ya kustaajabisha katika kuponya watu wenye ugonjwa wa kuhara. Njia yao ya kufanyia mizungu ilikuwa ni kuwalaza wagonjwa uso ukielekea chini karibu na ukingo wa jabali na kuramba ardhi pindi kwa pindi. Ni nini kilichofanya hilo lifanikiwe? Udongo kwenye miamba hiyo ulikuwa na kaolini, udongo-mgumu mweupe utumiwao kwa ukawaida katika dawa fulani za leo za kutibu kuhara.
20. Mizungu ilikujaje kutawala maisha za watu?
20 Mafanikio machache ya aina hiyo upesi yalibatili njia zote ambazo hazikufaulu yakaimarisha sifa ya waganga hao. Mara wakawa washiriki wanaoonwa kwa hofu nyingi na kujaliwa sana—makahini, machifu, washamani, waganga, walozi, wawasilianishi. Watu waliwaendea wakiwa na matatizo yao, kama yale ya kutaka kuponywa na kuzuia magonjwa, kupata vitu vilivyopotea, kutambua wezi, kukinga mavutano ya uovu, na kulipa kisasi. Hatimaye kukaja kuwa na jumla kubwa ya mazoea ya ushirikina na sherehe za kiibada zilizoshughulika na mambo hayo na pia matukio mengine maishani, kama uzazi, kubaleghe, kuposwa, ndoa, kifo, na maziko. Mara nguvu na fumbo la mizungu zikatawala kila sehemu ya maisha za watu.
Kucheza Ngoma za Mvua na Ulozi
21, 22. Ni nini maana ya “mizungu ya kuigiza”? Toa kielezi.
21 Ujapokuwa utofautiano mkubwa katika mazoea ya mizungu ya vikundi tofauti-tofauti vya watu, mawazo ya msingi kwa wazi ni yale yale. Kwanza, kuna wazo la kwamba kitu hutokeza kitu kinachofanana nacho, kwamba jambo fulani laweza kutokezwa kwa kuliiga. Hili wakati mwingine huitwa mizungu ya kuigiza. Kwa kielelezo, wakati upungufu wa mvua ulipotishia kuharibu mazao yao, Wahindu wa Omaha wa Amerika Kaskazini walicheza ngoma kuzunguka chombo cha maji. Ndipo mmoja wao akanywa maji kidogo na kuyatema hewani kwa kuigiza mnyunyizo au rasha-rasha. Au huenda mtu mwanamume akabingirika ardhini kama dubu aliyeumizwa ili kuhakikisha kwamba angefanikiwa katika kuwinda dubu.
22 Watu wengine walikuwa na sherehe za kiibada zenye madoido zaidi, kutia ndani nyimbo na matoleo. Wachina wangetengeneza drakoni mkubwa wa karatasi au mbao, kijimungu-mvua chao, na kumtembeza-tembeza kigwaride, au wangechukua sanamu ya kijimungu chao kutoka hekaluni na kuiweka kwenye jua ili ihisi joto na labda kupeleka mvua. Sherehe ya kiibada ya Wangoni wa Afrika Mashariki inatia ndani kumimina pombe ndani ya jungu lililozikwa ardhini katika hekalu la mvua kisha kusali, “Bwana Chauta, umefanya moyo wako kuwa mgumu kutuelekea sisi, wataka tufanye nini? Tutaangamia kweli kweli. Wape watoto wako mvua, pombe hiyo sisi tumekupa wewe.” Ndipo wanapokunywa pombe iliyosalia. Kisha kuimba na kucheza ngoma hufuata na kutikisa matawi yaliyochovywa katika maji.
23. Uchawi na ulozi vilisitawije? (Linganisha Mambo ya Walawi 19:31; 20:6, 27; Kumbukumbu la Torati 18:10-13.)
23 Wazo jingine lililo msingi wa mazoea ya mizungu ni kwamba vitu ambavyo vilikuwa mali ya mtu huendelea kumwongoza hata baada ya kutenganishwa na yeye. Hilo liliongoza kwenye zoea la kuroga mtu kwa kushughulika na kitu ambacho wakati mmoja kilikuwa mali ya mtu huyo. Hata katika Ulaya na Uingereza ya karne ya 16 na 17, watu walikuwa wangali wakiwaamini wachawi wa kike na wa kiume ambao wangeweza kusababisha madhara kwa watu kwa nguvu za aina hiyo. Njia hizo zilitia ndani mambo kama vile kufanyiza taswira ya nta ya mfano wa mtu na kuidunga kwa pini, kuandika jina lake juu ya kipande cha karatasi kisha kukichoma moto, kuzika kipande cha nguo yake, au kufanya mambo mengine kwenye nywele zake, kata za kucha za vidole vyake, jasho, au hata mavi. Kadiri ya mazoea hayo na mengine yaweza kuonyeshwa na uhakika wa kwamba Sheria za Bunge zilipitishwa katika Uingereza katika 1542, 1563, na 1604 zikitangaza uchawi ni kosa linalostahili kifo. Katika jinsi moja au nyingine, namna hii ya mizungu imezoewa na watu karibu katika kila taifa wakati wa enzi zote.
Wakati Ujao kwa Namna ya Ishara na Mikosi
24. (a) Uaguzi ni nini? (b) Wababuloni walizoeaje uaguzi?
24 Mara nyingi mizungu hutumiwa ili kufichua habari iliyofichwa au kuchungulia wakati ujao kwa njia ya ishara na mikosi. Hilo linaitwa uaguzi, na Wababuloni walijulikana kwa hilo. Kulingana na kitabu Magic, Supernaturalism, and Religion, “wao walikuwa mabingwa wa sanaa za sayansi ya kujua matukio kimbele, kutabiri wakati ujao kutokana na maini na matumbo ya wanyama waliochinjwa, kutokana na moto na moshi, na kutokana na mng’aro wa mawe ya thamani; walitabiri matukio kutokana na mvumo wa chemchemi na kutokana na maumbo ya mimea. . . . Ishara za anga, mvua, mawingu, upepo, na umeme zilifasiriwa kuwa zenye mkosi; kuatuka kwa fanicha na mabamba ya mbao kulitabiri matukio ya wakati ujao. . . Nzi na wadudu wengine, na pia mbwa, walikuwa ndio wachukuzi wa jumbe za mafumbo.”
25. Ezekieli na Danieli walirejezeaje zoea la uaguzi katika Babuloni ya kale?
25 Kitabu cha Biblia cha Ezekieli huripoti kwamba kwenye shughuli moja ya kivita, “mfalme wa Babeli alisimama penye njia panda, penye kichwa cha njia hizo mbili, ili atumie uganga; aliitikisa mishale huko na huko, akaziuliza terafi, akayatazama maini.” (Ezekieli 21:21) Wafanya viinimacho, walozi, na makahini wenye kuzoea mizungu walikuwa pia sehemu ya kawaida ya baraza la mfalme la Kibabuloni.—Danieli 2:1-3, 27, 28.
26. Ni nini namna moja ya uaguzi uliokuwa wenye kupendwa na wengi kati ya Wagiriki?
26 Watu wa mataifa mengine, ya Mashariki na Magharibi, pia walijihusisha katika namna nyingi za uaguzi. Wagiriki waliendea vinyago vyao kuhusu matukio makubwa ya kisiasa na pia mambo ya kimwili ya kibinafsi kama ndoa, usafiri, na watoto. Chenye kujulikana zaidi kati yavyo kilikuwa kinyago cha Delfi. Majibu, yaliyodhaniwa kuwa yametoka kwa kijimungu Apolo, yalitolewa kupitia kahini-mke, au Pithia, kwa njia ya sauti zisizoeleweka nazo zilifasiriwa na makahini kufanyiza beti zisizo na maana dhahiri. Kielelezo kizuri ni jibu alilopewa Kroesa, mfalme wa Lidia, ambalo lilisema hivi: “Kroesa akivuka Halyisi, ataangamiza milki yenye nguvu.” Ikawa kwamba milki hiyo yenye nguvu iliyoharibiwa ilikuwa ile yake mwenyewe. Kroesa alishindwa mikononi mwa Koreshi Mwajemi alipovuka Halyisi avamie Kapadokia.
27. Waroma walijihusisha katika uaguzi kwa kadiri gani?
27 Katika Magharibi ufundi wa uaguzi ulifikia kilele kwa Waroma, waliojishughulisha mno na mikosi na ishara karibu katika kila jambo walilofanya. Watu wa kila tabaka ya kijamii waliamini unajimu, uchawi, talasimu, utabiri wa matukio mema au mabaya, na namna nyingine nyingi za uaguzi. Na kulingana na mtaalamu mmoja wa historia ya Kiroma, Edward Gibbon, “namna mbalimbali za ibada, zilizoenea katika ulimwengu wa Kiroma, zote zilionwa na watu, kuwa za kweli hali moja.” Sisero, mwanatawala maarufu na mjuzi wa kuhutubu alikuwa mtaalamu wa kutazama mikosi katika mpuruko wa ndege. Mwanahistoria Mroma Petronia alionelea kwamba kwa kuamua kwa wingi wa dini na viibada katika miji fulani ya Kiroma, bila shaka kulikuwamo vijimungu vingi zaidi ya watu.
28. Wachina walizoeaje uaguzi katika nyakati za kale?
28 Katika Uchina, vipande zaidi ya 100,000 vya mifupa na magamba ya vinyago ya tarehe ya tangu mileani ya pili K.W.K. (Nasaba ya Shang) vimefukuliwa. Vilitumiwa na makahini wa Shang katika kutafuta uongozi wa kimungu kwa kila jambo kuanzia hali ya hewa mpaka mwendo wa majeshi. Makahini hao waliandika maswali katika hati ya kale juu ya mifupa hiyo. Ndipo wakaipasha moto mifupa hiyo na kuchunguza miatuko iliyotokea na kuandika majibu kwenye mifupa iyo hiyo. Wasomi fulani wanaamini kwamba mwandiko wa Kichina ulisitawishwa kutokana na hati hii ya kale.
29. Ni kanuni gani ya uaguzi iliyoandikwa katika I Ching?
29 Kitabu cha Kichina kilicho cha kale zaidi na chenye kujulikana sana kuwa kikizungumzia uaguzi ni I Ching (Kanuni ya Mabadiliko), chasemekana kuwa kiliandikwa na wamaliki Chou wawili wa kwanza, Wen Wang na Chou Kung, katika karne ya 12 K.W.K. Kina ufafanuzi mrefu wa uhusiano wa kani mbili zenye kupingana yin na yang (nyeusi-nyangavu, hasi-chanya, kike-kiume, mwezi-jua, dunia-mbingu, na kadhalika), ambazo Wachina wengi wangali wanaamini ndizo kanuni zinazoongoza mambo yote ya maisha. Chatoa wazo la kwamba kila jambo linabadilika daima na hakuna jambo la kudumu. Ili kufaulu katika utendaji wowote, ni lazima mtu ajue na kutenda kwa kupatana na mabadiliko yote ya dakika hiyo. Kwa hiyo, watu huuliza maswali na kupiga kura halafu kugeukia I Ching kwa ajili ya majibu. Wakati wa karne zote zilizopita, katika China I Ching kimekuwa msingi wa namna zote za utabiri wa matukio mema au mabaya, uaguzi wa kutumia maumbo ya ardhi (jiomansi) na namna nyingine za uaguzi.
Kutoka Elimu ya Nyota Mpaka Unajimu
30. Eleza juu ya kusitawi kwa elimunyota-anga ya mapema.
30 Utaratibu wa jua, mwezi, nyota, na sayari nyingine kwa muda mrefu umekuwa chanzo cha kustaajabisha watu duniani. Orodha za nyota za tarehe ya kule nyuma 1800 K.W.K. zimevumbuliwa katika Mesopotamia. Kwa kutegemea habari hiyo, Wababuloni waliweza kutabiri matukio mengi ya nyota za angani, kama vile kupatwa (eklipsi) kwa mwezi, kutoka na kutua kwa vikundi vya nyota, na miendo fulani ya sayari. Wamisri, Waashuri, Wachina, Wahindi, Wagiriki, Waroma, na watu wengine wa kale vilevile walichunguza anga na kutunza maandishi mengi ya matukio ya nyota za angani. Kutokana na maandishi hayo walitengeneza kalenda zao na kuratibu utendaji wao wa mwaka.
31. Elimunyota-anga ilitokezaje unajimu?
31 Kutokana na uchunguzi huo wa nyota za angani, ilionekana kwamba matukio fulani duniani yalielekea kupatana na matukio fulani ya angani. Kwa kielelezo, badiliko la majira lilifuata sana mwendo wa jua, maji ya bahari yalijaa na kushuka kwa kulingana na uso wa mwezi, mafuriko ya kila mwaka ya Naili sikuzote yalifuata kuonekana kwa Siriasi, nyota nyangavu kabisa. Mkataa asili ukawa kwamba magimba ya kimbingu yalihusika sana katika kusababisha matukio hayo na mengine duniani. Kwa kweli, Wamisri waliita Siriasi, Mleta Naili. Wazo la kwamba nyota ziliongoza matukio duniani upesi likaongoza kwenye dhana ya kwamba magimba ya kimbingu yangeweza kutegemewa ili kutabiri wakati ujao. Kwa hiyo elimunyota-anga ikatokeza unajimu. Mara, wafalme na wamaliki wakaweka wanajimu rasmi katika mabaraza yao ili waangalie nyota kuhusu mambo ya maana ya kitaifa. Lakini makabwela nao wakategemea nyota kuhusu mambo yao ya kibinafsi.
32. Wababuloni walizoea unajimu katika njia zipi?
32 Kwa mara nyingine, Wababuloni wahusika. Wao waliona nyota kuwa makao ya kimbingu ya vijimungu, kama vile mahekalu yalivyokuwa makao yao ya kidunia. Hilo lilitokeza wazo la kujumlisha nyota katika vikundi-vikundi na pia imani ya kwamba mivurugo mbinguni, kama vile kupatwa kwa jua na mwezi au kutokea kwa nyota fulani nyangavu au vimondo, ilikuwa ishara ya huzuni na vita duniani. Mamia ya ripoti ambazo wanajimu walitolea wafalme zilipatikana kati ya masalio ya kale yaliyofukuliwa katika Mesopotamia. Kwa kielelezo, nyingine zazo zilieleza kwamba kupatwa kwa mwezi kulikokuwa kunakaribia kulikuwa ishara ya kwamba adui fulani angeshindwa au kutokea kwa sayari fulani katika kikundi fulani cha nyota kungemaanisha “ghadhabu kubwa” duniani.
33. Isaya alisema nini juu ya Wababuloni “wazitazamao nyota”?
33 Kadiri ambayo Wababuloni walitegemea namna hii ya uaguzi yaweza kuonekana zaidi katika maneno ya kudhihaki ya nabii Isaya kwao alipokuwa akitabiri kuangamizwa kwa Babuloni: “Simama sasa na uganga wako, na wingi wa uchawi wako, uliojitaabisha nao tangu ujana wako . . . na wasimame hao wajuao falaki, wazitazamao nyota, watabirio kila mwezi mambo ya mwezi huo, wakakuokoe na mambo yatakayokupata.”—Isaya 47:12, 13.
34. Wale “mamajusi” waliomwendea mtoto mchanga Yesu walikuwa nani?
34 Kutoka Babuloni, unajimu ulipelekwa Misri, Ashuru, Uajemi, Ugiriki, Roma, na Uarabu. Katika Mashariki, Wahindu na Wachina pia walikuwa na mifumo yao ya unajimu yenye madoido. Wale “mamajusi” ambao mwevanjeli Mathayo aliripoti kuwa walimwendea mtoto mchanga Yesu walikuwa “wa mashariki.” (Mathayo 2:1, 2) Wasomi fulani huamini kwamba wanajimu hao yaweza kuwa walikuwa wa kikundi chenye mawazo tofauti ya unajimu wa Ukaldayo na Umedi-Uajemi kutoka Parthia, ambayo ilikuwa imekuwa mkoa wa Uajemi na baadaye ikawa Milki ya Parthia iliyo huru.
35. Ni nini kilichositawi katika unajimu kuanzia na wakati wa Wagiriki?
35 Hata hivyo, Wagiriki ndio waliositawisha unajimu ukawa namna ile inayozoewa leo. Katika karne ya pili W.K., Klaudio Ptolemy, mtaalamu Mgiriki wa elimunyota-anga katika Aleksandria, Misri, alikusanya katika vitabu vinne habari yote ya unajimu iliyokuwapo, vilivyoitwa Tetrabiblos, ambavyo vimekuwa maandishi ya msingi ya unajimu mpaka wa leo. Kutokana na hilo ukasitawi uitwao unajimu-uzazi, yaani, mfumo wa kubashiri wakati ujao wa mtu kwa kuchunguza chati yake ya kuzaliwa, au kupiga falaki—chati inayoonyesha vituo vya jua, mwezi, na sayari mbalimbali kati ya vikundi vya nyota kama zinavyoonekana kutoka mahali pa mtu pa kuzaliwa dakika ile ya kuzaliwa kwake.
36. Ni uthibitisho gani kwamba unajimu ulikuja kuwa wenye kustahika?
36 Kufikia karne za 14 na 15, unajimu ulikuwa umekubalika na wengi katika nchi za Magharibi. Vyuo vikuu viliufundisha kuwa fundisho, lililohitaji maarifa ya lugha na hisabati (hesabu). Wanajimu walionwa kuwa wasomi. Maandishi ya Shakespeare yamejaa marejezo ya uvutano wa kinajimu katika mambo ya kibinadamu. Kila baraza la kifalme na washarifu wengi wakaweka wanajimu wa kibinafsi kwa ajili ya uelekezi wakati wowote. Karibu hakuna utendaji—iwe ni vita, ujenzi, biashara, au usafiri—uliofanywa bila ya nyota kufikiriwa kwanza. Unajimu ulikuwa umekuwa wenye kustahika.
37. Maendeleo ya sayansi yameathirije unajimu?
37 Hata ingawa vitabu vya wataalamu wa elimunyota-anga kama Koperniko na Galileo, pamoja na utafiti ulioendelea wa kisayansi, vimeonyesha unajimu si sayansi halali, umeendelea mpaka wa leo. (Ona kisanduku, ukurasa 85.) Sanaa hii ya kifumbo, iliyoanzishwa na Wababuloni, ikasitawishwa na Wagiriki, na kupanuliwa zaidi na Waarabu, ingali ina uvutano mkubwa leo kwa viongozi wa Serikali na pia kwa mtu wa kawaida, wawe ni wa kutoka mataifa yaliyoendelea kitekinolojia au wa vijiji vilivyotengwa mbali katika nchi zinazositawi.
Yatakayotukia Yameandikwa Usoni na Katika Kiganja cha Mkono
38. Ni nini kilichoongoza kwenye namna zaidi za uaguzi zenye kuhusiana na mkono na uso wa kibinadamu?
38 Ikiwa kutafuta kwenye mbingu ishara na mikosi juu ya wakati ujao kwaonekana si halisi, kuna njia nyingi za karibu zaidi na zenye kufikilika kwa urahisi kwa wale wanaojihusisha na ufundi wa uaguzi. Zohar, au Sefer ha-zohar (Kiebrania, Kitabu cha Uzuri Mwingi), maandishi ya karne ya 13 ya imani ya mafumbo ya Kiyahudi, kilijulisha: “Kwenye kuba linaloufunika ulimwengu, tunaona maumbo mengi yanayofanyizwa na nyota na sayari. Yanafunua vitu vilivyofichwa na mafumbo makubwa. Hali moja, juu ya ngozi yetu inayomfunika binadamu kuna maumbo na tabia ambazo ndizo nyota za miili yetu.” Falsafa hii iliongoza kwenye njia nyingine zaidi za uaguzi, au kutabiri wakati ujao, kwa kuangalia uso na kiganja cha mkono ili kutafuta ishara za utabiri. Katika nchi za Mashariki na katika nchi za Magharibi pia, mazoea hayo yangali yameenea pote. Lakini ni wazi kwamba asili zayo zina mizizi katika unajimu na mizungu.
39. Fizionomonia ni nini, nayo imetumiwaje?
39 Fizionomonia ni utabiri wa matukio mema au mabaya kwa kuangalia alama za uso, kama vile umbo la macho, pua, meno, na masikio. Katika Strasbourg katika 1531, John fulani wa Indagine alichapisha kitabu juu ya habari hiyo ambamo alitokeza michoro dhahiri ya uso na maumbo mbalimbali ya macho, pua, masikio, na kadhalika, pamoja na fasiri zake. Yapendeza kujua kwamba alinukuu maneno ya Yesu Kristo kwenye Mathayo 6:22, “Basi jicho lako likiwa safi [“sahili,” NW], mwili wako wote utakuwa na nuru,” kuwa msingi wa kusema kwamba macho mapana, maangavu, na ya mviringo ni alama ya uaminifu-maadili na afya njema, hali macho yaliyoingia ndani na madogo yalikuwa ishara ya wivu, nia mbaya, na tuhuma. Hata hivyo, katika kitabu kama hicho, Compendium of Physiognomy, kilichochapishwa katika 1533, mtungaji Bartolommeo Cocle alidai kwamba macho mapana na mviringo ni ishara ya mtu kigeugeu na mvivu.
40. (a) Kairomansi ni nini? (b) Biblia ilitumiwaje ili kuunga mkono kairomansi?
40 Kulingana na waaguzi, baada ya kichwa, mkono ndio huonyesha kani za kutoka juu zaidi ya sehemu nyingine yoyote ya mwili. Kwa hiyo, kusoma mistari ya mkono ili kujua tabia ya mtu na yatakayotukia ni namna nyingine ya uaguzi inayopendwa na wengi—Kairomansi, ambayo kwa kawaida hurejezewa kwa njia rahisi kuwa kusoma kiganja cha mkono. Wakairomansi wa Enzi za Katikati walichunguza-chunguza Biblia ili iunge mkono ufundi wao. Wakatokeza mistari kama ile isemayo “Huufunga mkono wa kila binadamu; ili watu wote aliowaumba wajue [“kazi yake,” KJ] na “Ana wingi wa siku katika mkono wake wa kuume, utajiri na heshima katika mkono wake wa kushoto.” (Ayubu 37:7; Mithali 3:16) Vivimbevimbe, au miinuko, ya mkono ilichunguzwa pia kwa sababu ilidhaniwa kuwa iliwakilisha sayari na kwa hiyo ilifichua jambo fulani juu ya mtu huyo na wakati ujao wake.
41. Watu katika nchi za Mashariki huzoeaje uaguzi?
41 Utabiri wa matukio mema au mabaya kwa alama za uso na mkono ni wenye kupendwa sana na wengi katika nchi za Mashariki. Kando ya wasomaji watarazaki na washauri watoao huduma zao, wasio watarazaki na wale wenye kujifanyia wenyewe ni tele kwa sababu vitabu na vichapo vya kila kiwango vyapatikana kwa wingi. Mara nyingi watu hujihusisha na kusoma kiganja cha mkono kuwa namna ya kujitumbuiza, lakini wengi huchukua mambo hayo kwa uzito. Hata hivyo, kwa ujumla, ni mara chache watu wanaporidhika na kutumia namna moja tu ya uaguzi. Wanapokabiliwa na matatizo makubwa au maamuzi makubwa, wanaenda kwenye hekalu lao, liwe ni la Buddha, Tao, Shinto, au jingine, wakapate uelekezi kutoka vijimungu, ndipo kwa mnajimu akaangalie nyota, kwa mtabiri matukio mema au mabaya ili asome kiganja chao cha mkono na kutazama uso wao, na, baada ya yote hayo, hurudi kwao na kuulizia habari za wazazi wao wa kale waliokufa. Wanatumaini kupata jibu mahali fulani linaloekea kuwafaa.
Je! Ni Tafrija Isiyo na Madhara?
42. Tamaa ya asili ya watu kutaka kujua wakati ujao imewaongoza kwenye nini?
42 Ni jambo la asili kila mtu atake kujua mambo yatakayokuwa wakati ujao. Tamaa ya kupata mema na kuepuka yanayoweza kudhuru ni ya kila mtu. Ndiyo sababu watu katika enzi zote wametegemea roho na viabudiwa kwa ajili ya mwongozo. Kwa kufanya hivyo, walijihusisha katika kuwasiliana na roho, mizungu, unajimu, na mazoea mengine ya kishirikina. Nyakati zilizopita watu walivaa hirizi na talasimu ili wajilinde, na waliwaendea waganga na washamani wapate maponyo. Leo watu wangali wanabeba medali ya “Mtakatifu” Christopher au huvaa hirizi za “bahati njema,” na mikutano ya kuwasiliana na roho, mbao za kuagulia, matufe ya kifuwele, falaki, na karata za kutabiri jaha. Kuhusu kuwasiliana na roho na ushirikina, yaonekana ainabinadamu haikubadilika sana.
43. (a) Wengi huhisije juu ya kuwasiliana na roho, mizungu, na uaguzi? (b) Ni maswali gani juu ya mazoea ya kishirikina yahitaji kujibiwa?
43 Bila shaka, watu wengi hutambua kwamba mambo haya hayana maana ila ni ushirikina na kwamba hayana msingi halisi. Na huenda wakaongeza kwamba wao hufanya hivyo kwa ajili ya tafrija. Wengine hata hutoa hoja kwamba mizungu na uaguzi hunufaisha sana kwa sababu huwapa watu uhakikisho wa kisaikolojia ambao ama sivyo wangetishwa na vipingamizi wanavyokabili maishani. Lakini je! yote hayo ni tafrija isiyo na madhara au ni kichocheo cha kisaikolojia? Ni nini hasa chanzo cha mazoea ya kuwasiliana na roho na ya mizungu ambayo tumefikiria katika sura hii na pia yale mengine mengi ambayo hatukutaja?
44. Kimsingi, yaweza kusemwa nini juu ya tegemeo la mazoea yote hayo?
44 Tulipokuwa tukichunguza sehemu mbalimbali za kuwasiliana na roho, mizungu, na uaguzi, tumeona kwamba zakamatana sana na imani katika nafsi zilizokufa na kuwapo kwa roho, wema na waovu. Kwa hiyo, kimsingi, imani katika roho, mizungu, na uaguzi inategemea namna fulani ya itikadi ya kwamba kuna miungu mingi, na imani hiyo imetia mizizi katika fundisho la kutoweza kufa kwa nafsi ya kibinadamu. Je! huo ni msingi timamu wa mtu kujenga dini yake juu yao? Je! wewe ungechukua ibada inayotegemea msingi huo kuwa yenye kukubalika?
45. Ni swali gani juu ya chakula kilichotolewa kwa sanamu lililokabili Wakristo wa karne ya kwanza?
45 Wakristo katika karne ya kwanza walikabiliwa na maswali ayo hayo. Walikuwa wamezungukwa na Wagiriki na Waroma, pamoja na vijimungu na viabudiwa vyao vingi na pia sherehe zao za ibada za kishirikina. Sherehe moja ya ibada ilikuwa ni zoea la kuzitolea sanamu chakula halafu kushiriki kukila chakula hicho. Je! yeyote aliyependa Mungu wa kweli na aliyetaka kumpendeza ashiriki katika sherehe hizo za ibada? Angalia jinsi mtume Paulo alivyojibu swali hilo.
46. Paulo na Wakristo wa mapema waliamini nini juu ya Mungu?
46 “Basi kwa habari ya kuvila vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu; twajua ya kuwa sanamu si kitu katika ulimwengu, na ya kuwa hakuna Mungu ila mmoja tu. Kwa maana ijapokuwa wako waitwao miungu, ama mbinguni ama duniani, kama vile walivyoko miungu mingi na mabwana wengi; lakini kwetu sisi Mungu ni mmoja tu, aliye Baba, ambaye vitu vyote vimetoka kwake, nasi tunaishi kwake.” (1 Wakorintho 8:4-6) Kwake Paulo na Wakristo wa karne ya kwanza, dini ya kweli haikuwa ibada ya vijimungu vingi, si imani katika miungu mingi, bali ilikuwa ujitoaji kwa ‘Mungu mmoja aliye Baba,’ ambaye jina lake Biblia hufichua inaposema: “Wajue ya kuwa Wewe, uitwaye jina lako YEHOVA, Ndiwe peke yako Uliye juu, juu ya nchi yote.”—Zaburi 83:18.
47. Paulo alifunuaje utambulishi wa kweli wa ‘miungu na mabwana mbinguni au duniani’?
47 Hata hivyo, twapaswa kuangalia kwamba ingawa mtume Paulo alisema “sanamu si kitu,” yeye hakusema hawako “miungu” na “mabwana” ambao kwao watu waligeukia pamoja na mizungu, uaguzi, na dhabihu zao. Basi, hoja ni nini? Paulo aliionyesha wazi baadaye katika barua iyo hiyo alipoandika: “Lakini vitu vile [“mataifa” NW] wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu.” (1 Wakorintho 10:20) Ndiyo, kupitia miungu na mabwana wao, mataifa walikuwa hasa wanaabudu roho waovu—viumbe vya kimalaika, au vya kiroho, ambavyo vilimwasi Mungu wa kweli na kujiunga na kiongozi wavyo, Shetani Ibilisi.—2 Petro 2:4; Yuda 6; Ufunuo 12:7-9.
48. Ni hatari gani kutokana na mafumbo ingali ipo leo, nayo yaweza kuepukwaje?
48 Mara nyingi watu huhurumia waitwao watu wa kikale ambao walikuwa wametumikishwa na ushirikina na hofu zao. Husema wanachukizwa na dhabihu zenye umwagaji damu na sherehe za kikatili. Na kwa kufaa hivyo. Lakini, mpaka wa leo tungali twasikia juu ya ibada ya wazazi wa kale waliokufa na ya kiuchawi, ibada za kishetani, hata dhabihu za kutoa wanadamu. Ingawa hivyo vyaweza kuwa visa vya kupita kiasi, bado vyadhihirisha kwamba kupendezwa na mafumbo kungali kumechacha sana. Huenda kukaanza kama ‘tafrija isiyo na madhara’ na udadisi tu, lakini matokeo mara nyingi ni tanzia na kifo. Jinsi ilivyo hekima kutii onyo la Biblia: “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.”—1 Petro 5:8; Isaya 8:19, 20.
49. Ni nini litakalokuwa lengo la uchunguzi katika sura zifuatazo za kitabu hiki?
49 Tukiwa tumefikiria jinsi dini ilivyoanza, aina tofauti za ngano za kale, na fani (aina) mbalimbali za kuwasiliana na roho, mizungu, na ushirikina, sasa tutageuza uangalifu wetu kuelekea dini kubwa-kubwa zilizo rasmi zaidi za ulimwengu—Uhindu, Dini ya Buddha, Dini ya Tao, Dini ya Confucius, Dini ya Shinto, Dini ya Kiyahudi, makanisa ya Jumuiya ya Wakristo, na Uislamu. Zilianzaje? Zinafundisha nini? Zina uvutano gani juu ya waumini wazo? Maswali hayo na mengine yatafikiriwa katika sura zinazofuata.
[Blabu katika ukurasa wa 76]
Mizungu fulani ilionekana kuwa ilifanikiwa
[Sanduku katika ukurasa wa 85]
Je! Unajimu ni wa Kisayansi?
Unajimu hudai kwamba jua, mwezi, nyota, na sayari zaweza kuongoza mambo duniani na kwamba umbo la magimba haya ya kimbingu huathiri maisha ya mtu wakati wa dakika ya kuzaliwa kwake. Hata hivyo, mavumbuzi ya kisayansi yanatokeza hoja kubwa zenye kupinga:
▪ Vitabu vya wataalamu wa nyota na anga kama Koperniko, Galileo, na Kepler vimeonyesha kwamba dunia siyo kitovu cha ulimwengu wote mzima. Pia inajulikana sasa kwamba mara nyingi nyota zinazoonekana kuwa katika kikundi fulani kwa kweli hazijafungamanishwa katika kikundi fulani. Baadhi yazo huenda zikawa ndani sana katika anga la juu, hali nyingine huenda zikawa karibu kwa uhusianifu. Kwa hiyo, tabia zenye kuhusu kanda za vikundi mbalimbali vya nyota ni za kuwaziwa tu.
▪ Sayari Zohari, Kausi, na Utaridi hazikujulikana na wanajimu wa kwanza kwa sababu hazikuvumbuliwa mpaka darubini ilipobuniwa. Basi, “mavutano” yazo yalitolewaje sababu na chati za kinajimu zilizochorwa karne nyingi kabla ya hapo? Kuongezea hayo, kwa nini “uvutano” wa sayari moja uwe “mwema” na mwingine “mbaya,” hali sayansi inajua sasa kwamba kwa msingi zote ni matungamo ya mwamba usio na uhai au gesi, zikipita kasi katika anga la juu?
▪ Sayansi ya visadifu (tabia za urithi) hutuambia kwamba msingi wa vitabia vya utu wetu hufanyizwa, si wakati wa kuzaliwa, bali mimba inapotungwa, wakati moja ya mamilioni mengi ya chembe-chembe za shahawa kutoka kwa baba inapoungana na chembe-chembe moja ya yai kutoka kwa mama. Hata hivyo, unajimu hupiga falaki na kumwekea mtu nyota yake wakati wa dakika ile ya kuzaliwa. Tofauti hii ya karibu miezi tisa yapasa kumpa mtu mtazamo tofauti katika mambo ya kinajimu.
▪ Kupimwa kwa wakati wa safari ya jua kati ya vikundi vya nyota kama inavyoonwa na mtazamaji aliyepo duniani leo ni karibu mwezi mmoja nyuma ya ilivyokuwa miaka 2,000 iliyopita wakati chati na majedwali ya unajimu yalipochorwa. Hivyo, unajimu ungemweka mtu aliyezaliwa mwishoni Juni au mapema Julai kuwa Kansa (mnyetevu sana, mwenye moyo-mgeugeu, mnyamavu). Hata hivyo, kwa kweli wakati huo jua limo katika kikundi cha nyota Gemini, jambo ambalo lapasa kumfanya mtu huyo kuwa mwenye kuwasiliana na wengine, chapu-chapu, msemaji.
Kwa wazi, unajimu hauna msingi wa kujitegemeza ulio timamu wala wa kisayansi.
[Picha katika ukurasa wa 71]
Vioo vilivyovunjika, paka weusi, na namba fulani msingi wazo ni ushirikiana. Tarakimu ya Kichina kwa ajili ya “nne” husikika kama “kifo” katika Kichina na Kijapan
[Picha katika ukurasa wa 74]
Kushoto, Basilika ya Our Lady of Guadalupe, Meksiko, ambako Wakatoliki husali kwa ajili ya maponyo ya kimuujiza.
Kulia, Stonehenge, Uingereza, ambako Wadruidi wa kale husemekana waliabudu jua
[Picha katika ukurasa wa 80]
Watu fulani huendea washamani na wachawi
[Picha katika ukurasa wa 81]
Wengine huwa na mikutano yao ya kuwasiliana na roho, mbao za kuagulia, matufe ya kifuwele, karata za uaguzi, na watabiri-jaha
[Picha katika ukurasa wa 82]
Uaguzi katika nchi za Mashariki, kwa kutumia michoro juu ya magamba ya kobe na alama ya yin-yang, una historia ndefu
[Picha katika ukurasa wa 87]
Watu wengi hupiga falaki, wakiamini kwamba kituo cha jua, mwezi, sayari, na nyota wakati wa dakika ya mtu kuzaliwa huathiri maisha zao
[Picha katika ukurasa wa 90]
Kwa kutikisa kijiti cha jaha nje ya ala yacho, mjitoaji hupokea ujumbe na fasiri