Wayahudi, Wakristo, na Lile Tumaini la Kimesiya
“Mimi naamini kwa imani kamili kwamba Mesiya atakuja, na ijapokuwa aweza kukawia, bado kila siku nitangojea kuja kwake.”—Moses Maimonides (huitwa pia Rambam), (1135-1204).1
MESIYA! Imani ya kufika kwake ilitunzwa moyoni miongoni mwa Wayahudi kwa karne nyingi. Hata hivyo, Yesu wa Nazareti alipokuja, hatimaye Wayahudi walio wengi walimkataa kuwa siye Mesiya. Katika akili ya Wayahudi, Yesu hakutimiza mataraja yao.
“Mesiya” humaanisha “mpakwa-mafuta.” Miongoni mwa Wayahudi jina hilo la cheo lilikuja kumaanisha mzao wa Mfalme Daudi ambaye angeanzisha utawala mtukufu. (2 Samweli 7:12, 13) Kufikia siku za Yesu, Wayahudi walikuwa wameteseka kwa karne nyingi chini ya mfululizo wa watawala waonevu wasio Wayahudi. Wao walitamani mkombozi wa kisiasa.2 Kwa hiyo wakati Yesu wa Nazareti alipojitokeza akiwa ndiye Mesiya aliyengojewa kwa muda mrefu, kama vile ingetazamiwa mwanzoni kulikuwako msisimuko mwingi sana (Luka 4:16-22) Lakini Yesu hakuwa shujaa wa kisiasa, akiwakatisha tamaa sana Wayahudi. Kinyume cha hilo, yeye alidai kwamba Ufalme wake ‘haukuwa wa ulimwengu.’ (Yohana 18:36) Zaidi ya hilo, wakati ule Yesu hakuanzisha enzi tukufu ya Kimesiya iliyotangulia kuonwa na nabii Isaya. (Isaya 11:4-9) Na Yesu alipouawa kama mhalifu, taifa lile kwa ujumla liliacha kupendezwa naye.
Bila kuzuiwa na matukio hayo, wafuasi wa Yesu waliendelea kumtangaza kuwa ndiye Mesiya. Ni nini iliyokuwa sababu ya bidii yao yenye kutokeza? Ni imani ya kwamba kifo cha Yesu kilitimiza unabii, hasa unabii wa Isaya 52:13–53:12. Kwa sehemu huo wasomwa hivi:
“Ona, Mtumishi Wangu atasitawi, atakwezwa na kuinuliwa juu, . . . kwa kuwa alichipuka na kutokeza juu kama chipukizi, na kama mzizi kutoka katika ardhi kavu . . . Alidharauliwa, akakataliwa na watu, mtu wa kuteseka, na afahamianaye na maradhi, na ambaye watu humficha uso wao: Alidharauliwa, nasi hatukumstahi. Hakika alibeba maradhi yetu, na maumivu yetu alichukua . . . Alisetwa kwa sababu ya uovu wetu: mapigo ya hali njema yetu yalikuwa juu yake, na kwa mapigo yake tuliponywa. Sisi sote kama kondoo tulipotea, tuligeukia kila mmoja njia yake mwenyewe . . . Alionewa, ijapokuwa alijinyenyekeza na kinywa chake hakufumbua; kama mwana-kondoo ambaye huongozwa kwenye machinjo, . . . alikatiliwa mbali kutoka nchi ya walio hai. . . . Nao walimfanyia kaburi pamoja na waovu.”—JP.a
Mesiya Mwenye Kuteseka?
Je! Isaya alitabiri hapa Mesiya mwenye kuteseka, mwenye kufa? Waelezaji Wayahudi walio wengi wa kisasa husema hapana. Baadhi yao hudai kwamba Mtumishi Mwenye Kuteseka alikuwa taifa la Israeli lenyewe wakati wa uhamisho walo katika Babuloni. Wengine huhusianisha kuteseka na vipindi vya zile Krusedi au lile Teketezo la Umati la Nazi.3 Lakini je, maelezo hayo yanathibitika yanapochunguzwa sana? Ni kweli kwamba katika vifungu fulani vya maneno Isaya hulieleza taifa la Israeli kuwa “mtumishi” wa Mungu. Lakini yeye hulieleza Israeli kuwa mtumishi mpotovu, mwenye dhambi! (Isaya 42:19; 44:21, 22) Hivyo kichapo Encyclopaedia Judaica huonyesha tofauti hii: “Israeli halisi ni lenye dhambi na Mtumishi [katika Isaya 53], hana dhambi.”4
Kwa hiyo, baadhi yao hutoa hoja kwamba Mtumishi huwakilisha ‘kikundi cha walio wateule waadilifu’ katika Israeli ambacho kiliteseka kwa niaba ya Wayahudi wenye dhambi.5 Lakini Isaya hakusema kamwe juu ya wateule wowote kama hao. Tofauti na hilo, alitabiri kwamba taifa zima lingekuwa lenye dhambi! (Isaya 1:5, 6; 59:1-4; linganisha Danieli 9:11, 18, 19.) Pamoja na hayo, wakati wa vipindi vya mateso, Wayahudi waliteseka wawe walikuwa waadilifu au hawakuwa waadilifu.
Tatizo jingine: Mtumishi huyo aliteseka kwa ajili ya nani? Kichapo cha maelezo cha Kiyahudi Soncino hudokeza kwamba ni kwa ajili ya Wababuloni. Ikiwa ndivyo, ni nani aliyekiri kwamba Mtumishi huyo aliteseka ‘kwa sababu ya uovu wetu’? (Isaya 53:5) Je! ni jambo lenye kupatana na kufikiri kuzuri kuamini kwamba Wababuloni (au Wamataifa wengine wowote) wangekubali kwa njia yenye kutokeza hivyo—kwamba Wayahudi waliteseka kwa niaba yao?6
Kwa kupendeza, baadhi ya marabi (na idadi fulani tangu hapo) wa karne ya kwanza walimtambulisha Mtumishi mwenye kuteseka kuwa ndiye Mesiya.7 (Ona kisanduku katika ukurasa wa 11.) Maelfu ya Wayahudi walipata kuona ulingano usiokanushika kati ya Mtumishi Mwenye Kuteseka na Yesu wa Nazareti. Kama Mtumishi huyo, Yesu alikuwa wa asili maskini. Hatimaye, alidharauliwa na kuepukwa. Ijapokuwa yeye hakutimiza ushindi wowote wa kisiasa, alichukua maradhi ya wengine, akiponya kimwujiza magonjwa yao. Ajapokuwa bila hatia, alikufa likiwa tokeo la hukumu isiyo ya haki—tukio lililokusudiwa kimungu ambalo alikubali bila kuteta.
Mesiya Mwenye Kufa?
Kwa nini Mesiya alazimike kufa? Isaya 53:10 hueleza hivi: “Lakini BWANA alichagua kumseta kwa maradhi, ili, akijitoa awe toleo kwa ajili ya hatia, apate kuona uzao na awe na maisha marefu, na ili kupitia yeye kusudi la BWANA lipate kufanikiwa.” (Ta) Hilo liligusia lile zoea la Kilawi la kutoa wanyama ili kufunika dhambi au hatia. Mesiya angepatwa na kifo chenye aibu, lakini kama vile mnyama mwenye kutolewa dhabihu, kifo chake kingekuwa na thamani yenye kufunika.
Lakini Mesiya akifa, angewezaje kutimiza ule unabii mwingine mbalimbali kuhusu utawala wake wenye utukufu, sembuse ‘kuona uzao na kuwa na maisha marefu’? Kupatana na akili, ni kwa kufufuliwa kutoka katika wafu. (Linganisha 1 Wafalme 17:17-24.) Kufufuliwa kwa Mesiya kungetatua pia ule unabii unaoonekana kupingana katika Danieli 7:13, uliotabiri kwamba Mesiya angekuja kwa shangwe ya ushindi akiwa katika mawingu ya mbingu, na Zekaria 9:9, ambalo lilitabiri kwamba angekuja kwa unyenyekevu akiwa anampanda punda. Talmudi ilijaribu kueleza habari hizi zinazoelekea kupingana kwa kudai hivi: “Ikiwa zina ustahili, atakuja katika mawingu ya mbingu; la sivyo, akiwa mnyenyekevu na akiwa anampanda punda.” (Sanhedrini 98a)8 Hilo lingemaanisha kwamba unabii kwenye ama Danieli 7:13 ama Zekaria 9:9 ungebaki bila kutimizwa. Hata hivyo, kufufuliwa kwa Mesiya kungemruhusu kutimiza unabii huo wa mara mbili. Mwanzoni, angekuja kwa unyenyekevu ateseke na kufa. Baada ya ufufuo wake, angerudi katika utukufu na kuanzisha ule utawala wa Kimesiya wa kimbingu.
Maelfu ya mashahidi Wayahudi waliojionea kwa macho yao walishuhudia kwamba Yesu alifufuliwa kutoka katika wafu. (1 Wakorintho 15:6) Je! madai hayo yaweza kupuuzwa?
Uyuda na Yesu
Wayahudi walio wengi wa karne ya kwanza walimkataa Yesu kuwa siye Mesiya. Hata hivyo, alikuwa na matokeo makubwa sana juu ya Uyuda. Ingawa Yesu hutajwa mara chache sana katika Talmudi, yale machache yaliyosemwa hujaribu “kumdhihaki Yesu akiwa mtu kwa kumhesabia uzaliwa wa haramu, mizungu, na kifo chenye aibu.”b—The Jewish Encyclopedia.9
Msomi Myahudi Joseph Klausner hukubali kwamba hadithi hizo “huonekana kana kwamba zimenuiwa kimakusudi zipinganishe matukio yaliyoandikwa katika zile Gospeli.”11 Na kukiwa na sababu nzuri! Kanisa Katoliki lilikuwa limezidisha chuki ya Wayahudi juu ya Yesu kwa upingaji walo wa Usemiti. Liliwatenga Wayahudi mbali zaidi kwa kumtangaza Yesu kuwa ‘Mungu Mwana’ wa kuwaziwa—sehemu ya Utatu usioeleweka—kwa kupingana moja kwa moja na mafundisho ya Yesu mwenyewe. Kwenye Marko 12:29, Yesu alinukuu Torati, akisema hivi: “Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana Mmoja.”—Union Version; Kumbukumbu la Torati 6:4.
Ijapokuwa Uyuda ulikinza kuongolewa, “Ukristo ulikuwa na matokeo makubwa juu ya Uyuda. Ulilazimisha Marabi wabadili mkazo wao na katika visa fulani wabadili maoni yao.”12 Marabi wa vizazi vya mapema zaidi waliamini kwamba tumaini la Kimesiya lilienea katika Maandiko. Waliona miali ya tumaini hilo katika maandishi ya Biblia kama vile Mwanzo 3:15 na 49:10. Targumu ya Palestina ilitumia utimizo wa andiko hilo la kwanza katika “siku ya Mfalme Mesiya.”13 Kichapo Midrash Rabbah kilisema juu ya ule mstari wa pili hivi: “Hili lagusia juu ya Mesiya wa kifalme.” 14 Talmudi pia ilitumia unabii mbalimbali wa Isaya, Danieli, na Zekaria kuhusu Mesiya.15 “Manabii wote wametoa unabii juu ya siku za Mesiya peke yazo,” Talmudi, Sanhedrini 99a.16
Lakini chini ya mkazo wa jitihada za kuongoa za Jumuiya ya Wakristo, Uyuda ulikadiria upya maoni yao. Maandishi mengi ya Maandiko ambayo kwa muda mrefu yalikuwa yametumiwa juu ya Mesiya yalifasiriwa upya.17 Nyakati za kisasa zilipokuwa zikianza, chini ya uvutano wa uchambuzi wa Biblia, baadhi ya wasomi Wayahudi walikata maneno kwamba tumaini la Kimesiya halionekani katika Biblia hata kidogo!18
Hata hivyo, tumaini la Kimesiya lilipata kitu kama uzaliwa mpya wakati Taifa la Israeli lilipofanyizwa katika 1948. Harold Ticktin aandika hivi: ‘Vyama vilivyo vingi vya Kimesiya huona kutokea kwa Taifa la Israeli kuwa tukio kuu la kiunabii,’19 Ingawa hivyo, suala la kwamba Mesiya aliyengojewa kwa muda mrefu angefika wakati gani lilibaki bila kutatuliwa katika wazo la Kiyahudi. Talmudi chasema hivi: “Wakati mwonapo kizazi kimelemewa sana na taabu nyingi kama mto, ngojeni [Mesiya].” (Sanhedrini 98a)20 Hata hivyo, Mesiya wa Kiyahudi hakuja wakati wa taabu nyingi ya lile Teketezo la Umati wala wakati wenye msukosuko wa uzawa wa Taifa la Israeli. Mtu hujiuliza, ‘Ni taabu gani zaidi ambazo lazima ziwapate Wayahudi kabla ya Mesiya kuja?’
Kutafuta Mesiya
Tumaini la Kimesiya lilizaliwa na kusitawishwa na Wayahudi. Miongoni mwao tumaini hilo limefifia. Uangavu walo ni kama umezimwa na karne nyingi za kuteseka na kukatishwa tamaa. Kwa kinyume kabisa, mamilioni miongoni mwa mataifa, au wasio Wayahudi, wamekuja kumtafuta na hatimaye kumkubali Mesiya. Je! ni tukio lisilokusudiwa tu kwamba Isaya alisema juu ya Mesiya kwamba: “Yeye mataifa [wasio Wayahudi] watamtafuta”? (Isaya 11:10, JP) Je! Wayahudi hawapaswi pia kumtafuta Mesiya wao wenyewe? Sababu gani wajinyime tumaini walilolithamini sana moyoni?
Hata hivyo, ni kazi bure kutafuta Mesiya wa wakati ujao. Kama angekuja, angewezaje kujitambulisha kuwa mzao wa kweli wa Mfalme Daudi? Je! maandishi ya kiukoo hayakuharibiwa pamoja na hekalu la pili? Ingawa maandishi hayo yalikuwako katika siku za Yesu, dai lake la kuwa mzao halali wa Daudi halikukanushwa kamwe kwa mafanikio.c Je! yeyote mwenye kudai kuwa Mesiya wakati ujao angeweza kutoa vitambulisho kama hivyo wakati wowote? Hivyo lazima mtu atafute Mesiya aliyekuja wakati uliopita.
Hilo lataka kuchunguza upya habari juu ya Yesu, na kuondolea mbali mawazo ambayo mtu amekuwa nayo hapo kwanza. Ile michoro ya kanisa yenye sura hafifu haifanani ya namna ya kike na jinsi Yesu alivyokuwa hasa. Masimulizi ya Gospeli—yaliyoandikwa na Wayahudi—humwonyesha kuwa mwanamume mwenye nguvu nyingi, mwenye bidii katika tendo, rabi mwenye hekima isiyo ya kawaida. (Yohana 3:2) Kwa kweli, Yesu apita kwa mbali sana ndoto yoyote ambayo Wayahudi walipata kuwa nayo wakati wowote ya mkombozi wa kisiasa. Akiwa Mfalme mwenye kushinda, atatokeza, si taifa dhaifu la kisiasa, bali Ufalme wa kimbingu wenye nguvu nyingi zisizoshindika ambao utarudisha Paradiso duniani pote na ambao chini yao “mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo.”—Isaya 11:6, JP; Ufunuo 19:11-16.
Je! wewe utaishi katika enzi hiyo ya Kimesiya? Maimonides aliwashauri Wayahudi ‘wangojee tu Mesiya ajaye.’22 Hata hivyo, nyakati zetu ni zenye hatari sana, tusitake kuwa katika hatari ya kuwa tumekosa kujua kurudi kwake. Jamii yote ya kibinadamu yahitaji sana Mesiya, mkombozi kutoka kwa matatizo yanayotaabisha sayari hii. Kwa hiyo huu ndio wakati wa kumtafuta—kwa bidii, kwa tendo. Mashahidi wa Yehova wana hamu ya kukusaidia ufanye hivyo. Kumbuka, kutafuta Mesiya si tendo la uhaini kwa urithi wa Kiyahudi, kwa kuwa tumaini la Kimesiya limefungamanishwa na Uyuda. Na kwa kumtafuta Mesiya, huenda ukapata kwamba amekwisha kuja.
Marejezo
1. The Book of Jewish Knowledge, cha Nathan Ausubel, 1964, ukurasa wa 286; Encyclopaedia Judaica, 1971, Buku la 11, ukurasa 754.
2. The Messiah Idea in Jewish History, cha Julius H. Greenstone, 1973 (mwanzoni kilichapishwa katika 1906), ukurasa wa 75.
3. Encyclopaedia Judaica, 1971, Buku la 9, ukurasa wa 65; Soncino Books of the Bible—Isaiah, Kilichohaririwa na A. Cohen, 1949, ukurasa wa 260; You Take Jesus, I’ll Take God, cha Samuel Levine, 1980, ukurasa wa 25.
4. Encyclopaedia Judaica, 1971, Buku la 9, ukurasa wa 65.
5. Encyclopaedia Judaica, 1971, Buku la 9, ukurasa wa 65; The Suffering Servant in Deutero-Isaiah, cha Christopher R. North, Chapa ya Kwanza, 1948, ukurasa wa 9, 202-3.
6. Soncino Books of the Bible—Isaiah, kilichohaririwa na A. Cohen, 1949, ukurasa wa 261.
7. The Book of Isaiah, Kitabu cha maelezo cha Amos Chakham, 1984, ukurasa wa 575; The Targum of Isaiah, kilichohaririwa na J. F. Stennning, 1949, ukurasa wa 178; The Suffering Servant in Deutro-Isaiah, cha Christopher R. North, Chapa ya Kwanza, 1948, kurasa 11-15; Encyclopaedia Judaica, 1971, Buku la 9, ukurasa wa 65.
8. The Babylonian Talmud, kilichotafsiriwa na Dr. H. Freedma, 1959, Buku la 2, ukurasa wa 664.
9. The Jewish Encyclopedia, 1910, Buku la 7, ukurasa wa 170.
10. Israelis, Jews, and Jesus, cha Pinchas Lapide, 1979, kurasa 73-4.
11. Jesus of Nazareth—His Life, Times, and Teaching, cha Joseph Klausner, 1947, (kilichapishwa kwanza katika Uingereza katika 1925), ukurasa wa 19.
12. The Jewish People and Jesus Christ, cha Jakób Jocz, 1954 (kilichapishwa kwanza katika 1949), ukurasa wa 153.
13. Neophyti 1, Targum Palestinense, Ms de la Biblioteca Vaticana, Génesis, 1968, Buku la 1, kurasa 503-4; The Messiah: An Aramaic Interpretation, cha Samson H. Levey, 1974, kurasa 2-3.
14. Midrash Rabbah, kilichotafsiriwa na kuhaririwa na Dr. H. Freedman na Maurice Simon, 1961 (Chapa ya Kwanza 1939), Buku la 2, ukurasa wa 956; Chumash With Targum Onkelos, Haphtaroth and Rashi’s Commentary, kilichotafsiriwa na A. M. Silbermann na M. Rosenbaum, 1985, kurasa 245-6.
15. The Babylonian Talmud, kilichotafsiriwa na Dr. H. Freedman, 1959, Buku la 2, kurasa 663-5, 670-1 (Sanhedrini 98a, 98b).
16. New Edition of the Babylonian Talmud, kilichohaririwa na kutafsiriwa na Michael L. Rodkinson, 1903, Sehemu ya 4, Buku la 8, ukurasa wa 312 (Trakti Sanhedrini); The Babylonian Talmud, kilichotafsiriwa na Dr. H. Freedman, 1959, Buku la 2, ukurasa wa 670 (Sanhedrini 99a).
17. The Suffering Servant in Deutro-Isaiah, cha Christopher R. North. Chapa ya Kwanza, 1948, ukurasa wa 18: The Jewish People and Jesus Christ, cha Jakob Jocz, 1954, (kilichochapishwa kwanza katika 1949), kurasa 205-7, 282; The Pentateuch and Haftorahs, kilichohaririwa na Dr. J. H. Hertz, 1929-36, Buku la 1, ukurasa wa 202; Palestinian Judaism in New Testament Times, cha Werner Förster, kilichotafsiriwa na Gordon E. Harris, 1964, kurasa 199-200.
18. Encyclopaedia Judaica, 1971, Buku la 11, ukurasa wa 1407; U.S. Catholic, Desemba 1983, ukurasa wa 20.
19. U.S. Catholic, Desemba 1983, ukurasa wa 21; What Is Judaism?, cha Emil L. Fackenheim, 1987, kurasa 268-9.
20. The Babylonian Talmud, kilichotafsiriwa na Dr. H. Freedman, 1959, Buku la 2, ukurasa wa 663.
21. The Works of Josephus, kilichotafsiriwa na William Whiston, 1987, “Maisha ya Flavius Josephus,” 1:1-6, na “Flavius Josephus Against Apion,” kielezi cha chini juu ya 7:31, 32.
22. The Book of Jewish Knowledge, cha Nathan Ausubel, 1964, ukurasa wa 286.
23. The Targum of Isaiah, kilichohaririwa na J. F, Stenning, 1949, ukurasa wa 7, 178; The Messiah: An Aramaic Interpretation, cha Samson H. Levey, 1974, ukurasa wa 63, 66-7; The Suffering Servant in Deutro-Isaiah, cha Christopher R. North, Chapa ya Kwanza, 1948, ukurasa wa 11.
24. The Fifty-Third Chapter of Isaiah—According to the Jewish Interpreters, cha S. R. Driver na A. Neubauer, 1969, Buku la 2, ukurasa wa 7; New Edition of the Babylonian Talmud, kilichohaririwa na kutafsiriwa na Michael L. Rodkinson, 1903, Sehemu ya 4, Buku la 8, ukurasa wa 310.
25. The Fifty-Third Chapter of Isaiah—According to the Jewish Interpreters, cha S. R. Driver na A. Neubauer, 1969, Buku la 2, kurasa 374-5.
26. The Fifty-Third Chapter of Isaiah—According to the Jewish Interpreters, cha S. R. Driver na A. Neubauer, 1969, Buku la 2, ukurasa wa 10, 99-100.
[Maelezo ya Chini]
a Mitajo yote ya Maandiko ya Kiebrania imetolewa katika ama The Holy Scriptures (JP) au Tanakh (Ta), vyote viwili ni vya The Jewish Publication Society of America.
b Msomi Mwisraeli Pinchas Lapide asema hivi: “Vifungu vya maneno vya Kitalmudi juu ya Yesu . . . viliharibiwa kabisa, vikapotoshwa, au vikafutiliwa mbali na wakaguzi wa maandishi wa kanisa.” Hivyo “yaelekea sana kwamba mwanzoni Yesu alikuwa na uvutano mwingi zaidi juu ya fasihi ya kirabi zaidi ya vile vipande-vipande tulivyo navyo leo vinavyoshuhudia.”—Israelis, Jews, and Jesus.10
c Ona The Life of Flavius Josephus, 1:1-6.21
[Sanduku katika ukurasa wa 11]
Mtumishi Mwenye Kuteseka Katika Maandishi ya Kirabi
Kwa muda wa karne zilizopita hesabu fulani ya waandikaji Wayahudi wenye kuheshimiwa wameutumia unabii wa Isaya 52:13–53:12 kwa Mesiya:
Targumu ya Jonathan ben Uzziel (Karne ya 1 W.K.). Katika tafsiri yayo ya Isaya 52:13, Targumu yasema hivi: “Tazama, mtumishi wangu, yule Mpakwa-Mafuta (au, yule Mesiya) atafanikiwa.”23
Targumu ya Kibabuloni (Sanhedrini 98b) (c. karne ya 3 W.K.): “Mesiya—jina lake ni jipi? . . . Marabi husema, Mwenye ukoma [; wale] wa nyumba ya Rabi [husema, Mgonjwa], kama isemwavyo, ‘Hakika amebeba magonjwa yetu.’—Linganisha Isaya 53:4.24
Moses Maimonides (Rambam) (Karne ya 12): “Ni nini itakuwa namna ya kuja kwa Mesiya, na mahali pa kuonekana kwake kwa mara ya kwanza patakuwa wapi? . . . Kwa maneno ya Isaya [52:15], yakieleza namna ambayo katika hiyo wafalme watamsikia, Kwake yeye wafalme watafumba vinywa vyao.”25
Moses ibn Crispin Cohen (karne ya 14): Ninafurahi kufasiri [Isaya 53], kwa kupatana na fundisho la Marabi wetu, juu ya Mfalme Mesiya, na nitakuwa mwangalifu, kadiri niwezavyo, kushikamana na maana halisi: hivyo, ikiwezekana, nitaepuka mafasirio yenye kulazimishwa na yasiyoeleweka kwa urahisi ambayo kwayo wengine [waelezaji Wayahudi] wamekuwa na hatia.”26
[Picha katika ukurasa wa 10]
Wayahudi walio wengi walilikataa wazo la “Mesiya mwenye kuteseka.” Lilikuwa kinyume cha taraja lao la Mfalme mwenye kushinda.
[Picha katika ukurasa wa 12]
Ni Mesiya pekee awezaye kutokeza hali tukufu alizotabiri Isaya