Sura Ya Ishirini
Mkono wa Yehova Haujawa Mfupi
1. Hali ikoje katika Yuda, na watu wengi wanashangaa wakijiulizaje?
TAIFA la Yuda linadai eti lina uhusiano wa agano pamoja na Yehova. Hata hivyo, kila mahali ni matata tu. Haki ni haba. Uhalifu na ukandamizaji umeenea kila mahali. Na hali bora haziji kama ilivyotumainiwa. Kuna kasoro kubwa mahali fulani. Watu wengi wanashangaa wakijiuliza kama Yehova atarekebisha mambo. Hiyo ndiyo hali ya siku za Isaya. Lakini masimulizi ya Isaya kuhusu wakati huo si historia ya kale tu. Maneno yake yana maonyo ya kiunabii kwa watu wowote wanaodai eti wanamwabudu Mungu na kumbe wanapuuza sheria Zake. Na ule unabii ulioandikwa katika Isaya sura ya 59 unawapa kitia-moyo kichangamfu wale wote wanaojitahidi kumtumikia Yehova ijapokuwa wanaishi katika nyakati za magumu na hatari.
Watenganishwa na Mungu wa Kweli
2, 3. Kwa nini Yehova halindi Yuda?
2 Ebu wazia—watu wa agano la Yehova wamerudi nyuma wakawa waasi-imani! Wamempa kisogo Mfanyi wao, wakajiondoa chini ya mkono wake wa ulinzi. Basi wanasononeka vikali. Je, labda wanamlaumu Yehova kwa magumu yanayowapata? Isaya anawaambia hivi: “Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka [“haujawa mfupi ,” “NW”], hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.”—Isaya 59:1, 2.
3 Maneno hayo yamesemwa kinagaubaga, lakini ni ya kweli. Yehova angali Mungu wa wokovu. Kwa kuwa ndiye “Msikiaji wa sala,” Yeye husikiliza sala za watumishi wake waaminifu. (Zaburi 65:2, NW) Hata hivyo, hawabariki wakosaji. Watu hao wenyewe ndio wamefanya Yehova awatenganishe naye. Uovu wao wenyewe umemfanya afiche uso wake wasiuone.
4. Yuda anashtakiwa mambo gani?
4 Ukweli ni kwamba, matendo ya Yuda yamekuwa mabaya sana. Unabii wa Isaya unaorodhesha baadhi ya mashtaka yanayomkabili: “Mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu, na vidole vyenu vimetiwa unajisi kwa uovu; midomo yenu imenena uongo, ndimi zenu zimenong’ona ubaya.” (Isaya 59:3) Watu wanasema uwongo na mambo yasiyo ya haki. Usemi unaotaja ‘mikono iliyotiwa unajisi kwa damu’ unaonyesha kwamba wengine hata wameua. Loo, tendo hilo linamvunjia Mungu heshima kama nini, kwani, licha ya kukataza uuaji, yeye hukataza pia ‘kumchukia ndugu yako moyoni mwako’! (Mambo ya Walawi 19:17) Ile hali ya wakaaji wa Yuda ya kutenda dhambi bila kujizuia, na matokeo yasiyoepukika yanayowapata kwa sababu ya dhambi hiyo, inapasa kumkumbusha kila mmoja wetu leo kwamba tunahitaji kudhibiti mawazo na hisia zetu zenye dhambi. Ama sivyo, mwishowe tungeweza kufanya maovu ambayo yangetutenganisha na Mungu.—Waroma 12:9; Wagalatia 5:15; Yakobo 1:14, 15.
5. Ufisadi wa Yuda umekuwa wa kadiri gani?
5 Dhambi imeambukiza taifa zima kama ugonjwa. “Hapana adaiye kwa haki, wala hapana atetaye kwa kweli; hutumainia ubatili, hunena uongo; hupata mimba ya madhara, na kuzaa uovu.” (Isaya 59:4) Hakuna mtu anayesema mambo ya haki. Hata katika mahakama, ni nadra kupata mtu wa kutegemeka au aliye mwaminifu. Yuda amempa Yehova kisogo na kutumainia kupata msaada kwa kuungana na mataifa, hata anatumainia sanamu zisizo na uhai. Sanamu zote hizo ni “duni,” bure kabisa. (Isaya 40:17, 23; 41:29) Matokeo ni kwamba, wanapiga domo sana, wakisema upuuzi mtupu. Mipango inapangwa, lakini inapanguka na kuleta matata na madhara.
6. Matendo ya Jumuiya ya Wakristo yanafananaje na yale ya Yuda?
6 Ukosefu wa uadilifu na fujo zilizokuwa katika Yuda zina ulinganifu wa ajabu na zile zilizo katika Jumuiya ya Wakristo. (Ona “Jiji la Yerusalemu Lenye Uasi-Imani Linalingana na Jumuiya ya Wakristo,” katika ukurasa wa 294.) Vita viwili vikali vya ulimwengu vimepiganwa baina ya mataifa ambayo husemwa eti ni ya Kikristo. Hata sasa, ibada ya Jumuiya ya Wakristo imeshindwa kukomesha mauaji ya kufagilia mbali makabila fulani, na kuchinjana miongoni mwa washirika wake. (2 Timotheo 3:5) Ingawa Yesu aliwafundisha wafuasi wake kuutumaini Ufalme wa Mungu, mataifa ya Jumuiya ya Wakristo yanaendelea kutegemea silaha nyingi za kijeshi zilizojazana akibani, na kufanya mapatano ya kisiasa. (Mathayo 6:10) Kwa kweli, wengi wa watengenezaji wakuu wa silaha ulimwenguni wanapatikana katika mataifa ya Jumuiya ya Wakristo! Naam, hata Jumuiya ya Wakristo inatumainia “ubatili” kwa kutumainia jitihada za wanadamu na mashirika ili kupata usalama wa wakati ujao.
Kuvuna Matokeo Machungu
7. Kwa nini mbinu za Yuda zinatokeza madhara matupu?
7 Ibada ya sanamu na udanganyifu haziwezi kufanyiza jamii yenye hali njema. Sasa Wayahudi wasio waaminifu wanavuna matata ya mbegu walizopanda wenyewe kwa kutumainia jitihada za kibinadamu. Tunasoma hivi: “Huangua mayai ya fira, na kusuka wavu wa buibui; yeye alaye mayai yao hufa, na hilo livunjwalo hutoka nyoka.” (Isaya 59:5) Tangu kutungwa hadi kutunguliwa, mbinu za Yuda hazifanikiwi kamwe. Kuwaza kwao kubaya kunaleta madhara matupu. Ni sawa na vile tu mayai ya nyoka mwenye sumu yanavyoangua nyoka wenye sumu. Basi taifa linateseka.
8. Ni nini kinachoonyesha kwamba Yuda ana kasoro katika kuwaza kwake?
8 Wakaaji fulani wa Yuda wanaweza kufanya fujo ili wajilinde, lakini hawatafanikiwa. Kutumia mabavu hakuwezi kuwa bora kuliko kumtumainia Yehova na kufanya matendo ya uadilifu; ni kama vile tando za buibui zisivyoweza kuwa bora kuliko vazi la kujilinda na hali mbaya ya hewa. Isaya anatangaza hivi: “Nyavu zao hazitakuwa mavazi, wala hawatajifunika kwa kazi zao; kazi zao ni kazi za uovu, na vitendo vya udhalimu vimo mikononi mwao. Miguu yao hukimbilia mayai [“ubaya,” “NW”], nao hufanya haraka kumwaga damu isiyo na hatia; mawazo yao ni mawazo ya uovu; ukiwa na uharibifu zaonekana katika njia kuu zao.” (Isaya 59:6, 7) Yuda ana kasoro katika kuwaza kwake. Kwa kufanya fujo eti ajaribu kutatua matatizo yake, anaonyesha mwelekeo wa kutomwogopa Mungu. Hata kama wengi wa wale wanaoumizwa na fujo zake ni watu wasio na hatia, na hata kama baadhi yao ni watumishi halisi wa Mungu, ni shauri lao, yeye hajali.
9. Kwa nini amani ya kweli imewaponyoka kabisa viongozi wa Jumuiya ya Wakristo?
9 Maneno haya yaliyopuliziwa yanatukumbusha jinsi ambavyo Jumuiya ya Wakristo imemwaga damu. Hakika, Yehova atamtoza hesabu kwa kuwakilisha Ukristo vibaya sana! Jumuiya ya Wakristo imefuatia mwendo ulio mpotovu kama wa Wayahudi wa siku za Isaya kwa sababu viongozi wake wanaamini kwamba huo tu ndio mwendo unaofaa. Huku wanasema amani, na huku wanatenda matendo yasiyo ya haki. Jamani, unafiki gani huo! Amani ya kweli itazidi tu kuwaponyoka kabisa viongozi wa Jumuiya ya Wakristo, maadamu wanaendelea kutumia mbinu hiyo. Ni kama vile unabii unavyoendelea kusema: “Njia ya amani hawaijui; wala hapana hukumu ya haki katika miendo yao; wamejifanyizia njia zilizopotoka; kila apitaye katika njia hizo hajui amani.”—Isaya 59:8.
Kutanga-tanga Katika Giza la Kiroho
10. Isaya anafanya ungamo gani kwa niaba ya Yuda?
10 Yehova hawezi kuzibariki njia za Yuda zilizo kombokombo na zenye uharibifu. (Zaburi 11:5) Hivyo basi, akiongea kwa niaba ya taifa zima, Isaya anaungama hatia ya Yuda: “Hukumu ya haki i mbali nasi, wala haki haitufikilii; twatazamia nuru, na kumbe! latokea giza; twatazamia mwanga, lakini twaenda katika giza kuu. Twapapasa-papasa kutafuta ukuta kama kipofu, naam, twapapasa kama watu wasio na macho; twajikwaa wakati wa adhuhuri, kana kwamba ni wakati wa ukungu wa alfajiri; kati yao waliowanda tumekuwa kama wafu. Sisi sote twanguruma [“tunaendelea kuguna,” “NW”] kama dubu; twaomboleza kama hua.” (Isaya 59:9-11a) Wayahudi hawajaacha Neno la Mungu liwe taa kwa miguu yao na mwanga kwa njia yao. (Zaburi 119:105) Matokeo ni kwamba, mambo yao yanaonekana kuwa yenye giza. Hata kukiwa kweupe kabisa wakati wa adhuhuri, wanapapasa-papasa kana kwamba ni usiku. Ni kana kwamba wao ni wafu. Wanatamani sana kitulizo, kwa hiyo wanaguna kwa sauti kubwa kama madubu wenye njaa au waliojeruhiwa. Wengine wao wanalia-lia kwa kuomboleza kama njiwa wapweke.
11. Kwa nini matumaini ya Yuda ya kupata haki na wokovu ni ya bure?
11 Isaya anajua vizuri sana kwamba shida za Yuda zimetokana na kumwasi Mungu. Anasema hivi: “Twatazamia hukumu ya haki, lakini hapana; na wokovu, lakini u mbali nasi. Maana makosa yetu yamezidi kuwa mengi mbele zako, na dhambi zetu zashuhudia juu yetu; maana makosa yetu tunayo pamoja nasi, na maovu yetu tumeyajua; katika kukosa na kumkana BWANA, na katika kugeuka tusimfuate Mungu wetu, tukinena jeuri na uasi, na kukusudia maneno ya uongo na kuyatoa moyoni.” (Isaya 59:11b-13) Kwa kuwa wakaaji wa Yuda hawajatubu, bado wanahesabiwa ubaya wa dhambi walizotenda. Haki imeondoka nchini kwa sababu watu wamemwacha Yehova. Wamekuwa waongo wa mwisho, hata huwakandamiza ndugu zao. Ni sawasawa kabisa na wale waliomo katika Jumuiya ya Wakristo leo! Si kwamba tu wengi wanapuuza haki, bali pia wanawanyanyasa Mashahidi waaminifu wa Yehova wanaojaribu kufanya mapenzi ya Mungu.
Yehova Afanya Hukumu
12. Wenye madaraka ya kusimamia kufikilizwa kwa haki katika Yuda wana mtazamo gani?
12 Inaonekana hakuna haki, uadilifu, wala ukweli katika Yuda. “Hukumu imegeuka ikaenda nyuma, na haki inasimama mbali sana; maana kweli imeanguka katika njia kuu [“uwanja wa umma,” “NW”] na unyofu hauwezi kuingia.” (Isaya 59:14) Nyuma ya malango ya jiji katika Yuda, kuna viwanja vya umma ambapo wanaume wazee wanakutana kuzungumzia kesi. (Ruthu 4:1, 2, 11) Wanaume hao wanapaswa kuhukumu kwa uadilifu na kufuatia haki, wala si kukubali rushwa. (Kumbukumbu la Torati 16:18-20) Lakini wanahukumu kulingana na tamaa zao wenyewe zenye ubinafsi. Ubaya zaidi ni kwamba, wanaona ni rahisi kuwanasa watu wowote wanaojaribu kutenda mema kwa moyo mweupe. Tunasoma hivi: “Kweli imepunguka kabisa, na yeye auachaye uovu ajifanya kuwa mateka.”—Isaya 59:15a.
13. Yehova atafanya nini kwa kuwa mahakimu wa Yuda wanafanya kazi yao kizembe?
13 Wale wanaoshindwa kutoa sauti ya kupinga upotovu wa maadili wanasahau kwamba Mungu si kipofu, si mjinga, wala si mnyonge. Isaya anaandika hivi: “BWANA akaona hayo, akachukizwa kwa kuwa hapana hukumu ya haki. Akaona ya kuwa hapana mtu, akastaajabu kwa kuwa hapana mwombezi; basi, mkono wake mwenyewe ndio uliomletea wokovu; na haki yake ndiyo iliyomsaidia.” (Isaya 59:15b, 16) Kwa kuwa mahakimu waliowekwa wanafanya kazi yao kizembe, Yehova ataingilia mambo. Wakati atakapofanya hivyo, atatenda kwa uadilifu na kwa uwezo.
14. (a) Watu wengi leo wana mtazamo gani? (b) Yehova anajitayarishaje kuchukua hatua?
14 Leo kuna hali inayofanana na hiyo. Tunaishi katika ulimwengu ambamo watu wengi ‘wamekwisha kuishiwa na hisia zote za adili.’ (Waefeso 4:19) Watu wengi hawaamini kwamba Yehova ataingilia mambo ili kukomesha uovu duniani. Lakini unabii wa Isaya unaonyesha kwamba Yehova hufuatilia kwa makini mambo ya kibinadamu. Yeye hufanya hukumu, naye huchukua hatua zinazolingana na hukumu zake katika wakati wake mwenyewe. Je, hukumu zake ni za haki? Isaya anaonyesha kwamba ni za haki. Anaandika hivi kuhusu taifa la Yuda: “[Yehova] akajivika haki kama deraya kifuani, na chapeo cha wokovu kichwani pake, akajivika mavazi ya kisasi yawe mavazi yake, naye alivikwa wivu kama joho.” (Isaya 59:17) Maneno haya ya kiunabii yanaonyesha Yehova akiwa shujaa anayejiandaa kwa ajili ya pigano. Ameazimia kabisa kuleta wokovu aliokusudia. Ana uhakika kwamba uadilifu wake mwenyewe ni kamili na hauwezi kushindwa. Na atafanya hukumu zake kwa bidii na bila woga. Hakuna shaka kwamba haki itashinda.
15. (a) Wakristo wa kweli wataenendaje wakati Yehova afanyapo hukumu? (b) Ni nini linaloweza kusemwa juu ya hukumu za Yehova?
15 Leo katika nchi fulani fulani, maadui wasiotaka ile kweli wanajaribu kuzuia kazi ya watumishi wa Yehova kwa kueneza propaganda za uwongo na zenye kuwaharibia jina. Wakristo wa kweli hawasiti-siti kuitetea kweli, lakini hawatafuti kamwe kujilipizia kisasi. (Waroma 12:19) Hata wakati Yehova atakapomaliza kisa chake na Jumuiya ya Wakristo yenye uasi-imani, waabudu wa Yehova duniani hawatashiriki kuharibu jumuiya hiyo. Wanajua kwamba Yehova amejiwekea haki ya kulipiza kisasi, na kwamba atachukua hatua ifaayo wakati ufikapo. Unabii unatuhakikishia hivi: “Kadiri ya matendo yao, kwa kadiri iyo hiyo atawalipa, ukali kwao wampingao, malipo kwa adui zake; naye atavirudishia visiwa malipo.” (Isaya 59:18) Hukumu za Mungu zitakuwa za haki, lakini pia zitakuwa kamili kama katika siku za Isaya. Hata zitafika ‘visiwani,’ sehemu za mbali. Hakuna mtu atakayekuwa mbali au kando sana asiweze kufikiwa na hukumu za Yehova.
16. Ni nani watakaookoka hukumu za Yehova, na watajifunza nini kutokana na kuokoka kwao?
16 Yehova anawahukumu kwa uadilifu wale wanaojitahidi kufanya yaliyo sawa. Isaya anatabiri kwamba kuanzia pembe moja ya nchi hadi pembe nyingine—kwenye mapana na marefu yote ya dunia—watu wa jinsi hiyo wataokoka. Halafu ulinzi watakaopewa na Yehova utaimarisha sana kicho na heshima wanayompa. (Malaki 1:11) Tunasoma hivi: “Wataliogopa jina la BWANA toka magharibi, na utukufu wake toka maawio ya jua; maana yeye atakuja kama mkondo wa mto ufurikao, uendeshwao kwa pumzi ya BWANA.” (Isaya 59:19) Roho ya Yehova itaondoa vipingamizi vyote vinavyozuia kutimizwa kwa mapenzi yake, kama dhoruba yenye nguvu inayosukuma mafuriko makubwa ya maji ya uharibifu na kufagilia mbali vitu vyote vilivyo njiani. Roho ya Yehova ina nguvu nyingi kuliko nguvu yoyote ya mwanadamu. Atakapoitumia kufanya hukumu juu ya wanadamu na mataifa, atapata mafanikio yaliyo hakika na kamili.
Tumaini na Baraka kwa Wenye Kutubu
17. Mkombozi wa Sayuni ni nani, na anakomboa Sayuni lini?
17 Chini ya Sheria ya Musa, Mwisraeli aliyejiuza utumwani angeweza kununuliwa na mkombozi ili atoke utumwani. Mapema katika kitabu cha unabii cha Isaya, Yehova ameonyeshwa kuwa Mkombozi wa watu mmoja-mmoja wanaotubu. (Isaya 48:17) Sasa anaelezwa tena kuwa Mkombozi wa watu wanaotubu. Isaya anaandika hivi kuhusu ahadi ya Yehova: “Mkombozi atakuja Sayuni, kwao waachao maasi yao katika Yakobo, asema BWANA.” (Isaya 59:20) Ahadi hiyo yenye kutuliza moyo inatimizwa mwaka wa 537 K.W.K. Lakini ina utimizo zaidi. Mtume Paulo alinukuu maneno hayo katika fasiri ya Septuagint, akayatumia kuwahusu Wakristo. Aliandika hivi: “Kwa namna hii Israeli wote wataokolewa. Kama vile imeandikwa: ‘Mkombozi atakuja kutoka Zayoni na kugeuzia mbali mazoea ya kutomwogopa Mungu yatoke kwa Yakobo. Na hili ndilo agano kwa upande wangu pamoja nao, niondoleapo mbali dhambi zao.” (Waroma 11:26, 27) Kwa kweli, unabii wa Isaya unatumika hadi wakati wetu na hata baada ya hapo. Jinsi gani?
18. Yehova alitokeza “Israeli wa Mungu” wakati gani na jinsi gani?
18 Katika karne ya kwanza, mabaki wachache wa taifa la Israeli walimkubali Yesu kuwa Mesiya. (Waroma 9:27; 11:5) Siku ya Pentekoste 33 W.K., Yehova alimimina roho yake takatifu juu ya waamini karibu 120 wa mabaki hao, akawaingiza katika agano lake jipya lililopatanishwa na Yesu Kristo. (Yeremia 31:31-33; Waebrania 9:15) Siku hiyo kulitokea “Israeli wa Mungu,” yaani taifa jipya ambalo washirika wake hawatambulishwi kwa ukoo wa kimwili wa Abrahamu, bali kwa kuzaliwa na roho ya Mungu. (Wagalatia 6:16) Watu wasiotahiriwa wa Mataifa yasiyo ya Kiyahudi walihusishwa pia katika taifa hilo jipya, wa kwanza kati yao akiwa ni Kornelio. (Matendo 10:24-48; Ufunuo 5:9, 10) Hivyo Yehova Mungu aliwafanya kuwa wana, wakawa watoto wake wa kiroho, warithi wenzi wa Yesu.—Waroma 8:16, 17.
19. Yehova anafanya agano gani pamoja na Israeli wa Mungu?
19 Sasa Yehova anafanya agano pamoja na Israeli wa Mungu. Tunasoma hivi: “Tena katika habari zangu, hili ndilo agano langu nao, asema BWANA; roho yangu iliyo juu yako, na maneno yangu niliyoyatia kinywani mwako, hayataondoka kinywani mwako, wala kinywani mwa wana [“wazao,” “NW”] wako, wala kinywani mwa wajukuu wako, asema BWANA, tangu leo na hata milele.” (Isaya 59:21) Iwe maneno hayo yalitumika au hayakutumika kumhusu Isaya mwenyewe, hakika yalitimizwa katika Yesu, aliyehakikishiwa kwamba “ataona uzao wake.” (Isaya 53:10) Yesu alisema yale aliyokuwa amejifunza kutoka kwa Yehova, na roho ya Yehova ilikaa juu yake. (Yohana 1:18; 7:16) Basi ni vizuri kwamba hata ndugu zake na warithi wenzake, ambao ni washirika wa Israeli wa Mungu, wanapokea roho takatifu ya Yehova na kuhubiri ujumbe ambao wamejifunza kutoka kwa Baba yao wa kimbingu. Wote ‘wamefundishwa na Yehova.’ (Isaya 54:13; Luka 12:12; Matendo 2:38) Iwe ni kupitia Isaya au ni kupitia Yesu ambaye Isaya anamfananisha kiunabii, sasa Yehova anafanya agano kwamba hatabadilisha kamwe nafasi yao ichukuliwe na watu wengine, bali atawatumia milele wakiwa mashahidi wake. (Isaya 43:10) Hata hivyo, “wazao” wao ambao pia wanafaidika na agano hilo ni akina nani?
20. Ahadi ya Yehova kwa Abrahamu ilitimizwaje katika karne ya kwanza?
20 Nyakati za kale Yehova alimwahidi Abrahamu hivi: “Katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia.” (Mwanzo 22:18) Kupatana na jambo hilo, mabaki wachache wa Waisraeli wa asili waliomkubali Mesiya waliingia katika mataifa mengi, wakahubiri habari njema juu ya Kristo. Kwa kuanza na Kornelio, watu wengi wasiotahiriwa wa Mataifa yasiyo ya Kiyahudi ‘walijibariki’ kupitia Yesu, Mbegu ya Abrahamu. Wakawa sehemu ya Israeli wa Mungu na sehemu ya pili ya ile mbegu ya Abrahamu. Wao ni sehemu ya “taifa takatifu” la Yehova, ambalo utume wake ni ‘kutangaza kotekote sifa bora kabisa za yeye aliyewaita wao kutoka katika giza kuingia katika nuru yake ya ajabu.’—1 Petro 2:9; Wagalatia 3:7-9, 14, 26-29.
21. (a) Israeli wa Mungu wametokeza “wazao” gani nyakati za kisasa? (b) “Wazao” hao wanafarijiwaje na agano au mkataba ambao Yehova amefanya pamoja na Israeli wa Mungu?
21 Leo inaonekana kwamba idadi kamili ya Israeli wa Mungu imekusanywa. Na bado, mataifa yanaendelea kubarikiwa—tena sana. Jinsi gani? Ni kwa vile Israeli wa Mungu wamekuwa na “wazao,” yaani wanafunzi wa Yesu walio na tumaini la kupata uhai wa milele katika dunia-paradiso. (Zaburi 37:11, 29) “Wazao” hao wanafundishwa na Yehova pia na kuagizwa katika njia zake. (Isaya 2:2-4) Ingawa hawabatizwi kwa roho takatifu wala hawaonwi kuwa washiriki katika agano jipya, wanaimarishwa na roho takatifu ya Yehova kushinda vipingamizi vyote ambavyo Shetani huwawekea wanapofanya kazi ya kuhubiri. (Isaya 40:28-31) Sasa idadi yao inafikia mamilioni na inaendelea kuongezeka, huku wakitokeza wazao wao wenyewe. Agano au mkataba ambao Yehova amefanya na watiwa-mafuta huhakikishia “wazao” hao kwamba Yehova ataendelea kuwatumia kuwa wasemaji wake hadi milele.—Ufunuo 21:3, 4, 7.
22. Tunaweza kuwa na uhakika gani kuhusu Yehova, na hiyo inapaswa kuwa na matokeo gani kwetu?
22 Basi, acheni sisi sote tuendelee kumwamini Yehova daima. Yeye ana nia na pia uwezo wa kuokoa! Hakuna wakati ambao mkono wake utakuwa mfupi; sikuzote yeye atawakomboa watu wake waaminifu. Wote wanaomtumainia wataendelea kuyabeba maneno yake mema vinywani mwao “tangu leo na hata milele.”
[Sanduku katika ukurasa wa 294]
Jiji la Yerusalemu Lenye Uasi-Imani Linalingana na Jumuiya ya Wakristo
Yerusalemu, lile jiji kuu la taifa teule la Mungu, linafananisha tengenezo la Mungu la viumbe-roho wa kimbingu na pia jamii ya Wakristo watiwa-mafuta wanaofufuliwa mbinguni kuwa bibi-arusi wa Kristo. (Wagalatia 4:25, 26; Ufunuo 21:2) Hata hivyo, mara nyingi wakaaji wa Yerusalemu walikosa kuwa waaminifu kwa Yehova, na jiji hilo lilifafanuliwa kuwa kahaba na mwanamke mzinzi. (Ezekieli 16:3, 15, 30-42) Likiwa katika hali hiyo, jiji la Yerusalemu likawa mfano unaofaa kufananisha Jumuiya ya Wakristo yenye uasi-imani.
Yesu aliliita jiji la Yerusalemu “muuaji wa manabii na mpigaji kwa mawe wa hao waliotumwa kwake.” (Luka 13:34; Mathayo 16:21) Kama Yerusalemu lisilo aminifu, Jumuiya ya Wakristo inadai eti inamtumikia Mungu wa kweli, na kumbe inaziacha sana njia zake za uadilifu. Tunaweza kuwa na uhakika kwamba Yehova atahukumu Jumuiya ya Wakristo kwa kutumia viwango vile vile vya uadilifu alivyovitumia kuhukumu Yerusalemu lenye uasi-imani.
[Picha katika ukurasa wa 296]
Hakimu anapaswa kuhukumu kwa uadilifu, atafute haki, na asikubali rushwa zozote
[Picha katika ukurasa wa 298]
Hukumu za Yehova zitakuwa kama mto uliofurika, zifagilie mbali vipingamizi vyote vinavyozuia mapenzi yake kufanyika
[Picha katika ukurasa wa 302]
Yehova anafanya agano kwamba watu wake hawatapoteza kamwe pendeleo la kuwa mashahidi wake