Sura ya 8
Mungu Yumo Katika Hekalu Lake Takatifu
1, 2. (a) Nabii Isaya apata ono lake la hekalu lini? (b) Kwa nini Mfalme Uzia alipoteza upendeleo wa Yehova?
“KATIKA mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana [“Yehova,” “NW”] ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu.” (Isaya 6:1) Sura ya 6 ya kitabu cha Isaya yaanza kwa maneno hayo ya nabii huyo. Ni mwaka wa 778 K.W.K.
2 Kwa jumla, utawala wa Uzia wa miaka 52 akiwa mfalme wa Yuda ulikuwa wenye mafanikio sana. Kwa kuwa “a[li]fanya yaliyo ya adili machoni pa BWANA,” alitegemezwa na Mungu katika miradi yake ya kijeshi, ujenzi, na kilimo. Lakini mafanikio yake pia yakaja kumwangamiza. Hatimaye, moyo wake ukawa na kiburi, “akamwasi BWANA, Mungu wake; kwani aliingia hekaluni mwa BWANA, ili afukize uvumba.” Kwa sababu ya tendo hilo la kiburi na hasira kali yake juu ya makuhani waliomkosoa, Uzia alikufa mwenye ukoma. (2 Mambo ya Nyakati 26:3-22) Isaya alianza kutumikia akiwa nabii karibu wakati huo.
3. (a) Je, Isaya amwona Yehova kihalisi? Eleza. (b) Isaya aona mandhari gani, na kwa kusudi gani?
3 Hatuelezwi mahali alipo Isaya aonapo ono hilo. Lakini kwa wazi yale ayaonayo kwa macho yake halisi ni ono, wala hamwoni Mweza Yote kihalisi, kwa kuwa “hakuna mtu ambaye amemwona Mungu wakati wowote.” (Yohana 1:18; Kutoka 33:20) Ijapokuwa hivyo, bado ni jambo lenye kutisha kumwona Muumba, Yehova, hata katika ono. Aketiye katika kiti cha ufalme, kinachowakilisha daraka lake la kuwa Mfalme na Hakimu adumuye milele, ndiye Mtawala wa Ulimwengu Wote na aliye Chanzo cha utawala wote wa kiserikali wenye haki! Pindo za kanzu yake ndefu na yenye kuning’inia zalijaza hekalu. Isaya apewa wito wa kufanya utumishi wa unabii utakaotukuza nguvu kuu na haki ya Yehova. Ili kujitayarishia hilo, ataonyeshwa ono la utakatifu wa Mungu.
4. (a) Kwa nini hapana shaka kwamba ufafanuzi mbalimbali juu ya Yehova unaoonekana katika maono na kurekodiwa katika Biblia ni ufananisho? (b) Twajifunza nini juu ya Yehova kupitia ono la Isaya?
4 Isaya haelezi kuonekana kwa Yehova katika ono lake—tofauti na maono yaliyoripotiwa na Ezekieli, Danieli, na Yohana. Na masimulizi hayo yote yatofautiana juu ya mambo yanayoonekana huko mbinguni. (Ezekieli 1:26-28; Danieli 7:9, 10; Ufunuo 4:2, 3) Hata hivyo, lazima tuzingatie hali na kusudi za maono hayo. Hayo si ufafanuzi halisi wa kuwapo kwa Yehova. Jicho halisi haliwezi kuona kilicho cha kiroho, wala akili hafifu ya mwanadamu haiwezi kuelewa milki ya roho. Kwa hiyo, maono hayo yapasha habari inayopasa kuwasilishwa kwa maneno ya kibinadamu. (Linganisha Ufunuo 1:1.) Katika ono la Isaya, ufafanuzi wa sura ya Mungu si wa lazima. Ono hilo lamwarifu Isaya kuwa Yehova yumo katika hekalu lake takatifu na kwamba yeye ni mtakatifu na hukumu zake ni kamilifu.
Maserafi
5. (a) Maserafi ni nani, na jina hilo lamaanisha nini? (b) Kwa nini maserafi waficha nyuso zao na miguu yao?
5 Sikiliza! Isaya aendelea: “Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka.” (Isaya 6:2) Isaya sura ya 6 ndiyo mahali pekee katika Biblia panapotaja maserafi. Kwa wazi wao ni viumbe wa kimalaika wanaomtumikia Yehova, walio na mapendeleo ya juu sana na kuheshimiwa sana, ambao wako karibu na kiti cha ufalme cha Yehova mbinguni. Tofauti na Mfalme Uzia mwenye kiburi, wao wachukua vyeo vyao kwa unyenyekevu mno na kwa staha. Kwa sababu wako mahali alipo Mwenye Enzi Kuu wa mbinguni, wafunika nyuso zao kwa mabawa mawili; nao, kwa sababu wanapastahi mahali patakatifu, wafunika miguu yao kwa mabawa mawili mengine. Kwa kuwa wako karibu na Mwenye Enzi Kuu ya Ulimwengu Wote Mzima, maserafi hao wanyenyekea sana, ili wasikengeushe fikira kutoka kwa utukufu wa Mungu mwenyewe. Neno “maserafi,” limaanishalo “wenye moto” au “wenye kuwaka,” ladokeza kuwa wao wanang’aa, ingawa waficha nyuso zao kutoka kwa mng’ao mkubwa zaidi na utukufu wa Yehova.
6. Mahali pa maserafi pakoje kuhusiana na Yehova?
6 Maserafi hao waruka kwa mabawa mawili yaliyosalia, yamkini, kwa kuelea, au ‘kusimama,’ mahali pao. (Linganisha Kumbukumbu la Torati 31:15.) Profesa Franz Delitzsch aeleza hivi kuhusu mahali walipo: “Kwa kweli maserafi hawangeweza kuinuka juu ya kichwa cha Yule aliyeketi katika kiti cha ufalme, bali walielea juu ya kanzu Yake iliyojaza jumba.” (Commentary on the Old Testament) Yamkini jambo hilo lafaa. ‘Wanasimama juu ya,’ si wakiwa wakuu kuliko Yehova, bali kwa kumhudumia, huku wakitii na kuwa tayari kutumikia.
7. (a) Maserafi hao watimiza mgawo gani? (b) Kwa nini maserafi hao watangaza utakatifu wa Mungu mara tatu?
7 Basi, sasa wasikilize maserafi hao waliopendelewa! “Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni BWANA wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake.” (Isaya 6:3) Mgawo wao ni kuhakikisha kuwa utakatifu wa Yehova unatangazwa na utukufu wake unatambuliwa katika ulimwengu wote mzima, ambao dunia ni sehemu yake. Utukufu wake unaonekana katika vyote alivyoumba na hivi karibuni utatambuliwa na wakazi wote wa dunia. (Hesabu 14:21; Zaburi 19:1-3; Habakuki 2:14) Tangazo linalorudiwa mara tatu, “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,” si uthibitisho wa Utatu. Badala yake, utakatifu wa Mungu wakaziwa mara tatu. (Linganisha Ufunuo 4:8.) Utakatifu wa Yehova ni mkuu.
8. Ni nini latokea kufuatia matangazo ya maserafi hao?
8 Ijapokuwa idadi ya maserafi haitajwi, huenda kuna vikundi vya maserafi vilivyo karibu na kiti cha ufalme. Kwa wimbo mtamu, wao warudia mmoja baada ya mwingine lile tangazo la utakatifu na utukufu wa Mungu. Nasi twaona tokeo gani? Sikiliza tena Isaya aendeleapo: “Misingi ya vizingiti ikatikisika kwa sababu ya sauti yake aliyelia, nayo nyumba ikajaa moshi.” (Isaya 6:4) Katika Biblia, mara nyingi moshi au wingu hutoa uthibitisho wenye kuonekana wa kuwapo kwa Mungu. (Kutoka 19:18; 40:34, 35; 1 Wafalme 8:10, 11; Ufunuo 15:5-8) Huo huashiria utukufu ambao sisi wanadamu hatuwezi kukaribia.
Hastahili, Ingawa Asafishwa
9. (a) Ono hilo lamwathirije Isaya? (b) Ni tofauti gani iliyo wazi baina ya Isaya na Mfalme Uzia?
9 Ono hilo la kiti cha ufalme cha Yehova lamwathiri sana Isaya. Arekodi hivi: “Ndipo niliposema, Ole wangu! kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, BWANA wa majeshi.” (Isaya 6:5) Ni tofauti kubwa kama nini iliyopo baina ya Isaya na Mfalme Uzia! Uzia alijitwalia cheo cha ukuhani wenye kutiwa-mafuta naye akaingia kimabavu bila hofu katika Patakatifu pa hekalu. Ijapokuwa Uzia aliona vinara vya taa vya dhahabu, madhabahu ya uvumba ya dhahabu, na meza za “mkate wa Kuwapo,” yeye hakuona uso wa Yehova wenye kumpendelea wala kupokea utume wowote maalum kutoka kwake. (1 Wafalme 7:48-50; NW, kielezi-chini) Kwa upande mwingine, nabii Isaya haupuuzi ukuhani wala kuingia katika hekalu kimabavu. Ingawa hivyo, aona ono juu ya Yehova katika hekalu lake takatifu naye aheshimiwa kwa kupewa utume wa moja kwa moja kutoka kwa Mungu. Japo maserafi hawathubutu kumtazama Bwana wa hekalu aketiye katika kiti cha ufalme, Isaya aruhusiwa, katika ono, kumwona “Mfalme, BWANA [“Yehova,” NW] wa majeshi”!
10. Kwa nini Isaya aogopa sana aonapo ono hilo?
10 Tofauti anayoiona Isaya kati ya utakatifu wa Mungu na hali yake mwenyewe yenye dhambi yamfanya ahisi kuwa asiye safi hata kidogo. Akiwa na hofu nyingi afikiri kwamba atakufa. (Kutoka 33:20) Awasikia maserafi wakimsifu Mungu kwa midomo safi, ingawa midomo yake ni michafu nayo imechafuliwa hata zaidi kwa midomo ya watu anaokaa kati yao na ambao husikia usemi wao. Yehova ni mtakatifu, na watumishi wake lazima wadhihirishe sifa hiyo. (1 Petro 1:15, 16) Ijapokuwa Isaya tayari amechaguliwa kuwa msemaji wa Mungu, yeye ashtuka kwa kutambua hali yake yenye dhambi naye akosa midomo safi anayostahili msemaji wa Mfalme mtukufu na mtakatifu. Itikio mbinguni litakuwaje?
11. (a) Mmoja wa maserafi afanya nini, na tendo hilo lafananisha nini? (b) Kutafakari juu ya yale ambayo serafi amwambia Isaya kwaweza kutusaidiaje tunapohisi kutostahili tukiwa watumishi wa Mungu?
11 Badala ya kumfukuza Isaya mwenye hali ya chini kutoka mbele za kuwapo kwa Yehova, maserafi hao wamsaidia. Rekodi yataarifu: “Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu; akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa.” (Isaya 6:6, 7) Kwa njia ya ufananisho moto una nguvu ya kutakasa. Huku akitia kwenye midomo ya Isaya kaa la moto kutoka kwenye moto mtakatifu wa madhabahu, serafi huyo amhakikishia Isaya kuwa dhambi zake zimefunikwa vya kutosha kupata upendeleo na utume wa Mungu. Hilo latupatia tumaini kama nini! Sisi pia tu wenye dhambi na hatustahili kumkaribia Mungu. Lakini tumekombolewa kupitia dhabihu ya fidia yenye kustahili ya Yesu nasi twaweza kupata upendeleo wa Mungu na kumfikia katika sala.—2 Wakorintho 5:18, 21; 1 Yohana 4:10.
12. Isaya aona madhabahu gani, na moto husababisha nini?
12 Mtajo “madhabahu” watukumbusha tena kwamba hilo ni ono. (Linganisha Ufunuo 8:3; 9:13.) Ndani ya hekalu huko Yerusalemu, mlikuwemo madhabahu mawili. Kabla tu ya pazia la Patakatifu Zaidi Sana palikuwa madhabahu ndogo ya uvumba, na mbele ya mwingilio kwenye patakatifu palikuwa madhabahu kubwa ya dhabihu, ambapo moto ulikuwa ukiwaka daima. (Mambo ya Walawi 6:12, 13; 16:12, 13) Lakini madhabahu hizo za duniani zilikuwa za mfano, ziliwakilisha mambo makubwa zaidi. (Waebrania 8:5; 9:23; 10:5-10) Mfalme Solomoni alipolizindua hekalu, moto kutoka mbinguni ndio ulioteketeza matoleo ya kuteketezwa juu ya madhabahu. (2 Mambo ya Nyakati 7:1-3) Sasa pia moto kutoka katika madhabahu ya kweli, ya mbinguni, ndio unaoondoa uchafu wa midomo ya Isaya.
13. Yehova auliza swali gani, naye ahusisha nani asemapo “yetu”?
13 Basi na tusikilize pamoja na Isaya. “Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema, Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume mimi.” (Isaya 6:8) Kwa wazi, swali la Yehova limekusudiwa kujibiwa na Isaya, kwa sababu hakuna nabii mwingine wa kibinadamu aonekanaye katika ono hilo. Pasipo shaka hilo ni ombi kwa Isaya awe mjumbe wa Yehova. Lakini kwa nini Yehova auliza, “Ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu?” (Italiki ni zetu.) Kwa kubadili neno la umoja “nimtume” hadi neno la wingi “yetu,” Yehova sasa ajihusisha na angalau mtu mmoja mwingine. Nani huyo? Je, huyo siye Mwana wake mzaliwa-pekee, ambaye baadaye alikuja kuwa mwanamume Yesu Kristo? Kwa kweli, huyo ndiye Mwana yuleyule ambaye Mungu alimwambia, “Na tumfanye mtu kwa mfano wetu.” (Mwanzo 1:26; Mithali 8:30, 31) Naam, Mwana wake mzaliwa-pekee ndiye aliye katika makao ya mbinguni pamoja na Yehova.—Yohana 1:14.
14. Isaya aitikiaje ombi la Yehova, naye atuwekea kielelezo gani?
14 Isaya hasiti kuitikia! Haidhuru ni ujumbe wa aina gani, yeye ajibu kwa haraka: “Mimi hapa, nitume mimi.” Wala haulizi faida ambayo labda atapata kwa kukubali mgawo huo. Roho yake ya utayari ni kielelezo chema kwa watumishi wote wa Mungu leo, walio na utume wa kuhubiri ‘habari njema hii ya ufalme katika dunia yote inayokaliwa.’ (Mathayo 24:14) Kama vile Isaya, wao washikamana na mgawo wao kwa uaminifu nao watimiza “ushahidi kwa mataifa yote,” licha ya kutoitikia kulikoenea kotekote. Nao wasonga mbele katika tumaini, kama vile Isaya, kwa sababu wanajua kuwa utume wao umeidhinishwa na mamlaka kuu kupita zote.
Utume wa Isaya
15, 16. (a) Isaya apaswa kuwaambia nini “watu hawa,” nao wataitikiaje? (b) Je, itikio la watu hao lasababishwa na kosa fulani la Isaya? Eleza.
15 Yehova sasa atoa muhtasari wa mambo ambayo Isaya apaswa kusema na vile yatakavyopokewa: “Enenda, ukawaambie watu hawa, Fulizeni kusikia, lakini msifahamu; fulizeni kutazama, lakini msione. Uunoneshe moyo wa watu hawa, ukayatie uzito masikio yao, ukayafumbe macho yao; wasije wakaona kwa macho yao, na kusikia kwa masikio yao, na kufahamu kwa mioyo yao, na kurejea na kuponywa.” (Isaya 6:9, 10) Je, hayo yamaanisha kuwa Isaya apaswa kusema kwa kutojali na kukosa busara na kuwavunja moyo Wayahudi, hivyo awatenganishe na Yehova? Hata kidogo! Hao ni watu wa Isaya mwenyewe naye ana huruma ya kidugu kwao. Lakini maneno ya Yehova yaonyesha namna watu watakavyoupokea ujumbe wake, haidhuru ni kwa uaminifu jinsi gani Isaya atimiza kazi yake.
16 Watu ndio wenye lawama. Isaya ‘atafuliza’ kusema nao, bali hawataukubali ujumbe huo wala kupata ufahamu. Wengi wao watakuwa wakaidi na wasioitikia, kama vipofu na viziwi kabisa. Kwa kufuliza kuwaendea, Isaya atawaruhusu “watu hawa” waonyeshe kuwa hawataki kufahamu. Watathibitisha kuwa wanafunga akili na mioyo yao zisisikie ujumbe wa Isaya—ujumbe wa Mungu—kwao. Jinsi watu leo walivyo vivyo hivyo! Wengi sana kati yao hukataa kuwasikiliza Mashahidi wa Yehova wahubiripo habari njema ya Ufalme wa Mungu unaokuja.
17. Isaya arejezea nini aulizapo, “hata lini?”
17 Isaya ahangaika: “Ndipo nilipouliza, Ee Bwana, hata lini? Naye akanijibu, Hata miji itakapokuwa ukiwa, haina wenyeji, na nyumba zitakapokuwa hazina watu, na nchi hii itakapokuwa ganjo kabisa; hata BWANA atakapowahamisha watu waende mbali sana, na mahame yatakapokuwa mengi ndani ya nchi.” (Isaya 6:11, 12) Kwa kuuliza, “hata lini?” Isaya hamaanishi atawahubiria watu wasioitikia hata lini. Badala yake, awahangaikia watu naye auliza hali yao mbaya ya kiroho itaendelea hata lini na jina la Yehova litavunjiwa heshima duniani hata lini. (Ona Zaburi 74:9-11.) Hivyo basi, hali hiyo ya kipumbavu itaendelea hata lini?
18. Hali mbaya ya kiroho ya watu itaendelea hata lini, na je, Isaya ataishi hata aone utimizo kamili wa unabii huo?
18 Salala! Jibu la Yehova laonyesha kuwa hali mbaya ya kiroho ya watu hao itaendelea hata matokeo kamili ya kutomtii Mungu yatimizwe, kama yalivyotaarifiwa katika agano lake. (Mambo ya Walawi 26:21-33; Kumbukumbu la Torati 28:49-68) Taifa litaharibiwa, watu watahamishwa, na nchi itabaki ukiwa. Isaya hataishi hata aone jeshi la Wababiloni likiharibu Yerusalemu na hekalu lake mwaka wa 607 K.W.K., ingawa atatoa unabii kwa zaidi ya miaka 40, akiendelea hadi katika utawala wa Hezekia, kitukuu wa Mfalme Uzia. Ijapokuwa hivyo, Isaya atatimiza kwa uaminifu utume wake hadi afapo, zaidi ya miaka 100 kabla ya kutukia kwa msiba huo wa kitaifa.
19. Ijapo taifa hilo litakatwa kama mti, Mungu ampa Isaya uhakikisho gani?
19 Hapana shaka kwamba uharibifu utakaoifanya Yuda kuwa “ganjo kabisa” utakuja, lakini hali ni yenye tumaini fulani. (2 Wafalme 25:1-26) Yehova amhakikishia Isaya: “Ijapokuwa imebaki sehemu moja katika sehemu kumi ndani yake, italiwa hii nayo; kama mvinje na kama mwaloni, ambao shina lake limebaki, ingawa imekatwa; kadhalika mbegu takatifu ndiyo shina lake.” (Isaya 6:13) Naam, “sehemu moja katika sehemu kumi . . . mbegu takatifu,” itabaki, kama vile shina la mti mkubwa mno uliokatwa. Yamkini uhakikisho huo wamfariji Isaya—mabaki watakatifu watapatikana kati ya watu wake. Ijapo taifa hilo lachomwa kwa mara nyingine tena, kama mti mkubwa uliokatwa kwa minajili ya kuni, shina muhimu la mti wa ufananisho wa Israeli litabaki. Litakuwa mbegu, au uzao, mtakatifu kwa Yehova. Baadaye, litachipuka tena, na mti huo utakua upya.—Linganisha Ayubu 14:7-9; Danieli 4:26.
20. Sehemu ya mwisho ya unabii wa Isaya ilitimizwaje mwanzoni?
20 Je, maneno ya unabii huo yalitimia? Ndiyo. Miaka 70 baada ya nchi ya Yuda kuharibiwa, mabaki wenye kumhofu Mungu walirudi kutoka uhamishoni huko Babiloni. Walijenga upya hekalu na jiji, nao wakairudisha ibada ya kweli nchini humo. Kurudishwa huko kwa Wayahudi katika nchi yao waliyopewa na Mungu kulifanya utimizo wa pili wa unabii ambao Yehova alimpa Isaya uwezekane. Utimizo huo ulipaswa kuwa nini?—Ezra 1:1-4.
Utimizo Mbalimbali Mwingine
21-23. (a) Unabii wa Isaya katika karne ya kwanza ulitimizwa na akina nani, na jinsi gani? (b) Ni nani aliyekuwa “mbegu takatifu” katika karne ya kwanza, nayo ilihifadhiwaje?
21 Kazi ya unabii ya Isaya ilifananisha kazi ambayo Mesiya, Yesu Kristo, angefanya yapata miaka 800 baadaye. (Isaya 8:18; 61:1, 2; Luka 4:16-21; Waebrania 2:13, 14) Ingawa alikuwa mkuu kuliko Isaya, Yesu alikuwa na utayari uleule wa kutumwa na Baba yake wa mbinguni, akisema: “Tazama! Nimekuja kufanya mapenzi yako.”—Waebrania 10:5-9; Zaburi 40:6-8.
22 Kama vile Isaya, Yesu alitimiza kwa uaminifu kazi aliyopewa naye akakabili itikio lilelile. Wayahudi katika siku ya Yesu hawakuwa na nia ya kuukubali ujumbe huo kama wale aliohubiria nabii Isaya. (Isaya 1:4) Yesu alitumia vielezi katika huduma yake. Hilo liliwachochea wanafunzi wake kuuliza hivi: “Ni kwa nini wewe huwaambia kwa utumizi wa vielezi?” Yesu akajibu: “Nyinyi mmeruhusiwa kuzielewa siri takatifu za ufalme wa mbingu, lakini watu hao hawakuruhusiwa. Hii ndiyo sababu nawaambia kwa utumizi wa vielezi, kwa sababu, wakitazama, watazama bure, na wakisikia, wasikia bure, wala hawapati maana yake; na kuwaelekea wao unabii wa Isaya unapata utimizo, ambao husema, ‘Kusikia, mtasikia lakini kwa vyovyote hamtapata maana yake; na, kutazama, mtatazama lakini kwa vyovyote hamtaona. Kwa maana moyo wa watu hawa umekuwa usioitikia, na kwa masikio yao wamesikia bila itikio, nao wamefunga macho yao; ili wasipate kuona kamwe kwa macho yao na kusikia kwa masikio yao na kupata maana kwa mioyo yao na kurudi, nami niwaponye.’”—Mathayo 13:10, 11, 13-15; Marko 4:10-12; Luka 8:9, 10.
23 Kwa kunukuu kitabu cha Isaya, Yesu alikuwa akionyesha kuwa unabii huo una utimizo fulani katika siku yake. Mtazamo wa moyo wa watu kwa jumla ulikuwa kama wa Wayahudi katika siku ya Isaya. Walijifanya vipofu na viziwi wasipate ujumbe wake nao vivyo hivyo wakaharibiwa. (Mathayo 23:35-38; 24:1, 2) Hilo lilitukia wakati ambapo majeshi ya Roma yakiongozwa na Jenerali Tito yalishambulia Yerusalemu mwaka wa 70 W.K. na kulibomoa jiji hilo na hekalu lake. Ingawa hivyo, baadhi ya watu walikuwa wamemsikiliza Yesu na kuwa wanafunzi wake. Yesu aliwatangaza hao kuwa ‘wenye furaha.’ (Mathayo 13:16-23, 51) Alikuwa amewajulisha kuwa waonapo “Yerusalemu limezingirwa na majeshi yaliyopiga kambi,” yawapasa “[kuanza] kukimbia hadi kwenye milima.” (Luka 21:20-22) Kwa hiyo, “mbegu takatifu” iliyokuwa imedhihirisha imani na iliyokuwa imefanywa kuwa taifa la kiroho, “Israeli wa Mungu,” iliokolewa.a—Wagalatia 6:16.
24. Paulo alionyesha utimizo gani wa unabii wa Isaya, na jambo hilo laonyesha nini?
24 Karibu mwaka wa 60 W.K., mtume Paulo alikuwa katika kizuizi cha nyumbani huko Roma. Huko, yeye alipanga mkutano na “watu walio wakubwa wa Wayahudi” pamoja na wengine, naye akawapa “ushahidi kamili kuhusiana na ufalme wa Mungu.” Wengi wao walipokataa kukubali ujumbe wake, Paulo alieleza kuwa huo ni utimizo wa unabii wa Isaya. (Matendo 28:17-27; Isaya 6:9, 10) Kwa hiyo wanafunzi wa Yesu walitimiza utume unaofanana na ule wa Isaya.
25. Mashahidi wa Mungu leo wametambua nini, nao huitikiaje?
25 Vivyo hivyo, Mashahidi wa Yehova leo hutambua kwamba Yehova Mungu yumo katika hekalu lake takatifu. (Malaki 3:1) Kama vile Isaya, wao husema: “Mimi hapa, nitume mimi.” Wao hutangaza kwa bidii ujumbe unaotoa onyo juu ya mwisho unaokaribia wa mfumo huu wa mambo ulio mwovu. Hata hivyo, kama Yesu alivyoonyesha, ni watu wachache tu wanaofungua macho na masikio yao ili kuona na kusikia na kupata kuokolewa. (Mathayo 7:13, 14) Bila shaka, wenye furaha ni wale wanaoelekeza mioyo yao ipate kusikiliza na “kuponywa”!—Isaya 6:8, 10.
[Maelezo ya Chini]
a Mwaka wa 66 W.K., kwa sababu ya uasi wa Wayahudi, majeshi ya Roma yakiongozwa na Sesho Galo yalizingira Yerusalemu na kuingia ndani ya jiji hadi kwenye kuta za hekalu. Kisha yakaondoka, hivyo yakiwaruhusu wanafunzi wa Yesu wakimbilie kwenye milima ya Perea kabla ya Waroma kurejea mwaka wa 70 W.K.
[Picha katika ukurasa wa 94]
“Mimi hapa, nitume mimi.”
[Picha katika ukurasa wa 97]
“Hata miji itakapokuwa ukiwa, haina wenyeji”