Uzawa wa Mtoto Ulio Mkuu Zaidi Duniani Watangulia Usalama Ulimwenguni Pote
“Kwa maana kuna mtoto ambaye amezaliwa kwetu, kuna mwana ambaye tumepewa; na utawala wa mwana mfalme utakuja kuwa juu ya bega lake. Na jina lake ataitwa Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu, Baba ya Milele, Mwana Mfalme wa Amani.—Isaya 9:6, NW
1. Usalama ulimwenguni pote ni hakika chini ya nani, na tunajuaje hilo?
USALAMA ulimwenguni pote! Chini ya “Mwana Mfalme wa ulimwengu huu,” Shetani Ibilisi, ni ndoto isiyowezekana. (Yohana 12:31, The New English Bible) Lakini usalama ulimwenguni pote chini ya “Mwana Mfalme wa Amani,” Yesu Kristo, ni hakika kabisa. Yehova anatuhakikishia jambo hilo katika unabii unaohusu kuzaliwa na kazi ya “Mwana Mfalme wa Amani.” Tunasoma hivi katika Isaya 9:6, 7, NW: “Kwa maana kuna mtoto ambaye amezaliwa kwetu, kuna mwana ambaye tumepewa; na utawala wa Mwana Mfalme utakuja kuwa juu ya bega lake. Na jina lake ataitwa Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu, Baba ya Milele, Mwana Mfalme wa Amani. Kwa wingi wa utawala wa Mwana Mfalme na kwa amani hakutakuwa na mwisho, juu ya kiti cha ufalme cha Daudi na juu ya ufalme wake ili kuusimamisha kwa imara na kuuendeleza kwa njia ya haki na kwa njia ya uadilifu, kuanza sasa na mpaka wakati usiojulikana. Bidii yenyewe ya Yehova wa majeshi itafanya hilo.”
2. (a) Unabii wa Isaya 9:6, 7 ulitolewa chini ya hali gani? (b) Tunajuaje kwamba Yehova atashikamana bila kushindwa na agano alilofanya pamoja na Daudi kwa ajili ya ufalme wa milele katika ukoo wa nasaba yake?
2 Lo! ni unabii mzuri ajabu kama nini! Itasisimua kuuchunguza unabii huo juu ya uzawa wa mtoto ulio mkuu zaidi duniani. Lakini kabla ya kuweza kuthamini unabii huo kikamili, tunahitaji kukaza fikira kwenye hali ambazo chini yazo umetolewa. Ulikuwa wakati wa mpango wa kitaifa wa hila wakati wa siku za ufalme wa Yuda chini ya Mfalme Ahazi. Ingawa alikuwa asiyeaminika kwa Yehova, mfalme huyo aliruhusiwa aketi juu ya kiti cha ufalme cha Yehova. Alionyeshwa uvumilivu huo kwa sababu ya agano ambalo Yehova alikuwa amefanya pamoja na Daudi la ufalme wa milele katika nasaba yake. Ingawa Daudi alinyimwa pendeleo la kumjengea Yehova hekalu, Mungu alimpa yeye baraka tofauti. Baraka hiyo ilionyeshwa katika maneno yafuatayo ya nabii Nathani: “Tena [Yehova] anakuambia ya kwamba [Yehova] atakujengea nyumba. Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.” (2 Samweli 7:11, 16) Ahadi hiyo ya kimungu ilithibitika kuwa yenye kuridhisha sana kwa Mfalme Daudi hivi kwamba yeye alitazama mbele kwenye utimizo wayo wenye utukufu.
3. (a) Agano hilo pamoja na Daudi linapata utimizo pamoja na nani, na agano hilo lilikuwa la pekee jinsi gani? (b) Ibilisi alifanya nini kuwa mradi wake kuhusiana na agano hilo la Ufalme?
3 Agano hilo pamoja na Daudi linapata utimizo katika Mwana mkuu wa Daudi, Yesu Kristo, “Mwana Mfalme wa Amani.” Hakuna nyumba nyingine yo yote ya kifalme hapa duniani ambayo imefurahia agano kama hilo la ufalme, bila kuwa na mwisho kwa wingi wa utawala wa Mwana Mfalme wayo, bila mwisho wa amani. Lakini agano hilo la Ufalme lilitoa mwito wa ushindani kwa falme zote za ulimwengu ambazo Shetani ndiye mwana mfalme, au mtawala wazo. Basi Ibilisi pamoja na mashetani wake walifanya uwe mradi wao kujaribu kuharibu nyumba ya Daudi na hivyo wakomeshe mataraja yayo ya kuwa na mrithi mwenye kudumu. Shetani aliona wafuatao kuwa vyombo vilivyo tayari kutumiwa, Mfalme Resini wa Shamu, Mfalme Peka wa ufalme wa Israeli wa kabila kumi, na mfalme wa Ashuru.
Mpango wa Hila Dhidi ya Lile Agano la Ufalme
4. Ibilisi aliendeleaje katika jitihada zake za kukomesha utendaji wa agano la Ufalme wa Yehova lililofanywa pamoja na Daudi?
4 Mpango wa hila wa Ibilisi ulikuwa nini? Lengo lake lilikuwa kumlazimisha Mfalme Ahazi wa Yuda, kwa sababu ya woga, aingie katika muungano kwa kufanya mpango usiofaa pamoja na mfalme wa Ashuru. Ibilisi angefanyaje hivyo? Basi, alimfanya Mfalme Peka wa Israeli na Mfalme Resini wa Shamu waingie katika mpango wa hila dhidi ya nyumba ya Daudi. Walifanya mpango wa hila pamoja wa kumwondoa Ahazi kutoka kwenye kiti cha ufalme cha Yuda ili wamweke mwanamume wao, mwana wa Tabeeli, kuwa mfalme kibaraka wao. Huyu mwana wa Tabeeli alikuwa nani? Ni jambo la maana kwamba yeye hakuwa mzao wa nyumba ya Daudi. Hivyo, hakuwa mtu ambaye kwake agano la Mungu la Ufalme lingepitia mpaka lifikie Mrithi walo wa kudumu yule “Mwana Mfalme wa Amani.” Angekuwa mwanamume wao, si mwanamume wa Mungu, katika kiti cha ufalme cha Yuda. Hivyo Biblia inafunua wazi jitihada ya Shetani ya kukomesha utendaji wa agano la Ufalme wa Yehova lililofanywa pamoja na Daudi.
5, 6. Mfalme Ahazi aliitikiaje ule mpango wa hila uliofanywa dhidi ya nyumba ya Daudi, na ni ujumbe gani wenye kutia moyo aliopewa na Yehova?
5 Mfalme Ahazi aliitikiaje tisho hili? Yeye pamoja na watu wake walitetemeka sana kwa woga. Basi Yehova alimpa habari yenye kutia moyo ili amgeuze asifanye muungano wa ulinzi pamoja na mfalme wa mamlaka ya ulimwengu iliyokuwa ikiinuka, Ashuru. Yehova alimpeleka nabii wake Isaya akutane na Ahazi na kumpa ujumbe huu unaopatikana kwenye Isaya 7:4-9:
6 “Usiogope . . . kwa kuwa Shamu amekusudia mabaya juu yako, pamoja na Efraimu [mshiriki anayeongoza ufalme wa Israeli] na mwana wa Remalia [Peka], wakisema, Haya, na tupande ili kupigana na Yuda na kuwasumbua, tukabomoe mahali tupate kuingia, na kummilikisha mfalme ndani yake, huyo mwana wa Tabeeli. Bwana [Yehova] asema hivi, Neno hili halitasimama wala halitakuwa . . . kwamba hamtaki kusadiki, bila shaka hamtathibitika.”
Ishara ya Kushindwa kwa Ule Mpango wa Hila
7. (a) Ni nini kilichoongoza kwenye unabii wenye maana kubwa wa Isaya 7:14? (b) Uzawa wa Imanueli ulikuwa ishara yenye kutegemeka ya nini, nao wana wa Isaya walikuwa wakitumika kuwa nini?
7 Hivyo, Yehova alitabiri kupinduliwa kwa wananjama hao. Pindi iyo hiyo ukafika wakati wa kutolewa unabii wa kimungu wenye umaana wa kutikisa ulimwengu, kwa kuwa ulielekeza kwa Mrithi wa kifalme wa agano la Ufalme lililofanywa pamoja na Daudi. Lakini, ni nini kilichoongoza kwenye unabii huo wenye maana kubwa? Basi, Yehova alikuwa akizungumza na Mfalme Ahazi. Alimwambia Ahazi aombe ishara yo yote ya kimuujiza ambayo angefikiria, na Yehova angeifanya kama uhakikisho thabiti kwamba Mungu angevunja mpango wa hila dhidi ya nyumba ya Daudi. Lakini Ahazi alikataa kuomba ishara ya namna hiyo. Ni jambo gani lililotukia baadaye? Isaya 7:14 inatuambia hivi: “Kwa hiyo [Yehova] mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.” Jina hilo linamaanisha “Mungu Pamoja Nasi.” Kwa kuwa Imanueli pamoja na wana wawili wengine wa Isaya wangetumika kama ishara, nabii alisema hivi kwenye Isaya 8:18: “Angalieni, mimi na watoto hawa niliopewa na [Yehova] tu ishara na ajabu katika Israeli zitokazo kwa [ Yehova] wa majeshi.” Basi kuzaliwa kwa Imanueli kulikuwa ishara hakika kwamba wananjama wote pamoja na mpango wao wa hila dhidi ya agano la Ufalme wa Mungu na Mrithi wake hawangefaulu!
8. (a) Unabii kwenye lsaya7:15, 16 ulisema nini juu ya kivulana Imanueli, nayo matokeo yalikuwa nini? (b) Inaweza kuwa ni kwa sababu gani utambulisho wa Imanueli katika siku za Isaya unabaki bila uhakika?
8 Maandishi ya Biblia hayasemi ni nani aliyemzaa mwana aliyeitwa Imanueli. Huenda ikawa alikuwa bikira Myahudi aliyepata kuwa mke wa pili wa nabii Isaya. Kwa vyo vyote, unabii uliendelea kusema kwamba kabla kijana huyo hajawa na umri wa kutosha kutofautisha yaliyo mema na mabaya, wafalme wawili waliofanya mpango wa hila pamoja dhidi ya nyumba ya Daudi wangefikia mwisho wenye msiba. (Isaya 7:15, 16) Jambo hilo lilithibitika kuwa kweli. Uhakika wa kwamba utambulisho wa Imanueli katika siku za Isaya unaendelea kuwa bila uhakika kwetu yaweza kuwa ni kwa kusudi la kutokengeua fikira za vizazi vijavyo kutoka kwa Imanueli Mkubwa Zaidi wakati angetokea akiwa ishara ya kimuujiza kutoka mbinguni.
9. (a) Kutimizwa kwa ishara hiyo na kupinduliwa kwa mpango wa hila dhidi ya agano la Ufalme kulihakikisha nini? (b) Ni nini mpango wa hila wa ulimwengu wote ulio mkubwa zaidi ya yote uliopata kufanywa wakati wo wote?
9 Bila shaka, katika siku za Ahazi, kulikuwa na utimizo mdogo tu wa ishara na wa kupinduliwa kwa mpango wa hila wa ulimwengu dhidi ya agano la Mungu la Ufalme. Hata hivyo utimizo huo wa kwanza ulitoa uthibitisho wa kwamba ishara na mapinduzi ya mpango wa hila wa ulimwengu ungetimizwa kwa njia yenye maana kubwa katika wakati wetu wenye hatari. Leo tunakabiliana macho kwa macho na mpango wa hila wa ulimwengu wote ulio mkubwa zaidi ya wote uliopata kufanywa wakati wo wote. Katika maana gani? Katika maana ya kwamba mataifa yanapuuza kabisa mpango wa Yehova wa kuleta amani yenye kudumu, na hata yanapinga wajumbe wa “Mwana Mfalme wa Amani.” Mpango huo wa hila kwa kweli ni dhidi ya Mrithi wa agano la Ufalme, yule “Mwana Mfalme wa Amani.” Sasa, basi, namna gani kuhusu utimizo kamili wa unabii huu? Tukiifahamu ishara, basi tutathamini ya kwamba matokeo ya mwisho yatakayoupata mpango wa hila wa ulimwengu yamekwisha katwa.
Uzawa wa Yule “Mwana Mfalme wa Amani”
10. (a) Katika utimizo kamili wa Isaya 7:14, ni nani aliyetokeza mtoto akiwa ishara na Mrithi wa agano la Ufalme? (b) Mwanahistoria Mathayo anahusianishaje ishara ya Imanueli na nyumba ya Daudi?
10 Katika utimizo kamili wa unabii huo, bikira aliyemzaa mwana kama ishara na Mrithi wa agano la Ufalme alikuwa Mariamu, bikira Myahudi wa ukoo wa Mfalme Daudi. Malaika Gabrieli alimwambia kwamba angemzaa mwana ambaye angeitwa Yesu, na kwamba Yehova Mungu “atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake,” na kwamba “ufalme wake utakuwa hauna mwisho.” (Luka 1:26-33) Mathayo mwanahistoria aliyeongozwa na Mungu anahusianisha ishara ya Imanueli pamoja na nyumba ya Daudi. Tunasoma hivi kwenye Mathayo 1: 20-23: “Malaika wa [Yehova] alimtokea [Yusufu] katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa roho [takatifu]. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na [Yehova] kwa ujumbe wa nabii akisema, Tazama, bikira atachukua mimba, naye atazaa mwana; nao watamwita jina lake Imanueli; yaani, Mungu pamoja nasi.”
11. Uzawa uliotabiriwa wa Imanueli ulitukia wapi na lini?
11 Kuzaliwa huku kwa Imanueli kulikota-biriwa kulitukia wapi na lini? Macho yote ya Wayahudi yalielekezwa upande uliofaa na maneno ya Mika 5:2, yanayoelezwa kwenye Mathayo 2:6: “Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; kwa kuwa kwako atatoka mtawala atakayewachunga watu wangu Isra-eli.” Ilikuwa katika mwaka wa 2 K.W.K. katika mji wa Bethlehemu kwamba “Mwana Mfalme wa Amani” alizaliwa, na unabii wenye kusisimua wa Isaya 9:6, 7 ukaanza kutimizwa.
12, 13. Uzawa wa “Mwana Mfalme wa Amani” uliletea nani heshima kubwa, na uzawa huo ulikuwa pamoja na wonyesho gani wenye utukufu na wenye kustaajabisha?
12 Ni nani kati yetu asingeiona kuwa heshima na furaha kuwa mzazi wa yule ambaye angekuwa na cheo “Mwana Mfalme wa Amani”? Basi, jambo hilo lilimletea utukufu mkuu Baba wa kifalme wa huyu Mwana Mfalme. Kwa kweli, hasha, la hasha, Tiapana wakati mwingine wo wote uliotangulia ambapo uzawa wa kibinadamu umepata kuwa pamoja na wonyesho wenye utukufu na wenye kustaajabisha sana hivyo.
13 Malaika wa Yehova mwenye kung’aa aliwatokea wachungaji waliokuwa wakilinda makundi yao usiku makondeni nje ya Bethlehemu, na “utukufu wa (Yehova] ukawang’aria pande zote.” Halafu malaika akatangaza uzawa huo kwa kutimiza unabii wa kimungu, akisema: “Maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.” Kana kwamba jambo hilo halikuwa tukufu vya kutosha, kukatokea katika mbingu juu jeshi.la malaika wakimsifu Baba ya mwana huyo aliyezaliwa na kusema kana kwamba kwa sauti moja: “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.” Inafaa jinsi gani malaika kutangaza wakati wa uzawa wa yule aliyekusudiwa kuwa “Mwana Mfalme wa Amani” kwamba kungekuwako amani ya kimungu kwa wote ambao wana nia njema ya Mungu!—Luka 2:8-14.
14, 15. (a) Ni juu ya matukio gani wana wa kimbungu wa Mungu walimsifu Yehova? (b) Ni kwa sababu gani hakuna uzawa wa mtoto mwingine katika historia yote ya kibinadamu ungelingana na huo?
14 Muda mrefu kabla ya uzawa wa yeye ambaye angekuwa “Mwana Mfalme wa Amani,” malaika walikuwa wamemsifu Mungu katika pindi ya pekee. Huo ulikuwa wakati ambapo katika uumbaji, aliiweka misingi ya dunia. (Ayubu 38:4) Je! wewe umeona picha za dunia yetu ambazo zimechukuliwa na wasafiri wa anga za juu? Basi uliona jambo ambalo ni malaika tu waliokuwa wameona mpaka kufikia nyakati za karibuni. Na malaika waliitikiaje? Ayubu 38:7 hutuambia hivi: “Hapo nyota za asubuhi zilipoimba pamoja, na wana wote wa Mungu walipopiga kelele kwa furaha.”
15 Uzawa ulio mkuu zaidi uliopata kuiheshimu dunia hungekuwa tukio dogo ambalo kwa sababu yalo wana wa Mungu wangeunganisha sauti zao kwa wimbo wa sifa. Kama vile baba ya kidunia anavyopongezwa kwa uzawa wa mwana wake mzaliwa wa kwanza, vivyo hivyo Baba wa kimbingu aliyekuwa na daraka kwa uzawa huo mkuu zaidi uliopata kutukia duniani anastahili kutukuzwa katika nyimbo na washiriki wa jamaa yake ya kimbingu. Kikundi hicho cha waimbaji kizuri mno lazima kiwe kilimfurahisha Mtu wa kimungu kama nini kwa yeye kuwa baba kwa mara ya kwanza katika hali mpya kabisa! Hakuna wakati wo wote uliotangulia katika historia ya ulimwengu wote ambapo kumepata kuwa na uzawa wa mtoto unaoweza kulingana na ule wa yule aliyekusudiwa kuwa “Mwana Mfalme wa Amani.”
“Nuru Kuu” Yang’aa
16.Ni lini na jinsi gani kulikuwako utimizo zaidi wa Isaya sura ya 9?
16 Yesu alipoanza huduma yake ya hadharani, kulikuwako utimizo zaidi wa Isaya sura ya 9. Hii ilihusiana na mistari yake miwili ya kwanza, iliyotabiri kwamba “nuru kuu” ingeng’aa kwa watu “waliokwenda katika giza.” Tunaelezwa utimizo wa mistari hiyo na Mathayo mwanahistoria aliyeongozwa na Mungu kwenye sura ya 4, mistari 13 hadi 17: “[Yesu akatoka Nazareti, akaja akakaa Kapernaumu, mji ulioko pwani, mipakani mwa Zabuloni na Naftali: ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, Njia ya bahari, ng’ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa, Watu wale waliokaa katika giza wameona mwanga mkuu, Nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti Mwanga umewazukia. Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.”
17. Ni kwa sababu gani Yesu angewezesha nuru ing’ae juu ya watu katika Zabuloni na Naftali, na nuru hiyo ingemaanisha nini kwa watu waliokaa katika giza?
17 Zabuloni na Naftali zilikuwa upande wa mwisho wa kaskazini mwa Israeli na zilitia ndani wilaya ya Galilaya. Naftali ilikuwa mpakani mwa pwani yote ya magharibi mwa Bahari ya Galilaya. Kwa hiyo, kuhubiri kwa Yesu pamoja na wanafunzi wake habari njema za Ufalme wa Mungu katika sehemu hizo ndiko kulikofanya nuru ing’ae kwa watu ambao walikuwa wameketi gizani kwa muda mrefu. Yesu alisema hivi katika Yohana 8:12: “Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.” Kwa hiyo, kupitia kwa Yesu wale “waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti” waliwezeshwa kuwa na “nuru ya uzima” kwa kuwa alitoa uhai wake “uwe fidia ya wengi.” Yeye ndiye aliyetumiwa na Yehova kutoa nuru juu ya njia ambayo kwayo watu wangepata uzima.—Mathayo 4:23; 20:28.
18. (a) Ni kwa sababu gani hii “nuru kuu” haingekuwa ya watu wa Galilaya peke yao? (b) Ni nini kitakachozungumziwa katika makala inayofuata?
18 “Mwanga mkuu” huu unaotoa ukombozi kutoka katika kifo na udhalimu haukuwa kwa ajili ya watu wa Galilaya peke yao. Je! Isaya hakutabiri kwamba wingi wa serikali hiyo haungekuwa na mwisho? Na je! Isaya hakutabiri kwamba daraka la “MwanaMfalme wa Amani” lingekuwa kubwa mno? Ndiyo, kwa kuwa Isaya 9:6, 7, NW husema hivi: “Na jina lake ataitwa, Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu, Baba ya Milele, Mwana Mfalme wa Amani. Kwa wingi wa utawala wa Mwana Mfalme na kwa amani hakutakuwa na mwisho.” Katika makala itakayofuata, tutazungumzia daraka la Yesu Kristo akiwa “Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu, Baba ya Milele,” pamoja na “Mwana Mfalme wa Amani’’.
Wewe Unakumbuka—
◻ Ni mpango gani wa hila uliotokea katika siku za Mfalme Ahazi?
◻ Ni nini uliokuwa utimizo mdogo wa ishara ya Isaya7:14?
◻ Ni nini uliokuwa utimizo kamili wa ishara hiyo?
◻ Ni kwa sababu gani uzawa wa “Mwana Mfalme wa Amani” ulikuwa ndio uzawa wa mtoto ulio mkuu zaidi duniani?