Sura ya 9
Mtumaini Yehova Ukabilipo Janga
1. Kwa nini Wakristo leo watanufaika kwa kuchunguza Isaya sura ya 7 na ya 8?
ISAYA sura ya 7 na ya 8 zafunua mambo mawili tofauti-tofauti. Isaya na Ahazi walikuwa raia wa taifa lililo wakfu kwa Yehova; Mungu aliwapa wote wawili migawo, mmoja akawa nabii, na mwingine akawa mfalme wa Yuda; na wote walikabili tisho lilelile—uvamizi wa Yuda uliofanywa na majeshi ya adui yenye nguvu zaidi. Hata hivyo, Isaya alikabili tisho hilo akimtumaini Yehova, ilhali Ahazi alishikwa na hofu. Mbona wakatofautiana? Kwa sababu Wakristo leo vilevile wamezingirwa na majeshi yenye uhasama, yafaa wachunguze sura hizo mbili za Isaya ili wajue mafundisho yaliyomo.
Kukabili Uamuzi
2, 3. Isaya atoa muhtasari gani katika maelezo yake ya mwanzoni?
2 Kama vile msanii achoraye picha mpya kwa kutumia mistari mikubwa michache tu, vivyo hivyo Isaya aanza masimulizi yake kwa taarifa chache za jumla zinazoonyesha mwanzo na mwisho wa matukio anayokaribia kusimulia: “Ikawa katika siku za Ahazi, mwana wa Yothamu, mwana wa Uzia, mfalme wa Yuda, Resini, mfalme wa Shamu [“Siria,” “NW”], na Peka, mwana wa Remalia, mfalme wa Israeli, wakapanda wakaenda Yerusalemu ili kupigana nao, lakini hawakuweza kuushinda.”—Isaya 7:1.
3 Ni karne ya nane K.W.K. Ahazi amekuwa mfalme juu ya Yuda kwa kumrithi Yothamu babake. Resini, mfalme wa Siria, na Peka, mfalme wa ufalme wa kaskazini wa Israeli, wavamia Yuda, na majeshi yao yashambulia vikali. Hatimaye, watazingira Yerusalemu. Hata hivyo, mazingiwa hayo hayatafua dafu. (2 Wafalme 16:5, 6; 2 Mambo ya Nyakati 28:5-8) Kwa nini? Tutajifunza hayo baadaye.
4. Kwa nini moyo wa Ahazi na mioyo ya watu wake imejaa hofu?
4 Mwanzoni mwa vita, “watu wa nyumba ya Daudi wa[li]ambiwa kwamba Shamu [“Siria,” “NW”] wamefanya mapatano na Efraimu. Na moyo wake ukataharuki, na moyo wa watu wake, kama miti ya mwituni itikiswavyo na upepo.” (Isaya 7:2) Naam, Ahazi na watu wake watishika kusikia kuwa Wasiria na Waisraeli wameungana na kwamba majeshi yao sasa yamepiga kambi Efraimu (Israeli). Pale walipo ni mwendo wa siku mbili au tatu tu kutoka Yerusalemu!
5. Watu wa Mungu leo wafananaje na Isaya?
5 Yehova amwambia Isaya: “Haya, toka, umlaki Ahazi, wewe na Shear-yashubu mwana wako, huko mwisho wa mfereji wa birika la juu, katika njia kuu ya uwanja wa dobi.” (Isaya 7:3) Hebu wazia! Badala ya mfalme kwenda kumtafuta nabii wa Yehova na kuomba mwongozo wake, nabii apaswa kwenda kumtafuta mfalme! Ijapokuwa hivyo, Isaya amtii Yehova kwa utayari. Vivyo hivyo, watu wa Mungu leo huenda kwa utayari kuwatafuta watu waliojawa hofu kwa sababu ya misongo ya ulimwengu huu. (Mathayo 24:6, 14) Yaridhisha kama nini kwamba mamia ya maelfu kila mwaka wanaitikia ziara za wahubiri wa habari njema na kuushika mkono wenye kinga wa Yehova!
6. (a) Nabii ampasha Mfalme Ahazi ujumbe gani wenye kutia moyo? (b) Ni hali gani iliyopo leo?
6 Isaya amkuta Ahazi nje ya kuta za Yerusalemu, ambapo mfalme anakagua mifereji ya maji ya jiji, akijitayarishia mazingiwa yanayotarajiwa. Isaya ampasha ujumbe wa Yehova: “Angalia, ukatulie; usiogope wala usife moyo, kwa sababu ya mikia hii miwili ya vinga hivi vitokavyo moshi; kwa sababu ya hasira kali ya Resini na Shamu, na mwana wa Remalia.” (Isaya 7:4) Washambuliaji hao walipoharibu Yuda hapo mwanzoni, hasira yao ilikuwa kali kama moto. Sasa wao ni ‘mikia miwili ya vinga vitokavyo moshi’ tu. Ahazi hana haja ya kuogopa Mfalme Resini wa Siria wala Mfalme Peka wa Israeli, mwana wa Remalia. Leo hali iko hivyo. Viongozi wa Jumuiya ya Wakristo wamewanyanyasa vikali Wakristo wa kweli kwa karne nyingi. Hata hivyo, Jumuiya ya Wakristo sasa yafanana na vinga vilivyochomeka karibu kwisha. Siku zake zimeyoyoma.
7. Kwa nini jina la Isaya na la mwanaye yatumainisha?
7 Katika siku ya Ahazi, ujumbe wa Isaya, maana ya jina la Isaya na pia maana ya jina la mwanawe zawatumainisha wale wanaomtumaini Yehova. Pasipo shaka Yuda imo hatarini, lakini jina Isaya, limaanishalo “Wokovu wa Yehova,” huashiria kwamba Yehova atawakomboa. Yehova amwambia Isaya aandamane na Shear-yashubu mwanawe, ambaye jina lake lamaanisha “Mabaki Wachache Tu Ndio Watakaorudi.” Hata ufalme wa Yuda uangukapo hatimaye, Mungu atawarudisha mabaki kwa rehema kwenye nchi hiyo.
Si Vita Tu Kati ya Mataifa
8. Kwa nini shambulio dhidi ya Yerusalemu lahusisha mengi zaidi kuliko vita kati ya mataifa?
8 Yehova, kupitia Isaya, afunua mbinu ya adui za Yuda. Wanapanga mambo haya: “Haya, na tupande ili kupigana na Yuda na kuwasumbua, tukabomoe mahali tupate kuingia, na kummilikisha mfalme ndani yake, huyo mwana wa Tabeeli.” (Isaya 7:5, 6) Muungano wa Siria na Israeli wapanga kuvamia Yuda na kumwondoa Ahazi, mwana wa Daudi, na badala yake wamtawaze mtu wao. Kwa wazi, shambulio dhidi ya Yerusalemu sasa lahusisha mengi zaidi kuliko vita tu kati ya mataifa. Sasa ni pambano kati ya Shetani na Yehova. Kwa nini? Kwa sababu Yehova Mungu alifanya agano na Mfalme Daudi, hivyo akamhakikishia kwamba wanawe wangewatawala watu wa Yehova. (2 Samweli 7:11, 16) Shetani angepata ushindi ulioje iwapo angeweza kutawaza nasaba nyingine ya kifalme kwenye kiti cha ufalme huko Yerusalemu! Huenda hata akabatilisha kusudi la Yehova kuhusu kutokea kwa mrithi wa kudumu, ‘Mkuu wa Amani,’ katika nasaba ya Daudi.—Isaya 9:6, 7, linganisha NW.
Uhakikisho wa Yehova Wenye Upendo
9. Ni uhakikisho gani mbalimbali unaopasa kumtia moyo Ahazi na vilevile Wakristo leo?
9 Je, hila ya Siria na Israeli itafanikiwa? La. Yehova atangaza: “Neno hili halitasimama wala halitakuwa.” (Isaya 7:7) Yehova asema kupitia Isaya kwamba mazingiwa hayo ya Yerusalemu yatashindwa na pia “katika muda wa miaka sitini na mitano Efraimu atavunjika vipande vipande, asiwe kabila ya watu tena.” (Isaya 7:8) Naam, katika muda wa miaka 65 Israeli haitakuwapo tena ikiwa kabila ya watu.a Uhakikisho huo, wenye ratiba hususa ya wakati, wapasa kumtia moyo Ahazi. Vivyo hivyo, watu wa Mungu leo hutiwa nguvu kwa kujua ya kwamba wakati uliobaki wa ulimwengu wa Shetani unaisha.
10. (a) Wakristo wa kweli leo waweza kumwigaje Yehova? (b) Yehova amwomba Ahazi afanye nini?
10 Labda sura ya Ahazi yaonyesha shaka, kwa kuwa Yehova asema hivi kupitia Isaya: “Kwamba hamtaki kusadiki, bila shaka hamtathibitika.” Kwa subira, Yehova “akasema [“akaendelea kusema,” “NW”] na Ahazi.” (Isaya 7:9, 10) Ni kielelezo chema kama nini! Leo, ijapokuwa wengi hawaitikii haraka ujumbe wa Ufalme, ni vema tumwige Yehova kwa ‘kuendelea kusema’ tuzurupo tena na tena. Kisha Yehova amwambia Ahazi: “Jitakie ishara ya BWANA, Mungu wako; itake katika mahali palipo chini sana, au katika mahali palipo juu sana.” (Isaya 7:11) Ahazi aweza kuomba ishara, na Yehova ataifanya iwe uhakikisho kwamba atailinda nyumba ya Daudi.
11. Yehova ahakikisha nini asemapo ‘Mungu wako’?
11 Ona kwamba Yehova asema: ‘Jitakie ishara ya Mungu wako.’ Yehova ni mwenye fadhili kwelikweli. Tayari imeripotiwa kwamba Ahazi anaabudu miungu isiyo ya kweli na kufuata mazoea ya kipagani yenye kuchukiza. (2 Wafalme 16:3, 4) Licha ya hayo na licha ya mtazamo wa Ahazi wenye hofu, Yehova bado asema kuwa yeye ni Mungu wa Ahazi. Hilo latuhakikishia kuwa Yehova hawakatai wanadamu haraka-haraka. Ana nia ya kuwasaidia wale wanaokosea au wale ambao imani yao imekuwa dhaifu. Je, uhakikisho huo wenye upendo wa Mungu utamchochea Ahazi aukubali msaada wa Yehova?
Baada ya Shaka Sasa Ni Kutotii
12. (a) hazi aamua kuwa na mtazamo gani wenye kiburi? (b) Badala ya kumgeukia Yehova, Ahazi atafuta msaada kutoka kwa nani?
12 Ahazi ajibu kwa ukaidi: “Sitaitaka, wala sitamjaribu BWANA.” (Isaya 7:12) Haimaanishi kwamba Ahazi anatii maneno ya sheria: “Msimjaribu BWANA, Mungu wenu.” (Kumbukumbu la Torati 6:16) Karne kadhaa baadaye, Yesu ainukuu sheria hiyohiyo Shetani anapomshawishi. (Mathayo 4:7) Ingawa hivyo, kwa habari ya Ahazi, Yehova anamwomba airudie ibada ya kweli naye ajitolea kuimarisha imani yake kwa kufanya ishara. Ijapokuwa hivyo, Ahazi aamua kutafuta ulinzi kwingineko. Labda wakati huo ndipo mfalme atuma pesa nyingi huko Ashuru, ili asaidiwe kupambana na adui zake wa upande wa kaskazini. (2 Wafalme 16:7, 8) Wakati huohuo, jeshi la muungano wa Siria na Israeli lazunguka Yerusalemu na kulizingira.
13. waona badiliko gani katika mstari wa 13, nalo laashiria nini?
13 Akiwa bado anafikiria juu ya ukosefu wa imani wa mfalme, Isaya asema: “Sikilizeni sasa, enyi nyumba ya Daudi; Je! ni neno dogo kwenu kuwachosha wanadamu, hata mkataka kumchosha Mungu wangu pia?” (Isaya 7:13) Naam, ukaidi wa daima waweza kumchosha Yehova. Ona pia kwamba sasa nabii asema “Mungu wangu,” wala si “Mungu wako.” (Italiki ni zetu.) Badiliko hilo laashiria mabaya! Ahazi anapomkataa Yehova na kugeukia Ashuru, apoteza nafasi nzuri ya kurudisha uhusiano wake na Mungu. Na tusiharibu kamwe uhusiano wetu na Mungu kwa kuhatarisha itikadi zetu za Kimaandiko kwa ajili ya faida za muda mfupi.
Ishara ya Imanueli
14. ehova aonyeshaje uaminifu wake kwa agano lake na Daudi?
14 Yehova abaki mwaminifu kwa agano lake na Daudi. Ishara ilipendekezwa, nayo itatolewa! Isaya aendelea: “Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli. Siagi na asali atakula, wakati ajuapo kuyakataa mabaya na kuyachagua mema. Kwa maana kabla mtoto huyo hajajua kuyakataa mabaya na kuyachagua mema, nchi ile, ambayo wewe unawachukia wafalme wake wawili, itaachwa ukiwa.”—Isaya 7:14-16.
15. nabii uhusuo Imanueli wajibu maswali gani mawili?
15 Kuna habari njema kwa yeyote anayehofia kwamba wavamizi wataikomesha nasaba ya wafalme ya Daudi. Jina “Imanueli” lamaanisha “Pamoja Nasi Yuko Mungu.” Mungu yuko na Yuda naye hataruhusu agano Lake na Daudi libatilishwe. Kwa kuongeza, Ahazi na watu wake waelezwa yale atakayofanya Yehova na wakati ambapo atayafanya. Kabla mvulana Imanueli hajawa na umri wa kutosha kutofautisha mema na mabaya, mataifa adui yataharibiwa. Na hilo latokea kweli!
16. abda ni kwa nini Yehova hakumtambulisha Imanueli katika siku ya Ahazi?
16 Biblia haisemi Imanueli ni mwana wa nani. Ingawa hivyo, kwa kuwa mtoto Imanueli apaswa kuwa ishara na baadaye Isaya ataarifu kwamba yeye na watoto wake ni “ishara,” huenda Imanueli ni mwana wa nabii huyo. (Isaya 8:18) Labda Yehova akosa kumtambulisha Imanueli katika siku ya Ahazi ili asikengeushe vizazi vya baadaye kutoka kwa Imanueli Mkuu. Ni nani huyo?
17. a) manueli Mkuu zaidi ni nani, na kuzaliwa kwake kuliashiria nini? (b) Kwa nini watu wa Mungu waweza kupaaza sauti leo, “Pamoja nasi yuko Mungu”?
17 Mbali na kitabu cha Isaya, jina Imanueli lapatikana mara moja tu katika Biblia, kwenye Mathayo 1:23. Yehova alimpulizia Mathayo auhusishe unabii wa kuzaliwa kwa Imanueli na kuzaliwa kwa Yesu, Mrithi mwenye haki wa kiti cha ufalme cha Daudi. (Mathayo 1:18-23) Kuzaliwa kwa Imanueli wa kwanza kulikuwa ishara ya kwamba Mungu hakuiacha nyumba ya Daudi. Hali kadhalika, kuzaliwa kwa Yesu, Imanueli Mkuu, kulikuwa ishara ya kwamba Mungu hakuwaacha wanadamu wala agano lake la Ufalme na nyumba ya Daudi. (Luka 1:31-33) Huku mwakilishi mkuu wa Yehova akiwa miongoni mwa wanadamu, Mathayo angeweza kusema kwa dhati, ‘Pamoja nasi yuko Mungu.’ Leo, Yesu ni Mfalme anayetawala mbinguni naye yuko pamoja na kutaniko lake duniani. (Mathayo 28:20) Naam, watu wa Mungu wana sababu zaidi ya kupaaza sauti kwa ujasiri: “Pamoja Nasi Yuko Mungu!”
Matokeo Zaidi ya Ukosefu wa Uaminifu
18.(a) wa nini maneno ya Isaya yanayofuata yawaogofya mno wanaomsikiliza? (b) Ni badiliko gani liko karibu kutokea?
18 Ingawa maneno yake ya karibuni zaidi yafariji, taarifa ifuatayo ya Isaya yawaogofya wanaomsikiliza: “BWANA ataleta juu yako, na juu ya watu wako, na juu ya nyumba ya baba yako, siku zisizokuja bado, tangu siku ile aliyoondoka Efraimu kutoka katika Yuda; yaani, mfalme wa Ashuru.” (Isaya 7:17) Naam, msiba unakuja, kwa mkono wa mfalme wa Ashuru. Tazamio la kutawaliwa na Waashuri wakatili mno hapana budi lamfanya Ahazi na watu wake wakose usingizi kwa siku nyingi. Ahazi amefikiri kwamba kufanya urafiki na Ashuru kutamwokoa mkononi mwa Israeli na Siria. Naam, hatimaye mfalme wa Ashuru ataitikia ombi la Ahazi na kushambulia Israeli na Siria. (2 Wafalme 16:9) Labda hiyo ndiyo sababu Peka na Resini watalazimika kuacha kuzingira Yerusalemu. Hivyo, muungano wa Siria na Israeli hautaweza kutwaa Yerusalemu. (Isaya 7:1) Ingawa hivyo, Isaya sasa awaambia wasikilizaji wake walioshtuka kwamba Ashuru, wanayotarajia iwalinde, itakuwa mkandamizaji wao!—Linganisha Mithali 29:25.
19. Tukio hili la kihistoria lina onyo gani kwa Wakristo leo?
19 Masimulizi hayo ya kweli na ya kihistoria yana onyo kwa Wakristo leo. Tusongwapo, huenda tukashawishiwa kuridhiana kanuni za Kikristo, na kuukataa ulinzi wa Yehova. Kufanya hivyo ni kukosa busara, ni kama kujiua, kama inavyokuja kudhihirika kwa maneno zaidi ya Isaya. Nabii aendelea kufafanua jinsi ambavyo uvamizi wa Ashuru utaifanya nchi na watu wake.
20. “Inzi” na “nyuki” ni nani, nao watafanya nini?
20 Isaya agawa matangazo yake katika sehemu nne, kila moja likitabiri yatakayotendeka “katika siku hiyo”—yaani, siku ambapo Ashuru yashambulia Yuda. “Itakuwa katika siku hiyo BWANA atampigia kelele inzi aliye katika pande za mwisho za mito ya Misri, na nyuki aliye katika nchi ya Ashuru nao watakuja na kutulia katika mabonde yaliyo ukiwa, na katika pango za majabali, na juu ya michongoma yote, na juu ya malisho yote.” (Isaya 7:18, 19) Majeshi ya Misri na Ashuru, mfano wa mabumba ya inzi na nyuki, yatakaza fikira zao kwenye Bara Lililoahidiwa. Huo hautakuwa uvamizi wa muda mfupi. “Inzi” na “nyuki” watatulia na kuingia katika kila pembe ya nchi.
21. Mfalme wa Ashuru atakuwaje kama wembe?
21 Isaya aendelea: “Katika siku hiyo Bwana atanyoa kichwa na malaika ya miguuni, kwa wembe ulioajiriwa pande za ng’ambo ya Mto, yaani, kwa mfalme wa Ashuru, nao utazimaliza ndevu nazo.” (Isaya 7:20) Sasa inayotajwa ni Ashuru pekee, iliyo tisho kuu. Ahazi amwajiri mfalme wa Ashuru ‘anyoe’ Siria na Israeli. Hata hivyo, “wembe ulioajiriwa” kutoka eneo la Frati utakinyoa kabisa “kichwa” cha Yuda, na hata kuziondoa ndevu!
22. Isaya atumia vielelezo gani ili kuonyesha matokeo ya uvamizi wa Ashuru unaokaribia?
22 Matokeo yatakuwa nini? “Katika siku hiyo itakuwa ya kwamba mtu atalisha ng’ombe mke mchanga na kondoo wake wawili; kisha itakuwa, kwa sababu wanyama hao watatoa maziwa mengi, atakula siagi; kwa maana kila mtu aliyesalia katika nchi hii atakula siagi na asali.” (Isaya 7:21, 22) Waashuri watakapokuwa ‘wameinyoa’ nchi hiyo, ni watu wachache sana watakaobaki hivi kwamba ni mifugo michache tu itakayohitajika kwa chakula. “Siagi na asali” zitaliwa—hakuna kitu kingine chochote, hakuna divai, wala mkate, wala mazao makuu mengineyo. Kana kwamba ni kukazia kadiri ya ukiwa, Isaya asema mara tatu kwamba mahali palipokuwa nchi nzuri, penye kuzaa sana, sasa patakuwa mahali pa mibigili na miiba. Waendao mashambani watahitaji “mishale na upinde” kwa kujilinda dhidi ya wanyama wa mwituni wanaootea vichakani. Mashamba yaliyofyekwa yatakuwa mahali pa kukanyagwa na ng’ombe na kondoo. (Isaya 7:23-25) Unabii huo waanza kutimizwa katika siku ya Ahazi mwenyewe.—2 Mambo ya Nyakati 28:20.
Matabiri Sahihi
23. (a) Isaya sasa aamuriwa afanye nini? (b) Ishara kwenye ubao yathibitishwaje?
23 Sasa Isaya airudia hali iliyopo. Yerusalemu likiwa lingali limezingirwa na muungano wa Siria na Israeli, Isaya aripoti: “BWANA akaniambia, Ujipatie ubao mkubwa ukaandike juu yake kwa kalamu ya binadamu, Kwa Maher-shalal-hash-bazi; nami nitajipatia mashahidi waaminifu ili kuandika habari, yaani, Uria, kuhani, na Zekaria, mwana wa Yeberekia.” (Isaya 8:1, 2) Jina Maher-shalal-hash-bazi lamaanisha “Fanya Hima, Ewe Nyara! Amekuja Upesi Kwenye Nyara.” Isaya awaomba wanaume wawili wanaoheshimiwa katika jumuiya washuhudie aandikapo jina lake kwenye ubao mkubwa, ili kwamba baadaye waweze kuthibitisha uasilia wa hati hiyo. Hata hivyo, ishara hiyo itathibitishwa na ishara ya pili.
24. Ishara ya Maher-shalal-hash-bazi yapasa kuwaathirije watu wa Yuda?
24 Isaya asema: “Nami nikamwendea huyo nabii mke, naye akapata mimba, akazaa mtoto mwanamume. Kisha BWANA akaniambia, Mwite jina lake Maher-shalal-hash-bazi. Kwa maana kabla mtoto huyo hajapata kujua kusema, Baba yangu, na Mama yangu, hazina za Dameski na mateka ya Samaria yatachukuliwa mbele ya mfalme wa Ashuru.” (Isaya 8:3, 4) Ubao huo mkubwa na mvulana aliyezaliwa hivi punde zitakuwa ishara kwamba karibuni Ashuru itawapora wakandamizaji wa Yuda, yaani, Siria na Israeli. Karibuni kadiri gani? Kabla mvulana huyo hajaweza kutamka maneno ambayo vitoto vingi hujifunza kwanza—“Baba” na “Mama.” Utabiri barabara kama huo wapasa kuimarisha imani ya watu katika Yehova. Au labda utawafanya wengine wamdhihaki Isaya na wanawe. Hata iweje, maneno ya unabii wa Isaya yatimia.—2 Wafalme 17:1-6.
25. Siku za Isaya zafananaje na wakati wetu?
25 Maonyo yaliyorudiwa-rudiwa ya Isaya yaweza kuwafundisha Wakristo. Mtume Paulo alitufunulia kwamba katika tukio hilo la kihistoria, Isaya alifananisha Yesu Kristo na wana wa Isaya wakafananisha wanafunzi watiwa-mafuta wa Yesu. (Waebrania 2:10-13) Yesu, kupitia wafuasi wake watiwa-mafuta duniani, amekuwa akiwakumbusha Wakristo wa kweli uhitaji wa ‘kufuliza kuwa macho’ katika nyakati hizi zenye hatari. (Luka 21:34-36) Na wakati huohuo, wapinzani wasiotubu wanaonywa juu ya kuharibiwa kwao kunakokuja, ijapo mara nyingi maonyo hayo hudhihakiwa. (2 Petro 3:3, 4) Utimizo wa unabii mbalimbali uhusuo wakati katika siku ya Isaya wahakikisha kuwa ratiba ya wakati ya Mungu kwa siku yetu pia “haina budi kuja, haitakawia.”—Habakuki 2:3.
“Maji” Yenye Kuangamiza Kabisa
26, 27. (a) Isaya atabiri matukio gani? (b) Maneno ya Isaya yaonyesha nini kwa watumishi wa Yehova leo?
26 Isaya aendelea na maonyo yake: “Kwa sababu watu hawa wameyakataa maji ya Shiloa yapitayo polepole, na kufurahi kwa ajili ya Resini na huyo mwana wa Remalia, basi sasa angalia; Bwana aleta juu yao maji ya huo Mto, yenye nguvu, mengi sana, nayo ni mfalme wa Ashuru na utukufu wake wote; naye atakuja, na kupita juu ya mifereji yake yote, atafurika juu ya kingo zake zote; naye atapita, atapita kwa kasi na kuingia Yuda; atafurika na kupita katikati, atafika hata shingoni; na kule kuyanyosha mabawa yake kutaujaza upana wa nchi yako, Ee Imanueli.”—Isaya 8:5-8.
27 “Watu hawa,” ufalme wa kaskazini wa Israeli, wakataa agano la Yehova na Daudi. (2 Wafalme 17:16-18) Kwa maoni yao, agano hilo ni hafifu kama maji yanayotiririka ya Shiloa, mfereji unaoleta maji Yerusalemu. Wanafurahia vita yao dhidi ya Yuda. Lakini dharau hilo halitakosa kuadhibiwa. Yehova atawaruhusu Waashuri ‘wafurike,’ au wapindue, Siria na Israeli, kama vile Yehova atakavyoiruhusu sehemu ya kisiasa ya ulimwengu ifurike milki ya dini isiyo ya kweli. (Ufunuo 17:16; linganisha Danieli 9:26.) Kisha, Isaya asema, “maji” yanayofurika “[y]atapita kwa kasi na kuingia Yuda,” na kufika “hata shingoni,” hadi Yerusalemu, ambako kichwa (mfalme) cha Yuda chatawala.b Katika wakati wetu, vivyo hivyo wafishaji wa kisiasa wa dini isiyo ya kweli watavamia watumishi wa Yehova na kuwazingira “hata shingoni.” (Ezekieli 38:2, 10-16) Tokeo litakuwa nini? Basi, ni nini kinachotukia wakati wa Isaya? Je, Waashuri wafurika kupitia kuta za jiji na kuwafagilia mbali watu wa Mungu? La. Mungu yuko pamoja nao.
Msiogope—“Mungu Yu Pamoja Nasi”!
28. Licha ya juhudi nyingi za adui zao, Yehova ahakikishia Yuda nini?
28 Isaya aonya: “Fanyeni ghasia, enyi kabila za watu [wapingao watu wa agano wa Mungu], nanyi mtavunjwa vipande vipande; tegeni masikio, ninyi nyote wa nchi zilizo mbali; jikazeni viuno, nanyi mtavunjwa vipande vipande; jikazeni viuno, nanyi mtavunjwa vipande vipande. Fanyeni shauri pamoja, nalo litabatilika; semeni neno, lakini halitasimama; kwa maana Mungu yu pamoja nasi.” (Isaya 8:9, 10) Maneno hayo yatimia miaka kadhaa baadaye, wakati wa utawala wa Hezekia, mwana mwaminifu wa Ahazi. Waashuri watishapo Yerusalemu, malaika wa Yehova aangamiza 185,000 kati yao. Kwa wazi, Mungu yu pamoja na watu wake na pamoja na nasaba ya Daudi. (Isaya 37:33-37) Katika pigano linalokuja la Har–Magedoni, vivyo hivyo Yehova atamtuma Imanueli Mkuu kuwavunja vipande vipande adui Zake na kuwaokoa wote wanaomtumaini Yeye.—Zaburi 2:2, 9, 12.
29. (a) Wayahudi wa siku ya Ahazi watofautianaje na wale wa siku za Hezekia? (b) Kwa nini watumishi wa Yehova leo huepuka kujiingiza katika miungano ya kidini na ya kisiasa?
29 Tofauti na Wayahudi katika siku ya Hezekia, watu wa wakati wa Ahazi wakosa kuwa na imani katika ulinzi wa Yehova. Wao wapendelea muungano, au “njama,” (BHN), pamoja na Waashuri wakiwa ngome dhidi ya muungano wa Siria na Israeli. Hata hivyo, “mkono” wa Yehova wamchochea Isaya kuilaani “njia ya watu hawa,” au mtazamo unaopendwa. Aonya hivi: “Msihofu kwa hofu yao, wala msiogope. BWANA [“Yehova,” “NW”] wa majeshi ndiye mtakayemtakasa; na awe yeye hofu yenu, na awe yeye utisho wenu.” (Isaya 8:11-13) Wakizingatia hayo, watumishi wa Yehova leo hujilinda dhidi ya kupanga njama na, au kuyatumaini, mabaraza ya kidini na mashirikisho ya kisiasa. Watumishi wa Yehova wana hakika kamili katika uwezo wa Mungu wa kuwalinda. Kwani, ikiwa ‘Yehova yuko upande wetu, mwanadamu atatutenda nini?’—Zaburi 118:6, NW.
30. Watu wasiomtumaini Yehova watapatwa na nini hatimaye?
30 Isaya arudia kusema tena kwamba Yehova atathibitika kuwa “mahali patakatifu,” ulinzi, kwa wanaomtumaini. Kinyume cha hilo, wanaomkataa “watajikwaa juu yake, na kuanguka na kuvunjika, na kunaswa na kukamatwa”—vitenzi vitano vyenye nguvu vinavyoondoa shaka yoyote kuhusu yatakayowapata wale wasiomtumaini Yehova. (Isaya 8:14, 15) Katika karne ya kwanza, vivyo hivyo wale waliomkataa Yesu walijikwaa na kuanguka. (Luka 20:17, 18) Mwisho kama huo unawangojea watu wa leo wanaokataa kumwunga mkono Mfalme wa mbinguni aliyetawazwa, Yesu.—Zaburi 2:5-9.
31. Wakristo wa kweli leo waweza kufuataje kielelezo cha Isaya na cha wale wanaosikiliza mafundisho yake?
31 Katika siku ya Isaya, si wote wanaojikwaa. Isaya asema: “Ufunge huo ushuhuda, ukaitie muhuri sheria kati ya wanafunzi wangu. Nami nitamngojea BWANA, awafichaye uso wake nyumba ya Yakobo, nami nitamtazamia.” (Isaya 8:16, 17) Isaya pamoja na wale wanaotii mafundisho yake hawataiacha Sheria ya Mungu. Wao waendelea kumtumaini Yehova, hata ingawa wenzao wahalifu wakataa na hivyo kumfanya Yehova awafiche uso wake. Na tufuate kielelezo cha wale wanaomtumaini Yehova na tuazimie vivyo hivyo kushikamana na ibada safi!—Danieli 12:4, 9; Mathayo 24:45; linganisha Waebrania 6:11, 12.
“Ishara” na “Ajabu”
32. (a) Ni nani walio “ishara na ajabu” leo? (b) Kwa nini Wakristo wapaswa kuonekana tofauti na ulimwengu?
32 Sasa Isaya atangaza: “Angalieni, mimi na watoto hawa niliopewa na BWANA tu ishara na ajabu katika Israeli, zitokazo kwa BWANA wa majeshi, yeye akaaye katika mlima Sayuni.” (Isaya 8:18) Naam, Isaya, Shear-yashubu, na Maher-shalal-hash-bazi ni ishara za makusudi ya Yehova kwa Yuda. Leo pia, Yesu na ndugu zake watiwa-mafuta ni ishara. (Waebrania 2:11-13) Na “umati mkubwa” wa “kondoo wengine” wamejiunga nao katika hiyo kazi yao. (Ufunuo 7:9, 14; Yohana 10:16) Bila shaka, ishara ni muhimu ikiwa tu yaonekana waziwazi katika mazingira yake. Hali kadhalika, Wakristo hutimiza utume wao wakiwa ishara iwapo tu waonekana waziwazi kwamba wao ni tofauti na ulimwengu huu, wakimtumaini Yehova kikamili na kutangaza kwa ujasiri makusudi yake.
33. (a) Wakristo wa kweli wameazimia kufanya nini? (b) Sababu gani Wakristo wa kweli watasimama imara?
33 Basi, wote na washike viwango vya Mungu, wala si vile vya ulimwengu huu. Endelea kuonekana waziwazi kwa ujasiri—kama ishara—ukitekeleza utume aliopewa Isaya Mkuu, Yesu Kristo: ‘Tangaza mwaka . . . uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu.’ (Isaya 61:1, 2; Luka 4:17-21) Naam, mafuriko ya Ashuru yatapakaapo duniani kote—hata yakifikia shingo zetu—Wakristo wa kweli hawatafagiliwa mbali. Tutasimama imara kwa sababu “Mungu yu pamoja nasi.”
[Maelezo ya Chini]
a Ili kupata mambo ya ziada juu ya utimizo wa unabii huo, ona Insight on the Scriptures, Buku la 1, ukurasa wa 62 na wa 758, lililochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
b Ashuru pia yafananishwa na ndege ambaye mabawa yake yaliyonyoshwa “[ya]ujaza upana wa nchi yako.” Kwa hiyo, jeshi la Ashuru litajaza pembe zote za nchi.
[Picha katika ukurasa wa 103]
Isaya aliandamana na Shear-yashubu alipompasha Ahazi ujumbe wa Yehova
[Picha katika ukurasa wa 111]
Sababu gani Isaya aliandika “Maher-shalal-hash-bazi” kwenye ubao mkubwa?