Mtumaini Yehova—Si “Mpango wa Hila!”
1. Hali ya tengenezo lionekanalo la Yehova ilikuwa nini wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza?
WAKATI wa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza, hesabu za watu wa Yehova zilikuwa zimepunguzwa sana na matendo ya kuasi imani moja kwa moja. Mateso yaliyochochewa na adui za kidini yaliwaka pia dhidi yao. Makao makuu yao ya Brooklyn, New York, yalifungwa Tena, walikuwa bila usaidizi wa msimamizi wa Sosaiti, mwandishi-mweka-hazina, meneja wa afisi, na mwandikaji.mmoja wa wafanya kazi wa uhariri, na wawakilishi wengine wanne wa Sosaiti—wote wakiwa wamefungwa gerezani katika gereza kuu la Atlanta, Georgia. Ilionekana kama kwamba mwisho ulikuwa umekuja kwa Wanafunzi wa Biblia waliozaliwa kwa roho na kwamba utukuzo wao wa kimbingu ulikuwa karibu. Lakini sivyo!
2. Ni unabii gani wa Isaya uliokuwa na utumizi wa kisasa katika 1919?
2 Kwa kweli, katika masika ya 1919 maswali yaliyotokezwa na nabii Isaya yangeweza kutamkwa tena katika utumizi wa kisasa wa Isaya 66:6-8, NW; “Kuna sauti ya mngurumo kutoka kwenye mji ule, sauti kutoka kwenye hekalu lile! Ndiyo sauti ya Yehova akilipa kwa adui zake kinachostahiliwa. Kabla mwanamke yule hajaanza kuingia katika maumivu ya kujifungua alizaa. Kabla maumivu ya kujifungua hayajaweza kumjia huyo, hata alitokeza mtoto wa kiume. Ni nani amesikia juu ya jambo kama hilo? Ni nani ameona mambo kama haya? Je! nchi [hali ya ufanisi mtukufu wa kiroho] itazaliwa kwa maumivu ya kuzaa katika siku moja? Au je! taifa litazaliwa katika wakati mmoja? Kwa maana Sayuni imeingia katika maumivu ya kuzaa na pia ikazaa wana wa mwanamke huyo.”
3. Ni ushuhuda gani uliokuwapo katika 1919 kwamba mwanamke Sayuni alikuwa amezaa wana wake na kwamba “taifa” jipya lilikuwa limezaliwa “katika wakati mmoja”?
3 Wanafunzi wa Biblia wa Kimataifa walifanya mkusanyiko wao wa kwanza wa baada ya vita katika Cedar Point, Ohio, Septemba 1-8, 1919, wakiwa kama kwamba wamefufuliwa kutoka kwa wafu. Msimamizi wa Sosaiti, mwandishi-mweka-hazina, meneja wa afisi, na wengine waliokuwa wamefungwa, wakiwa wameondolewa mashtaka yote, walikuwapo kwa ajili ya pindi hiyo yenye furaha. Wakusanyikaji walifurahi Msimamizi Rutherford alipotangaza kuchapishwa kwa gazeti jipya, The Golden Age—linalojulikana leo kuwa Amkeni! Pia, ubatizo wa watu wapya zaidi ya 200 walio wakfu ulifanywa. Tengenezo la kitheokrasi la Yehova lilizaa wana walo kwenye maisha ya utendaji katika kipindi kile cha baada ya vita. Jambo hilo lilihitaji kuwe na taratibu mpya za upainia, ndiyo, za kujasiria, kwa upande wa “taifa” lililokuwa ni kama kwamba limezaliwa kwa mpigo mmoja na kukaa katika “nchi” iliyozaliwa kwa mara moja.
4. (a) Yote hayo yangekuwa na tokeo gani juu ya ‘Babuloni Mkuu’? (b) Ufichuzi wa msimamo halisi ‘Babuloni Mkuu’ pamoja na mamlaka za kimbingu zinazozidi nguvu za kibinadamu ndio utangulizi wa nini?
4 Hali hiyo ilikuwa yenye mwito wa ushindani. Ilitokea kwa kuishtukia ‘Babuloni Mkuu,’ ile milki ya ulimwengu ya dini ya uwongo. Washiriki wayo, hasa Jumuiya ya Wakristo, walifadhaika sana. Jumuiya hiyo ilihisi kwamba amani yayo ilikuwa ikikanyagwa. Sasa hifadhi ambayo jumuiya hiyo ilikuwa nayo ya kuwa mdai asiyeweza kufanyiwa ushindani kuhusu utendaji wa kidini ilitiwa hatarini Ingefunuliwa wazi ili uhusiano wayo na mamlaka za kimbingu zenye nguvu zinazozidi zile za kibinadamu uonekane ulivyokuwa kweli kweli, si uhusiano pamoja na yule Mungu wa Biblia Takatifu, bali na “mungu wa huu mfumo wa mambo”—Shetani, yule mwenye kumwendeleza Mpinga-Kristo aliyetabiriwa katika unabii wa Biblia. (2 Wakorintho 4:4; 1 Yohana 2:18, NW) Ufunuzi huo ulikuwa utangulizi tu wa maumivu yake ya kifo. Ndipo Hakimu Mkuu wa ulimwengu wote mzima atakapomtia mkononi moja kwa moja na kumwua, asimpe njia ya kuponyoka kutoka kwa waliokuwa wapenzi wake ambao sasa wangekuwa wenye hasira kali sana, hawara zake za kisiasa.
5. (a) Kwa sababu gani Jumuiya ya Wakristo itapatikana bila kujihadhari, na jumuiya hiyo inaonwaje na yule Mungu wa Biblia? (b) Ni jambo gani ambalo ‘Babuloni Mkuu’ haoni?
5 Hata Jumuiya ya Wakristo, iliyo na Biblia ambayo inatabiri yote hayo, itapatikana bila kujihadhari. Jumuiya hiyo itatumaini tangazo lijalo la “amani na usalama” kama linavyotungwa na mataifa ambamo jumuiya hiyo imeendesha kawaida zayo za kidini. Wakati ule ule, makanisa yayo yanapitisha sahani za sadaka, yakijitajirisha yenyewe kutokana na michango iliyotumbukizwa humo. Hata hivyo, kwa maoni ya yule Mungu wa Maandiko Matakatifu jumuiya hiyo ni “maskini, na kipofu, na uchi.” Haimtumaini Yehova, wala haitumii kwa faida mambo yaliyo bora kweli kweli ambayo yeye anaandaa. (Ufunuo 3:17, 18) Haiuoni mwandiko ukutani. Tunamaanisha nini kwa kusema hivyo?
Mwandiko Ukutani Watokea
6. Ni serikali gani kubwa ya kale ya ulimwengu inayoingia akilini sasa, na watu halisi wa Yehova walikuwa wakiendeleaje wakati huo?
6 Ili tufahamu, lazima tutazame nyuma kwenye saa zile za mwisho-mwisho za serikali kubwa ya tatu ya ulimwengu katika historia ya Biblia, Babuloni, katika kingo za Mto Eufrate. Belshaza alikuwa ndiye mtawala wa mwisho juu ya Babuloni, ambayo ilikuwa kutia ndani uwanja wa Mnara wa Babeli, ambapo Mungu mwenye nguvu zote aliivuruga lugha ile moja tu ya wajenzi, akawatawanya. (Mwanzo 11:1-9) Wakati wa saa za mwisho-mwisho za Babuloni, watu halisi wa Yehova, Wayahudi, walikuwa wahamishwa-mateka katika nchi hiyo ya kipagani. Lakini miaka yao 70 ya utekwa ilikaribia kumalizika.
7. (a) Kwa sababu gani Mfalme Belshaza aliwafanyia karamu watu wake wa vyeo vya juu akiwa na uhakika kamili? (b) Ni jambo gani lililotukia wakati wa karamu hiyo, na tokeo likawa nini juu ya mfalme huyo?
7 Wamedi na Waajemi walioungana, ambao wangekuwa ndio serikali kubwa ya nne ya ulimwengu katika historia ya Biblia, walikuja dhidi ya mji wa Babuloni uliokuwa umeimarishwa sana kwa ngome, ukionekana kama kwamba haungeweza kupenywa. Mto Eufrate ulitiririka kupita katikati ya mji huo, ukiwa na magati ya kuegeshea mashua kando-kando ya kingo za mto huo ambapo ndipo ilipokuwa ikifunguliwa milango yenye sehemu mbili-mbili ya shaba ya kuta za mji. Akiwa na uhakika kamili kwamba mji ulikuwa na usalama, Mfalme Belshaza alifanya “karamu kubwa kwa ajili ya elfu moja ya watu wake wa vyeo vya juu”—karamu ambayo ikawa ndiyo yake ya mwisho. Kwa ghafula, kulitokea ukutani mkono wenye kusogea-sogea, katika umbali alioweza kuuona Belshaza. Na mkono huo uliandika maneno yale yenye msiba “MENE, MENE, TEKELI na PARSINI.” (Danieli 5:1, 5, 25, NW) Hiyo ilikuwa katika usiku wa Oktoba 5, 539 K.W.K. Maneno hayo yalikuwa na uzito wa kugutusha sana. Mfalme Belshaza alitikisika kwa hofu. Ebu sasa ngojeni! Waiteni wenye hekima—wafanya miujiza ya uchawi na wanajimu waliokuwa na sifa ya kuweza kueleza ishara na viashirio vya mambo yajayo. Lakini mkorogo wa mwandiko wa maneno hayo ya mwujiza, ambayo wao hata hawakuweza kuusoma, uliyazidi maarifa yao. Sasa jambo gani lifanywe?
8, 9. (a) Ikiwa ndiyo njia pekee, ni mwendo gani uliopendekezwa kwa mfalme? (b) Ni jinsi gani Danieli alivyoufasiri mwandiko wa mkono ukutani? (c) Kwa sababu gani karamu kubwa ya Mfalme Belshaza ilitokeza unabii huo wa kuogopesha sana?
8 Tumeni mtu akaite Myahudi mmoja. Nini? Ati Myahudi? Ndiyo, mmoja wa wale wana wa kifalme na masharifu waliokuwa wametolewa Yerusalemu katika nchi ya kwake akaletwa na Maliki Nebukadreza mpaka Babuloni ili azoezwe kwa ajili ya utumishi wa kiserikali. Basi, ikiwa ndiyo njia pekee, ndilo jambo bora ambalo lingeweza kufanywa. Danieli ndiye aliyependekezwa na malkia-mama kuwa mwanamume wa hekima—mwanamume ambaye angeweza kufumbua mambo yaliyokorogeka na kuyafasiri. (Danieli 5:10-12) Tunaweza kuhisi unyamavu mwingi ulioenea chumba kile cha karamu wakati Danieli, alipofuata ombi la Mfalme Belshaza akaanza kumfasiria maneno hayo ya kifumbo maliki huyo wa serikali kubwa ya tatu ya ulimwengu katika historia ya Biblia pamoja na watu wake wa vyeo vya juu.
9 Danieli anaendelea kusema: “Kwa hiyo kutoka mbele yake kulikuwa kukipelekwa upande wa nyuma wa mkono, na mwandiko huu huu ukachorwa. Na huu ndio mwandiko uliochorwa: MENE, MENE, TEKELI na PARSINI. Hii ndiyo fasiri ya neno lile: MENE, Mungu amezihesabu siku za ufalme wake na ameumaliza. TEKELI, wewe umepimwa ratili katika mizani na umepatikana kuwa mpungufu. PERESI,a ufalme wako umegawanywa na kupewa kwa Wamedi na Waajemi.” (Danieli 5:24-28, NW) Mfalme Belshaza na watu wake wa vyeo vya juu na wanawake waandamani wao walikuwa wamekuwa wakionyesha dharau la makusudi la kunajisi ibada ya Mungu wa Danieli. Jinsi gani? Kwa kunywa divai kutokana na vyombo vya dhahabu vilivyokuwa vimechukuliwa kutoka hekalu la Yehova katika Yerusalemu wakati wa uharibifu wa mji huo mtakatifu katika mwaka 607 K.W.K. Hiyo ilikuwa kama kuongeza ufidhuli wenye dharau kwa umizo lililofanywa.—Danieli 5:3, 4, 23.
Sairasi Aliyetabiriwa Achukua Usukani
10, 11. (a) Yehova alikuwa amemtabiri nani kuwa mwenye kushinda Babuloni, na ni jinsi gani Isaya alivyoeleza ushinde uliokuwa ukija? (b) Ni jinsi gani Yehova alivyoutimiza unabii huu na kuleta adhabu ambayo Mfalme Belshaza na watu wake vyenye vyeo vya juu walistahili?
10 Kwenye Isaya 45:1-3, NW, Mungu Aliye Juu Zaidi alikuwa ametabiri hivi: “Hili ndilo Yehova amesema kwa mpakwa mafuta wake, kwa Sairasi, ambaye mkono wake wa kuume mimi nimeushika, kutiisha mbele yake mataifa, ili kwamba mimi nipate kuvua viuno vya wafalme; kufungua mbele yake milango ile yenye sehemu mbili-mbili, hivi kwamba hata malango yale hayatafungwa: ‘Mbele yako wewe mimi mwenyewe nitaenda, na mifuro ya nchi mimi nitainyoosha. Milango ya shaba mimi nitavunja vipande-vipande, na fito zile za chuma mimi nitazikata zianguke. Na mimi nitakupa wewe hazina zilizo katika giza na hazina zilizofichwa katika mahali-mahali pa maficho, ili kwamba wewe upate kujua kwamba mimi ni Yehova, Yule anayekuita wewe kwa jina lako.’”
11 Ili kutimiza unabii huo, Yehova alitia katika akili ya Sairasi Mwajemi fikira ya kuyageuzia kando maji ya Mto Eufrate na kuyaelekezea kando yakaingie katika ziwa fulani la kule. Ndipo, baada ya sakafu ya mto kuondolewa maji yote, askari za Sairasi walipiga miguu chini katika sakafu ya mto wakiwa wamefichwa na usiku, wakasonga moja kwa moja mpaka ndani katikati ya mji. Kwa kuwa milango ile yenye sehemu mbili-mbili iliyokuwa mbele ya maji ilikuwa imeachwa wazi, wao waliupanda ukingo wa mto wakaingia katika sebule lile lenye karamu, wakawalemea walinzi. Kwa hiyo karamu ya Mfalme Belshaza ikafikia mwisho wenye msiba ukiwa ni adhabu ambayo yeye na watu wake wa vyeo vya juu walistahili—kwa sababu walimtenda kwa aibu, dharau, na fedheha “yule Bwana wa mbingu” kwa kutumia vibaya vyombo vya hekaluni vilivyoibwa kutoka kao takatifu la Yehova katika Yerusalemu.
12. (a) Kwa kuwa Isaya alikuwa ametabiri kwamba Sairasi angeshinda Babuloni, kwa sababu gani Danieli anampa Dario Mmedi sifa ya kuteka Babuloni? (b) Dario na mshirika wake, Sairasi Mwajemi, walitangulia kufananisha nani?
12 Mstari wa mwisho wa Danieli sura ya 5 unasema kwamba baada ya Mfalme Belshaza kuuawa, Dario Mmedi “aliupokea ufalme, akiwa karibu na umri wa miaka sitini na miwili.” Kwa kuwa Dario alikuwa mkubwa kwa umri kuliko Sairasi Mwajemi, Danieli alimhesabia mfalme huyo Mwamedi sifa ya kuteka Babuloni. Yeye alitawala kutoka 539 mpaka 537 K.W.K. akiwa ndiye mtawala wa kifalme juu ya milki ya muungano wa Umedi na Uajemi. Anamfananisha vizuri Yehova Mungu. Mshirika wa Dario, Sairasi Mwajemi, alitangulia kufananisha Yesu Kristo, ambaye ndiye atakayetumiwa kwa umashuhuri zaidi na Yehova kupindua na kuharibu ‘Babuloni Mkuu,’ milki ya ulimwengu ya dini ya uwongo.
13, 14. Bila shaka Danieli alimwonyesha nini Sairasi Mwajemi, na ni jinsi gani kitabu cha Ezra kilichoandikwa baada ya wakati wa uhamisho kinavyoanza?
13 Sairasi alipokipanda kiti cha kifalme kutawala muungano wa Umedi na Uajemi katika 537 K.W.K., bila shaka nabii Danieli alimwonyesha unabii wa Yehova uliomhusu yeye kama ulivyopatikana kwenye Isaya 45. Kitabu cha Ezra kilichoandikwa baada ya wakati wa uhamisho kinaanza kwa maneno haya:
14 “Na katika mwaka wa kwanza wa Sairasi mfalme wa Uajemi, ili kwamba neno la Yehova kutoka kinywa cha Yeremia [kwa habari ya uhamisho kuwa miaka 70 katika urefu (Yeremia 25:12; 29:10, 14)] liweze kutimizwa, Yehova aliiamsha roho ya Sairasi mfalme wa Uajemi hivi kwamba yeye akafanya mlio upite katika sehemu zote za milki yake, na pia kwa maneno yaliyoandikwa, akisema: ‘Hili ndilo jambo ambalo Sairasi mfalme wa Uajemi amesema, “Falme zote za dunia Yehova yule Mungu wa mbingu amenipa mimi, na yeye mwenyewe amenipa utume nimjengee nyumba katika Yerusalemu, ulio katika Yuda. Ye yote aliyemo miongoni mwenu kati ya watu wake wote, Mungu wake na athibitike kuwa pamoja naye. Kwa hiyo acheni huyo apande kwenda Yerusalemu, ulio katika Yuda, na kuijenga upya nyumba ya Yehova yule Mungu wa Israeli—yeye ndiye Mungu wa kweli—ambayo ilikuwa katika Yerusalemu.”—Ezra 1:1-3, NW.
Yule Sairasi Mkubwa Zaidi Ashinda ‘Babuloni Mkuu’
15. (a) Ni wakati gani Sairasi mfananishwa alipoanza kutawala? (b) Ni msimamo gani usioondoleka ambao Mashahidi wa Yehova wanachukua kwa habari ya mpango wa hila pamoja na Umoja wa Mataifa, na kwa sababu gani?
15 Sairasi Mkuu wa kisasa aliye mfananishwa alianza kutawala katika 1914 mwishoni mwa “nyakati zilizowekwa za mataifa,” kama ilivyotabiriwa na Yesu mwenyewe kwenye Luka 21:24 (NW) Kwa kuupuuza kabisa uhakika huo wenye maana ulimwenguni pote, mataifa ndani ya Umoja wa Mataifa yaliamua kujifanyia mwaka 1986 uwe Mwaka wa Amani ya Kimataifa yao. Lakini Mashahidi wa Yehova hawapatikani kwa vyo vyote bila kujihadhari kuhusiana na jambo hilo. Wakati tangazo lililotabiriwa la “amani na usalama” litakapofanywa mwishowe, wao hawatajiunga na wafuasi wa kisiasa na washirika wenye urafiki wa ‘Babuloni Mkuu’ katika kula karamu ya fanikio hilo kubwa katika tarehe hii iliyosonga sana katika historia ya mataifa ya kilimwengu. Wao hawatetei mpango wa hila pamoja na Umoja wa Mataifa au chombo kinginecho chote cha kuletea amani. (Isaya 8:12, NW) Wao wanatumia maneno ya Isaya 8:20 kama kipingio, kusema hivi: “Kwenye sheria na kwenye ushuhuda! Ikiwa wao hawasemi kulingana na neno hili, wao hawana nuru ya pambazuko.” (New International Version) Nao wakitoa sababu kwa msimamo wao usioondoleka, wanasema: “Kwa maana Mungu yuko pamoja na sisi!” (Isaya 8:10, NW) Kusema wazi, hiyo inamaanisha kwamba Yehova Mungu hashiriki sehemu yo yote katika hatua zao za kisiasa zinazochaguliwa na mataifa kwa ajili ya “amani na usalama” bali, anazipinga kiwazi.
16. Ni jinsi gani neno la kiunabii kwenye Ufunuo 17:16, 17 litaonyeshwa kwa ukamili kuwa la kweli na kukiwa na tokeo gani juu ya watu wa Yehova?
16 Kwa kufanya maarifa ya ustadi, Yehova atamtumia Sairasi wake Mkubwa Zaidi atie ndani ya moyo na akili ya viongozi wa kisiasa wa ulimwengu fikira ya kugeuka dhidi ya ‘Babuloni Mkuu,’ ile milki ya ulimwengu ya dini ya uwongo. Wao watamguta-guta mpaka afe, kama kwamba ni kwa pembe za mnyama-mwitu mkali sana. Neno la kiunabii kwenye Ufunuo 17 litaonyeshwa kwa ukamili kuwa la kweli na Mashahidi wa Yehova duniani watafanya shangwe ya yubile juu ya jambo hilo.—Ufunuo 17:16, 17; 19:1-3.
Kuuendeleza Ushirika Wetu Unaofaa Pamoja na Yehova
17. Ingawa Mashahidi wa Yehova si sehemu ya ‘Babuloni Mkuu,’ watawala wa ulimwengu watafanya nini?
17 Ndipo, ingawa Mashahidi wa Yehova si sehemu ya ‘Babuloni Mkuu’ bali ni wafichuzi dhahiri wake, na ingawa wao hawajashiriki sehemu yo yote katika mambo ya kisiasa ya ulimwengu huu, wanasiasa hao wasiofuata dini watageuka dhidi ya Mashahidi wenye kusalia. Wakiwa wamepiga moyo konde kuwa watawala watumia nguvu wenye uongozi kamili juu ya sehemu zote za jamii ya kibinadamu duniani, wanasiasa hao watawarushia dharuba yenye uzito kamili Mashahidi wa Aliye Mkuu Zaidi, ambaye ndiye Chanzo cha serikali yote yenye uadilifu.
18. Ni tendo gani la kuogopesha sana atakalofanya Yehova, liifunike Gharika ya siku za Noa ionekane kama si kitu?
18 Sasa hapa ndipo itakapokuwa lazima Mwenye Enzi Kuu aliye Mwenye Nguvu Zote wa mbingu na dunia ajiingize na kuwafanya waharabu hao wa ‘Babuloni Mkuu’ wajue na kufahamu kwamba Yule ambaye amekuwa na Mashahidi wa karne ya 20 ni Mungu wa kikweli, Mungu mwenye nguvu zote—Mungu anayestahili kupewa ibada ya moyo wote isiyogawanyika na viumbe wake hapa chini katika kibago cha miguu yake, duniani. Atafanya hivyo kwa namna yenye kutia hofu nyingi ambayo itafanya utaya wa chini wa vinywa vya Mashahidi wake wenye kutazama wakiwa kando-kando lishuke kwa mzubao. Yeye atafanya maarifa yake matukufu ya kivita yasiyotangulia kuwa na kifani yafikie ushindi wa kimungu. (Ufunuo 16:14, 16; 19:19-21) Hiyo itamaanisha mfumo huu mwovu wa mambo wenye kuongozwa na Ibilisi utakoma kwa kishindo kitakachoipita kwa mbali Gharika ya siku za Noa iliyouharibu ulimwengu.
19. Yehova atakuwa na mashahidi gani kwa habari ya kujiondolea malawama akiwa ndiye Mwenye Enzi Kuu wa Ulimwengu Wote Mzima, na jambo hilo litaonyesha nini?
19 Sawasawa na vile Yehova alivyokuwa na mashahidi wa kuushuhudia mwisho wa ulimwengu wa kale katika Gharika iliyozamisha wanadamu wote waliokuwa nje ya safina, ndivyo yeye atakavyokuwa na mashahidi papa hapa duniani, kwa kadiri kubwa zaidi, kwa habari ya kitendo chake kisichoweza kurudiwa cha kujiondolea malawama akiwa ndiye Mwenye Enzi Kuu wa Ulimwengu Wote Mzima. (2 Petro 3:6, 7, 13, 14) Hao watakuwa ni wale wanaomtumaini yeye ili kupata amani na usalama katikati ya ulimwengu huu uliohukumiwa maangamizi. Mwenye furaha atakuwa wewe kuhesabiwa miongoni mwa Mashahidi hao watakaopendelewa kimwujiza. Amani na usalama wako utakuwa umeonyeshwa kuwa unatoka kwa Yehova Mungu wala si kutoka kwenye muungano wo wote, au mpango wa hila, na serikali za kisiasa za mfumo huu wa mambo wenye kuongozwa na Ibilisi.
20. Yehova atatokezaje, nasi tumepiga moyo konde tufanye nini?
20 Yehova Mungu atatokeza kwa utukufu akiwa ndiye Yule mwenye haki ya kuabudiwa na kutumikiwa akiwa Aliye Mkuu Kimungu —Mungu wa miungu, Yule wa peke yake kabisa ambaye maneno ya mtunga zaburi aliyeongozwa na roho ya Mungu yalielekezwa kwake: “Hata tangu wakati usiojulikana mpaka wakati usiojulikana wewe ndiwe Mungu.” (Zaburi 90:2, NW) Tukiwa na uthamini unaoendelea kukua wakati wote, acheni sisi tuendeleze tumaini letu katika Yehova Mungu na ushirika wetu pamoja naye kupitia Sairasi Mkubwa Zaidi, Yesu Kristo.
[Maelezo ya Chini]
a “Parsini” ndiyo hesabu ya wingi ya neno “Peresi” na inamaanisha “migawanyiko.”
Je! Wewe Unakumbuka?
◻ Ni jambo gani asiloliona‘Babuloni Mkuu’?
◻ Tokeo lenye msiba la karamu ya Belshaza lilitangulia kufananisha nini?
◻ Ni nani atakayeshinda ‘Babuloni Mkuu’?
◻ Ni msimamo gani ambao Mashahidi wa Yehova wanachukua kwa habari ya mpango wa hila pamoja na Umoja wa Mataifa?
◻ Kwa sababu gani wote wanaoweka tumaini lao katika Yehova ili kupata amani na usalama watakuwa wenye furaha?
[Picha katika ukurasa wa 25]
Danieli aufasiri mwandiko ule wa kifumbo kuwa ujumbe wa maangamizi kwa milki ya Kibabuloni