Sura ya 11
Ole Wao Waasi!
1. Yeroboamu alifanya kosa gani kubwa?
WATU wa Yehova wa agano walipogawanyika na kuwa falme mbili, ufalme wa kaskazini wa makabila kumi ukawa chini ya utawala wa Yeroboamu. Mfalme huyo mpya alikuwa mtawala mwenye uweza na nguvu. Lakini hakuwa na imani kamili katika Yehova. Kwa sababu hiyo alifanya kosa kubwa lililoathiri vibaya historia yote ya ufalme wa kaskazini. Sheria ya Kimusa iliwaamuru Waisraeli wafunge safari mara tatu kwa mwaka ya kwenda hekaluni huko Yerusalemu, jiji ambalo sasa lilikuwa katika ufalme wa kusini wa Yuda. (Kumbukumbu la Torati 16:16) Akihofia kuwa safari hizo za kawaida zingewafanya raia zake wafikirie kuhusu kuungana tena na ndugu zao wa kusini, Yeroboamu “a[li]fanyiza ng’ombe wawili wa dhahabu, akawaambia watu, Ni vigumu kwenu kupanda kwenda Yerusalemu; tazama, hii ndiyo miungu yenu, enyi Israeli, iliyowapandisha kutoka nchi ya Misri. Akamweka mmoja katika Betheli, na wa pili akamweka katika Dani.”—1 Wafalme 12:28, 29.
2, 3. Kosa la Yeroboamu liliathirije Israeli?
2 Kwa muda fulani, ilionekana kwamba mpango wa Yeroboamu umefanikiwa. Hatua kwa hatua watu wakaacha kwenda Yerusalemu nao wakaanza kuabudu mbele ya ng’ombe hao wawili. (1 Wafalme 12:30) Hata hivyo, zoea hilo la kidini la uasi lilifisidi ufalme wa kaskazini wa makabila kumi. Miaka iliyofuata, hata Yehu, aliyekuwa amefanya bidii yenye kustahili pongezi ya kuondolea mbali ibada ya Baali katika Israeli, aliendelea kuinamia ndama hao wa dhahabu. (2 Wafalme 10:28, 29) Uamuzi mbaya sana wa Yeroboamu ulisababisha mambo gani mengine? Misukosuko ya kisiasa na watu kuteseka.
3 Kwa sababu ya uasi wa Yeroboamu, Yehova alisema kuwa uzao wake haungetawala katika nchi hiyo, na mwishowe msiba mbaya sana ungeukumba ufalme wa kaskazini. (1 Wafalme 14:14, 15) Neno la Yehova likatimia kweli. Wafalme saba kati ya wafalme wa Israeli walitawala kwa miaka miwili au kwa muda usiozidi huo—baadhi yao kwa siku chache tu. Mfalme mmoja alijiua, na sita wakauawa na watu wenye tamaa ya makuu walionyakua kiti cha ufalme. Hasa baada ya utawala wa Yeroboamu wa Pili, uliokwisha karibu mwaka wa 804 K.W.K. huku Uzia akitawala katika Yuda, Israeli ilikumbwa na ghasia, jeuri, na mauaji. Kwa sababu ya hali hizo, Yehova apeleka onyo, au “neno,” la moja kwa moja kupitia Isaya kwa ufalme wa kaskazini. “Bwana alimpelekea Yakobo neno, likamfikilia Israeli.”—Isaya 9:8.a
Kiburi na Kujisifu Hutokeza Hasira ya Kisasi ya Mungu
4. Yehova apeleka “neno” gani dhidi ya Israeli, na kwa nini?
4 “Neno” la Yehova halitapuuzwa. “Watu wote watajua, yaani, Efraimu na yeye akaaye Samaria, wasemao kwa kiburi na kwa kujisifu nafsi zao.” (Isaya 9:9) “Yakobo,” “Israeli,” “Efraimu,” na “Samaria” yote hurejezea ufalme wa kaskazini wa Israeli, ambapo Efraimu ndilo kabila kubwa na Samaria ni jiji kuu. Neno la Yehova dhidi ya ufalme huo ni taarifa kali ya hukumu, kwa kuwa Efraimu imekuwa kaidi katika uasi nayo imeshupaa katika kujisifu mbele za Yehova. Mungu hatawalinda watu hao wasipate matokeo ya njia zao mbovu. Watalazimika kusikia, au kuzingatia, neno la Mungu.—Wagalatia 6:7.
5. Waisraeli wakosaje kuathiriwa na hukumu za Yehova?
5 Hali ziendeleapo kuwa mbaya, watu wapata hasara kubwa, kutia ndani nyumba zao—ambazo kwa kawaida hujengwa kwa matofali ya udongo na mbao zisizo ghali. Je, hali hiyo yafanya mioyo yao inyenyekee? Je, watatii manabii wa Yehova na kumrudia Mungu wa kweli?b Isaya arekodi jibu la watu hao wenye kujisifu: “Matofali yameanguka, lakini sisi tutajenga kwa mawe yaliyochongwa; mikuyu imekatwa lakini sisi tutaweka mierezi badala yake.” (Isaya 9:10) Waisraeli wamkaidi Yehova na kuwakataa manabii wake, wanaowaeleza sababu ya kupatwa na magumu hayo. Ni kana kwamba watu hao wanasema: ‘Huenda tukapoteza nyumba zilizojengwa kwa matofali ya udongo ziharibikazo upesi na mbao zisizo ghali, ila tutalipia hasara hiyo kwa kujenga upya kwa vifaa bora—mawe yaliyochongwa na mierezi!’ (Linganisha Ayubu 4:19.) Yehova hana jingine ila kuzidi kuwatia nidhamu.—Linganisha Isaya 48:22.
6. Yehova adhoofishaje mbinu za mwungano wa Siria na Israeli dhidi ya Yuda?
6 Isaya aendelea: “BWANA atawainua adui wa Resini juu yake.” (Isaya 9:11a) Mfalme Peka wa Israeli na Mfalme Resini wa Siria wameungana. Wanapanga njama ya kuvamia ufalme wa Yuda wa makabila mawili na kumtawaza mfalme fulani kibaraka—“mwana wa Tabeeli”—kwenye kiti cha ufalme cha Yehova katika Yerusalemu. (Isaya 7:6) Lakini njama hiyo itaambulia patupu. Resini anao adui wenye nguvu, na Yehova “atawainua” adui hao dhidi “yake,” Israeli. Neno “atawainua” lamaanisha kuwaruhusu wapige vita vya ushindi vitakavyoharibu mwungano huo na malengo yake.
7, 8. Ushindi wa Ashuru dhidi ya Siria una matokeo gani kwa Israeli?
7 Kuvunjika kwa mwungano huo kwaanza Ashuru ishambuliapo Siria. “Mfalme wa Ashuru akapanda juu ya Dameski [jiji kuu la Siria], akautwaa, akawahamisha watu wake mateka mpaka Kiri, akamwua Resini.” (2 Wafalme 16:9) Baada ya kupoteza mshirika wake mwenye nguvu, Peka atambua kwamba mbinu zake dhidi ya Yuda zimekomeshwa. Kwa hakika, muda mfupi baada ya kifo cha Resini, Hoshea amwua Peka, na kunyakua kiti cha ufalme huko Samaria.—2 Wafalme 15:23-25, 30.
8 Siria, mshirika wa awali wa Israeli, sasa ni kibaraka wa Ashuru, utawala wenye nguvu zaidi katika eneo hilo. Isaya atabiri kuhusu namna Yehova atakavyoutumia mwungano huo mpya wa kisiasa: “[Yehova] atawachochea adui zake [Israeli]; Waashuri [“Wasiria,” “NW”] upande wa mbele, na Wafilisti upande wa nyuma, nao watamla Israeli kwa kinywa kilicho wazi. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.” (Isaya 9:11b, 12) Naam, Siria sasa ni adui ya Israeli, lazima Israeli ijitayarishe kushambuliwa na Ashuru na Siria. Uvamizi huo wafanikiwa. Ashuru yamfanya Hoshea mnyakuzi kuwa mtumishi wake, na kutoza ushuru mkubwa mno. (Makumi kadhaa ya miaka mapema, Ashuru ilipokea kiasi kikubwa cha ushuru kutoka kwa Mfalme Menahemu wa Israeli.) Maneno ya nabii Hosea ni barabara kabisa: “Wageni wamekula nguvu zake [za Efraimu]”!—Hosea 7:9; 2 Wafalme 15:19, 20; 17:1-3.
9. Kwa nini twaweza kusema kuwa Wafilisti washambulia “upande wa nyuma”?
9 Je, Isaya hasemi pia kwamba Wafilisti watavamia “upande wa nyuma”? Ndiyo. Kabla ya siku za dira zenye kutegemea uvutano wa sumaku, Waebrania waliashiria upande kwa kutegemea macheo ya jua. Kwa hiyo, “upande wa mbele” ulikuwa mashariki, ilhali magharibi, makao ya pwani ya Wafilisti, ilikuwa “upande wa nyuma.” Kwa habari hii, huenda “Israeli” inayotajwa katika Isaya 9:12 ikatia ndani Yuda kwa sababu Wafilisti walivamia Yuda wakati wa utawala wa Ahazi, aliyetawala siku za Peka, na kutwaa majiji na ngome kadhaa za Yudea na kuzifanya makazi yao. Sawa na Efraimu iliyo kaskazini, Yuda yastahili nidhamu hiyo kutoka kwa Yehova, kwa sababu Yuda pia imejaa uasi.—2 Mambo ya Nyakati 28:1-4, 18, 19.
Toka ‘Kichwa Hata Mkia’—Taifa la Waasi
10, 11. Yehova ataleta adhabu gani dhidi ya Israeli kwa sababu ya uasi wao wenye kuendelea?
10 Licha ya mateso yake yote—na licha ya matangazo makali ya manabii wa Yehova—ufalme wa kaskazini waendelea kuasi dhidi ya Yehova. “Watu hao hawakumwelekea yeye aliyewapiga, wala kumtafuta BWANA [“Yehova,” “NW”] wa majeshi.” (Isaya 9:13) Basi, nabii huyo asema: “BWANA atakata katika Israeli kichwa na mkia, kuti na nyasi, katika siku moja. Mzee mwenye kuheshimiwa ndiye kichwa, na nabii afundishaye uongo ndiye mkia. Kwa maana wawaongozao watu hawa ndio wawakoseshao, na hao walioongozwa na watu hao wameangamia.”—Isaya 9:14-16.
11 “Kichwa” na “kuti” zawakilisha “mzee mwenye kuheshimiwa”—viongozi wa taifa. “Mkia” na “nyasi” zarejezea manabii wa uwongo wanaotamka maneno yawapendezayo viongozi wao. Msomi mmoja wa Biblia aandika: “Manabii wasio wa kweli waitwa mkia, kwa maana walikuwa watu wenye utovu mkubwa zaidi wa kiadili, na kwa maana walikuwa wafuasi vibaraka na waungaji mkono wa watawala waovu.” Profesa Edward J. Young asema hivi kuhusu manabii hao wasio wa kweli: “Hawakuwa viongozi hata kidogo bali walifuata tu waendako viongozi na kusifu-sifu na kujipendekeza, kama mkia wa mbwa unaotikiswa-tikiswa.”—Linganisha 2 Timotheo 4:3.
Hata ‘Wajane na Mayatima’ Ni Waasi
12. Ufisadi umepenya kadiri gani katika jamii ya Israeli?
12 Yehova ndiye Mtetezi wa wajane na mayatima. (Kutoka 22:22, 23) Ijapokuwa hivyo, sikia asemayo Isaya sasa: “Bwana hatawafurahia vijana wao, wala hatawahurumia yatima zao wala wajane wao; maana kila mtu ni mnajisi, dhalimu, na kila ulimi hunena upumbavu. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.” (Isaya 9:17) Uasi umefisidi tabaka zote za jamii, kutia ndani wajane na mayatima! Yehova awatuma manabii wake kwa saburi, akitumaini kuwa watu hao watabadili njia zao. Kwa kielelezo, “Ee Israeli, mrudie BWANA, Mungu wako; maana umeanguka kwa sababu ya uovu wako,” asihi Hosea. (Hosea 14:1) Hapana budi Mtetezi wa wajane na mayatima ahuzunika sana kwa kulazimika kutekeleza hukumu dhidi yao pia!
13. Twaweza kujifunza nini kutokana na ile hali katika siku ya Isaya?
13 Sawa na Isaya, twaishi katika nyakati za hatari kabla ya siku ya hukumu ya Yehova dhidi ya waovu. (2 Timotheo 3:1-5) Basi, ni muhimu kwa Wakristo wa kweli, haidhuru hali yao maishani, wadumu wakiwa safi kiroho, kiadili, na kiakili ili waendelee kupata upendeleo wa Mungu. Kila mmoja na alinde kwa bidii uhusiano wake na Yehova. Yeyote aliyeponyoka kutoka katika “Babiloni Mkubwa” na ‘asishiriki pamoja naye dhambi zake’ tena.—Ufunuo 18:2, 4.
Ibada Isiyo ya Kweli Hutokeza Jeuri
14, 15. (a) Ibada ya roho waovu huleta nini? (b) Isaya atabiri kwamba Israeli itapata mateso gani yanayoendelea?
14 Ibada isiyo ya kweli kwa hakika ni kuabudu roho waovu. (1 Wakorintho 10:20) Kama ilivyodhihirika kabla ya Furiko, uvutano wa roho waovu husababisha jeuri. (Mwanzo 6:11, 12) Basi, haishangazi kwamba Israeli inapoasi na kuanza kuabudu roho waovu, jeuri na uovu wajaa nchini.—Kumbukumbu la Torati 32:17; Zaburi 106:35-38.
15 Kwa maneno yenye nguvu, Isaya afafanua kuenea kwa uovu na jeuri katika Israeli: “Uovu huteketeza kama moto; huila mibigili na miiba, naam, huwaka katika vichaka vya mwitu, nao hupaa juu katika mawingu mazito ya moshi. Kwa sababu ya hasira ya BWANA wa majeshi nchi hii inateketea kabisa; watu hawa nao ni kama kuni zitiwazo motoni; hapana mtu amhurumiaye ndugu yake. Hupokonya upande wa mkono wa kuume, nao huona njaa! hula upande wa mkono wa kushoto, wala hawashibi! watakula kila mtu nyama ya mkono wake mwenyewe. Manase anamla Efraimu, naye Efraimu anamla Manase; nao wawili pamoja watakuwa juu ya Yuda. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.”—Isaya 9:18-21.
16. Maneno ya Isaya 9:18-21 yatimizwaje?
16 Kama moto usambaao kichaka kwa kichaka, jeuri yasambaa haraka isiweze kudhibitiwa nayo upesi yavifikia “vichaka vya mwitu,” ikisababisha moto mkubwa wa mwituni wa jeuri. Waelezaji wa Biblia Keil na Delitzsch wasema kwamba kiwango cha jeuri ni cha “kujiangamiza kikatili sana wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vyenye vurugu. Huku wakiwa hawana hisia zozote, walinyafuana pasipo kuridhika.” Labda makabila ya Efraimu na Manase yatajwa hapa kwa sababu hayo ndiyo wawakilishi wakuu wa ufalme wa kaskazini na, wakiwa wazao wa wana wawili wa Yosefu, ndio wenye udugu wa karibu zaidi kati ya yale makabila kumi. Hata hivyo, licha ya hayo, hawakomeshi jeuri yao ya kuuana ndugu kwa ndugu ila tu wapiganapo vita na Yuda iliyo kusini.—2 Mambo ya Nyakati 28:1-8.
Waamuzi Wafisadi Wakabili Mwamuzi Wao
17, 18. Mifumo ya kisheria na ya utawala ya Israeli ina ufisadi gani?
17 Kisha Yehova akaza jicho lake lenye kuhukumu juu ya waamuzi wafisadi wa Israeli na maofisa wengine. Wao hutumia vibaya mamlaka yao kwa kuwapora maskini na waliotaabishwa ambao huwaendea ili kutafuta haki. Isaya asema: “Ole wao wawekao amri zisizo za haki, na waandishi waandikao maneno ya ushupavu; ili kumpotosha mhitaji asipate haki yake, na kuwanyang’anya maskini wa watu wangu haki yao; ili wajane wawe mateka yao, na kuwafanya yatima waliofiwa na baba zao kuwa mawindo yao!”—Isaya 10:1, 2.
18 Sheria ya Yehova hukataza namna zote za ukosefu wa haki: “Msitende yasiyo haki katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi mwenye nguvu.” (Mambo ya Walawi 19:15) Maofisa hao waipuuza sheria hiyo, na kujiwekea “amri zisizo za haki” ili kuhalalisha wizi ulio wazi na wenye ukatili sana—kutwaa mali chache za wajane na mayatima. Kwa wazi, miungu vipofu ya Israeli haioni ukosefu huo wa haki, lakini Yehova auona. Kupitia Isaya, Yehova sasa awakazia fikira waamuzi hao waovu.
19, 20. Hali ya waamuzi wafisadi wa Israeli itabadilishwaje, na “utukufu” wao utakuwaje?
19 “Nanyi mtafanya nini siku ya kujiliwa, na wakati wa uangamivu, utakaokuja kutoka mbali sana? Je! mtamkimbilia nani mpate msaada? na utukufu wenu mtauacha wapi? Watainama chini ya wafungwa tu, wataanguka chini yao waliouawa.” (Isaya 10:3, 4a) Wajane na mayatima hawana waamuzi wenye haki wa kukata rufani kwao. Basi yastahili sana kwa kuwa Yehova sasa awauliza waamuzi hao Waisraeli wafisadi watamwendea nani kwa sababu sasa Yehova anataka watoe hesabu. Naam, karibuni watatambua kuwa “ni jambo lenye kuhofisha kuanguka katika mikono ya Mungu aliye hai.”—Waebrania 10:31.
20 “Utukufu” wa waamuzi hao waovu—fahari ya kilimwengu, staha, na uwezo unaotokana na mali na cheo chao—hautadumu. Baadhi yao watakuwa wafungwa wa vita, “watainama chini,” au kuchutama, kati ya wafungwa wengine, ilhali wengine nao watauawa, na maiti za waliokufa vitani zitafunika maiti zao. “Utukufu” wao watia ndani mali yao waliyopata kwa ufisadi, itakayoporwa na adui.
21. Kwa kuzingatia adhabu ambazo Israeli imepata, je, hasira ya Yehova juu yao imekoma?
21 Isaya amalizia ubeti huu wa mwisho kwa onyo lenye kuhofisha: “Pamoja na hayo yote [ole zote ambazo zimelipata taifa hilo kufikia sasa] hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.” (Isaya 10:4b) Naam, Yehova angali na mengi ya kuambia Israeli. Mkono wa Yehova ulionyoshwa hautarudishwa nyuma hata atoapo pigo la mwisho na lenye kuangamiza kwa ufalme wa kaskazini ulioasi.
Usinaswe Kamwe na Lisilo la Kweli na Kujipenda
22. Twaweza kujifunza nini kutokana na yale yaliyopata Israeli?
22 Neno la Yehova kupitia Isaya lililemea sana Israeli nalo ‘halikumrudia bila mafanikio.’ (Isaya 55:10, 11) Historia yarekodi mwisho wenye kuhuzunisha wa ufalme wa kaskazini wa Israeli, nasi twaweza tu kuwazia mateso waliyovumilia wakazi wake. Vivyo hivyo, neno la Mungu litatimizwa juu ya mfumo wa mambo uliopo, hasa juu ya Jumuiya ya Wakristo yenye kuasi. Basi, ni muhimu kama nini kwa Wakristo kutosikiliza propaganda za uwongo, zenye kumpinga Mungu! Kwa sababu ya Neno la Mungu, mbinu za werevu za Shetani zimekwisha fichuliwa, ili zisipate kutushinda kama zilivyowashinda watu wa Israeli ya kale. (2 Wakorintho 2:11) Sisi sote na tusiache kamwe kumwabudu Yehova “kwa roho na kweli.” (Yohana 4:24) Tukifanya hivyo, mkono wake ulionyoshwa hautawapiga waabudu wake kama vile ulivyoipiga Efraimu yenye kuasi; mikono yake itawakumbatia kwa shauku, naye atawasaidia kutembea katika barabara iendayo kwenye uhai udumuo milele katika dunia paradiso.—Yakobo 4:8.
[Maelezo ya Chini]
a Isaya 9:8–10:4 ina beti nne (mafungu ya shairi), kila mmoja ukimalizika kwa kibwagizo chenye kutisha: “Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.” (Isaya 9:12, 17, 21; 10:4) Mtindo huo wa kifasihi huunganisha Isaya 9:8–10:4 kuwa “neno” moja kuu. (Isaya 9:8) Pia ona kwamba “mkono [wa Yehova] umenyoshwa hata sasa,” si kwa ajili ya kuleta upatanisho, bali kuhukumu.—Isaya 9:13.
b Manabii wa Yehova waliotumwa kwa ufalme wa kaskazini wa Israeli ni pamoja na Yehu (siye yule mfalme), Eliya, Mikaya, Elisha, Yona, Odedi, Hosea, Amosi, na Mika.
[Picha katika ukurasa wa 139]
Uovu na jeuri zasambaa katika Israeli kama moto wa mwituni
[Picha katika ukurasa wa 141]
Yehova atawatoza hesabu wale wanaowaonea wengine