Sura ya 16
Mtumaini Yehova Upate Mwongozo na Ulinzi
1, 2. Watu wa Mungu wakabili hatari gani katika karne ya nane K.W.K., na wengi wao wana mwelekeo wa kutafuta ulinzi kutoka kwa nani?
KAMA tulivyoona katika sura zilizotangulia za kitabu hiki, watu wa Mungu wakabili tisho lenye kutia woga katika karne ya nane K.W.K. Waashuri wenye hamu ya kumwaga damu wanaharibu nchi moja baada ya nyingine, na muda si muda watashambulia ufalme wa kusini wa Yuda. Wakazi wa nchi hiyo watatafuta ulinzi kutoka kwa nani? Wao wako katika uhusiano wa agano pamoja na Yehova na yawapasa kumtegemea ili awasaidie. (Kutoka 19:5, 6) Mfalme Daudi alifanya hivyo hasa. Alikiri hivi: “BWANA [“Yehova,” NW] ndiye jabali langu, na ngome yangu, na mwokozi wangu.” (2 Samweli 22:2) Hata hivyo, yaonekana kwamba wengi katika karne ya nane K.W.K. hawamtumaini Yehova kuwa ngome yao. Wao wana mwelekeo wa kutegemea Misri na Ethiopia, wakitumaini kwamba mataifa hayo mawili yatawakinga dhidi ya uvamizi wa Ashuru wenye kutisha. Wamekosea.
2 Kupitia Isaya nabii wake, Yehova aonya kwamba kukimbilia Misri au Ethiopia kutatokeza msiba. Maneno yaliyopuliziwa ya nabii huyo yaandaa fundisho lenye manufaa kwa watu wa siku yake nayo yana fundisho lenye thamani kwetu kuhusu umuhimu wa kumtumaini Yehova.
Nchi Yenye Umwagikaji wa Damu
3. Fafanua jinsi ambavyo Ashuru ilizingatia sana uwezo wa kijeshi.
3 Waashuri walijulikana kwa sababu ya uwezo wao wa kijeshi. Kitabu cha Ancient Cities chataarifu hivi: “Waliabudu nguvu, nao wangesali tu kwa sanamu kubwa za mawe, simba na mafahali ambao miguu yao, mabawa yao ya tai, na vichwa vyao vya kibinadamu vyenye nguvu mno vilikuwa ishara ya nguvu, moyo mkuu, na ushindi. Kazi ya taifa hilo ilikuwa vita, na makuhani walichochea vita daima.” Basi yafaa kwamba Nahumu, nabii wa Biblia, alifafanua Ninawi, jiji kuu la Ashuru, kuwa “mji wa damu.”—Nahumu 3:1.
4. Waashuri walitiaje hofu katika mioyo ya mataifa mengine?
4 Mbinu za kivita za Waashuri zilikuwa zenye ukatili usio wa kawaida. Mawe yaliyochongwa ya nyakati hizo yaonyesha wapiganaji Waashuri wakitwaa mateka kwa kutumia kulabu zilizotiwa puani au midomoni. Walitumia mikuki kuwapofusha baadhi ya mateka. Mwandiko mmoja wasema kuhusu ushindi fulani ambapo jeshi la Ashuru liliwakata mateka wake vipande-vipande na kujenga vilima viwili nje ya jiji—kimoja cha vichwa na kingine cha miguu na mikono. Watoto wa washinde walichomwa kwa moto. Hapana budi kwamba hofu iliyotokezwa na ukatili huo iliwasaidia Waashuri kijeshi, kwa kuwa iliwavunja moyo wale waliopinga majeshi yao.
Vita Dhidi ya Ashdodi
5. Ni nani aliyekuwa mtawala Mwashuri mwenye nguvu katika siku ya Isaya, na masimulizi ya Biblia kumhusu yalithibitishwaje?
5 Katika siku ya Isaya, Milki ya Ashuru ilikuwa na nguvu isiyo na kifani chini ya Mfalme Sargoni.a Kwa miaka mingi, wahakiki walitilia shaka kuwepo kwa mtawala huyo, kwa maana hawakufahamu juu ya mtajo wowote kumhusu katika maandishi ya kilimwengu. Hata hivyo, baada ya muda, waakiolojia walivumbua magofu ya jumba la kifalme la Sargoni, hivyo basi masimulizi ya Biblia yakathibitishwa.
6, 7. (a) Huenda ni kwa nini Sargoni aamuru Ashdodi lishambuliwe? (b) Kuanguka kwa Ashdodi kwaathirije jirani za Ufilisti?
6 Isaya aelezea kifupi kuhusu mojawapo ya vita vya kijeshi vya Sargoni: “Jemadari yule alipofika Ashdodi, alipotumwa na Sargoni mfalme wa Ashuru; naye alipigana na Ashdodi akautwaa.” (Isaya 20:1)b Kwa nini Sargoni aamuru Ashdodi, jiji la Wafilisti, lishambuliwe? Sababu moja ni kwamba Ufilisti yashirikiana na Misri, na Ashdodi, makao ya hekalu la Dagoni, liko kwenye barabara inayopita kandokando ya pwani kutoka Misri hadi Palestina. Kwa hiyo jiji hilo lipo mahali muhimu sana. Iwapo latekwa, hiyo yaweza kuonwa kuwa hatua ya mwanzo-mwanzo ya kushinda Misri. Kwa kuongezea, rekodi za Ashuru zaripoti kuwa Azuri, mfalme wa Ashdodi, alikuwa akipanga njama dhidi ya Ashuru. Basi, Sargoni amwondoa mfalme huyo mwenye kuasi naye amweka Ahimiti, ndugu mdogo wa mfalme huyo, kwenye kiti cha ufalme. Hata hivyo, hilo halitatui matatizo. Uasi mwingine wazuka, na mara hii Sargoni achukua hatua kali zaidi. Aamuru Ashdodi lishambuliwe, nalo lazingirwa na kushindwa. Labda andiko la Isaya 20:1 larejezea tukio hilo.
7 Kuanguka kwa Ashdodi ni tisho kwa jirani zake, hasa kwa Yuda. Yehova ajua kuwa watu wake wana mwelekeo wa kutegemea “mkono wa nyama,” kama vile Misri au Ethiopia zilizo upande wa kusini. Basi, amtuma Isaya aigize onyo kali.—2 Mambo ya Nyakati 32:7, 8.
‘Aenda Uchi, Miguu Haina Viatu’
8. Isaya atekeleza igizo gani lililopuliziwa la unabii?
8 Yehova amwambia Isaya: “Haya, uvue nguo ya magunia viunoni mwako, na viatu vyako miguuni mwako.” Isaya atii amri ya Yehova. “Naye akafanya hivyo akaenda uchi, miguu yake haina viatu.” (Isaya 20:2, 3a) Nguo ya magunia ni vazi lenye kukwaruza ambalo mara nyingi huvaliwa na manabii, wakati mwingine kwa kufungamana na ujumbe wenye onyo. Hiyo pia huvaliwa katika nyakati zenye hatari au mtu asikiapo habari za misiba. (2 Wafalme 19:2; Zaburi 35:13; Danieli 9:3) Je, Isaya kweli atembea uchi kabisa bila vazi lolote lile? Si lazima iwe hivyo. Neno la Kiebrania lililotafsiriwa “uchi” laweza pia kurejezea kutovaa kikamili au kuvaa nguo chache. (1 Samweli 19:24, NW, kielezi-chini) Basi huenda Isaya alivua tu vazi lake la nje, naye akabaki na vazi fupi la ndani. Mara nyingi mateka wa kiume huonyeshwa namna hiyo katika michongo ya Waashuri.
9. Tendo la Isaya lina maana gani ya unabii?
9 Maana ya tendo la Isaya lisilo la kawaida haikosi kufafanuliwa: “BWANA akasema, Kama vile mtumishi wangu Isaya anavyokwenda uchi, hana viatu, awe ishara na ajabu kwa muda wa miaka mitatu juu ya Misri na juu ya Kushi; vivyo hivyo mfalme wa Ashuru atawachukua uchi, wafungwa wa Misri, na watu wa Kushi [“Ethiopia,” “NW”] waliohamishwa, watoto kwa wazee, hawana viatu, matako yao wazi, Misri iaibishwe.” (Isaya 20:3b, 4) Naam, karibuni Wamisri na Waethiopia watachukuliwa mateka. Hakuna yeyote atakayeokoka. Hata “watoto kwa wazee” watanyang’anywa mali zao zote na kupelekwa uhamishoni. Kwa kutumia mfano huo wenye kukatisha tamaa, Yehova awaonya wakazi wa Yuda kwamba itakuwa kazi bure kwao kutumaini Misri na Ethiopia. Anguko la mataifa hayo litasababisha “uchi” kwao—aibu kubwa sana kwao!
Matumaini Yaangamia, Utukufu Wafifia
10, 11. (a) Watu wa Yuda wataitikiaje watambuapo kuwa Misri na Ethiopia hazina uwezo wa kukabili Ashuru? (b) Kwa nini huenda wakazi wa Yuda wakawa na mwelekeo wa kutumaini Misri na Ethiopia?
10 Kisha, Yehova atoa ufafanuzi wa unabii juu ya itikio la watu wake watambuapo kuwa Misri na Ethiopia, ambazo ni kimbilio wanalotumaini, hazina uwezo mbele ya Waashuri. “Watafadhaika, na kuona haya kwa ajili ya Kushi [“Ethiopia,” “NW”], matumaini yao, na Misri, utukufu wao. Na mwenyeji wa nchi ya pwani atasema katika siku hiyo, Angalia, haya ndiyo yaliyowapata watu wale tuliowatumaini, ambao tuliwakimbilia watuokoe na mfalme wa Ashuru; na sisi je! twawezaje kupona?”—Isaya 20:5, 6.
11 Yuda ni kama tu nchi nyembamba ya pwani ikilinganishwa na serikali za Misri na Ethiopia. Labda baadhi ya wakazi wa “nchi [hiyo] ya pwani” wasisimuliwa na utukufu wa Misri—piramidi zake zenye kuvutia, mahekalu yake marefu, na nyumba zake kubwa zinazozungukwa na bustani, mashamba ya matunda, na madimbwi. Usanifu wa majengo ya Misri wenye utukufu waonekana kuwa uthibitisho wa hali ya utulivu na hali ya kudumu. Kwa hakika nchi hiyo haiwezi kuharibiwa! Labda Wayahudi pia wavutiwa na wapiga-mishale, magari, na wapanda-farasi wa Ethiopia.
12. Yuda apaswa kumtumaini nani?
12 Kwa kuzingatia onyo la Isaya lililoigizwa na pia maneno ya Yehova ya unabii, yeyote anayedai kuwa mtu wa Mungu na ambaye ana mwelekeo wa kutumaini Misri na Ethiopia apasa kufikiri kwa uzito. Ni bora kama nini amtumaini Yehova badala ya binadamu wa dunia! (Zaburi 25:2; 40:4) Mambo yazidipo kudhihirika, Yuda ateseka vibaya sana mikononi mwa mfalme wa Ashuru, na baadaye, aona Babiloni ikiharibu hekalu na jiji lake kuu. Ingawa hivyo, “moja katika sehemu kumi,” “mbegu takatifu,” yabaki, kama shina la mti mkubwa. (Isaya 6:13) Wakati ufikapo, ujumbe wa Isaya utaimarisha sana imani ya kikundi hicho kidogo kinachoendelea kumtumaini Yehova!
Mtumaini Yehova
13. Ni mibano gani inayowakabili watu wote—wenye kuamini na vilevile wasioamini—leo?
13 Onyo katika Isaya kuhusu ubatili wa kutumaini Misri na Ethiopia si historia tu isiyo na maana. Hilo ni lenye thamani inayotumika leo. Twaishi katika “nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo.” (2 Timotheo 3:1) Kuharibika kwa mambo ya kifedha, umaskini ulioenea sana, misukosuko ya kisiasa, machafuko ya kijamii, na vita vidogo au vikubwa vimeathiri vibaya sana wale wanaodhihaki utawala wa Mungu na vilevile wale wanaomwabudu Yehova. Swali linalomkabili kila mmoja wetu ni, ‘Nitapata msaada kutoka kwa nani?’
14. Kwa nini twapaswa kumtumaini Yehova pekee?
14 Huenda wengine wakavutiwa na watu wa leo wenye uwezo wa kifedha, wanasiasa, na wanasayansi, wanaopiga domo kuhusu kutatua matatizo ya mwanadamu kwa kutumia utaalamu na tekinolojia ya mwanadamu. Hata hivyo, Biblia yasema waziwazi hivi: “Ni heri kumkimbilia BWANA. Kuliko kuwatumainia wakuu.” (Zaburi 118:9) Mbinu zote za mwanadamu za kuleta amani na usalama hazitafaulu kwa sababu ya jambo lililotaarifiwa na nabii Yeremia: “Ee BWANA, najua ya kuwa njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu.”—Yeremia 10:23.
15. Tumaini pekee kwa wanadamu wenye taabu liko wapi?
15 Basi, ni lazima watumishi wote wa Mungu wasivutiwe isivyofaa na mambo yaonekanayo kuwa yenye nguvu au yenye hekima ya ulimwengu huu. (Zaburi 33:10; 1 Wakorintho 3:19, 20) Tumaini pekee kwa wanadamu wenye taabu lategemea Muumba, Yehova. Wale wanaomtumaini wataokolewa. Kama mtume Yohana mwenye kupuliziwa alivyoandika, “ulimwengu unapitilia mbali na ndivyo na tamaa yao, lakini yeye ambaye hufanya mapenzi ya Mungu hudumu milele.”—1 Yohana 2:17.
[Maelezo ya Chini]
a Wanahistoria humrejezea mfalme huyo kuwa Sargoni wa Pili. Mfalme wa mapema zaidi, asiye wa Ashuru, bali wa Babiloni, aitwa “Sargoni wa Kwanza.”
b “Jemadari” ni jina la cheo linalorejezea amiri jeshi mkuu wa jeshi la Ashuru, ambaye labda ndiye mtu wa pili mwenye uwezo mkubwa zaidi katika milki hiyo.
[Picha katika ukurasa wa 209]
Waashuri walikuwa na kawaida ya kuwapofusha baadhi ya mateka wao
[Picha katika ukurasa wa 213]
Huenda watu fulani wakavutiwa na mafanikio ya mwanadamu, lakini ni afadhali kumtumaini Yehova