Sura ya 20
Yehova Ni Mfalme
1, 2. (a) Ni nani watakaopata hasira ya kisasi ya Yehova? (b) Je, Yuda itaepuka adhabu, nasi twajuaje?
BABILONI, Ufilisti, Moabu, Siria, Ethiopia, Misri, Edomu, Tiro, Ashuru—zote zitapata hasira ya kisasi ya Yehova. Isaya ametabiri misiba itakayoyakumba mataifa na majiji hayo yenye uhasama. Hata hivyo, itakuwaje kwa Yuda? Je, wakazi wa Yuda wataepuka adhabu ya njia zao zenye dhambi? Rekodi ya kihistoria yajibu, la hasha!
2 Fikiria lililotukia Samaria, jiji kuu la ufalme wa Israeli wa makabila kumi. Taifa hilo halikushika agano kati yake na Mungu. Halikujitenga na mazoea machafu ya mataifa jirani. Badala yake, wakazi wa Samaria ‘waliunda mambo mabaya ili wamkasirishe BWANA . . . Kwa hiyo BWANA akawaghadhibikia Israeli sana, akawahamisha mbali na uso wake.’ Baada ya kung’olewa nchini mwao, “Waisraeli walichukuliwa mateka kutoka nchi yao wenyewe, waende nchi ya Ashuru.” (2 Wafalme 17:9-12, 16-18, 23; Hosea 4:12-14) Mambo yaliyoikumba Israeli ni ishara ya mabaya kwa ufalme jirani wa Yuda.
Isaya Atabiri Ukiwa wa Yuda
3. (a) Kwa nini Yehova auacha ufalme wa Yuda wa makabila mawili? (b) Yehova ameazimia kufanya nini?
3 Wafalme kadhaa wa Yuda walikuwa waaminifu, lakini wengi hawakuwa waaminifu. Hata chini ya wafalme waaminifu, kama vile Yothamu, watu hawakuachilia mbali kabisa ibada isiyo ya kweli. (2 Wafalme 15:32-35) Uovu wa Yuda wafikia kilele wakati wa utawala wa Mfalme Manase mwenye tamaa ya kumwaga damu ambaye, kwa mujibu wa mapokeo ya Kiyahudi, amwua nabii Isaya mwaminifu kwa kuamuru akatwe vipande-vipande kwa msumeno. (Linganisha Waebrania 11:37.) Mfalme huyo mwovu “akawakosesha Yuda na wenyeji wa Yerusalemu, hata wakazidi kufanya mabaya kuliko mataifa, aliowaharibu BWANA mbele ya wana wa Israeli.” (2 Mambo ya Nyakati 33:9) Chini ya utawala wa Manase, nchi yachafuliwa hata zaidi kuliko wakati Wakanaani walipoitawala. Basi, Yehova atangaza: “Angalia, naleta mabaya juu ya Yerusalemu na juu ya Yuda, hata kila mtu asikiaye, masikio yake yatawasha yote mawili. . . . Nami nitaifuta Yerusalemu, kama mtu afutavyo sahani, kuifuta na kuifudikiza. Nami nitawatupa mabaki ya urithi wangu, na kuwatia mikononi mwa adui zao; nao watakuwa nyara na mateka kwa adui zao wote; kwa sababu wametenda yaliyo mabaya machoni pangu, na kunikasirisha.”—2 Wafalme 21:11-15.
4. Yehova ataitendaje Yuda, na unabii huo watimizwaje?
4 Kama vile sahani inayofudikizwa na kumwaga chakula chote, ndivyo watu wote wakaao nchini humo watakavyoondolewa. Ukiwa huo unaokuja juu ya Yuda na Yerusalemu ndio tena habari za unabii wa Isaya. Aanza hivi: “Tazama, BWANA ameifanya dunia kuwa tupu, aifanya ukiwa, aipindua, na kuwatawanya wakaao ndani yake.” (Isaya 24:1) Unabii huo watimizwa wakati majeshi ya Babiloni yanayovamia chini ya Mfalme Nebukadreza yaharibupo Yerusalemu na hekalu lake na kuangamiza wakazi wa Yuda kwa upanga, njaa kuu, na magonjwa ya kuambukiza. Wayahudi wengi wanaosalia wapelekwa mateka huko Babiloni, na wachache wabakio watorokea Misri. Kwa hiyo nchi ya Yuda yaharibiwa na kufanywa ukiwa kabisa. Hata mifugo haibaki. Nchi hiyo iliyohamwa yawa nyika ya magofu yenye kusononesha yakaliwayo na wanyama na ndege wa mwituni.
5. Je, yeyote ataepuka hukumu ya Yehova? Eleza.
5 Je, yeyote huko Yuda atapendelewa wakati wa hukumu inayokuja? Isaya ajibu: “Itakuwa kama ilivyo hali ya watu, ndivyo itakavyokuwa hali ya kuhani; kama ilivyo hali ya mtumwa, ndivyo itakavyokuwa hali ya bwana wake; kama ilivyo hali ya mjakazi, ndivyo itakavyokuwa hali ya bibi yake; kama ilivyo hali yake anunuaye, ndivyo itakavyokuwa hali yake auzaye; kama ilivyo hali yake akopeshaye, ndivyo itakavyokuwa hali yake akopaye; kama ilivyo hali yake atwaaye faida, ndivyo itakavyokuwa hali yake ampaye faida. Dunia hii itafanywa tupu kabisa, na kuharibiwa kabisa; maana BWANA amenena neno hilo.” (Isaya 24:2, 3) Mali na mapendeleo ya utumishi hekaluni hayatabadili hali. Hakuna upendeleo wowote. Nchi imefisidiwa sana hivi kwamba kila mtu—makuhani, watumishi na mabwana, wanunuzi na wauzaji—sharti waende uhamishoni.
6. Kwa nini Yehova aiondoa baraka yake nchini humo?
6 Ili yeyote asikose kuelewa, Isaya afafanua kwa ukamili msiba huo unaokuja naye aeleza sababu yake: “Dunia inaomboleza, inazimia; ulimwengu unadhoofika, unazimia; watu wakuu wa dunia wanadhoofika. Tena dunia imetiwa unajisi kwa watu wanaoikaa; kwa maana wameziasi sheria, wameibadili amri, wamelivunja agano la milele. Ndiyo sababu laana imeila dunia hii, na hao wanaoikaa wameonekana kuwa na hatia, ndiyo sababu watu wanaoikaa dunia wameteketea, watu waliosalia wakawa wachache tu.” (Isaya 24:4-6) Waisraeli walipopewa nchi ya Kanaani, ilikuwa “nchi imiminikayo maziwa na asali.” (Kumbukumbu la Torati 27:3) Licha ya hayo, waliendelea kuitegemea baraka ya Yehova. Iwapo wangeshika amri na maagizo yake kwa uaminifu, nchi ‘ingezaa mazao yake,’ lakini iwapo wangeziasi sheria na amri zake, jitihada zao za kulima nchi ‘zingetumiwa bure’ na nchi ‘haingezaa mazao yake.’ (Mambo ya Walawi 26:3-5, 14, 15, 20) Laana ya Yehova ‘ingeila nchi hiyo.’ (Kumbukumbu la Torati 28:15-20, 38-42, 62, 63) Basi Yuda lazima itarajie kupatwa na laana hiyo.
7. Agano la Sheria lingekuwaje baraka kwa Waisraeli?
7 Miaka ipatayo 800 kabla ya siku ya Isaya, Waisraeli walifanya uhusiano wa agano na Yehova kwa hiari, nao wakakubali kushikamana nalo. (Kutoka 24:3-8) Masharti ya agano la Sheria yalisema kuwa iwapo wangetii sheria za Yehova, wangepata baraka zake tele lakini iwapo wangekiuka agano hilo, wangepoteza baraka zake na adui zao wawatwae mateka. (Kutoka 19:5, 6; Kumbukumbu la Torati 28:1-68) Agano hilo la Sheria, lililotolewa kupitia Musa, lingetumika kwa muda usio dhahiri. Lingewalinda Waisraeli hadi kufika kwa Mesiya.—Wagalatia 3:19, 24.
8. (a) Watu ‘wameziasije sheria’ na ‘kuibadili amri’? (b) “Wakuu” wanakuwa wa kwanza ‘kudhoofika’ kwa njia zipi?
8 Lakini watu “wamelivunja agano la milele.” Wameziasi sheria za Mungu, wakizipuuza. “Wameibadili amri,” wakifuata mazoea ya sheria tofauti na zile ambazo Yehova alitoa. (Kutoka 22:25; Ezekieli 22:12) Basi, watu hao wataondolewa nchini humo. Hukumu inayokuja haitakuwa na rehema yoyote. ‘Watakaodhoofika’ kwanza baada ya Yehova kuondoa ulinzi na upendeleo wake ni “wakuu,” watu mashuhuri. Kwa utimizo wa hayo, uharibifu wa Yerusalemu ukaribiapo, kwanza Wamisri wawafanya wafalme wa Yuda kuwa vibaraka wao, kisha Wababiloni nao wafanya vivyo hivyo. Baadaye, Mfalme Yekonia na washiriki wengineo wa familia ya kifalme ni miongoni mwa watu wa kwanza kupelekwa utekwani Babiloni.—2 Mambo ya Nyakati 36:4, 9, 10.
Furaha Yatoweka Nchini
9, 10. (a) Kilimo chatimiza fungu gani katika Israeli? (b) Yamaanisha nini kila mtu ‘kukaa chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake’?
9 Taifa la Israeli ni jamii ya wakulima. Tangu Waisraeli walipoingia katika Bara Lililoahidiwa, wameanza maisha ya ukulima na ufugaji. Basi, sehemu kubwa ya sheria zilizotolewa kwa Israeli yahusu kilimo. Amri yatolewa kuhusu pumziko la sabato kwa nchi kila mwaka wa saba ili rutuba ipate kurejea udongoni. (Kutoka 23:10, 11; Mambo ya Walawi 25:3-7) Misherehekeo mitatu ya kila mwaka ambayo taifa laamriwa kusherehekea yaratibiwa kufungamana na misimu ya kilimo.—Kutoka 23:14-16.
10 Mashamba ya mizabibu yamejaa nchini mwote. Maandiko huonyesha divai, zao la mzabibu, kuwa zawadi kutoka kwa Mungu ‘inayomfurahisha mtu moyo wake.’ (Zaburi 104:15) Kila mtu ‘kukaa chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake,’ humaanisha kuna ufanisi, amani, na usalama chini ya utawala mwadilifu wa Mungu. (1 Wafalme 4:25; Mika 4:4) Msimu mwema wa divai huonwa kuwa baraka nao ni chanzo cha kuimba na kufurahi. (Waamuzi 9:27; Yeremia 25:30) Kama sivyo mambo ni kinyume. Mizabibu inaponyauka au kukosa kuzaa zabibu na mashamba ya mizabibu yanapogeuka kuwa na mimea ovyo ya miiba, ni uthibitisho kwamba Yehova ameiondoa baraka yake—wakati wa huzuni kubwa.
11, 12. (a) Isaya atumiaje mashamba ya mizabibu na mazao yake kutoa kielezi cha hali zitakazotokana na hukumu ya Yehova? (b) Isaya afafanua matazamio gani yenye huzuni?
11 Kwa kufaa basi, Isaya atumia mashamba ya mizabibu na mazao yake kutoa kielezi cha hali zinazotokana na kuondolewa kwa baraka ya Yehova nchini: “Divai mpya inaomboleza, mzabibu umedhoofika, watu wote waliochangamka moyo wanaugua. Sauti ya furaha ya matoazi inakoma; kelele yao wafurahio imekwisha; furaha ya kinubi inakoma. Hawatakunywa divai pamoja na nyimbo; kileo kitakuwa uchungu kwao wakinywao. Mji wa machafuko umebomolewa; kila nyumba imefungwa, asipate kuingia mtu awaye yote. Pana kilio katika njia kuu kwa sababu ya divai; furaha yote imetiwa giza, na changamko la nchi limetoweka. Ndani ya mji umebaki ukiwa, na lango lake limepigwa kwa uharibifu.”—Isaya 24:7-12.
12 Matoazi na vinubi ni vyombo vizuri vinavyotumiwa kumsifu Yehova na kuonyesha furaha. (2 Mambo ya Nyakati 29:25; Zaburi 81:2) Nyimbo zake hazitasikika wakati huu wa hukumu ya Mungu. Hakutakuwapo mavuno yenye furaha ya zabibu. Hakutakuwapo sauti zenye furaha katika magofu ya Yerusalemu, lango lake likiwa “limepigwa kwa uharibifu” na nyumba zake zikiwa ‘zimefungwa,’ asipate kuingia mtu awaye yote. Hayo ni matazamio yenye huzuni kama nini kwa wakazi wa nchi ambayo kwa kawaida ni yenye rutuba!
Mabaki ‘Wapaza Sauti kwa Furaha’
13, 14. (a) Yehova ametoa sheria zipi zinazohusu kuvuna? (b) Isaya atumiaje sheria zinazohusu kuvuna ili kutoa kielezi kwamba watu fulani wataokoka hukumu ya Yehova? (c) Ingawa misimu yenye huzuni ya majaribu inakuja, Wayudea waaminifu waweza kuwa na uhakika gani?
13 Wanapovuna zeituni, Waisraeli hupiga miti kwa fito ndipo matunda yaanguke. Kulingana na Sheria ya Mungu, hawaruhusiwi kupanda matawi ya miti ili kuvuna zeituni zilizobakia. Wala hawapaswi kukusanya zabibu zilizobaki baada ya kuvuna mashamba yao ya mizabibu. Mabaki ya mavuno yapasa kuachiwa maskini—ili “mgeni, na yatima, na mjane”—wayaokote. (Kumbukumbu la Torati 24:19-21) Kwa kutumia sheria hizo zinazojulikana vema, Isaya atoa kielezi cha jambo linalofariji kwamba kutakuwapo watakaookoka hukumu ya Yehova inayokuja: “Maana katikati ya dunia, katikati ya mataifa, itakuwa hivi; kama wakati utikiswapo mzeituni, kama wakati waokotapo zabibu baada ya mavuno yake. Hawa watainua sauti zao, watapiga kelele [“watapaza sauti kwa furaha” “NW”]; kwa sababu ya utukufu wa BWANA watapiga kelele toka baharini. Basi, mtukuzeni BWANA katika mashariki, litukuzeni jina la BWANA, Mungu wa Israeli, katika visiwa vya bahari. Toka pande za mwisho wa dunia tumesikia nyimbo, Atukuzwe mwenye haki”!—Isaya 24:13-16a.
14 Kama vile matunda fulani hubaki mtini au kwenye mzabibu baada ya mavuno, vivyo hivyo kutakuwapo watu fulani watakaobaki baada ya Yehova kutekeleza hukumu yake—“waokotapo zabibu baada ya mavuno yake.” Kama ilivyorekodiwa kwenye mstari wa 6, tayari nabii amewataja, akisema “watu waliosalia wakawa wachache tu.” Lakini, hata kama ni wachache, kutakuwapo watakaookoka uharibifu wa Yerusalemu na Yuda, na baadaye mabaki watarudi kutoka utekwani ili kuijaza nchi tena. (Isaya 4:2, 3; 14:1-5) Ingawa wanyofu wa moyo watapitia misimu ya majaribu, waweza kuwa na hakika kwamba kutakuwapo ukombozi na furaha wakati ujao. Wenye kuokoka wataona neno la unabii la Yehova likiendelea kuwa wazi nao watatambua kwamba Isaya amekuwa nabii wa kweli wa Mungu. Watajawa na furaha waonapo utimizo wa unabii mbalimbali wa urudisho. Toka kokote kule walikotawanyika—iwe katika visiwa vya Mediterania upande wa Magharibi, Babiloni katika Mashariki, au mahali pengine popote palipo mbali—watamsifu Mungu kwa sababu wameokolewa, nao wataimba: “Atukuzwe Mwenye Haki”!
Hakuna Kuponyoka Hukumu ya Yehova
15, 16. (a) Isaya ahisije juu ya mambo yatakayowapata watu wake? (b) Ni mambo gani yatawakumba wakazi wasio waaminifu nchini humo?
15 Hata hivyo, ni mapema mno kufurahi sasa. Isaya awaleta watu wa siku yake kwenye hali iliyopo, akitaarifu: “Ndipo niliposema, Kukonda kwangu! kukonda kwangu! ole wangu! Watenda hila wametenda hila, naam, watendao hila wametenda hila sana. Hofu, na shimo, na mtego, vi juu yako, Ee mwenye kukaa duniani. Itakuwa kila akimbiaye sauti ya hofu ataanguka katika shimo; na kila apandaye na kutoka shimoni atanaswa na mtego; kwa maana madirisha yaliyo juu yamewekwa wazi, na misingi ya dunia inatikisika. Dunia kuvunjika, inavunjika sana; dunia kupasuka, imepasuka sana; dunia kutikisika, imetikisika sana. Dunia inalewa-lewa kama mlevi, nayo inawaya-waya kama machela; na mzigo wa dhambi zake utailemea; nayo itaanguka, wala haitainuka tena.”—Isaya 24:16b-20.
16 Isaya ahuzunika sana kwa sababu ya mambo yatakayowapata watu wake. Hali ya mambo inayomzunguka yamfanya awe na hisia za ugonjwa na ole. Watendao hila wamejaa nao wasababisha hofu kwa wakazi nchini humo. Yehova atakapoondoa ulinzi wake, wakazi wa Yuda wasio waaminifu watapata hofu mchana na usiku. Maisha yao yatakuwa mashakani. Haitawezekana kuponyoka msiba utakaowakumba kwa sababu ya kuziacha amri za Yehova na kuipuuza hekima yake. (Mithali 1:24-27) Maafa yatakuja hata kama watendao hila nchini humo, wanaojaribu kuwashawishi watu kwamba kila jambo litakuwa sawasawa, watumia maneno yasiyo ya kweli na udanganyifu ili kuwaongoza kwenye uharibifu. (Yeremia 27:9-15) Adui kutoka nje wataingia na kuwapora na kuwateka nyara. Hayo yote yamtaabisha sana Isaya.
17. (a) Kwa nini haitawezekana kuponyoka? (b) Nguvu za hukumu ya Yehova ziachiliwapo kutoka mbinguni, ni nini kitakachotukia nchini?
17 Ijapokuwa hivyo, ni lazima nabii atangaze kuwa haitawezekana kuponyoka. Kokote watakakojaribu kukimbilia watu, watakamatwa. Huenda wengine wakaponyoka msiba mmoja, lakini watanaswa katika mwingine—usalama hautakuwapo. Itakuwa kama mnyama aepukaye kuanguka shimoni, kisha anaswa mtegoni. (Linganisha Amosi 5:18, 19.) Nguvu za hukumu ya Yehova zitaachiliwa kutoka mbinguni nazo zitatikisa misingi ya nchi. Kama mlevi, nchi inalewa-lewa na kuanguka, huku imelemewa na mzigo wa dhambi isiweze kuinuka tena. (Amosi 5:2) Hukumu ya Yehova ni ya kukata maneno. Uharibifu na ukiwa kamili zitaikumba nchi.
Yehova Atamiliki kwa Utukufu
18, 19. (a) Huenda usemi “jeshi la mahali palipo juu” warejezea nani, nao wakusanywaje “katika shimo”? (b) Huenda “jeshi la mahali palipo juu” litazingatiwaje “baada ya muda wa siku nyingi”? (c) Yehova awazingatiaje “wafalme wa dunia”?
18 Unabii wa Isaya sasa watia ndani mambo mengi zaidi, ukitaja utekelezaji wa mwisho wa kusudi la Yehova: “Itakuwa katika siku hiyo, BWANA ataliadhibu jeshi la mahali palipo juu katika mahali palipo juu, na wafalme wa dunia katika dunia; nao watakusanywa pamoja kama vile wakusanywavyo wafungwa katika shimo nao watafungwa katika gereza; na baada ya muda wa siku nyingi watajiliwa. Ndipo mwezi utatahayari, na jua litaona haya; kwa kuwa BWANA wa majeshi atatawala katika mlima wa Sayuni, na katika Yerusalemu, na mbele ya wazee wake kwa utukufu.”—Isaya 24:21-23.
19 Huenda usemi “jeshi la mahali palipo juu” warejezea roho waovu walio “watawala wa ulimwengu wa giza hili, . . . majeshi ya roho waovu katika mahali pa kimbingu.” (Waefeso 6:12) Hao wameathiri sana serikali za ulimwengu. (Danieli 10:13, 20; 1 Yohana 5:19) Lengo lao ni kuwageuza watu kutoka kwa Yehova na ibada yake safi. Wao wafaulu kama nini kushawishi Israeli kufuata mazoea machafu ya mataifa yanayowazunguka na hivyo wastahili hukumu ya Mungu! Lakini hatimaye ni lazima Shetani na roho wake waovu watoe hesabu kwa Mungu ageuzapo uangalifu wake kwao na kwa watawala wa dunia, “wafalme wa dunia katika dunia,” ambao wamewashawishi wamwache Mungu na kuvunja sheria zake. (Ufunuo 16:13, 14) Akizungumza kwa mfano, Isaya asema kwamba watakusanywa na ‘kufungwa katika gereza.’ “Baada ya muda wa siku nyingi,” labda Shetani na roho wake waovu (lakini si “wafalme wa dunia katika dunia”) waachiliwapo kwa muda mfupi mwishoni mwa Utawala wa Miaka Elfu wa Yesu Kristo, Mungu atawapa adhabu ya mwisho inayowafaa.—Ufunuo 20:3, 7-10.
20. Katika nyakati za kale na leo vilevile, Yehova ‘anakuwa mfalme’ jinsi gani na lini?
20 Basi sehemu hiyo ya unabii wa Isaya iliwaacha Wayahudi wakiwa na uhakikisho mzuri sana. Katika wakati wa Yehova ufaao, angesababisha kuanguka kwa Babiloni la kale na kuwarudisha Wayahudi nchini kwao. Mwaka wa 537 K.W.K., aonyeshapo nguvu zake na enzi yake kuu kwa niaba ya watu wake, ingeweza kusemwa kikweli kuwahusu: “Mungu wako anamiliki [“amekuwa mfalme,” NW]!” (Isaya 52:7) Leo, Yehova ‘alikuwa mfalme’ mwaka wa 1914 alipomweka Yesu Kristo kuwa Mfalme katika Ufalme Wake wa mbinguni. (Zaburi 96:10) Pia, ‘alikuwa mfalme’ mwaka wa 1919 alipoonyesha nguvu zake za kifalme kwa kuwakomboa Israeli wa kiroho kutoka utumwa wa Babiloni Mkubwa.
21. (a) ‘Mwezi utatahayari jinsi gani, nalo jua litaonaje haya’? (b) Ni mwito gani unaosikika kote utakaokuwa na utimizo wake mkuu?
21 Yehova ‘atakuwa mfalme’ tena amwangamizapo Babiloni Mkubwa na sehemu iliyobaki ya mfumo huu mwovu wa mambo. (Zekaria 14:9; Ufunuo 19:1, 2, 19-21) Baadaye, utawala wa Ufalme wa Yehova utakuwa mtukufu sana hivi kwamba mwezi unaomulika usiku na jua lenye kung’aa adhuhuri hazitaufikia kwa utukufu. (Linganisha Ufunuo 22:5.) Kitamathali, jua na mwezi zitaona haya kujilinganisha na utukufu wa Yehova wa majeshi. Utawala wa Yehova utakuwa mkuu kuliko zote. Wote wataziona nguvu zake na utukufu wake mkuu. (Ufunuo 4:8-11; 5:13, 14) Hilo ni tazamio zuri kama nini! Wakati huo, mwito wa Zaburi 97:1 utasikika duniani kote katika utimizo wake mkuu: “BWANA [“Yehova,” NW] ametamalaki [“amekuwa mfalme,” NW], nchi na ishangilie. Visiwa vingi na vifurahi.”
[Picha katika ukurasa wa 262]
Nyimbo na furaha hazitasikika tena nchini
[Picha katika ukurasa wa 265]
Watu fulani wataokoka hukumu ya Yehova, kama vile matunda yanavyobaki mtini baada ya mavuno
[Picha katika ukurasa wa 267]
Isaya ahuzunika juu ya jambo litakalowapata watu wake
[Picha katika ukurasa wa 269]
Wala jua wala mwezi hazitafikia utukufu wa Yehova