Sura ya 23
Endelea Kumngojea Yehova
1, 2. (a) Isaya sura ya 30 yazungumzia nini? (b) Sasa tutachunguza maswali gani?
KATIKA Isaya sura ya 30, twasoma juu ya matangazo zaidi kutoka kwa Mungu dhidi ya waovu. Hata hivyo, sehemu hii ya unabii wa Isaya yakazia baadhi ya sifa za Yehova zenye kusisimua. Kwa kweli, sifa za Yehova zafafanuliwa waziwazi hivi kwamba twaweza kuona kitamathali kuwapo kwake kunakofariji, kusikia sauti yake ya kuongoza, na kuhisi mguso wake wenye kuponya.—Isaya 30:20, 21, 26.
2 Ijapokuwa hivyo, wenzi wa Isaya, wakazi waasi wa Yuda, wakataa kumrudia Yehova. Badala yake, wanamtumaini mwanadamu. Yehova aonaje jambo hilo? Na sehemu hiyo ya unabii wa Isaya yawasaidiaje Wakristo leo kuendelea kumngojea Yehova? (Isaya 30:18) Hebu tuone.
Upumbavu na Kuelekea Msiba
3. Yehova afichua njama gani?
3 Kwa muda fulani, viongozi wa Yuda wamekuwa wakipanga njama kisiri ya kutafuta njia ya kuepuka kuwa chini ya nira ya Ashuru. Hata hivyo, Yehova amekuwa akiwatazama. Sasa aifichua njama yao: “Ole wa watoto waasi; asema BWANA; watakao mashauri lakini hawayataki kwangu mimi; wajifunikao kifuniko lakini si cha roho yangu; wapate kuongeza dhambi juu ya dhambi; waendao kutelemkia Misri.”—Isaya 30:1, 2a.
4. Watu wa Mungu walio waasi wameifanyaje Misri kuwa badala ya Mungu?
4 Viongozi wanaopanga njama washtuka kama nini wasikiapo njama yao ikifichuliwa! Kusafiri hadi Misri ili kufanya mwungano nayo, mbali na kuwa uchokozi dhidi ya Ashuru, ni uasi dhidi ya Yehova Mungu. Wakati wa Mfalme Daudi, taifa hilo lilimtegemea Yehova kama ngome nalo likakimbilia ‘uvuli wa mbawa zake.’ (Zaburi 27:1; 36:7) Sasa ‘wanajitia nguvu kwa nguvu za Farao’ na “kutumainia kivuli cha Misri.” (Isaya 30:2b) Wameifanya Misri kuwa badala ya Mungu! Huo ni uhaini ulioje!—Soma Isaya 30:3-5.
5, 6. (a) Kwa nini kuungana na Misri ni kosa lenye kusababisha kifo? (b) Ni safari gani ya mapema waliyofunga watu wa Mungu ikaziayo upumbavu wa safari hii ya kwenda Misri?
5 Isaya atoa habari zaidi, kana kwamba anajibu wazo lolote la kwamba safari hiyo ya Misri ni ya matembezi tu. “Ufunuo juu ya hayawani wa Negebu. Katikati ya nchi ya taabu na dhiki, ambayo hutoka huko simba jike na simba, nyoka na joka la moto arukaye, huchukua mali zao mabegani mwa punda wachanga, na hazina zao juu ya nundu za ngamia.” (Isaya 30:6a) Ni wazi kwamba safari hiyo imepangwa vema. Wajumbe wapanga msafara wa ngamia na punda, wakiwapakia bidhaa zenye bei ghali na kusafiri hadi Misri kupitia nyika yenye ukiwa iliyojaa simba wanaonguruma na nyoka wenye sumu. Hatimaye, wajumbe wafika waendako na kukabidhi Wamisri hazina zao. Wanadhani kwamba sasa wamejinunulia ulinzi. Hata hivyo, Yehova asema: “Waende kwa watu ambao hawatawafaa kitu. Kwa maana Misri huwasaidia bure, bila faida; kwa hiyo nimemwita, Rahabu aketiye kimya.” (Isaya 30:6b, 7) “Rahabu,” “yule joka,” alifananisha Misri. (Isaya 51:9, 10) Huahidi kila kitu lakini haifanyi lolote. Mwungano kati yake na Yuda ni kosa lenye kusababisha kifo.
6 Isaya afafanuapo safari ya wajumbe hao, huenda watu wanaomsikiliza wakakumbuka safari kama hiyo iliyofanywa siku za Musa. Baba zao wa zamani walitembea katika ‘jangwa hilo kubwa lenye kitisho.’ (Kumbukumbu la Torati 8:14-16) Ingawa hivyo, katika siku ya Musa, Waisraeli walikuwa wakisafiri kutoka Misri na kutoka utumwani. Mara hii wajumbe wanasafiri kwenda Misri na kuingia utumwani hasa. Huo ni upumbavu ulioje! Tusifanye kamwe uamuzi usio wa busara kama huo kwa kubadili uhuru wetu wa kiroho kwa utumwa!—Linganisha Wagalatia 5:1.
Ujumbe wa Nabii Wapingwa
7. Kwa nini Yehova amwambia Isaya aandike onyo Lake kwa Yuda?
7 Yehova amwambia Isaya aandike ujumbe ambao ameutangaza kitambo kidogo ili ‘uwe kwa ajili ya majira yatakayokuja, kwa ushuhuda hata milele.’ (Isaya 30:8) Ni lazima katazo la Yehova dhidi ya kukazia miungano na wanadamu kuliko kumtegemea Yeye lirekodiwe kwa faida ya vizazi vya baadaye—kutia ndani sisi. (2 Petro 3:1-4) Lakini kuna uhitaji wa haraka zaidi wa rekodi iliyoandikwa. “Watu hawa ni watu waasi, watoto wasemao uongo, watoto wasiotaka kuisikia sheria ya BWANA.” (Isaya 30:9) Watu wamekataa shauri la Mungu. Basi, ni lazima iandikwe ili wasikane baadaye kwamba hawakupokea onyo linalofaa.—Mithali 28:9; Isaya 8:1, 2.
8, 9. (a) Viongozi wa Yuda wajaribuje kuwaharibu manabii wa Yehova? (b) Isaya aonyeshaje kwamba hatatishika?
8 Isaya sasa atoa kielelezo cha mtazamo wa uasi wa watu hao. “[Wamewaambia] waonaji, Msione; na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, tuambieni maneno laini, hubirini maneno yadanganyayo.” (Isaya 30:10) Kwa kuwaamuru manabii waaminifu wakome kusema mambo ya “haki,” au ya kweli, na badala yake waseme mambo “laini” na “yadanganyayo,” au yasiyo ya kweli, viongozi wa Yuda waonyesha kuwa wanataka masikio yao yatekenywe. Wanataka kusifiwa, wala si kuhukumiwa. Kwa maoni yao, nabii yeyote asiyetaka kutoa unabii unaowapendeza apaswa ‘kutoka katika njia, ageuke kutoka katika mapito.’ (Isaya 30:11a) Aidha, apaswa kusema mambo yanayopendeza masikio au akome kabisa kuhubiri!
9 Wapinzani wa Isaya wasisitiza: “Mkomesheni Mtakatifu wa Israeli mbele yetu.” (Isaya 30:11b) Isaya na akome kusema katika jina la Yehova, “Mtakatifu wa Israeli”! Jina hilo la cheo lawaudhi hasa kwa sababu viwango vya juu vya Yehova hufichua hali yao mbaya. Isaya atendaje? Yeye atangaza: “Mtakatifu wa Israeli asema hivi.” (Isaya 30:12a) Isaya asema pasipo kusita maneno yaleyale ambayo wapinzani wake wachukia kusikia. Hatatishika. Hicho ni kielelezo kizuri kama nini kwetu! Ni sharti Wakristo wasilegeze kamwe msimamo wao kuhusu kutangaza ujumbe wa Mungu. (Matendo 5:27-29) Sawa na Isaya, wao huendelea kutangaza: ‘Yehova amesema hivi’!
Matokeo ya Uasi
10, 11. Uasi wa Yuda utakuwa na matokeo gani?
10 Yuda imekataa neno la Mungu, ikauamini uwongo, na kuutumainia “ukaidi.” (Isaya 30:12b) Matokeo yatakuwa nini? Badala ya Yehova kuachilia hali kama ilivyo, atalikomesha taifa hilo! Hayo yatatendeka ghafula na kwa ukamilifu, kama Isaya anavyokazia kwa kutumia kielezi. Uasi wa taifa hilo ni kama “mahali palipobomoka, palipo tayari kuanguka patokezapo katika ukuta mrefu, ambapo kuvunjika kwake huja ghafula kwa mara moja.” (Isaya 30:13) Kama vile uvimbe unaozidi kutokeza katika ukuta mrefu usababishavyo hatimaye kuanguka kwa ukuta, ndivyo uasi wa watu wa siku ya Isaya unaozidi kuongezeka utakavyosababisha kuanguka kwa taifa hilo.
11 Kwa kutumia kielezi kingine, Isaya aonyesha ukamilifu wa uharibifu unaokuja: “Atapavunja kama chombo cha mfinyanzi kivunjwavyo, akikivunja-vunja asiache kukivunja, hata hakipatikani katika vipande vyake kigae kitoshacho kutwaa moto jikoni, au kuteka maji kisimani.” (Isaya 30:14) Uharibifu wa Yuda utakuwa kamili sana kiasi cha kutobaki kitu chochote chenye faida—hata kigae kikubwa vya kutosha kutwaa majivu-moto jikoni au kuteka maji kisimani hakitabaki. Kikomo hicho chaaibisha kama nini! Vivyo hivyo, uharibifu unaokuja wa watu wanaoasi dhidi ya ibada ya kweli leo utakuwa wa ghafula na kamili.—Waebrania 6:4-8; 2 Petro 2:1.
Msaada wa Yehova Wakataliwa
12. Watu wa Yuda waweza kuepukaje uharibifu?
12 Ijapokuwa hivyo, watu wanaomsikiliza Isaya waweza kuepuka uharibifu huo. Kuna njia ya kuponyokea. Nabii aeleza: “Bwana MUNGU, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi, Kwa kurudi na kustarehe mtaokolewa; nguvu zenu zitakuwa katika kutulia na kutumaini.” (Isaya 30:15a) Yehova yuko tayari kuwaokoa watu wake—iwapo waonyesha imani kwa “kustarehe,” au kwa kukoma kujaribu kupata wokovu kupitia miungano ya kibinadamu, na kwa “kutulia,” au kwa kuonyesha tumaini katika nguvu za ulinzi za Mungu kwa kutoogopa. “Lakini,” Isaya awaambia watu hao, “hamkukubali.”—Isaya 30:15b.
13. Viongozi wa Yuda watumaini nini, na je, tumaini hilo lastahili?
13 Kisha Isaya afafanua: “Bali ninyi mlisema, La! maana tutakimbia juu ya farasi; basi, ni kweli, mtakimbia; tena, Sisi tutakimbia juu ya wanyama waendao upesi; basi, wale watakaowafuatia watakuwa wepesi.” (Isaya 30:16) Wayudea wanadhani kwamba farasi wenye mbio, badala ya Yehova, ndio watakaowaokoa. (Kumbukumbu la Torati 17:16; Mithali 21:31) Hata hivyo, nabii ajibu kwamba tumaini lao litakuwa ndoto kwa sababu adui zao watawapita. Hata wingi hautawafaidi kitu. “Elfu moja watakimbia kwa kukemewa na mtu mmoja; kwa kukemewa na watano mtakimbia.” (Isaya 30:17a) Majeshi ya Yuda yatajawa na hofu na kukimbia kwa kukemewa na adui wachache tu.a Mwishowe, ni mabaki tu watakaoachwa, wakiwa peke yao, “kama mlingoti juu ya kilele cha mlima, na kama bendera juu ya kilima.” (Isaya 30:17b) Kupatana na unabii huo, jiji la Yerusalemu linapoharibiwa mwaka wa 607 K.W.K., ni mabaki tu wanaosalia.—Yeremia 25:8-11.
Faraja Kati ya Hukumu
14, 15. Maneno ya Isaya 30:18 yawatolea wakazi wa Yuda faraja gani katika nyakati za kale na pia Wakristo wa kweli leo?
14 Maneno hayo yenye kuamsha fikira yanapokuwa yangali masikioni mwa wale wanaomsikiliza Isaya, namna ya ujumbe wake yabadilika. Tisho la msiba labadilika kuwa ahadi ya baraka. “Kwa ajili ya hayo BWANA atangoja, ili awaonee huruma, na kwa ajili ya hayo atatukuzwa [“atainuka,” “BHN”], ili awarehemu; kwa maana BWANA ni Mungu wa hukumu; heri wote wamngojao.” (Isaya 30:18) Maneno hayo yanatia moyo kama nini! Yehova ni Baba mwenye huruma anayetamani kuwasaidia wanawe. Yeye hufurahia kuonyesha rehema.—Zaburi 103:13; Isaya 55:7.
15 Maneno hayo yenye kutia moyo yahusu mabaki Wayahudi ambao kwa rehema waruhusiwa kuokoka uharibifu wa Yerusalemu mwaka wa 607 K.W.K. na wale wachache wanaorudi kwenye Bara Lililoahidiwa mwaka wa 537 K.W.K. Hata hivyo, maneno hayo ya nabii yanawafariji Wakristo leo pia. Twakumbushwa kwamba Yehova “atainuka” kwa niaba yetu na kuukomesha ulimwengu huu mwovu. Waabudu waaminifu waweza kuwa na uhakika kwamba Yehova—“Mungu wa hukumu”—hatauruhusu ulimwengu wa Shetani uendelee kuwapo hata kwa siku moja zaidi kupita ilivyo haki. Basi, wale “wamngojao” wana sababu nyingi za kufurahi.
Yehova Huwafariji Watu Wake kwa Kujibu Sala
16. Yehova huwafariji jinsi gani waliovunjika moyo?
16 Hata hivyo, huenda wengine wakavunjika moyo kwa sababu ukombozi haujaja haraka kama walivyotarajia. (Mithali 13:12; 2 Petro 3:9) Acheni wapate faraja kutokana na maneno yafuatayo ya Isaya, yanayokazia jambo la pekee juu ya utu wa Yehova. “Kwa maana watu watakaa katika Sayuni huko Yerusalemu; wewe hutalia tena; hakika yake atakuonea rehema nyingi kwa sauti ya kilio chako; asikiapo ndipo atakapokujibu.” (Isaya 30:19) Isaya aonyesha wororo kupitia maneno hayo kwa kubadilika kutoka kwa neno la wingi “awaonee” katika mstari wa 18 hadi kwa neno la umoja “wewe” katika mstari wa 19. Yehova anapowafariji wenye taabu, yeye hushughulika na kila mtu kibinafsi. Kama vile Baba, yeye hamwulizi mwana aliyevunjika moyo, ‘Mbona usiwe na nguvu kama ndugu yako?’ (Wagalatia 6:4) Badala yake, yeye humsikiliza kila mmoja kwa makini. Kwa kweli, “asikiapo ndipo atakapokujibu.” Maneno hayo yanatia moyo kama nini! Waliovunjika moyo waweza kuimarishwa sana wakisali kwa Yehova.—Zaburi 65:2.
Sikiliza Mwongozo wa Sauti ya Mungu kwa Kusoma Neno Lake
17, 18. Hata katika nyakati za magumu, Yehova huandaaje mwongozo?
17 Isaya aendeleapo kutoa hotuba yake, awakumbusha wanaomsikiliza kwamba shida itakuja. Watu watapata “chakula cha shida na maji ya msiba.” (Isaya 30:20a) Shida na msiba watakazopata wakiwa chini ya mazingiwa zitakuwa za kawaida kama vile chakula na maji zilivyo vitu vya kawaida. Ijapokuwa hivyo, Yehova yuko tayari kuwaokoa wenye mioyo minyofu. “Waalimu [“Mfunzi Mtukufu,” “NW”] wako hawatafichwa tena, ila macho yako yatawaona waalimu wako; na masikio yako yatasikia neno nyuma yako, likisema, Njia ni hii, ifuateni; mgeukapo kwenda mkono wa kulia, na mgeukapo kwenda mkono wa kushoto.”—Isaya 30:20b, 21.b
18 Yehova ndiye “Mfunzi Mtukufu.” Hakuna mwalimu mwingine anayelingana naye. Ingawa hivyo, watu wawezaje ‘kumwona’ na ‘kumsikia’? Yehova hujifunua kupitia manabii wake, ambao maneno yao yamerekodiwa katika Biblia. (Amosi 3:6, 7) Leo, waabudu waaminifu wasomapo Biblia, ni kana kwamba sauti ya Mungu iliyo kama ya baba inawaelekeza njia ya kufuata na kuwasihi warekebishe mwendo wa tabia yao ili waitembee. Kila Mkristo apaswa kusikiliza kwa makini Yehova asemapo kupitia Biblia na kupitia vichapo vinavyotegemea Biblia, vinavyoandaliwa na “mtumwa mwaminifu na mwenye busara.” (Mathayo 24:45-47) Kila mmoja na ajitahidi kuisoma Biblia, kwa ‘maana ni maisha yake.’—Kumbukumbu la Torati 32:46, 47; Isaya 48:17.
Tafakari Baraka za Wakati Ujao
19, 20. Wale wanaoitikia sauti ya Mfunzi Mtukufu watapata baraka gani?
19 Wale wanaoitikia sauti ya Mfunzi Mtukufu watazitupa sanamu zao za kuchongwa, zitakuwa kwao kama kitu chenye kuchukiza. (Soma Isaya 30:22.) Kisha, wale wanaoitikia watapata baraka za ajabu. Isaya azifafanua baraka hizo, kama ilivyorekodiwa kwenye Isaya 30:23-26, ambao ni unabii mzuri wa urudisho unaotimizwa mara ya kwanza mabaki ya Wayahudi warudipo kutoka utekwani mwaka wa 537 K.W.K. Leo, unabii huo hutusaidia kuona baraka za ajabu ambazo Mesiya aleta katika paradiso ya kiroho sasa na katika Paradiso halisi ya wakati ujao.
20 “Atatoa mvua juu ya mbegu zako, upate kuipanda nchi hii; na mkate wa mazao ya nchi, nayo itasitawi na kuzaa tele; katika siku hiyo ng’ombe zako watakula katika malisho mapana. Ng’ombe pia na wana-punda wailimao nchi watakula chakula kilichokolea, kilichopepetwa kwa ungo na kwa pepeo.” (Isaya 30:23, 24) Mkate—chakula kilicho na lishe tele—utakuwa chakula kikuu cha mwanadamu kila siku. Nchi itazaa kwa wingi sana hivi kwamba hata wanyama watafaidika. Mifugo italishwa “chakula kilichokolea”—nyasi inayohifadhiwa kwa ajili ya vipindi maalumu. Chakula hicho hata ‘kimepepetwa’—utayarishaji ambao kwa kawaida hufanyiwa nafaka inayokusudiwa kuliwa na watu. Isaya aandika hapo mambo mazuri kama nini ya kuonyesha ubora wa baraka za Yehova juu ya wanadamu waaminifu!
21. Fafanua ukamilifu wa baraka zitakazokuja.
21 “Juu ya kila mlima mrefu, na juu ya kila kilima kilichoinuka, itakuwapo mito na vijito vya maji.” (Isaya 30:25a)c Isaya atoa mfano unaokazia ukamilifu wa baraka za Yehova. Hakuna upungufu wa maji—kitu chenye thamani kitakachotiririka, siyo katika mabonde tu, bali pia katika kila mlima, “juu ya kila mlima mrefu, na juu ya kila kilima kilichoinuka.” Naam, njaa haitakuwapo. (Zaburi 72:16) Isitoshe, uangalifu wa nabii huyo wageukia hata mambo yaliyo juu kuliko milima. “Nuru ya mwezi itakuwa kama nuru ya jua, na nuru ya jua itaongezeka mara saba, kama nuru ya siku saba, katika siku ile BWANA atakapofunga mapigo ya watu wake, na kuliponya pigo la jeraha yao.” (Isaya 30:26) Huo ni upeo wenye kusisimua kama nini wa unabii huu mtukufu! Utukufu wa Mungu utang’aa katika fahari. Baraka watakazopata waabudu waaminifu wa Mungu zitakuwa nyingi sana—mara saba—kuliko chochote ambacho wamewahi kupata hapo awali.
Hukumu na Furaha
22. Tofauti na baraka ambazo waaminifu watapata, Yehova atawatenda waovu nini?
22 Sauti ya Isaya yabadilika tena atoapo ujumbe huu. “Tazama” yeye asema, kana kwamba ataka wasikilizaji wake wasikilize kwa makini. “Jina la BWANA linakuja kutoka mbali sana, linawaka kwa hasira yake, kwa moshi mwingi sana unaopaa juu; midomo yake imejaa ghadhabu, na ulimi wake ni moto ulao.” (Isaya 30:27) Hadi sasa, Yehova hajaingilia kati, akiwaruhusu adui za watu wake wafuate mwendo wao wenyewe. Sasa yeye asonga karibu zaidi—kama mvua ya radi—ili kutekeleza hukumu. “Pumzi yake ni kijito kifurikacho, kifikacho hata shingoni, kupepeta mataifa kwa ungo wa ubatili; na lijamu ikoseshayo itakuwa katika taya za watu.” (Isaya 30:28) Adui za watu wa Mungu watazungukwa kwa “kijito kifurikacho,” watatikiswa kijeuri “kwa ungo,” na kuzuiwa kwa “lijamu.” Wataharibiwa.
23. Ni nini kinachosababisha “furaha ya moyo” kwa Wakristo leo?
23 Sauti ya Isaya yabadilika tena afafanuapo hali yenye furaha ya waabudu waaminifu ambao watarudi nchini kwao siku moja. “Mtakuwa na wimbo kama vile wakati wa usiku, ishikwapo sikukuu takatifu, mtakuwa na furaha ya moyo kama vile mtu aendapo na filimbi katika mlima wa BWANA, aliye Mwamba wa Israeli.” (Isaya 30:29) Wakristo wa kweli leo hupata “furaha ya moyo” kama hiyo watafakaripo kuhukumiwa kwa ulimwengu wa Shetani; ulinzi anaowapa Yehova, “mwamba wa wokovu;” na baraka za Ufalme zitakazokuja.—Zaburi 95:1.
24, 25. Unabii wa Isaya wakaziaje uhalisi wa hukumu inayokuja dhidi ya Ashuru?
24 Baada ya usemi huo wa furaha, Isaya arudia habari ya hukumu na kutaja chombo cha hasira ya Mungu. “BWANA atawasikizisha watu sauti yake ya utukufu, naye atawaonyesha jinsi mkono wake ushukavyo, na ghadhabu ya hasira yake, na mwako wa moto ulao, pamoja na dhoruba, na tufani, na mvua ya mawe ya barafu. Maana kwa sauti ya BWANA, Mwashuri atavunjika-vunjika, yeye apigaye kwa bakora.” (Isaya 30:30, 31) Kupitia ufafanuzi huo wa waziwazi, Isaya akazia uhalisi wa hukumu ya Mungu juu ya Ashuru. Ni kana kwamba Ashuru imesimama mbele za Mungu na kutetemeka ionapo ‘mkono wake wa hukumu ushukao.’
25 Nabii aendelea: “Kila pigo la fimbo iliyoamriwa, ambayo BWANA ataliweka juu yake [Ashuru], litakuwa pamoja na matari na vinanda, na kwa mapigano yenye kutikisa atapigana nao. Maana Tofethi imewekwa tayari tokea zamani, naam, imewekwa tayari kwa mfalme huyo; ameifanya kubwa, inakwenda chini sana; tanuru yake ni moto na kuni nyingi; pumzi ya BWANA, kama mto wa kiberiti, huiwasha.” (Isaya 30:32, 33) Tofethi, iliyo katika Bonde la Hinomu, imetumiwa hapa kama mahali pa mfano pawakapo moto. Kwa kuonyesha kuwa Ashuru hatimaye itajikuta huko, Isaya akazia uharibifu wa ghafula na mkamilifu utakaokuja juu ya taifa hilo.—Linganisha 2 Wafalme 23:10.
26. (a) Matangazo ya Yehova dhidi ya Ashuru yanatimizwaje leo? (b) Wakristo leo huendeleaje kumngojea Yehova?
26 Ingawa ujumbe huo wa hukumu watolewa dhidi ya Ashuru, maana ya unabii wa Isaya yahusu mambo mengine zaidi. (Waroma 15:4) Yehova atakuja kitamathali tena kutoka mbali ili kufurika, kutikisa, na kutia lijamu wote wanaowaonea watu wake. (Ezekieli 38:18-23; 2 Petro 3:7; Ufunuo 19:11-21) Siku hiyo na ije upesi! Kwa sasa, Wakristo wanangojea kwa hamu siku ya ukombozi. Wao hupata nguvu kwa kutafakari maneno yenye kusisimua yaliyorekodiwa katika Isaya sura ya 30. Maneno hayo huwatia moyo watumishi wa Mungu wathamini pendeleo la sala, wajitahidi katika kujifunza Biblia, na watafakari juu ya baraka za Ufalme zitakazokuja. (Zaburi 42:1, 2; Mithali 2:1-6; Waroma 12:12) Basi maneno ya Isaya hutusaidia sisi sote kuendelea kumngojea Yehova.
[Maelezo ya Chini]
a Ona kwamba iwapo Yuda ingalikuwa yenye uaminifu, jambo lililo kinyume cha hilo lingalitendeka.—Mambo ya Walawi 26:7, 8.
b Hapo ndipo mahali pekee katika Biblia ambapo Yehova aitwa “Mfunzi Mtukufu.”
c Andiko la Isaya 30:25b lasema: “Katika siku ya machinjo makuu itakapoanguka minara.” Katika utimizo wa mwanzoni, huenda maneno hayo yarejezea kuanguka kwa Babiloni, uliofungua njia kwa Israeli kufurahia baraka zilizotabiriwa kwenye Isaya 30:18-26. (Ona fungu la 19.) Huenda yakarejezea pia uharibifu kwenye Har–Magedoni, utakaofanya iwezekane kuwe na utimizo mtukufu zaidi wa baraka hizo katika ulimwengu mpya.
[Picha katika ukurasa wa 305]
Katika siku ya Musa, Waisraeli waliponyoka kutoka Misri. Katika siku ya Isaya, Yuda yaenda Misri kutafuta msaada
[Picha katika ukurasa wa 311]
“Juu ya kila kilima kilichoinuka, itakuwapo mito na vijito vya maji”
[Picha katika ukurasa wa 312]
Yehova atakuja “kwa hasira yake, kwa moshi mwingi sana”