KUUTAZAMA ULIMWENGU
Kuimulika Mashariki Ya Kati
Ikiwa mojawapo ya maeneo ya kwanza kuwa na maendeleo duniani, Mashariki ya Kati ina utajiri mwingi wa hazina za vitu vya kale.
Watengeneza Divai Wa Kanaani
Katika mwaka wa 2013, wachimbuaji wa vitu vya kale waligundua hifadhi ya divai katika eneo la Kanaani, iliyokuwepo kwa miaka 3,700. Hifadhi hiyo ya divai ilikuwa na mitungi mikubwa 40 ambayo katika siku zetu inaweza kutosha kwenye chupa 3,000 za divai. Mchimbuaji mmoja aliyechunguza mabaki yaliyokuwa katika mitungi hiyo alisema kwamba Wakanaani walitengeneza divai kwa makini sana. Alisema hivi: “Watengenezaji wa divai walitumia mchanganyiko uleule kwa uangalifu katika kila mtungi.”
JE WAJUA? Biblia inataja kuhusu utengenezaji wa “divai bora” na kuhifadhiwa kwa divai kwenye mitungi mikubwa katika Israeli la kale.—Wimbo wa Sulemani 7:9; Yeremia 13:12.
Ongezeko la Watu
Kulingana na ripoti ya gazeti la Guardian, watoto 560,000 zaidi walizaliwa nchini Misri katika mwaka wa 2012 ukilinganisha na mwaka wa 2010. Magued Osman wa shirika la utafiti nchini Misri linaloitwa Baseera, anasema hivi: “Hilo ni ongezeko kubwa zaidi katika historia ya nchi ya Misri.” Ikiwa ongezeko hilo litaendelea, baadhi ya wataalamu wanasema kwamba nchi hiyo itakumbwa na ukosefu mkubwa sana wa maji, umeme, na chakula.
JE WAJUA? Kulingana na Biblia, Mungu amekusudia wanadamu ‘waijaze dunia’ kwa kiwango kinachofaa, na kila mtu apate mahitaji ya kutosha.—Mwanzo 1:28; Zaburi 72:16.
Sarafu Zilizohifadhiwa Zagunduliwa
Sarafu za shaba zaidi ya 100 zenye maandishi “Mwaka wa Nne,” ziligunduliwa karibu na njia kuu nchini Israel. Mwaka unaotajwa ni mwaka wa nne wa uasi wa Wayahudi dhidi ya Waroma (69-70 W.K.) —uasi uliosababisha uharibifu wa Yerusalemu. Msimamizi wa uchimbuaji huo, Pablo Betzer, alisema hivi: “Inaonekana mtu fulani alihofia kwamba mwisho ulikuwa unakaribia, labda kwa kuwa aliona jeshi la Waroma likikaribia mji huo. Hivyo, akaficha sarafu hizo akitumaini kwamba baadaye atakuja kuzichukua.”
JE WAJUA? Katika mwaka wa 33 W.K., Yesu alitabiri kwamba jeshi la Roma lingezingira jiji la Yerusalemu. Aliwasihi Wakristo wakimbilie milimani ili wasiharibiwe.—Luka 21:20-24.