Hukumu ya Yehova Dhidi ya Wafundishaji Bandia
“Katika manabii wa Yerusalemu nimeona neno linalochukiza sana; hufanya zinaa; huenenda katika maneno ya uongo . . . wote pia wamekuwa kama Sodoma kwangu, na wenyeji wake kama Gomora.”—YEREMIA 23:14.
1. Kwa nini mtu ajishughulishaye na ufundishaji wa kimungu huchukua daraka zito sana?
YEYOTE ajishughulishaye na ufundishaji wa kimungu huchukua daraka zito sana. Yakobo 3:1 laonya hivi: “Msiwe waalimu [wafundishaji, NW] wengi, mkijua ya kuwa tutapata hukumu kubwa zaidi.” Ndiyo, wafundishaji wa Neno la Mungu wako chini ya daraka zito zaidi la kutoa hesabu inayokubalika kuliko Wakristo kwa ujumla. Hilo litamaanisha nini kwa wale wanaokuwa wafundishaji bandia? Acheni tutazame hali ilivyokuwa katika siku za Yeremia. Tutaona jinsi hali hiyo ilivyotangulia kufananisha yale yanayotukia leo.
2, 3. Yehova alitoa hukumu gani kupitia Yeremia kuhusu wafundishaji bandia wa Yerusalemu?
2 Katika 647 K.W.K., mwaka wa 13 wa utawala wa Mfalme Yosia, Yeremia aliagizwa kuwa nabii wa Yehova. Yehova alikuwa na lalamiko dhidi ya Yuda, kwa hiyo alimtuma Yeremia kulijulisha. Manabii au wafundishaji bandia wa Yerusalemu, walikuwa wakifanya ‘mambo ya kuchukiza sana’ machoni pa Mungu. Ubaya wao ulikuwa mkubwa sana hivi kwamba Mungu alifananisha Yerusalemu na Yuda kuwa kama Sodoma na Gomora. Yeremia sura ya 23 hutuambia juu ya hilo. Mstari wa 14 wasema hivi:
3 “Katika manabii wa Yerusalemu nimeona neno linalochukiza sana; hufanya zinaa; huenenda katika maneno ya uongo, hutia nguvu mikono ya watendao maovu, hata ikawa hapana mtu arejeaye na kuuacha uovu wake; wote pia wamekuwa kama Sodoma kwangu, na wenyeji wake kama Gomora.”
4. Kielelezo cha adili mbaya cha wafundishaji wa Yerusalemu kinafananishwaje katika Jumuiya ya Wakristo leo?
4 Ndiyo, manabii au wafundishaji hao, waliweka vielelezo vibaya sana vya kiadili wao wenyewe na kwa kweli, waliwatia watu moyo wafanye vivyo hivyo. Angalia hali zilizomo katika Jumuiya ya Wakristo leo! Je! wao hawako kama wale wa siku za Yeremia? Leo makasisi huruhusu wazinzi na wagoni-jinsia-moja waendelee kuwa miongoni mwao nao hata huwaruhusu waongoze shughuli za kanisa. Je! yashangaza kwamba washiriki wengi sana wa kanisa walioandikishwa ni wakosa adili pia?
5. Kwa nini hali ya kukosa adili ya Jumuiya ya Wakristo ni mbaya zaidi ya ile ya Sodoma na Gomora?
5 Yehova alifananisha wakaaji wa Yerusalemu na wale wa Sodoma na Gomora. Lakini hali ya kukosa adili ya Jumuiya ya Wakristo ni mbaya zaidi ya ile ya Sodoma na Gomora. Ndiyo, hata ni yenye kulaumika zaidi machoni pa Yehova. Wafundishaji wayo hupuuza kanuni za kiadili za Kikristo. Na hilo husababisha hali ya adili zilizodhoofika ambamo ndani yayo mna vishawishi vya hila vya kila aina ili kufanya yaliyo mabaya. Hali hiyo ya adili imeenea sana hivi kwamba ubaya leo huonwa kuwa jambo la kawaida.
‘Kuenenda Katika Maneno ya Uongo’
6. Yeremia alisema nini juu ya ubaya wa manabii wa Yerusalemu?
6 Sasa ona yale ambayo mstari wa 14 wasema juu ya manabii wa Yerusalemu. Wao walikuwa ‘wakienenda katika maneno ya uongo.’ Na sehemu ya mwisho ya mstari wa 15 yasema: “Kutoka kwa manabii hao wa Yerusalemu kukufuru [uasi-imani, NW] kumeingia katika nchi yote.” Kisha, katika mstari wa 16 waongeza hivi: “BWANA, [Yehova, NW] wa majeshi asema hivi, Msisikilize maneno ya manabii wakiwatabiria; huwafundisha ubatili; hunena maono ya mioyo yao wenyewe; hayakutoka katika kinywa cha BWANA, [Yehova, NW].”
7, 8. Kwa nini makasisi wa Jumuiya ya Wakristo ni kama manabii bandia wa Yerusalemu, na hilo limewaathirije waenda-kanisani?
7 Kama wale manabii bandia wa Yerusalemu, makasisi wa Jumuiya ya Wakristo pia hutembea katika maneno ya uongo, wakieneza mafundisho ya uasi-imani, mafundisho yasiyopatikana katika Neno la Mungu. Baadhi ya mafundisho hayo bandia ni gani? Kutokufa kwa nafsi, Utatu, purgatori, na moto wa helo wa kuwatesa watu milele. Wao pia hutekenya masikio ya wasikilizaji wao kwa kuhubiri yale ambayo watu hutaka kusikia. Wao hukariri kwamba hakuna msiba unaokabili Jumuiya ya Wakristo kwa sababu ina amani ya Mungu. Lakini makasisi wanasema “maono ya mioyo yao wenyewe.” Si kweli. Wale waaminio uongo huo wanatiwa sumu kiroho. Wao wanadanganywa wakielekezwa kwenye uharibifu wao!
8 Fikiria yale ambayo Yehova husema juu ya wafundishaji hao bandia katika mstari wa 21: “Mimi sikuwatuma manabii hao, lakini walikwenda mbio; sikusema nao, lakini walitabiri.” Ndivyo ilivyo leo, makasisi hawajatumwa na Mungu, wala hawafundishi kweli zake. Matokeo ni nini? Kutokuifahamu Biblia kunakosikitisha kumo miongoni mwa waenda-kanisani kwa sababu wahubiri wao huwalisha falsafa za kilimwengu.
9, 10. (a) Wafundishaji bandia wa Yerusalemu walikuwa na ndoto za aina gani? (b) Makasisi wa Jumuiya ya Wakristo vilevile wamefundishaje “ndoto za uongo”?
9 Isitoshe, makasisi leo huhubiri matumaini bandia. Angalia mstari wa 25: “Nimesikia waliyoyasema manabii wanaotabiri uongo kwa jina langu, wakisema, Nimeota ndoto; nimeota ndoto.” Hizo ni ndoto za aina gani? Mstari wa 32 watuambia: “Tazama, mimi ni juu ya hao wanaotabiri ndoto za uongo, asema BWANA, [Yehova, NW], na kuzisema, na kuwakosesha watu wangu kwa uongo wao, na kwa majivuno yao ya upuzi, lakini mimi sikuwatuma, wala sikuwapa amri; wala hawatawafaidia watu hawa hata kidogo, asema BWANA, [Yehova, NW].”
10 Ni ndoto zipi au matumaini gani bandia, ambayo makasisi wamefundisha? Kwamba tumaini pekee la mwanadamu kupata amani na usalama leo ni Umoja wa Mataifa. Katika miaka ya hivi karibuni wao wameuita UM kuwa “tumaini la mwisho kwa mapatano na amani,” “baraza kuu zaidi la amani na haki,” “tumaini kuu la kilimwengu kwa ajili ya amani ya ulimwengu.” Hayo ni madanganyo makubwa kama nini! Tumaini pekee kwa ainabinadamu ni Ufalme wa Mungu. Lakini makasisi hawahubiri na kufundisha kweli juu ya serikali hiyo ya kimbingu, ambayo ilikuwa kichwa kikuu cha mahubiri ya Yesu.
11. (a) Wafundishaji bandia wa Yerusalemu walikuwa na tokeo jipi baya juu ya jina la Mungu? (b) Tofauti na jamii ya Yeremia, wafundishaji bandia wa kidini wa leo wamefanya nini kuhusu jina la Mungu mwenyewe?
11 Mstari wa 27 watuambia mambo zaidi. “Wanaodhania ya kuwa watawasahaulisha watu wangu jina langu kwa ndoto zao, wanazomhadithia kila mtu jirani yake, kama vile baba zao walivyolisahau jina langu, kwa ajili ya Baali.” Manabii bandia wa Yerusalemu waliwafanya watu kusahau jina la Mungu. Je! wafundishaji bandia wa kidini wa leo wamefanya vivyo hivyo? Kwa ubaya zaidi, wao hulificha jina la Mungu, Yehova. Wao hufundisha kwamba si lazima kulitumia, na huliondoa kutoka katika tafsiri zao za Biblia. Nao hupinga kwa dhati yeyote anayefundisha watu kwamba jina la Mungu ni Yehova. Lakini jamii ya Yeremia, mabaki ya Wakristo wapakwa kwa roho, pamoja na waandamani wao, wamefanya kama vile Yesu alivyofanya. Wao wamefundisha mamilioni juu ya jina la Mungu.—Yohana 17:6.
Kufunua Kulaumiwa Kwao
12. (a) Kwa nini kuna hatia kubwa ya damu kwa upande wa wafundishaji bandia wa kidini? (b) Ni nini limekuwa fungu la makasisi katika vita viwili vya ulimwengu?
12 Jamii ya Yeremia imefunua tena na tena makasisi kuwa wafundishaji bandia wanaoongoza makundi yao katika barabara pana ya uharibifu. Ndiyo, mabaki wamefanya ionekane wazi kwa nini waotaji ndoto hao wanastahili hukumu kali ya Yehova. Kwa kielelezo, watumishi wa Yehova mara nyingi wamerejezea Ufunuo 18:24, linalosema kwamba katika Babiloni Mkubwa mlipatikana damu ya “wote waliouawa juu ya nchi.” Fikiria vita vyote vilivyopiganwa kwa sababu ya tofauti za kidini. Jinsi wafundishaji bandia wa kidini walivyo na hatia kubwa ya damu! Mafundisho yao yamesababisha migawanyiko yakaendeleza chuki kati ya wale wenye imani tofauti na vikundi vya taifa tofauti. Kuhusu Vita ya Ulimwengu 1, kitabu Preachers Present Arms chasema: “Makasisi waliipa vita umaana wa juhudi yao ya kiroho na msukumo. . . . Kwa njia hiyo kanisa likaja kuwa sehemu ya mfumo wa vita.” Ilikuwa vivyo hivyo katika Vita ya Ulimwengu 2. Makasisi waliunga mkono kwa dhati mataifa yenye kupigana na kubariki majeshi yao. Vita viwili vya ulimwengu vilianza katika Jumuiya ya Wakristo ambavyo wanadini walichinjana wao kwa wao. Mafarakano ya kilimwengu na ya kidini katika Jumuiya ya Wakristo huendelea kusababisha umwagikaji wa damu hadi wakati wa sasa. Ni tokeo baya kama nini kwa sababu ya mafundisho yao bandia!
13. Yeremia 23:22 lathibitishaje kwamba makasisi wa Jumuiya ya Wakristo hawana uhusiano na Yehova?
13 Tafadhali tazama Yeremia sura ya 23, mstari wa 22: “Lakini kama wangalisimama katika [kikundi changu cha usiri, NW], ndipo wangaliwasikizisha watu wangu maneno yangu, na kuwageuza waziache njia zao mbaya, na uovu wa matendo yao.” Ikiwa manabii wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo walikuwa wakisimama katika kikundi cha usiri cha Yehova, katika uhusiano wa karibu naye kana kwamba ni mtumishi mwaminifu mwenye akili, basi wao pia wangekuwa wakiishi kwa viwango vya Mungu. Wao pia wangalikuwa wakifanya watu wa Jumuiya ya Wakristo wasikie maneno ya Mungu mwenyewe. Badala ya hivyo, wafundishaji bandia wa ki-siku-hizi wamewafanya wafuasi wao wawe watumishi waliopofushwa wa Mpinzani wa Mungu, Shetani Ibilisi.
14. Ni kufunuliwa kupi kwenye nguvu kwa makasisi wa Jumuiya ya Wakristo kulikotolewa katika 1958?
14 Kufunuliwa kwa makasisi na jamii ya Yeremia kumekuwa kwenye nguvu. Kwa kielelezo, kwenye Kusanyiko la Kimataifa la Mashahidi wa Yehova la Mapenzi ya Kimungu la 1958 katika Jiji la New York, kaimu msimamizi wa Watch Tower Society alitoa taarifa iliyosema hivi kwa sehemu: “Bila maneno yoyote ya vipengee au ya kusita tunajulisha kisababishi kikuu cha uhalifu, utundu, chuki, ugomvi, ubaguzi wote, . . . na mvurugo wa kichaa kuwa ni dini isiyofaa, dini bandia; mchochezi wayo akiwa adui asiyeonekana wa binadamu, Shetani Ibilisi. Watu wenye hatia kubwa kwa ajili ya hali za ulimwengu ni wafundishaji na viongozi wa kidini; na wenye kulaumika zaidi kati yao ni makasisi wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo. . . . Baada ya miaka hii yote tangu Vita ya Ulimwengu 1, uhusiano wa Jumuiya ya Wakristo na Mungu ni kama ule wa Israeli katika siku ya Yeremia. Ndiyo, Jumuiya ya Wakristo yakabili uharibifu wenye kuogofya na wenye kuangamiza zaidi ya ule ambao Yeremia aliona ukipata Yerusalemu.”
Hukumu Dhidi ya Wafundishaji Bandia
15. Ni unabii upi mbalimbali juu ya amani uliotolewa na makasisi? Je! huo utatimizwa?
15 Lijapokuwa onyo hilo, makasisi wametendaje tangu wakati huo? Kama vile mstari wa 17 uripotivyo: “Daima huwaambia wao wanaonidharau, BWANA, [Yehova, NW] amesema, Mtakuwa na amani; nao humwambia kila mtu aendaye kwa ukaidi wa moyo wake, Hamtapatwa na ubaya wo wote.” Je! hiyo ni kweli? La! Yehova atafunua ubandia wa unabii huo wa makasisi. Yeye hatatimiza yale wanayosema katika jina lake. Hata hivyo, uhakika bandia wa makasisi wa kuwa na amani na Mungu ni wenye kudanganya sana!
16. (a) Ni nini hali ya adili ya ulimwengu huu, na ni nani washirikio daraka la kuisababisha? (b) Jamii ya Yeremia inafanya nini juu ya maoni ya kiadili yenye kushusha heshima ya ulimwengu huu?
16 Je! wewe unafikiri hivi, ‘Eti nini, mimi nidanganywe na mafundisho bandia ya makasisi? Haiwezekani kamwe!’ Usiwe na uhakika sana hivyo! Kumbuka kwamba mafundisho bandia ya makasisi yamechochea hali mbaya sana ya kiadili yenye hila. Mafundisho yao ya uendekezaji hufanya karibu kila kitu kiwe chafaa, hata kiwe kimekosa adili jinsi gani. Na hali hiyo ya maadili yaliyodhoofika yaenea katika nyanja zote za vitumbuizo, sinema, televisheni, magazeti, na muziki. Basi, ni lazima sisi tuwe waangalifu sana, tusije tukavutwa na hali ya maadili yaliyodhoofika ambayo huvutia kwa hila. Vijana waweza kunaswa na vidio na muziki wenye kushusha heshima. Kumbuka kwamba mwelekeo wa watu leo wa kwamba jambo lolote lile lafaa ni tokeo la moja kwa moja la mafundisho bandia ya makasisi na kushindwa kwao kushikilia viwango vyenye uadilifu vya Mungu. Jamii ya Yeremia yapigana dhidi ya maoni hayo yasiyo ya adili na kusaidia watumishi wa Yehova wakatae ule ubaya unaodidimisha Jumuiya ya Wakristo.
17. (a) Kulingana na Yeremia, ni hukumu gani ambayo ingelipata Yerusalemu lenye uovu? (b) Ni nini kitakachoipata Jumuiya ya Wakristo hivi karibuni?
17 Wafundishaji bandia wa Jumuiya ya Wakristo watapokea hukumu gani kutoka kwa Yehova, yule Hakimu mkuu? Mistari 19, 20, 39, na 40 yajibu hivi: “Tazama, tufani ya BWANA, [Yehova, NW], yaani, ghadhabu yake, imetokea; ni dhoruba ya kisulisuli; itapasuka, na kuwaangukia waovu vichwani. Hasira ya BWANA, [Yehova, NW] haitarudi, hata atakapokwisha kuyatimiza makusudi ya moyo wake. . . . Nitawasahau ninyi kabisa, nami nitawatupilia mbali, pamoja na mji huu niliowapa ninyi na baba zenu, mtoke mbele za uso wangu; nami nitaleta juu yenu aibu ya milele, na fedheha ya daima, ambayo haitasahauliwa.” Yote hayo yalipata Yerusalemu lenye uovu na hekalu lalo, na sasa msiba kama huo utaipata Jumuiya ya Wakristo yenye uovu hivi karibuni!
Kujulisha ‘Mzigo wa Yehova’
18, 19. Yeremia alitangazia Yuda “mzigo [upi] wa Yehova,” hilo likiwa na maana gani hasa?
18 Kwa hiyo, jamii ya Yeremia na waandamani wao wana daraka gani? Mstari wa 33 watuambia: “Na watu hawa, au nabii, au kuhani, atakapokuuliza, akisema, Mzigo wa BWANA, [Yehova, NW] ni nini? ndipo utawaambia, [‘Ninyi watu ndio mzigo—Oh ni mzigo ulioje!’ NW] BWANA, [Yehova, NW] asema, Nitawatupilia mbali.”
19 Neno la Kiebrania kwa “mzigo” lina maana mbili. Laweza kurejezea tangazo la kimungu lenye uzito au jambo linalolemea mtu na kumchosha. Hapa usemi “mzigo wa [BWANA, [Yehova, NW]” warejezea unabii mzito—tangazo kwamba Yerusalemu lilitazamia maangamizo. Je! watu walipenda kusikia semi za kiunabii zenye uzito jinsi hiyo ambazo Yeremia aliwapa tena na tena kutoka kwa Yehova? La, watu walimdhihaki Yeremia: ‘Ni unabii (mzigo) gani ambao unao sasa? Tuna hakika unabii wako utakuwa mzigo mwingine wenye kuchosha!’ Lakini Yehova aliwaambia nini? Haya: “Ninyi watu ndio mzigo—Oh ni mzigo ulioje! Nami kwa hakika nitawaacha, (NW).” Ndiyo, watu hao walikuwa mzigo kwa Yehova, naye angewaondoa ili wasimlemee tena.
20. “Mzigo wa BWANA, [Yehova, NW]” ni nini leo?
20 Leo “mzigo wa BWANA, [Yehova, NW]” ni nini? Ni ujumbe mzito wa kiunabii wa Neno la Mungu. Huo umejaa balaa, ukitangaza uharibifu wa karibuni wa Jumuiya ya Wakristo. Kwa habari ya watu wa Yehova, sisi tuna daraka zito la kujulisha ‘mzigo huo wa Yehova.’ Kadiri mwisho ukaribiavyo, ni lazima tuwaambie wote kwamba watu waliokengeuka wa Jumuiya ya Wakristo ni “mzigo,” ndiyo, “Oh ni mzigo ulioje!” kwa Yehova Mungu, na kwamba hivi karibuni yeye ataondolea mbali “mzigo” huo kwa kuiacha Jumuiya ya Wakristo ipatwe na msiba.
21. (a) Kwa nini Yerusalemu liliharibiwa katika 607 K.W.K.? (b) Baada ya Yerusalemu kuharibiwa, ni nini kilichowapata manabii bandia na kumpata nabii wa kweli wa Yehova, hilo likitupa sisi uhakikishio gani leo?
21 Yehova ilitekelezwa katika siku ya Yeremia Wababiloni walipoharibu Yerusalemu katika 607 K.W.K. Kama ilivyotolewa unabii, hiyo ilikuwa ‘aibu na fedheha’ kwa Waisraeli hao wakaidi, wasio waaminifu. (Yeremia 23:39, 40) Liliwaonyesha kwamba Yehova, ambaye walikuwa wamekosa kumheshimu mara kwa mara, hatimaye alikuwa amewaacha wapatwe na matokeo ya ubaya wao. Hatimaye vinywa vya manabii wao bandia wenye kiburi vilinyamazishwa. Lakini, kinywa cha Yeremia kiliendelea kutoa unabii. Yehova hakumwacha. Kupatana na kiolezo hicho, Yehova hataacha jamii ya Yeremia wakati hukumu yake nzito iongozapo kwenye kuponda na kuwaangamiza makasisi wa Jumuiya ya Wakristo na wale wanaoamini uongo wao.
22. Hukumu za Yehova zitafanya Jumuiya ya Wakristo iwe katika hali gani?
22 Ndiyo, hali ya Jumuiya ya Wakristo itakuwa kama ile ya Yerusalemu baada ya 607 K.W.K. ya kuachwa ukiwa, bila kukaliwa, baada ya kunyang’anywa mali yayo na kufunuliwa kwa aibu. Hiyo ndiyo hukumu istahiliyo ambayo Yehova ametangaza dhidi ya wafundishaji bandia. Hukumu hiyo haitashindwa kutimia. Kama vile ule ujumbe wote mbalimbali wa kuonya uliopuliziwa wa Yeremia ulivyotimia nyakati za kale, ndivyo utakavyotimia katika utimizo wao wa ki-siku-hizi. Kwa hiyo, acheni tuwe kama Yeremia. Bila hofu, acheni tuwajulishe watu juu ya mzigo wa kiunabii wa Yehova, ili wajue kwa nini kipimo kamili cha hukumu yake yenye uadilifu kinakuja juu ya wafundishaji wote bandia wa kidini!
Maswali ya Kupitia
◻ Yerusalemu la kale lilikuwa baya kadiri gani kutokana na maoni ya Yehova?
◻ Jumuiya ya Wakristo ‘imeenenda katika maneno ya uongo’ katika njia zipi?
◻ Kulaumika kwa makasisi wa ki-siku-hizi kumefunuliwaje?
◻ Ni “mzigo [upi] wa BWANA, [Yehova, NW]” unaojulishwa sasa?
[Picha katika ukurasa wa 8]
Manabii wa Yerusalemu walitenda “neno linalochukiza sana”
[Picha katika ukurasa wa 9]
“Hunena maono ya mioyo yao wenyewe”
[Picha katika ukurasa wa 10]
Yerusalemu baada ya kuharibiwa kwalo, laonyesha mwisho kabisa wa Jumuiya ya Wakristo