Msalaba
Maana: Chombo ambacho Yesu Kristo aliuawa juu yake huitwa na walio wengi katika Jumuiya ya Wakristo kuwa msalaba (Kiingereza, cross). Neno hilo la Kiingereza linatokana na neno la Kilatini, crux.
Kwa nini vichapo vya Mashahidi wa Yehova humwonyesha Yesu akiwa juu ya mti na mikono yake ikiwa juu ya kichwa chake badala ya kuwa juu ya msalaba kama kawaida?
Neno la Kigiriki lililotafsiriwa “msalaba” katika tafsiri nyingi za kisasa za Biblia (“mti wa mateso” katika NW) ni stau·rosʹ. Katika Kigiriki cha kale, neno hilo lilimaanisha mti ulionyooka au nguzo tu. Baadaye likaja pia kutumiwa kurejezea mti wenye kijiti kilichokingamana ambao watu waliuawa juu yake. The Imperial Bible-Dictionary inakubali jambo hilo, inaposema, “Neno la Kigiriki linalotafsiriwa msalaba [stau·rosʹ], kwa kufaa lilirejezea mti, nguzo iliyonyooka au kipande cha mhimili, ambacho kitu chochote kinaweza kutundikwa juu yake, au ambacho kinaweza kutumiwa kuchomeka katika [kuzungushia ua] kiwanja. . . . Hata kati ya Waroma crux (chanzo cha neno la Kiingereza cross), yaonekana kwamba mwanzoni ilikuwa nguzo iliyonyooka.”—Iliyohaririwa na P. Fairbairn (London, 1874), Buku la 1, uku. 376.
Je, hivyo ndivyo ilivyokuwa Mwana wa Mungu alipouawa? Ni jambo linalostahili kuangaliwa kwamba Biblia pia inatumia neno xyʹlon kutambulisha chombo kilichotumiwa. A Greek-English Lexicon, ya Liddell na Scott, inafafanua neno hili hivi: “Mti uliokatwa na ulio tayari kutumiwa, ukuni, ubao, n.k. . . . kipande cha mti, gogo, boriti, nguzo . . . bakora, rungu, . . . mti ambao wahalifu walitundikwa juu yake . . . mbao, mti mbichi.” Inasema pia “katika AJ, msalaba,” na kutaja Matendo 5:30 na 10:39 kuwa mifano. (Oxford, 1968, uku. 1191, 1192) Hata hivyo, katika mistari hiyo UV, ZSB, na VB hutafsiri xyʹlon kuwa “mti.” (Linganisha tafsiri hiyo na Wagalatia 3:13; Kumbukumbu 21:22, 23.)
Kitabu The Non-Christian Cross, cha J. D. Parsons (London, 1896), kinasema: “Hakuna hata sentensi moja katika yale maandishi mengi yanayofanyiza Agano Jipya katika Kigiriki cha kwanza, inayotoa hata uthibitisho usio wa moja kwa moja unaoonyesha kwamba mti uliotumiwa katika kisa cha Yesu ulikuwa tofauti na miti ya kawaida; ingewezekanaje basi mti huo haukuwa kipande kimoja cha mti bali vipande viwili vilivyopigiliwa misumari pamoja, kwa namna ya msalaba. . . . Walimu wetu wanatupotosha sana wanapotafsiri neno stauros kuwa ‘msalaba’ wakati wa kutafsiri hati za Kigiriki za Kanisa katika lugha za kwetu, na kuunga mkono tendo hilo kwa kuweka ‘msalaba’ katika kamusi zetu kuwa ndiyo maana ya stauros bila kueleza kwa uangalifu kwamba kwa vyovyote, hiyo haikuwa ndiyo maana ya msingi ya neno hilo katika siku za Mitume, haikuwa maana yake ya msingi mpaka muda mrefu baadaye, na basi ikawa hivyo, kwa sababu tu ya kwamba, ijapokuwa ukosefu wa uthibitisho wa kuunga mkono, ilikuwa ni kwa sababu fulani au nyingine iliyodhaniwa kwamba mti ule ambao Yesu aliuawa juu yake ulikuwa na umbo hilo hususa.”—Uku. 23, 24; ona pia The Companion Bible (Thetford, England, 1974), Nyongeza Na. 162.
Hivyo uthibitisho mwingi unaonyesha kwamba Yesu alikufa juu ya mti ulionyooka wala si juu ya msalaba kama unavyojulikana.
Kulingana na historia, msalaba wa Jumuiya ya Wakristo ulitoka wapi?
“Vitu mbalimbali, vya tangu zamani za kale kabla ya Ukristo, vimepatikana, vikiwa na alama za misalaba yenye maumbo mbalimbali, karibu katika sehemu zote za ulimwengu wa kale. Misalaba mingi ya aina hiyo imepatikana India, Siria, Uajemi na Misri . . . Matumizi ya msalaba kama mfano wa kidini katika nyakati za kabla ya Ukristo na kati ya mataifa yasiyo ya Kikristo yanaweza kuonwa kwamba yalienea kila mahali, na katika visa vingi sana yalihusiana na namna fulani ya ibada ya vitu vya asili.”—Encyclopædia Britannica (1946), Buku la 6, uku. 753.
“Umbo la [msalaba wenye mbao mbili] lilianzia Ukaldayo ya kale, na lilitumiwa kama mfano wa mungu Tamuzi (akiwa katika umbo la Tau ya kifumbo, herufi ya kwanza ya jina lake) katika nchi hiyo na katika nchi jirani, kutia ndani Misri. Kufikia katikati ya karne ya 3 W.K., makanisa yalikuwa yameacha, au yalikuwa yamepotosha, mafundisho fulani ya imani ya Kikristo. Ili kuongeza sifa ya kanisa lililoasi, wapagani walipokewa katika makanisa bila kuzaliwa upya kupitia imani, na kwa mambo mengi waliruhusiwa kuendelea kuwa na ishara na mifano yao ya kipagani. Kwa hiyo Tau au T, katika namna zake za kawaida, huku kipande chake cha mti uliokingamana kikiwa kimeshushwa, ilianza kutumiwa kuwakilisha msalaba wa Kristo.”—An Expository Dictionary of New Testament Words (London, 1962), W. E. Vine, uku. 256.
“Ni ajabu, lakini ni ukweli mtupu kwamba Msalaba umetumiwa kama ishara takatifu, zamani za kale kabla ya kuzaliwa Kristo, na tangu wakati huo katika nchi ambazo hazijaathiriwa na mafundisho ya Kanisa. . . . Bakusi wa Ugiriki, Tamuzi wa Tiro, Beli wa Ukaldayo, na Odini wa Norse, wote waliwakilishwa na msalaba kwa waabudu wao.”—The Cross in Ritual, Architecture, and Art (London, 1900), G. S. Tyack, uku. 1.
“Makuhani wa Misri na wafalme Maaskofu walibeba . . . msalaba wenye umbo la ‘Crux Ansata’ ukiwa mfano wa mamlaka yao wakiwa makuhani wa Mungu-Jua nao uliitwa ‘Ishara ya Uhai.’”—The Worship of the Dead (London, 1904), Kanali J. Garnier, uku. 226.
“Maumbo mbalimbali ya misalaba yanapatikana kila mahali katika minara ya ukumbusho na makaburi ya Misri, na wataalamu wengi huiona kuwa mifano ya kiungo cha uzazi cha kiume au ya ngono. . . . Katika makaburi ya Misri crux ansata [msalaba wenye mviringo au kipini juu yake] inapatikana kando ya mfano wa kiungo cha uzazi.”—A Short History of Sex-Worship (London, 1940), H. Cutner, uku. 16, 17; ona pia The Non-Christian Cross, uku. 183.
“Misalaba hiyo ilitumiwa kama mifano ya mungu-jua wa Babiloni, [Ona kitabu], na inaonekana mara ya kwanza katika sarafu ya Yulio Kaisari, 100-44 K.W.K., na kisha juu ya sarafu iliyoundwa na mrithi wa Kaisari (Agusto), 20 K.W.K. Juu ya sarafu za Konstantino mfano unaoonekana mara nyingi ni [Ona kitabu]; lakini mfano huohuo unatumiwa bila mviringo unaouzunguka, na pamoja na mikono minne yenye kulingana iliyo wima na iliyolala; na huo ndio mfano uliotukuzwa kwa njia ya pekee kuwa ‘Gurudumu la Jua’. Inapasa kuelezwa kwamba Konstantino alikuwa mwabudu wa mungu-jua, na hakuingia katika ‘Kanisa’ mpaka miaka 25 hivi baada ya ile hadithi kwamba aliona msalaba kama huo mbinguni.”—The Companion Bible, Nyongeza Na. 162; ona pia The Non-Christian Cross, uku. 133-141.
Je, kutukuza msalaba ni tendo la Kimaandiko?
1 Kor. 10:14: “Wapendwa wangu, ikimbieni ibada ya sanamu.” (Sanamu ni mfano au kiwakilishi kinachosujudiwa, kutukuzwa, au kuabudiwa.)
Kut. 20:4, 5, UV: “Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia.” (Ona kwamba Mungu aliwaamuru watu wake hata wasifanye mfano wa kusujudiwa.)
Ona maelezo haya katika New Catholic Encyclopedia: “Kiwakilishi cha kifo cha ukombozi cha Kristo katika Golgotha hakionekani katika sanaa ya viwakilishi ya karne za kwanza za Ukristo. Wakristo wa kwanza, kwa kufuata amri ya Agano la Kale inayokataza sanamu za kuchongwa, walikataa kufanyiza hata chombo cha Mateso ya Bwana.”—(1967), Buku la 4, uku. 486.
Kichapo History of the Christian Church kinasema hivi kuhusu Wakristo wa karne ya kwanza: “Msalaba haukutumiwa wala hapakuwa na mfano wake.”—(New York, 1897), J. F. Hurst, Buku la 1, uku. 366.
Je, kuna makosa ikiwa mtu anaupenda msalaba, lakini hauabudu?
Wewe utaonaje rafiki yako mpendwa sana akiuawa kwa sababu ya mashtaka ya uwongo? Je, utatengeneza mfano wa chombo kilichotumiwa kumuua? Je, utakipenda, au utaona ni afadhali kukiepuka?
Katika Israeli la kale, Wayahudi wasio waaminifu waliomboleza kifo cha mungu wa uwongo, Tamuzi. Yehova alisema kwamba yale waliyofanya yalikuwa “machukizo.” (Eze. 8:13, 14) Kulingana na historia, Tamuzi alikuwa mungu wa Babiloni, na mfano wake ulikuwa msalaba. Tangu mwanzo wake katika siku za Nimrodi, Babiloni ilimpinga Yehova nayo ilikuwa adui wa ibada ya kweli. (Mwa. 10:8-10; Yer. 50:29) Kwa hiyo, mtu akiupenda msalaba, atakuwa akiuheshimu mfano wa ibada inayompinga Mungu wa kweli.
Kama inavyoelezwa katika Ezekieli 8:17, Wayahudi waasi-imani pia ‘walinyoosha chipukizi kuelekea pua ya Yehova.’ Yeye aliliona hilo kuwa “machukizo” na kitu cha ‘kumtia uchungu.’ Kwa nini? Kulingana na maelezo ya watu fulani, “chipukizi,” lilikuwa kiwakilishi cha kiungo cha uzazi cha kiume, kilichotumiwa katika ibada ya viungo vya uzazi. Basi, Yehova ataonaje mtu anapotumia msalaba, ambao, kama tulivyokwisha kuona, ulikuwa mfano uliotumiwa zamani za kale katika ibada ya viungo vya uzazi?