Gari La Yehova La Kimbingu Liko Katika Mwendo
“Na magurudumu hayo yaliitwa Kisulisuli, nami nalisikia.”—EZEKIELI 10:13.
1. Ni namna gani ya usafiri ambayo Yehova anayo?
KATIKA siku hizi zenye jeti maridadi, huenda viongozi wa ulimwengu wakahisi wamefikia upeo wa usafiri bora kabisa. Hata hivyo, miaka 2,600 iliyopita Yehova alifunulia nabii Ezekieli kwamba Yeye ana namna ya usafiri wa hali bora kupita wote, ambao mfano wake hakuna mhandisi amepata kuuona. Ni gari kubwa mno, lenye kutia hofu! Je! laonekana kuwa jambo geni kwamba Muumba husafiri kwa kisafirishaji mfano wa gari? La, kwa kuwa gari la kimbingu la Ye-hova ni tofauti sana na lolote lililobuniwa na wanadamu.
2. Ezekieli sura ya 1 yaonyesha gari la kimbingu la Yehova likiwaje, na kwanza nabii avuta uangalifu wetu kwenye nani?
2 Katika sura 1 ya unabii wa Ezekieli, Yehova anaonyeshwa kuwa amepanda gari kubwa mno la kimbingu. Gari hili lenye magurudumu manne lenye kuvuvia hofu laweza kufanya maajabu. Ezekieli aliliona gari hili la kimbingu katika njozi katika 613 K.W.K., akiwa kando ya mmoja wa mifereji ya Babuloni ya kale. Kwanza nabii avuta uangalifu wetu kwa wale wanaotumikia gari la kimbingu la Yehova. Tusomapo, acheni tujaribu kuona njozi ya aliyoyaona Ezekieli.
Viumbe Hai Wanne
3. Ni nini kionyeshwacho na zile nyuso nne za kila mmoja wa makerubi wanne?
3 Ezekieli aripoti hivi: “Nikaona, na tazama, upepo wa dhoruba ulitoka upande wa kaskazini, wingu kubwa sana, pamoja na moto, ukifanya duara ya nuru, na mwangaza pande zote . . . Kukatokea katikati yake mfano wa viumbe hai vinne.” (Ezekieli 1:4, 5) Kila kimojapo viumbe hai vinne hivi, au makerubi, kilikuwa na mabawa manne na nyuso nne. Vilikuwa na uso wa simba, kuonyesha haki ya Yehova; uso wa ng’ombe ndume, kuonyesha nguvu za Yehova; na uso wa tai, kuonyesha hekima Yake. Pia vilikuwa na uso wa mwanadamu, kuwakilisha upendo wa Yehova.—Kumbukumbu 32:4; Ayubu 12:13; Isaya 40:26; Ezekieli 1:10; 1 Yohana 4:8.
4. Kwa nini makerubi walikuwa na nyuso nne, na makerubi walikuwa kama nini kwa mwendo?
4 Kila kerubi alikuwa na uso wenye kutazama katika mmoja wa pande nne. Hivyo, makerubi hao wangeweza kugeuza mwendo mara ile ile na kuufuata uso uliotazama upande uliotamaniwa. Lakini makerubi hao walikuwa kama nini kwa mwendo? Naam, wangeweza kusonga kwa mwendo wa umeme! (Ezekieli 1:14) Hakuna gari lolote lililofanyizwa na binadamu limepata kamwe kufikia mwendo huo.
5. Ezekieli alielezaje magurudumu ya gari na vivimbe vyayo?
5 Ghafula, magurudumu ya gari hilo yatokea. Jinsi yasivyo ya kawaida! Mistari 16 na 18 yasema: “Kuonekana kwake na kazi yake kulikuwa kana kwamba ni gurudumu ndani ya gurudumu lingine. . . . Vivimbe vyake vilikuwa virefu, vya kutisha; nayo yote manne, vivimbe vyake vimejaa macho pande zote.” Gurudumu moja kando ya kila kerubi lingefanya magurudumu manne yawe katika mahali panne penye kuhusiana. Magurudumu hayo yaling’aa nuru kama rangi ya zabarajadi, jiwe la manjano au chanikiwiti lenye kuona ndani au lenye kupenyeza nuru. Laongeza nuru na uzuri kwenye njozi hii tukufu. Kwa kuwa vivimbe vya magurudumu ‘vilijaa macho pande zote,’ hayakuwa yakienda upofu-upofu katika upande wowote tu. Na magurudumu hayo yalikuwa ya kimo kirefu mno, hivyo yakiweza kwenda umbali mkubwa kwa mzunguko mmoja tu wa mhimili wayo. Hayo, kama wale makerubi wanne, yangeweza kwenda kasi kama umeme.
Magurudumu Ndani ya Magurudumu
6. (a) Ilikuwaje kwamba gari lilikuwa na magurudumu ndani ya magurudumu? (b) Magurudumu yalipatanisha mwelekeo wa mwendo wao na nini?
6 Na jambo jingine lilikuwa lisilo la kawaida. Kila gurudumu lilikuwa na gurudumu ndani yalo la kipenyo kilekile na likiwa limewekwa kwa kukingama ndani ya gurudumu la nje. Ni kwa njia hiyo tu ingeweza kusemwa kwamba magurudumu “yalikwenda pande zote nne.” (Mstari 17) Mara moja, magurudumu yangeweza kubadili upande kwa sababu kulikuwako gurudumu lililoelekea katika kila upande. Magurudumu yalipatanisha upande yanakoenda na ule wa wale makerubi wanne. Kwa yale magurudumu manne, umbo la gari la Mungu lingeweza kwenda kwa utegemezo usioonekana kama chelezo chenye nguvu kinachoshikiliwa juu na kushoni ya hewa kipitapo juu ya maji.
7. Ni nini kilichokuwa chanzo cha nguvu za magurudumu?
7 Magurudumu yalipata wapi nguvu hiyo ya kujipatanisha na miendo yote ya wale makerubi wanne? Kutoka kwa roho takatifu ya Mungu Mweza Yote. Mstari wa 20 wasema: “Kila mahali ambako roho hiyo ilitaka kwenda, walikwenda . . . Roho ya viumbe hai ilikuwa ndani ya magurudumu.” Kani ya utendaji ile ile isiyoonekana ya Mungu iliyokuwa ndani ya makerubi ilikuwa katika magurudumu hayo.
8. Magurudumu yalipewa jina gani, na kwa nini?
8 Magurudumu hayo yana jina “Kisulisuli.” (Ezekieli 10:13) Kwa wazi jina hilo lilitokana na yale ambayo kila gurudumu hufanya. Laviringika au kuzunguka vuruvuru. Kuiita sehemu hii ya gari kwa jina kama hilo huvuta uangalifu kwenye mwendo ambao katika huo gari la kimbingu huenda. Ingawa magurudumu yalo yalikwenda vuruvuru kwa mwendo wa kasi sana, sikuzote yangeweza kuona njia yayo kwa sababu yalijaa macho.
9. Ezekieli alielezaje kilichokuwa juu ya yale magurudumu manne yenye kwenda kasi?
9 Lakini sasa acheni tutazame tuone ni nini kilicho juu ya magurudumu manne hayo yenye urefu wa kutisha, yenye kwenda kasi. Mstari wa 22 wa sura ya 1 wasema: “Tena juu ya vichwa vya viumbe hai palikuwa na kitu mfano wa anga, kama rangi ya bilauri, lenye kutisha, limetandwa juu ya vichwa vyao.” Anga hilo, lijapokuwa gumu, lilikuwa lenye kupenyeza nuru, “kama rangi ya bilauri, lenye kutisha.” Lilikuwa likimeremeta kama maelfu ya almasi wakati jua lizipigapo. Ni lenye kuvuvia hofu kweli kweli!
Yule Mpandaji wa Gari Tukufu
10. (a) Ni maelezo ya jinsi gani ambayo yatolewa juu ya kiti cha enzi na Aliye juu ya kiti cha enzi? (b) Ni nini chaonyeshwa na uhakika wa kwamba Mpandaji wa gari amezungukwa katika utukufu?
10 Kwa wazi, gari lasimama ili Mpandaji walo anene na Ezekieli. Juu ya anga, kuna mfanano wa kiti cha enzi, yakuti samawi, au buluu nzito. Pana Mtu fulani juu ya kiti cha enzi ambaye kuonekana kwake ni kama mwanadamu wa dunia. Umbo la kibinadamu ndilo lingeweza kumsaidia Ezekieli vizuri zaidi athamini udhihirisho huu wa kimungu. Lakini umbo hilo la kibinadamu lilifunikwa kwa utukufu, hivi kwamba liliwaka kama kaharabu, mchanganyiko wenye kuwaka wa fedha na dhahabu. Ni uzuri ulioje wenye kumetameta! Tokea kiuno cha umbo hili lililo kama mwanamume utukufu mzuri huo ulitanuka kuelekea juu na chini pia. Hivyo umbo lote limezungukwa kwa utukufu. Hii yaonyesha kwamba Yehova ni mtukufu isivyoelezeka. Zaidi ya hilo, Mpandaji wa gari ana upinde mzuri ukiambatana naye. Jinsi upinde unavyowasilisha utulivu na ustarehe baada ya dhoruba! Akiwa na mwelekeo huo wa utulivu, Yehova anadumisha sifa zake za hekima, haki, nguvu, na upendo katika usawa mkamilifu.
11. Ezekieli aliathiriwaje na njozi ya gari na kiti cha enzi cha Yehova?
11 Gari na kiti cha ufalme cha Yehova vimezungukwa na nuru na rangi za kupendeza. Ni tofauti kama nini na Shetani, mkuu wa giza na mafumbo mabaya ya ulimwengu wa roho! Naye Ezekieli aliathiriwaje na yote haya? “Nami nilipoona,” yeye asema, “nalianguka kifudifudi, nikasikia sauti ya mmoja anenaye.”—Ezekieli 1:28.
Kile Kilichoonyeshwa na Gari
12. Ni nini kifananishwacho na gari la kimbingu la Yehova?
12 Ni nini chenye kufananishwa na gari hili la ajabu? Ni lile tengenezo la kimbingu la Yehova Mungu. Hilo ni jumuiya ya viumbe wake wote wa roho watakatifu katika makao yasiyoonekana—maserafi, makerubi, na malaika. Kwa kuwa Yehova ndiye Mungu Aliye Juu Zaidi, viumbe wake wote wa roho wametiishwa chini yake, naye awapanda katika maana ya kuwatawala kwa fadhili na kuwatumia kulingana na kusudi lake.—Zaburi 103:20.
13. (a) Kwa nini yaweza kusemwa kwamba Yehova hupanda tengenezo lake? (b) Njozi ya gari la Yehova lenye magurudumu manne likiwa katika mwendo yakuathirije wewe?
13 Yehova hupanda tengenezo hili kana kwamba juu ya gari, akisababisha liende kokote roho yake yalihimiza kwenda. Halikimbii kwa fujo huku na huku, bila udhibiti au usimamizi wenye akili. Mungu haachi tengenezo hili liende upande wowote ambao lingeweza kuwa na mbetuko wa kuuelekea. Bali, lafuata mielekezo yake. Pamoja, wote wanasonga mbele kwa umoja hadi utimizo kamili wa makusudio ya Mungu. Ni tengenezo zuri kama nini la kimbingu linalofunuliwa na njozi hii ya gari la kimbingu la Yehova lenye magurudumu manne likiwa mwendoni! Kupatana na hilo, tengenezo la Yehova linaonyeshwa kuwa la pembe nne za mraba, likiwa katika usawa mkamilifu.
Awekwa Kuwa Mlinzi
14. Nani afananishwa na nabii Ezekieli?
14 Lakini ni nani anayewakilishwa na nabii Ezekieli? Kutokana na mambo hakika ya historia, ni wazi kwamba lile baraza la Mashahidi wa Yehova wapakwa-mafuta limeshirikishwa na gari la kimbingu. Hivyo, Ezekieli huwakilisha vizuri mabaki wapakwa-mafuta wa Mashahidi wa Yehova tangu mwaka 1919. Tengenezo la Yehova la kimbingu liliwasiliana kiroho na mabaki wapakwa-mafuta katika mwaka huo, kuwahuisha wakiwa Mashahidi wa Yehova kwenye ulimwengu wote. (Linganisha Ufunuo 11:1-12.) Tengenezo hilo lililo mfano wa gari lilikuwa katika mwendo wakati huo, kama lilivyo hata leo. Kwa uhakika, magurudumu yalo ya maendeleo yanazunguka kwa haraka zaidi ya wakati mwingineo. Yehova anapanda kasi kusonga mbele!
15. Sauti ya Mpandaji wa gari la kimbingu yasema nini, na Ezekieli apokea utume gani?
15 Ezekieli alitamani kujua ni kwa nini gari hili la kimbingu lilikuwa limekuja mbele yake na kusimama. Alipata kujua kwa kuwa sauti ilitoka kwa yule Mmoja aketiye juu ya gari. Kwa kulemewa na hisia kwa kuona ajabu hii, Ezekieli alijiangusha chini kifudifudi. Sikiliza wakati sauti ya Mpandaji wa gari la kimbingu isemapo: “Mwanadamu, simama kwa miguu yako, nami nitasema nawe.” (Ezekieli 2:1) Ndipo Yehova anapompa Ezekieli utume wa kuwa mlinzi na kuonya nyumba ya Israeli yenye kuasi. Hata anapewa utume wa kunena kwa jina la kimungu. Jina la Ezekieli humaanisha “Mungu Huimarisha.” Vivyo hivyo Mungu ameimarisha jamii ya Ezekieli na kuipeleka iende, akiwaweka wawe mlinzi kwa Jumuiya ya Wakristo.
16, 17. (a) Njozi ya gari la kimbingu ilimnufaishaje Ezekieli? (b) Katika siku yetu, uelewevu wa njozi ya gari la kimbingu umeathirije jamii ya Ezekieli na umati mkubwa?
16 Njozi ya gari la kimbingu ilithibitika kuwa yenye kumletea fikira nzito na kumduwaza Ezekieli, lakini pia ilimtayarisha kwa ajili ya utume wake akiwa mlinzi ili kusikizisha onyo la uharibifu wa Yerusalemu uliokuwa ukija. Ndivyo imekuwa leo. Uelewevu wao wa njozi ya gari la kimbingu la Yehova likiwa katika mwendo umekuwa na uvutano mkubwa juu ya mabaki wapakwa-mafuta. Katika 1931 walijifunza zaidi juu ya njozi ya Ezekieli, kama ilivyofunuliwa katika Vindication, Kitabu cha Kwanza. Wakati huo walijawa na uthamini mzito hivi kwamba kuanzia toleo la Oktoba 15, 1931, hadi lile la Agosti 1, 1950, muundo wa jalada la mbele la gazeti Mnara wa Mlinzi (Kiingereza) ulikuwa na wazo la msanii la njozi ya Ezekieli ya gari la kimbingu kwenye pembe ya juu ya mkono wa kulia. Hivyo, jamii ya Ezekieli imetekeleza utume waliopewa, nao wamekuwa wakitumikia wakiwa mlinzi, wakisikizisha onyo la kimungu. Wakati wa uharibifu wenye moto wa Jumuiya ya Wakristo kutoka kwa Yehova akiwa amekalia kiti chake cha enzi juu ya gari la kimbingu haujapata kamwe kukaribia kama sasa!
17 Leo, umati mkubwa wa watu wenye mfano wa kondoo wanashirikiana na mabaki wapakwa-mafuta. (Ufunuo 7:9) Pamoja, wanasikizisha onyo la uharibifu unaokuja juu ya Jumuiya ya Wakristo na mfumo huu wote wa mambo wa kiibilisi. Kazi hiyo ya kuonya inaendelea kwa haraka, na kama inavyoonyeshwa kwenye Ufunuo 14:6, 7, malaika wanaiunga mkono.
Kusonga Pamoja na Gari la Kimbingu
18. Ni nini lazima kifanywe ili kupata utegemezo wenye kuendelea wa malaika, nasi twapaswa kuwa na hisia nyepesi kufanya nini?
18 Malaika hao wenye kujitiisha husonga mbele kwa upatano wakiwa tengenezo la Mungu la kimbingu huku wakisaidia watumishi wa Yehova wa kidunia kutimiza utume wao wa kujulisha wazi maonyo ya hukumu ya kimungu. Ikiwa sisi tunatamani ulinzi na mwongozo wenye kuendelea wa watumishi hawa wenye uweza wa Mungu, sisi pia ni lazima tusonge mbele kwa upatano na kwenda sambamba na kisulisuli cha ufananisho. Zaidi ya hilo, tukiwa sehemu ya tengenezo lionekanalo la Yehova lenye kwenda sambamba na gari lake la kimbingu, ni lazima tuwe na hisia nyepesi kufuata miongozo ya roho ya Mungu. (Linganisha Wafilipi 2:13.) Ikiwa sisi ni Mashahidi wa Yehova, ni lazima tusonge upande mmoja na gari la kimbingu. Hakika ni lazima tusitende makusudio yenye kupingana nalo. Tunapopewa mwelekezo katika njia tupaswayo kuendea, tunapaswa kuufuata. Hivyo, kundi haligawanyiki.—1 Wakorintho 1:10.
19. (a) Kama vile magurudumu ya gari la kimbingu yalivyo na macho kotekote kuyazunguka, ni lazima watu wa Yehova wawe chonjo kwa jambo gani? (b) Mwendo wetu wa kitendo wapasa kuwa nini katika nyakati hizi zenye msukosuko?
19 Macho kuzunguka mviringo wote wa magurudumu ya gari huonyesha hali ya kuwa chonjo. Kama vile tengenezo la kimbingu lilivyo chonjo, ndivyo lazima nasi tuwe chonjo kuunga mkono tengenezo la Yehova la kidunia. Kundini, tunaweza kuonyesha uungaji mkono huo kwa kushirikiana na wazee wa kwetu. (Waebrania 13:17) Na katika nyakati hizi za msukosuko, Wakristo wanahitaji kushikamana kwa ukaribu sana na tengenezo la Yehova. Hatutaki kujifasiria matukio, kwa kuwa tukifanya hivyo hatungekuwa tukienda pamoja na lile gari la kimbingu la Yehova. Acheni sikuzote tujiulize, ‘Gari la kimbingu linakwenda njia gani?’ Tukisonga mbele pamoja na tengenezo lionekanalo, tutakuwa pia tukisonga mbele na lile tengenezo lisiloonekana.
20. Ni shauri gani zuri ambalo mtume Paulo atoa kwenye Wafilipi 3:13-16?
20 Kwa habari hii, Paulo aliandika hivi: “Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu. Basi, sisi tulio wakamilifu natuwaze hayo; na hata mkiwaza mengine katika jambo lo lote, Mungu atawafunulia hilo nalo. Lakini, hapo tulipofika na tuenende katika [kawaida, NW] lilo hilo.”—Wafilipi 3:13-16.
21. Ni kwa kufuata kawaida gani yawezekana kufanya maendeleo ya kiroho pamoja na tengenezo la Mungu?
21 Hapa neno “kawaida” halimaanishi zoea baya tu tusimoweza kujitoa. Watumishi wa Yehova wana kawaida nzuri ambayo kwayo wanafanya maendeleo ya kiroho. Ni kawaida ya kujitia katika funzo la kibinafsi la Biblia, kuhudhuria mikutano ya kundi, kuhubiri ha-bari njema za Ufalme kwa kawaida, na kuonyesha sifa za tengenezo la kimbingu la Mungu. Kawaida hiyo huwawezesha wafuate miongozo ya tengenezo la kimbingu la Yehova lililo kama gari. Kwa kudumu katika namna hii, tutafikia mradi wetu, iwe ni zawadi ya uhai usiokufa katika mbingu au uhai wa milele katika dunia paradiso.
22. (a) Ili mabaki wapakwa-mafuta na umati mkubwa wa kondoo wengine wapangwe kitengenezo kwa mwungamano, ni lazima nini lifanywe? (b) Ni nini kisichoepuka kuonwa na Yehova?
22 Kama vile Yohana 10:16 ionyeshavyo, “kondoo wengine” na jamii ya Ezekieli wangekuwa wamepangwa kitengenezo kwa mwungamano. Hivyo, ni jambo la maana sana wote katika tengenezo la Yehova waelewe maana kamili na ubora wa njozi iliyoandikwa katika Ezekieli sura 1 ikiwa wataenda kwa mapatano na gari la kimbingu la Mungu. Njozi yalo yatusaidia kuthamini kwamba twapaswa kwenda kwa upatano na tengenezo la Mungu, lionekanalo na lisiloonekana. Zingatieni, akilini, pia kwamba macho ya Yehova “hukimbia-kimbia duniani mwote, ili ajionyeshe mwenye nguvu kwa ajili ya hao, waliokamilika moyo kuelekea kwake.” (2 Nyakati 16:9) Hakuna hata jambo moja ambalo huepuka kuonwa na Yehova, hasa lolote linalohusu kusudi lake la kujitetea kuwa Mwenye Enzi Kuu wa Ulimwengu Wote Mzima.
23. Gari la kimbingu la Yehova likiwa katika mwendo, ni lazima sisi tufanye nini?
23 Kwa uhakika gari la kimbingu la Yehova liko katika mwendo leo. Karibuni kila kitu kitaletwa kwenye utukufu kupatana na Mtukufu aendeshaye gari hilo—yote kwa kumtetea yeye kuwa Bwana Mwenye Enzi Kuu wa ulimwengu wote mzima. Maserafi wake, makerubi, na malaika wanatutegemeza katika kazi yetu kubwa ya kuhubiri ulimwenguni pote. Basi, acheni sisi tusonge mbele na twende mbele na tengenezo la kimbingu la Yehova. Lakini ni jinsi gani twaweza kuendelea sambamba na gari hilo la kimbingu lenye kwenda kasi?
Wewe Ungejibuje?
◻ Ni sifa gani ziwakilishwazo na wale viumbe hai wanne walioonwa na Ezekieli?
◻ Gari la kimbingu la Yehova lafananisha nini?
◻ Nani afananishwa na Ezekieli nabii wa Mungu?
◻ Uelewevu wa gari la kimbingu la Yehova umeathirije jamii ya Ezekieli na umati mkubwa?