HEKALU
Nyumba ya kimungu, mahali patakatifu au patakatifu, iwe ni pa kihalisi au pa kiroho, panapotumiwa kwa ajili ya ibada. Neno la Kiebrania heh·khalʹ, linalotafsiriwa “hekalu,” pia linamaanisha “jumba la mfalme.” Maneno ya Kigiriki hi·e·ronʹ na na·osʹ hutafsiriwa “hekalu” na yanaweza kurejezea majengo yote ya hekalu au hekalu lenyewe; nyakati nyingine neno na·osʹ, linalomaanisha “patakatifu” au “makao ya kimungu,” hurejezea hasa vyumba vitakatifu vya ndani ya hekalu.—TazamaMAHALI PATAKATIFU.
Hekalu la Sulemani. Mfalme Daudi alitamani sana kumjengea Yehova nyumba, ili kulihifadhi sanduku la agano, lililokuwa “linakaa katikati ya vitambaa vya mahema.” Yehova alipendezwa na pendekezo la Daudi lakini akamwambia kwamba kwa kuwa alimwaga damu nyingi vitani, mwanawe (Sulemani) angepewa pendeleo la kujenga hekalu. Hilo halimaanishi kwamba Mungu hakukubaliana na vita ambavyo Daudi alipigana kwa ajili ya jina la Yehova na watu wake. Hata hivyo, hekalu lilipaswa kujengwa kwa amani na mtu mwenye amani.—2Sa 7:1-16; 1Fa 5:3-5; 8:17; 1Nya 17:1-14; 22:6-10.
Gharama za Ujenzi. Baadaye Daudi alinunua uwanja wa kupuria wa Ornani (Arauna) Myebusi kwenye Mlima Moria kwa ajili ya kujenga hekalu. (2Sa 24:24, 25; 1Nya 21:24, 25) Alikusanya talanta 100,000 za dhahabu, talanta 1,000,000 za fedha, na shaba na chuma kwa wingi sana, na pia akatoa mchango kutoka kwa mali zake mwenyewe wa talanta 3,000 za dhahabu na talanta 7,000 za fedha. Pia alipokea kutoka kwa wakuu mchango wa dhahabu ya talanta 5,000 na dariki 10,000 na fedha ya talanta 10,000, na pia chuma na shaba kwa wingi. (1Nya 22:14; 29:3-7) Kwa ujumla, alikusanya talanta 108,000 na dariki 10,000 za dhahabu na talanta 1,017,000 za fedha, zenye thamani ya kisasa ya dola za Marekani 48,337,047,000. Sulemani mwanawe hakutumia kiasi hicho chote kujenga hekalu; kiasi kilichobaki alikiweka katika hazina ya hekalu.—1Fal 7:51; 2Nya 5:1.
Wafanyakazi. Mfalme Sulemani alianza kujenga hekalu la Yehova katika mwaka wa nne wa utawala wake (1034 K.W.K.), katika mwezi wa pili, Zivu, akitumia ramani ambayo Daudi alipewa na Mungu. (1Fal 6:1; 1Nya 28:11-19) Kazi hiyo ilifanywa kwa kipindi cha miaka saba. (1Fal 6:37, 38) Hiramu, Mfalme wa Tiro, alipewa ngano, shayiri, mafuta, na divai, naye akaleta mbao kutoka Lebanoni pamoja na wafanyakazi stadi wa mbao na mawe, na mtaalamu mmoja, ambaye pia aliitwa Hiramu, na baba yake alikuwa Mtiro na mama yake Mwisraeli wa kabila la Naftali. Alikuwa fundi stadi wa dhahabu, fedha, shaba, chuma, mbao, na vitambaa.—1Fal 5:8-11, 18; 7:13, 14, 40, 45; 2Nya 2:13-16.
Ili kupanga kazi, Sulemani aliwaandikisha wanaume 30,000 Waisraeli, akawatuma Lebanoni walikuwa vikundi vitatu vya watu 10,000 na kila kikundi kilifanya kazi kwa zamu ya mwezi mmoja, na kukaa nyumbani kwa miezi miwili. (1Fal 5:13, 14) Pia, aliandikisha vibarua 70,000 kutoka kwa “wakaaji wageni” waliokuwa nchini, na wakataji wa mawe, 80,000. (1Fal 5:15; 9:20, 21; 2Nya 2:2) Pia, Sulemani aliwaweka wakuu 550 na wakuu wasaidizi 3,300 ili wasimamie kazi. (1Nya 5:16; 9:22, 23) Inaonekana kwamba 250 kati yao walikuwa Waisraeli na 3,600 walikuwa “wakaaji wageni” katika Israeli.—2Nya 2:17, 18.
Urefu wa “mkono” uliotumiwa. Katika mazungumzo yafuatayo ya vipimo vya mahekalu matatu—yaliyojengwa na Sulemani, Zerubabeli, na Herode—tutatumia vipimo vya mkono wenye urefu wa sentimita 44.5 (inchi 17.5). Hata hivyo, inawezekana walitumia mkono mrefu zaidi wa sentimita 51.8 (inchi 20.4).—Linganisha na 2Nya 3:3 (ambalo linataja urefu wa mikono “kulingana na kipimo cha awali,” labda mikono hiyo ilikuwa mirefu kuliko mikono iliyotumiwa baadaye) na Eze 40:5; tazama MKONO.
Ramani na vifaa. Hekalu, ambalo lilikuwa jengo la kifahari zaidi, lilijengwa kwa ramani yenye muundo wa hema la ibada. Hata hivyo, vipimo vya ndani vya Patakatafu na Patakatifu Zaidi vilikuwa vikubwa kuliko vya hema la ibada. Patakatifu palikuwa na urefu wa mikono 40 (mita 17.8; futi 58.3), upana wa mikono 20 (mita 8.9; futi 29.2), na inaonekana lilikuwa na urefu wa mikono 30 (mita 13.4; futi 43.7). (1Fal 6:2, 17) Patakatifu Zaidi palikuwa mraba wenye mikono 20 kila upande. (1Fal 6:20; 2Nya 3:8) Pia, juu ya Patakatifu Zaidi kulikuwa na vyumba vya darini vilivyokuwa na urefu wa mikono 10 (mita 4.5; futi 14.6) hivi. (1Nya 28:11) Pia, kulikuwa na jengo kando ya hekalu lililozunguka pande tatu za hekalu, ambalo lilikuwa na vyumba vya kuhifadhi vitu, na kadhalika.—1Ki 6:4-6, 10.
Hekalu lilijengwa hasa kwa mawe na mbao. Sakafu ya vyumba hivyo ilifunikwa kwa mbao za mberoshi; upande wa ndani wa kuta ulikuwa na mbao za mierezi zenye michoro ya makerubi, mitende, na maua; kuta na dari ilifunikwa kabisa kwa dhahabu. (1Fal 6:15, 18, 21, 22, 29) Milango ya Patakatifu (kwenye mwingilio wa hekalu) ilitengenezwa kwa mbao za mberoshi—zilizochongwa na kufunikwa kwa bamba jembamba la dhahabu. (1Ki 6:34, 35) Mwingilio kati ya Patakatifu na Patakatifu Zaidi ulitengenezwa kwa mbao za mfuta, ambazo pia zilichongwa na kufunikwa kwa dhahabu. Ingawa kulikuwa na milango, bado kulikuwa na pazia kama lile lililokuwa katika hema la ibada. (Linganisha na 2Nya 3:14.) Makerubi wawili wakubwa waliotengenezwa kwa mbao za mfuta, zilizofunikwa kwa dhahabu, walikuwa kwenye Patakatifu Zaidi. Chini yao kulikuwa na sanduku la agano.—1Fal 6:23-28, 31-33; 8:6; pia tazama KERUBI Na. 1.
Vyombo vyote vya patakatifu vilikuwa vya dhahabu: madhabahu ya uvumba, meza kumi za mikate ya wonyesho, vinara kumi vya taa, na vyombo vingine. Kando ya mwingilio wa Patakatifu (chumba cha kwanza) kulikuwa na nguzo mbili za shaba, zilizoitwa “Yakini” na “Boazi.” (1Fal 7:15-22, 48-50; 1Nya 28:16; 2Nya 4:8; tazama BOAZI, II.) Ua wa ndani ulitengenezwa kwa mbao za mierezi na mawe yaliyochongwa. (1Fal 6:36) Vitu vilivyokuwa katika ua, madhabahu ya kutolea dhabihu, “bahari [kubwa] ya kuyeyushwa,” magari kumi ya mabeseni ya maji, na vyombo vingine vilitengenezwa kwa shaba. (1Fal 7:23-47) Kulikuwa na vyumba vya kulia chakula kuzunguka ua.—1Nya 28:12.
Jambo la pekee kuhusu ujenzi wa hekalu hilo ni kwamba mawe yote yalichongewa kwenye eneo yalipochimbwa, hivi kwamba yalitoshea vizuri kwenye eneo la ujenzi. “Hakuna nyundo wala mashoka wala kifaa chochote cha chuma kilichosikika katika nyumba hiyo ilipokuwa ikijengwa.” (1Fal 6:7) Kazi hiyo ilikamilishwa kwa miaka saba na nusu (kuanzia majira ya kuchipua ya 1034 K.W.K. hadi majira ya kupukutika [Buli, mwezi wa nane] 1027 K.W.K.).—1Fal 6:1, 38.
Kuzinduliwa. Katika mwezi wa saba, yaani, Ethanimu, inaelekea katika mwaka wa 12 wa utawala wa Sulemani (1026 K.W.K.), Sulemani aliwakusanya wanaume Waisraeli huko Yerusalemu kwa ajili ya kuzinduliwa kwa hekalu na Sherehe ya Vibanda. Hema la ibada pamoja na vifaa vyake vitakatifu lililetwa, na sanduku la agano likawekwa ndani ya Patakatifu Zaidi. (Tazama PATAKATIFU ZAIDI.) Kisha wingu la Yehova likalifunika hekalu. Sulemani akambariki Yehova na kutaniko la Israeli, na akiwa amesimama kwenye jukwaa la pekee mbele ya madhabahu ya shaba ya kutolea dhabihu (tazama MADHABAHU), akatoa sala ndefu akimsifu Yehova na kuomba upendo mshikamanifu na rehema kwa ajili ya wale waliomgeukia Mungu ili kumwogopa na kumtumikia, Waisraeli na watu wa mataifa mengine. Dhabihu kubwa ilitolewa, ilitia ndani ng’ombe 22,000 na kondoo 120,000. Uzinduzi ulifanywa kwa siku 7, na Sherehe ya Vibanda kwa siku 7, na baadaye, siku ya 23 ya mwezi, Sulemani akawaacha watu waende nyumbani wakiwa na shangwe wakimshukuru Yehova kwa wema na ukarimu wake.—1Fal 8; 2Nya 5:1–7:10; tazama SULEMANI (Kuzinduliwa kwa hekalu).
Historia. Hekalu hilo lilidumu mpaka mwaka wa 607 K.W.K., lilipoharibiwa na jeshi la Babiloni likiongozwa na Mfalme Nebukadneza. (2Fal 25:9; 2Nya 36:19; Yer 52:13) Waisraeli walipojihusisha na ibada ya uwongo, Mungu aliruhusu mataifa yashambulie Yuda na Yerusalemu, na nyakati nyingine walipora hazina ya hekalu. Pia, kuna vipindi ambapo hekalu lilipuuzwa. Mfalme Shishaki wa Misri alipora hazina ya hekalu (993 K.W.K.) katika siku za Rehoboamu mwana wa Sulemani, miaka 33 tu baada ya hekalu kuzinduliwa. (1Fal 14:25, 26; 2Ch 12:9) Mfalme Asa (977-937 K.W.K.) aliiheshimu nyumba ya Yehova, lakini ili kulinda Yerusalemu, kwa upumbavu alimhonga Mfalme Ben-hadadi wa kwanza wa Siria, kwa fedha na dhahabu kutoka kwa hazina ya hekalu, ili kuvunja agano lake na Baasha mfalme wa Israeli.—1Fal 15:18, 19; 2Nya 15:17, 18; 16:2, 3.
Baada ya kipindi cha msukosuko na kupuuzwa kwa hekalu, Mfalme Yehoashi wa Yuda (898-859 K.W.K.) alisimamia kazi ya kulirekebisha hekalu. (2Fal 12:4-12; 2Nya 24:4-14) Katika siku za Amazia mwanawe, Yehoashi mfalme wa Israeli alilipora. (2Fal 14:13, 14) Mfalme Yothamu (777-762 K.W.K.) alifanya kazi ya ujenzi katika eneo la hekalu, na kujenga “lango la juu.” (2Fal 15:32, 35; 2Nya 27:1, 3) Mfalme Ahazi wa Yuda (761-746 K.W.K.) alipeleka hazina za hekalu kwa Tiglathi-pileseri wa Tatu, mfalme wa Ashuru, ili kumhonga na pia akalichafua hekalu kwa kuondoa madhabahu ya shaba iliyokuwa hakaluni na badala yake akajenga madhabahu iliyofanana na ile iyokuwa Damasko. (2Fal 16:5-16) Mwishowe akafunga malango ya nyumba ya Yehova.—2Nya 28:24.
Hezekia, mwana wa Ahazi (745-717 K.W.K.) alijitahidi kabisa kurekebisha uovu wa baba yake. Mwanzoni kabisa mwa utawala wake, alilifungua tena hekalu na kulisafisha. (2Nya 29:3, 15, 16) Hata hivyo, baadaye, kwa sababu ya kumwogopa Senakeribu mfalme wa Ashuru, Hezekia aling’oa milango na miimo ya hekalu ambayo yeye mwenyewe aliagiza ifunikwe kwa dhahabu, akaipeleka kwa Senakeribu.—2Fal 18:15, 16.
Lakini Hezekia alipokufa, kwa miaka 50 hekalu lilichafuliwa na halikurekebishwa. Manase mwanawe (716-662 K.W.K.) alifanya uovu kuliko wafalme wote wa Yuda waliomtangulia, akajenga nguzo “kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni katika nyua mbili za nyumba ya Yehova.” (2Fal 21:1-5; 2Nya 33:1-4) Kufikia wakati wa Manase, mjukuu wa Yosia (659-629 K.W.K.), jengo hilo ambalo zamani lilikuwa lenye fahari lilikuwa limeharibika. Inaonekana halikuwa na mpangilio na vitu vilitapakaa, kwa maana Kuhani Mkuu Hilkia alipopata kitabu cha Sheria (inaelekea ni hati ya awali iliyoandikwa na Musa) lilikuwa jambo la kustaajabisha. (2Fal 22:3-13; 2Nya 34:8-21) Baada ya hekalu kurekebishwa na kusafishwa, walisherehekea Pasaka kubwa zaidi tangu siku za nabii Samweli. (2Fal 23:21-23; 2Nya 35:17-19) Huo ulikuwa wakati wa huduma ya nabii Yeremia. (Yer 1:1-3) Tangu wakati huo hadi hekalu lilipoharibiwa, liliendelea kuwa wazi na kutumiwa na makuhani, ingawa wengi wao walikuwa waovu.
Hekalu Lililojengwa na Zerubabeli. Kama nabii Isaya aliyetumwa na Yehova alivyotabiri, Yehova alimtumia Koreshi mfalme wa Uajemi kuwakomboa Waisraeli kutoka mikononi mwa Babiloni. (Isa 45:1) Pia, Yehova aliwachochea watu wake wakiongozwa na Zerubabeli wa kabila la Yuda warudi Yerusalemu. Walirudi mwaka wa 537 K.W.K., baada ya nchi kukaa ukiwa kwa miaka 70, kama nabii Yeremia alivyotabiri, kwa kusudi la kujenga upya Yerusalemu. (Ezr 1:1-6; 2:1, 2; Yer 29:10) Jengo hilo, ingawa halikuwa na utukufu kama hekalu la Sulemani, lilidumu kwa muda mrefu zaidi, karibu miaka 500, tangu 515 K.W.K. hadi mwishoni kabisa mwa karne ya kwanza K.W.K. (Hekalu lililojengwa na Sulemani lilitumiwa kwa karibu miaka 420, kuanzia 1027 hadi 607 K.W.K.)
Koreshi aliagiza hivi: “Na mkaaji mgeni yeyote, popote alipo, majirani zake wamsaidie kwa kumpa fedha na dhahabu, mali na wanyama wa kufugwa, pamoja na toleo la hiari kwa ajili ya nyumba ya Mungu wa kweli, iliyokuwa Yerusalemu.” (Ezr 1:1-4) Vilevile Koreshi alirudisha vyombo 5,400 vya dhahabu na fedha ambavyo Nebukadneza alichukua katika hekalu la Sulemani.—Ezr 1:7-11.
Katika mwezi wa saba (Ethanimu, au Tishri) wa mwaka wa 537 K.W.K., madhabahu ilijengwa; na mwaka uliofuata, msingi wa hekalu jipya uliwekwa. Kama Sulemani alivyofanya, wajenzi waliwakodisha Wasidoni na Watiro walete mbao za mierezi kutoka Lebanoni. (Ezr 3:7) Wajenzi walivunjwa moyo na upinzani, hasa kutoka kwa Wasamaria, na baada ya miaka 15 wapinzani hao walimchochea mfalme wa Uajemi apige marufuku kazi hiyo.—Ezr 4.
Wajenzi waliacha kazi ya kujenga hekalu na kuanza kufanya mambo mengine, basi Yehova aliwatuma manabii Hagai na Zekaria wawachochee waanze tena ujenzi mwaka wa pili wa Dario wa Kwanza (520 K.W.K.), kisha agizo likatolewa lililounga mkono agizo la awali la Koreshi na kuagiza pesa zitolewe katika hazina ya mfalme, ili kununua vitu ambavyo wajenzi na makuhani walihitaji. (Ezr 5:1, 2; 6:1-12) Kazi ya ujenzi iliendelea, na nyumba ya Yehova ikakamilishwa siku ya tatu ya Adari katika mwaka wa sita wa Dario (inaelekea ni Machi 6 mwaka wa 515 K.W.K.), kisha Wayahudi wakazindua hekalu lililojengwa upya na wakasherehekea Pasaka.—Ezr 6:13-22.
Hatujui mengi kuhusu ramani ya ujenzi wa hekalu hili la pili. Agizo la Koreshi liliidhinisha ujenzi wa jengo lenye kimo cha ‘mikono 60 [c. 27 m; 88 ft], upana wa mikono 60, na safu tatu za mawe makubwa yaliyobingirishwa na kuwekwa mahali pake na safu moja ya mbao.” Urefu wake haukutajwa. (Ezr 6:3, 4) Lilikuwa na vyumba vya kulia chakula na maghala (Ne 13:4, 5), lilikuwa na vyumba vya darini , na inawezekana lilikuwa na majengo mengine, kama ilivyokuwa katika hekalu la Sulemani.
Hekalu hilo la pili halikuwa na sanduku la agano, inaonekana lilipotea kabla Nebukadneza hajateka na kulipora hekalu la Sulemani mwaka wa 607 K.W.K. Kulingana na masimulizi ya Kiapokrifa ya kitabu cha kwanza cha Makabayo (1:21-24, 57; 4:38, 44-51), kulikuwa na kinara kimoja cha taa badala ya vinara kumi kama ilivyokuwa katika hekalu la Sulemani; pia kinataja madhabahu ya dhahabu, meza ya mkate wa wonyesho, na vyombo, vilevile madhabahu ya dhabihu za kuteketezwa, ambayo, inafafanuliwa kuwa ya mawe, tofauti na madhabahu ya shaba iliyokuwa katika hekalu la Sulemani. Baada ya madhabahu hiyo kuchafuliwa na Mfalme Antioko Epifane (mwaka wa 168 K.W.K.), ilijengwa upya kwa mawe kwa mwongozo wa Yudasi Makabayo.
Hekalu Lililojengwa Upya na Herode. Maandiko hayalifafanui hekalu hilo kwa undani. Josephus hasa ndiye anayelifafanua, kwa kuwa aliliona hekalu hilo na kuandika kuhusu ujenzi wake katika maandishi ya The Jewish War na Jewish Antiquities. Mishna ya Kiyahudi inatoa habari fulani, pia kuna habari chache ambazo zimepatikana na watu wanaochimba vitu vya kale. Basi ufafanuzi tutakaotoa unategemea vyanzo hivyo, na huenda nyakati nyingine ukatiliwa shaka.—PICHA, Buku la. 2, uku. 543.
Katika The Jewish War (I, 401 [xxi, 1]), Josephus anasema kwamba Herode alilijenga upya hekalu katika mwaka wa 15 wa utawala wake, lakini kwenye Jewish Antiquities (XV, 380 [xi, 1]), anasema ilikuwa mwaka wa 18. Kwa ujumla, wasomi hukubaliana na tarehe hiyo ya pili, ingawa hatuwezi kuthibitisha kwa uhakika wakati ambao Herode alianza kutawala, na jinsi Josephus alivyopata tarehe hiyo. Patakatifu palijengwa kwa miezi 18, lakini ua, na sehemu nyingine zilijengwa kwa miaka minane. Wayahudi fulani walipomwendea Yesu Kristo mwaka wa 30 W.K., na kusema, “Hekalu hili lilijengwa kwa miaka 46” (Yoh 2:20), inaonekana Wayahudi hao walikuwa wakizungumza kuhusu kazi iliyokuwa ikiendelea kwenye majengo yaliyokuwa kwenye ua kufikia wakati huo. Kazi hiyo ilikamilishwa miaka sita hivi kabla ya hekalu hilo kuharibiwa mwaka wa 70 W.K.
Kwa kuwa Wayahudi walimchukia Herode na hawakumwamini, hawakumruhusu ajenge upya hekalu, kama alivyopendekeza, hadi alipoandaa vifaa vilivyohitajiwa kwa ajili ya jengo hilo jipya. Kwa sababu hiyohiyo, hawakuliona hekalu hilo kuwa la tatu, bali kama lililojengwa upya, na walizungumzia tu hekalu la kwanza na la pili (hekalu la Sulemani na la Zerubabeli).
Kuhusu vipimo ambavyo Josephus aliandika, Kamusi ya Smith Dictionary of the Bible (1889, Vol. IV, uku. 3203) inasema: “Vipimo vyake vya mlazo ni sahihi sana hivi kwamba tunadhani alipokuwa akiandika aliiona kwa macho ramani ya jengo hilo iliyokuwa katika idara ya jenerali wa jeshi la Tito. Ni tofauti na vipimo vyake vya kimo, vingi vikiwa vimezidishwa, hata mara mbili. Kwa kuwa majengo hayo yote yalibomolewa jiji lilipozingirwa, hatuwezi kumlaumu kwa makosa ya vipimo vya kimo.”
Mistari ya nguzo na malango. Josephus aliandika kwamba Herode alizidisha mara mbili ukubwa wa eneo la hekalu, akajenga kuta kubwa za mawe kwenye miteremko ya Mlima Moria na kusawazisha eneo lililokuwa kwenye kilele cha mlima huo. (The Jewish War, I, 401 [xxi, 1]; Jewish Antiquities, XV, 391-402 [xi, 3]) Mishna (Middot 2:1) inasema kwamba Hekalu la Mlimani lilikuwa na ukubwa wa mikono 500 (mita 223; futi 729) ya mraba. Ukingoni mwa eneo hilo kulikuwa na mistari ya nguzo. Hekalu hilo liliangalia Mashariki, kama mahekalu yaliyotangulia. Upande huo ulikuwa na eneo la nguzo za Sulemani, lililokuwa na mistari mitatu ya nguzo za marumaru. Pindi moja, majira ya baridi kali, Wayahudi fulani walimwendea Yesu hapo na kumuuliza kama alikuwa Kristo. (Yoh 10:22-24) Pia, kulikuwa na mistari ya nguzo upande wa Kaskazini na Magharibi ingawa zilikuwa ndogo kwa kulinganishwa na Nguzo za Kifalme zilizokuwa Kusini, ambazo zilikuwa na mistari minne ya nguzo za Wakorintho, jumla ya nguzo 162, na safu tatu. Nguzo hizo zilikuwa na unene mkubwa hivi kwamba watu watatu wangeweza kushikana mikono kuizunguka nguzo moja, na zilikuwa ndefu kuliko zile nguzo nyingine.
Inaonekana kulikuwa na malango manane yaliyoelekea kwenye eneo la hekalu: manne Magharibi, mawili Kusini, moja Mashariki, na lingine Kaskazini. (Tazama LANGO, GATEWAY [Malango ya Hekalu].) Kwa sababu ya malango hayo, ua wa kwanza, yaani, ua wa Watu wa Mataifa, ulitumiwa pia kama njia ya mkato, wasafiri walipendelea kupita hapo badala ya kuzunguka nje ya eneo la hekalu.
Ua wa Watu wa Mataifa. Eneo la Ua wa Watu wa Mataifa lilizungukwa na mistari ya nguzo, na eneo hilo liliitwa hivyo kwa sababu Watu wa Mataifa waliruhusiwa kuingia hapo. Hapo ndipo ambapo Yesu, mwanzoni mwa huduma yake na karibu na mwisho wa huduma yake duniani, aliwafukuza watu waliokuwa wameifanya nyumba ya Baba yake iwe nyumba ya biashara.—Yoh 2:13-17; Mt 21:12, 13; Mr 11:15-18.
Kulikuwa na nyua kadhaa ambazo mtu alipita kabla ya kufika kwenye jengo la katikati, yaani, patakatifu penyewe. Kila ua uliofuata ulikuwa na kiwango cha juu cha utakatifu kuliko ua uliotangulia. Baada ya kupita Ua wa Watu wa Mataifa, kulikuwa na ukuta wenye kimo cha mikono mitatu (mita 1.3; futi 4.4), na nafasi za kuingilia. Juu ya ukuta huo kulikuwa na mawe makubwa yaliyoandikwa onyo kwa Kigiriki na Kilatini. Maandishi ya Kigiriki yalisema hivi (kulingana na tafsiri moja): “Mtu yeyote wa taifa la kigeni asiingie katika eneo lililozingirwa na uzio unaozunguka patakatifu. Atakayepatikana atabeba hatia ya kifo chake.” (The New Westminster Dictionary of the Bible, iliyohaririwa na H. Gehman, 1970, uku. 932) Mtume Paulo aliposhambuliwa na umati hekaluni, ni kwa sababu Wayahudi walieneza uvumi kwamba alikuwa amemwingiza Mtu wa Mataifa katika eneo ambalo hakuruhusiwa kuingia. Paulo anatukumbusha kuhusu ukuta huo, ingawa alikuwa akizungumzia “ukuta” kwa njia ya mfano, tunaposoma kwamba Kristo ‘aliuharibu ukuta’ uliowatenganisha Wayahudi na Watu wa Mataifa.—Efe 2:14; Mdo 21:20-32.
Ua wa Wanawake. Mtu alipanda ngazi 14 ili kufika kwenye Ua wa Wanawake. Wanawake walienda hapo ili kuabudu. Kati ya vitu vingine, kulikuwa na masanduku ya michango kwenye Ua wa Wanawake, na Yesu alikuwa amesimama karibu na sanduku moja alipompongeza mjane kwa kutoa yote aliyokuwa nayo. (Lu 21:1-4) Kulikuwa na majengo kadhaa katika ua huo.
Ua wa Waisraeli na Ua wa Makuhani. Ili kufika kwenye Ua wa Waisraeli kulikuwa na ngazi kubwa kumi na tano zenye muundo wa nusu duara, ambapo wanaume waliokuwa safi kisherehe waliingia. Upande wa nje wa ukuta wa ua huo kulikuwa na maghala.
Pia, kulikuwa na Ua wa Makuhani uliofanana na ua wa hema la ibada. Ndani yake kulikuwa na madhabahu iliyotengenezwa kwa mawe ambayo hayakuwa yamechongwa. Kulingana na Mishna, ua huo ulikuwa na sakafu yenye ukubwa wa mikono 32 (mita 14.2; futi 46.7) ya mraba. (Middot 3:1) Josephus anasema ua huo ulikuwa mkubwa zaidi. (The Jewish War, V, 225 [v, 6]; ona MADHABAHU [Madhabahu ya Baada ya Utekwa].) Makuhani walipanda kwenye madhabahu kupitia sehemu yenye mwinuko. Kulingana na Mishna pia kuna ‘beseni’ lililotumiwa. (Middot 3:6) Pia, kulikuwa na majengo kadhaa kuzunguka ua huo.
Hekalu. Kama lile hekalu la zamani, hekalu hili lilikuwa na vyumba viwili, Patakatifu na Patakatifu Zaidi. Ili kufikia sakafu ya jumba hilo ungepanda ngazi 12 kutoka kwenye Ua wa Makuhani. Kulikuwa na vyumba vidogo kando kando mwa jumba hilo kama vile vilivyokuwa katika hekalu la Sulemani na kulikuwa na chumba cha juu. Mwingilio ulikuwa na milango ya dhahabu, kila moja ya milango hiyo ikiwa na kimo cha mita 24.5 au futi 80.2 na upana wa mita 7.1 au futi 23.3. Upande wa mbele wa jumba hilo ulikuwa mpana zaidi ya upande wa nyuma, ukiwa na sehemu zilizotokeza pande zote zenye urefu wa mita 8.9 au futi 29.2 kila upande. Patakatifu palikuwa na urefu wa mita 17.8 au futi 58.3 na upana wa mita 8.9 au futi 29.2. Ndani ya Patakatifu kulikuwa na kinara cha taa, meza ya mkate wa wonyesho, na madhabahu ya uvumba—yote yalitengenezwa kwa dhahabu.
Katika mwingilio wa Patakatifu Zaidi kulikuwa na pazia nzito maridadi lililopambwa vizuri. Yesu alipokufa pazia hilo lilipasuka mara mbili kutoka juu mpaka chini, likafunua kwamba sanduku la agano halikuwa katika Patakatifu Zaidi. Mahali pa Sanduku hilo kulikuwa na jiwe ambalo kuhani mkuu alinyunyizia damu Siku ya Upatanisho. (Mt 27:51; Ebr 6:19; 10:20) Chumba hicho kilikuwa na urefu wa mita 8.9 au futi 29.2 na upana wa mita 8.9 au futi 29.2.
Wayahudi walitumia eneo la hekalu kama ngome wakati Waroma walipozingira jiji la Yerusalemu mwaka wa 70 W.K. Wao wenyewe waliteketeza mistari ya nguzo, lakini askari Mroma aliteketeza hekalu lenyewe kinyume na mapenzi ya amiri-jeshi mkuu wa jeshi la Roma Tito, na hivyo kutimiza maneno haya ya Yesu kuhusu majengo ya hekalu: “Hakuna jiwe litakaloachwa hapa juu ya jiwe nalo lisiangushwe chini.”—Mt 24:2; The Jewish War, VI, 252-266 (iv, 5-7); VII, 3, 4 (i, 1).
Hekalu Kubwa la Kiroho la Yehova. Maskani iliyotengenezwa na Musa na mahekalu yaliyotengenezwa na Sulemani, Zerubabeli, na Herode yalikuwa mifano tu. Jambo hilo lilionyeshwa na mtume Paulo alipoandika kwamba maskani, na mambo ya msingi yaliyokuwamo ambayo yalikuwa pia katika mahekalu ya baadaye, ilikuwa “mfano wa uhalisi na kivuli cha vitu vya mbinguni.” (Ebr 8:1-5; ona pia 1Fa 8:27; Isa 66:1; Mdo 7:48; 17:24.) Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo yanafunua uhalisi wa mambo hayo. Maandiko hayo yanaonyesha kwamba maskani na mahekalu yaliyojengwa na Sulemani, Zerubabeli, na Herode, pamoja na mambo yake yote, yanawakilisha hekalu kubwa la kiroho la Yehova, “hema la kweli, ambalo Yehova alisimamisha, na si mwanadamu.” (Ebr 8:2) Kama inavyoonyeshwa na sehemu mbalimbali zilizokuwapo, hekalu hilo la kiroho ni mpango wa kumfikia Yehova katika ibada kwa msingi wa dhabihu ya upatanisho ya Yesu Kristo.—Ebr 9:2-10, 23.
Barua kwa Waebrania iliyoongozwa na roho takatifu inasema kwamba katika hekalu hilo la kiroho Patakatifu Zaidi ni “mbinguni kwenyewe,” eneo ambalo Mungu yupo. (Ebr 9:24) Kwa vile Patakatifu Zaidi ni “mbinguni kwenyewe,” basi Patakatifu na ua wa makuhani, na sehemu zake, lazima zinahusianishwa na vitu vya duniani, vitu vinavyohusiana na Yesu Kristo wakati wa huduma yake duniani na wafuasi wake ambao ni “washiriki wa mwito wa mbinguni.”—Ebr 3:1.
Pazia lilitenganisha Patakatifu na Patakatifu Zaidi; katika kisa cha Yesu lilifananisha “mwili wake,” ambao alihitaji kuutoa uwe dhabihu, kuuacha milele, ili aweze kuingia mbinguni, Patakatifu Zaidi halisi. (Ebr 10:20) Wakristo watiwa-mafuta lazima pia wapite kizuizi hicho cha mwili kinachowazuia kumfikia Mungu huko mbinguni. Basi Patakatifu panawakilisha hali yao wakiwa wana wa Mungu waliozaliwa kwa roho, walio na tumaini la kuishi mbinguni, nao watapokea thawabu yao mbinguni watakapoacha miili yao ya nyama katika kifo.—1Ko 15:50; Ebr 2:10.
Wakiwa bado katika Patakatifu halisi, wale ambao wametiwa mafuta kwa roho takatifu na wanaotumikia wakiwa makuhani wa cheo cha chini pamoja na Kristo wanaweza kufurahia nuru ya kiroho, kama kutoka kwa kinara cha taa; kula chakula cha kiroho, kama kutoka kwa meza ya mkate wa wonyesho; na kutoa sala, sifa, na utumishi kwa Mungu, kama kutoa uvumba yenye harufu tamu katika madhabahu ya uvumba ya dhahabu. Patakatifu pa hekalu la mfano palifichwa pasionekane na watu wa nje, vivyo hivyo, wale ambao si watiwa-mafuta hawawezi kuelewa mtu anajuaje kwamba yeye ni mwana wa Mungu aliyezaliwa kwa roho au mtu anahisije anapotiwa mafuta.—Ufu 14:3.
Katika ua wa kale wa hekalu kulikuwa na madhabahu ya kutoa dhabihu. Hilo liliwakilisha maandalizi ya Mungu, kulingana na mapenzi yake, ya dhabihu kamilifu ya kibinadamu inayokomboa wazao wa Adamu. (Ebr 10:1-10; 13:10-12; Zb 40:6-8) Katika hekalu la kiroho ua unahusianishwa na hali inayopatana na dhabihu hiyo. Katika kisa cha Yesu, ulikuwa mwili wake mkamilifu wa kibinadamu uliofanya dhabihu ya uhai wake ikubalike. Wafuasi wake wote watiwa-mafuta wanatangazwa kuwa waadilifu kwa msingi wa imani yao katika dhabihu ya Kristo, na hivyo Mungu anawaona kuwa wakamilifu wakiwa katika mwili.—Ro 3:24-26; 5:1, 9; 8:1.
Sehemu za “hema la kweli,” hekalu kubwa la kiroho la Mungu, zilikuwapo katika karne ya kwanza W.K. Hilo linaonyeshwa na maneno ya Paulo aliporejezea maskani iliyotengenezwa na Musa, alipoandika kwamba ilikuwa “mfano kwa ajili ya wakati uliowekwa ambao upo sasa,” yaani, kitu ambacho kilikuwapo wakati Paulo alikuwa akiandika maneno hayo. (Ebr 9:9) Hekalu hilo lilikuwapo wakati Yesu alipotoa thamani ya dhabihu yake katika Patakatifu Zaidi, mbinguni kwenyewe. Kwa kweli lazima lilikuwapo mwaka wa 29 W.K., wakati Yesu alipotiwa mafuta kwa roho takatifu atumikie akiwa Kuhani Mkuu zaidi wa Yehova.—Ebr 4:14; 9:11,12.
Yesu Kristo anaahidi Wakristo waliozaliwa kwa roho kwamba yule atakayeshinda, atakayevumilia kwa uaminifu hadi mwisho, atamfanya kuwa ”nguzo katika hekalu la Mungu wangu, naye hataondoka ndani yake tena kwa vyovyote.” (Ufu 3:12) Huyo atapewa nafasi ya kudumu huko “mbunguni kwenyewe,” Patakatifu Zaidi halisi.
Ufunuo 7:9-15 linafunua “umati mkubwa” wa waabudu wengine wa Yehova wakimtolea ibada safi katika hekalu la kiroho. Wale wanaofanyiza “umati mkubwa” hawatambulishwi kuwa makuhani wa cheo cha chini. Wale wanaofanyiza “umati mkubwa” wanasemwa kuwa “wamefua kanzu zao na kuzifanya nyeupe katika damu ya Mwana-Kondoo.” Kwa sababu ya imani yao katika dhabihu ya Kristo, wanahesabiwa kuwa waadilifu na hilo linafanya iwezekane kwao kuhifadhiwa katika “dhiki kuu,” kwa hiyo wanasemwa kuwa “wametoka katika ile dhiki kuu” wakiwa waokokaji.
Andiko la Isaya 2:1-4 na Mika 4:1-4, lilitabiri kuhusu ‘kuinuliwa’ kwa “mlima wa nyumba ya Yehova” katika “siku za mwisho,” na pia kuhusu kukusanywa kwa watu wa “mataifa yote” katika “nyumba ya Yehova.” Kwa vile hakujakuwa na hekalu halisi la Yehova huko Yerusalemu tangu mwaka wa 70 W.K., lazima maandiko hayo yanarejezea, si jengo halisi, bali kuinuliwa kwa ibada ya kweli katika maisha ya watu wa Yehova wakati wa “siku za mwisho” na kukusanywa kwa watu wa mataifa yote ili kuabudu katika hekalu kubwa la kiroho la Yehova.
Ufafanuzi wa ndani wa hekalu la Yehova unapatikana pia katika Ezekieli sura ya 40-47, lakini si hekalu lililojengwa juu ya Mlima Moria huko Yerusalemu, wala halingetoshea kwenye mlima huo. Kwa hiyo, lazima ni mfano mwingine wa hekalu kubwa la kiroho la Mungu. Mambo yanayokaziwa katika simulizi hilo ni kuhusu maandalizi yanayotoka kwenye hekalu na tahadhari zinazofuatwa ili kuwazuia wote wasiofaa wasiingie na kuabudu katika nyua zake.
Hekalu aliloona Ezekieli katika maono. Katika mwaka wa 593 K.W.K., mwaka wa 14 baada ya Yerusalemu kuharibiwa pamoja na hekalu la Sulemani lililokuwa katika jiji hilo, Ezekieli aliyekuwa kuhani na nabii, alipelekwa katika maono juu ya mlima mrefu sana, na aliona hekalu kubwa la Yehova. (Eze 40:1, 2) Ezekieli aliagizwa awaambie “watu wa nyumba ya Israeli” kila kitu alichoona ili kuwaaibisha Wayahudi waliopelekwa uhamishoni na kuwafanya watubu na pia kuwafariji waaminifu. (Eze 40:4; 43:10, 11) Maono hayo yalikuwa na vipimo hususa. Vipimo vilivyotumiwa vilikuwa “utete” (utete mrefu ulikuwa sawa na mita 3.11; futi 10.2) na “mkono” (mkono mrefu ulikuwa sawa na sentimita 51.8; inchi 20.4). (Eze 40:5, maelezo ya chini) Vipimo hivyo hususa vimefanya baadhi ya watu waamini kwamba hekalu katika maono hayo lililikuwa kielelezo cha hekalu ambalo baadaye lilijengwa na Zerubabeli, Wayahudi wahamishwa waliporudi. Hata hivyo, hakuna uthibitisho wa kutosha kuunga mkono wazo hilo.
Eneo lote la hekalu lilikuwa mraba wa mikono 500 kila upande. Lilikuwa na ua wa nje, ua wa ndani uliokuwa juu, hekalu na madhabahu yake, vyumba kadhaa vya kulia chakula, na jengo upande wa magharibi, yaani, upande wa nyuma wa hekalu. Kulikuwa na malango sita ya kuingilia, matatu kwa ajili ya ua wa ndani na matatu kwa ajili ya ua wa nje wa hekalu. Malango hayo yaliangalia upande wa kaskazini, mashariki na kusini, na kila lango la ndani lilitazamana na lango la nje. (Eze 40:6, 20, 23, 24, 27) Upande wa ndani wa ukuta kulikuwa na sakafu ya chini. Ilikuwa na upana wa mikono 50 (mita 25.9; futi 85), sawa na urefu wa malango. (Eze 40:18, 21) Hekalu lilikuwa na vyumba thelathini vya kulia chakula ambavyo huenda watu walivitumia kula dhabihu za ushirika. (Eze 40:17) Katika zile pembe nne za ua wa nje kulikuwa na mahali ambapo makuhani walipikia vipande vya dhabihu ambazo watu walileta kulingana na Sheria; na inaelekea walikula katika vyumba hivyo vya kulia chakula. (Eze 46:21-24) Sehemu iliyobaki ya ua wa nje kati ya sakafu ya chini na malango ya ua wa ndani ilikuwa na upana wa mikono 100.—Eze 40:19, 23, 27.
Vyumba vya kulia chakula vya makuhani vilikuwa karibu na hekalu na vilitenganishwa na vyumba vya watu. Viwili kati ya vyumba hivyo, pamoja na vyumba viwili vya kulia chakula vya waimbaji wa hekalu, vilikuwa katika ua wa ndani karibu na malango makubwa ya ndani. (Eze 40:38, 44-46) Makuhani pia walikuwa na vyumba vya kulia, vilivyokuwa kaskazini na kusini mwa patakatifu. (Eze 42:1-12) Vyumba hivyo vilitumiwa kula chakula, lakini pia makuhani walivitumia kuvua mavazi ya kitani waliyotumia katika utumishi wa hekalu kabla ya kwenda katika ua wa nje. (Eze 42:13, 14; 44:19) Pia katika eneo hilo, upande wa nyuma kulikuwa na sehemu ambazo makuhani walitumia kupikia na kuokea, sehemu hizo zilitumiwa kwa kusudi lilelile kama zile za ua wa nje, lakini zilitumiwa kwa ajili ya makuhani pekee.—Eze 46:19, 20.
Ili mtu aingie ua wa ndani, alipaswa kuvuka ua wa nje na kutumia lango la ua wa ndani. Ukingo wa ua wa ndani ulikuwa na urefu wa mikono 150 (mita 77.7; futi 255) kutoka ukingo wa ua wa nje upande wa mashariki, kaskazini na kusini. Ua wa ndani ulikuwa na upana wa mikono 200 (mita 103.6; futi 340). (Andiko la Ezekieli 40:47 linasema ua wa ndani ulikuwa na urefu wa mikono 100 mraba. Inaelekea eneo hilo linarejelea eneo lililo mbele ya hekalu ambalo linafikiwa kupitia malango ya ndani.) Madhabahu yalikuwa kwenye ua wa ndani.—Eze 43:13-17; tazama MADHABAHU (Madhabahu ya Hekalu la Ezekieli).
Ili kuingia chumba cha kwanza cha patakatifu, chenye urefu wa mikono 40 (mita 20.7; futi 68) na upana wa mikono 20 (mita 10.4; futi 34), kulikuwa na mlango wenye bawaba mbili. (Eze 41:23, 24) Ndani ya chumba hicho kulikuwa na “meza iliyo mbele za Yehova,” yaani, madhabahu ya mbao.—Eze 41:21, 22.
Kuta za nje za patakatifu zilikuwa na vyumba vyenye upana wa mikono minne (mita 2; futi 6.8) vilivyokuwa vimejengwa ukutani. Kulikuwa na ghorofa tatu, zenye vyumba 30 kwa kila ghorofa, kwenye ukuta wa magharibi, kaskazini, na kusini. (Eze 41:5, 6) Ili kupanda ghorofa hizo, upande wa kaskazini na upande wa kusini kulikuwa na njia zilizopindapinda, huenda zilikuwa ngazi za duara. (Eze 41:7) Upande wa magharibi au nyuma ya hekalu, kulikuwa na jengo lililoitwa bin·yanʹ, “jengo lililokuwa magharibi,” ambalo huenda lilianzia kaskazini kuelekea kusini. (Eze 41:12) Ingawa baadhi ya wasomi wamesema kwamba jengo hilo ni hekalu au patakatifu, hakuna uthibitisho wowote wa ulinganifu huo katika kitabu cha Ezekieli; “jengo lililokuwa magharibi,” lilitofautiana na patakatifu kwa umbo na vipimo. Bila shaka jengo hilo lilitumiwa kwa njia fulani kuhusiana na utumishi wa patakatifu. Katika upande wa magharibi wa hekalu la Sulemani,kulikuwa na jengo au majengo yanayofanana na jengo hilo.—Linganisha 2 Fal. 23:11 na 1 Nya. 26:18.
Patakatifu Zaidi palikuwa na umbo sawa na Patakafu Zaidi katika hekalu la Sulemani, palikuwa mraba wa mikono 20. Katika maono, Ezekieli aliona utukufu wa Yehova ukija kutoka mashariki na kulijaza hekalu. Yehova aliliita hekalu hilo “mahali pa kiti changu cha ufalme.”—Eze 43:1-7.
Ezekieli anaeleza kuhusu ukuta wenye urefu wa tete 500 (mita 1,555; futi 5,100) kila upande kuzunguka hekalu. Baadhi ya wasomi wanaamini kwamba ukuta huo ulikuwa umbali wa mita 600 (futi 2,000) kutoka ua ulipokuwa, na eneo hilo lilizungukwa na ukuta “ili kutenganisha kitu kitakatifu na kitu cha matumizi ya kawaida.”—Eze 42:16-20.
Ezekieli pia aliona kijito kikitiririka “kuelekea mashariki kutoka chini ya kizingiti cha hekalu” na kusini mwa madhabahu, na kikaongezeka na kuwa mto mkubwa wenye kina kikapita Araba na kuelekea upande wa kaskazini kabisa wa Bahari ya Chumvi. Mto huo uliponya maji ya Bahari yenye chumvi nayo yakawa na samaki wengi.—Eze 47:1-12.
Wakristo Watiwa Mafuta—Ni Hekalu la Kiroho. Wakristo watiwa mafuta walio duniani wanafananishwa na vitu vingi, kutia ndani hekalu. Ufananisho huo unafaa kwa kuwa roho ya Mungu hukaa katika kutaniko la watiwa mafuta. Paulo aliwaandikia Wakristo huko Efeso “katika muungano na Kristo Yesu,” wale ambao “mlitiwa muhuri kupitia . . . kwa roho takatifu iliyoahidiwa,” akisema: “Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ndiye jiwe la msingi la pembeni. Katika muungano naye, jengo lote likiwa limeunganishwa kwa upatano, linakua ili kuwa hekalu takatifu kwa ajili ya Yehova. Katika muungano naye, ninyi pia mnajengwa pamoja muwe mahali pa Mungu pa kukaa kupitia roho.” (Efe 1:1, 13; 2:20-22) Watu hao ‘waliotiwa muhuri,’ wamejengwa juu ya Msingi wa Kristo, idadi yao inatajwa kuwa 144,000. (Ufu 7:4; 14:1) Mtume Petro anawaita ‘mawe yaliyo hai yaliyojengwa kuwa nyumba ya kiroho kwa kusudi la ukuhani mtakatifu.’—1Pe 2:5.
Kwa kuwa makuhani hao wadogo ni “jengo la Mungu,” hataruhusu hekalu hili la kiroho lichafuliwe. Paulo anakazia utakatifu wa hekalu hilo la kiroho, na hatari itakayompata yeyote atakayejaribu kulichafua, anapoandika hivi: “Je, hamjui kwamba ninyi ni hekalu la Mungu, na kwamba roho ya Mungu inakaa ndani yenu? Yeyote akiliangamiza hekalu la Mungu, Mungu atamwangamiza; kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, nanyi ni hekalu hilo.”—1Ko 3:9, 16, 17; tazama pia 2Ko 6:16.
Yehova Mungu na Mwanakondoo ‘Ndio Hekalu Lake.’ Yohana alipoona Yerusalemu Jipya likishuka kutoka mbinguni, alisema: “Sikuona hekalu ndani yake, kwa maana Yehova Mungu Mweza-Yote ndiye hekalu lake, na pia Mwanakondoo.” (Ufu 21:2, 22) Kwa kuwa washiriki wa Yerusalemu Jipya watauona moja kwa moja uso wa Yehova mwenyewe, hawatahitaji hekalu ili kumwabudu. (1Yo 3:2; Ufu 22:3, 4) Wale wanaofanyiza Yerusalemu Jipya watamtolea Mungu moja kwa moja utumishi mtakatifu chini ya ukuhani mkuu wa Mwanakondoo, Yesu Kristo. Kwa sababu hiyo Mwanakondoo anashirikiana na Yehova kuwa hekalu la Yerusalemu Jipya.
Mlaghai. Mtume Paulo alipokuwa akionya kuhusu uasi ambao ungetokea, alimtaja “mtu wa uasi sheria” kuwa ameketi “katika hekalu la Mungu, akijionyesha waziwazi kuwa mungu.” (2Th 2:3, 4) “Mtu [huyo] wa uasi sheria” ni mwasi imani, mwalimu wa uwongo, basi anajiketisha katika kile anachodai kwa uwongo kuwa ni hekalu.—Tazama MTU WA UASI SHERIA.
Matumizi ya Mfano. Pindi moja, Wayahudi walipomwomba Yesu ishara, alijibu: “Libomoeni hekalu hili, na kwa siku tatu nitalisimamisha.” Wayahudi walidhani alikuwa akizungumzia majengo ya hekalu, lakini mtume Yohana anaeleza hivi: “Alikuwa akizungumza kuhusu hekalu la mwili wake.” Yehova, Baba yake Yesu alipomfufua siku ya tatu baada ya kufa, wanafunzi walikumbuka na kuelewa maneno hayo na wakayaamini. (Yoh 2:18-22; Mt 27:40) Alifufuliwa, lakini hakuwa na mwili wa kibinadamu, mwili wake ulitolewa uwe fidia; ingawa mwili huo haukuona uharibifu, lakini Mungu aliuondoa, kama vile dhabihu ilivyoteketezwa kwenye madhabahu. Yesu alipofufuliwa, alikuwa mtu yuleyule, mwenye utu uleule, katika mwili mpya uliofanyizwa kwa ajili ya makao yake mapya, mbingu za kiroho.—Lu 24:1-7; 1Pe 3:18; Mt 20:28; Mdo 2:31; Ebr 13:8.
[Picha kwenye ukurasa wa xxx]
Tangazo katika ua wa hekalu la Yerusalemu linalowaonya Watu wa Mataifa wasikaribie