Sura Ya Nane
Aokolewa Asiliwe na Simba!
1, 2. (a) Dario Mmedi alipangaje milki yake iliyopanuka? (b) Fafanua wajibu na mamlaka ya maliwali.
BABILONI lilikuwa limeanguka! Fahari yake ya karne moja likiwa serikali ya ulimwengu ilikuwa imekomeshwa kwa saa chache tu. Ulikuwa mwanzo wa muhula mpya—muhula wa Wamedi na Waajemi. Akitawala baada ya Belshaza, Dario Mmedi alikuwa na kazi ngumu ya kupanga milki yake iliyopanuka.
2 Mojawapo ya kazi za kwanza alizofanya Dario ilikuwa kuweka rasmi maliwali 120. Yaaminika kwamba nyakati nyingine wale waliokuwa na vyeo hivyo walichaguliwa miongoni mwa watu wa ukoo wa mfalme. Vyovyote vile, kila liwali alisimamia wilaya kubwa au wilaya ndogo ya milki hiyo. (Danieli 6:1) Wajibu wake ulitia ndani kukusanya kodi na kuzipeleka kwa makao ya mfalme. Ingawa alichunguzwa pindi kwa pindi na mwakilishi aliyezuru wa mfalme, liwali alikuwa na mamlaka kubwa. Jina la cheo chake lilimaanisha “mlinzi wa Ufalme.” Katika mkoa wake, liwali alionwa kuwa mfalme mdogo, mwenye mamlaka zote ila tu zile za mtawala wa nchi.
3, 4. Kwa nini Dario alimpendelea Danieli, naye akampa cheo gani?
3 Danieli alikuwa na fungu gani katika mpango huo mpya? Je, Dario Mmedi angemstaafisha nabii huyo Myahudi aliyezeeka, ambaye sasa alikuwa na umri wa miaka tisini na kitu? La, hasha! Huenda Dario alifahamu kwamba Danieli alikuwa amefasiri kwa usahihi kuanguka kwa Babiloni na kwamba utabiri huo ulihitaji ufahamu unaopita ule wa binadamu. Isitoshe, Danieli alikuwa amezoea kwa miaka mingi kushughulika na vikundi mbalimbali vya mateka katika Babiloni. Dario alitaka kuishi kwa amani na raia zake aliokuwa ametoka tu kuwashinda. Kwa hiyo, bila shaka angetaka mtu mwenye hekima na uzoefu kama Danieli awe mshauri wake. Akiwa na cheo gani?
4 Lingekuwa jambo lenye kushangaza iwapo Dario angemweka Danieli, mhamishwa Myahudi, awe liwali. Lakini hebu wazia zile rabsharabsha wakati ambapo Dario alitangaza uamuzi wake wa kumfanya Danieli awe mmoja wa mawaziri watatu ambao wangesimamia maliwali! Si hilo tu bali pia kwamba Danieli “alipata sifa,” akijithibitisha kuwashinda mawaziri wenzake. Kwa kweli, alikuwa na “roho bora.” Hata Dario aliazimu kumweka juu ya ufalme wote.—Danieli 6:2, 3.
5. Lazima wale mawaziri na maliwali wengine walihisije Danieli alipopewa cheo, na kwa nini?
5 Wale mawaziri wengine na maliwali lazima wawe walijawa hasira. Kwani, hawangevumilia kumwona Danieli—asiye Mmedi wala Mwajemi wala mshiriki wa familia ya mfalme—akiwa na mamlaka juu yao! Dario angewezaje kumkweza mgeni na kumpa umaarufu huo, akiwaruka watu wa nchi yake mwenyewe, hata watu wa familia yake mwenyewe? Lazima jambo hilo lilionekana kuwa lisilo la haki. Isitoshe, yaonekana kwamba maliwali waliuona uaminifu-maadili wa Danieli kuwa kizuizi kisichotakikana dhidi ya mazoea yao yasiyo ya haki na ya ufisadi. Hata hivyo, mawaziri na maliwali hao hawakuthubutu kumfikia Dario juu ya jambo hilo. Kwani, Dario alimstahi sana Danieli.
6. Mawaziri na maliwali walijaribuje kumshushia Danieli heshima, na kwa nini jitihada zao hazikufua dafu?
6 Kwa hiyo, wanasiasa hao wenye wivu wakapanga njama miongoni mwao. Walijaribu “kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme.” Je, namna alivyotimiza madaraka yake ingeweza kuwa na kosa lolote? Je, alikuwa mtu asiyefuatia haki? Mawaziri na maliwali hao hawakuweza kupata uzembe wowote au ufisadi wowote katika njia ambayo Danieli alitimiza wajibu wake. “Hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo,” wakajadiliana, “tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu wake.” Na hivyo ndivyo watu hao wenye hila walivyopanga njama. Walidhani ingemkomesha Danieli daima dawamu.—Danieli 6:4, 5.
NJAMA YA UUAJI YAANZA KUTEKELEZWA
7. Mawaziri na maliwali walimpendekezea mfalme nini, nao walifanyaje hivyo?
7 Dario alifikiwa na msafara wa mawaziri na maliwali ‘waliokusanyika pamoja mbele ya mfalme.’ Usemi wa Kiaramu unaotumiwa hapa una wazo la rabsharabsha zenye kelele. Yaonekana kwamba watu hao walifanya ionekane kana kwamba walikuwa na jambo la dharura la kumwambia Dario. Huenda walifikiri kwamba hangezusha maswali juu ya pendekezo lao ikiwa wangemwambia kwa usadikisho na kana kwamba ni jambo lililohitaji kuchukuliwa hatua mara moja. Kwa hiyo, wakataja jambo hilo moja kwa moja, wakisema: “Mawaziri wote wa ufalme, na manaibu, na maamiri, na madiwani, na maliwali wamefanya shauri pamoja ili kuweka amri ya kifalme; na kupiga marufuku, ya kwamba mtu ye yote atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme atatupwa katika tundu la simba.”a—Danieli 6:6, 7.
8. (a) Kwa nini Dario angeona sheria iliyopendekezwa kuwa yenye kupendeza? (b) Mawaziri na maliwali walikusudia nini hasa?
8 Rekodi za kihistoria zathibitisha kwamba lilikuwa jambo la kawaida kwa wafalme wa Mesopotamia kuonwa na kuabudiwa kama miungu. Kwa hiyo, bila shaka Dario alipendezwa na pendekezo hilo. Pia huenda jambo hilo lilionekana kuwa lenye faida. Kumbuka kwamba Dario alikuwa mgeni kwa watu waliokuwa wakiishi Babiloni. Sheria hiyo mpya ingemwimarisha akiwa mfalme, nayo ingechochea halaiki za watu waliokuwa wakiishi Babiloni wawe waaminifu na kuunga mkono serikali hiyo mpya. Ingawa hivyo, mawaziri na maliwali hawakupendezwa na hali nzuri ya mfalme walipokuwa wakipendekeza amri hiyo. Kusudi lao la kweli lilikuwa kumnasa Danieli, kwa kuwa walijua kwamba ilikuwa desturi yake kusali kwa Mungu mara tatu kwa siku kwenye madirisha yaliyo wazi katika chumba chake cha paa.
9. Kwa nini sheria hiyo mpya haingewatatiza watu wengi wasio Wayahudi?
9 Je, kizuizi hicho cha sala kingetatiza jumuiya zote za kidini za Babiloni? Sivyo, hasa kwa kuwa katazo hilo lingedumu mwezi mmoja tu. Isitoshe, ni watu wachache sana wasio Wayahudi ambao wangeona kuabudu mwanadamu kwa muda kuwa kuridhiana. Msomi mmoja wa Biblia ataarifu hivi: “Kumwabudu mfalme kulikuwa kawaida kwa mataifa hayo yenye kuabudu sanamu sana; na kwa hiyo Wababiloni walipoagizwa wamwabudu mshindi—Dario Mmedi—kama mungu, walikubali mara moja kufanya hivyo. Wayahudi peke yao ndio walioudhika na dai hilo.”
10. Wamedi na Waajemi waliionaje sheria iliyotungwa na mfalme wao?
10 Vyovyote vile, wageni wa Dario walimhimiza ‘apige marufuku, akatie sahihi maandiko hayo, yasibadilike, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi, isiyoweza kubadilika.’ (Danieli 6:8) Katika Mashariki ya kale, mapenzi ya mfalme yalionwa kuwa sheria kamili. Hilo lilitokeza dhana ya kwamba hangeweza kukosea. Hata sheria ambayo ingesababisha vifo vya watu wasio na hatia ilipaswa kuendelea kutumika!
11. Danieli angeathiriwaje na amri iliyotolewa na Dario?
11 Bila kumfikiria Danieli, Dario akatia sahihi amri hiyo. (Danieli 6:9) Kwa kufanya hivyo, alitia sahihi hati ya kuidhinisha kifo cha waziri wake aliyemthamini zaidi. Ndiyo, bila shaka Danieli angeathiriwa na amri hiyo.
DARIO ALAZIMIKA KUTOA HUKUMU KALI
12. (a) Danieli alifanya nini mara tu alipopata kujua juu ya sheria hiyo mpya? (b) Ni nani waliokuwa wakimtazama Danieli, na kwa nini?
12 Upesi Danieli akapata kujua juu ya sheria hiyo iliyokataza kutoa sala. Mara moja, akaingia nyumbani mwake na kwenda kwenye chumba cha paa, ambapo madirisha yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu.b Huko, Danieli akaanza kusali kwa Mungu “kama ilivyokuwa kawaida yake.” (BHN) Huenda Danieli alifikiri alikuwa peke yake, lakini waliompangia njama walikuwa wakimtazama. Ghafula,“waliingia ndani,” yamkini kwa njia ileile walivyokusanyika kwa rabsharabsha walipomwendea Dario. Sasa walikuwa wakiona kwa macho yao wenyewe—Danieli alikuwa “akiomba dua na kumsihi Mungu wake.” (Danieli 6:10, 11, BHN) Mawaziri na maliwali walikuwa na uthibitisho wote waliouhitaji wa kumshtaki Danieli mbele ya mfalme.
13. Adui za Danieli waliripoti nini kwa mfalme?
13 Adui za Danieli walimwuliza Dario kwa hila: “Je! hukuitia sahihi ile marufuku, ya kwamba kila mtu atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme, atatupwa katika tundu la simba?” Dario akajibu, akasema: “Neno hili ni kweli, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi isiyoweza kubadilika.” Sasa wapanga-njama hao wakasema mambo waziwazi. “Yule Danieli, aliye mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda, hakujali wewe, Ee mfalme, wala ile marufuku uliyoitia sahihi, bali aomba dua mara tatu kila siku.”—Danieli 6:12, 13.
14. Yaonekana ni kwa nini mawaziri na maliwali walimrejezea Danieli kuwa “mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda”?
14 Ni jambo lenye kutokeza kwamba mawaziri na maliwali walimrejezea Danieli kuwa “mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda.” Yaonekana kwamba walitaka kukazia kwamba Danieli ambaye Dario alikuwa amemkweza na kumpa umaarufu hivyo kwa hakika hakuwa mtu wa maana ila mtumwa Myahudi tu. Waliamini kwamba kwa sababu hiyo, alikuwa chini ya sheria—hata iwe mfalme alihisi namna gani juu yake!
15. (a) Dario alitendaje alipopashwa habari na mawaziri na maliwali? (b) Mawaziri na maliwali walionyeshaje hata zaidi kwamba walimdharau Danieli?
15 Huenda mawaziri na maliwali walimtarajia mfalme awathawabishe kwa kazi yao ya kupeleleza kwa werevu. Ikiwa ndivyo, basi waliambulia patupu. Dario alitaabishwa sana na habari alizopashwa. Badala ya kumkasirikia Danieli au kuagiza atupwe kwenye tundu la simba mara moja, Dario alijaribu siku nzima kumwokoa. Lakini hakufua dafu. Punde si punde wapanga-njama wakarudi, na bila haya wakadai Danieli auawe.—Danieli 6:14, 15.
16. (a) Kwa nini Dario alimheshimu Mungu wa Danieli? (b) Dario alikuwa na matumaini gani kuhusu Danieli?
16 Dario alihisi kwamba hana la kufanya kuhusu hilo. Sheria haingeweza kutanguliwa, wala “kosa” la Danieli halingeweza kusamehewa. Dario angeweza tu kumwambia Danieli “Mungu wako unayemtumikia daima, yeye atakuponya.” Yaonekana Dario alimheshimu Mungu wa Danieli. Yehova ndiye aliyekuwa amempa Danieli uwezo wa kutabiri kuanguka kwa Babiloni. Pia Mungu alikuwa amempa Danieli “roho bora,” iliyomtofautisha na wale mawaziri wengine. Huenda Dario alijua kwamba makumi ya miaka mapema, Mungu huyohuyo alikuwa amewaokoa vijana watatu Waebrania wasiteketee kwenye tanuru ya moto. Yamkini, mfalme alitumaini kwamba Yehova angemwokoa Danieli, kwa kuwa Dario hangeweza kubadili sheria aliyokuwa ametia sahihi. Basi, Danieli akatupwa katika tundu la simba.c Kisha, “likaletwa jiwe, likawekwa mdomoni mwa lile tundu; naye mfalme akalitia muhuri kwa muhuri yake mwenyewe, na kwa muhuri ya wakuu wake, lisibadilike neno lo lote katika habari za Danieli.”—Danieli 6:16, 17.
BADILIKO LENYE KUTOKEZA
17, 18. (a) Ni nini kionyeshacho kwamba Dario alisononeshwa na hali ya Danieli? (b) Ni nini kilichotukia mfalme aliporudi kwenye tundu la simba asubuhi iliyofuata?
17 Dario aliyesononeka akarudi kwenye makao yake. Hakuna wanamuziki walioletwa kumtumbuiza, kwa kuwa hakutaka. Badala yake, Dario alikesha kitandani usiku kucha, akifunga. “Usingizi wake ukampaa.” Alfajiri, Dario alienda haraka kwenye tundu la simba. Akapaaza sauti kwa huzuni: “Ee Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu wako, unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa?” (Danieli 6:18-20) Alishangaa na kutulizwa alipojibiwa!
18 “Ee mfalme, uishi milele.” Kwa salamu hiyo yenye staha, Danieli alionyesha kwamba hakuwa na uhasama kumwelekea mfalme. Alitambua kwamba matatizo yake hayakutokana na Dario, bali yalitokana na mawaziri na maliwali wenye husuda. (Linganisha Mathayo 5:44; Matendo 7:60.) Danieli akaendelea kusema: “Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno.”—Danieli 6:21, 22.
19. Mawaziri na maliwali walikuwa wamemdanganyaje Dario na kumwongoza kwa hila?
19 Lazima maneno hayo yawe yaliisumbua dhamiri ya Dario kama nini! Muda wote huo alijua kwamba Danieli hakuwa amefanya lolote la kustahili kutupwa kwenye tundu la simba. Dario alijua vizuri kwamba mawaziri na maliwali walikuwa wamepanga njama ya kumfanya Danieli auawe na kwamba walikuwa wamemwongoza mfalme kwa hila ili watimize nia zao zenye ubinafsi. Kwa kusisitiza kwamba “mawaziri wote wa ufalme” walikuwa wamependekeza amri hiyo ipitishwe, walidokeza kwamba Danieli pia alikuwa ameombwa maoni kuhusu hilo. (Italiki ni zetu.) Dario angewaonyesha watu hao wenye hila cha mtema kuni baadaye. Hata hivyo, kwanza alitoa amri Danieli atolewe kwenye tundu la simba. Kimuujiza, Danieli hakuwa amekwaruzwa hata kidogo!—Danieli 6:23.
20. Ni nini kilichowapata adui za Danieli waliokuwa na uchungu na uovu?
20 Sasa, kwa kuwa Danieli alikuwa salama salimini, Dario akawa na shughuli nyingine. “Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale watu waliomshitaki Danieli, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto wao, na wake zao; na wale simba wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande vipande, kabla hawajafika chini ya tundu.”d—Danieli 6:24.
21. Katika kushughulika na washiriki wa familia za wakosaji, ni tofauti gani iliyokuwapo kati ya Sheria ya Kimusa na sheria za tamaduni fulani za kale?
21 Huenda kuua wapanga-njama pamoja na wake zao na watoto wao kukaonwa kuwa ukali wa kupita kiasi. Kinyume cha hilo, Sheria ambayo Mungu alitoa kupitia nabii Musa ilitaarifu hivi: “Mababa wasiuawe kwa ajili ya watoto wao, wala watoto wasiuawe kwa ajili ya baba zao; kila mtu na auawe kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe.” (Kumbukumbu la Torati 24:16) Hata hivyo, katika tamaduni fulani za kale, kwa kawaida washiriki wa familia waliuawa pamoja na mkosaji, ikiwa alifanya kosa kubwa. Huenda hilo lilifanywa ili washiriki wa familia wasiweze kulipiza kisasi baadaye. Hata hivyo, tendo hilo dhidi ya familia za mawaziri na maliwali halikusababishwa na Danieli. Yaelekea, Danieli alisononeshwa na maafa ambayo watu hao waovu walikuwa wamesababishia familia zao.
22. Dario alitoa tangazo gani jipya?
22 Mawaziri na maliwali wenye kupanga njama walikuwa wamekufa. Dario alitoa tangazo lililotaarifu hivi: “Mimi naweka amri, ya kwamba katika mamlaka yote ya ufalme wangu watu watetemeke na kuogopa mbele za Mungu wa Danieli; maana yeye ndiye Mungu aliye hai, adumuye milele, na ufalme wake ni ufalme usioharibika, na mamlaka yake itadumu hata mwisho. Yeye huponya na kuokoa, hutenda ishara na maajabu mbinguni na duniani, ndiye aliyemponya Danieli na nguvu za simba.”—Danieli 6:25-27.
MTUMIKIE MUNGU DAIMA
23. Danieli aliweka kielelezo gani kuhusu kazi yake ya kimwili, nasi twawezaje kuwa kama yeye?
23 Danieli aliweka kielelezo kizuri kwa wote wanaomtumikia Mungu leo. Siku zote alikuwa na mwenendo mzuri. Katika kazi yake ya kimwili, Danieli “alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake.” (Danieli 6:4) Vivyo hivyo, Mkristo apaswa kufanya kazi yake ya kuajiriwa kwa bidii. Hilo halimaanishi awe mfanyabiashara mshindani anayetafuta mali kwa kila hali au anayepuuza hali-njema ya wengine ili kupata mafanikio zaidi. (1 Timotheo 6:10) Maandiko humtaka Mkristo atimize wajibu wake wa kikazi kwa kufuatia haki na kwa nafsi yote, “kama kwa Yehova.”—Wakolosai 3:22, 23; Tito 2:7, 8; Waebrania 13:18.
24. Danieli alijithibitishaje kuwa asiyeridhiana kwa habari ya ibada?
24 Danieli hakuridhiana ibada yake. Desturi yake ya kusali ilijulikana na watu wote. Isitoshe, mawaziri na maliwali walijua vizuri kwamba Danieli aliichukua ibada yake kwa uzito. Kwa kweli, walisadiki kwamba angedumisha kawaida yake hata ikiwa sheria iliikataza. Ni kielelezo kizuri kama nini kwa Wakristo leo! Wao pia wana sifa ya kutanguliza ibada ya Mungu. (Mathayo 6:33) Hilo lapaswa kuonekana waziwazi, kwa kuwa Yesu aliwaamuru hivi wafuasi wake: “Acheni nuru yenu ing’ae mbele ya watu, ili wapate kuona kazi zenu bora na kumpa utukufu Baba yenu aliye katika mbingu.”—Mathayo 5:16.
25, 26. (a) Huenda watu fulani wakakata kauli gani juu ya jinsi Danieli alivyotenda? (b) Kwa nini Danieli aliona badiliko katika kawaida yake kuwa sawa na kuridhiana?
25 Huenda wengine wakasema kwamba Danieli angeepuka mnyanyaso kwa kusali kwa Yehova kisiri kwa kipindi cha siku 30. Kwani, hakuna kikao hususa kinachohitajiwa ili kusikiwa na Mungu. Mungu hata anaweza kutambua kutafakari kwa moyo. (Zaburi 19:14) Hata hivyo, Danieli aliona badiliko lolote katika kawaida yake kuwa sawa na kuridhiana. Kwa nini?
26 Kwa kuwa desturi ya Danieli ya kusali ilijulikana na wengi, wangeonaje ikiwa angeacha tu mara moja? Huenda watazamaji wangekata kauli kwamba Danieli aliogopa mwanadamu na kwamba amri ya mfalme ilipita sheria ya Yehova. (Zaburi 118:6) Lakini Danieli alionyesha kwa matendo yake kwamba alijitoa kwa Yehova peke yake. (Kumbukumbu la Torati 6:14, 15; Isaya 42:8) Bila shaka, kwa kufanya hivyo Danieli hakudhihaki sheria ya mfalme kwa kukosa staha. Hata hivyo, hakuogopa na kuridhiana. Danieli aliendelea tu kusali katika chumba chake cha paa, “kama ilivyokuwa kawaida yake,” (BHN) kabla ya amri ya mfalme.
27. Watumishi wa Mungu leo wanawezaje kuwa kama Danieli katika (a) kunyenyekea mamlaka zilizo kubwa? (b) kumtii Mungu kuwa mtawala kuliko wanadamu? (c) kujitahidi kuishi kwa amani na watu wote?
27 Watumishi wa Mungu leo wanaweza kujifunza kutokana na kielelezo cha Danieli. Wao hudumisha “ujitiisho kwa mamlaka zilizo kubwa,” wakitii sheria za nchi wanamoishi. (Waroma 13:1) Walakini, sheria za mwanadamu zinapopingana na za Mungu, watu wa Yehova hudumisha msimamo wa mitume wa Yesu, waliotaarifu hivi kwa ujasiri: “Lazima sisi tumtii Mungu kuwa mtawala kuliko wanadamu.” (Matendo 5:29) Wanapofanya hivyo, Wakristo hawaanzishi maasi dhidi ya mamlaka. Badala yake, kusudi lao ni kuishi tu kwa amani na watu wote ili wapate “kuendelea kuishi maisha yaliyo shwari na matulivu pamoja na ujitoaji-kimungu kamili.”—1 Timotheo 2:1, 2; Waroma 12:18.
28. Danieli alimtumikiaje Mungu “daima”?
28 Dario alitaja mara mbili kwamba Danieli alikuwa akimtumikia Mungu “daima.” (Danieli 6:16, 20) Shina la neno la Kiaramu litafsiriwalo “daima” lamaanisha “kuzunguka.” Ladokeza wazo la mzunguko wenye kuendelea, au kitu chenye kuendelea. Ushikamanifu-maadili wa Danieli ulikuwa vivyo hivyo. Ulifuata mwendo uliojulikana. Ilijulikana wazi Danieli angefanyaje ikiwa angekabili majaribu, madogo au makubwa. Angedumisha mwenendo wake wa zaidi ya makumi kadhaa ya miaka—mwenendo wa uaminifu-mshikamanifu kwa Yehova.
29. Leo watumishi wa Yehova wanawezaje kunufaika na mwenendo mwaminifu wa Danieli?
29 Leo watumishi wa Mungu wanataka kufuata mwenendo wa Danieli. Kwa kweli, mtume Paulo alionya kwa upole Wakristo wote wafikirie kielelezo cha watu wa kale wenye kumcha Mungu. Kupitia imani, “wa[li]tekeleza uadilifu, wakapata ahadi,” na huenda kuhusu Danieli, “wakaziba vinywa vya simba.” Tukiwa watumishi wa Yehova leo, na tuonyeshe imani na kudumu kama Danieli na “tukimbie kwa uvumilivu shindano la mbio lililowekwa mbele yetu.”—Waebrania 11:32, 33; 12:1.
[Maelezo ya Chini]
a Kuwepo kwa “tundu la simba” huko Babiloni kwathibitishwa na ushuhuda wa maandishi ya kale yanayoonyesha kwamba watawala wa nchi za Mashariki walifuga wanyama wa pori katika bustani zao.
b Chumba cha paa kilikuwa chumba cha faragha ambacho mtu angeweza kwenda ikiwa hakutaka kusumbuliwa.
c Huenda tundu hilo la simba lilikuwa shimo la chini ya ardhi lenye mdomo upande wa juu. Huenda pia lilikuwa na milango au viunzi vya chuma ambavyo vingeweza kuinuliwa ili kuruhusu wanyama waingie.
d Neno “waliomshitaki” latafsiriwa kutokana na usemi wa Kiaramu ambao pia waweza kutafsiriwa “waliomchongea.” Hilo laonyesha nia mbovu ya adui za Danieli.
UMEFAHAMU NINI?
• Kwa nini Dario Mmedi aliamua kumtumia Danieli katika cheo kikubwa?
• Mawaziri na maliwali walipanga njama gani mbaya? Yehova alimwokoaje Danieli?
• Umejifunza nini kwa kusikiliza kielelezo cha Danieli cha uaminifu?
[Picha katika ukurasa wa 114]
[Picha katika ukurasa wa 121]
[Picha katika ukurasa wa 127]
Danieli alimtumikia Yehova “daima.” je, ndivyo unavyofanya?