Kitabu Cha Biblia Namba 27—Danieli
Mwandikaji: Danieli
Mahali Kilipoandikiwa: Babuloni
Uandikaji Ulikamilishwa: c. (karibu) 536 K.W.K.
Wakati Uliohusishwa: 618—c. (karibu) 536 K.W.K.
1. Ni historia ya aina gani iliyo katika Danieli, nayo yakazia nini?
KATIKA siku hii ambapo mataifa yote ya dunia yamesimama katika ukingo wa msiba, kitabu cha Danieli chaleta kwenye fikira ujumbe mbalimbali wa kiunabii ulio na umaana mzito. Ijapokuwa vitabu vya Biblia vya Samweli, Wafalme, na Mambo ya Nyakati vyategemea msingi wa kumbukumbu za maandishi ya mashahidi waliojionea mambo kwa macho yao wenyewe juu ya historia ya ufalme mwakilishi wa Mungu (nasaba ya Kidaudi), Danieli akaza fikira juu ya mataifa ya ulimwengu na kutoa njozi za mambo ya mbele juu ya kung’ang’ania mamlaka kwa zile falme kubwa za kuanzia wakati wa Danieli mpaka “wakati wa mwisho.” Hiyo ni historia ya ulimwengu ikiwa imeandikwa mapema. Yaongoza mpaka kwenye upeo wenye kuvuta sana fikira katika kuonyesha mambo yanayotimia “siku za mwisho.” Kama Nebukadreza, lazima mataifa yajifunze kwa magumu “ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu” na kwamba mwishowe yeye ampa huyo mmoja “aliye mfano wa mwanadamu,” yule Mesiya na Kiongozi, Kristo Yesu. (Dan. 12:4; 10:14; 4:25; 7:13, 14; 9:25; Yn. 3:13-16) Kwa kuelekeza fikira za ukaribu kwenye utimizo mbalimali wa kiunabii wa kitabu cha Danieli kilichopuliziwa na Mungu, tutathamini kwa ukamili zaidi nguvu za Yehova za kutoa unabii na mahakikishio yake juu ya kuwapa watu wake ulinzi na baraka.—2 Pet. 1:19.
2. Ni nini kinachohakikisha kwamba Danieli alikuwa mtu halisi, naye alitoa unabii wakati wa kipindi gani chenye kujaa matukio?
2 Kitabu hicho kimepewa jina kulingana na mwandikaji wacho. “Danieli” (Kiebrania: Da·ni·ye’lʹ) lamaanisha “Hakimu Wangu Ni Mungu.” Ezekieli, ambaye aliishi wakati ule ule, ahakikisha kwamba Danieli alikuwa mtu halisi, akimtaja jina pamoja na Nuhu na Ayubu. (Eze. 14:14, 20; 28:3) Danieli aonyesha tarehe ya mwanzo wa kitabu chake kuwa “mwaka wa tatu wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mfalme wa Yuda.” Hiyo ilikuwa 618 K.W.K., mwaka wa tatu wa Yehoyakimu akiwa mfalme kibaraka wa Nebukadreza.a Njozi za kiunabii za Danieli ziliendelea mpaka mwaka wa tatu wa Koreshi, karibu 536 K.W.K. (Dan. 1:1; 2:1; 10:1, 4) Lo! ni miaka yenye kujaa matukio kama nini iliyohusika katika muda wa maisha wa Danieli! Siku zake za mapema zilitumiwa chini ya ufalme wa Mungu katika Yuda. Halafu akiwa mkuu aliye kijana, akiwa pamoja na waandamani wake Wayudea walio wakuu, yeye akapelekwa Babuloni akaishi muda wote wa kuinuka na kuanguka kwa hiyo serikali kubwa ya tatu ya ulimwengu katika historia ya Biblia. Danieli aliendelea kuishi akatumikia akiwa ofisa wa serikali katika ile serikali kubwa ya nne ya ulimwengu ya Umedi-Uajemi. Lazima iwe Danieli aliishi karibu miaka mia moja.
3. Ni nini kinachothibitisha kukubaliwa na uasilia wa kitabu cha Danieli?
3 Sikuzote kitabu cha Danieli kimetiwa katika orodha ya Kiyahudi ya Maandiko yaliyopuliziwa na Mungu. Vipande vya kitabu cha Danieli vimepatikana miongoni mwa vile vya vitabu vingine vinavyokubalika katika Hati-Kunjo za Bahari ya Chumvi, baadhi yavyo vikiwa ni vya tarehe ya kuanzia nusu ya kwanza ya karne ya kwanza K.W.K. Hata hivyo, uthibitisho wa maana hata zaidi juu ya uasilia wa kitabu hicho wapatikana katika marejezo yacho katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo. Yesu ataja jina la Danieli waziwazi katika unabii wake juu ya “umalizio wa mfumo wa mambo,” ambamo yeye afanya manukuu kadhaa kutokana na kitabu hicho.—Mt. 24:3, NW; ona pia Dan. 9:27; 11:31; na 12:11—Mt. 24:15 na Mk. 13:14, NW; Dan. 12:1—Mt. 24:21; Dan. 7:13, 14—Mt. 24:30.
4, 5. Akiolojia imeondoleaje mbali madai ya wachambuzi wa Biblia kuhusiana na Danieli?
4 Ingawa wachambuzi wa Biblia wametilia shaka ukweli wa kihistoria wa kitabu cha Danieli, mavumbuzi ya kiakiolojia kwa miaka iliyopita yameyamaliza nguvu kabisa maoni wanayoshikilia. Kwa kielelezo, wachambuzi hao walifanyia mzaha wenye dharau taarifa ya Danieli kwamba Belshaza alikuwa mfalme katika Babuloni wakati ambapo Nabonido alikuwa akisemwa kuwa ndiye mtawala. (Dan. 5:1) Sasa akiolojia imethibitisha kwa kadiri isiyoweza kutiliwa shaka kwamba Belshaza alikuwa mtu halisi na kwamba alikuwa mfalme-mwenzi wa Nabonido katika miaka ya mwisho ya Milki ya Kibabuloni. Kwa kielelezo, maandishi-kabari ya kale yanayoelezwa kuwa “Simulizi la Aya la Nabonido” yathibitisha waziwazi kwamba Belshaza alikuwa na mamlaka ya kifalme kule Babuloni na yaeleza namna alivyokuwa mtawala-mwenzi wa Nabonido.b Uthibitisho mwingine wa maandishi-kabari waunga mkono maoni ya kwamba Belshaza alitimiza madaraka ya kifalme. Bamba moja, la tarehe ya mwaka wa 12 wa Nabonido, lina kiapo kilichofanywa katika jina la Nabonido, mfalme, na Belshaza, mwana wa mfalme, hivyo kuonyesha kwamba Belshaza alikuwa na daraja moja na babake.c Hilo pia ni jambo la kupendeza katika kueleza kwa nini Belshaza alijitolea kumfanya Danieli “mtu wa tatu katika ufalme” ikiwa angeweza kufasiri ule mwandiko ukutani. Nabonido angeonwa kuwa ndiye wa kwanza, Belshaza angekuwa wa pili, na Danieli angetangazwa kuwa ndiye mtawala wa tatu. (Dan. 5:16, 29) Mtafiti mmoja asema hivi: “Marejezo ya maandishi-kabari yanayogusia habari za Belshaza yametokeza nuru nyingi sana juu ya jukumu alilotimiza hivi kwamba mahali pake katika historia panafunuka wazi. Kuna maandishi mengi yanayoonyesha kwamba Belshaza alikaribia kuwa na cheo na fahari inayolingana na ya Nabonido. Imethibitishwa hakika kwamba kulikuwa na utawala wenye sehemu mbili katika muda mwingi wa umaliki wa mwisho wa Babuloni Mpya. Nabonido alitumia mamlaka iliyo kubwa zaidi akiwa katika ua wake katika Tema katika Uarabu, hali Belshaza alitenda akiwa mfalme-mwenzi katika bara la maskani ya kwao, huku Babuloni ikiwa ndicho kitovu cha maongozi. Kuna uthibitisho wa kwamba Belshaza hakuwa naibu-mfalme aliye mnyonge; yeye aliaminishwa ‘ule umaliki.’”d
5 Watu fulani wamejaribu kukanusha simulizi la Danieli juu ya lile tanuri la moto (sura 3), wakisema kwamba ni hekaya tu. Barua ya kale ya Kibabuloni yasomwa hivi kwa sehemu: “Ndivyo asemavyo Rîm-Sin Bwana wako: Kwa sababu amemtupa kivulana-mtumwa ndani ya joko, wewe mtupe mtumwa ndani ya tanuri.” Inapendeza kwamba, akiirejezea, G. R. Driver alieleza kwamba adhabu hiyo “yaonekana katika hadithi ya Wanaume Watakatifu Watatu (Dan. III 6, 15, 19-27).”e
6. Ni sehemu gani mbili zinazofanyiza kitabu cha Danieli?
6 Wayahudi walitia kitabu cha Danieli, si pamoja na Manabii, bali na Maandishi. Kwa upande mwingine, Biblia ya Kiswahili hufuata utaratibu wa orodha ya Septuagint ya Kigiriki na Vulgate ya Kilatini kwa kuweka Danieli kati ya manabii wa umaana mkubwa na mdogo. Kwa kweli kuna sehemu mbili kuhusiana na kitabu hicho. Ya kwanza kati yazo, ambayo ni sura ya 1 hadi ya 6, yafuata utaratibu wa kuorodhesha mfuatano wa matukio wakati inapoonyesha mambo yaliyopata Danieli na waandamani wake katika utumishi wa kiserikali kuanzia 617 K.W.K. hadi 538 K.W.K. (Dan. 1:1, 21) Sehemu ya pili, iliyo na sura ya 7 hadi ya 12, imeandikwa kwa kutumia mtajo wa nafsi ya kwanza, Danieli mwenyewe akiwa ndiye mwenye kuandika, na yasimulia njozi za faragha na mahoji ya kimalaika ambayo Danieli alikuwa nayo kuanzia karibu 553 K.W.K.f hadi karibu 536 K.W.K. (7:2, 28; 8:2; 9:2; 12:5, 7, 8) Sehemu hizo mbili zikiwa pamoja zafanyiza kile kitabu kimoja cha Danieli kilicho na upatani.
YALIYOMO KATIKA DANIELI
7. Ni nini kinachoongoza kwenye mwingio wa Danieli na waandamani wake katika utumishi wa serikali ya Babuloni?
7 Matayarisho kwa ajili kutumikia Nchi (1:1-21). Katika 617 K.W.K. Danieli aja Babuloni pamoja na Wayahudi watekwa. Vyombo vitakatifu kutoka hekalu la Yerusalemu vyaletwa pia, navyo vyawekwa katika nyumba-hazina ya kipagani. Danieli na waandamani wake watatu Waebrania wamo miongoni mwa vijana Wayudea wa kifalme wanaochaguliwa kwa ajili ya mtaala (mafunzo) wa miaka mitatu wa mazoezi katika jumba la mfalme. Akiwa ameazimia moyoni mwake asijichafue kwa vyakula vitamu-vitamu vya kipagani na divai ya mfalme, Danieli apendekeza mtihani wa siku kumi wa kula mboga. Matokeo ya mtihani huo ni yenye kibali kwa Danieli na waandamani wake, na Mungu awapa maarifa na hekima. Nebukadreza awaweka rasmi hao wanne wasimame mbele yake wakiwa washauri. Mstari wa mwisho sura ya 1, ambao huenda ukawa uliongezwa muda mrefu baada ya kile kisehemu kinachoutangulia kuwa kimeandikwa, waonyesha kwamba Danieli alikuwa angali katika utumishi wa kifalme kwa miaka ipatayo 80 baada ya yeye kwenda uhamishoni, hiyo ingekuwa ni karibu 538 K.W.K.
8. Ni ndoto na fasiri gani ambayo Mungu afunulia Danieli, na Nebukadreza aonyeshaje uthamini wake?
8 Ndoto ya taswira (mchongo) wa kuogopesha sana (2:1-49). Katika mwaka wa pili wa umaliki wake (yawezekana kuanzia tarehe ya uharibifu wa Yerusalemu katika 607 K.W.K.), Nebukadreza afadhaishwa sana na ndoto fulani. Makuhani wake wenye kuzoea mizungu washindwa kufunua ndoto hiyo na fasiri yake. Awatolea zawadi kubwa-kubwa, lakini wao wakataa kwa uthabiti kwamba hakuna mmoja ila miungu anayeweza kuonyesha mfalme jambo analouliza. Mfalme akasirika sana na kuagiza kwamba wanaume wale wenye hekima wauawe. Kwa kuwa wale Waebrania watiwa ndani ya amri ya uamuzi huo, Danieli aomba wakati ili afunue ndoto ile. Danieli na waandamani wake wasali kwa Yehova ili wapate mwongozo. Yehova afunulia Danieli ndoto ile na maana yayo, na ndipo yeye aenda mbele ya mfalme na kusema: “Yuko Mungu mbinguni afunuaye siri, naye amemjulisha mfalme Nebukadreza mambo yatakayokuwa siku za mwisho.” (2:28) Danieli aeleza ndoto ile ilivyokuwa. Ni kuhusu taswira kubwa sana. Kichwa cha taswira (sanamu) hiyo ni cha dhahabu, kifua chayo na mikono ni vya fedha, tumbo na mapaja ni ya shaba, na miguu ni ya chuma, huku nyayo zikiwa nusu chuma na nusu udongo. Jiwe fulani laipiga taswira na kuiponda nalo lawa mlima mkubwa unaojaa dunia nzima. Hiyo yamaanisha nini? Danieli ajulisha kwamba mfalme wa Babuloni ndiye kichwa cha dhahabu. Baada ya ufalme wake kutafuata ufalme wa pili, wa tatu, na wa nne. Mwishowe, “Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele . . . ; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele.” (2:44) Akiwa na shukrani na uthamini, mfalme ahimidi Mungu wa Danieli kuwa “Mungu wa miungu” na kufanya Danieli “kuwa mkubwa juu ya uliwali wote wa Babeli, na kuwa liwali mkuu juu ya wote wenye hekima wa Babeli.” Waandamani watatu wa Danieli wafanywa wasimamizi katika ufalme ule.—2:47, 48.
9. Ni mambo gani yanayotokea kutokana na msimamo imara wa wale Waebrania watatu wa kukataa ya ibada ya taswira?
9 Waebrania watatu waokoka katika lile tanuri la moto (3:1-30). Nebukadreza asimamisha taswira kubwa ya dhahabu, yenye kimo cha dhiraa 60 (meta 27), na aagiza watawala wa milki ile wakusanyike kwa ajili ya kuwekwa wakfu kwa taswira hiyo. Muziki maalumu unaposikiwa, wote wapaswa kuanguka chini na kuabudu taswira hiyo. Wowote wasiofanya hivyo watatupwa ndani ya lile tanuri lenye kuwaka moto mkali. Yaripotiwa kwamba waandamani watatu wa Danieli, Shadraki, Meshaki, na Abednego, hawakutii jambo hilo. Wao waletwa mbele ya mfalme aliye na hasira kali, ambapo washuhudia hivi kwa ujasiri: “Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa . . . Sisi hatukubali . . . kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.” (3:17, 18) Kwa kujawa na ghadhabu kali, mfalme aagiza tanuri litiwe moto mara saba kuliko ilivyo desturi na kwamba wale Waebrania watatu wafungwe na kutupwa ndani. Katika kufanya hivyo, hao ambao wangelikuwa watekelezaji-hukumu wauawa na ule mwali wenye moto. Nebukadreza aingiwa na hofu kuu. Ni nini hiki anachokiona katika tanuri lile? Wanaume wanne watembea-tembea bila madhara katikati ya moto ule, na “sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu.” (3:25) Mfalme awaita wale Waebrania watatu wakanyage nje ya moto ule. Wao watoka nje, bila kuungua unywele, bila hata harufu ya moto wenyewe juu yao! Kama tokeo la msimamo wao wa kishujaa kwa ajili ya ibada ya kweli, Nebukadreza atangaza kuhusu uhuru wa ibada kwa ajili ya Wayahudi katika sehemu zote za milki.
10. Nebukadreza alipata ndoto gani ya kuogopesha inayohusisha “nyakati saba,” na je! ilitimizwa juu yake?
10 Ndoto ya zile “nyakati saba” (4:1-37). Ndoto hiyo imo katika kumbukumbu ya maandishi ikiwa imeonyeshwa kuwa ni maandishi yaliyonakiliwa na Danieli kutokana na hati moja ya mambo ya kiserikali ya Babuloni. Iliandikwa na Nebukadreza aliyenyenyekezwa. Kwanza Nebukadreza akiri uweza na ufalme wa Mungu Aliye Juu Zaidi. Halafu asimulia ndoto yenye kutia hofu kuu na jinsi ilivyotimizwa juu yake mwenyewe. Yeye aliona mti uliofika mbinguni na ukatoa makao na chakula kwa ajili ya mnofu wote. Mlinzi akapaaza sauti hivi: ‘Ukateni mti. Kifungeni kisiki chao pingu ya chuma na shaba. Nyakati saba zipite juu yacho, kusudi ijulikane kuwa Aliye juu anatawala katika ufalme wa wanadamu na humtawaza juu yake aliye mnyonge.’ (4:14-17) Danieli alifasiri ndoto ile, akijulisha kwamba mti ule uliwakilisha Nebukadreza. Utimizo wa ndoto hiyo ya kiunabii ulifuata baada ya muda mfupi. Mfalme alipatwa na usumbufu wa kichaa alipokuwa akionyesha kiburi kikuu; naye akaishi kama hayawani kondeni kwa miaka saba. Baada ya hapo, utimamu wake wa akili ulirudishwa, naye akakiri ukuu wa Yehova wazidi wa wengine wote.
11. Ni wakati wa anasa gani isiyo ya adili ambapo Belshaza aona ule mwandiko wa mkono unaomaanisha msiba, Danieli aufasirije, nao watimizwaje?
11 Karamu ya Belshaza: mwandiko wa mkono wafasiriwa (5:1-31). Sasa ni ule usiku wenye msiba wa Oktoba 5, 539 K.W.K. Mfalme Belshaza, mwana wa Nabonido, akiwa mfalme-mwenzi wa Babuloni, afanya karamu kubwa kwa ajili ya waheshimiwa wake elfu moja. Mfalme huyo, akiwa chini ya uvutano wa divai, aitisha vile vyombo vitakatifu vya dhahabu na fedha kutoka kwenye hekalu la Yehova, na Belshaza na wageni wake wavinywea, katika anasa yao isiyo ya adili, huku wakisifu miungu yao ya kipagani. Mara hiyo mkono watokea na kuandika ukutani ujumbe uliofichika maana. Mfalme atetemeka kwa woga. Wanaume wake wenye hekima washindwa kufasiri mwandiko huo. Mwishowe Danieli aletwa ndani. Mfalme afanya toleo la kumfanya awe wa tatu katika ufalme ikiwa aweza kusoma na kufasiri mwandiko ule, lakini Danieli amwambia ajiwekee mwenyewe zawadi zake. Ndipo aendelea kujulisha mwandiko ule na maana yao: “MENE, MENE, TEKELI, NA PERESI. . . . Mungu ameuhesabu ufalme wako na kuukomesha. . . . Umepimwa katika mizani nawe umeonekana kuwa umepunguka. . . . Ufalme wako umegawanyika, nao wamepewa Wamedi na Waajemi.” (5:25-28) Usiku uo huo Belshaza auawa, na Dario Mmedi apokea ufalme ule.
12. Njama aliyotungiwa Danieli yabatilishwaje, ndiposa Dario atoa amri gani?
12 Danieli katika tundu la simba (6:1-28). Maofisa wakuu katika serikali ya Dario wamtungia Danieli madhara kwa kumfanya mfalme apitishe sheria inayoweka katazo la siku 30 juu ya kuomba mungu yeyote au mwanadamu isipokuwa mfalme peke yake. Mtu yeyote asiyeitii atatupwa kwenye simba. Danieli akataa kutii sheria hiyo yenye kuathiri ibada yake na kugeukia Yehova katika sala. Yeye atupwa ndani ya lile tundu la akina simba. Kwa mwujiza, malaika wa Yehova afunga vinywa vya simba hao, na asubuhi yake Mfalme Dario afurahi sana kupata Danieli akiwa bila madhara. Wale maadui sasa watolewa waliwe na simba hao, na mfalme aamrisha kwamba Mungu wa Danieli ahofiwe, kwa kuwa “yeye ndiye Mungu aliye hai.” (6:26) Danieli apata ufanisi katika utumishi wa serikali muda wote huo mpaka kuingia utawala wa Koreshi.
13. Katika ndoto moja ya faragha, ni njozi gani ambayo Danieli apata kuhusu hayawani-mwitu wanne na ule utawala wa Ufalme?
13 Njozi za wale hayawani (7:1–8:27). Twarudi kwenye “mwaka wa kwanza wa Belshaza,” ambaye utawala wake kwa wazi ulianza katika 553 K.W.K. Danieli apokea ndoto ya faragha, ambayo aiandika katika Kiaramu.g Yeye aona hayawani wanne wakubwa wa kutisha wakitokea kila mmoja kwa zamu. Wa nne ana nguvu isiyo ya kawaida, na pembe ndogo yaja juu miongoni mwa pembe nyingine zake ‘ikinena maneno makuu.’ (7:8) Mkale wa Siku atokea na kuchukua kiti chake. “Maelfu elfu” wamhudumia. “Mmoja aliye mfano wa mwanadamu” aja mbele yake ‘na apewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie.’ (7:10, 13, 14) Ndipo Danieli apokea fasiri ya njozi ya wale hayawani wanne. Wao wawakilisha wafalme, au falme nne. Pembe ndogo yainuka kutoka miongoni mwa zile pembe kumi zilizo juu ya yule hayawani wa nne. Hiyo yawa yenye uweza na kufanya vita juu ya watakatifu. Hata hivyo, Mahakama ya kimbingu yachukua hatua ‘kuwapa watakatifu wa Aliye juu ufalme, na mamlaka, na ukuu wa ufalme, chini ya mbingu zote.’—7:27.
14. Ni njozi gani ambayo Danieli apata yenye kuhusu beberu na kondoo ndume mwenye pembe mbili? Gabrieli aielezaje njozi hiyo?
14 Miaka miwili baadaye, muda mrefu kabla ya anguko la Babuloni, Danieli aona njozi nyingine, ambayo yeye aandika katika Kiebrania. Beberu aliye na pembe yenye kutokeza wazi kati ya macho yake ang’ang’ana na kumshinda kondoo ndume mwenye kiburi aliye na pembe mbili. Ile pembe kuu ya beberu yavunjwa, halafu zatokea pembe nne zilizo ndogo kuliko hiyo. Kutoka kwa moja ya hizo yaja pembe ndogo inayokuwa kuu, hata kufikia kukaidi jeshi la mbingu. Kipindi cha siku 2,300 chatabiriwa mpaka wakati ambapo mahali patakatifu pataletwa ndani ya “hali inayofaa.” (8:14, NW) Gabrieli aeleza Danieli njozi ile. Yule kondoo ndume asimamia wafalme wa Umedi na Uajemi. Yule beberu ni mfalme wa Ugiriki, ambaye ufalme wake utavunjwa uwe sehemu nne. Baadaye, mfalme mwenye sura kali atasimama “kushindana naye aliye Mkuu wa wakuu.” Kwa kuwa njozi ile “ni ya wakati ujao baada ya siku nyingi,” lazima Danieli aiweke ikiwa siri kwa wakati uliopo.—8:25, 26.
15. Ni nini kinachosababisha Danieli asali kwa Yehova, na sasa Gabrieli ajulisha nini kuhusu “majuma sabini”?
15 Mesiya yule Kiongozi atabiriwa (9:1-27). “Mwaka wa kwanza wa Dario . . . wa Wamedi” wampata Danieli akichunguza unabii wa Yeremia. Kwa kujua kwamba ule ukiwa wa Yerusalemu uliotabiriwa kuwa wa miaka 70 wakaribia kumalizika, Danieli asali kwa Yehova katika kuungama dhambi zake mwenyewe na zile za Israeli. (Dan. 9:1-4; Yer. 29:10) Gabrieli atokea, kujulisha kwamba kutakuwa na “majuma sabini . . . ili kukomesha makosa, na kuishiliza dhambi, na kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu.” Mesiya Kiongozi atakuja mwishoni mwa majuma 69, na baada ya hapo akatiliwe mbali. Agano litawekwa likiwa bado katika utendaji kwa ajili ya wengi mpaka mwisho wa lile juma la 70, na, mwishowe, kutakuwa na ukiwa na kuuliwa mbali.—Dan. 9:24-27.
16. Ni chini ya hali gani malaika amtokea tena Danieli?
16 Kaskazini yakabiliana na kusini, Mikaeli asimama (10:1–12:13). Ni “mwaka wa tatu wa Koreshi,” na kwa sababu hiyo ni karibu 536 K.W.K., si muda mrefu baada ya kurudi kwa Wayahudi Yerusalemu. Baada ya kufunga kwa majuma matatu, Danieli yuko kwenye ukingo wa mto Hidekeli. (Dan. 10:1, 4; Mwa. 2:14) Malaika amtokea na kumweleza kwamba ‘mkuu wa Uajemi’ alimpinga asimjie Danieli lakini “Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele,” alimsaidia. Sasa yeye asimulia kwa Danieli njozi moja iliyo kwa ajili ya “siku za mwisho.”—Dan. 10:13, 14.
17. Ni historia gani ya kiunabii juu ya mfalme wa kaskazini na mfalme wa kusini ambayo sasa Danieli aandika?
17 Wakati inapofunguka, njozi hii yenye kunasa fikira yanena juu ya nasaba ya Kiajemi na mng’ang’ano ambao itakuja kuwa nao pamoja na Ugiriki. Mfalme mwenye uweza atasimama akiwa na eneo lenye kupanuka sana la utawala, lakini ufalme wake utavunjwa uwe sehemu nne. Mwishowe kutakuwa na mistari miwili mirefu ya wafalme, mfalme wa kusini akiwa katika upinzani na mfalme wa kaskazini. Mng’ang’anio huo wa mamlaka utakuwa wa kuvurutana huku na huko. Wafalme hao wenye ubaya usiorekebika wataendelea kunena uwongo kwenye meza moja. Kwenye “wakati ulioamriwa,” ile vita itawaka tena. Dharau itafanywa juu ya utakato wa patakatifu pa Mungu, na “chukizo la uharibifu” litawekwa mahali hapo. (11:29-31) Mfalme wa kaskazini atamnenea Mungu wa miungu mambo ya ajabu na kumpa utukufu mungu wa ngome. Katika “wakati wa mwisho” ambapo mfalme wa kusini ajitia katika msukumano pamoja na mfalme wa kaskazini, mfalme wa kaskazini atafurika aingie ndani ya mabara mengi, akiingia pia “katika hiyo nchi ya uzuri.” Kwa kusumbuliwa na ripoti zitokazo mashariki na kaskazini, yeye ataenda kwa hasira kali na kupiga “hema zake za kifalme kati ya bahari na mlima mtakatifu wa uzuri.” Kwa hiyo, “yeye atalazimika kuienda njia yote hadi mwisho wake, na hakutakuwako msaidiaji yeyote kwake.” (NW)—11:40, 41, 45.
18. Ni mambo gani yanayotukia wakati wa kusimama kwa Mikaeli ‘upande wa wana wa watu wa Mungu’?
18 Njozi hiyo kuu yaendelea kusema: Mikaeli aonekana amesimama ‘upande wa wana wa watu wa Mungu.’ Kutakuwa na “wakati wa taabu” usiopata kuwa na kifani katika historia ya kibinadamu, lakini wale ambao watapatikana wameandikwa katika kitabu kile wataponyoka. Wengi wataamka kutoka mavumbi waje kwenye uhai wa milele, “na walio na hekima watang’aa kama mwangaza wa anga.” Wao wataleta wengi kwenye uadilifu. Danieli atakitia muhuri kitabu kile “hata wakati wa mwisho.” “Je! itakuwa muda wa miaka mingapi hata mwisho wa mambo haya ya ajabu?” Malaika ataja vipindi vya nyakati tatu na nusu, siku 1,290, na siku 1,335 na kusema kwamba “walio na hekima ndio watakaoelewa.” Wenye furaha ni hao! Mwishowe, malaika atolea Danieli ahadi yenye kumpa uhakikishio kwamba yeye atapumzika na kisha asimame kwa ajili ya kura yake kwenye “mwisho wa siku hizo.”—12:1, 3, 4, 6, 10, 13.
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
19. Ni vielelezo gani vizuri vya ukamilifu na kutegemea Yehova kwa sala vinavyopatikana katika kitabu cha Danieli?
19 Wote ambao wamepiga moyo konde kudumisha ukamilifu katika ulimwengu usio na urafiki kwao wangefaa kufikiria kielelezo kizuri cha Danieli na waandamani wake watatu. Hata tisho lenyewe liwe kali jinsi gani, wao waliendelea kuishi kwa kufuata kanuni za kimungu. Wakati maisha zao zilipokuwa hatarini, Danieli alitenda “kwa busara na hadhari” na akiwa na staha kwa mamlaka ya mfalme iliyo kuu zaidi. (2:14-16) Suala lile lilipofanywa kuwa lazima, Waebrania wale watatu waliona ni afadhali kuwa kwenye tanuri la moto uwakao badala ya kufanya kitendo kimoja cha ibada ya sanamu, na Danieli aliona ni afadhali kuwa kwenye pango la simba badala ya kupoteza pendeleo lake la sala kwa Yehova. Katika kila kisa Yehova alitoa ulinzi. (3:4-6, 16-18, 27; 6:10, 11, 23) Danieli mwenyewe atoa kielelezo kizuri sana cha kutegemea Yehova Mungu kwa sala.—2:19-23; 9:3-23; 10:12.
20. Ni njozi gani nne zilizoandikwa kuhusu zile serikali kubwa za ulimwengu, na kwa nini kufikiria njozi hizo leo kwaimarisha imani?
20 Kupitia njozi za Danieli kwasisimua na kuimarisha imani. Kwanza, fikiria zile njozi nne kuhusu serikali kubwa za ulimwengu: (1) Kuna ile njozi juu ya taswira yenye kutia hofu, ambayo kichwa chayo cha dhahabu chawakilisha nasaba ya wafalme wa Kibabuloni kuanzia na Nebukadreza, ambayo baada yayo zainuka falme nyingine tatu, kama zilivyofananishwa na sehemu nyingine za mfano huo. Hizo ndizo falme zinazopondwa na lile “jiwe,” nalo lawa “ufalme ambao hautaangamizwa milele,” Ufalme wa Mungu. (2:31-45) (2) Ndipo zafuata zile njozi za faragha za Danieli, ya kwanza ikiwa ya wale hayawani wanne, wakiwakilisha “wafalme wanne.” Hao wako kama simba, dubu, chui mwenye vichwa vinne, na hayawani mmoja mwenye meno makubwa ya chuma, pembe kumi, na baadaye pembe ndogo moja. (7:1-8, 17-28) (3) Halafu, kuna ile njozi juu ya kondoo ndume (Umedi-Uajemi), yule beberu (Ugiriki), na ile pembe ndogo. (8:1-27) (4) Mwishowe, tuna ile njozi juu ya mfalme wa kusini na mfalme wa kaskazini. Danieli 11:5-19 yasimulia kwa usahihi ushindani uliokuwa kati ya vichipukizi vya Misri na vya Seleucus ambavyo vilitokana na Milki ya Kigiriki ya Aleksanda kufuatia kifo cha Aleksanda katika 323 K.W.K. Kuanzia mstari 20 unabii waendelea kufuatisha mwendo wa mataifa yaliyofuatana ya kusini na kaskazini. Mrejezo wa Yesu kuhusu “chukizo la uharibifu” (11:31), katika unabii wake juu ya ishara ya kuwapo kwake, waonyesha kwamba huku kung’ang’ania mamlaka kwa wale wafalme wawili kwaendelea moja kwa moja mpaka “umalizio wa mfumo wa mambo.” (Mt. 24:3, NW) Uhakikisho ambao unabii huo watoa wafariji kama nini kwamba katika “wakati wa taabu, [ambao] mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo,” Mikaeli mwenyewe atasimama ili kuondoa mataifa yasiyomcha Mungu na kuletea ainabinadamu watiifu amani!—Dan. 11:20–12:1.
21. Unabii wa Danieli wa “majuma sabini” ulipataje utimizo wa kustaajabisha?
21 Halafu, kuna unabii wa Danieli juu ya “majuma sabini.” Baada ya majuma 69 “masihi aliye mkuu” angetokea. Kwa kustaajabisha, miaka 483 (69 kuzidisha na miaka 7) baada ya “kuwekwa amri” ya kujenga upya Yerusalemu, kama ilivyoruhusiwa na Artashasta katika mwaka wake wa 20 na kutekelezwa na Nehemia katika Yerusalemu, Yesu wa Nazareti alibatizwa katika Mto Yordani na kupakwa mafuta kwa roho takatifu, akawa Kristo, au Mesiya (yaani, Mpakwa-Mafuta).h Hiyo ilikuwa katika mwaka 29 C.E. Baada ya hapo, kama vile Danieli pia alikuwa ametabiri, kulikuja ‘uangamivu’ wakati Yerusalemu lilipoachwa ukiwa katika 70 C.E.—Dan. 9:24-27; Luka 3:21-23; 21:20.
22. Ni somo gani ambalo twapata kutokana na kunyenyekezwa kwa Nebukadreza?
22 Katika ndoto ya Nebukadreza kuhusu ule mti uliokatwa ukaangushwa, kama vile ilivyoandikwa na Danieli katika sura ya 4, yasimuliwa kwamba mfalme, ambaye alijisifia matimizo yake mwenyewe na akawa ana uhakika katika uweza wake mwenyewe, alinyenyekezwa na Yehova Mungu. Yeye alifanywa aishi kama hayawani wa kondeni mpaka alipotambua “ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, awaye yote.” (Dan. 4:32) Je! sisi leo tutakuwa kama Nebukadreza, tukijisifia matimizo yetu na kuweka uhakika wetu katika uweza wa wanadamu, mpaka Mungu alazimike kufikiliza adhabu kwetu, au tutakiri kwa hekima kwamba Yeye ndiye Mtawala katika ufalme wa ainabinadamu, na tuweke uhakika wetu katika Ufalme wake?
23. (a) Tumaini la Ufalme lakaziwaje katika Danieli yote? (b) Kitabu hiki cha unabii chapasa kututia moyo tufanye nini?
23 Tumaini la Ufalme lakaziwa katika sehemu zote za kitabu cha Danieli kwa njia yenye kutia imani! Yehova Mungu aonyeshwa kuwa ndiye Mwenye Enzi Aliye Mkuu Zaidi anayesimamisha Ufalme ambao hautaangamizwa kamwe na ambao utaponda falme nyingine zote. (2:19-23, 44; 4:25) Hata wafalme wapagani Nebukadreza na Dario walishurutishwa kukiri kwamba Yehova ana ukuu uzidio wa wengine wote. (3:28, 29; 4:2, 3, 37; 6:25-27) Yehova akwezwa na kutukuzwa kuwa Mkale wa Siku anayehukumu lile suala la Ufalme na kumpa “mmoja aliye mfano wa mwanadamu” ile “mamlaka, na utukufu, na ufalme [wa milele], ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie.” “Watakatifu wa Aliye juu” ndio washiriki pamoja na Kristo Yesu, “Mwana wa Adamu,” katika ule Ufalme. (Dan. 7:13, 14, 18, 22; Mt. 24:30; Ufu. 14:14) Yeye ndiye Mikaeli, mwana-mfalme aliye mkuu, ambaye anatumia mamlaka yake ya Ufalme kuponda na kukomesha falme zote za ulimwengu huu mwovu. Kuelewa unabii huo mbalimbali na njozi hizo kwapasa kuwatie moyo wapenda-uadilifu wajitie bidii na kwenda mbio huko na huko katika kurasa za Neno la Mungu ili kupata ‘mambo ya ajabu’ ya makusudi ya Ufalme wa Mungu ambayo twafunuliwa kupitia kitabu cha Danieli kilichopuliziwa na Mungu na chenye mafaa.—Dan. 12:2, 3, 6.
[Maelezo ya Chini]
a Insight on the Scriptures, Buku 1, ukurasa 1269.
b Insight on the Scriptures, Buku 1, ukurasa 283.
c Archaeology and the Bible, 1949, George A. Barton, ukurasa 483.
d The Yale Oriental Series · Researchers, Buku 15, 1929.
e Archiv für Orientforschung, Buku 18, 1957-58, ukurasa 129.
f Kwa wazi Belshaza alianza kutawala akiwa mfalme-mwenzi kuanzia mwaka wa tatu wa Nabonido. Kwa kuwa yaaminiwa Nabonido alianza utawala wake katika 556 K.W.K., mwaka wa tatu wa utawala wake na “mwaka wa kwanza wa Belshaza” kwa wazi ulikuwa 553 K.W.K.—Danieli 7:1; ona Insight on the Scriptures, Buku 1, ukurasa 283; Buku 2, ukurasa 457.
g Danieli 2:4b–7:28 iliandikwa katika Kiaramu, hali sehemu nyingineyo ya kitabu hicho iliandikwa katika Kiebrania.
h Nehemia 2:1-8; ona pia Insight on the Scriptures, Buku 2, kurasa 899-901.