Kitabu Cha Biblia Namba 16—Nehemia
Mwandikaji: Nehemia
Mahali Kilipoandikiwa: Yerusalemu
Uandikaji Ulikamilishwa: Baada ya 443 K.W.K.
Wakati Uliohusishwa: 456-baada ya 443 K.W.K.
1. Nehemia alikuwa na cheo gani cha kutumainika, na jambo kuu akilini mwake lilikuwa nini?
NEHEMIA, ambaye jina lake lamaanisha “Yah Hufariji,” alikuwa mtumishi Myahudi wa Artashasta (Longimano) mfalme Mwajemi. Alikuwa mnyweshaji wa mfalme. Hicho kilikuwa cheo cha kutumainika na chenye heshima kubwa, cha kutamanika, kwa maana kiliwezesha kufikia mfalme nyakati ambazo alikuwa na akili yenye furaha na tayari kupeana vibali. Hata hivyo, Nehemia alikuwa mmoja wa wale wahamishwa waaminifu waliopendelea Yerusalemu zaidi ya ‘kisababishi chochote cha kuonea shangwe’ ya kibinafsi. (Zab. 137:5, 6, NW) Cheo wala mali ya kimwili si ndivyo vilivyokuwa vya maana zaidi katika mawazo ya Nehemia bali, badala yake, kurejeshwa kwa ibada ya Yehova.
2. Ni hali gani yenye kusikitisha iliyomhuzunisha Nehemia, lakini ni wakati gani uliowekwa uliokuwa ukikaribia?
2 Katika 456 K.W.K. wale ‘waliosalia wa uhamisho,’ baki la Kiyahudi lililokuwa limerudi Yerusalemu, hawakuwa wakifanikiwa. Walikuwa katika hali ya kuombolezea. (Neh. 1:3) Ukuta wa mji ulikuwa mabomoko, na watu walikuwa suto katika macho ya wapinzani wao waliokuwako daima. Nehemia alihuzunika sana. Hata hivyo, ulikuwa ni wakati uliowekwa wa Yehova kwamba jambo fulani lifanywe juu ya ukuta wa Yerusalemu. Kuwe maadui au kusiwe, Yerusalemu pamoja na ukuta walo wenye kulinda lazima vijengwe kuwa alama ya wakati kuhusiana na unabii ambao Yehova alikuwa amempa Danieli kuhusiana na kuja kwa Mesiya. (Dan. 9:24-27) Kwa hiyo, Yehova alielekeza matukio, akitumia Nehemia mwaminifu na mwenye bidii ili kutimiza mapenzi ya kimungu.
3. (a) Ni nini kinachothibitisha Nehemia kuwa mwandikaji, na kitabu hicho kilikujaje kuitwa Nehemia? (b) Ni tofauti ya muda gani inayotenganisha kitabu hiki na kitabu cha Ezra, na kitabu cha Nehemia chahusisha miaka gani?
3 Bila shaka Nehemia ndiye mwandikaji wa kitabu chenye jina lake. Taarifa ya kufungua, “Habari za Nehemia, mwana wa Hakalia,” na matumizi ya usemi wa kujitaja katika kuandika vyathibitisha hilo waziwazi. (Neh. 1:1) Hapo awali vitabu vya Ezra na Nehemia vilikuwa kitabu kimoja, kilichoitwa Ezra. Baadaye, Wayahudi walikigawanya kitabu hicho kuwa Ezra wa Kwanza na wa Pili, na bado baadaye Ezra wa Pili kikaja kujulikana kuwa Nehemia. Katikati ya matukio ya kumalizia ya kitabu cha Ezra na matukio ya kufungua ya kitabu cha Nehemia kuna muda wa miaka 12, ambao ndipo historia yao yahusu kile kipindi tokea mwisho wa 456 K.W.K. hadi baada ya 443 K.W.K.—1:1; 5:14; 13:6.
4. Kitabu cha Nehemia chapatanaje na Maandiko mengine yote?
4 Kitabu cha Nehemia chapatana na Andiko jingine lote lililopuliziwa na Mungu, ambalo kwa kufaa hicho ni sehemu yalo. Kina mitajo mingi ya Sheria, kikirejeza kwenye mambo kama vile mapatano ya ndoa pamoja na wageni (Kum. 7:3; Neh. 10:30), mikopo (Law. 25:35-38; Kum. 15:7-11; Neh. 5:2-11), na Sikukuu ya Vibanda (Kum. 31:10-13; Neh. 8:14-18). Zaidi ya hayo, kitabu hicho chatia alama ya mwanzo wa utimizo wa unabii wa Danieli kwamba Yerusalemu lingejengwa upya lakini kukawa na upinzani, “katika nyakati za taabu.”—Dan. 9:25.
5. (a) Ni ushuhuda kutoka vyanzo gani unaoonyesha mwaka wa kutawazwa kwa Artashasta kuwa 475 K.W.K.? (b) Ni tarehe gani inayotia alama mwaka wake wa 20? (c) Vitabu vya Nehemia na Luka vyahusianaje katika utimizo wa unabii wa Danieli juu ya Mesiya?
5 Vipi juu ya tarehe 455 K.W.K. ya safari ya Nehemia ya kwenda Yerusalemu ili kujenga upya ukuta wa mji huo? Ushuhuda wenye kutegemeka wa kihistoria kutoka vyanzo vya Kigiriki, Kiajemi, na Kibabuloni huelekeza kwenye 475 K.W.K. kuwa mwaka wa kutawazwa kwa Artashasta na 474 K.W.K. kuwa mwaka wake wa kwanza wa kukalia kiti cha enzi.a Hilo lingefanya mwaka wake wa ishirini kuwa 455 K.W.K. Nehemia 2:1-8 huonyesha ilikuwa katika masika ya mwaka huo, katika mwezi wa Kiyahudi wa Nisani, kwamba Nehemia, mnyweshaji wa mfalme, alipopokea ruhusa ya mfalme ya kurejesha na kujenga upya Yerusalemu, na ukuta walo, na malango yalo. Unabii wa Danieli ulitaarifu kwamba majuma 69 ya miaka, au miaka 483, ingeanza “tangu kuwekwa amri ya kutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu hata zamani zake masihi aliye mkuu”—unabii ambao ulitimizwa kwa njia yenye kutokeza wakati wa kupakwa mafuta kwa Yesu katika 29 W.K., tarehe ambayo yaweza kupatanishwa na historia ya kilimwengu na ya Kibiblia pia.b (Dan. 9:24-27; Luka 3:1-3, 23) Kweli kweli, vitabu vya Nehemia na Luka vyahusiana kwa njia yenye kutokeza na unabii wa Danieli katika kuonyesha Yehova Mungu kuwa Mtungaji na Mtimizaji wa unabii wa kweli! Kweli kweli Nehemia ni sehemu ya Maandiko yaliyopuliziwa na Mungu.
YALIYOMO KATIKA NEHEMIA
6. (a) Ni ripoti gani inayosababisha Nehemia asali kwa Yehova, na ni ombi gani analokubali mfalme? (b) Wayahudi waitikiaje mpango wa Nehemia?
6 Nehemia atumwa Yerusalemu (1:1–2:20). Nehemia ahangaishwa sana na ripoti fulani kutoka kwa Hanani, ambaye amerejea Shushani kutoka Yerusalemu akiwa na habari za hali mbaya sana ya Wayahudi kule na hali ya kubomoka kwa ukuta na malango. Afunga na kusali kwa Yehova kuwa “Mungu wa mbinguni, Mungu mkuu, mwenye kuogofya, mwenye kutimiza agano lake na rehema zake kwa hao wampendao na kuzishika amri zake.” (1:5) Aungama dhambi za Israeli na kuomba Yehova akumbuke watu Wake kwa sababu ya jina Lake, sawa na alivyomwahidi Musa. (Kum. 30:1-10) Mfalme amwulizapo Nehemia juu ya sababu ya sura yake ya huzuni, Nehemia amwambia juu ya hali ya Yerusalemu na aomba ruhusa arudi na kujenga upya jiji na ukuta walo. Ombi lake lakubaliwa, na bila kukawia afunga safari kwenda Yerusalemu. Kufuatia uchunguzi wa wakati wa usiku wa ukuta wa jiji hilo ili ajue kazi iliyo mbele, afunua mpango wake kwa Wayahudi, akikazia mkono wa Mungu katika jambo hilo. Ndiposa wasema: “Haya! na tuondoke tukajenge.” (Neh. 2:18) Wasamaria majirani na wengine wasikiapo kwamba kazi imeanza, waanza kudhihaki na kufanya mzaha.
7. Kazi yaendeleaje, na ni hali gani inayotaka kupangwa upya kitengenezo?
7 Ukuta wajengwa upya (3:1–6:19). Kazi kwenye ukuta yaanza mnamo siku ya tatu ya mwezi wa tano, na makuhani, wakuu, na watu wakishirikiana katika kazi hiyo. Malango na kuta za jiji hilo zatengenezwa kulikoharibika kwa kasi. Sanbalati Mhoroni adhihaki: “Wayahudi hawa wanyonge wanafanyaje? . . . watamaliza katika siku moja?” Tobia Mwamoni, aongezea dharau yake hivi: “Hata hiki wanachokijenga, angepanda mbweha, angeubomoa ukuta wao wa mawe.” (4:2, 3) Ukuta ufikiapo nusu ya kimo chao, muungano wa wapinzani wawa na kasirani na wafanya njama ya kukwea na kupigana na Yerusalemu. Lakini Nehemia asihi Wayahudi wakumbuke ‘Yehova, aliye mkuu mwenye kuogofya’ na kupigania familia zao na nyumba zao. (4:14) Kazi hiyo yapangwa kitengenezo upya ili kukabiliana na hali hiyo ya wasiwasi; wengine wasimama wakilinda kwa mikuki hali wengine wafanya kazi panga zao zikiwa viunoni.
8. Nehemia ashughulikiaje matatizo miongoni mwa Wayahudi wenyewe?
8 Hata hivyo, kuna matatizo pia miongoni mwa Wayahudi wenyewe. Wengine wao wanatoza riba waabudu wenzao wa Yehova, kinyume cha sheria yake. (Kut. 22:25) Nehemia asahihisha hali hiyo, akishauri juu ya kutopenda mali, na watu wakubali kwa nia. Nehemia mwenyewe, wakati wa miaka yake yote 12 ya uliwali, tangu 455 K.W.K. hadi 443 K.W.K., hadai kamwe mkate anaostahili liwali kwa sababu ya utumishi mzito ulio juu ya watu.
9. (a) Nehemia akabilianaje na mbinu za hila za kukomesha ujenzi? (b) Ukuta wakamilishwa baada ya wakati gani?
9 Sasa maadui wajaribu mbinu za hila zaidi ili kukomesha ujenzi. Wamwalika Nehemia ateremke kwa ajili ya mkutano, lakini yeye ajibu kwamba hana wakati wa kuacha kazi kubwa anayofanya. Sanbalati sasa ashtaki Nehemia juu ya uasi na mpango wa kujifanya mwenyewe mfalme katika Yuda, na kisiri akodi Myahudi mmoja aogofye Nehemia ili ajifiche kimakosa katika hekalu. Nehemia akataa kutishwa, na kwa utulivu na kwa utiifu aendelea na kazi yake aliyogawiwa na Mungu. Ukuta wakamilishwa “katika muda wa siku hamsini na mbili.”—Neh. 6:15.
10. (a) Watu waishi wapi, na ni uandikishaji gani unaofanywa? (b) Sasa ni kusanyiko gani linaloitishwa, na programu ya siku ya kwanza ni nini?
10 Kuwaagiza watu (7:1–12:26). Kuna watu na nyumba chache katika jiji hilo, kwa maana Waisraeli walio wengi wanaishi nje kwa kulingana na urithi wao wa kikabila. Mungu amwelekeza Nehemia akusanye wakuu na watu wote ili waandikishwe kinasaba. Katika kufanya hivyo, achunguza maandishi ya wale waliorejea kutoka Babuloni. Kisha kusanyiko la siku nane laitishwa kwenye uwanja wa umma (watu wote) uliokuwa kando ya Lango la Maji. Ezra afungua programu akiwa juu ya jukwaa la mbao. Abariki Yehova na kisha asoma kitabu cha Sheria ya Musa tangu alfajiri hadi adhuhuri. Asaidiwa kwa njia yenye uwezo na Walawi wengine, wanaoeleza Sheria kwa watu na waendelea ‘kusoma kwa sauti ya kusikilika kitabu, Sheria ya Mungu wa kweli, ikielezwa maana yake, hata wakayafahamu yaliyosomwa.’ (8:8) Nehemia ahimiza watu wale karamu na kushangilia na kuthamini nguvu za maneno haya: “Furaha ya BWANA [Yehova, NW] ni nguvu zenu.”—8:10.
11. Ni mkutano gani wa pekee unaofanywa mnamo siku ya pili, na kusanyiko laendeleaje kushangilia?
11 Mnamo siku ya pili ya kusanyiko, wakuu wa watu wafanya mkutano maalumu pamoja na Ezra ili kupata muono-ndani katika Sheria. Wajifunza juu ya Sikukuu ya Vibanda ambayo yapasa kusherehekewa katika mwezi uo huo wa saba, na bila kukawia wapanga kujenga vibanda kwa ajili ya sikukuu hiyo kwa Yehova. Kuna “furaha kubwa sana” wakikaa katika vibanda kwa siku saba, wakisikiliza siku baada ya siku kusomwa kwa Sheria. Mnamo siku ya nane, wafanya kusanyiko la makini, “kama ilivyoagizwa.”—Neh. 8:17, 18; Law. 23:33-36.
12. (a) Ni kusanyiko gani linalofanywa katika mwezi uo huo, likiwa na kichwa gani cha habari? (b) Ni azimio gani linalopitishwa? (c) Ni mpango gani unaofanywa kwa ajili ya kujaza watu Yerusalemu?
12 Mnamo siku ya 24 ya mwezi uo huo, wana wa Israeli wakusanyika tena na kuchukua hatua ya kujitenga na wageni wote. Wasikiliza usomaji maalumu wa Sheria na kisha pitio lenye kuchunguza moyo la shughuli za Mungu pamoja na Israeli, lenye kutolewa na kikundi cha Walawi. Hiki chawa kichwa cha habari: “Simameni, mkamhimidi BWANA [Yehova, NW], Mungu wenu, tangu milele na hata milele. Na lihimidiwe jina lako tukufu, lililotukuka kuliko baraka zote na sifa zote.” (Neh. 9:5) Wachukua hatua ya kuungama dhambi za mababu wao na kwa unyenyekevu waomba baraka za Yehova. Hilo lafanywa kwa namna ya azimio linaloshuhudiwa na muhuri wa wawakilishi wa taifa hilo. Kikundi chote chakubali kujiondoa kwenye ndoa pamoja na vikundi vya watu wa bara hilo, kushika Sabato, na kutoa kwa ajili ya utumishi na wafanya kazi wa hekalu. Mtu mmoja kati ya kila kumi achaguliwa kwa kura akae kwa kudumu katika Yerusalemu, ndani ya ukuta.
13. Ni programu gani ya kusanyiko inayotia alama ya kuwekwa wakfu kwa ukuta, na kwatokea mipango gani?
13 Ukuta wawekwa wakfu (12:27–13:3). Kuwekwa wakfu kwa ukuta uliojengwa upya ni pindi ya wimbo na furaha. Ni pindi ya kusanyiko jingine. Nehemia apanga kuwe kwaya (vikundi vya waimbaji) mbili kubwa za kutoa shukrani na maandamano ya kutembea juu ya ukuta kwenye pande za mkabala (zinazoelekeana), hatimaye zikiungana katika dhabihu kwenye nyumba ya Yehova. Mipango yafanywa kwa ajili ya michango ya kimwili ili kutegemeza makuhani na Walawi kwenye hekalu. Usomaji zaidi wa Biblia hufunua kwamba Waamoni na Wamoabi hawapaswi kuruhusiwa kuingia ndani ya kundi, na kwa hiyo waanza kutenga kundi lote lililochangamana kutoka kwa Israeli.
14. Eleza maovu yanayotokea wakati Nehemia hayupo, na hatua anazochukua ili kuyaondoa.
14 Kuondoa uchafu (13:4-31). Baada ya kutumia kipindi fulani katika Babuloni, Nehemia arejea Yerusalemu na kukuta kwamba maovu mapya yamenyemelea miongoni mwa Wayahudi. Jinsi mambo yalivyobadilika haraka! Kuhani mkuu Eliashibu hata ametengeneza jumba la kulia chakula katika ua wa hekalu kwa ajili ya matumizi ya Tobia, Mwamoni, mmoja wa maadui wa Mungu. Nehemia hapotezi wakati wowote. Aondosha vyombo vya Tobia na kuagiza majumba yote ya kulia chakula yasafishwe. Pia, akuta kwamba michango ya mali ya Walawi haiendelei, kwa hiyo waenda nje ya Yerusalemu kutafuta riziki. Biashara imepamba moto katika jiji. Sabato haiadhimishwi. Nehemia awaambia: “Mwazidi kuleta ghadhabu juu ya Israeli kwa kuinajisi sabato.” (13:18) Afunga malango ya jiji siku ya Sabato ili wafanya biashara wasiingie, na awaagiza watoke kwenye ukuta wa jiji. Lakini kuna uovu unaozidi huo, jambo walilokuwa wamekubali kwa makini hawatafanya tena. Wameleta wake wageni, wapagani ndani ya jiji. Tayari uzao wa miungano hiyo hauneni tena lugha ya Kiyahudi. Nehemia awakumbusha kwamba Sulemani alitenda dhambi kwa sababu ya wake wageni. Kwa sababu ya dhambi hiyo, Nehemia afukuza mjukuu wa Eliashibu kuhani mkuu.c Kisha apanga kwa utaratibu ukuhani na kazi ya Walawi.
15. Nehemia atoa ombi gani la unyenyekevu?
15 Nehemia amalizia kitabu chake kwa ombi jepesi na la unyenyekevu: “Nikumbuke, Ee Mungu wangu, ili unitendee mema.”—13:31.
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
16. Ni kwa njia zipi Nehemia ni kielelezo kizuri sana kwa wote wapendao ibada ya haki?
16 Ujitoaji kimungu wa Nehemia wapasa kuwa kichocheo kwa wote wapendao ibada ya haki. Yeye aliacha cheo chenye kibali ili awe mwangalizi mnyenyekevu miongoni mwa watu wa Yehova. Hata alikataa mchango wa kimwili uliokuwa haki yake, na alilaani vikali kupenda mali kuwa ni mtego. Mfuatio wenye bidii na uendelezaji wa ibada ya Yehova ndiyo mambo ambayo Nehemia alitilia moyo taifa lote. (5:14, 15; 13:10-13) Nehemia alikuwa kielelezo kizuri sana kwetu katika kuwa asiye na ubinafsi hata kidogo na mwenye busara, mwanamume mwenye kuchukua hatua, asiyehofu kwa ajili ya uadilifu mbele ya hatari. (4:14, 19, 20; 6:3, 15) Yeye alikuwa na hofu inayofaa ya Mungu na alipendezwa katika kujenga watumishi wenzake katika imani. (13:14; 8:9) Kwa jitihada kubwa alitumia sheria ya Yehova, hasa kama ilivyohusiana na ibada ya kweli na kukataa mavutano ya kigeni, kama vile ndoa na wapagani.—13:8, 23-29.
17. Ni jinsi gani Nehemia ni kielelezo pia katika maarifa na katika kutumia sheria ya Mungu?
17 Katika kitabu chote ni wazi kwamba Nehemia alikuwa na maarifa mengi ya sheria ya Yehova, naye aliyatumia vizuri. Aliomba baraka ya Mungu kwa sababu ya ahadi ya Yehova kwenye Kumbukumbu la Torati 30:1-4, akiwa na imani kamili kwamba Yehova angetenda kwa uaminifu-mshikamanifu kwa niaba yake. (Neh. 1:8, 9) Yeye alipanga makusanyiko mengi, hasa ili kufahamisha Wayahudi mambo yaliyoandikwa zamani. Katika usomaji wao wa Sheria, Nehemia na Ezra walikuwa wenye bidii kufanya Neno la Mungu liwe wazi kwa watu na kulitekeleza kwa kulitumia.—8:8, 13-16; 13:1-3.
18. Uongozi wa kisala wa Nehemia wapasa kukazia masomo gani kwa waangalizi wote?
18 Tegemeo kamili la Nehemia kwa Yehova na maombi yake ya unyenyekevu vyapasa kututia moyo tusitawishe mtazamo kama huo wa kutegemea Mungu kwa njia ya sala. Angalia jinsi sala zake zilivyotukuza Mungu, zilivyoonyesha kukiri dhambi za watu wake, na kuomba kwamba jina la Yehova litakaswe. (1:4-11; 4:14; 6:14; 13:14, 29, 31) Kwamba mwangalizi huyu mwenye bidii alikuwa mwenye mamlaka yenye nguvu kati ya watu wa Mungu yaonyeshwa na utayari ambao walifuata mwelekezo wake wa hekima na shangwe waliyopata katika kufanya mapenzi ya Mungu pamoja naye. Jinsi alivyo kielelezo chenye kuchochea kweli kweli! Hata hivyo, kusipokuwapo mwangalizi mwenye hekima, jinsi kupenda mali, ufisadi, na uasi-imani wa moja kwa moja vilivyopenya haraka! Hakika hilo lapasa kuonyesha uzito kwa waangalizi wote miongoni mwa watu wa Mungu leo uhitaji wa kuwa hai, chonjo, wenye bidii kwa ajili ya faida za ndugu zao Wakristo, na wenye uelewevu na imara katika kuwaongoza katika njia za ibada ya kweli.
19. (a) Nehemia alitumiaje Neno la Mungu ili kuimarisha uhakika katika ahadi za Ufalme? (b) Tumaini la Ufalme linasisimuaje watumishi wa Mungu leo?
19 Nehemia alionyesha tegemeo lenye nguvu kwa Neno la Mungu. Si kwamba tu alikuwa mwalimu mwenye bidii wa Maandiko bali pia aliyatumia katika kuhakikisha urithi wa kinasaba na utumishi wa makuhani na Walawi miongoni mwa watu wa Mungu waliorejeshwa. (Neh. 1:8; 11:1–12:26; Yos. 14:1–21:45) Lazima hilo liwe lilikuwa kitia-moyo kikubwa kwa baki la Kiyahudi. Lilitia nguvu uhakika wao katika ahadi tukufu zilizokuwa zimetolewa hapo awali kuhusu Mbegu na mrejesho mtukufu zaidi utakaokuja chini ya Ufalme Wake. Tumaini katika mrejesho wa Ufalme ndilo huchochea watumishi wa Mungu wapigane kwa moyo mkuu kwa ajili ya faida za Ufalme na kuwa wenye shughuli katika kujenga ibada ya kweli duniani pote.
[Maelezo ya Chini]
a Insight on the Scriptures, Vol. 2 pages 613-16.
b Insgiht on the Scriptures, Vol. 2 pages 899-901.
c Wanahistoria fulani Wayahudi hudai kwamba mjukuu huyu wa Eliashibu aliitwa Manase na kwamba, yeye na baba-mkwe wake, Sanbalati, alijenga hekalu juu ya Mlima Gerizimu, ambalo likawa kitovu cha ibada ya Kisamaria na ambamo alitumikia akiwa kuhani wakati wa maisha yake. Gerizimu ndio ule mlima unaorejezewa na Yesu kwenye Yohana 4:21.—The Second Temple in Jerusalem, 1908, W. Shaw Caldecott, kurasa 252-5; ona Mnara wa Mlinzi (Kiingereza), Julai 15, 1960, kurasa 425-6.