Ndoto ya Nebukadreza—Ni Nini Maana ya Sehemu Mbalimbali za Ile Sanamu Ambayo Nebukadreza Aliona Katika Ndoto?
NI WAZI kwamba sanamu hiyo yahusu utawala wa dunia na kusudi la Yehova Mungu kuhusu utawala huo. Hilo linaonyeshwa wazi katika ufafanuzi wa Danieli uliopuliziwa. Kichwa cha dhahabu kiliwakilisha Nebukadreza, yule ambaye, kwa ruhusa ya kimungu, alikuwa amepata mamlaka akiwa mtawala mkuu wa ulimwengu na, kwa umaana zaidi, alikuwa amepindua ufalme halisi wa Yuda. Hata hivyo, katika kusema, “Wewe u kichwa kile cha dhahabu,” haionekani kwamba Danieli alikazia umaana wa kichwa hicho juu ya Nebukadreza pekee. Kwa kuwa zile sehemu nyinginezo za mwili ziliwakilisha falme, ni wazi kwamba kichwa kiliwakilisha nasaba ya wafalme wa Kibabiloni kutoka kwa Nebukadreza hadi anguko la Babiloni wakati wa Mfalme Nabonido na mwana wake Belshaza.—Danieli 2:37, 38.
Kwa hiyo ufalme uliowakilishwa na kifua na mikono ya fedha ungekuwa serikali ya muungano wa Umedi na Uajemi, uliopindua Babiloni katika 539 K.W.K. Huo ulikuwa “mdogo kuliko” nasaba ya wafalme wa Babiloni lakini si katika maana ya kuwa na eneo dogo zaidi la kutawala au ya kuwa na nguvu ndogo zaidi kijeshi au kiuchumi. Kwa hiyo ukuu wa Babiloni waweza kuhusianishwa na kuwa kwayo serikali iliyopindua ufalme halisi wa Mungu katika Yerusalemu, ambayo ni sifa isiyokuwa ya serikali ya muungano wa Umedi na Uajemi. Nasaba ya watawala wa ulimwengu wa Umedi na Uajemi iliishia na Dario wa 3 (Kodomano), ambaye majeshi yake yalishindwa kabisa na Aleksanda yule Mmakedonia katika 331 K.W.K. Hivyo Ugiriki ndiyo serikali inayowakilishwa na tumbo na viuno vya shaba vya sanamu hiyo.—Danieli 2:39.
Utawala wa Ugiriki, au wa Kiheleni uliendelea, ingawa ulikuwa umegawanyika, mpaka uliposhindwa hatimaye na serikali ya Roma iliyokuwa ikiinuka. Hivyo Serikali ya Ulimwengu ya Roma yaonekana katika sanamu hiyo ikiwa imefananishwa na ile madini yenye thamani ndogo zaidi lakini iliyo ngumu zaidi, chuma, iliyopatikana miguuni pa sanamu hiyo kubwa. Nguvu za Roma za kuvunja na kuponda-ponda falme zenye upinzani, zinazoonyeshwa katika unabii huo, zinajulikana vema katika historia. (Danieli 2:40) Hata hivyo, Roma pekee haiwezi kutimiza matakwa ya kuwakilisha miguu na nyayo za miguu za sanamu hiyo, kwani utawala wa Milki ya Roma haukuona mwisho wa ndoto hiyo ya kiunabii, yaani, kuja kwa lile jiwe la ufananisho lililochongwa kutoka mlima na pia kuponda kwalo sanamu nzima na baadaye kuijaza dunia nzima.
Hivyo, maelezo ya baadhi ya wafafanuzi wa Biblia yanafanana sana na yale ya M. F. Unger, asemaye: “Ndoto ya Nebukadreza, iliyofafanuliwa na Danieli, yasimulia mwendo na mwisho wa ‘nyakati za Wasio Wayahudi’ (Luka 21:24; Ufu. 16:19); yaani, ya serikali za ulimwengu za Wasio Wayahudi zitakazoharibiwa kwenye Kuja kwa Pili kwa Kristo. . . . ile sehemu yenye vidole kumi vya miguu itakuwa hali ya utawala wa ulimwengu wa Wasio Wayahudi wakati wa kurudi kwa lile Jiwe la Kupiga (Dan. 2:34, 35). . . . Kwenye kuja kwa kwanza kwa Kristo wala pigo la ghafula lenye kishindo halikutukia wala ile hali ya vidole kumi vya miguu haikutukia.” (Unger’s Bible Dictionary, 1965, uku. 516) Danieli mwenyewe alimwambia Nebukadreza kwamba ndoto hiyo ilihusiana na “mambo yatakayokuwa siku za mwisho” (Danieli 2:28), na kwa kuwa hilo jiwe la ufananisho laonyeshwa kuwa lawakilisha Ufalme wa Mungu, yaweza kutazamiwa kwamba utawala unaofananishwa na miguu na nyayo za miguu za chuma ungefikia hadi wakati wa kusimamishwa kwa Ufalme huo na hadi wakati uchukuapo hatua ya ‘kuvunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu.’—Danieli 2:44.
Historia yaonyesha kwamba, ingawa Milki ya Roma ilifurahia urefusho wa muda wa kutawala kwa namna ya Milki Takatifu ya Roma ya taifa la Kijerumani, hatimaye hiyo ilishindwa na serikali ya Uingereza iliyokuwa ikiinuka na ambayo wakati mmoja ilikuwa imetawalwa nayo. Kwa sababu ya kuwa na ukaribu wa kijamii na kutenda kwa njia ileile kwa ujumla, leo Uingereza na United States hurejezewa mara nyingi kuwa Serikali ya Ulimwengu ya Uingereza na Amerika, utawala mkuu wa sasa katika historia ya ulimwengu.
Mchanganyiko wa chuma na udongo katika vidole vya miguu vya hiyo sanamu kubwa vyaonyesha kwa wazi hali itakayodhihirika karibuni katika wonyesho wa mwisho wa utawala wa ulimwengu wa kisiasa. Kwingineko katika Maandiko, udongo unatumiwa kwa ufananisho kusimamia watu wa kimwili, waliofanyizwa kutoka mavumbi ya dunia. (Ayubu 10:9; Isaya 29:16; Warumi 9:20, 21) Hivyo ufafanuzi wa Danieli waonekana kufananisha udongo na “mbegu za wanadamu,” ambao unapochanganywa hutokeza udhaifu katika ile inayofananishwa na vidole kumi vya miguu vya sanamu hiyo. Hilo laonyesha udhaifu na ukosefu wa ushikamano katika nguvu zilizo kama chuma za sehemu ya mwisho ya utawala wa ulimwengu wa falme za kidunia. (Danieli 2:41-43) Mwanadamu wa kawaida angekuwa na uvutano zaidi katika mambo ya serikali. Kwa sababu “kumi” hutumiwa kwa upatano katika Biblia ili kuonyesha ukamili, kwa wazi vile vidole kumi vya miguu vyawakilisha mfumo mzima wa utawala duniani pote wakati ambapo Ufalme wa Mungu unasimamishwa na kuchukua hatua dhidi ya serikali za kilimwengu.—Linganisha Ufunuo 17:12-14.
Ile sanamu ya dhahabu iliyosimamishwa na Nebukadreza baadaye kwenye Uwanda wa Dura haihusiani moja kwa moja na ile sanamu kubwa ya ndoto. Kwa sababu ya mipanuko yayo—kimo cha kyubiti 60 (meta 27) na upana wa kyubiti 6 pekee (meta 2.7) (au uwiano wa kumi kwa moja)—haionekani kuwa ilikuwa sanamu yenye umbo la kibinadamu, isipokuwa kama ilikuwa na nguzo ndefu sana, iliyokuwa ndefu kuliko hiyo sanamu yenyewe yenye umbo la kibinadamu. Umbo la kibinadamu lina uwiano wa nne kwa moja tu kwa habari ya kimo na upana. Kwa hiyo huenda ikawa sanamu hiyo ilikuwa yenye asili ya ufananisho zaidi, labda kama yale mawe yenye umbo la yai ya Misri ya kale.—Danieli 3:1.