Sura Ya Kumi Na Tano
Wafalme Washindani Waingia Katika Karne ya 20
1. Mwanahistoria mmoja husema ni nani waliokuwa viongozi wa Ulaya ya karne ya 19?
“ULAYA ya karne ya kumi na tisa ina nguvu fulani ambazo hazikuwa zimepata kuonekana awali,” aandika mwanahistoria Norman Davies. Aongeza kusema hivi: “Ulaya ilikuwa na nguvu nyingi kuliko wakati mwingine wowote: ikiwa na nguvu za kiufundi, nguvu za kiuchumi, nguvu za kitamaduni, na nguvu kuliko mabara mengine.” Viongozi wa “‘karne yenye nguvu’ na ushindi huko Ulaya,” asema Davies, “kwanza kabisa ni Uingereza . . . na makumi ya miaka baadaye, Ujerumani.”
“WATANUIA KUTENDA MADHARA”
2. Karne ya 19 ilipokuwa ikiisha, ni serikali gani zilizokuwa “mfalme wa kaskazini” na “mfalme wa kusini”?
2 Karne ya 19 ilipokaribia kwisha, Milki ya Ujerumani ilikuwa “mfalme wa kaskazini” na Uingereza ilikuwa “mfalme wa kusini.” (Danieli 11:14, 15) “Katika habari za wafalme hao wawili,” akasema malaika wa Yehova, “mioyo yao watanuia kutenda madhara, nao watasema uongo walipo pamoja mezani.” Aendelea kusema: “Lakini hilo halitafanikiwa; maana mwisho utatokea wakati ulioamriwa.”—Danieli 11:27.
3, 4. (a) Ni nani aliyekuwa maliki wa kwanza wa Milki ya Ujerumani, na ni ushirikiano gani ulioundwa? (b) Maliki Wilhelm alifuata sera gani?
3 Januari 18, 1871, Wilhelm wa Kwanza akawa maliki wa kwanza wa Milki ya Ujerumani. Akamweka Otto von Bismarck awe waziri mkuu. Akinuia kuisitawisha hiyo milki mpya, Bismarck aliepuka kupambana na mataifa mengine naye akafanya ushirikiano na Austria-Hungaria na Italia, ulioitwa Shirikisho la Nchi Tatu. Lakini punde si punde masilahi ya mfalme huyo mpya wa kaskazini yakagongana na masilahi ya mfalme wa kusini.
4 Baada ya Wilhelm wa Kwanza na Frederick wa Tatu aliyetawala baada yake kufa mwaka wa 1888, Wilhelm wa Pili mwenye umri wa miaka 29 akaanza kutawala. Wilhelm wa Pili, au Maliki Wilhelm, alimlazimisha Bismarck ajiuzulu naye alitumia sera ya kuzidisha uvutano wa Ujerumani kotekote ulimwenguni. “Chini ya utawala wa Wilhelm wa Pili,” asema mwanahistoria mmoja, “[Ujerumani] ilikuwa yenye kujigamba na yenye uchokozi.”
5. Wafalme hao wawili waliketije “pamoja mezani,” nao walizungumzia nini huko?
5 Zari Nicholas wa Pili wa Urusi alipopanga kuwe na mkutano wa amani huko Hague, Uholanzi, Agosti 24, 1898, kulikuwa na wasiwasi miongoni mwa mataifa. Mkutano huo na mkutano uliofuata mwaka wa 1907 ulianzisha Mahakama Yenye Kudumu ya Mapatano huko Hague. Kuwa washiriki wa mahakama hiyo kulifanya Milki ya Ujerumani na Uingereza zionekane kana kwamba zilipendelea amani. Ziliketi “pamoja mezani,” zikionekana kuwa zenye urafiki, lakini ‘mioyo yao ilinuia kutenda madhara.’ Mbinu ya ‘kusema uwongo walipo pamoja mezani’ haingeweza kuendeleza amani ya kweli. Kuhusu tamaa za kisiasa, kiuchumi, na kijeshi, hakuna chochote ambacho ‘kingefanikiwa’ kwa sababu mwisho wa wafalme hao wawili “utatokea wakati ulioamriwa” na Yehova Mungu.
‘KINYUME CHA AGANO TAKATIFU’
6, 7. (a) Mfalme wa kaskazini alirudije “mpaka nchi yake”? (b) Mfalme wa kusini alitendaje kufuatia uvutano wenye kuongezeka wa mfalme wa kaskazini?
6 Akiendelea, malaika wa Mungu alisema hivi: “Ndipo [mfalme wa kaskazini] atakaporudi mpaka nchi yake mwenye utajiri mwingi; na moyo wake utakuwa kinyume cha hilo agano takatifu; naye atafanya kama apendavyo, na kurudi mpaka nchi yake.”—Danieli 11:28.
7 Maliki Wilhelm alirudi ‘nchini,’ au kwenye hali ya kidunia, ya mfalme wa kale wa kaskazini. Jinsi gani? Kwa kutokeza utawala wa maliki uliokusudiwa kupanua Milki ya Ujerumani na kuzidisha uvutano wake. Wilhelm wa Pili alifuatia miradi ya kuanzisha koloni katika Afrika na kwingineko. Akitaka kushindana na ukuu wa Uingereza baharini, aliunda jeshi lenye nguvu la majini. “Jeshi la majini la Ujerumani lilianza likiwa duni tu na kukua mpaka likawa la pili baada ya Uingereza katika miaka kumi hivi,” chasema kichapo The New Encyclopædia Britannica. Ili kuudumisha ukuu huo, Uingereza ililazimika kupanua jeshi lake la majini. Uingereza ilifanya maelewano na Ufaransa na maelewano kama hayo pamoja na Urusi, hivyo ikifanyiza Maelewano ya Nchi Tatu. Sasa Ulaya ilikuwa imegawanyika na kuwa kambi mbili za kijeshi— Shirikisho la Nchi Tatu upande mmoja na Maelewano ya Nchi Tatu upande wa pili.
8. Milki ya Ujerumani ilipataje “utajiri mwingi”?
8 Milki ya Ujerumani ilifanya mambo kwa hima, ikapata “utajiri mwingi” kwa kuwa Ujerumani ilikuwa sehemu kubwa ya Shirikisho la Nchi Tatu. Austria-Hungaria na Italia zilikuwa nchi za Kikatoliki. Kwa hiyo, lile Shirikisho la Nchi Tatu lilipendelewa na papa, ilhali mfalme wa kusini, na sehemu kubwa ya Maelewano ya Nchi Tatu isiyo ya Kikatoliki, hakupendelewa.
9. Mfalme wa kaskazini alikuwaje ‘kinyume cha agano takatifu’ moyoni?
9 Vipi juu ya watu wa Yehova? Kwa muda mrefu walikuwa wametangaza kwamba “nyakati zilizowekwa rasmi za mataifa” zingeisha mwaka wa 1914.a (Luka 21:24) Mwaka huo, Ufalme wa Mungu mikononi mwa Mrithi wa Mfalme Daudi, Yesu Kristo, ulianza kutawala mbinguni. (2 Samweli 7:12-16; Luka 22:28, 29) Mapema hata kufikia Machi 1880, gazeti la Watch Tower lilihusisha utawala wa Ufalme wa Mungu na kumalizika kwa “nyakati zilizowekwa rasmi za mataifa,” au “nyakati za Wasio Wayahudi.” (King James Version) Lakini moyo wa mfalme wa kaskazini wa Ujerumani ulikuwa ‘kinyume cha agano takatifu la ufalme.’ Badala ya kuukiri utawala wa Ufalme, Maliki Wilhelm ‘alifanya apendavyo’ kwa kuendeleza hila za kuutawala ulimwengu. Ingawaje, kwa kufanya hivyo alipanda mbegu za Vita ya Ulimwengu ya Kwanza.
MFALME ‘AVUNJIKA MOYO’ VITANI
10, 11. Vita ya Ulimwengu ya Kwanza ilianzaje, na huo ulikuwaje “wakati ulioamriwa”?
10 “Kwa wakati ulioamriwa [mfalme wa kaskazini] atarudi,” malaika akatabiri, “na kuingia upande wa kusini; lakini wakati wa mwisho mambo hayatakuwa kama yalivyokuwa wakati wa kwanza.” (Danieli 11:29) “Wakati ulioamriwa” wa Mungu wa kukomesha utawala wa Wasio Wayahudi duniani ulifika mwaka wa 1914 aliposimamisha Ufalme wa kimbingu. Juni 28 mwaka huo, haramia mmoja Mserbia alimwua Dyuki-Mkuu wa Austria Francis Ferdinand na mke wake huko Sarajevo, Bosnia. Hilo ndilo lililochochea Vita ya Ulimwengu ya Kwanza.
11 Maliki Wilhelm alihimiza Austria-Hungaria zilipize kisasi dhidi ya Serbia. Wakiwa na uhakika kwamba Ujerumani itaiunga mkono, Austria-Hungaria ikatangaza vita dhidi ya Serbia Julai 28, 1914. Lakini Urusi ikasaidia Serbia. Ujerumani ilipotangaza vita dhidi ya Urusi, Ufaransa (mshiriki wa Maelewano ya Nchi Tatu) ikaunga mkono Urusi. Kisha Ujerumani ikatangaza vita dhidi ya Ufaransa. Ili kufanya jiji la Paris lifikike kwa urahisi, Ujerumani ikashambulia Ubelgiji, ambayo ilikuwa imehakikishiwa na Uingereza kwamba haingehusika vitani. Kwa hiyo, Uingereza ikatangaza vita dhidi ya Ujerumani. Mataifa mengine yakahusika, na Italia ikahama toka upande mmoja kwenda wa pili. Wakati wa vita hiyo, Uingereza ikafanya Misri iwe chini ya himaya yake ili kumzuia mfalme wa kaskazini asiuzuie Mfereji wa Suez na kuivamia Misri, nchi ya kale ya mfalme wa kusini.
12. Wakati wa vita ya ulimwengu ya kwanza, ni katika maana gani ‘mambo hayakuwa kama yalivyokuwa wakati wa kwanza’?
12 “Licha ya ukubwa na nguvu za Mataifa ya Muungano,” chasema kichapo The World Book Encyclopedia, “yaonekana Ujerumani ilikuwa karibu kushinda vita hiyo.” Katika mapambano ya awali kati ya wafalme hao wawili, Milki ya Roma, ikiwa mfalme wa kaskazini, ilikuwa imeshinda mfululizo. Wakati huu, ‘mambo hayakuwa kama yalivyokuwa wakati wa kwanza.’ Mfalme wa kaskazini alishindwa vitani. Akitoa sababu ya hilo, malaika alisema hivi: “Merikebu za Kitimu zitakuja kupigana naye; basi atavunjika moyo.” (Danieli 11:30a) “Merikebu za Kitimu” zilikuwa nini?
13, 14. (a) “Merikebu za Kitimu” zilizokuja kupigana na mfalme wa kaskazini zilikuwa nini hasa? (b) Merikebu zaidi za Kitimu zilikujaje vita ya ulimwengu ya kwanza ilipokuwa ikiendelea?
13 Wakati wa Danieli, Kitimu ilikuwa Saiprasi. Mapema katika vita ya ulimwengu ya kwanza, Saiprasi ilitekwa na Uingereza. Isitoshe, kulingana na kichapo The Zondervan Pictorial Encyclopedia of the Bible, jina Kitimu “hutia ndani pia M[agharibi] kwa ujumla, lakini hasa M[agharibi] yenye mabaharia.” Tafsiri ya New International Version hutafsiri maneno “merikebu za Kitimu” kuwa “merikebu za pwani za magharibi.” Wakati wa vita ya ulimwengu ya kwanza, merikebu za Kitimu zilikuwa meli za Uingereza hasa, iliyokuwa pwani ya magharibi ya Ulaya.
14 Vita ilipoendelea polepole, Jeshi la Majini la Uingereza liliimarishwa na merikebu zaidi za Kitimu. Mei 7, 1915, nyambizi ya Ujerumani iitwayo U-20 ilizamisha merikebu ya raia iitwayo, Lusitania karibu na pwani ya kusini ya Ireland. Waamerika 128 walikuwa miongoni mwa watu waliokufa. Baadaye, Ujerumani ilipigana kwa kutumia nyambizi hadi Atlantiki. Hatimaye, Aprili 6, 1917, Rais Woodrow Wilson wa Marekani akatangaza vita dhidi ya Ujerumani. Akiwa ameongezewa ukuu na manowari na vikosi vya Marekani, mfalme wa kusini—sasa akiwa Serikali ya Ulimwengu ya Uingereza na Marekani—alikuwa katika vita kikamili dhidi ya mfalme mpinzani.
15. Mfalme wa kaskazini ‘alivunjika moyo’ lini?
15 Kwa kuwa alishambuliwa na Serikali ya Ulimwengu ya Uingereza na Marekani, mfalme wa kaskazini ‘akavunjika moyo’ na kushindwa Novemba mwaka wa 1918. Wilhelm wa Pili akakimbilia uhamishoni huko Uholanzi, na Ujerumani ikawa jamhuri. Lakini mfalme wa kaskazini hakuwa ametokomea.
MFALME ATENDA “KADIRI APENDAVYO”
16. Kulingana na unabii, mfalme wa kaskazini alitendaje baada ya kushindwa?
16 “Naye [mfalme wa kaskazini] atarudi na kulighadhibikia hilo agano takatifu; na kutenda kadiri apendavyo; naam, atarudi, na kuwasikiliza walioacha hilo agano takatifu.” (Danieli 11:30b) Ndivyo alivyotabiri malaika, na ndivyo ilivyotimia.
17. Ni nini kilichoongoza kwenye kutokea kwa Adolf Hitler?
17 Baada ya vita kwisha mwaka wa 1918, Mataifa ya Muungano walioshinda waliwekea Ujerumani mkataba wa amani wa kumwadhibu. Wajerumani waliyaona masharti ya mkataba huo kuwa makali, nayo ile jamhuri mpya ilikuwa dhaifu tokea mwanzo. Ujerumani ilijikokota kwa miaka kadhaa ikiwa na taabu nyingi na ikapatwa na ule Mshuko Mkuu wa Kiuchumi ambao ulisababisha watu milioni sita wapoteze kazi zao. Mapema katika miaka ya 1930, wakati barabara wa kutokea kwa Adolf Hitler ulikuwa umetimia. Akawa waziri mkuu Januari 1933 na mwaka uliofuata akawa rais wa milki ambayo Wanazi waliita Milki ya Tatu.b
18. Hitler ‘alitendaje kadiri alivyopenda’?
18 Punde baada ya kupata mamlaka, Hitler alianzisha shambulio kali dhidi ya “agano takatifu,” lililowakilishwa na ndugu watiwa-mafuta wa Yesu Kristo. (Mathayo 25:40) Katika hilo alitenda “kadiri apendavyo” dhidi ya Wakristo hao wenye uaminifu-mshikamanifu, akiwanyanyasa wengi wao kikatili. Hitler alifanikiwa kiuchumi na kidiplomasia, akitenda “kadiri apendavyo” pia katika nyanja hizo. Baada ya miaka michache aliifanya Ujerumani kuwa serikali kubwa ulimwenguni.
19. Hitler alijiunga na nani akitafuta kuungwa mkono?
19 Hitler ‘aliwasikiliza walioacha hilo agano takatifu.’ Hao walikuwa nani? Yaonekana ni viongozi wa Jumuiya ya Wakristo, waliodai kuwa na uhusiano wa kiagano pamoja na Mungu lakini wakakoma kuwa wanafunzi wa Yesu Kristo. Hitler alifanikiwa kuungwa mkono na “walioacha hilo agano takatifu.” Kwa kielelezo, alifanya mkataba na papa wa Roma. Mwaka wa 1935, Hitler alianzisha Wizara ya Mambo ya Kanisa. Mojawapo ya miradi yake ilikuwa kufanya makanisa ya Kievanjeli yawe chini ya serikali.
“WENYE SILAHA” WASIMAMA UPANDE WA MFALME
20. Ni “wenye silaha” gani ambao mfalme wa kaskazini alitumia, naye aliwatumia dhidi ya nani?
20 Upesi Hitler akaingia vitani, kama vile malaika alivyotabiri kwa usahihi: “Wenye silaha watasimama upande wake, nao watapatia unajisi mahali patakatifu, ndiyo ngome, nao wataondoa sadaka ya kuteketezwa ya kila siku.” (Danieli 11:31a) “Wenye silaha” walikuwa majeshi ya mfalme wa kaskazini yaliyotumiwa kupigana na mfalme wa kusini katika Vita ya Ulimwengu ya Pili. Septemba 1, 1939, “wenye silaha” wa Nazi walivamia Poland. Siku mbili baadaye, Uingereza na Ufaransa zikatangaza vita dhidi ya Ujerumani ili kuisaidia Poland. Ndivyo Vita ya Ulimwengu ya Pili ilivyoanza. Poland ilishindwa haraka, na punde baadaye majeshi ya Ujerumani yakamiliki Denmark, Norway, Uholanzi, Ubelgiji, Luxembourg, na Ufaransa. “Mwishoni mwa mwaka wa 1941,” chasema kichapo The World Book Encyclopedia, “Ujerumani ya Nazi ilitawala bara hilo.”
21. Mambo yalimgeukaje mfalme wa kaskazini wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili, na matokeo yakawa nini?
21 Ingawa Ujerumani na Muungano wa Sovieti ulikuwa umefanya Mkataba wa Urafiki, Ushirikiano, na Kutovuka Mipaka, Hitler alivamia eneo la Sovieti Juni 22, 1941. Tendo hilo lilifanya Muungano wa Sovieti ujiunge na Uingereza. Jeshi la Sovieti lilipigana vikali licha ya kuwa awali majeshi ya Ujerumani yalikuwa yamesonga mbele sana. Desemba 6, 1941, jeshi la Ujerumani lilishindwa huko Moscow. Siku iliyofuata, Japani iliyokuwa ikiunga mkono Ujerumani ikalipua kombora katika Bandari ya Pearl, Hawaii. Alipopata kujua juu ya hilo, Hitler akawaambia wasaidizi wake hivi: “Sasa hatuwezi kushindwa katika vita hii.” Desemba 11 alitangaza vita dhidi ya Marekani haraka-haraka bila kufikiri. Lakini alidharau nguvu za Muungano wa Sovieti na Marekani. Jeshi la Sovieti likishambulia upande wa mashariki, na Uingereza na Marekani zikishambulia upande wa magharibi, punde si punde mambo yakamgeuka Hitler. Majeshi ya Ujerumani yalipoteza eneo moja baada ya jingine. Baada ya Hitler kujiua, Ujerumani ikajisalimisha kwa hayo Mataifa ya Muungano, Mei 7, 1945.
22. Mfalme wa kaskazini ‘alinajisije mahali patakatifu na kuondoa sadaka ya kuteketezwa ya kila siku’?
22 Wenye silaha wa Nazi “watapatia unajisi mahali patakatifu, ndiyo ngome, nao wataondoa sadaka ya kuteketezwa ya kila siku,” akasema malaika. Katika Yuda la kale mahali patakatifu palikuwa sehemu ya hekalu katika Yerusalemu. Hata hivyo, Wayahudi walipomkataa Yesu, Yehova aliwakataa pamoja na hekalu lao. (Mathayo 23:37–24:2) Tangu karne ya kwanza W.K., hekalu la Yehova limekuwa la kiroho, patakatifu pa patakatifu pakiwa mbinguni na ua wa kiroho ukiwa duniani, ambamo ndugu watiwa-mafuta wa Yesu, Kuhani wa Cheo cha Juu, hutumikia. Tangu miaka ya 1930 na kuendelea, “umati mkubwa” umeabudu ukishirikiana na mabaki ya watiwa-mafuta na kwa hiyo wanasemwa kwamba wanatumikia ‘katika hekalu la Mungu.’ (Ufunuo 7:9, 15; 11:1, 2; Waebrania 9:11, 12, 24) Katika nchi zilizo chini yake, mfalme wa kaskazini alinajisi ua wa kidunia wa hekalu kwa kuwanyanyasa bila huruma mabaki watiwa-mafuta na waandamani wao. Aliwanyanyasa vikali sana hivi kwamba “sadaka ya kuteketezwa ya kila siku”—dhabihu ya hadharani ya sifa kwa jina la Yehova—iliondolewa. (Waebrania 13:15) Hata hivyo, licha ya kuteseka vibaya, Wakristo watiwa-mafuta waaminifu pamoja na “kondoo wengine” waliendelea kuhubiri wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili.—Yohana 10:16.
‘CHUKIZO LASIMAMISHWA’
23. “Chukizo” lilikuwa nini katika karne ya kwanza?
23 Mwisho wa vita ya ulimwengu ya pili ulipokaribia, jambo jingine lilitukia, kama vile malaika wa Mungu alivyokuwa ametabiri. “Nao watalisimamisha chukizo la uharibifu.” (Danieli 11:31b) Yesu pia alikuwa amesema juu ya “chukizo.” Katika karne ya kwanza, lilikuwa jeshi la Roma ambalo lilikuja Yerusalemu mwaka wa 66 W.K. ili kukomesha uasi wa Wayahudi.c—Mathayo 24:15; Danieli 9:27.
24, 25. (a) “Chukizo” ni nini leo? (b) ‘Chukizo lilisimamishwa’ lini na jinsi gani?
24 Ni “chukizo” gani “limesimamishwa” leo? Yaonekana ni mwigizo ‘wenye kuchukiza’ wa Ufalme wa Mungu. Hilo lilikuwa Ushirika wa Mataifa, yule hayawani-mwitu mwenye rangi nyekundu-nyangavu aliyeingia abiso, au aliyekoma kuwepo akiwa shirika la amani ya ulimwengu, Vita ya Ulimwengu ya Pili ilipozuka. (Ufunuo 17:8) Hata hivyo, “hayawani-mwitu” huyo alipaswa “kupanda kutoka katika abiso.” Alipanda wakati ambapo Umoja wa Mataifa, ukiwa na mataifa washiriki 50 kutia ndani na uliokuwa Muungano wa Sovieti, ulianzishwa Oktoba 24, 1945. Kwa hiyo, “chukizo” lililotabiriwa na malaika—Umoja wa Mataifa—likasimamishwa.
25 Ujerumani ilikuwa adui mkubwa wa mfalme wa kusini katika vita vyote viwili vya ulimwengu nayo ilikuwa mfalme wa kaskazini. Ni nani ambaye angekuwa mfalme wa kaskazini baada yake?
[Maelezo ya Chini]
a Ona Sura ya 6 ya kitabu hiki.
b Milki Takatifu ya Roma ilikuwa milki ya kwanza, nayo Milki ya Ujerumani ikawa ya pili.
c Ona Sura ya 11 ya kitabu hiki.
UMEFAHAMU NINI?
• Mwishoni mwa karne ya 19, ni serikali gani zilizokuwa mfalme wa kaskazini na mfalme wa kusini?
• Wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza, ni katika njia gani matokeo ya pambano hilo kwa mfalme wa kaskazini ‘hayakuwa kama yalivyokuwa wakati wa kwanza’?
• Baada ya Vita ya Ulimwengu ya Kwanza, Hitler alifanyaje Ujerumani ikawa serikali kubwa ulimwenguni?
• Matokeo ya ushindani kati ya mfalme wa kaskazini na mfalme wa kusini wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili yalikuwa nini?
[Chati/Picha katika ukurasa wa 268]
WAFALME KATIKA DANIELI 11:27-31
Mfalme wa Mfalme wa
Kaskazini Kusini
Danieli 11:27-30a Milki ya Ujerumani Uingereza, kisha
(Vita ya Ulimwengu Serikali ya Ulimwengu ya
ya Kwanza) Uingereza na Marekani
Danieli 11:30b, 31 Milki ya Tatu ya Hitler Serikali ya Ulimwengu
(Vita ya Ulimwengu ya Uingereza na
ya Pili) Marekani
[Picha]
Rais Woodrow Wilson pamoja na Mfalme George wa Tano
[[Picha]
Wakristo wengi walinyanyaswa kwenye kambi za mateso
[Picha]
Viongozi wa Jumuiya ya Wakristo walimuunga mkono Hitler
[Picha]
Gari ambamo Dyuki-Mkuu Ferdinand aliuawa
[Picha]
Wanajeshi wa Ujerumani, Vita ya Ulimwengu ya Kwanza
[Picha katika ukurasa wa 257]
Huko Yalta mwaka wa 1945, Waziri Mkuu wa Uingereza Winston Churchill, Rais Franklin D. Roosevelt wa Marekani, na Waziri Mkuu wa Sovieti Joseph Stalin walikubaliana juu ya mipango ya kumiliki Ujerumani, kuunda serikali mpya huko Poland, na kufanya mkutano wa kuanzisha Umoja wa Mataifa
[Picha katika ukurasa wa 258]
1. Dyuki-Mkuu Ferdinand 2. Jeshi la majini la Ujerumani 3. Jeshi la majini la Uingereza 4. Lusitania 5. Tangazo la Vita la Marekani
[Picha katika ukurasa wa 263]
Adolf Hitler alikuwa na uhakika wa kushinda vita baada ya Japani iliyounga mkono Ujerumani wakati wa vita, kulipua Bandari ya Pearl kwa makombora