Mfalme Fulani Atia Unajisi Patakatifu pa Yehova
“Lakini watu wamjuao Mungu wao watakuwa hodari [watashinda, NW].”—DANIELI 11:32.
1, 2. Ni pambano jipi lenye kutazamisha ambalo limetia alama historia ya kibinadamu kwa muda wa zaidi ya miaka 2,000?
WAFALME wawili washindana kufa na kupona ili kupata ukuu. Wa kwanza apata mamlaka zaidi, kisha yule mwingine, na vita hiyo yaendelea kwa muda wa zaidi ya miaka elfu mbili. Katika siku yetu pigano hilo limeathiri watu walio wengi duniani na limetahini uaminifu-maadili wa watu wa Mungu. Hilo laisha kwa tukio lisilotazamiwa na yeyote ya serikali hizo mbili. Historia hiyo ya kimbele yenye kutazamisha ilifunuliwa kwa yule nabii wa kale Danieli.—Danieli, sura ya 10 hadi ya 12.
2 Unabii huo wahusiana na uadui wenye kuendelea kati ya mfalme wa kaskazini na mfalme wa kusini na ulizungumzwa kwa urefu katika kitabu “Your Will Be Done on Earth.”a Katika kitabu hicho ilionyeshwa kwamba awali mfalme wa kaskazini alikuwa ni Siria, kaskazini mwa Israeli. Baadaye, daraka hilo lilichukuliwa na Roma. Mwanzoni, mfalme wa kusini alikuwa ni Misri.
Pambano Katika Wakati wa Mwisho
3. Kulingana na huyo malaika, ule unabii kuhusu mfalme wa kaskazini na mfalme wa kusini ungeeleweka lini, na jinsi gani?
3 Malaika aliyekuwa akimfunulia Danieli mambo hayo alisema hivi: “Lakini wewe, Ee Danieli, yafunge maneno haya, ukakitie muhuri kitabu, hata wakati wa mwisho; wengi wataenda mbio huko na huko, na maarifa yataongezeka.” (Danieli 12:4) Ndiyo, unabii huo wahusiana na wakati wa mwisho—kipindi kilichoanza katika 1914. Katika wakati huo uliotiwa alama, wengi ‘wangeenda mbio huko na huko’ katika Maandiko Matakatifu, na kwa msaada wa roho takatifu, ujuzi wa kweli, kutia na uelewevu wa unabii wa Biblia, ungekuwa mwingi. (Mithali 4:18) Tuzidipo kuingia katika wakati huo zaidi na zaidi, mambo mengi zaidi na zaidi juu ya ule unabii mwingi wa Danieli yameeleweshwa wazi. Basi, tunapaswa kuelewaje unabii wa mfalme wa kaskazini na mfalme wa kusini katika 1993, sasa ikiwa miaka 35 baada ya kutangazwa kwa kitabu “Your Will Be Done on Earth”?
4, 5. (a) Mwaka 1914 unaonekana wapi katika unabii wa Danieli kuhusu mfalme wa kaskazini na mfalme wa kusini? (b) Kulingana na yule malaika, nini lingetukia katika 1914?
4 Mwanzo wa wakati wa mwisho katika 1914 ulitiwa alama na ile vita ya ulimwengu ya kwanza na ile misononeko mingine ambayo Yesu alitabiri. (Mathayo 24:3, 7, 8) Je! twaweza kuuona mwaka huo katika unabii wa Danieli? Ndiyo. Mwanzo wa wakati wa mwisho ni ule “wakati ulioamriwa” unaorejezewa kwenye Danieli 11:29. (Ona “Your Will Be Done on Earth,” kurasa 269-70.) Ulikuwa wakati ulioamriwa tayari na Yehova katika siku ya Danieli, kwa kuwa ulikuja mwishoni mwa ile miaka 2,520 iliyoonyeshwa katika yale matukio yenye umaana wa kiunabii ya Danieli sura ya 4.
5 Miaka hiyo 2,520, tangu uharibifu wa Yerusalemu wa 607 K.W.K. katika ujana wa Danieli hadi 1914 W.K., iliitwa “nyakati zilizowekwa za mataifa.” (Luka 21:24, NW) Ni matukio gani ya kisiasa ambayo yangetia alama mwisho wazo? Malaika mmoja alimfunulia Danieli hilo. Malaika huyo alisema hivi: “Kwa wakati ulioamriwa [mfalme wa kaskazini] atarudi, na kuingia upande wa kusini; lakini wakati wa mwisho mambo hayatakuwa kama yalivyokuwa wakati wa kwanza.”—Danieli 11:29.
Mfalme Ashindwa Vita Moja
6. Katika 1914, ni nani aliyekuwa mfalme wa kaskazini, na ni nani aliyekuwa mfalme wa kusini?
6 Kufikia 1914 daraka la mfalme wa kaskazini lilikuwa limechukuliwa na Ujerumani, ambayo kiongozi wayo alikuwa Kaiser Wilhelm. (“Kaiser,” kutokana na lile jina la cheo la Kiroma “Kaisari.”) Mwanzo wa uadui mwingi katika Ulaya ulikuwa kabiliano jingine zaidi katika ule mfululizo wa makabiliano kati ya mfalme wa kaskazini na mfalme wa kusini. Daraka la huyo wa pili, mfalme wa kusini, sasa lilikuwa limechukuliwa na Uingereza, ambayo upesi ilitwaa Misri, iliyokuwa awali milki ya mfalme wa kusini. Vita ilipoendelea, Uingereza iliungwa mkono na koloni yayo ya zamani, United States ya Amerika. Mfalme wa kusini akawa ile serikali ya ulimwengu ya Uingereza na Amerika, milki yenye nguvu zaidi katika historia.
7, 8. (a) Katika vita ya ulimwengu ya kwanza, ilikuwaje kwamba “mambo hayakuwa kama yalivyokuwa wakati wa kwanza”? (b) Nini lililokuwa tokeo la vita ya ulimwengu ya kwanza, lakini kulingana na unabii huo, mfalme wa kaskazini aliitikiaje?
7 Katika mapambano yaliyotangulia kati ya hao wafalme wawili, Milki ya Kiroma, ikiwa mfalme wa kaskazini, ilikuwa imeshinda daima. Wakati huu, ‘mambo hayakuwa kama yalivyokuwa wakati wa kwanza.’ Kwa nini sivyo? Kwa sababu mfalme wa kaskazini alishindwa katika vita hiyo. Sababu moja ni kwamba “merikebu za Kitimu” zilikuja dhidi ya mfalme wa kaskazini. (Danieli 11:30) Merikebu hizo zilikuwa nini? Katika wakati wa Danieli, Kitimu ilikuwa Saiprasi, na mapema katika vita ya ulimwengu ya kwanza, Saiprasi ilitwaliwa na Uingereza. Zaidi ya hayo, kulingana na The Zondervan Pictorial Encyclopedia of the Bible, jina Kitimu “linapanuliwa kutia ndani M[agharibi] kwa ujumla, lakini M[agharibi] ya kibaharia [hasa].” New International Version hufasiri usemi “merikebu za Kitimu” kuwa “merikebu za pwani za magharibi.” Katika vita ya ulimwengu ya kwanza, merikebu za Kitimu zilithibitika kuwa merikebu za Uingereza, zilizokuwa karibu na pwani ya magharibi ya Ulaya. Baadaye Manowari za Uingereza ziliimarishwa na merikebu kutoka ile kontinenti ya magharibi ya Amerika Kaskazini.
8 Chini ya shambulio hilo, mfalme wa kaskazini ‘alivunjika moyo’ akakubali kushindwa katika 1918. Lakini hakumalizwa. “Atarudi na kulighadhibikia hilo agano takatifu; na kutenda kadiri apendavyo [kwa mafanikio, NW]; naam, atarudi, na kuwasikiliza walioacha hilo agano takatifu.” (Danieli 11:30) Ndivyo alivyoahidi yule malaika, na ndivyo ilivyothibitika kuwa.
Mfalme Atenda kwa Mafanikio
9. Ni nini lililoongoza kwenye mwinuko wa Adolf Hitler mamlakani, naye ‘alitendaje kwa mafanikio’?
9 Baada ya vita, katika 1918, yale Mataifa ya Muungano yenye ushindi yalilazimisha Ujerumani kufuata mkataba wa amani wenye kuadhibu, ambao yaonekana ulikusudiwa kuwaweka Wajerumani katika hali ya karibu kufa njaa kwa wakati ujao usiojulikana. Likiwa tokeo, baada ya kupepesuka kwa miaka kadhaa katika hali ya msononeko mwingi, Ujerumani ilikuwa tayari kwa mwinuko wa Adolf Hitler mamlakani. Alipata mamlaka iliyo kuu zaidi katika 1933 na papo hapo akaanza shambulio kali dhidi ya “hilo agano takatifu,” lililowakilishwa na ndugu za Yesu Kristo wapakwa. Katika hilo alitenda kwa mafanikio dhidi ya Wakristo hao waaminifu-washikamanifu, akiwanyanyasa wengi wao kikatili.
10. Akitafuta utegemezo, Hitler alijaribu kuungana na nani, na kukiwa na matokeo gani?
10 Hitler alikuwa na mafanikio mengi ya kiuchumi na ya kibalozi, akitenda kwa mafanikio katika mambo hayo pia. Katika muda wa miaka michache, akafanya Ujerumani iwe serikali yenye nguvu, akisaidiwa na wale “walioacha hilo agano takatifu.” Hao walikuwa nani? Kwa wazi, walikuwa viongozi wa Jumuiya ya Wakristo, waliodai kuwa na uhusiano wa agano na Mungu lakini waliokuwa wameacha zamani kuwa wanafunzi wa Yesu Kristo. Kwa njia yenye kufaulu Hitler alitoa wito kwa wale “walioacha hilo agano takatifu” ili apate utegemezo wao. Papa katika Roma alifanya mapatano pamoja naye, na Kanisa la Roma Katoliki, na pia makanisa ya Kiprotestanti katika Ujerumani, yalimwunga Hitler mkono muda wote wa utawala wake wenye kuogofya wa miaka 12.
11. Mfalme wa kaskazini ‘alipatiaje unajisi mahali patakatifu’ na ‘kuondoa sadaka ya kila siku’?
11 Hitler alifanikiwa sana hivi kwamba alienda vitani, kama vile yule malaika alivyotabiri kwa usahihi. “Na wenye silaha watasimama upande wake, nao watapatia unajisi mahali patakatifu, ndiyo ngome, nao wataondoa sadaka ya kuteketezwa ya kila siku.” (Danieli 11:31a) Katika Israeli la kale, patakatifu palikuwa sehemu ya hekalu katika Yerusalemu. Hata hivyo, Wayahudi walipomkatalia mbali Yesu, Yehova alikatalia mbali wao na hekalu lao. (Mathayo 23:37–24:2) Tangu karne ya kwanza, hekalu la Yehova limekuwa la kiroho hasa, patakatifu zaidi palo pakiwa mbinguni na likiwa na ua wa kiroho duniani ambao katika huo ndugu wapakwa za Yesu, yule Kuhani wa Juu, hutumikia. Tangu miaka ya 1930, ule mkutano mkubwa umeabudu kwa kushirikiana na mabaki ya wapakwa; kwa hiyo, husemwa kuwa wanatumikia ‘katika hekalu la Mungu.’ (Ufunuo 7:9, 15; 11:1, 2; Waebrania 9:11, 12, 24) Ua wa kidunia wa hekalu ulitiwa unajisi kwa ule mnyanyaso usiolegezwa juu ya mabaki ya wapakwa na wenzi wao katika mabara ambako mfalme wa kaskazini alitawala. Mnyanyaso huo ulikuwa mkali sana hivi kwamba ile sadaka ya kuteketezwa ya daima—ile dhabihu ya hadharani ya sifa kwa jina la Yehova—iliondolewa. (Waebrania 13:15) Bado, historia yaonyesha kwamba kujapokuwa kule kuteseka kubaya sana, Wakristo wapakwa waaminifu, pamoja na wale “kondoo wengine,” waliendelea kuhubiri kichinichini.—Yohana 10:16.
Lile “Chukizo”
12, 13. Lile “chukizo” lilikuwa nini, na—kama ilivyoonwa kimbele na mtumwa mwaminifu mwenye akili—lilisimamishwa upya lini na kwa jinsi gani?
12 Mwisho wa vita ya ulimwengu ya pili ulipokuwa karibu, kulikuwa tukio jingine. “Watalisimamisha chukizo la uharibifu.” (Danieli 11:31b) Hilo “chukizo,” ambalo Yesu pia alitaja, lilikuwa tayari limetambuliwa kuwa Ushirika wa Mataifa, yule hayawani-mwitu mwenye ranginyekundu-nyangavu ambaye kulingana na Ufunuo aliingia katika abiso. (Mathayo 24:15; Ufunuo 17:8; ona Light, Kitabu cha Pili, ukurasa 94.) Aliingia humo wakati Vita ya Ulimwengu 2 ilipoanza. Hata hivyo, kwenye Ulimwengu Mpya Kusanyiko la Kitheokrasi la Mashahidi wa Yehova katika 1942, Nathan H. Knorr, msimamizi wa tatu wa Watch Tower Bible and Tract Society, alizungumzia unabii wa Ufunuo 17 akaonya kwamba yule hayawani angeinuka tena kutoka katika abiso.
13 Historia ilihakikisha ukweli wa maneno yake. Kati ya Agosti na Oktoba 1944, katika Dumbarton Oaks katika United States, kazi ilianza kuhusu hati ya katiba ya lile ambalo lingeitwa Umoja wa Mataifa. Hati hiyo ya katiba ilikubaliwa na mataifa 51, kutia ndani ile iliyokuwa Muungano wa Sovieti, na ilipoanza kutenda kazi katika Oktoba 24, 1945, kwa kweli ule Ushirika wa Mataifa uliokuwa umekufa ukatoka katika abiso.
14. Utambulisho wa mfalme wa kaskazini ulibadilika lini na jinsi gani?
14 Ujerumani ilikuwa imekuwa adui mkuu wa mfalme wa kusini katika vile vita vyote viwili vya ulimwengu. Baada ya Vita ya Ulimwengu 2, sehemu ya Ujerumani ilijiunga upya na mfalme wa kusini. Lakini ile sehemu nyingine ya Ujerumani ikajiunga na milki nyingine yenye nguvu. Nchi za Kikomunisti zilizoungana, ambazo sasa zilitia ndani sehemu ya Ujerumani, zilipinga kwa nguvu ule muungano wa Uingereza na Amerika, na ule ushindani kati ya wale wafalme wawili ukawa Vita Baridi.—Ona “Your Will Be Done on Earth,” kurasa 264-84.
Mfalme na Lile Agano
15. Ni nani ‘wafanyao maovu juu ya agano,’ nao wamekuwa na uhusiano gani na mfalme wa kaskazini?
15 Sasa yule malaika asema hivi: “Wao wafanyao maovu juu ya hilo agano atawapotosha kwa maneno ya kujipendekeza.” (Danieli 11:32a) Ni nani hao wafanyao maovu juu ya hilo agano? Tena, waweza kuwa tu viongozi wa Jumuiya ya Wakristo, wanaodai kuwa Wakristo lakini kwa matendo yao hulitia unajisi jina lenyewe la Ukristo. Katika vita ya ulimwengu ya pili, “Serikali ya Sovieti ilijaribu sana kupata msaada wa kimwili na wa kiadili wa Makanisa ili kulinda bara la mama.” (Religion in the Soviet Union, cha Walter Kolarz) Baada ya vita hiyo, viongozi wa kanisa walijaribu kudumisha urafiki huo ijapokuwa ile sera ya serikali ambayo sasa ilikuwa ni mfalme wa kaskazini ya kutoamini kuwako kwa Mungu.b Hivyo, Jumuiya ya Wakristo ikawa sehemu ya huu ulimwengu zaidi ya wakati mwingine wowote—uasi-imani wenye kuchukiza machoni pa Yehova.—Yohana 17:14; Yakobo 4:4.
16, 17. Ni nani “hao walio wenye hekima,” nao wamekuwa na hali gani na mfalme wa kaskazini?
16 Lakini, namna gani Wakristo wa kweli? “Lakini watu wamjuao Mungu wao watakuwa hodari [watashinda, NW], na kutenda mambo makuu. Na hao walio wenye hekima katika watu watafundisha wengi; hata hivyo wataanguka kwa upanga, na kwa moto, na kwa kufungwa, na kwa kutekwa nyara, siku nyingi.” (Danieli 11:32b, 33) Wakristo wanaoishi chini ya mfalme wa kaskazini hawajawa sehemu ya ulimwengu, ingawa ‘wanaitii mamlaka iliyo kuu’ ifaavyo. (Warumi 13:1; Yohana 18:36) Wakiwa waangalifu kumlipa Kaisari yaliyo ya Kaisari, wao pia walimpa “Mungu yaliyo ya Mungu.” (Mathayo 22:21) Kwa sababu hiyo, uaminifu-maadili wao ulitahiniwa.—2 Timotheo 3:12.
17 Tokeo lilikuwa nini? ‘Walishinda’ na ‘kuanguka’ pia. Walianguka kwa kuwa walinyanyaswa na kuteseka sana, hata wengine wakauawa. Lakini walishinda kwa kuwa waliendelea wakiwa waaminifu, kwa sehemu kubwa. Naam, waliushinda ulimwengu, kama vile Yesu alivyoushinda ulimwengu. (Yohana 16:33) Zaidi ya hayo, hawakuacha kamwe kuhubiri, hata ikiwa walijipata wenyewe gerezani au katika kambi ya mateso. Kwa kufanya hivyo, ‘walifundisha wengi.’ Ujapokuwa mnyanyaso, katika mabara mengi yaliyotawalwa na mfalme wa kaskazini, idadi za Mashahidi wa Yehova ziliongezeka. Kwa sababu ya uaminifu wa “hao walio wenye hekima,” sehemu yenye kupanuka daima ya ule “mkutano mkubwa” imetokea katika mabara hayo.—Ufunuo 7:9-14.
18. Mabaki ya wapakwa wanaoishi chini ya mfalme wa kaskazini wamepokea “msaada kidogo” upi?
18 Akisema juu ya mnyanyaso wa watu wa Mungu, yule malaika alitabiri hivi: “Basi watakapoanguka, watasaidiwa kwa msaada kidogo.” (Danieli 11:34a) Hilo lilitukiaje? Kwanza, ushindi wa mfalme wa kusini katika vita ya ulimwengu ya pili ulitokeza kitulizo kingi sana kwa Wakristo walioishi chini ya yule mfalme mshindani. (Linganisha Ufunuo 12:15, 16.) Halafu, wale walionyanyaswa na mfalme wa kaskazini aliyefuata walipata kitulizo mara kwa mara, na ile Vita Baridi ilipoanza kumalizika, viongozi wengi walikuja kung’amua kwamba Wakristo waaminifu si tisho na hivyo wakawapa utambuzi wa kisheria.c Pia, msaada mkubwa umetokana na zile idadi zenye kuongezeka za mkutano mkubwa, za wale ambao wameitikia kule kuhubiri kwa uaminifu kwa wapakwa na kuwasaidia, kama isimuliwavyo kwenye Mathayo 25:34-40.
Kusafishwa kwa Watu wa Mungu
19. (a) Wengine ‘waliambatanaje nao kwa maneno ya kujipendekeza’? (b) Ni nini kinachomaanishwa na ule usemi “hata wakati wa mwisho”? (Ona kielezi-chini.)
19 Si wote waliodhihirisha kupendezwa katika kumtumikia Mungu wakati huo waliokuwa na madhumuni nzuri. Yule malaika alionya hivi: “Wengi wataambatana nao kwa maneno ya kujipendekeza. Na baadhi yao wenye hekima wataanguka, ili kuwatakasa, na kuwasafisha, na kuwafanya weupe, hata wakati wa mwisho; kwa maana ni kwa wakati ulioamriwa, ambao haujaja.”d (Danieli 11:34b, 35) Wengine walionyesha kupendezwa na kweli lakini hawakuwa na nia ya kujiweka wakfu kikweli kumtumikia Mungu. Wengine walioonekana kukubali habari njema kwa kweli walikuwa wapelelezi wa wale wenye mamlaka. Ripoti kutoka bara moja yasomwa hivi: “Baadhi ya watu hao wasio wanyoofu walikuwa Wakomunisti wenye kukiri kuwa hivyo waliokuwa wamepenya ndani ya tengenezo la Bwana, wakajionyesha kuwa na bidii nyingi, na hata walikuwa wamewekwa katika vyeo vya juu vya utumishi.”
20. Kwa nini Yehova aliwaruhusu Wakristo wengine waaminifu ‘waanguke’ kwa sababu ya wale wanafiki wenye kupenya ndani?
20 Hao wenye kupenya ndani walisababisha waaminifu wengine waanguke mikononi mwa wale wenye mamlaka. Kwa nini Yehova aliruhusu mambo kama hayo yatendeke? Ili kutakasa, kusafisha. Kama vile Yesu ‘alivyojifunza kutii kwa mateso yaliyompata,’ ndivyo zile nafsi zenye uaminifu zilivyojifunza uvumilivu kutokana na kutahiniwa kwa imani yao. (Waebrania 5:8; Yakobo 1:2, 3; linganisha Malaki 3:3.) Hivyo ‘wanatakaswa, kusafishwa na kufanywa weupe.’ Kushangilia kwingi kwawangoja waaminifu hao wakati ulioamriwa ufikapo ili uvumilivu wao uthawabishwe. Hilo litaonwa tuzungumziapo zaidi juu ya unabii wa Danieli.
[Maelezo ya Chini]
a Kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., na kutolewa katika Kiingereza katika 1958 kwenye “Mapenzi ya Kimungu” Kusanyiko la Kimataifa la Mashahidi wa Yehova.
b Toleo la Novemba 1992 la World Press Review lilikazia makala kutoka katika The Toronto Star iliyosema hivi: “Katika miaka kadhaa ambayo imepita, Warusi wameona njozi nyingi za historia ya nchi yao ambazo wakati mmoja hazikuweza kukanushwa, zikimumunyika mbele ya mambo ya hakika. Lakini kule kufunuliwa kwa ushirikiano wa kanisa pamoja na utawala wa kikomunisti kwawakilisha pigo lenye kudhoofisha zaidi.”
c Ona Mnara wa Mlinzi, Julai 15, 1991, kurasa 8-11.
d “Hata wakati wa mwisho” ingeweza kumaanisha “katika wakati wa mwisho.” Neno linalotafsiriwa hapa kuwa “hata” laonekana katika maandishi-awali ya Kiaramu ya Danieli 7:25 na hapo humaanisha “katika” au “kwa.” Neno hilo lina maana iyo hiyo katika maandishi-awali ya Kiebrania ya 2 Wafalme 9:22, Ayubu 20:5, na Waamuzi 3:26. Hata hivyo, katika tafsiri nyingi za Danieli 11:35, linafasiriwa “hata,” na ikiwa huo ndio uelewevu sahihi, basi ni lazima “wakati wa mwisho” hapa uwe wakati wa mwisho wa uvumilivu wa watu wa Mungu.—Linganisha “Your Will Be Done on Earth,” ukurasa 286.
Je! Wakumbuka?
◻ Kwa nini sisi leo tutazamie kuwa na uelewevu wa wazi zaidi juu ya unabii wa Danieli?
◻ Mfalme wa kaskazini ‘alighadhibikaje na kutenda kwa mafanikio’?
◻ Kutokea tena kwa lile “chukizo” kulionwaje kimbele na jamii ya mtumwa?
◻ Ni jinsi gani mabaki ya wapakwa ‘walianguka, wakashinda, na kupokea msaada kidogo’?
[Picha katika ukurasa wa 15]
Chini ya Hitler, mfalme wa kaskazini alipona kabisa kutoka katika ushinde wake wa 1918 mikononi mwa mfalme wa kusini
[Picha katika ukurasa wa 16]
Viongozi wa Jumuiya ya Wakristo walijaribu kusitawisha uhusiano na mfalme wa kaskazini
[Hisani]
Zoran/Sipa Press