Simba—“Paka” Wenye Manyoya na Wenye Fahari wa Afrika
NA MLETA-HABARI WA “AMKENI!” KATIKA KENYA
NI WAKATI wa mapambazuko katika Tambarare za Serengeti zilizoko Afrika. Katika hewa tulivu ya asubuhi, sisi tumo ndani ya gari letu aina ya Land Rover na twalitazama kundi la simba-majike na watoto wao. Ngozi zao za rangi ya kahawia-njano ni laini, zenye kung’aa na ni za kidhahabu, zikipatana kwa umaridadi na ile nyasi ndefu iliyokauka. Watoto hao wachanga ni wenye machachari na wana nguvu nyingi. Wanaruka na kucheza wakiizunguka miili mikubwa ya majike, wasiojali vitendo vyao vya kuchekesha.
Kwa ghafula kundi hilo latulia. Macho yote yageuzwa, yakikazwa kuelekea mbali. Kutoka mahali petu pa kutazamia palipoinuka, twafuatilia mwelekeo wa macho yao nasi twatambua kile ambacho macho yao yanalenga. Nuru ya alfajiri yafunua umbo lenye fahari la simba-dume mkubwa. Macho yetu na yake yakutana anapotukazia macho. Twaanza kutetemeka, si kutokana na baridi ya asubuhi, bali kwa kutambua kuwa sisi ndio anaotazama. Anaonekana mwenye kutia hofu, na maridadi vilevile. Manyoya mengi mno ya kidhahabu yenye mistari myeusi hukipa kichwa chake kikubwa umbo. Macho yake makubwa yana rangi ya kaharabu na yako chonjo. Hata hivyo, familia yake yavuta uangalifu wake, naye awageuzia macho yake kwa utaratibu na kuwaendea.
Hatua zake ni za madaha, naam, za kifalme. Bila kututupia jicho mara ya pili, yeye apita karibu sana mbele ya gari letu na kuwaendea wale majike na watoto wao. Wote wainuka ili kumlaki na, mmoja baada ya mwingine, wasukumiza nyuso zao dhidi ya domo lake kakamavu kwa kufuata mtindo wa jamii ya paka wa kuamkiana kwa kusuguana mashavu. Linapoingia katikati ya kundi, hilo dume lajibwaga chini kana kwamba limechoka kwa kutembea nalo lajibingirisha kwa mgongo. Wengine wanauiga uchovu wake, na punde si punde kundi lote lalala usingizi wa kijuujuu katika miali ya kwanza ya jua la asubuhi lenye kuchangamsha. Mbele yetu twaona picha ya amani na uradhi iliyofanyizwa katikati ya nyasi za kidhahabu, zenye kupulizwa na upepo za tambarare hiyo iliyo wazi.
Kiumbe Mwenye Kupendeza na Kuvutia Sana
Labda hakuna mnyama ambaye ameyasisimua mawazo ya mwanadamu kuliko simba. Zamani sana, wasanii Waafrika walipamba sehemu za juu za miamba kwa mifano ya simba wakiwinda. Majumba ya kifalme na mahekalu ya kale yalipambwa kwa sanamu za mawe za simba waliojaa manyoya. Leo, watu huenda kwa wingi kwenye bustani za wanyama ili kujionea wanyama hao wa jamii ya paka wenye kuvutia. Simba ametukuzwa katika vitabu na sinema, kama ile ya Born Free, ambayo ni masimulizi halisi juu ya mtoto wa simba aliyeachwa yatima, akatunzwa na binadamu, baadaye akaachwa huru kwenda mbugani. Vilevile katika hadithi—ambazo kwa sehemu ni hekaya, na kwa sehemu zina ukweli fulani—simba amelaumiwa kuwa mla-watu mwovu. Si ajabu kwamba simba huonwa kuwa kiumbe mwenye kuvutia sana!
Simba waweza kuwa wakali sana na, mara kwa mara, waanana na wenye kucheza-cheza kama watoto wa paka. Wao hukoroma kimya-kimya wanaporidhika ingawa wanaweza kutoa mngurumo mkubwa sana ambao husikika umbali wa kilometa nane. Nyakati nyingine wao huonekana kuwa wazembe na wenye uchovu, lakini wanaweza kwenda kwa kasi ya kushangaza. Mwanadamu amempa simba sifa ya daima kwa ajili ya ushujaa wake, naye humfananisha mtu aliye jasiri na simba.
Simba—Mnyama wa Jamii ya Paka Mwenye Ujamii
Simba ni baadhi ya wanyama wa jamii ya paka wanaopenda ujamii zaidi. Hali yao inakuwa njema wakiwa katika makundi ya kifamilia, ambayo yaweza kuwa na idadi ya kuanzia washiriki wachache tu hadi kufikia zaidi ya 30. Kundi la simba hufanyizwa na kikundi cha simba-majike ambao huenda wakawa wa jamaa za karibu. Wao huishi, huwinda, na kuzaa pamoja. Uhusiano huu wa karibu, ambao huenda ukadumu maisha yao yote, huandaa msingi wa familia ya simba na huisaidia isiangamie.
Kila kundi la simba lina dume moja au zaidi la simba waliokomaa ambao hushika doria na kutia alama mipaka ya eneo la kundi hilo la simba. Kutoka kwenye ncha ya pua lao jeusi hadi sehemu ya mwisho ya mikia yao yenye manyoya, hayawani hawa wenye fahari waweza kufikia urefu wa zaidi ya meta tatu, na uzito wa zaidi ya kilogramu 225. Ingawa madume ndio hutawala kundi, ni majike ndio huongoza. Kwa kawaida simba-majike ndio huanzisha utendaji, kama kwenda kwenye kivuli au kuanza kuwinda.
Kwa kawaida simba-majike huzaa mara moja kwa miaka miwili. Simba wachanga huzaliwa wakiwa wasiojiweza kabisa. Kulea simba wachanga ni kazi ya jumuiya nzima, nao majike huwahami na kuwanyonyesha wachanga walio katika kundi. Watoto hukua haraka; wanapofikia umri wa miezi miwili, tayari huwa wanakimbia na kucheza. Huangukiana wenyewe kama watoto wa paka, hupigana mwereka, hurukia wenzao, na huruka huku na huku katika nyasi ndefu. Wao huvutiwa sana na chochote ambacho husongea nao hurukia vipepeo, hukimbiza wadudu, na kupigana mwereka na vijiti na pia miti. Watoto hao hawawezi kujizuia wasicheze na mkia wa mama yao ambao yeye huupiga huku na huku, akiwashawishi wauchezee.
Kila kundi la simba huishi katika eneo lenye mipaka dhahiri na ambalo laweza kuwa na ukubwa wa eka nyingi sana. Simba hupendelea maeneo yaliyoinuka yenye maji mengi na kivuli kinachowakinga kutokana na jua kali la adhuhuri. Huko wao huishi miongoni mwa ndovu, twiga, nyati, na wanyama wengine wanaoishi katika maeneo tambarare. Maisha ya simba hugawanywa baina ya kulala usingizi kwa muda wa saa nyingi na vipindi vifupi vya kuwinda na kupandana. Ukweli ni kwamba, simba wanaweza kuonwa wakipumzika, wakilala, au wakikaa kwa muda wa saa 20 kwa siku, jambo linaloshangaza. Wakiwa usingizini, huonekana wenye amani na wasio wakali. Hata hivyo, usidanganyike—simba ni mmoja wa hayawani-mwitu walio wakali zaidi!
Mwindaji
Jioni-jioni, mbuga iliyokaushwa kwa jua yaanza kupoa. Hao simba-majike watatu tunaowatazama sasa wanaanza kuamka kutoka usingizi wao wa adhuhuri. Njaa yawafanya “paka” hao waanze kutembea huku na huku, wakinusanusa hewa huku wakitazama ng’ambo ya mbuga inayozidi kuwa manjano. Sasa ni kilele cha kuhama kwa kongoni, na maelfu ya paa hao wasio na sura ya kuvutia wanajilisha kwa utulivu upande wa kusini kutoka mahali tulipo. Hao “paka” watatu sasa wanaelekea upande huo. Wanajigawanya kwa eneo kubwa, nao wananyemelea kwa mwendo laini kupitia eneo hilo lenye mashimo-shimo. Hao “paka” wenye rangi ya kahawia-njano wanatokomea ndani ya nyasi ndefu nao wanalikaribia hilo kundi la wanyama wasioshuku lolote kwa ukaribu upatao meta 30. Ndipo “paka” hao wanaamua kutenda. Kwa mwendo wa kasi mno, wao waingia ndani ya kundi hilo la kongoni waliotaharuki. Kundi hilo latimka kuelekea pande zote, viumbe hao walioshikwa na hofu wakikimbia ili kuokoa uhai wao. Mamia ya kwato zinazokimbia zaiponda ardhi, zikitifua wingu la vumbi jekundu. Vumbi linapopungua, twawaona hao simba-majike watatu wamesimama peke yao, wakihema kwa nguvu. Windo lao limewahepa. Labda watafaulu kupata fursa nyingine ya kuwinda usiku huu, au huenda wasipate. Ijapokuwa ni wepesi na hukimbia kasi sana, simba hufaulu tu kwa asilimia 30 kila mara wawindapo. Hivyo njaa ni moja ya vitisho vikubwa ambavyo simba hukabili.
Nguvu za simba aliyekomaa ni zenye kutokeza. Wakiwinda wakiwa kundi, hao wameonekana wakiangusha na kuua wanyama wenye uzani unaozidi kilogramu 1,300. Simba hufikia mwendo wa kilometa 59 kwa saa wanapoanza kukimbiza windo, lakini hawawezi kuendelea na kasi hiyo kwa muda mrefu. Kwa sababu hiyo, wao hutumia mbinu za kunyemelea na kuvamia ili kujipatia chakula. Simba-majike huua asilimia 90 ya mawindo, hata hivyo wenye kupata sehemu kubwa ya chakula hicho ni madume. Windo linapokuwa haba, nyakati nyingine simba wanakuwa na njaa sana hivi kwamba wanawafukuza watoto wao wasile nyama.
Anayewindwa
Zamani za kale simba mwenye fahari alitembea-tembea sehemu zote za bara la Afrika na pia sehemu kadhaa za Asia, Ulaya, India, na Palestina. Kwa sababu yeye ni mwindaji, simba hushindana na mwanadamu. Kwa kuwa alitisha mifugo na kuwadhuru watu, simba akawa kiumbe wa kupigwa risasi mara tu aonekanapo. Idadi ya watu inayoongezeka haraka imeyapunguza sana makazi ya simba. Leo, nje ya Afrika, kuna mamia machache tu ya simba wanaoishi porini. Siku zetu simba wanakuwa salama kutoka kwa mwanadamu ikiwa tu wamo katika maeneo yanayolindwa na mbuga za kuhifadhi wanyama.
Kwa furaha, kuna mabadiliko yatakayomjia huyu hayawani mwenye fahari. Biblia huufafanua wakati ujao ambapo simba ataishi kwa amani na wanadamu. (Isaya 11:6-9) Muumba wetu mwenye upendo karibuni atalifanya jambo hili litimie. Wakati huo “paka” mwenye manyoya mengi na fahari wa Afrika ataishi kwa upatano na amani pamoja na uumbaji mwingine wote.
[Sanduku katika ukurasa wa 19]
Simba ANGURUMAPO
SIMBA wanajulikana kwa uwezo wao wa kipekee wa kuvumisha mngurumo mkubwa ambao waweza kusikika umbali wa kilometa nyingi. Mngurumo wa simba umeonwa kuwa moja ya “sauti za asili zenye kuvutia zaidi.” Kwa kawaida simba hunguruma saa za giza na kunapopambazuka. Madume kwa majike hunguruma, na nyakati nyingine kundi lote la simba hutoa sauti za pamoja katika mngurumo wa umoja.
Wanasayansi wanaowachunguza simba wadokeza kuwa kunguruma hutimiza mambo kadhaa. Madume hunguruma ili kufahamisha wengine mipaka ya maeneo yao na, kama wonyesho wa uchokozi, ili kuwaonya simba-madume wengine ambao huenda wakaingia maeneo yao. Kwa kufaa, Biblia iliwarejezea watawala Waashuri na Wababiloni waliokuwa wachokozi, wenye kiburi, na wenye pupa kuwa “wana-simba” wanaonguruma ambao waliwapinga kijeuri na kuwaangamiza watu wa Mungu.—Isaya 5:29; Yeremia 50:17.
Kunguruma huwasaidia washiriki wa kundi moja la simba kupatana tena ikiwa umbali au giza vimewatenganisha. Baada ya kuua windo, kutoa sauti kwa njia hii huwafahamisha washiriki wengineo wa kundi hilo la simba juu ya mahali palipo mlo. Ikiirejezea tabia hii, Biblia yasema: “Mwana-simba atalia pangoni mwake, ikiwa hakupata kitu?”—Amosi 3:4.
Kwa kushangaza, wanapowawinda wanyama wa mwituni, simba hawatumii ngurumo kama mbinu ya kushtua windo. Katika kitabu chake The Behavior Guide to African Mammals, Richard Estes asema kwamba “hakuna chochote kinachoonyesha kuwa simba hunguruma kimakusudi ili kuwaingiza wanyama wanaowindwa katika mtego wa kuzingirwa (kwa yale niliyojionea wanyama ambao huwindwa na simba kwa kawaida hupuuza mingurumo ya simba).”
Kwa nini, basi, Biblia humrejezea Shetani kama ‘simba angurumaye akitafuta sana kumnyafua mtu fulani’? (1 Petro 5:8) Ingawa wanyama wa mwituni huonekana kama wasioogopeshwa na mngurumo wa simba, hali ni tofauti inapomhusu mwanadamu na mifugo yake. Ile sauti ya mngurumo wa simba inayotisha, ikitoa mwangwi katika giza la usiku, ingemwogopesha na kumtisha yeyote asiyelindwa salama ndani ya nyumba iliyofungwa milango. Zamani sana ilisemwa kwa usahihi hivi: “Simba amekwisha kunguruma, ni nani asiyeogopa?”—Amosi 3:8.
Shetani ni stadi wa kutumia woga ili kufanya watu wamtii. Kwa uzuri, watu wa Mungu wana rafiki mwenye nguvu. Wakiwa na imani yenye nguvu katika utegemezo wa Yehova, wao waweza kumkinza kwa mafanikio huyu “simba [mwenye nguvu] anayenguruma.” Wakristo wanatiwa moyo ‘kuchukua msimamo wao dhidi yake, wakiwa thabiti katika imani.’—1 Petro 5:9.