Tamasha za Kutoka Bara Lililoahidiwa
Yafa Bandari ya Kale Yenye Sifa
ISRAELI YA KALE ilikuwa na pwani ndefu yenye mchanga mwingi. Hata hivyo Waisraeli hawakujulikana hasa kuwa mabaharia. Huenda kisababishi kilikuwa namna pwani yao ilivyokuwa.
Ilikaribia kuwa kama ufuo na pwani yenye miinuko isiyosumbuliwa-sumbuliwa, iliyofanyizwa kwa mchanga uliopelekwa baharini na Mto Nailo.a Kama ungekuwa umesafiri merikebuni kuipita kutoka mpaka wa Misri, hungepata bandari yenye kutokeza sana kiasili kusini mwa Mlima Karmeli.
Lakini katikati hivi mwa pwani ya Israeli ungeona jiji la Yafa kwenye kilima. Kama picha inavyoonyesha, mlolongo wa miamba iliyo majini karibu na pwani ulifanyiza ghuba ndogo. Ingawa bandari iliyotokezwa ilikuwa ndogo kuliko ile iliyokuwa kaskazini kidogo mwa Acre (Ptolemais), bado ilifanya Yafa iwe yenye sifa. (Matendo 21:7) Mpaka Herode Mkubwa alipojenga bandari isiyo ya asili ya Kaisaria, Yafa palikuwa ndipo mahali bora pa meli kutia gudi kando ya pwani. Jambo hili linadhihirisha marejezo fulani ya Biblia kuhusu Yafa.
Alipokuwa akijitoa ili amsaidie Sulemani kujenga hekalu, Hiramu mfalme wa Tiro alisema: “Sisi tutakuletea wewe [miti kutoka Lebanoni] ikiwa kama vyelezo baharini mpaka Yafa, na wewe kwa upande wako utaipandisha juu Yerusalemu.” (2 Nyakati 2:1, 11, 16, NW) Huenda ikawa vyelezo hivyo viliondoka katika bandari za Kifoinike za Tiro au Sidoni. (Isaya 23:1, 2; Ezekieli 27:8, 9) Vikipitia Karmeli, vyelezo vya mierezi viliteremshwa Yafa. Kutoka huko mierezi hiyo ingeweza kupelekwa Yerusalemu, kilometa 55 mashariki/kusini mashariki. Pia Yafa ilikuwa bandari ya kutia gudi kwa mbao za mierezi wakati Wayahudi walipolijenga upya hekalu baada ya utekwa.—Ezra 3:7.
Labda wafanya kazi walioandamana na mbao hizo walisafiri katika meli za Kifoinike, sawa na kiolezo hiki. Unapolichunguza, kumbuka kwamba baada ya Yehova kumpa Yona mgawo wa kwenda Ninawi, mnabii huyo alitorokea upande mwingine. “[Yona] akatelemka hata Yafa, akaona merikebu inayokwenda Tarshishi; basi, akatoa nauli, akapanda merikebuni, aende pamoja nao Tarshishi, ajiepushe na uso wa Bwana [Yehova, NW].”—Yona 1:1-3.
Inaonekana kwamba Yona alipanda aina hii ya meli ya shehena iliyokuwa na hali nzuri kustahili kusafiri baharini, nayo ingeiweza ile safari ndefu ya kutoka Yafa kwenda Tarshishi (ambayo yaelekea ilikuwa Hispania ya kale). Labda ilikuwa na omo iliyoinuka na kupindika, ambayo karibu nayo palining’inia nanga ya jiwe. Wasafiri, wapiga makasia, na mizigo fulani ingeweza kutoshea kwenye sitaha, ambayo haionyeshwi katika kiolezo hiki. Kulikuwa na ngama chini ya sitaha, ambako mizigo zaidi ilikuwa ikiwekwa na ambako Yona alilala. Meli hiyo ilikuwa imetengenezwa kwa mbao madhubuti za msunobari na ilikuwa na mlingoti mmoja wa mwerezi wa kutegemeza tanga kubwa la kitani. Angalia kwamba kila upande una mstari wa makasia marefu (labda ya mti Ulaya kutoka Bashani). Sasa wazia meli hiyo ikiwa baharini na ikiwa inatishwa na dhoruba kali. Wasikie wale mabaharia wakiipaazia sauti miungu yao ili iwasaidie mpaka hatimaye wanalazimika kumtupa Yona baharini ili wao wenyewe wasiangamie. —Ezekieli 27:5-9; Yona 1:4-15.
Yafa ya karne ya kwanza ilikuwa makao ya kundi la Wakristo, ambao wengine wao huenda wakawa walikuwa wafanya kazi katika gudi au mabaharia zamani. Mshiriki wa kundi hili la bandarini lenye shughuli nyingi alikuwa Mwanamke Myahudi Dorkasi (Tabitha). “Mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa.” Katika mwaka 36 W.K., Dorkasi alishikwa na ugonjwa akafa, na jambo hilo likafanya wengi sana walie wakizikumbuka kazi zake nyingi zilizo nzuri. Wakristo wenzi walimleta mtume Petro kutoka Lida (Lod ya ki-siku-hizi, karibu na uwanja wa ndege wa Tel Aviv) mpaka Yafa. Petro alimfufua dada huyu mpendwa, muujiza ambao ‘ulijulikana katika mji mzima wa Yafa; watu wengi wakamwamini Bwana.”—Matendo 9:36-42.
Petro alikaa Yafa kwa muda katika nyumba ya Simoni, mtengeneza ngozi. Mtume alipata njozi hapa iliyomwongoza achukue ndugu fulani wa kundi la Yafa kwenda nao kaskazini katika barabara ya pwani kwenye bandari mpya ya Kaisaria. Akiwa huko Petro alimhubiri na kumbatiza Kornelio ofisa wa jeshi la Roma, mtu wa kwanza asiye Myahudi asiyetahiriwa kuwa Mkristo mpakwa-mafuta kwa roho. (Matendo 9:43–10:48) Lo, lazima kuwe kulitokea shangwe na msisimuko ulioje katika Yafa wakati akina ndugu walirudi wakiwa na habari za ukuzi huu wenye maana katika historia ya Kikristo!
Leo wageni wengi huzuru Yafa, ambayo ni sehemu ya Tel Aviv-Jaffa, na kwa urahisi wanaweza kukumbuka matukio ya Kibiblia yaliyotukia kwenye bandari hii yenye sifa.
[Maelezo ya Chini]
a Unaweza kuona pwani hii yenye mchanga mwingi kwa urahisi katika picha ya satelaiti katika jalada la 1989 Calendar of Jehovah’s Witnesses. Kalenda hii pia inaandaa picha kubwa zaidi ya mandhari ya Yafa iliyo juu.
[Hisani ya picha katika ukurasa wa 16]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.