Yona Ajifunza Juu ya Rehema ya Yehova
YEHOVA ana mgawo kwa ajili ya nabii wake Yona. Wakati ni karne ya tisa K.W.K., na Yeroboamu 2 atawala katika Israeli. Yona atoka Gath-heferi, jiji la Wazebuloni. (Yoshua 19:10, 13; 2 Wafalme 14:25) Mungu amtuma Yona kwenda Ninawi, jiji kuu la Ashuru, lililo umbali wa zaidi ya kilometa 800 kaskazini-mashariki mwa mji wake wa nyumbani. Apaswa kuwaonya Waninawi kuwa wao wakabili uharibifu kutoka kwa Mungu.
Huenda Yona akawa alifikiri: ‘Niende jiji hilo na taifa hilo? Wao hata hawajajitoa kwa Mungu? Waashuri hao wenye tamaa ya kumwaga damu hawakufanya agano na Yehova kamwe kama walivyofanya Waisraeli. Huenda hata watu wa taifa hilo wakauona ujumbe wangu kuwa tisho na wapate ushindi wa kivita dhidi ya Israeli! Si mimi! Sitaenda. Nitakimbilia Yafa na kusafiri kwa merikebu kuelekea upande tofauti—kuelekea Tarshishi, hadi mwisho ule mwingine wa Bahari Kuu. Hilo ndilo nitakalofanya!’—Yona 1:1-3.
Hatari Baharini!
Upesi Yona yuko Yafa kwenye ufuo wa Mediterania. Alipa nauli na kuingia kwenye merikebu ielekeayo Tarshishi, ambayo kwa kawaida huonwa kuwa Hispania, zaidi ya kilometa 3,500 magharibi mwa Ninawi. Mara waanzapo safari, huyo nabii mchovu ashuka hata pande za ndani za merikebu na kulala. Kabla ya muda mrefu, Yehova avumisha upepo mkubwa baharini, na kila baharia mwenye hofu alilia mungu wake amsaidie. Hiyo merikebu yabingirika na kutupwatupwa hivi kwamba mizigo yatupwa baharini ili kuifanya iwe nyepesi. Hata hivyo kuvunjika kwa merikebu ni dhahiri, naye Yona amsikia nahodha akisema: “Una nini, Ewe ulalaye usingizi? amka, ukamwombe Mungu wako; labda Mungu huyo atatukumbuka, tusipotee.” Yona ainuka na kwenda kwenye jukwaa la merikebu.—Yona 1:4-6.
“Haya, na mpige kura,” wasema mabaharia, “mpate kujua mabaya haya yametupata kwa sababu ya nani.” Kura ikamwangukia Yona. Wazia wasiwasi wake mabaharia wamuulizapo: “Tafadhali utuambie, wewe ambaye mabaya haya yametupata kwa sababu yako; kazi yako ni kazi gani? nawe umetoka wapi? nchi yako ni nchi ipi? nawe u mtu wa kabila gani?” Yona asema kuwa yeye ni Mwebrania anayemwabudu “BWANA [“Yehova,” NW], Mungu wa mbingu” na kuwa ana hofu yenye kicho kwa “aliyeziumba bahari na nchi kavu.” Dhoruba imewajia kwa kuwa anakimbia kutoka kwa kuwapo kwa Yehova badala ya kupeleka ujumbe wa Mungu Ninawi kwa utii.—Yona 1:7-10.
Mabaharia wauliza: “Tukutende nini, ili bahari itulie?” Bahari izidipo kuchafuka, Yona asema: “Nikamateni, mnitupe baharini; basi bahari itatulia; kwa maana najua ya kuwa ni kwa ajili yangu tufani hii imewapata.” Bila kutaka kumtupa mtumishi wa Yehova baharini apatwe na kifo, hao watu wajaribu kurudi pwani. Kwa kukosa mafanikio mabaharia hao walia hivi: “Twakuomba, Ee BWANA [“Yehova,” NW], twakuomba, tusiangamie kwa ajili ya uhai wa mtu huyu, wala usitupatilize kwa ajili ya damu isiyo na hatia; kwa maana wewe, BWANA [“Yehova,” NW], umefanya kama ulivyopenda.”—Yona 1:11-14.
Baharini!
Basi, hao mabaharia wamtupa Yona baharini. Azamapo kwenye bahari iliyochafuka, bahari yaanza kutulia. Waonapo hilo, ‘watu hao waanza kumwogopa Yehova mno, wanamtolea Yehova sadaka, na kuweka nadhiri.’—Yona 1:15, 16.
Maji yamfunikapo Yona, bila shaka yeye atoa sala. Kisha ahisi akiteremkia mahali laini akiteleza na kuingia sehemu kubwa zaidi. Ajabu ni kwamba bado aweza kupumua! Akiondoa mwani kichwani mwake, Yona ajikuta akiwa mahali pa kipekee kabisa. Hilo ni kwa sababu ‘BWANA aliweka tayari samaki mkubwa ili ammeze Yona, naye Yona akawa ndani ya tumbo la samaki yule muda wa siku tatu, mchana na usiku.’—Yona 1:17.
Sala ya Yona Yenye Hisia Nyingi
Akiwa tumboni mwa samaki mkubwa, Yona apata wakati wa kusali. Baadhi ya maneno yake hufanana na zaburi kadhaa. Yona baadaye alirekodi sala zake zenye kuonyesha kukata tumaini na kujuta. Kwa kielelezo, yeye aliona kuwa tumbo la samaki lingekuwa Sheoli, kaburi lake. Hivyo aliomba: “Nalimlilia BWANA kwa sababu ya shida yangu, naye akaniitikia; katika tumbo la kuzimu [“Sheoli,” NW] naliomba, nawe ukasikia sauti yangu.” (Yona 2:1, 2) Nyimbo Mbili za Mikweo—huenda zilizoimbwa na Waisraeli waliokuwa wakienda Yerusalemu kwa ajili ya misherehekeo—huonyesha mawazo ayo hayo.—Zaburi 120:1; 130:1, 2.
Akitafakari juu ya kutupwa kwake baharini, Yona asali: “Maana [wewe Yehova] ulinitupa vilindini, ndani ya moyo [katikati ya] wa bahari; gharika ya maji ikanizunguka pande zote; mawimbi yako yote na gharika zako zote zimepita juu yangu.”—Yona 2:3; linganisha Zaburi 42:7; 69:2.
Yona ahofu kuwa kukosa kutii kwake kutampotezea kibali cha Mungu na kuwa hatapata tena kuliona hekalu la Mungu. Yeye asali: “Nami nikasema, Nimetupwa mbali na macho yako; lakini nitatazama [“nitawezaje kutazama,” NW] tena kukabili hekalu lako takatifu.” (Yona 2:4; linganisha Zaburi 31:22.) Hali ya Yona yaonekana kuwa mbaya sana hivi kwamba asema: “Maji yalinizunguka, hata nafsini mwangu [yakihatarisha uhai wake]; vilindi vilinizunguka; mwani [uliokuwa baharini] ulikizinga kichwa changu.” (Yona 2:5; linganisha Zaburi 69:1.) Wazia hali ya Yona, kwa kuwa yeye aongeza: “Nalishuka hata pande za chini za milima [ndani ya samaki]; hiyo nchi na mapingo yake [kama yale ya kaburi] yalinifunga hata milele; lakini umeipandisha nafsi yangu kutoka shimoni [katika siku ya tatu], Ee BWANA, Mungu wangu.”—Yona 2:6; linganisha Zaburi 30:3.
Ingawa angali ndani ya tumbo la samaki, Yona hafikiri hivi: ‘Nimeshuka moyo sana hivi kwamba siwezi kusali.’ Badala ya hilo, yeye asali: “Roho yangu ilipozimia ndani yangu [karibu kufa], nalimkumbuka BWANA [katika imani, akiwa Mmoja asiyelinganika katika nguvu na rehema]; maombi yangu yakakuwasilia katika hekalu lako takatifu.” (Yona 2:7) Kutoka hekalu la kimbingu, Mungu alimsikia Yona na kumwokoa.
Kwa kumalizia Yona asali: “Watu waangaliao mambo ya ubatili na uongo [kwa kutumainia mifano isiyo na uhai ya miungu isiyo ya kweli] hujitenga na rehema zao wenyewe [kwa kumwacha Mmoja aonyeshaye sifa hiyo]; lakini mimi nitakutolea sadaka [Yehova Mungu] kwa sauti ya shukrani; nitaziondoa nadhiri zangu [za wakati huu au katika pindi nyingine]. Wokovu hutoka kwa BWANA.” (Yona 2:8, 9; linganisha Zaburi 31:6; 50:14.) Akijua kuwa ni Mungu pekee awezaye kumwokoa na mauti, huyo nabii mwenye kutubu (sawa na Wafalme Daudi na Sulemani waliomtangulia) amhesabia Yehova wokovu.—Zaburi 3:8; Mithali 21:31.
Yona Atii
Baada ya kufikiri sana na kutoa sala yenye bidii, Yona ahisi akisukumwa nje kupitia kijia kilekile alichoingilia. Hatimaye, atapikwa kwenye nchi kavu. (Yona 2:10) Akiwa mwenye shukrani kwa ajili ya ukombozi, Yona atii neno la Mungu: “Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa; ukaihubiri habari nitakayokuamuru.” (Yona 3:1, 2) Yona aanza safari kuelekea jiji kuu la Ashuru. Ajuapo siku hiyo ni siku gani atambua kuwa alikuwa katika tumbo la samaki kwa siku tatu. Huyo nabii avuka Mto Frati kwenye mpindo wao mkuu wa magharibi, asafiri kuelekea mashariki kupitia kaskazini mwa Mesopotamia, afika kwenye Mto Tigri, na mwishowe kufika kwenye lile jiji kuu.—Yona 3:3.
Yona aingia Ninawi, jiji kubwa. Atembea kwa siku moja halafu atangaza: “Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa.” Je, Yona amepata ujuzi wa lugha ya Kiashuri kimuujiza? Hatuambiwi. Lakini hata ikiwa aongea kwa Kiebrania na mwingine atafsiri, upigaji mbiu wake una matokeo. Watu wa Ninawi waanza kuweka imani kwa Mungu. Wao wapiga mbiu kuwepo kwa mfungo na wajifunika nguo za magunia, kuanzia aliye mkubwa kupita wote hadi aliye mdogo kupita wote. Hilo neno limfikiapo mfalme wa Ninawi, ainuka toka kiti chake cha ufalme, atoa mavazi yake rasmi, ajifunika kwa nguo za magunia, na kuketi kwenye majivu.—Yona 3:4-6.
Yona ashangaa jinsi gani! Mfalme Mwashuri atuma watangazaji wakiwa na tangazo: “Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng’ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe?”—Yona 3:7-9.
Waninawi watenda kulingana na mwito wa mfalme. Mungu aonapo kuwa wamegeuka kutoka kwa njia yao mbaya, aghairi juu ya lile angamizo ambalo alisema angewaletea, naye aacha kulileta. (Yona 3:10) Kwa sababu ya toba, unyenyekevu, na imani yao, Yehova aamua kutowahukumu alivyokusudia.
Nabii Aliyenuna
Siku 40 zapita na hakuna lolote linalolipata Ninawi. (Yona 3:4) Akitambua kuwa Waninawi hawataharibiwa, Yona achukizwa sana na kukasirika sana halafu aomba: “Nakuomba, Ee BWANA; sivyo hivyo nilivyosema, hapo nilipokuwa katika nchi yangu? Hii ndiyo sababu nalifanya haraka kukimbilia Tarshishi; kwa maana nalijua ya kuwa wewe u Mungu mwenye neema, umejaa huruma, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, nawe waghairi mabaya. Basi, sasa, Ee BWANA, nakuomba, uniondolee uhai wangu; maana ni afadhali nife mimi kuliko kuishi.” Mungu ajibu kwa kuuliza: “Je, unatenda vema kukasirika?”—Yona 4:1-4.
Baada ya hayo, Yona atembea kwa hasira kuondoka huo mji. Akielekea mashariki ajitengenezea kibanda ili aketi chini ya kivuli chacho hata aonapo litakalolipata hilo jiji. Kisha Yehova kwa sababu ya huruma ‘aweka tayari mtango, aufanya ukue juu ya Yona, ili uwe kivuli juu ya kichwa chake, na kumponya katika hali yake mbaya.’ Jinsi Yona aufurahiavyo huo mtango! Lakini Mungu apanga buu liushambulie huo mmea kwenye mapambazuko, nao waanza kunyauka. Upesi umekauka kabisa. Mungu pia aweka tayari upepo wa mashariki wenye joto. Jua sasa lamchoma nabii kichwani, hivi kwamba azimia. Aendelea kujiombea kifo. Ndiyo, Yona asema kwa kurudia-rudia: “Ni afadhali nife mimi kuliko kuishi.”—Yona 4:5-8.
Yehova sasa anena. Amuuliza Yona: “Je! unatenda vema kukasirika kwa ajili ya mtango?” Yona ajibu: “Ndiyo, natenda vema kukasirika hata kufa.” Kimsingi, Yehova sasa amwambia nabii: “Umeuhurumia mtango, ambao hukuufanyia kazi, wala kuuotesha; uliomea katika usiku mmoja, na kuangamia katika usiku mmoja.” Mungu akaendelea kusababu: “Na mimi, je! haikunipasa kuuhurumia Ninawi, mji ule mkubwa; ambao ndani yake wamo watu zaidi ya mia na ishirini elfu, wasioweza kupambanua katika mkono wao wa kulia na mkono wao wa kushoto; tena wamo wanyama wa kufugwa wengi sana?” (Yona 4:9-11) Jibu sahihi ni wazi.
Yona atubu na kuendelea kuishi mpaka aandika kitabu cha Biblia chenye jina lake. Alijuaje kuwa mabaharia walimhofu Yehova, wakamtolea sadaka, na kuweka nadhiri? Kwa upulizio wa Mungu au huenda hekaluni kutoka kwa mmoja wa mabaharia au abiria.—Yona 1:16; 2:4.
“Ishara ya Nabii Yona”
Waandishi na Mafarisayo walipomuuliza Yesu Kristo awaonyeshe ishara, yeye alisema: “Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona.” Yesu akaongezea: “Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi.” (Mathayo 12:38-40) Siku za Kiyahudi zilianza kwenye mshuko-jua. Kristo alikufa Ijumaa alasiri, Nisani 14, 33 W.K. Mwili wake uliwekwa kaburini kabla ya jua kutua siku hiyo. Nisani 15 ilianza jioni hiyo na kuendelea hadi mshuko-jua wa Jumamosi, siku ya saba na ya mwisho ya juma. Wakati huo Nisani 16 ilianza na kuendelea hadi kutua kwa jua kwenye ile siku tuiitayo Jumapili. Hivyo, Yesu alikuwa mfu kaburini angalau kwa kipindi fulani cha wakati cha siku ya Nisani 14, alikuwa kaburini siku nzima ya Nisani 15, na kukaa kaburini wakati wa saa za usiku za Nisani 16. Wanawake fulani walipokuja kaburini asubuhi ya Jumapili, alikuwa tayari amefufuliwa.—Mathayo 27:57-61; 28:1-7.
Yesu alikuwa kaburini kwa sehemu za siku tatu. Hivyo adui zake wakapata “ishara ya nabii Yona,” lakini Kristo akasema: “Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, nao watawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona; na hapa yupo aliye mkuu kuliko Yona.” (Mathayo 12:41) Kweli ilioje! Wayahudi walikuwa na Yesu Kristo miongoni mwao—nabii aliye mkubwa sana kuliko Yona. Ingawa Yona alikuwa ishara ya kutosha kwa Waninawi, Yesu alihubiri akiwa na mamlaka kuu zaidi na uthibitisho wa kumuunga mkono kuliko alivyofanya nabii huyo. Hata hivyo, Wayahudi kwa ujumla hawakuamini.—Yohana 4:48.
Wakiwa taifa Wayahudi hawakumkubali kwa unyenyekevu Nabii mkubwa zaidi ya Yona, nao hawakudhihirisha imani katika Yeye. Lakini namna gani babu zao wa kale? Wao pia hawakuwa na imani na roho ya unyenyekevu. Kwa hakika, yaonekana Yehova alimtuma Yona aende Ninawi ili kuonyesha tofauti kati ya Waninawi wenye kutubu na Waisraeli wenye shingo ngumu, ambao hawakuwa na imani na unyenyekevu.—Linganisha Kumbukumbu la Torati 9:6, 13.
Namna gani juu ya Yona mwenyewe? Alijifunza jinsi rehema ya Mungu ilivyo kuu. Na zaidi, jinsi Yehova alivyoitikia kunung’unika kwa Yona juu ya rehema iliyoonyeshwa Waninawi wenye kutubu yapaswa kutuzuia tusilalamike Baba yetu wa kimbingu awarehemupo watu siku zetu. Kwelikweli, na tushangilie kwamba kila mwaka maelfu humgeukia Yehova kwa imani na mioyo minyenyekevu.