Kitabu cha Biblia Namba 34—Nahumu
Mwandikaji: Nahumu
Mahali Kilipoandikiwa: Yuda
Uandikaji Ulikamilishwa: Kabla ya 632 K.W.K.
1. Ni nini kinachojulikana juu ya Ninawi la kale?
“UFUNUO juu ya Ninawi.” (Nah. 1:1) Unabii wa Nahumu wafunguka kwa maneno hayo yenye dalili mbaya. Lakini kwa nini yeye akafanya hilo julisho rasmi la maangamizi? Ni jambo gani linalojulikana juu ya Ninawi la kale? Historia ya jiji hilo yaelezwa kwa muhtasari na Nahumu kwa maneno matatu: “mji wa damu!” (3:1) Vichuguu viwili vilivyoko katika ukingo wa mashariki wa Mto Tigri, mkabala (kuelekeana) wa jiji la ki-siku-hizi la Mosul, katika Iraq ya kaskazini, vyaonyesha mahali lilipokuwa Ninawi la kale. Lilikuwa limetiwa ngome imara kwa kuta na mahandaki yenye maji na lilikuwa ndilo jiji kuu la Milki ya Ashuru katika sehemu ya pili ya historia yayo. Hata hivyo, mwanzo wa jiji hilo warudi nyuma kwenye siku za Nimrodi, “hodari wa kuwinda wanyama mbele za BWANA [Yehova, NW]. . . . Akatoka katika nchi ile akaenda mpaka Ashuru, akajenga Ninawi.” (Mwa. 10:9-11) Hivyo Ninawi lilikuwa na mwanzo mbaya. Likaja kujulikana sana hasa katika tawala za Sargoni, Senakeribu, Esar-hadoni, na Ashurbanipali, katika kipindi cha mwisho-mwisho cha Milki ya Kiashuri. Lilijitajirisha kutokana na vitu vya kuporwa kufuatia vita na kushinda sehemu mbalimbali, na likapata sifa kwa sababu ya watawala walo kutenda umati wa waliotekwa kwa ukatili wa kinyama.a Asema hivi C. W. Ceram, katika ukurasa 266 wa kitabu chake Gods, Graves and Scholars (1954): “Kilichofanya Ninawi likumbukwe sana katika fahamu za ainabinadamu si mambo yale mengine hasa bali mauaji ya kukusudia, kuchukua nyara kinguvu, kukandamiza watu, na kutenda kijeuri walio dhaifu; kwa vita na namna zote za jeuri ya kimwili; kwa matendo ya nasaba ya watawala wenye kumwaga damu waliokandamiza watu kwa kuwaogofya na ambao mara nyingi walikomeshwa na washindani wakali kuliko wao wenyewe.”
2. Dini ya Ninawi ilikuwa ya aina gani?
2 Namna gani juu ya dini ya Ninawi? Liliabudu miungu ya namna nyingi, mingi yayo ikiwa iliingizwa humo kutoka Babuloni. Watawala walo waliomba sana miungu hiyo walipokuwa wakienda nje ili kuharibu na kuua kabisa, na makuhani walo wenye pupa walichochea shughuli za jiji hilo za kujipatia ushindi, huku wao wakitazamia kulipwa kutokana na nyara zilizotekwa. Katika kitabu chake Ancient Cities (1886, ukurasa 25), W. B. Wright asema hivi: “Wao waliabudu nguvu, na walikuwa wakitoa sala zao kuelekea sanamu kubwa sana za mawe, simba na mafahali ambao mikono na miguu yao minene, mabawa yao ya tai, na vichwa vyao vya kibinadamu vilikuwa vifananishi vya nguvu, ushujaa, na ushindi. Kupigana kulikuwa ndiyo shughuli ya lile taifa, na makuhani walikuwa wachochea-vita wa wakati wote. Sana-sana wao walipewa riziki yao kutokana na nyara za ushindi, na ilipangwa kwa uthabiti kwamba wao wawe wakipewa fungu lisilobadilika la asilimia fulani ya nyara hizo kabla wengine hawajashiriki, kwa maana jamii hiyo ya wateka-nyara ilikuwa ya kidini mno.”
3. (a) Ni kwa njia gani maana ya jina la Nahumu yafaa? (b) Unabii wa Nahumu ni wa kipindi gani?
3 Ingawa ni mfupi, unabii wa Nahumu umejawa na upendezi. Yote tunayojua juu ya nabii mwenyewe yamo katika mstari ule wa ufunguzi: “Kitabu cha maono aliyoyaona Nahumu, Mwelkoshi.” Jina lake (Kiebrania, Na·chumʹ) lamaanisha “Mfariji.” Kwa uhakika ujumbe wake haukuwa faraja yoyote kwa Ninawi, lakini kwa watu halisi wa Mungu, ulimaanisha kupata kitulizo hakika cha kudumu cha kutoka kwa adui hodari asiyeridhika. Ni lenye faraja, pia, kwamba Nahumu hataji dhambi za watu wake mwenyewe. Ingawa sasa mahali Elkoshi ilipokuwa hapajulikani kwa uhakika, yawezekana kwamba unabii huo uliandikwa katika Yuda. (Nah. 1:15) Anguko la Ninawi, lililotukia katika 632 K.W.K., lilikuwa bado la siku za usoni wakati Nahumu alipoandika unabii wake, naye alinganisha tukio hilo na anguko la No-amoni (Thebesi, katika Misri) lililotukia muda mfupi kabla ya hapo. (3:8) Kwa sababu hiyo, lazima Nahumu awe aliandika unabii wake wakati fulani katika kipindi hicho.
4. Ni sifa gani za uandikaji zinazoonekana wazi katika kitabu cha Nahumu?
4 Mtindo wa kitabu hiki unakitofautisha. Hakina maneno mengi mno isivyohitajiwa. Njia yacho ya kueleza mambo kwa uthabiti mwingi na kulingana na uhalisi wa maisha yapatana na kuwa kwacho sehemu ya miandiko iliyopuliziwa na Mungu. Nahumu azidi wengine kwa nguvu za kueleza mambo, za kugusa hisia-moyo, na za lugha ya kutazamisha, na pia kwa maelezo yenye staha, kusimulia mambo kwa njia iliyo wazi ya kitamathali (mfano), na kupanga vifungu vya maneno yake kwa njia iliyo wazi sana ajabu. (1:2-8, 12-14; 2:4, 12; 3:1-5, 13-15, 18, 19) Sehemu kubwa ya sura ya kwanza yaonekana kuwa katika mtindo wa shairi la kufuatia mpangilio wa herufi za alfabeti. (1:8, NW, kielezi-chini) Mtindo wa Nahumu waongezewa uzuri na kushikilia kwake kichwa cha habari moja tu. Yeye ana chuki nyingi kabisa kuhusu adui mwenye hila wa Israeli. Yeye haoni jambo jingine lolote ila maangamizi ya Ninawi.
5. Ni nini kinachothibitisha uasilia wa unabii wa Nahumu?
5 Uasilia wa unabii wa Nahumu wathibitishwa na usahihi wa kutimizwa kwao. Katika siku ya Nahumu, ni nani mwingine ila nabii wa Yehova angalithubutu kutabiri kwamba lile jiji kuu lenye kiburi la mamlaka ya ulimwengu ya Ashuru iliyo kubwa ulimwenguni lingeweza kutiwa pengo kwenye “malango ya mito,” ikulu yayo ikomeshwe, nayo yenyewe iwe “utupu, na ukiwa, na uharibifu”? (2:6-10) Matukio yaliyofuata yalionyesha kwamba kweli kweli unabii huu ulipuliziwa na Mungu. Kumbukumbu za matukio ya kila mwaka za mfalme Nabopolassa wa Babuloni zaeleza hivi juu ya kutekwa kwa Ninawi na Wamedi na Wababuloni: “Jiji [waliligeuza] likawa vilima vya mabomoko na [ma]rundo (ya vifusi . . . ).”b Uangamivu wa Ninawi ulikuwa kamili sana hivi kwamba hata mahali lilipokuwa jiji hilo palisahauliwa kwa karne nyingi. Wachambuzi fulani walipata kudhihaki Biblia juu ya wazo hilo, wakisema kwamba Ninawi lisingaliweza kamwe kuwa lilikuwako.
6. Ni kitu gani kimefukuliwa mahali lilipokuwa jiji la kale la Ninawi ambacho chatetea usahihi wa Nahumu?
6 Hata hivyo, kuongezea uthibitisho zaidi wa uasilia wa Nahumu, mahali pa Ninawi paligunduliwa, na machimbuzi yakaanzwa huko katika karne ya 19. Ilikadiriwa kwamba mamilioni ya tani za ardhi zingehamishwa ili kupachimbua pote. Ni kitu gani kimefukuliwa katika Ninawi? Ni vitu vingi vinavyounga mkono usahihi wa unabii wa Ninawi! Kwa kielelezo, masalio ya majengo ya kale na michoro yalo vyashuhudia matendo yalo ya ukatili, na kuna masalio ya maumbo makubwa sana ya sanamu za fahali na simba wenye mabawa. Si ajabu kwamba Nahumu alinena juu yalo kuwa “kao la simba”!—2:11.c
7. Ni nini kinachounga mkono kukubaliwa kwa Nahumu?
7 Uhalali wa Nahumu waonyeshwa na kukubaliwa kwa kitabu hicho na Wayahudi kuwa ni sehemu ya Maandiko yaliyopuliziwa na Mungu. Chapatana kwa ukamili na sehemu nyingine yote ya Biblia. Unabii huo umetamkwa kwa jina la Yehova, kikitoa ushuhuda mfasaha juu ya sifa zake na ukuu wake upitao wa wengine wote.
YALIYOMO KATIKA NAHUMU
8. Ni hukumu gani ya maangamizi inayotangaziwa Ninawi, lakini kwa Yuda ni habari gani njema?
8 Tangazo la Yehova juu ya Ninawi (1:1-15). “BWANA [Yehova, NW] ni Mungu mwenye wivu [mwenye kutoza ibada isiyotia ndani wengine, NW], naye hujilipiza kisasi.” Kwa maneno hayo nabii atokeza tamasha kwa ajili ya “ufunuo juu ya Ninawi.” (1:1, 2) Ingawa Yehova ni mpole wa kasirani, mwone sasa akionyesha kisasi kwa kutumia upepo na tufani. Milima yatikisika, vilima vyayeyuka, na dunia yainuka-inuka. Ni nani awezaye kusimama mbele ya joto la kasirani yake? Hata hivyo, Yehova ni ngome kwa ajili ya wale wanaotafuta kimbilio katika yeye. Lakini Ninawi limehukumiwa maangamizi. Litafutiliwa mbali kwa furiko, na “mateso hayatainuka mara ya pili.” (1:9) Yehova atafuta jina lalo na miungu yalo. Yeye atalizika. Kwa utofautisho wenye kuburudisha, zipo habari njema kwa Yuda! Ni nini hizo? Mhubiri wa amani awaita waadhimishe sikukuu zao na kulipa nadhiri zao, kwa maana adui, “yule asiyefaa kitu,” amehukumiwa maangamizi. “Amekwisha kukatiliwa mbali.”—1:15.
9. Twapata maono gani ya kiunabii juu ya ushinde wa Ninawi?
9 Maono ya mapema ya uharibifu wa Ninawi (2:1–3:19). Nahumu atokeza mwito wa ushindani wenye dhihaka kwamba Ninawi lijiimarishe kupambana na mtawanyaji anayekuja. Yehova atakusanya tena walio wake mwenyewe, ‘fahari ya Yakobo na ya Israeli.’ Ona ngao na vazi la rangi nyekundu sana la watu walio hodari na vyuma vya pua vya rangi-moto vilivyoungwa kwenye “magari [yake] ya vita katika siku ya kujitengeza kwake”! Magari-vita yaendelea ‘kufanya mshindo’ katika barabara zile, yakikimbia kama meme za mvua. (2:2-4) Sasa sisi twapata maono ya kiunabii juu ya pigano lile. Waninawi wajikwaa na kufanya haraka kukinga ukuta lakini wapi. Malango ya mto yafunguka, ikulu yakomeshwa na wajakazi waomboleza na kupiga-piga mioyo yao. Wanaume wenye kutoroka waamriwa wasimame tuli, lakini hakuna mmoja anayegeukia nyuma. Jiji latekwa nyara na kuachwa ukiwa. Mioyo yayeyuka. Yako wapi sasa hayo makao ya simba? Simba amejaza pango lake mawindo kwa ajili ya wana-simba wake, lakini Yehova ajulisha rasmi hivi: “Tazama, mimi ni juu yako.” (2:13) Ndiyo, Yehova atachoma kabisa vyombo vyote vya kivita vya Ninawi, apeleke upanga kumeza simba walo wachanga, na kukatilia nje mawindo yalo kutoka duniani.
10. Ninawi lafichuliwa kuwa nini, na mwisho walo wazidi kuelezwaje?
10 “Ole wake mji wa damu . . . umejaa mambo ya uongo na unyang’anyi.” Sikia sauti ya mcharazo wa kiboko na ya gurudumu lenye kutatarika. Ona farasi mwenye kwenda kasi, gari-vita lenye kuruka-ruka, mpanda-farasi, mwali wa upanga, na mmweko wa mkuki—halafu, tungamo kubwa sana la mizoga. “Mizoga haina mwisho.” (3:1, 3) Na sababu ni nini? Ni kwa sababu limenasa mataifa kwa matendo yalo ya umalaya na kuzinasa familia kwa matendo ya ulozi. Kwa mara ya pili Yehova ajulisha rasmi hivi: “Tazama, mimi ni juu yako.” (3:5) Ninawi litafichuliwa kuwa mwanamke mzinzi na litekwe nyara, msiba walo uwe si afadhali kuliko ule wa No-amoni (Tebesi), ambalo Ashuru ilipeleka ndani ya utumwa. Ngome zalo ni kama tini mbivu, ambazo ‘zikitikisika zaanguka katika kinywa chake alaye.’ (3:12) Mashujaa walo wa vita ni kama wanawake. Hakuna kinachoweza kuokoa Ninawi lisipatwe na moto na upanga. Wanaume wenye kulilinda watatoroka kama bumba la nzige katika siku yenye jua, na watu walo watatawanywa. Mfalme wa Ashuru atajua kwamba hakuna kitulizo, wala hakuna maponyo kwa huu uangamivu mkubwa. Wote wenye kusikia ripoti hiyo watapiga makofi, kwa maana wote wameteseka kutokana na ubaya wa Ashuru.
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
11. Ni kanuni gani za kimsingi za Biblia zinazotolewa kielezi katika Nahumu?
11 Unabii wa Nahumu watoa kielezi cha kanuni fulani za kimsingi za Biblia. Maneno ya kufungua ya njozi yarudia sababu ya Mungu ya kutoa ya pili ya zile Amri Kumi: “BWANA [Yehova, NW] ni Mungu mwenye wivu.” Mara tu baada ya hilo yeye ajulisha uhakika wa yeye ‘kulipa kisasi juu ya adui zake.’ Kiburi cha ukatili na miungu ya kipagani ya Ashuru haikuweza kuiokoa na mtekelezo wa hukumu ya Yehova. Twaweza kuwa na uhakika kwamba kwa wakati wake vivyo hivyo Yehova atafikiliza haki kwa waovu wote. “BWANA [Yehova, NW] si mwepesi wa hasira, ana uweza mwingi, wala hatamhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe.” Hivyo haki na ukuu wa Yehova vyakwezwa kuliko uangamizaji wake wa Ashuru yenye nguvu. Ninawi ukaja kuwa “utupu, na ukiwa, na uharibifu.”—1:2, 3; 2:10.
12. Ni mrejesho gani anaotangaza Nahumu, na unabii wake waweza kukamatanishwaje na tumaini la Ufalme?
12 Kinyume cha Ninawi ‘kukatiliwa mbali,’ Nahumu ajulisha rasmi mrejesho wa ‘fahari ya Yakobo na ya Israeli.’ Pia Yehova apeleka habari za furaha kwa watu wake: “Tazama, juu ya milima iko miguu yake aletaye habari njema, atangazaye amani.” Habari hizo za amani zina uhusiano fulani na Ufalme wa Mungu. Twajuaje hilo? Ni wazi kwa sababu ya matumizi ya Isaya ya usemi uo huo, lakini akiuongezea maneno haya: “Aletaye habari njema ya mambo mema, yeye autangazaye wokovu, auambiaye Sayuni, Mungu wako anamiliki!” (Nah. 1:15; 2:2; Isa. 52:7) Kisha, mtume Paulo katika Warumi 10:15 atumia usemi huo kwa wale ambao Yehova awatuma wakiwa wahubiri Wakristo wa habari njema. Wao hupiga mbiu juu ya “habari njema ya ufalme.” (Mt. 24:14) Kwa uhalisi wa maana ya jina lake, Nahumu atoa faraja kwa wote wanaotafuta amani na wokovu unaoambatana na Ufalme wa Mungu. Wote hao watajua kwa uhakika kwamba ‘Yehova ni mwema, ni ngome siku ya taabu kwa wale wamkimbiliao.’—Nah. 1:7.
[Maelezo ya Chini]
a Insight on the Scriptures, Buku 1, ukurasa 201.
b Insight on the Scriptures, Buku 1, ukurasa 955.
c Ancient Near Eastern Texts, kilichohaririwa na J. B. Pritchard, 1974, ukurasa 305; vifungo vya duara na mraba ni vyao; Insight on the Scriptures, Buku 1, ukurasa 958.