-
“Mimi Ni . . . Mnyenyekevu Moyoni”‘Njoo Uwe Mfuasi Wangu’
-
-
SURA YA TATU
“Mimi Ni . . . Mnyenyekevu Moyoni”
“Tazama! Mfalme wako anakuja kwako”
1-3. Yesu anaingia Yerusalemu jinsi gani, na kwa nini watu fulani wanashangaa?
WATU huko Yerusalemu wana shangwe nyingi. Mtu mkuu anakuja! Nje ya jiji, watu wamekusanyika kando ya barabara. Wana hamu kubwa ya kumpokea mtu huyo kwa sababu watu fulani kati yao wanasema kwamba ni mrithi wa Mfalme Daudi na ana haki ya kuwa Mtawala wa Israeli. Wengi wao wana matawi ya mitende ya kumpungia; na wengine wanatandaza mavazi yao na matawi ya miti barabarani ili kuonyesha kwamba wanamheshimu. (Mathayo 21:7, 8; Yohana 12:12, 13) Inaonekana wengi wao wanataka kuona jinsi atakavyoingia jijini.
2 Huenda wengine wanatazamia aingie kwa fahari nyingi. Bila shaka, wanawajua watu fulani mashuhuri waliokuwa na misafara ya kifahari. Kwa mfano, Absalomu mwana wa Daudi alipojitangaza kuwa mfalme, alituma wanaume 50 wakimbie mbele ya gari lake. (2 Samweli 15:1, 10) Mtawala Mroma, Kaisari Yulio alidai mengi hata zaidi; pindi moja aliongoza msafara wa ushindi hadi kwenye bunge la Roma, akiwa amezingirwa na tembo 40 waliokuwa wamebeba taa! Hata hivyo, sasa watu wa Yerusalemu wanamngojea mtu mkuu hata zaidi. Iwe umati huo unajua au haujui, huyo ndiye Masihi, mwanadamu mkuu zaidi aliyewahi kuishi. Lakini, Mfalme huyo wa wakati ujao anapoingia jijini, wengine wanashangaa.
3 Hawaoni magari, wakimbiaji, farasi, wala tembo. Yesu amepanda punda, mnyama ambaye watu humtumia kubeba mizigo.a Yesu pamoja na punda huyo hawakuwa na mapambo yoyote. Badala ya matandiko ya gharama kubwa, wafuasi wa karibu wa Yesu wametandika mavazi mgongoni mwa punda huyo. Kwa nini Yesu alichagua kuingia Yerusalemu kwa njia ya unyenyekevu, licha ya kwamba watu wengine ambao hawakuwa muhimu kama yeye walisisitiza kuingia kwa fahari kubwa?
4. Biblia ilitabiri nini kuhusu jinsi ambavyo Mfalme wa Kimasihi angeingia Yerusalemu?
4 Yesu anatimiza unabii huu: “Shangilia sana . . . Paza sauti kwa ushindi, Ee binti ya Yerusalemu. Tazama! mfalme wako anakuja kwako. Yeye ni mwadilifu, analeta wokovu, ni mnyenyekevu, na amepanda punda.” (Zekaria 9:9) Unabii huo ulionyesha kwamba siku moja Mtiwa Mafuta wa Mungu, Masihi, angeenda Yerusalemu na kuwaonyesha watu kwamba yeye ndiye Mfalme aliyewekwa rasmi na Mungu. Pia, kuingia jijini kwa kutumia punda kungefunua sifa yake yenye kupendeza ya unyenyekevu.
-
-
“Mimi Ni . . . Mnyenyekevu Moyoni”‘Njoo Uwe Mfuasi Wangu’
-
-
a Kitabu kimoja kinapozungumzia tukio hilo, kinasema kwamba wanyama hao “ni viumbe wa hali ya chini.” Kwa kuongezea kinasema: “Wanajikokota-kokota, ni wakaidi, wanatumiwa na maskini kufanya kazi, na sura yao haivutii.”
-