Sura ya 43
Jiji Lenye Uzuri wa Kung’aa
Njozi ya 16—Ufunuo 21:9–22:5
Habari: Elezo la Yerusalemu Jipya
Wakati wa utimizo: Baada ya dhiki kubwa na Shetani kutiwa ndani ya abiso
1, 2. (a) Ni wapi malaika mmoja anakopeleka Yohana akaone Yerusalemu Jipya, na sisi tunaona tofauti gani hapa? (b) Ni kwa nini huu ndio upeo mtukufu wa Ufunuo?
MALAIKA alikuwa amempeleka Yohana jangwani akamwonyeshe Babuloni Mkubwa. Sasa mmojapo wa kikundi icho hicho cha kimalaika anaongoza Yohana kwenda kwenye mlima mrefu sana. Lo! anaona kitu tofauti kama nini! Hapa hapana jiji chafu, lenye ukosefu wa adili kama kahaba wa Kibabuloni, bali Yerusalemu Jipya—lenye kutakata, la kiroho, takatifu—nalo linashuka kutoka katika mbingu yenyewe.—Ufunuo 17:1, 5.
2 Hata Yerusalemu la kidunia halikuwa na utukufu kama huu. Yohana atuambia: “Na akaja mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na mabakuli saba yaliyojaa tauni saba za mwisho, na yeye akanena na mimi na kusema: ‘Njoo hapa, mimi nitaonyesha wewe bibi-arusi, mke wa Mwana-Kondoo.’ Kwa hiyo yeye akapeleka mimi mbali katika nguvu za roho kwenye mlima mkubwa na mrefu sana, na yeye akaonyesha mimi jiji takatifu Yerusalemu likija chini kutoka katika mbingu kutoka kwa Mungu na likiwa na utukufu wa Mungu.” (Ufunuo 21:9-11a, NW) Kutoka mahali hapo penye kufaa pa mlima huo mrefu kama mnara, Yohana anakagua jiji zuri katika vijambo vyalo vyote vyenye kupendeza. Watu wa imani wamekuwa na taraja lenye hamu nyingi la kuja kwalo tangu aina ya binadamu ilipoanguka ndani ya dhambi na kifo. Hatimaye ndilo hili! (Warumi 8:19; 1 Wakorintho 15:22, 23; Waebrania 11:39, 40) Ni jiji la kiroho zuri mno, lenye kufanyizwa kwa washika ukamilifu washikamanifu 144,000, lenye uzuri wa kung’aa katika utakatifu walo na likirudisha utukufu wenyewe wa Yehova. Huu ndio upeo mtukufu wa Ufunuo!
3. Yohana anaelezaje uzuri wa Yerusalemu Jipya?
3 Yerusalemu Jipya ni lenye kutia kimako kwa uzuri walo: “Mnururisho walo ulikuwa kama jiwe la thamani kubwa mno, kama jiwe la yaspa lenye kung’aa kwa uangavu sana kama fuwele. Lilikuwa lina ukuta mkubwa na ulioinuka juu sana na lilikuwa lina malango kumi na mawili, na kwenye malango malaika kumi na wawili, na majina yalikuwa yamechorwa ambayo ni yale ya makabila kumi na mawili ya wana wa Israeli. Katika mashariki kulikuwa na malango matatu, na kaskazini malango matatu, na kusini malango matatu, na magharibi malango matatu. Ukuta wa jiji ulikuwa pia na mawe ya msingi kumi na mawili, na juu yayo majina kumi na mawili ya mitume wa Mwana-Kondoo.” (Ufunuo 21:11b-14, NW) Inafaa kama nini kwamba gezo la kwanza ambalo Yohana anarekodi ni la uangavu wenye kuwaka! Lenye kung’aa kama bibi-arusi mpya, Yerusalemu Jipya linakuwa mwenzi anayefaa kwa Kristo. Huwaka kikweli, kama inavyoufaa uumbaji wa “Baba wa mianga ya kimbingu.”—Yakobo 1:17, NW.
4. Ni nini kinachoonyesha kwamba Yerusalemu Jipya si taifa la Israeli wa mnofu?
4 Kwenye malango yalo 12, yamechorwa majina ya makabila 12 ya Israeli. Kwa hiyo, jiji hili la ufananisho ni lenye 144,000, waliotiwa muhuri “kutoka kila kabila la wana wa Israeli.” (Ufunuo 7:4-8, NW) Kupatana na hili, juu ya mawe ya msingi 12 yako majina ya wale mitume 12 wa Mwana-Kondoo. Ndiyo, Yerusalemu Jipya si taifa la kimnofu lenye kuasisiwa juu ya wana 12 wa Yakobo. Ni Israeli wa kiroho, lenye kuasisiwa juu ya “mitume na manabii.”—Waefeso 2:20, NW.
5. Ni nini kinachomaanishwa na “ukuta mkubwa na ulioinuka juu sana” wa Yerusalemu Jipya na uhakika wa kwamba malaika wanawekwa kwenye kila mwingilio?
5 Jiji hili la ufananisho lina ukuta mkubwa mno. Katika nyakati za kale, kuta za jiji zilijengwa kwa ajili ya usalama na ili kuzuia maadui. Ukuta wa Yerusalemu Jipya “mkubwa na ulioinuka juu sana” huonyesha kwamba li salama kiroho. Hakuna adui ya uadilifu, hakuna yeyote aliye mchafu na asiye haki, atakayeweza kupata kuingia. (Ufunuo 21:27) Lakini kwa wale wanaoruhusiwa waingie ndani, kuingia ndani ya jiji hili lenye uzuri ni kama kuingia Paradiso. (Ufunuo 2:7) Baada ya Adamu kutolewa nje, makerubi waliwekwa kwenye upande wa mbele wa Paradiso hiyo ya kwanza kabisa kuzuia nje wanadamu wachafu. (Mwanzo 3:24) Hali moja na hiyo, malaika wamewekwa kwenye kila mwingilio wa Yerusalemu jiji takatifu ili kuhakikisha usalama wa kiroho wa jiji. Kweli kweli, katika muda wote wa siku za mwisho, malaika wamekuwa wakilinda kundi la Wakristo wapakwa-mafuta, ambalo huwa Yerusalemu Jipya ili lisipatwe na uchafu wa Kibabuloni.—Mathayo 13:41.
Kulipima Jiji
6. (a) Yohana anaelezaje kupimwa kwa jiji, na kupimwa huku kunaonyesha nini? (b) Ni nini kinachoweza kueleza kwamba kipimo kilichotumiwa kilikuwa “kulingana na kipimo cha binadamu, wakati uo huo cha malaika”? (Ona kielezi cha chini.)
6 Yohana aendelea na simulizi lake: “Sasa mmoja ambaye alikuwa akinena na mimi alikuwa akishika mwanzi wa dhahabu ukiwa kipimo, ili kwamba yeye apate kupima jiji na malango yalo na ukuta walo. Na jiji lina miraba minne, na urefu walo ni mkubwa kama upana walo. Na yeye akapima jiji kwa mwanzi, farlong’i elfu kumi na mbili; urefu na upana walo na kimo vi sawa. Pia, yeye akapima ukuta walo, kyubiti mia moja na arobaini na nne, kulingana na kipimo cha binadamu, wakati uo huo cha malaika.” (Ufunuo 21:15-17, NW) Wakati patakatifu pa hekalu palipopimwa, hilo lilidhaminia utimizo wa makusudi ya Yehova juu yapo. (Ufunuo 11:1) Sasa, kupimwa kwa Yerusalemu Jipya na malaika huonyesha jinsi makusudi ya Yehova kwa habari ya jiji hili tukufu yasivyoweza kubadilika.a
7. Ni jambo gani lenye kutokeza kuhusu vipimo vya jiji hilo?
7 Hili ni jiji lenye kutokeza kama nini! Mchemraba kamilifu farlong’i 12,000 (kilometa zapata 2,220) katika mzingo, likizungukwa na ukuta wa kyubiti 144, au meta 64, za kimo. Hakuna jiji halisi lingeweza kuwa na vipimo kama hivyo. Lingefunika eneo lenye ukubwa wa takribani mara 14 ya Israeli ya ki-siku-hizi, na lingeenda juu kama mnara kwa takribani kilometa 560 kuingia ndani ya anga la juu zaidi! Ufunuo ulitolewa kwa ishara. Kwa hiyo, vipimo hivi vinatuambia nini juu ya Yerusalemu Jipya la kimbingu?
8. Ni nini kinachomaanishwa na (a) kuta za jiji za juu zenye kyubiti 144? (b) kipimo cha jiji chenye farlong’i 12,000? (c) jiji kuwa na umbo la mchemraba mkamilifu?
8 Kuta za juu zenye kyubiti 144 hutukumbusha kwamba jiji limefanyizwa kwa wana wa Mungu waliolelewa kiroho. Tarakimu 12 inayoonekana katika vipimo vya jiji—vyenye farlong’i 12,000 za urefu, upana, na kimo zikiwa sawa—hutumiwa kitamathali katika mazingira ya kitengenezo katika unabii wa Biblia. Kwa sababu hiyo, Yerusalemu Jipya ni mpango wa kitengenezo uliobuniwa vizuri sana kwa ajili ya kutimiza kusudi la Mungu la milele. Yerusalemu Jipya, pamoja na Mfalme Yesu Kristo, ni tengenezo la Ufalme wa Yehova. Halafu kuna umbo la jiji: mchemraba mkamilifu. Katika hekalu la Solomoni, Patakatifu Zaidi Sana, ulimokuwa uwakilisho wa kimfano wa kuwapo kwa Yehova, mlikuwamo mchemraba mkamilifu. (1 Wafalme 6:19, 20) Basi, inafaa kama nini kwamba Yerusalemu Jipya, likimulikwa na utukufu wa Yehova mwenyewe, huonwa kuwa mchemraba mkamilifu, wa kadiri kubwa! Vipimo vyalo vyote ni vyenye kusawazika kikamilifu. Ni jiji lisilo na kasoro za ukawaida, au taksiri.—Ufunuo 21:22.
Vifaa vya Ujenzi Vyenye Thamani
9. Yohana anaelezaje vifaa vya ujenzi vya jiji?
9 Yohana aendeleza elezo lake: “Sasa muundo wa ukuta walo ulikuwa yaspa, na jiji lilikuwa dhahabu safi kama kioo changavu. Misingi ya kuta za jiji ilikuwa imerembwa kwa kila namna ya jiwe la thamani: msingi wa kwanza ulikuwa yaspa, wa pili safirosi, ule wa tatu kalkedoni, wa nne emeraldi, wa tano sardoniksi, wa sita sardiosi, wa saba krisolito, wa nane berulosi, wa tisa topazi, wa kumi krisoprasosi, wa kumi na moja hayakintho-buluu, ule wa kumi na mbili amethistosi. Pia, malango kumi na mawili yalikuwa lulu kumi na mbili; kila lango lilikuwa limefanyizwa kwa lulu moja. Na njia pana ya jiji ilikuwa dhahabu safi, kama kioo chenye kuona ndani.”—Ufunuo 21:18-21, NW.
10. Ni nini kinachomaanishwa na uhakika wa kwamba jiji limejengwa kwa yaspa, dhahabu, na “kila namna ya jiwe la thamani”?
10 Mjengo wa jiji ni wenye uzuri wa kung’aa kikweli. Badala ya vifaa vya ujenzi vya kidunia, visivyodumu kama udongo-mnamo au jiwe, sisi tunasoma juu ya yaspa, dhahabu iliyosafishwa, na “kila namna ya jiwe la thamani.” Lo! jinsi hivyo vinavyotaswiri vifaa vya ujenzi vya kimbingu! Hakuna kitu kingeweza kuwa na uzuri mno zaidi ya hilo. Sanduku la agano la kale lilikuwa limefunikwa kwa dhahabu safi, na katika Biblia elementi hii mara nyingi huwakilisha vitu ambavyo ni vizuri na vyenye thamani. (Kutoka 25:11; Mithali 25:11; Isaya 60:6, 17) Lakini Yerusalemu Jipya zima, na hata njia pana yalo, vimejengwa kwa “dhahabu safi kama kioo changavu,” kutaswiri uzuri na thamani asilia inayoshinda wazo.
11. Ni nini kinachohakikisha kwamba wale wanaojumlika kuwa Yerusalemu Jipya watawaka kwa ubora ulio wa juu zaidi sana wa usafi wa kiroho?
11 Hakuna msafishaji vito binadamu anayeweza kutokeza dhahabu yenye usafi hivyo. Lakini Yehova ndiye Msafishaji Stadi. Yeye huketi “akiwa msafishaji na mtakasaji fedha,” na yeye husafisha washiriki waaminifu mmoja mmoja wa Israeli wa kiroho “kama dhahabu na kama fedha,” akiondoa kutoka kwao taka zote. Watu mmoja mmoja ambao wamesafishwa na kutakaswa kikweli, hao pekee ndio mwishowe watajumlika kuwa Yerusalemu Jipya, na katika njia hii Yehova hujenga jiji kwa vifaa vya ujenzi vilivyo hai ambavyo huwaka kwa ubora wa juu zaidi sana wa usafi wa kiroho.—Malaki 3:3, 4, NW.
12. Ni nini kinachoashiriwa na uhakika wa kwamba (a) misingi ya jiji imerembwa kwa vito vya thamani 12? (b) malango ya jiji ni lulu?
12 Hata misingi ya jiji ni mizuri, ikiwa imerembwa kwa vito vya thamani 12. Hii hukumbusha akilini kuhani mkuu wa Kiyahudi, ambaye katika siku za kisherehe alivalia efodi iliyotiwa njumu za mawe yenye thamani tofautitofauti 12 ambayo kidogo yafanana na haya ambayo yameelezwa hapa. (Kutoka 28:15-21) Hakika si sadifa! Badala ya hivyo, hukazia utendaji wa kikuhani wa Yerusalemu Jipya, ambalo Yesu, Kuhani Mkuu, ndiye “taa” yalo. (Ufunuo 20:6; 21:23; Waebrania 8:1) Pia, zile manufaa za huduma ya Yesu ya ukuhani-mkuu huwasilishwa kwa aina ya binadamu kupitia Yerusalemu Jipya. (Ufunuo 22:1, 2) Malango 12 ya jiji, kila moja likiwa lulu moja ya uzuri mkubwa, hukumbusha kielezi cha Yesu kilichofananisha Ufalme na lulu moja ya thamani kubwa. Wote ambao huingia kupitia malango haya watakuwa wamekwisha onyesha uthamini wa kweli kwa ajili ya thamani za kiroho.—Mathayo 13:45, 46; linga Ayubu 28:12, 17, 18.
Jiji la Nuru
13. Halafu, Yohana anasema nini kwa habari ya Yerusalemu Jipya, na kwa nini jiji halihitaji hekalu lolote halisi?
13 Wakati wa Solomoni, lililokuwa lenye kutokeza zaidi katika Yerusalemu ni hekalu lililojengwa mahali palipoinuka zaidi sana pa jiji katika Mlima Moria kuelekea kaskazini. Lakini vipi Yerusalemu Jipya? Yohana asema: “Na mimi sikuona hekalu ndani yalo, kwa maana Yehova Mungu Mweza Yote ndiye hekalu lalo, pia Mwana-Kondoo. Na jiji hilo halina uhitaji wa jua wala mwezi kung’aa juu yalo, kwa maana utukufu wa Mungu ulilinururisha, na taa yalo ilikuwa ni Mwana-Kondoo.” (Ufunuo 21:22, 23, NW) Kwa kweli, hakuna haja ya kujenga hekalu halisi hapa. Hekalu la kale la Kiyahudi lilikuwa kigezo, na uhalisi wa kigezo hicho, hekalu kubwa la kiroho, umekuwako tangu Yehova alipompaka mafuta Yesu awe Kuhani Mkuu katika 29 W.K. (Mathayo 3:16, 17; Waebrania 9:11, 12, 23, 24) Pia hekalu hutangulia kudokezea jamii ya kikuhani ikitoa dhabihu kwa Yehova kwa ajili ya watu. Lakini wale wote ambao wanajumlika kuwa Yerusalemu Jipya ni makuhani. (Ufunuo 20:6) Na dhabihu kubwa, uhai mkamilifu wa kibinadamu wa Yesu, umekwisha tolewa mara moja kwa wakati wote. (Waebrania 9:27, 28) Na zaidi, Yehova anafikilika kibinafsi na yeyote anayeishi katika jiji.
14. (a) Ni kwa nini Yerusalemu Jipya halihitaji jua na mwezi kung’aa juu yalo? (b) Unabii wa Isaya ulitabiri nini kwa habari ya tengenezo la ulimwengu wote mzima la Yehova, na Yerusalemu Jipya lahusikaje katika hili?
14 Utukufu wa Yehova ulipopita karibu na Musa kwenye Mlima Sinai, ulifanya uso wa Musa kung’aa kwa uangavu mkubwa sana hivi kwamba yeye alilazimika kuufunika usionwe na Waisraeli wenzake. (Kutoka 34:4-7, 29, 30, 33) Basi, wewe unaweza kuwazia uangavu wa jiji ambalo hunururishwa daima na utukufu wa Yehova? Jiji kama hilo halingeweza kuwa na wakati wa usiku. Halingekuwa na uhitaji wa jua wala mwezi halisi. Lingekuwa likitoa nuru kwa umilele. (Linga 1 Timotheo 6:16.) Yerusalemu Jipya huoshwa na aina kama hiyo ya uangavu wenye kung’aa. Kweli kweli, bibi-arusi huyu pamoja na Bwana-arusi Mfalme wake wanakuwa ndio jiji kuu la tengenezo la Yehova la ulimwengu wote mzima—“mwanamke” wake, “Yerusalemu juu”—ambaye kwa habari zake Isaya aliandika hivi: “Kwako wewe jua halitathibitika tena kuwa nuru wakati wa mchana, na kwa uangavu mwezi wenyewe hautakupa wewe nuru tena. Na lazima Yehova awe kwako wewe nuru yenye kudumu kwa wakati usio dhahiri, na Mungu wako uzuri wako. Jua lako halitashuka tena, wala mwezi wako hautafifia; kwa maana Yehova mwenyewe atakuwa kwa ajili yako nuru yenye kudumu kwa wakati usio dhahiri, na siku za kuomboleza kwako zitakuwa zimekwisha kuja kwenye utimilifu.”—Isaya 60:1, 19, 20; Wagalatia 4:26, NW.
Nuru kwa Ajili ya Mataifa
15. Ni maneno gani ya Ufunuo juu ya Yerusalemu Jipya ambayo ni kama ya unabii wa Isaya?
15 Unabii uu huu ulitabiri pia: “Na mataifa kwa hakika yataenda kwenye nuru yako, na wafalme kwa uangavu wa kung’aa kwako.” (Isaya 60:3, NW) Ufunuo unaonyesha kwamba maneno haya yangetia ndani Yerusalemu Jipya: “Na mataifa yatatembea kwa njia ya nuru yalo, na wafalme wa dunia wataleta utukufu wao ndani yalo. Na malango yalo hayatafungwa hata kidogo mchana, kwa maana usiku hautakuwa huko. Na wao wataleta utukufu na heshima ya mataifa ndani yalo.”—Ufunuo 21:24-26, NW.
16. Ni nani walio “mataifa” ambayo yatatembea kwa njia ya nuru ya Yerusalemu Jipya?
16 Ni nani walio “mataifa” haya yanayotembea kwa njia ya nuru ya Yerusalemu Jipya? Hao ni watu, waliokuwa wakati mmoja sehemu ya mataifa ya huu ulimwengu mbovu, ambao huitikia nuru inayotolewa kupitia jiji hili tukufu la kimbingu. Wa kwanza kabisa katika hao ni umati mkubwa, ambao tayari umetoka katika “mataifa yote na makabila na vikundi vya watu na ndimi” na ambao huabudu Mungu mchana na usiku wakiwa kampuni moja na jamii ya Yohana. (Ufunuo 7:9, 15, NW) Baada ya Yerusalemu Jipya kuja chini kutoka katika mbingu na Yesu kutumia funguo za kifo na za Hadesi kufufua wafu, wao wataungwa na mamilioni zaidi, ambao hapo awali walitoka katika “mataifa,” wanaokuja kumpenda Yehova na Mwana wake, Mume wa Yerusalemu Jipya aliye mithili ya Mwana-Kondoo.—Ufunuo 1:18.
17. Ni nani walio “wafalme wa dunia” ambao ‘huleta utukufu wao’ ndani ya Yerusalemu Jipya?
17 Basi, ni nani wale “wafalme wa dunia” ambao ‘wanaleta utukufu wao ndani yalo’? Wao si wafalme halisi wa dunia wakiwa kikundi, kwa maana wao wanaenda chini kwenye uharibifu wakipiga vita dhidi ya Ufalme wa Mungu kwenye Har–Magedoni. (Ufunuo 16:14, 16; 19:17, 18) Je! wafalme wangeweza kuwa watu mashuhuri wa mataifa wanaokuwa sehemu ya umati mkubwa, au je! wao ni wafalme waliofufuliwa ambao wanatii Ufalme wa Mungu katika ulimwengu mpya? (Mathayo 12:42) Hata, kwa sababu kwa sehemu iliyo kubwa, utukufu wa wafalme kama hao ulikuwa wa kilimwengu na tangu hapo umefifia. Basi, “wafalme wa dunia,” wanaoleta utukufu wao ndani ya Yerusalemu Jipya lazima wawe 144,000, ambao ‘walinunuliwa kutoka kila kabila na ulimi na kikundi cha watu na taifa’ wakatawale wakiwa wafalme pamoja na Mwana-Kondoo, Yesu Kristo. (Ufunuo 5:9, 10; 22:5, NW) Wanaleta utukufu wao waliopewa na Mungu ndani ya jiji waongezee mng’ao walo.
18. (a) Ni nani ambao hawataruhusiwa kuingia katika Yerusalemu Jipya? (b) Ni nani pekee watakaoruhusiwa kuingia ndani ya hilo jiji?
18 Yohana aendelea: “Lakini kitu chochote kisicho kitakatifu na yeyote ambaye huendeleza kitu cha kunyarafisha na uwongo hataingia ndani yalo kwa vyovyote; ila wale tu walioandikwa katika hati-kunjo ya uhai ya Mwana-Kondoo. (Ufunuo 21:27, NW) Hakuna kitu kilichotiwa waa na mfumo wa mambo wa Shetani kinachoweza kuwa sehemu ya Yerusalemu Jipya. Hata ingawa malango yalo yanafunguliwa daima, hakuna yeyote “ambaye huendeleza kitu cha kunyarafisha na uwongo” atakayeruhusiwa kuingia. Hakutakuwa na waasi-imani katika jiji hilo wala mshiriki yeyote wa Babuloni Mkubwa. Na ikiwa wowote wanajaribu kuchafua jiji kwa kufisidi washiriki walo wa wakati ujao wakiwa wangali duniani, jitihada zao zinafanywa kuwa za bure. (Mathayo 13:41-43) “Wale tu walioandikwa katika hati-kunjo ya uhai ya Mwana-Kondoo,” 144,000 ndio mwishowe huingia ndani ya Yerusalemu Jipya.b—Ufunuo 13:8; Danieli 12:3, NW.
Mto wa Maji ya Uhai
19. (a) Yohana huelezaje Yerusalemu Jipya likiwasilisha baraka kwa aina ya binadamu? (b) “Mto wa maji ya uhai” hutiririka lini, na twajuaje?
19 Lile jiji lenye uzuri wa kung’aa litawasilisha baraka tukufu kwa aina ya binadamu duniani. Hilo ndilo Yohana anafuata kujifunza: “Na yeye akanionyesha mto wa maji ya uhai, mwangavu kama fuwele ukitiririka nje kutoka kiti cha ufalme cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kuteremka chini katikati ya njia pana yalo.” (Ufunuo 22:1, 2a, NW) “Mto” huu hutiririka lini? Kwa kuwa huo hutiririka “nje kutoka kiti cha ufalme cha Mungu na cha Mwana-Kondoo,” hiyo ingeweza kuwa tu baada ya siku ya Bwana kuanza katika 1914. Huo ndio uliokuwa wakati wa lile tukio lililotolewa habari kwa kupulizwa kwa tarumbeta ya saba na tangazo tukufu: “Sasa kumetukia wokovu na nguvu na ufalme wa Mungu wetu na mamlaka ya Kristo wake.” (Ufunuo 11:15; 12:10, NW) Katika nyakati za mwisho, roho na bibi-arusi wamekuwa wakiwaalika watu wenye mwelekeo unaofaa wanywe maji ya uhai bure. Maji ya mto huo yataendelea kupatikana kwa ajili ya watu kama hao mpaka mwisho wa mfumo huu wa mambo na, baadaye kuendelea katika ulimwengu mpya, wakati Yerusalemu Jipya ‘linapokuja chini kutoka katika mbingu kutoka kwa Mungu.’—Ufunuo 21:2, NW.
20. Ni nini kinachoonyesha kwamba kipimo fulani cha maji ya uhai tayari kinapatikana?
20 Hii si mara ya kwanza ambapo maji yenye kutoa uhai yametolewa kwa aina ya binadamu. Alipokuwa duniani, Yesu alisema juu ya maji ambayo yalitoa uhai wa milele. (Yohana 4:10-14; 7:37, 38) Na zaidi, Yohana anakaribia kusikia mwaliko wenye upendo: “Roho na bibi-arusi hufuliza kusema: ‘Njoo!’ Na acha yeyote anayesikia aseme: ‘Njoo!’ Na acha yeyote anayeona kiu aje; acha yeyote ambaye anataka atwae maji ya uhai bure.” (Ufunuo 22:17, NW) Mwaliko huo huvumishwa hata sasa, kuonyesha kwamba tayari kipimo fulani cha maji ya uhai kinapatikana. Lakini katika ulimwengu mpya, maji hayo yatatiririka kutoka katika kiti cha ufalme cha Mungu na kupitia Yerusalemu Jipya yakiwa mto halisi.
21. Ni nini kinachowakilishwa na “mto wa maji ya uhai,” na njozi ya Ezekieli ya mto huu hutusaidiaje kujua?
21 Huu “mto wa maji ya uhai” ni nini? Maji halisi ni elementi muhimu kwa uhai. Mtu anaweza kuendelea kuishi bila chakula kwa majuma kadhaa, lakini bila maji yeye atakufa kwa muda kama wa juma moja. Pia maji ni kitu kinachosafisha na ni muhimu kwa afya. Hivyo, maji ya uhai lazima yawakilishe kitu fulani cha maana kabisa kwa uhai na afya ya aina ya binadamu. Nabii Ezekieli alionyeshwa pia njozi moja ya huu “mto wa maji ya uhai,” na katika njozi yake, mto huo ulitiririka kwenda nje kutoka hekalu na kuteremka chini kuingia ndani ya ile Baharifu. Kisha, muujiza wa miujiza! Mkusanyiko huo wa maji yasiyo na uhai, uliojaa kemikali uligeuzwa kuwa maji matamu yenye kujaa samaki! (Ezekieli 47:1-12) Ndiyo, mto wa kinjozi unakumbusha kitu fulani ambacho hapo awali kilikuwa kifu, kuthibitisha kwamba mto wa maji ya uhai ni picha ya uandalizi wa Mungu kupitia Yesu Kristo kwa ajili ya kurudisha uhai mkamilifu kwa jamii ya kibinadamu ‘yenye ufu.’ Mto huu ni “mwangavu kama fuwele,” kuonyesha usafi na utakatifu wa uandalizi wa Mungu. Si kama “maji” ya Jumuiya ya Wakristo yenye madoa ya damu, yenye kuleta kifo.—Ufunuo 8:10, 11.
22. (a) Mto hutoka wapi, na kwa nini hili lafaa? (b) Ni nini kinachohusishwa katika maji ya uhai, na mto huu wa ufananisho unatia ndani nini?
22 Huo mto hutoka kwenye “kiti cha ufalme cha Mungu na cha Mwana-Kondoo.” Hii inafaa, kwa kuwa msingi wa maandalizi yenye kutoa uhai ya Yehova ni dhabihu ya ukombozi, na hiyo iliandaliwa kwa sababu Yehova “alipenda ulimwengu kadiri hiyo hivi kwamba yeye alitoa Mwana mzaliwa-pekee wake, ili kwamba kila mmoja anayejizoeza imani katika yeye asipate kuharibiwa bali awe na uhai wa milele.” (Yohana 3:16, NW) Maji ya uhai huhusisha pia Neno la Mungu, ambalo husemwa kuwa maji katika Biblia. (Waefeso 5:26) Hata hivyo, mto wa maji ya uhai hutia ndani si ukweli tu bali pia kila uandalizi mwingine wa Yehova, wenye kutegemea dhabihu ya Yesu, kwa ajili ya kuponesha wanadamu watiifu kutoka dhambi na kifo na kuwapa uhai wa milele.—Yohana 1:29; 1 Yohana 2:1, 2.
23. (a) Ni kwa nini inafaa kwamba mto wa maji ya uhai hutiririka kupitia njia pana ya Yerusalemu Jipya? (b) Ni ahadi gani ya kimungu aliyopewa Abrahamu itatimizwa wakati maji ya uhai yatatiririka kwa utele?
23 Wakati wa Utawala wa Miaka Elfu, manufaa za ule ukombozi zitatumiwa kikamili kupitia ukuhani wa Yesu na makuhani walio chini yake 144,000. Kwa kufaa, basi, mto wa maji ya uhai hutiririka kupitia katikati ya njia pana ya Yerusalemu Jipya. Walio washiriki walo ni Israeli wa kiroho, ambao pamoja na Yesu hujumlika kuwa mbegu ya kweli ya Abrahamu. (Wagalatia 3:16, 29) Kwa hiyo, maji ya uhai yanapotiririka kwa utele kupitia katikati ya njia pana ya jiji la ufananisho, “mataifa yote ya dunia” yatapata fursa kamili ya kujibarikia yenyewe kwa njia ya mbegu ya Abrahamu. Ahadi ya Yehova kwa Abrahamu itatimizwa kikamili.—Mwanzo 22:17, 18.
Miti ya Uhai
24. Yohana anaona nini sasa katika pande zote mbili za mto wa maji ya uhai, nayo ni picha ya nini?
24 Katika njozi ya Ezekieli, mto hata ukawa mvo, na nabii akaona ikikua katika pande zao zote mbili namna zote za miti yenye kuzaa matunda. (Ezekieli 47:12) Lakini Yohana anaona nini? Hili: “Na upande huu wa mto na upande ule kulikuwa na miti ya uhai ikifanyiza mazao kumi na mawili ya tunda, ikitoa matunda yayo kila mwezi. Na majani ya miti yalikuwa kwa ajili ya kuponeshwa kwa mataifa.” (Ufunuo 22:2b, NW) Hii “miti ya uhai” lazima pia iwe picha ya uandalizi wa Yehova kwa ajili ya kutoa uhai wa milele kwa aina ya binadamu tiifu.
25. Ni uandalizi gani ulio tele ambao Yehova hufanyia binadamu waitikivu katika Paradiso ya tufe lote?
25 Lo! ni uandalizi tele kama nini ambao Yehova anafanyia binadamu waitikivu! Si kwamba wanaweza kushiriki tu hayo maji ya uhai yenye kuburudisha bali waweza wakatunda kutoka miti hiyo namna namna yenye kuendelea ya matunda yenye kudumisha uhai. Oh, laiti wazazi wetu wa kwanza wangalitosheka na uandalizi unaofanana na huu ‘wenye kutamanika’ katika Paradiso ya Edeni! (Mwanzo 2:9) Lakini sasa Paradiso ya tufe lote ipo hapa, na Yehova hata hufanya uandalizi kupitia majani ya miti hiyo ya ufananisho kwa ajili ya “kuponeshwa kwa mataifa.”c Ukiwa wa hali ya juu zaidi kuliko dawa yoyote, ya miti-shamba au nyingineyo, ambayo hutolewa leo, utumizi wenye kutuliza wa majani hayo ya ufananisho utainua aina ya binadamu yenye kuitikadi kwenye ukamilifu wa kiroho na kimwili.
26. Yamkini pia miti ya uhai inatia ndani nini, na kwa nini?
26 Miti hiyo, ikiwa inatiliwa maji vizuri na mto, huenda kwa kuongezea ikatia ndani washiriki 144,000 wa mke wa Mwana-Kondoo. Wanapokuwa duniani hao pia wanakunywa kutokana na uandalizi wa Mungu kwa ajili ya uhai kupitia Yesu Kristo. Ndugu hao za Yesu waliozaliwa kwa roho wanaitwa kiunabii “miti mikubwa ya uadilifu.” (Isaya 61:1-3, NW; Ufunuo 21:6) Tayari wao wamefanyiza tunda jingi la kiroho kwa sifa ya Yehova. (Mathayo 21:43) Na wakati wa Utawala wa Miaka Elfu, watashiriki sehemu ya kutoa maandalizi ya ukombozi ambayo yatatumika kwa “kuponeshwa kwa mataifa” dhambi na kifo.—Linga 1 Yohana 1:7.
Hakuna Usiku Tena
27. Ni baraka zipi zaidi anazotaja Yohana kwa ajili ya wale wanaopendelewa kuingia ndani ya Yerusalemu Jipya, na ni kwa nini inasemwa kwamba “hakutakuwa tena na laana yoyote”?
27 Kuingia ndani ya Yerusalemu Jipya—hakika, hakungeweza kuwa na pendeleo zuri ajabu kupita hilo! Fikiri tu—hao ambao wakati mmoja walikuwa binadamu dhalili, wasiokamilika watafuata Yesu kuingia ndani ya mbingu wakawe sehemu ya mpango huo mtukufu! (Yohana 14:2) Yohana hutoa wazo moja la baraka zitakazofurahiwa na hawa, akisema: “Na hakutakuwa tena na laana yoyote. Bali kiti cha ufalme cha Mungu na cha Mwana-Kondoo vitakuwa ndani ya jiji, na watumwa wake watatolea yeye utumishi mtakatifu; na wao wataona uso wake, na jina lake litakuwa juu ya vipaji vya nyuso zao.” (Ufunuo 22:3, 4, NW) Wakati ukuhani wa Kiisraeli ulipopata kuwa mfisadi, ulipatwa na laana ya Yehova. (Malaki 2:2) “Nyumba” isiyo na imani ya Yerusalemu ilitamkwa na Yesu imeachwa. (Mathayo 23:37-39) Lakini katika Yerusalemu Jipya, “hakutakuwa tena na laana yoyote.” (Linga Zekaria 14:11.) Wakaaji walo wote wamekwisha tahiniwa katika moto wa majaribu hapa duniani, na wakiwa wamekwisha pata ushindi, watakuwa ‘wamekwisha vaa kutofisidika na kutokufa.’ Kwa habari yao, Yehova anajua, kama vile alivyojua kwa habari ya Yesu, kwamba hawataangukia mbali kamwe. (1 Wakorintho 15:53, 57) Na zaidi, “kiti cha ufalme na cha Mwana-Kondoo” kitakuwa huko, kufanya jiji hilo kuwa salama kwa umilele wote.
28. Ni kwa nini washiriki wa Yerusalemu Jipya wana jina la Mungu limeandikwa juu ya kipaji cha uso wao, na ni taraja gani lenye kusisimua lililo mbele yao?
28 Kama Yohana mwenyewe, washiriki wote wa wakati ujao wa hilo jiji la kimbingu ni “watumwa” wa Mungu. Wakiwa hivyo, wana jina la Mungu likiwa limeandikwa kwa kuonekana wazi juu ya kipaji cha uso wao, kumtambulisha yeye kuwa Mwenye wao. (Ufunuo 1:1; 3:12) Wao watalihesabu kuwa pendeleo lisilokadirika kumtolea utumishi mtakatifu wakiwa sehemu ya Yerusalemu Jipya. Yesu alipokuwa duniani, aliwapa ahadi yenye kusisimua hao waliotazamiwa kuwa watawala, akisema: “Wenye furaha ni wale walio safi katika moyo, kwa kuwa wao wataona Mungu.” (Mathayo 5:8, NW) Jinsi hawa watumwa watakuwa wenye furaha kumwona na kumwabudu Yehova kihalisi na kinaganaga!
29. Ni kwa nini Yohana husema juu ya Yerusalemu Jipya kwamba “usiku utakuwa hauko tena”?
29 Yohana aendelea: “Pia, usiku utakuwa hauko tena, na wao hawana uhitaji wa nuru ya taa wala wao hawana nuru ya jua, kwa sababu Yehova Mungu atatoa nuru juu yao.” (Ufunuo 22:5a, NW) Yerusalemu la kale, kama jiji jingine lolote duniani, lilitegemea jua kuwa nuru wakati wa mchana na nuru ya mwezi na nuru ya kubuniwa wakati wa usiku. Lakini katika Yerusalemu Jipya la kimbingu kutoa nuru kama huko kutakuwa si kwa lazima kabisa. Jiji hilo litamulikwa na Yehova mwenyewe. “Usiku” huenda ukatumiwa pia katika maana ya kitamathali, kurejezea janga au mtenganisho na Yehova. (Mika 3:6; Yohana 9:4; Warumi 13:11, 12) Hakungeweza kuwa na usiku wa aina hiyo katika kuwapo kwenye utukufu na kwenye kung’aa kwa Mungu mweza yote.
30. Yohana anamaliziaje njozi nzuri mno, na Ufunuo unatuhakikishia nini?
30 Yohana anafunga njozi hii nzuri mno kwa kusema kwa habari ya hawa watumwa wa Mungu: “Na wao watatawala wakiwa wafalme milele na milele.” (Ufunuo 22:5b, NW) Ni kweli, mwishoni mwa miaka elfu, manufaa za ukombozi zitakuwa zimekwisha tumiwa kwa utimilifu, na Yesu atamtolea Baba yake jamii ya kibinadamu iliyokamilishwa. (1 Wakorintho 15:25-28) Analofikiria Yehova kwa ajili ya Yesu na 144,000 baada ya hapo, sisi hatujui. Lakini Ufunuo unatuhakikishia kwamba utumishi mtakatifu wao uliopendelewa kwa Yehova utaendelea kwa umilele wote.
Upeo Wenye Furaha wa Ufunuo
31. (a) Ni upeo gani unaotiwa alama na njozi ya Yerusalemu Jipya? (b) Yerusalemu Jipya hutimiza nini kwa ajili ya waaminifu wengine wa aina ya binadamu?
31 Utimizo wa njozi hii ya Yerusalemu Jipya, mke wa Mwana-Kondoo, ndio upeo wenye furaha ambao kwao Ufunuo unaelekeza, na kwa kufaa hivyo. Wakristo wenzi wa Yohana wa karne ya kwanza ambao kwanza ndio waliopelekewa kitabu walitazamia kuingia ndani ya jiji hilo wakiwa roho watawala wenzi pamoja na Yesu Kristo. Baki la Wakristo wapakwa-mafuta ambao wangali hai leo duniani wana tumaini ilo hilo. Hivyo Ufunuo unasonga mbele kuelekea upeo wao mtukufu, wakati bibi-arusi aliyekamilika anapoungana na Mwana-Kondoo. Kisha, kwa njia ya Yerusalemu Jipya, manufaa za dhabihu ya ukombozi ya Yesu zitatumiwa juu ya aina ya binadamu, hivi kwamba hatimaye waaminifu wote wataingia ndani ya uhai wa milele. Katika njia hiyo bibi-arusi, Yerusalemu Jipya, akiwa msaidizi-mwenzi mshikamanifu wa Bwana-arusi Mfalme wake, atashiriki katika kujenga kwa umilele dunia mpya yenye uadilifu—yote hayo kwa utukufu wa Yehova Bwana Mwenye Enzi Kuu wetu.—Mathayo 20:28; Yohana 10:10, 16; Warumi 16:27.
32, 33. Tumejifunza nini kutokana na Ufunuo, na itikio letu la kutoka moyoni limepaswa kuwa nini?
32 Basi, tunahisi shangwe kama nini tunapokaribia kufunga mazungumzo yetu juu ya kitabu cha Ufunuo! Tumeona jitihada za mwisho za Shetani na mbegu yake zikibatilishwa kabisa na hukumu zenye uadilifu za Yehova zikifikilizwa mpaka utimilifu. Babuloni Mkubwa lazima aondoke asiweko milele, akifuatwa na elementi fisadi mno nyingine zote za ulimwengu wa Shetani. Shetani mwenyewe na roho waovu wake watatiwa ndani ya abiso na baadaye kuharibiwa. Yerusalemu Jipya litatawala pamoja na Kristo kutoka katika mbingu huku ufufuo na hukumu zikiwa zinaendelea, na mwishowe aina ya binadamu iliyokamilishwa itakuja kufurahia uhai wa milele katika dunia Paradiso. Jinsi Ufunuo unavyotaswiri kwa wazi sana vitu hivi vyote! Jinsi inavyoimarisha azimio letu la ‘kujulisha wazi hizi habari njema za milele kuwa taarifa teremeshi kwa kila taifa na kabila na ulimi na kikundi cha watu’ walio duniani leo! (Ufunuo 14:6, 7, NW) Je! wewe unajitumikisha mwenyewe kwa ukamili katika kazi hii kubwa?
33 Mioyo yetu ikiwa inajaa asante hivyo, acheni sisi tuangalie maneno ya kumalizia ya Ufunuo.
[Maelezo ya Chini]
a Uhakika wa kwamba kipimo kilichotumiwa kilikuwa “kulingana na kipimo cha binadamu, wakati uo huo cha malaika” huenda ukahusiana na uhakika wa kwamba jiji hilo linafanyizwa kwa 144,000, ambao awali walikuwa binadamu lakini ambao huwa viumbe vya roho miongoni mwa malaika.
b Angalia kwamba “hati-kunjo ya uhai ya Mwana-Kondoo” ina majina ya 144,000 tu wa Israeli wa kiroho. Hivyo inatofautiana na “hati-kunjo ya uhai” ambayo inatia ndani wale ambao wanapokea uhai wa milele duniani.—Ufunuo 20:12, NW.
c Angalia kwamba usemi “mataifa” mara nyingi hurejezea wale ambao si wa Israeli wa kiroho. (Ufunuo 7:9; 15:4; 20:3; 21:24, 26, NW) Tumizi la usemi huo hapa halidokezi kwamba aina ya binadamu itaendelea kuwa imepangwa katika vikundi vya kitaifa vyenye kutengana wakati wa Utawala wa Miaka Elfu.